Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Nashon William Bidyanguze (10 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, na mimi naomba nichangie hotuba ya Mheshimiwa Rais zote mbili, lakini pia naomba nichukue nafasi hii kwanza niwashukuru wananchi wa Jimbo la Kigoma Kusini kwa kunileta Bungeni kwa kura nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naomba niseme na niungane na wananchi wengine ambao wanasema kwamba Rais Magufuli ni chaguo la Mungu na ni kweli Rais Magufuli ni chaguo la Mungu. (Makofi)

Mimi kwenye Jimbo langu eneo kubwa ni eneo la maji, lakini Mheshimiwa Rais amekubali kukarabati meli ya Mv Liemba. Hivi sasa imeanza kukarabatiwa, lakini Mheshimiwa Rais siyo hivyo tu amekubali kutengeneza meli mbili moja itabeba watu na mizigo yao, lakini moja itabeba mizigo peke yake. Jimbo langu ni wahanga wa usafiri wa maji kwa maana hiyo wanatumia usafiri wa mitungwi ambayo inatumia mbao, kwa maana hiyo kumekuwa na ajali nyingi sana, lakini meli hizi zikitengenezwa zikikamilika tutakuwa wananchi wa Kigoma Kusini tumepata ufumbuzi na watu watasafiri kwa raha mstarehe kwa maana kutakuwa hakuna ajali lakini pia watasafirisha mizigo yao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wakati anapita jimboni kunadi sera za Chama cha Mapinduzi kuomba kura na kuniombea kura mimi alikubali kuongeza zahanati, kuongeza Hospitali ya Wilaya nyingine kwa maana Jimbo langu ni kubwa sana katika majimbo ya Mkoa wa Kigoma, alikubali kuongeza hospitali nyingine ya Wilaya maana yake mimi nakwenda kuwa na hospitali mbili za Wilaya ni jambo la kumshukuru sana Mheshimiwa Rais katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie katika habari ya uvuvi. Katika jimbo langu wananchi wanajishughulisha na uvuvi, namshukuru Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi aliweza kuwasikiliza wananchi wangu waliotoka jimboni kuja kuzungumzia malalamiko ya suala zima ya kanuni zilizokuwa siyo rafiki na wao na Mheshimiwa Waziri alionesha kabisa kusikitishwa kwa nini hizo kanuni ziliwekwa vile, kwa hiyo, nina imani Mheshimiwa Gekul ambaye ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi hili jambo anakwenda kulitatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili jambo litakwenda kuleta uchumi mzuri katika Jimbo la Kigoma Kusini kwa maana ya uvuvi, lakini pia Mheshimiwa jimbo langu wananchi wanajishughulisha na kilimo cha mpunga pamoja na mahindi na mihogo. Lakini ipo changamoto moja ambayo kwa kweli naomba Serikali iweze kusaidia, ni wanyama kwa maana ya mamba katika majaruba yale ya mpunga kwa mfano Kyala yaani watu wanakufa kwa sababu ya mamba ni wengi sana, tumejaribu kuwaambia watu wa mifugo wajaribu kupunguza wale mamba yaani mamba wale wana uwezo wa kuchukua binadamu yaani mmoja kwa kila siku, sasa fikiria kwa mwaka mzima ni watu wangapi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mpango kwa taarifa nzuri aliyoleta mbele yetu na naomba nichangie eneo la kilimo na uvuvi kama muda utanitosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichukue nafasi hii niwashukuru Wanajimbo la Kigoma Kusini kwa kunichagua, lakini pia nikishukuru Chama Cha Mapinduzi kuweza kurudisha jina langu ili niweze kupeperusha bendera ya kutetea Jimbo la Kigoma Kusini ambapo nilishinda kwa kishindo na pia Mheshimiwa Rais alipata kura nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwashukuru familia, hawa watu kama wasingeweza kunipa support nisingeweza kufika hapa nilipo; mke wangu pamoja na watoto lakini zaidi sana ndugu yangu mmoja ambaye anaitwa Gervas; Mkurugenzi wa World Worth. Huyu mtu alilfika kwenye mkutano wa kampeni wakati mimi nazindua tarehe 11 Oktoba, 20. Aliwaambia wananchi, mkimchagua huyu bwana Bidyanguze mimi nitamchangia milioni 50 kuongezea kwenye Mfuko wa Jimbo wa Serikali. Jambo la ajabu sana, kwa hiyo nataka nikwambie kuanzia sasa tayari katika Mfuko wa Jimbo ule ambao nilifadhiliwa na mwanaume yule tayari nilishapeleka milioni 12 mifuko ya cement 600 ya thamani ya milioni 12. Huyo mtu lazima nimpongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nichangie Mpango huu kwenye eneo la kilimo. Kilimo ni kweli ndiyo uti wa mgongo, lakini kwa bahati mbaya sana naomba nishauri Serikali, bado haijaweka miundombinu mizuri yaani ile ambayo inatamanisha wananchi waweze kupenda kilimo. Serikali bado inasaidia tu wale ambao wameitikia kilimo, mimi najiuliza wako vijana wengi wanaingia shule za sekondari wanamaliza vyuo vikuu, wote hawa plan yao ni kuajiriwa. Naamini Serikali haina uwezo wa kuajiri wote hao, sasa tufanyeje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Serikali ije na mpango wa kushawishi wananchi, hawa vijana ambao ni kundi kubwa, waweze kupenda kilimo. Kilimo wanakikimbia, si tunao majimboni kule, wapo ambao wamesoma wamemaliza vyuo vikuu lakini hawana kazi, lakini ukiwaambia twende tujiajiri kwenye kilimo hawana habari na hicho kitu. Sasa nadhani katika eneo hili la kilimo, yuko mchangiaji mmoja amezungumza vizuri na sikumbuki vizuri, hivi tathmini ya wanafunzi ya wanaokwenda kujifunza kilimo kusoma masomo ya kilimo hivi ni wangapi? Naona kama ni wachache sana, kwa sababu gani? Kilimo wanakikimbia na wale ambao wanalima wanakwenda kuchoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nadhani Wizara ya Kilimo ije na mpango ambao utatengeneza ushawishi ili watu waweze kulima. Kilimo kimetafsiriwa kwamba ni kwenda na jembe la mkono kwenda kulima, mtu aliyesoma hawezi kwenda kulima kwa kilimo hicho. Kwa hiyo tunatakiwa Serikali ije na mpango wa