Supplementary Questions from Hon. Nashon William Bidyanguze (8 total)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niishukuru Serikali na Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini pia naomba nimuulize swali kwamba eneo lile ni eneo ambalo lina watu wengi kwa maana kata sita katika ukanda ya maji na wakati mwingine kivuko kilichopo huwa kinasombwa na maji kupelekea wananchi wale wanaathirika kwa muda mrefu zaidi na eneo lile lina vituo viwili vya afya ambavyo vina ambulance mbili.
Kwa hiyo, naomba Serikali ione namna ya kufanya haraka katika kuhakikisha kwamba wananchi wale wa Jimbo la Kigoma Kusini katika maeneo yale ya kata sita wanapata ufumbuzi wa jambo hili. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Nashon kwa kufuatilia jambo hili la barabara hii ya Ilagala. Niseme tu mimi Mkoa wa Kigoma nimefanyakazi na barabara hii naifahamu sana, ni kweli anachosema na ndiyo maana Serikali imeamua kutengeneza hili daraja ili kuondokana na adha hii.
Mheshimiwa Spika, tunavyoongea tayari Serikali iko kwenye hatua ya manunuzi ya kufuata Mhandisi Mshauri ambayo inasimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kusombwa na vivuko ni kweli kwamba kwenye daraja hili huu mto Maragalasi ni mto wenye zaidi ya kilometa 300 kwahiyo inawezekana kivuko hiki kinapata changamoto kwasababu ya magogo ambayo yanasombwa na mito na ndiyo maana usiku kivuko hiki huwa hakifanyikazi ila tu kinafanyakazi kunapotokea emergency.
Kwa hiyo tutaendelea na utaratibu huo huo lakini tutahakikisha kwamba hiyo barabara hilo daraja linakamilika mara mara fedha itakapopatikana. Ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa NaibU Spika, Waziri haoni kwamba kwa namna moja au nyingine anasababisha watumishi hawa kufanya kazi katika mazingira magumu na hasa muda ni mrefu maana Halmashauri ile imeanzishwa mwaka 2013 na tayari kuna baadhi ya watumishi wamekwishastaafu. Kwa hiyo naomba commitment ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo hili hawa wananchi wapiga kura wangu wanakwenda kulipwa lini fedha hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetangulia kusema katika majibu yangu ya msingi kwamba tunatambua madeni ya watumishi wetu katika Halmashauri ya Uvinza na Serikali imeendelea kuweka mipango kwa maana ya kutenga fedha kwenye bajeti ili kuhakikisha kwamba hayo madeni yatakwenda kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, madeni haya yanalipwa kwa kutumia fedha za matumizi mengineyo kwa maana ya OC, lakini pia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri.
Na hivyo tunaendelea kuwaelekeza Wakurugenzi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na kwa muktadha huu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza waanze kutenga fedha kwa ajili ya kuwalipa watumishi wale madeni yao kwa awamu ili watumishi wale sasa waweze kufanya kazi kwa kuwa na motisha kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anasema.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa zaidi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba na Serikali pia inaendelea kufanya uhakiki wa madeni hayo na kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunawalipa wale watumishi stahiki zao za yale madeni.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru Serikali kwa majibu mazuri yaliyotolewa mbele hapa, lakini ninalo swali moja la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jimbo langu la Kigoma Kusini linao urefu wa barabara hii ya Simbo kwenda Kalya ndio hiyo ambayo inazalisha hizo barabara tatu nilizozisema. Barabara ya Kalya kwenda Sibwesa inatoka nje ya nchi kwa sababu kuna bandari pale Sibwesa, lakini barabara hii pia ya Lubalisi inatoka nje ya mkoa na hii ya Kalya – Ubanda inatoka nje ya mkoa.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa naiomba Serikali iangalie kuweza kuipa kipaumbele barabara hizi kwa sababu zinaufungua mkoa kupitia Halmashauri ya Kigoma Kusini kwa maana ya Jimbo la Kigoma Kusini, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge alichoomba ni kwamba Serikali tuizingatie ile barabara na mimi nipokee ombi lake kwa sababu tumeshakiri katika jibu letu la msingi kwamba moja hiyo barabara tumeitambua na kuiingiza katika mpango. Awali TARURA wakati inaanzishwa tulikuwa tulikabidhiwa barabara zenye urefu wa kilometa 108,000; kwa hiyo sasa hivi kuna ongezeko la barabara karibu 36,000 mpya.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa barabara hizo ambazo zimetambulika ni pamoja na hizi barabara ambazo Mheshimiwa Mbunge umeziainisha. Kwa hiyo, kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha na tutakavyoendelea kuziweka katika mpango basi barabara hiyo tutaipa kipaumbele katika mwaka wa fedha unaokuja.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, naomba nishukuru pia kwa Serikali kutoa majibu mazuri lakini bado naomba niulize swali moja la nyongeza.
