Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Daniel Baran Sillo (5 total)

MHE. SILLO D. BARAN Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza migogoro ya mipaka kati ya Hifadhi ya Tarangire na Vijiji vya Gijedabung, Ayamango, Gedamar na Mwada katika Jimbo la Babati Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilihakiki mpaka wa Hifadhi ya Taifa Tarangire mwaka 2004 kwa kutumia Tangazo la Serikali Na. 160 la tarehe 19 Juni, 1970 ambapo alama za mipaka ziliwekwa ardhini. Kazi hiyo ilifanywa na wataalam kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Spika, uhakiki huo ulibainisha kuwa: (i) hifadhi ilikuwa imechukua baadhi ya maeneo ya Vijiji vya Mwikantsi (Hekta 1,014) na Sangaiwe, Kata ya Mwada (Hekta 536), hivyo maeneo haya yalirejeshwa kwa wananchi. (ii) wananchi pia, walichukua maeneo ya hifadhi katika Vijiji vya Ayamango (Hekta 2,986.3), Gedamar ( Hekta 2,185.1), Gijedabung (Hekta 1,328.2), Quash (Hekta 1,587.9) na Orng’andida (Hekta 930.6) ambavyo vimerejeshwa.

Mheshimiwa Spika, katika Vijiji vya Quash na Orng’ndida maeneo yaliyoangukia ndani ya mpaka wa hifadhi hayakuwa na watu, hivyo ilikuwa rahisi kuyarejesha hifadhini. Upande wa maeneo ya Vijiji vya Ayamango, Gedamar na Gijedabung uthamini wa mali za wananchi ambao walikuwa ndani ya mpaka wa hifadhi ulifanyika. Jumla ya kiasi cha shilingi za Kitanzania 175,050,924 zililipwa kwa wananchi hao kama fidia ya mali, posho ya usumbufu, posho ya makazi na posho ya usafiri kwa wote waliotakiwa kuhama. Malipo hayo ya fidia yalifanyika kama ilivyokuwa imepangwa na wananchi waliondoka ndani ya hifadhi.
MHE. SILLO D. BARAN aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Dareda – Bashnet – Dongobesh kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Dareda – Bashnet hadi Dongobesh yenye urefu wa kilometa 54 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania- TANROADS ambapo kilometa 10 zimejengwa kwa kiwango cha lami na kilometa 44 ni za changarawe. Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Dareda – Bashnet hadi Dongobeshi kwa kiwango cha lami. Kazi hii ilifanywa na Mhandisi Mshauri Luptan Consults Ltd kwa kushirikiana na Mhandisi Consultancy Ltd kwa gharama ya shilingi milioni 398. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, wakati ujenzi kwa kiwango cha lami ukisubiri upatikanaji wa fedha, Wizara yangu kupitia TANROADS inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 513.594 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hiyo. Ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Afya Bashnet baada ya Serikali ya Kijiji kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na mpango wa kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kuendelea na ujenzi wa vituo vya afya nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Babati. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya ya Babati kupitia mapato yake ya ndani imetenga shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya Bashnet katika eneo lenye ukubwa wa ekari 12.6 lililotengwa na Serikali ya Kijiji.

Mhjeshimiwa Spika, Ujenzi huo utaanza katika mwaka wa fedha 2021/2022 kama ilivyopangwa.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza upembuzi yakinifu na ujenzi wa miundombinu ya maji katika Ziwa Madunga ili kutatua tatizo sugu la maji katika Kata ambazo hazina maji Jimbo la Babati Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa Babati Vijijini ni asilimia 74. Kwa lengo la kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Serikali inaendelea na utafiti wa ubora na uwingi wa maji katika chanzo cha Ziwa Madunga. Utafiti huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2021 na usanifu wa miundombinu ya maji utakamilika katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022.
MHE. REGINA N. QWARAY K.n.y. MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka kati ya Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu na Vjiji vya Olacity na Minjingu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro kati ya Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu na Vijiji vya Olacity na Minjingu ulitokana na vijiji kutokutambua mipaka halisi kati ya vijiji hivyo na kiwanda, hivyo kusababisha wananchi kutoka katika vijiji hivyo kuingia na kufanya maendeleo katika eneo la kiwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwezi Januari, 2021 Serikali ilifanya uhakiki wa mpaka wa Kiwanda cha Minjingu na vijiji vinavyozunguka kiwanda hicho na kubaini kuwa kuna jumla ya kaya 83 ndani ya eneo la kiwanda ambapo kaya kutoka Vijiji vya Olacity na Minjingu ni miongoni mwa vijiji hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa kaya hizo, kaya 40 za wahanga wa mafuriko ambazo ziliombewa na Kijiji cha Minjingu makazi ya muda ndani ya eneo la kiwanda, lakini baada ya muda wa makubaliano kuisha, kaya hizo zimegoma kuondoka katika eneo la kiwanda, hivyo kusababisha kuwepo kwa mgogoro huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaielekeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Manyara kukutana na pande zote mbili zinazohusika ili kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo ifikapo Desemba, 2021.