kusaidia kutoa mashamba maana mashamba yenyewe kuyapata ni kazi. Mashamba yapatikane kwa njia nyepesi kama vile ambavyo Serikali inahamasisha uwekezaji tuhamasishe uwekezaji ndani ya kilimo kwa watu wetu hawa vijana, tukishafanya hivyo, watu watakipenda kilimo, lakini mwisho wa siku lazima kilimo kile Serikali iweke utaratibu wa kupata masoko kwa ajili ya mazao hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mkulima kwa kiasi fulani, niliwahi kulima maeneo ya Tanga kule, lakini tuliwahi kupata mahindi mengi wakati fulani nadhani ilikuwa elfu mbili kumi na ngapi sijui, lakini Serikali kwa sababu ya kuhitaji kutunza chakula ndani ya nchi ilikataza watu kusafirisha mazao nje ya nchi. Hata hivyo, yenyewe Serikali haikuwa tayari kuyanunua. Sasa wewe fikiria, mtu amekwishalima na amekwishavuna, asafirishe akauze, apate fedha anazuiliwa na Serikali ni jambo jema, lakini basi yanunue hayo mazao. Kwa hiyo nafikiri kwenye eneo la kilimo tukilifanyia kazi ni sehemu nzuri sana ya kuajiri watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ufugaji pia; ufugaji ni kama kilimo. Sisi Kigoma tunalo Ziwa Tanganyika lina samaki wengi sana lakini elimu haipo ya uvuaji wa samaki, ni eneo moja ambalo kama Serikali ingejikita kufundisha na kutoa nyenzo kwa ajili ya watu waweze kuvua, nadhani vijana wetu hawa ambao wako katika shule na wanaingia kwenye shule na vyuo vikuu wangeweza kujikita baada ya kutoka kule, kuja kuingia kwenye habari ya uvuaji wa samaki. Habari hii ni ajira kubwa sana na ingeleta tija kubwa sana na fedha nyingi kwenye kuongeza kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nafikiri hili nalo lazima tuliangalie sana, kuliko kufikiria tu kwamba lazima mtu asome awe nani. Nasema hivi, watu wengi sasa hivi wanafikiria kila mtu awe Mbunge, wanafikiri kwamba kwenye Ubunge kidogo kuna nafuu, lakini Jimbo la Kigoma Kusini, Jimbo la Mwibara na mengine, hivi wote kama watafikiria kuja huku ni kwa nini? Ni kwa sababu inaonekana kidogo Mbunge akirudi kutoka Bungeni, anakuja amevaa vizuri, anaonekana anafaa. Kwa hiyo, nadhani Serikali iwekeze katika kilimo na uvuvi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuchangia hayo. Ahsante (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Waziri wa Maji. Waziri wa Maji huyu ametokea kwenye nafasi ya Naibu Waziri, inaonekana Mheshimiwa Rais alimwona pale alipokuwa akitenda kazi kwenye nafasi yake ya Unaibu Waziri ndipo akaona ampandishe daraja awe Waziri kamili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Meneja wa RUWASA pale kwenye Jimbo langu la Kigoma Kusini, pale Uvinza, naye ni mpya, lakini ameanza kazi vizuri. Ameanza kwa kutembelea kata zote na kuhakikisha anaona vijiji ambavyo havina maji aweze kuona namna ambavyo anawapatia maji wananchi wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na Wabunge wenzangu waliojaribu kusema namna ambavyo Wizara inaweza ikatengeneza miradi ya maji ya kitaifa. Jimbo langu liko pembezoni mwa Ziwa Tanganyika. Jimbo langu lina kata 16, lakini ni kata tatu tu ndio zina maji, lakini vijiji viko 61, vijiji ambavyo vina maji havifiki 10. Pia ni jambo la kushangaza sana kwamba, maji wananchi wanayaona, lakini uwezo wa kuyachukua hawana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama ambavyo Serikali kupitia Wizara ya Maji imeweka utaratibu wa kuchukua maji katika Ziwa Viktoria na kuyafikisha katika mikoa mbalimbali na hapa Dodoma yanakuja. Kwa nini Mheshimiwa Waziri asione namna ya kubuni mpango wa kuanzisha mradi mkubwa katika eneo lile kwa kutumia maji yale ya Ziwa Tanganyika ambayo mradi ule ungeenda mpaka kwenye Wilaya ya Nkasi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi katika jimbo letu, kama nilivyotaja, tuko karibu sana na maji, lakini iko miradi ambayo ilipelekwa ambayo mpaka sasa haijakamilika. Kwa mfano, Lukoma; uko mradi mmoja mzuri sana wa maji ulianzishwa mwaka 2010. Mpaka leo tunavyozungumza mradi ule ulikuwa na asilimia 80, lakini mpaka sasa haujaanza. Kijiji cha Lukoma watu wanasubiri maji hawayaoni, lakini fedha ya Serikali ilikwenda kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba, miradi hii ambayo Wizara inaianzisha wakati mwingine ni tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anatakiwa awe na mpango madhubuti, mpango ambao utampelekea kuonesha kwamba, amefanya maamuzi magumu. Miradi ambayo ni ya pesa nyingi, lakini itakuwa na matokeo mazuri kuliko vimiradi vidogovidogo ambavyo vinakuwa na pesa kidogokidogo na mwisho wa siku miradi ile haikamiliki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fikiria Kata hiyo ya Lukoma ambayo ina mradi wa maji huu wa mwaka 2010 ambao mpaka sasa haujakamilika na kata ile ina vijiji saba. Hivyo vijiji vyote havina maji, ila nashukuru tu kwamba, Mgambazi ndio kijiji kimoja ambacho katika vijiji saba ambacho kina maji. Pia Mwakizega uko mradi ambao ulianzishwa mwaka 2020, lakini mpaka sasa mradi huo haujaanza. Mabomba yapo, lakini tatizo ni viunganishi kama Waheshimiwa Wabunge wenzangu walivyozungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mlela pia upo mradi wa maji, kisima kilishachimbwa, lakini mradi ule wananchi wanaendelea kusubiri hawapati maji. Kandaga vile vile ndio kijiji ambacho mimi natokea, kijiji hicho kilichimbiwa visima, lakini bahati mbaya kumbe visima vile vilivyochimbwa inaonekana upembuzi yakinifu haukufanywa vizuri, vile visima havina maji, lakini fedha ya Serikali ilitumika katika eneo lile. Kwa hiyo, leo tunasubiri labda Mradi ule wa Mlela ambao tayari umeshachimbwa kisima na