Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ally Anyigulile Jumbe (20 total)

MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mfumo huu wa Stakabadhi Ghalani umewafanya wananchi na wakulima wa kokoa wasipate pesa papo kwa papo kama ambavyo Serikali leo imejibu; na kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ni tofauti kabisa na uhalisia ulioko kule field, je, anachukua hatua gani kwa watu ambao wametoa taarifa ambazo sio sahihi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa zao la kokoa linalimwa na watu kwenye nyumba/kaya zao na siyo mashamba makubwa na wanatumia muda mwingi kukusanya hizo kokoa kidogo kidogo na pesa zinazolipwa zinachukua muda mrefu na kwamba makampuni yanayonunua yanaanza kwanza kukubaliana wao kwa wao pamoja na makato makubwa, je, Serikali inachukua hatua gani kudhibiti haya matatizo yaliyopo kwa wakulima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza anaposema taarifa tulizotoa sio sahihi; taarifa tulizotoa ni sahihi, wakulima wamelipwa kutokana na takwimu tulizonazo na uthibitisho tulionao. Kwa hiyo, kama ana kesi maalum ya mkulima ama wakulima ambao hawajalipwa atuletee hiyo kesi na tutaishughulikia kwa wakati na inavyostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba kupitia Bunge lako Wabunge wanapoinuka na kusema kwamba, kuna mkulima X hajalipwa na sisi Wizara tunapoomba kwamba, tuleteeni uthibitisho, tunaomba mtuletee uthibitisho, mjadala huu usiishie humu ndani. Mtuletee uthibitisho, ili tuweze ku- resolve tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, taarifa tulizotoa ni sahihi. Hoja iliyoko ya kwamba, mkulima anapovuna, anapokausha, anapopeleka kwenye chama cha msingi mpaka inapoenda kwenye chama kikuu ni vizuri tukaelewa kwamba, cocoa inakusanywa kidogokidogo; mkulima atavuna kilo moja, baada ya siku chache atavuna kilo kadhaa, baada ya siku chache atavuna kilo kadhaa atapeleka kwenye chama cha msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna hoja kwamba, tujadiliane kupunguza muda wa kutoka kwenye chama cha msingi kwenda kwenye mnada, lakini hatuwezi kurudisha mfumo ambao ni maarufu kama njemke ambao wakulima walikuwa wanafuatwa majumbani na wanakusanyiwa cocoa yao na wanapewa bei ndogo na walanguzi hao ndio wanapeleka kwenye mnada, hatutaruhusu huo mfumo. Kama kuna changamoto kwenye mfumo wa malipo, tuujadili huo mfumo wa malipo na kama Waheshimiwa wana maoni watuletee, lakini Wizara sasa hivi tunatengeneza utaratibu wa kuondoa mfumo wa kuhifadhi mazao ya cocoa kwenye maghala binafsi na yatatumika maghala ya Serikali. Tutaanza pia kuuzia katika AMCOS, badala ya kuleta kwenye chama kikuu cha ushirika, ili tuweze kupunguza time kati ya mnada na malipo ya mkulima. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hospitali ya Kyela jengo la mama na mtoto liliungua. Je, ni lini Serikali sasa itamalizia pesa zilizobaki kwa ajili ya jengo la mama na mtoto katika hospitali ya Kyela?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUNGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimhakikishie Mheshimiwa Jumbe kwamba hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ni moja ya hospitali ambazo nazifahamu sana kwa sababu nimekuwa mganga mkuu wa Kyela kwa zaidi ya miaka tis ana nimekuwa sehemu ya uendelezaji wa miundombinu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela. Ninafahamu kwamba ni kweli wodi ilipata ajali ya moto na Serikali imesha peleka fedha na kazi za ukarabati wa wodi ile zinaendela.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimhakikishie kwamba katika Mpango ujao tumetenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakamilisha ukarabati wa wodi ile iliyopata ajali ya moto ili iweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Jumbe kwamba jambo hilo linafanyiwa kazi na mara fedha zitakapopatikana basi ukamilishaji wa wodi ile utafanyika ili tuendelee kutoa huduma kama ambavyo tunatarajia.
MHE. ALLY A. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; Serikali kama kawaida imekuwa ikifanya kazi kubwa sana kwenye elimu. Sasa hivi imetokea wanafunzi wanaotoka kidato cha nne wanachaguliwa moja kwa moja kwenda kwenye vyuo.

