Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ravia Idarus Faina (2 total)

MHE: RAVIA IDARUS FAINA aliuliza: -

Je, Kwa nini Vyama vya Michezo ikiwemo TFF na TOC vimekuwa vikibadili Katiba zao kwa lengo la kulinda viongozi waliopo madarakani na kudhibiti watanzania wengine wasigombee nafasi katika vyama hivyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uhai siku ya leo tukaendelea kutimiza wajibu wetu sisi Wabunge wa Bunge hili. Lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kuniamini tena na kunifanya Naibu katika Wizara hii. Mheshimiwa Rais nakushukuru sana. Lakini la tatu pia, niwatakie kila la kheri wanahabari wote kote nchini na duniani pia katika maadhimisho ya siku yao ya uhuru wa vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ravia Idarus Faina, Mbunge wa Makunduchi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Vyama vya Michezo Tanzania vinasajiliwa kwa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa na 12 ya Mwaka 1967 na marekebisho yake Na. 6 Mwaka 1971 pia namba 3 ya Mwaka 2018; pamoja na kanuni za msajili za Mwaka 1999.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mahitaji ya kubadili katiba za vyama kujitokeza na kufanyika katiba hizo haziwezi kuanza kufanya kazi, mpaka zisajiliwe upya na Msajili wa Vyama vya Michezo ambaye hupitia upya, kuona kama kanuni zinazosimamia Michezo na Sheria zingine za nchi zimeangaliwa. Iwapo msajili atabaini kuwa suala ambalo limeingizwa katika katiba halina maslahi kwa Chama na Taifa ikiwemo masuala ya utawala bora; Msajili amepewa mamlaka ya kisheria kukataa usajili huo kwa mujibu wa Kanuni za Usajili za Mwaka 1999, kifungu 11(3)(a) na (b).

Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Shirikisho la TFF na TOC haijawahi kubadili katiba zao kwa lengo la kulinda viongozi walioko madarakani kwa kuwa, mabadiliko hayo yote ya kikatiba ni lazima yakidhi vigezo vya usajili vinavyosimamiwa na msajili wa vyama na vilabu vya Michezo nchini, ikiwemo utawala bora na ukomo wa muda wa uongozi chini ya BMT.
MHE. RAVIA IDARUS FAINA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Ofisi za NIDA katika Wilaya ya Kusini Unguja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ravia Idarus Faina, Mbunge wa Jimbo la Makunduchi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na Ofisi za Wilaya kwa ajili ya kuwafikishia wananchi huduma za usajili na utambuzi wa vitambulisho karibu na maeneo yao. Katika kutekeleza mpango huo, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imefanikiwa kufungua ofisi 150 katika Wilaya zote za Tanzania Bara na Visiwani.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya NIDA katika Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja itajengwa katika Mwaka wa Fedha 2022/2023. Nakushukuru.