wataalam wale wanasema inawezekana yale maji wakayasogeza pale Kandaga ambapo ni vijiji vinafuatana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasubiri hiyo neema kama itapatikana na naomba nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa kweli katika eneo hili, tukiweza kumpitishia bajeti yake basi aweze kuniona, atembelee katika jimbo langu aone hiki kilio ninachokitoa kwa uhalisia kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile pana mradi pale Ilagala. Ule Mradi wa Ilagala bahati mbaya sana ni mradi ambao haukushirikisha wananchi. Walichimba kisima na bahati mbaya sana kile kisima kina maji ya chumvi wakati Ilagala kuna Mto Malagarasi, mto ambao una maji baridi. Sasa wananchi wanajiuliza, Wizara ya Maji kwa nini watuletee maji ya chumvi wakati sisi tuna maji baridi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mradi ule ni kama vile hauwezi kufanya kazi kwa sababu, wananchi hawataki kabisa yale maji. Kwa hiyo, tukienda kule Mheshimiwa Waziri nina imani atapata uchungu mkubwa kuona namna ambavyo anaweza kubadilisha ili tuweze kuwatengenezea pump ili wapate maji yale ya Mto Malagarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwambao mwa Ziwa Tanganyika lina kata nane, lakini katika kata zile ndio kata ambazo kwa kweli, kimsingi mvua zinaponyesha wananchi wanapata shida ya tatizo lile la kipindupindu, kwa sababu ziwa liko bondeni wananchi wanaishi juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati mwingine kutokana na mazingira yalivyo lazima walazimike kuchota maji ya ziwani ili waweze kujikimu na yale maji yanakuwa yameshachafuka kutokana na vinyesi ambavyo, maana vyoo vipo, lakini vyoo wakati mwingine vikifurika maana yake lazima choo kile kiende kule ziwani. Kwa hiyo, kuondoa tatizo la kipindupindu katika Kata za Sunuka, Sigunga, Helembe, Buhingu ni kuhakikisha kwamba tunapata miradi ya maji mikubwa ambayo inatokana na maji ya kutoka Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fikiria Sigunga ina vijiji vitatu lakini hakuna hata kijiji kimoja kina mradi wa maji. Hiyo Sunuka ambayo nimeitaja ina vijiji nane, lakini kuna kijiji kimoja tu kina ndio mradi wa maji.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nirudie kumwomba Mheshimiwa Waziri, tuongozane kwenda Jimboni, ili niweze kwenda kumwonesha matatizo yaliyoko jimboni kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu, Wizara ya Miundombinu. Naomba nilete masikitiko yangu kwa barabara kubwa hii ambayo inatoka Tabora kwenda Kigoma. Kwanza, naomba nichukue nafasi hii nimpongeze na kumshukuru Rais wa Awamu ya Nne, ndiye aliyetuunganisha na mikoa mingine sisi Kigoma pale alipotutengenezea Daraja la Mto Malagarasi na likaitwa Kikwete. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipo kipande kilibaki cha kilometa 51 ambacho kinatokea Mpeta baada ya kuvuka Daraja la Mheshimiwa Kikwete mpaka Uvinza ni kilometa 51, hili eneo limekuwa ni tatizo kwa muda mrefu sana. Unatoka Dar-es-Salaam, Dodoma, Tabora, unakwenda mpaka Kigoma lakini eneo hilo ndilo limebaki na vumbi, ni jambo la ajabu sana. Wananchi wanajiuliza hivi kuna nini? Kwa hiyo, naomba Waziri pamoja na kwamba nimeona kwenye bajeti yake ameitaja, lakini naomba nisisitize na wananchi wasikie kwamba barabara hiyo nimeitaja, ni kero kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ipo barabara nyingine ya Uvinza kwenda Kasulu nayo ni kero sana na ni barabara fupi sana. Kwa kweli, naomba katika bajeti hii hii barabara nayo iweze kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ipo nyingine inatoka Uvinza kwenda Mpanda kupita Mishamo. Hii nayo ni barabara ambayo kwa kweli ni ya kimkakati, ikiwekwa lami na sisi Kigoma tutakuwa tumeondokana na lawama na malalamiko kama ya wale wenzetu waliokuwa wanasema wametengwa. Sisi tumetengwa kwa sababu tumetengenezewa barabara za lami lakini vipande vimebaki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Kigoma Kusini, wewe ni shahidi, ulipokuwa ukitokea kwenye msiba wa marehemu Mbunge wetu ambaye alitangulia mbele ya haki, Mheshimiwa Nditiye, wakati unarudi kutoka Kigoma kwenda Mbeya ulipotea. Ulichukua barabara ambayo sio yenyewe, ile barabara ni ya Simbo – Kalya, ulikwenda kurudia kwenye kivuko cha pale kwenye Mto Malagarasi, pale ndiyo uliposhtuka kwamba barabara ile sio yenyewe, nakupa pole sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuja kuambiwa kwamba Naibu Spika alipotea alidhani hii barabara inakwenda Mbeya. Ukweli barabara ile kama itajengwa vizuri inayo access ya kwenda Mbeya, ulikuwa hujakosea, sema kule mbele ungepata shida sana. Barabara ambayo ungepita badaye ni kutoka Rukoma kwenda Ikuburu na Rubalisi baadaye inapita Mwese halafu ndio ungeingia sasa Mpanda kwenda sasa Kalya. Hii barabara ni muhimu sana kwa sababu ni barabara ya mkoa lakini inakwenda kuishia Kalya peke yake. Ni barabara nzuri bado tunatumia changarawe na kwa kweli kupitia nafasi hii nimpongeze Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Kigoma Bwana Eng. Choma, hii barabara anaingalia sana lakini bado kuna vipande ambavyo vina shida.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele imeshagonga.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema tu kwamba Daraja la Mto Malagarasi pale ulipokwamia ni tatizo, lakini nashukuru Wizara imetenga shilingi milioni 250 kwa ajili ya upembuzi yakinifu. Nina imani daraja hilo litaenda kujengwa. Naomba niunge mkono hoja. (Makofi/Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, uliniita mchangiaji wa tatu, nipo hapa William Nashon.