Sasa nilitaka kuuliza na wengine hawana uwezo kabisa na wazazi wao wameshindwa kuwalipia na utakuta ana division one au two. Sasa nilitaka kuuliza je, Serikali inawasaidiaje hawa vijana ambao wanashindwa uwezo wa kwenda huko vyuoni kwa ajili ya kuwasaidia wafike huko vyuoni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimwa Naibu Spika, napenda kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jumbe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Jumbe anazungumza kwamba wapo wanafunzi ambao wanafaulu lakini nafasi za kujiunga kwenye elimu ya juu zimekuwa ni changamoto na suala kubwa hapa ni kuweza kufanya upanuzi. Nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Jumbe na Wabunge wote kwamba tumesaini sasa mkopo kutoka Benki ya Dunia katika mradi wetu wa HIT ambao zaidi ya dola za Kimarekani milioni 425,000 ambazo zinakwenda kufanya upanuzi mkubwa pamoja na ukarabati wa miundombinu katika vyuo vikuu. Tutakapofanya ukarabati huu tunaamini tutaongeza nafasi za udahili na kuondoa changamoto hii ya wanafunzi wengi ambao wamefaulu vizuri lakini kuachwa kwenye vyuo vyetu. Nafasi hizo zitakapoongezeka tunaamini wanafunzi hawa wote ambao watakaofaulu wataweza kupata nafasi ya kwenda kuingia katika vyuo vyetu, asante sana.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Leo ningekuwa CAG kwa majibu haya ningetoa hati hafifu. Haiwezekani leo tunazungumza mambo ya 2013 wakati aliyekuwa Waziri Mheshimiwa Mizengo Pinda mwaka tarehe 8 Januari, 2015 alisema kwamba sasa wataanza utaratibu wa kupeleka mgodi huu TANESCO na kupeleka kwa STAMICO, lakini kumekuwa na ahadi hizi nyingi zikiendelea. Wananchi wa Wilaya ya Kyela, Wilaya ya Rungwe na Ileje wanachotaka ni kujua tarehe mahsusi ambayo suala hili linaenda kutekelezeka, la kuanza mgodi hiyo ni. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, la pili, kumekuwa na matamko mengi ya malipo haya. Tarehe 29 Novemba, 2018 walisema STAMICO sasa imesha-save hela ya Serikali, lakini tarehe 12 Septemba aliyekuwa Naibu Waziri Mheshimiwa Nyongo alisema TRA wanawatafuta hawa TAN Power ambao walisema…

SPIKA: Sasa swali!

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ndiyo naomba nipate tarehe ya kulipwa ili na mimi nikienda Jimboni nikawaambie wananchi kwamba Serikali sasa inalipa pesa. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba jambo hili limekuwa ni la muda mrefu kama ambavyo tarehe ya kukabidhiwa mgodi kwenda Serikalini imekuwa ya mwaka 2013, lakini pia tujue kwamba uwekezaji katika mgodi ni uwekezaji unaohitaji fedha. Katika kipindi hiki ni kweli kwamba pia Shirika letu la STAMICO limekuwa likipitia maboresho makubwa ya kulipa uwezo wa kuendelea kufanya shughuli zake. Kwa hiyo, ahadi hizi ambazo zimekuwa ni za muda mrefu, tunapenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa jinsi ambavyo shirika limeboreshwa na kwa jinsi ambavyo Serikali imejitahidi kuwa inalipa mapunjo hasa ya muda mrefu, hatimaye tumewaelekeza Shirika letu la STAMICO pamoja na TANESCO kwamba hata sisi hatuko tayari kuendelea kuchukua fedheha ya kuambiwa tuna hati chafu, badala yake wafanye jitihada zinazowezekana ili waweze kupata mtaji na hatimaye mgodi wa Kyela uweze kufunguliwa.