Katika Vijiji vya Ilalangulu, Chagu, Katumba na Songambele ni maeneo ambayo yanazungukwa na msitu wa Halmashauri na ambao msitu ule wakati mwingine wananchi wanapata shida ya kutekwa na hivyo kukosa mawasiliano.
Naomba Serikali itoe majibu kwamba ni lini hasa hawa wananchi nao wataweza kupata nafuu ya kupata mawasiliano kwenye vijiji vyao?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema katika jibu langu la msingi na pia kwa maelekezo ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara 61(j) ni haki ya msingi kwa kila wananchi wanaoishi ndani ya nchi yetu kupata mawasiliano; hivyo tunaamini kabisa kwamba baada ya kufanya tathmini na kujiridhisha ukubwa wa tatizo tutaenda kuchukua hatua na kuhakikisha kwamba wanafikishiwa mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika maeneo ambayo yako pembezoni na maeneo ambayo ni ya mbuga tunaamini kwamba katika mkataba huu ambao Mheshimiwa Waziri anaenda kuusimamia ili usainiwe maeneo 90 yanaenda kupata utatuzi wa changamoto wa mawasiliano baada ya kukamilika kwa ujenzi wa minara 90. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira kipindi ambacho Serikali itakuwa tayari basi tutahakikisha kwamba mawasiliano katika eneo hilo itakuwa imetatuliwa ahsante sana.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri, lakini pia ninalo swali moja la nyongeza; kwamba, Uvinza ndipo kunapopatikana malighafi ya kutengeneza saruji. Sasa nataka nijue Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba, kiwanda hicho kinajengwa ili wananchi waweze kupata ajira ya muda mfupi, lakini na muda mrefu na ili tuweze kukamata soko la DRC na Burundi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon William, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mbunge kwa kufuatilia. Amekuwa anafuatilia sana kuhusiana na ujenzi wa kiwanda katika Wilaya ya Uvinza, lakini mkakati wa Serikali ni kuendelea kuboresha miundombinu wezeshi ili kuvutia wawekezaji zaidi katika ujenzi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi ni mashahidi sasa hivi Kigoma itaenda kufunguka kwa sababu Mheshimiwa Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, anaunganisha gridi ya Taifa ya umeme katika Mkoa huo. Maana yake hii ni miundombinu wezeshi ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. Kwa hiyo, tunaamini kwa uboreshaji wa miundombinu hii wezeshi, pamoja na barabara tutavutia wawekezaji zaidi ambao watakuja kujenga pia katika Wilaya ya Uvinza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunaendelea kufanya juhudi za makusudi ili kuvutia wawekezaji zaidi ambao watajenga viwanda katika ukanda huo wa ziwa ili kushika soko katika nchi za jirani, kama alivyosema. Nakushukuru sana.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, kwanza naomba niishukuru Serikali kwa kujenga Chuo cha VETA pale Uvinza.
Sasa nauliza; ni lini chuo kile kitafanya kazi ili watoto wa pale waweze kuanza kuingia chuoni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Nashon, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna vyuo vyetu 25 vya Wilaya ambavyo tulianza ujenzi wake toka mwaka 2021 na ujenzi ule uko kwenye hatua za mwisho. Hivi sasa tunatengeneza samani au tunasambaza samani pamoja na vifaa vya kufundishia. Ni matarajio yetu katika mwaka ujao, 2023 vyuo hivi 25 vya Wilaya pamoja na vile vinne vya mikoa vitaanza kutoa mafunzo rasmi. Nakushukuru.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali la nyongeza.
Ni lini Serikali itajenga kituo cha polisi cha Wilaya Uvinza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu Wilaya ya Uvinza ni miongoni mwa wilaya mpya ambazo hazina vituo vya polisi, na kwa hiyo katika mkakati wetu wa kuhakikisha mikoa na wilaya zote ambazo hazina vituo vinajengewa vituo hivyo Uvinza ni eneo mojawapo litakalo zingatiwa katika ujenzi wa vituo vipya vya polisi.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali la nyongeza.
Ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji wa Kata ya Kazuramimba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, miradi yote ambayo ipo kwenye utekelezaji, tunaendelea kwa kasi nzuri sana kuhakikisha inaisha ndani ya wakati. Mheshimiwa Mbunge kama tulivyozungumza, tutasimama kwa pamoja kuhakikisha mradi huu unaisha ndani ya wakati. (Makofi)