MWENYEKITI: Ulipoitwa hukuwepo.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwepo.

MWENYEKITI: Haukusimama lakini.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisimama, nilikuwepo.

MWENYEKITI: Haya endelea.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu sana ambayo ni Wizara ya Mawasiliano. Kwanza naomba nimpongeze ndugu yangu Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya. Wizara hii ni Wizara nyeti sana, kwa sababu sasa hivi kwa kweli wananchi wameshaelimishwa na wanazo simu zao na njia nyingi ni kutumia simu. Ukitaka kulipia maji, ni lazima utumie simu, lakini pia ukitaka kulipia umeme lazima utumie simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna shida kwenye mtandao huu wa kulipia umeme. Nadhani mnaweza mkaona kabisa, yaani hakuna namna ya kulipia umeme, kuna shida sana. Kwa hiyo, bado Wizara ina kazi kweli ya kufanya hii shughuli ili iweze kuwa na ufanisi mkubwa kuliko ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Wilaya ya Uvinza ambayo kwa kweli ni Wilaya ambayo watu waliitikia sana katika utaratibu huu wa wananchi kuwa na simu, kwa sababu hakuna namna nyingine, maisha ni simu. Kwa hiyo, Wizara hii ni Wizara ambayo inawagusa watu. Kwangu ninazo kata 16, lakini zipo kata nne, zote zina matatizo ya mawasiliano. Yaani ukienda kule Mbunge unafanya ziara, hata kama ningekwenda na Waziri, yaani siku hiyo tunashinda hakuna mawasiliano kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, ni Kata ya Mtegowanoti, yaani haina mawasiliano kabisa na hakuna mnara hata mmoja; ya pili ni Kata ya Kandaga hasa katika Kijiji cha Kandaga chenyewe. Kwa kweli na Kijiji kile ndipo ninapotokea; mimi nikishaingia kijijini pale, hakuna mawasiliano mpaka kesho nitoke kule, niende eneo lingine ambalo lina mawasiliano. Ni aibu sana. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kwakweli jambo hili Mheshimiwa Waziri aweze kuliangalia hasa katika eneo langu hilo la Kandaga na vijiji hivi ambavyo nimevitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Herembe ina vijiji vitatu, lakini vyote havina mawasiliano; Kata ya Igalula ina vijiji saba lakini vijiji ambavyo vina mawasiliano ni viwili; ambavyo ni Lukoma pamoja na Igalula yenyewe, vilivyobaki vyote, havina mawasiliano. Sasa kwa kweli ukiangalia hili ni tatizo. Ukienda kule wananchi wanamlalamikia Mbunge kwamba ni vipi sisi tumetengwa? Mbona wengine wana mawasiliano, sisi inakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nadhani, kwa kuwa na sisi Serikali inao mtandao wa TTCL, kwa nini basi tusiweze kupata minara ya TTCL ili tuweze kuondokana na hilo tatizo? Kwa sababu makampuni mengine haya yanafanya kazi kibiashara zaidi, lakini mtandao wetu huu wa kampuni ya TTCL, pamoja na kwamba na yenyewe inafanya kazi kibiashara, lakini pia mtandao ni wa Serikali. Kwa maana hiyo, ina huduma pia. Wenzetu hawa hawana huduma; wakiweka eneo mtandao au huo mnara, wakiona hali siyo nzuri ya mapato, wanahamisha. Sasa wakihamisha wale wachache maana yake wanaobaki, hawana huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, katika Jimbo langu eneo la mawasiliano, tukimaliza bajeti yake yeye mwenyewe Waziri twende Pamoja. Haiwezekani tuwe marafiki, halafu mimi nyumba inaungua. Mheshimiwa Waziri nitafurahi sana tukienda wote huko ili uone. Simu zako utazima, kwa sababu hutakuwa na uwezo wa kuzitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. Kama Mheshimiwa atanifanyia hivyo, basi hata shilingi yake sitashika. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimpongeze Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayofanya. Lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa jinsi alivyoweza kutatua mgogoro wa wavuvi katika Mkoa wa Kigoma kwa maana ya Majimbo matatu; Kigoma Kaskazini, Kigoma Mjini na Kigoma Kusini ambalo ndilo jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ametusaidia sana pale ambapo walikuja wale wavuvi na wakaja na agenda zao zilizosababisha Mheshimiwa Waziri kifuta baadhi ya kanuni ambazo hazikuwa rafiki. Mheshimiwa Waziri, nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa jinsi ambavyo mpango wa Serikali uliopo ni wa kuhakikisha kwamba inanunua meli za uvuvi katika Bahari Kuu ili nasi tuweze kufaidi samaki wale ambao watatusababishia kuongeza Pato la Taifa katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli tunasikitika sana wananchi tunapoona kwamba tunalo ziwa kuu lakini tumekuwa hatupati faida itokanayo na samaki wale katika ziwa kuu. Lakini inaonekana mpango wa Serikali ni kwamba sasa itanunua meli nne ambazo zitahakikisha kwamba zinavua samaki ambao watasababisha tupate mapato makubwa kutoka kwenye chanzo hiki cha mapato ambacho tumekiacha kwa muda mrefu. Hii naomba niwapongeze Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri kwa hii ambayo itakwenda kuongeza uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, alivyomaliza kutatua ule mgogoro katika zile kanuni kwenye jimbo langu pamoja na majimbo ya wenzangu wa Kigoma ambayo nafahamu kabisa utatuzi ule alikuwa anaendana na wavuvi wale wa Ziwa Tanganyika lakini katika Mkoa ule wa Katavi pamoja na Wilaya ile ya Tanganyika, na wenyewe walikuwemo katika ule ujumbe. Nina imani kwamba ukanda wote ule tatizo sasa hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo moja; naomba uige mfano wa Wizara ya Madini ambayo ina wachimbaji wadogo. Lakini wachimbaji wadogo wale wamewekewa utaratibu ambao Serikali imewatambulisha kwenye mabenki na sasa wanakopesheka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wetu katika Ziwa Tanganyika wanatumia vifaa ambavyo ni duni. Na ndiyo maana wakati mwingine samaki hawawezi kupatikana vizuri kwa sababu hakuna utaalam wa kisasa. Naomba katika eneo hili wavuvi wa Ziwa Tanganyika, pamoja na maeneo mengine waweze kukopesheka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atengeneze utaratibu kama ambavyo Wizara ile ya Madini imeweza kufika mahali sasa wachimbaji wadogo wanaweza kukopesheka. Hii sekta ya uvuvi pia ni sekta muhimu. Wakopesheke. Pia Wizara iweke utaratibu namna ambavyo baada ya kupata samaki wale waweze kuhifadhika kwenye majokofu ili waweze kuuzwa hata baadaye, lakini samaki wanapopatikana bado wabichi wanalazimika kuwauza harakaharaka ili wasiweze kuoza. Sasa wanapoteza fedha kwa sababu hawawezi kuweka, lakini kama wataweka maana yake watauza wakati ambao soko lipo. Hili naomba Mheshimiwa Waziri ulichukue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye eneo la ufugaji wa ng’ombe kwa maana ya mifugo. Amezungumza mchangiaji mwenzangu kwamba Wasukuma ndio watu ambao kwa kweli wanajishirikisha na mifugo. Jimbo langu lina vijiji 61; wote wanaofuga ng’ombe pale wao wanaochunga ng’ombe kule katika vijiji vile ni Wasukuma, sisi Waha hatufugi ng’ombe. Kama vile Mheshimiwa Spika alivyokuwa akizungumza kwamba Serikali haifugi ng’ombe na sisi Waha hatufugi ng’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba, ng’ombe wale ni wengi. Katika wilaya yangu ile, kwenye jimbo langu, tuna ng’ombe takribani 200,000 na hawa ng’ombe wamezagaa. Hakuna mpango wowote lakini wanasumbua wananchi ambao wanajishirikisha na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika eneo hili naomba nimshukuru Waziri kwa sababu alifika jimboni kwangu akaenda kutatua mgogoro ambao kwa kweli ulikuwa ni mkubwa katika eneo moja, ingawaje maeneo mengine hakufika, pale ambapo aliruhusu kwamba kwenye eneo ambapo alitoa hekta 6,000 ziweze kutumika kwa wafugaji. Hilo ni jambo ambalo wananchi wamelifurahia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona bado kuna eneo lingine, kwa mfano kata nane za ukanda wa maji, bado hukufika na hukutoa maelekezo yoyote, na huko ndiko kwenye matatizo ya kuingiliana wale wafugaji wanapoingia kwenye maeneo ya wakulima. Kesi ziko nyingi mno na ng’ombe wakishaingia kwenye shamba, hata ungeenda mahakamani, kesi inaamuliwa kwamba ng’ombe ndio wamekula; sasa unashitakije ng’ombe? Inakuwa ni ngumu sana. Kwa hiyo, naomba katika eneo hilo Wizara iweze kuja na mpango wa kuhakikisha kwamba hizi ranchi ambazo zipo ambazo hazitumiki basi ziweze kutumika sasa katika kipindi hiki ambacho hazitumiki Wizara iweze kuwapa wananchi waendelee kuzitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tunajinasibu kwamba sisi nchi yetu ni nchi ya tatu katika mifugo. Sasa Serikali katika eneo hili imefanyaje? Imewatengea maeneo gani? Unakuta ni migogoro. Kwenye maeneo ya wakulima kuna migogoro ya wakulima, lakini kwenye maeneo ya ranchi wakati mwingine pia wakiingia kwenye ranch kuna matatizo tena katika maeneo hayo. Sasa nadhani Wizara ingekuja na mpango ikatenga maeneo kwa ajili ya hawa ambao nao ni wafugaji na ni eneo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimalizie kwa kusema kuwa eneo hili Serikali bado haijawekeza. Kwa sababu jiulize; hawa ng’ombe 200,000 katika jimbo langu, kuna majosho mawili tu. Sasa tunasema nchi yetu ni nchi ya tatu katika mifugo kwa Afrika, sasa kwa nini tusifike mahali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye hotuba ya Waziri wa Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya katika wizara hii pia na Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pia naomba nimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara hii kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya. Tunao ushahidi mkubwa kwamba nchi yetu ilikuwa na giza, lakini sasa mwanga unaonekana, pamoja na kwamba zipo changamoto. Lakini nipongeze Serikali kwa kazi nzuri ambayo imefanywa ya kuhakikisha kwamba tunapata megawatt 2115 katika bwawa lile la Mwalimu Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli huo utakuwa ni ufumbuzi wa kudumu kuondokana na giza tuliokuwa nalo katika nchi yetu, lakini pia ni kwamba kutokana na umeme ni mwingi ambao utakwenda kuuzwa katika nchi jirani maana yake bwawa lile litakwenda kuongeza pato la Taifa pale ambapo tutakwenda kuuza umeme katika nchi jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili jambo la kupongeza sana Awamu ya Tano ambayo iliingia mkataba na ilifanya maamuzi magumu kwa kuhakikisha kwamba bwawa lile linajengwa pamoja na kwamba mipango ile ilikuwepo kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia niipongeze Serikali kwa kuingia mkataba wa kuona namna ya kujenga ile eneo la Malagarasi pale Igamba ambayo kwa kweli ni katika Jimbo langu la Kigoma Kusini huu mradi unakwenda kutekelezwa kulingana na hotuba ya Waziri wa Nishati naomba Mheshimiwa Waziri mradi huu unaonekana utaanza Septemba mwaka huu na utakwenda kuisha Septemba tena 2024, maana yake ni miaka minne.

Mheshimiwa Spika, naomba Mkoa wa Kigoma umekuwa ukitumia mafuta, umeme wa mafuta kwa muda mrefu sana na ndiyo maana unaweza kuona kwamba kimkoa hatuna viwanda, isingewezekana kupata kiwanda au viwanda katika eneo ambalo tunatumia umeme wa mafuta. Ambao umeme wa mafuta una gharama kubwa sana katika uendeshaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninayo imani, kwamba mradi huu ambao una megawatt 49.5 utakwenda kuwa ufumbuzi na wa Mkoa wa Kigoma kwa ujumla, lakini ninayo imani kutokana na bajeti yako na ulivyoonyesha, umeonyesha kabisa kwamba umeme wa grid ya Taifa utawahi kuingia Kigoma kabla ya mradi huu ambao utajengwa pale, pale Igamba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona ulitakiwa kufanya ziara kwenye Mkoa wa Kigoma pale Nguruka ambapo tayari kumeshaandaliwa na palishajengwa kwa ajili ya kupokelea umeme ambao ndiyo utakuwa unapoozewa pale. Lakini ninayofuraha kuona kwamba mpango wako Mheshimiwa Waziri kuingiza umeme wa grid ya Taifa Kigoma maana yake upande mmoja wa Tabora unaingilia Nguruka ambapo ni kwenye Jimbo langu pale katika Kijiji cha Mgaza pameshajengwa tayari, compound imeshakamilika.

Mheshimiwa Spika, lakini pia umeme mwingine wa grid ya Taifa unaingilia Kankoko kutokea Nyakanazi hii mipango miwili ikikamilika Mheshimiwa Waziri kwa kweli na sisi Kigoma tutakuwa tumepata ukombozi kutoka kwenye giza. Na ninayo imani sasa wawekezaji watakuja kwa ajili ya kuwekeza viwanda katika mkoa wetu ili na sisi mkoa wetu uweze kuinuka kiuchumi na wananchi wetu wa Kigoma waweze kupata ajira, kwa sababu bila viwanda ni vigumu sana kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika eneo hili la Ujenzi wa Igamba nimefurahi kuona kwamba tayari fedha zimekwisha patikana kwa ajili ya fidia, wananchi katika eneo hili walitwaliwa maeneo yao kwa muda mrefu na walizuiliwa wasiendelee kwa hiyo walikuwa hawawezi kufanya chochote kwa sababu ya mradi huo, lakini naona kabisa kwamba sasa fedha ya fidia nayo pia imepatikana. Naomba Mheshimiwa Waziri jambo hili uende kulifanyia kazi ili wananchi wale waweze kupata fidia katika maeneo ambayo waliyaachia kwa ajili ya mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu kuna vijiji 61 ni kweli vipo vijiji 17 tayari vimekwishapata umeme na maana yake kuna vijiji 14 bado havijapata umeme kabisa, lakini kwamba hata hivi vijiji 17 ambavyo vimekwishapata umeme ni katika maeneo tu kama Waheshimiwa Wabunge wenzangu wanavyoongea. Na hii imetuletea malalamiko makubwa sana sisi Wabunge, tunalalamikiwa sana kwamba kwanini umeme unakuja hapa na baadaye kwenye vitongoji vingine umeme haufiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapata wakati mgumu katika kujibu maswali tunaomba Mheshimiwa Waziri hili jambo lifanyie kazi. Nafurahi kuona kwamba unao mpango mzuri kwamba tayari makandarasi wameshapatikana na nimekuwa nikikusumbua sana, lakini mpango wa Serikali ni kwamba umeme utapatikana 2022 kwa maana ya nchi nzima, kwa maana ya vijiji vyote.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba wakandarasi hawa ambao sasa wameteuliwa waweze kwenda kuondoa hizi kero pamoja na kwamba tunatakiwa tuendelee kumaliza vile vijiji 14, lakini pia huku kwenye vijiji 17 ambavyo tayari vina umeme lakini kuna maeneo mbalimbali hayana umeme katika vijiji hivi kwenye vitongoji na hiyo kazi pia iendelee kupunguza malalamiko.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Kigoma Kusini zipo Kata nne, Sigunga, Mgambo, Kalya na Igalula, kata hizi zinatumia umeme wa jua, wananchi hawa wamekuwa wakilalamika sana kila siku napigiwa simu kwamba kwanini mkandarasi huyu ambaye ni Jumeme kwanini anawauzia umeme unit moja shilingi 4000. Shilingi 4000 tunakuwa na bei mbili kwenye nchi moja hivi hawa wananchi tunawaonaje, tunawasaidiaje Mheshimiwa Waziri, nimekwisha kuja kwako mara nyingi sana, lakini ulionyesha kutatua tatizo hili na leo pia umetoa tamko, lakini pia bado nakuomba ziara yako ya kwenda Kigoma kutokea Tabora iendelee kuwepo na nitaomba nishirikiane na wewe unipe taarifa lini utakwenda nione uende kutoa tamko ili kusudi hawa watu wakome, wakome kabisa. (Makofi)

SPIKA: Ahsante, Ahsante Mheshimiwa Bidyanguze.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naoamba basi niweze kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niunge mkono hoja kwa sababu Kamati hii ni yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anafanya kazi vizuri na pia kwenye jimbo langu amenijengea madarasa 196. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimshukuru na kumpongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati kwa kuwasilisha taarifa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najikita kwenye eneo moja kulingana na dakika ambazo ni chache; eneo la watoto wanaopata mimba katika shule zetu za Sekondari na Msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo imeruhusu sasa watoto wale ambao wamepata ajali ya kupata mimba watarudi tena shuleni kusoma baada ya kuwa wanaendelea kunyonyesha. Hilo ni jambo jema na wananchi wamelifuarahia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili isije kuonekana Serikali sasa imeruhusu mimba za shuleni. Hili ni jambo la kuangalia sana; kwamba kwanza kwenye familia zenyewe ambako hawa watoto ndiyo wanatoka, tuvunje ukimya, tuzungumze hili suala la mimba, tusiwafiche watoto wetu. Kama mwanaume utashindwa kuongea na kijana wako, basi tafuta namna ambavyo ujumbe utamfikia kijana wako, lakini kama huna uwezo wa kuongea na msichana basi tafuta hata shangazi aweze kuongea na huyu msichana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ni vizuri pia ije na mpango mwingine. Niliwahi kuzunguza wakati fulani kwenye semina nikasema Serikali ilete mtaala ambao utasababisha kufundishwa wale watoto wafikie hatua ya kujua kwamba mimba inapatikana wakati gani. Kwa sababu ile ni ajali. Ni ajali. Hakuna mtoto anayetegemea kupata mimba, hakuna. Anakwenda kusoma ilia pate elimu. Kwa nini anapata mimba; anapata mimba kwa sababu ni ajali. Na anapata mimba kwa sababu wakati mwingine hajui kwamba ile mimba anaipatapataje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa wale ni wanafunzi na wanasoma, basi wafikishwe kwenye eneo la kalenda, kwamba ukitaka kuthubutu kufanya jambo hilo, basi tarehe hii na hii usithubutu hicho kitendo. Kabisa. Kama mwenzangu aliyechangia aliposema kwamba…

T A A R I F A

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, taarifa.

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba kitendo cha ngono kwa mila na desturi za Mtanzania na kwa imani za dini zetu zote haipaswi mtoto kufundishwa namna ya kukifanya na kwamba kufanya hivyo ni sawa na kuhalalisha dhambi hiyo ya uzinzi. Ahsante. (Makofi)

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo lazima tulizungumze kwenye familia zetu lakini pia tulipeleke na shuleni. Bila kufanya hivyo Serikali itaonekana sasa kuruhusu hawa watoto waliopata mimba shuleni na warudi tena kusoma shuleni, itaonekana imehamasisha wanafunzi kupata hizo mimba. Naamini kabisa mimba zile zinapatikana kama vile ajali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niishauri Serikali; habari ya kukataa kufundisha somo hili tutakuwa tunajipotezea muda kwa sababu tunaposema kwamba kujamiiana ni dhambi, ni sawa ni dhambi, lakini lazima tufikie mahali kwamba no, usifanye ngono kipindi hiki na hiki, ndiyo. Tufike mahali hilo tuliseme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja tena. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini pia naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kuweza kusimama hapa Bungeni niweze kuchangia kwenye hotuba hii ya Waziri wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya yote naomba nimshukuru Rais wetu mpendwa Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya katika nchi yetu na hasa katika Jimbo langu la Kigoma Kusini. Nimeshuhudia na wananchi wameshuhudia kupata madarasa 196 kwenye eneo la Sekondari na madarasa kwenye shule shikizi. Ni jambo kubwa sana na shule hizi zimekuwa ni mpya zaidi sasa kuliko shule zile za msingi. Naomba katika eneo hili shule za msingi nazo Mheshimiwa Waziri uzione kwamba zimebakia chini sana na zimebaki na majengo mabovu sana nimeona kwenye hotuba yako ya bajeti umeonyesha kutenga fedha kwa ajili ya shule kongwe naomba na mimi kwenye Jimbo langu liangalie sana ziko shule nyingi ambazo kwa kweli zina majengo mabovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano iko shule moja katika Kata ya Itebula na ni shule yenyewe ya Itebula kwa kweli mpaka watoto wamehama kujaribu kusomea kwenye vyumba vichache ambavyo kidogo kuna nafuu na mimi kwenye mfuko wangu wa Jimbo nimepeleka fedha pale angalau nijaribu kuokoa hali ya shule ile na hali ya wale watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kwenye eneo la ahadi za viongozi wakuu. Nakumbuka Mheshimiwa Hayati Magufuli wakati anaomba kura kwenye Jimbo langu eneo lile la Uvinza aliahidi kilometa tano za barabara ya lami lakini nashukuru kwamba angalau kuna kilomita mbili zinaendelea kujengwa. Lakini pia aliahidi kilomita tano Nguruka bado hata kilomita moja haijajengwa, sasa naomba Mheshimiwa Waziri kwenye eneo hili la ahadi za Viongozi wetu Wakuu kwa kweli uweke nguvu sana kwa sababu inapunguza imani ya wananchi na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Magufuli aliahidi kutoa Shilingi Milioni 10 kwenye kituo cha afya pale Kazulamimba wananchi wanashangaa hivi ni kweli Milioni 10 inaweza ikashindikana kupelekwa pale Kazulamimba ambapo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ni jambo la kushangaza sana na mimi wamekuwa wakinisumbua sana wanasema Mheshimiwa Mbunge ni namna gani Milioni 10 haijafika. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri upeleke Milioni 10 Kazulamimba kwa sababu tayari wameshajenga boma wanahitaji kuendeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa alitoa ahadi ya kupandisha hadhi kituo cha afya cha pale Nguruka na kilishapanda hadhi kwa hiyo tunasubiri Mheshimiwa Waziri uweze kuleta fedha kwa ajili ya kujenga sasa majengo kwa ajili ya kuendeleza sasa hospitali ile ambayo ilishapandishwa hadhi. Nilijenga hoja wakati ule naomba kura wananchi na Mheshimiwa Rais alikuwepo kwamba Nguruka mpaka kwenye hospitali ya Wilaya ilipo ni umbali wa kilometa 100 kwa hiyo Mheshimiwa alikubali kuongeza hadhi ya kituo kile na kilishapanda hadhi naomba uweke fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna ahadi ambazo alipokuja Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Ummy Mwalimu alikubali kujenga kituo cha afya chenye hadhi ya hospitali zaidi kidogo ya kituo cha Afya kule ukanda wa maji, eneo moja linaitwa Lukome na ninashukuru Serikali fedha Shilingi 250,000,000 zimeshakuja na ujenzi unaendelea naomba kwenye bajeti hii Mheshimiwa Waziri uongeze fedha ili tuweze kumalizia ujenzi wa hospitali ile kwa sababu inakuwa ni hospitali ya rufaa kwa sababu eneo lile na Mheshimiwa Ummy alitengeneza historia kutoka Makao Makuu ya Wilaya kwenda Kalya ni kilometa 300 kwa hiyo unaweza ukaona ni eneo kubwa sana ambalo linahitaji huduma hiyo ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri Ummy alikubali kufungua barabara ambayo inatoka Kalya kwenda Sumbawanga, alikubali kutoa Shilingi Bilioni Moja na Milioni Mia Tano, naomba ahadi hiyo uiandike ili kusudi mwaka huu wa fedha tuweze kupata hiyo fedha tuweze kufungua hiyo barabara. Pia aliahidi kujenga jengo moja la wodi ya wanaume na watoto pale kwenye kituo cha afya cha Kalya, naomba ahadi hizi Mheshimiwa kwa sababu wewe sasa ndiyo umeingia kwenye kiatu ambacho alikuwa amevaa Waziri Ummy hili jambo uweze kulichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo kwakweli mambo yanaenda vizuri na naomba nipongeze…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze kwa mchango wako.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, na niseme naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii na mimi nikupongeze kwa kuchaguliwa kwako lakini naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja katika kumpongeza Waziri wa Elimu pamoja na Naibu wake pamoja na staff yake nzima kwa kazi nzuri wanayofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba nijikite kwenye eneo moja lakini yatakuwa maeneo mawili. Moja ni kwenye shule mbili ambazo zimetelekezwa pale kwenye Jimbo langu ambazo ni shule za Wizara hii ya Elimu ni shule moja ya Lugufu Boys na shule moja ya Lugufu Girls. Hizi ni shule za Wizara ya Elimu, shule hizi zimetelekezwa kwa sababu hazijapata miundombinu ya maji pamoja na umeme. Naomba Mheshimiwa Waziri unisaidie kwenye jambo hili kwa sababu hizi hazipo chini ya Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi Jimbo langu lina Tarafa tatu. Nilikuwa naomba Tarafa ya Nguruka tupate high school kwa sababu tuna sekondari nyingi. Lakini pia naomba kwenye Tarafa ya Buhingu, Buhingu Sekondari ipandishwe hadhi iwe shule ya high school kwa sababu eneo langu la Jimbo ni kubwa sana. Kutoka mwanzo wa jimbo mpaka mwisho wa jimbo ni kilomita 400. Kwa hiyo unaweza ukaona kabisa kwamba kila tarafa kuna haja ya kuwa na high school. Kwa hiyo watu wa Nguruka wako tayari kupokea high school kwenye Shule yao ya Nguruka Sekondari lakini pia Buhingu wako tayari kupokea high school kwenye Shule yao ya Buhingu. Naomba Mheshimiwa jambo hili unisadie.

Mheshimiwa Naibu Spika, liko jambo ambalo mimi ninaomba nilizungumze; ni jambo la kitaifa. Kwanza naomba nipongeze Serikali kwa kukubali kuwarudisha shuleni wanafunzi waliopata ujauzito; kwamba baada ya kuwa wamejifungua basi warudi kusoma na huku wakiendelea kunyonyesha. Hili ni jambo jema sana na naomba nikuhakikishie wananchi wamelifurahia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye eneo hili mimi ninaona bado kuna hatari kubwa sana, kwa sababu kwa taarifa ya mwaka jana, mimba za shuleni zilikuwa 8,000, ni nyingi sana! Kwa hiyo, Serikali lazima iweke mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba inapunguza hizi mimba shuleni. Lakini hili ambalo Serikali imelifanya la kuona namna ya kuwarudisha waliopata mimba, baada ya kujifungua warudi shuleni huku wakinyonyesha watoto wao. Mimi naona kama hili jambo litaongeza idadi ya mimba. Kwa sababu wale 8,000 walipata mimba lakini wakiamini kwamba hawawezi kwenda shuleni kwa sababu wamepata mimba. Sasa watakapokuwa wamepata mimba na wakarudi shuleni kusoma huku wakinyonyesha mimi ninaona kabisa kuna hatari ya mimba kuongezeka shuleni.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, kwa kuwa pia hata Kamati yangu imelizungumza hili na kuona, kwamba kuwe na elimu kwenye eneo lile la mimba shuleni. Kwa maana itapunguza sasa kile kitendo cha kuongeza mimba shuleni.

Mheshimiwa Waziri hili jambo usipoliangalia litaleta shida kwa sababu pamoja na kwamba wananchi wamefurahia lakini mimba zitakapoongezeka wananchi wataandama. Kwa hiyo itakuwa kashfa kwa Serikali kuona yenyewe imechochea mimba shuleni kwa sababu imeruhusu sasa watoto waliokuwa wamepata mimba wajifungue na warudi shuleni wakiendelea kunyonyesha watoto wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kitakachotokea mle darasani yawezekana ikawa ni darasa ambalo linafundisha wazazi waliojifungua. Kwa hiyo, naomba hili nizungumze kwa msisitizo. Nakumbuka hili jambo kuna kikao cha Bunge wakati fulani niliwahi kulizungumza, nadhani lilikuwa Bunge la mwezi wa tisa. Kwa kweli naomba nirudie ili kusudi lisije kuleta taharuki baadaye kwa wananchi wetu watakapokuja kuilaumu Serikali kuona kwamba yenyewe ndiyo imesababisha mimba za shuleni kuweza kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)