Mheshimiwa Spika, kwa mustakabali huo, naendelea kuwaagiza STAMICO pamoja na TANESCO kwamba, wakatafute fedha na ndivyo tulivyoongea kwamba sasa ifikie mahali watafute fedha, kama ni kutenga bajeti, kama ni kwa ushirika na partners wafanye hivyo ili hatimaye jambo hili liweze kufikia mwisho. Nakushukuru sana.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya dawa yanayojitokeza katika zahanati zetu ni sawa na yanayojitokeza katika Zahanati za Ipinda, Kyela na hata pale mijini. Ni mpaka lini tutasubiri tatizo hili liishe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha; kwanza bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba lakini pili, imeendelea kuboresha sana upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vyetu. Ni kweli pamoja na maboresho haya bado kuna changamoto ya upatikanaji wa dawa katika baadhi ya vituo na halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo ambayo Serikali tumeyatoa, kwanza ni kuhakikisha watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wanatumia vizuri fedha zitokanazo na uchangiaji wa huduma za afya kwa maana ya cost sharing. Tumejifunza kwamba baadhi ya halmashauri hazitumii vizuri fedha za cost sharing na tumewapa maelekezo kuhakikisha angalau asilimia 50 hadi 60 ya fedha za uchangiaji zinakwenda kununua dawa, vitendanishi na vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika swali la msingi, Serikali imeendelea kuongeza bajeti na itaendelea kuboresha upatikanaji wa dawa kwa kuongeza bajeti na kusimamia matumizi bora ya dawa katika vituo vyetu. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kulifanyia kazi suala hilo. Pia niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu sisi ni Madiwani katika mabaraza yetu kufuatilia kwa karibu matumizi ya dawa katika vituo vyetu na kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha makusanyo yanakuwa bora zaidi.
MHE. ALLY A. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza naomba unipe nafasi pia nikushukuru wewe na Bunge hili tukufu kwa niaba ya Wananchi wa Kyela, pia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuhakikisha kwamba baadhi ya wananchi wanapata msaada hasa wale walioathirika na mafuriko. Naomba niseme ahsante sana kwa Mama yetu Rais wetu ambaye ndiyo anayeongoza nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kama ifuatavyo; nikweli kuna Scheme ambazo zimetajwa za Ngana na Makwale, hizi skimu zimechukuwa tumito tudogo na tuchache sana ambayo tuna maji machache.

Sasa naomba niulize Serikali je, wanampango gani wa kutumia Mito ya Mbaka, Rufirio na Kiwila, mbali na Songwe ambayo ina maji mengi na ya msimu wote ili kujenga mabwawa makubwa kama ilivyofanyika utafiti na JICA miaka 1969 mpaka 1970 ili pia tupunguze mafuriko?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kyela tunaelekea kupata mwekezaji mzuri ambaye yuko tayari kuendeleza zaidi ya hekari elfu 10 akishirikiana na wananchi, lakini pia yuko tayari kujenga kiwanda kikubwa ambacho kita-process mpunga. Je, Serikali itakuwa tayari kushirikiana na mwekezaji huyo na sisi kwa Pamoja? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili la mwekezaji, wala halihitaji majadiliano marefu, kama mwekezaji yupo na serious investors karibu Wizara ya Kilimo tukaenaye, tujadiliane naye tuone anahitaji msaada gani ili tuweze kusaidiana kuweza kufikia adhima ya kuwekeza na haya ni maelekezo ya Serikali wala hatutomsumbua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mito miwili aliyoitaja nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge; mfano maeneo yete yaliyokubwa na mafuriko sasa hivi kwa maana kuanzia Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo ya Kyela kwa maana ya Mkoa wa Mbeya na maeneo mengine, wataalamu wetu wa Wizara ya Kilimo wapo sasa hivi wameshakwenda kwa ajili ya kufanya tathimini na ingawa kuna stand ya JICA na zipo stand zingine ambazo zilifanywa katika baadhi ya maeneo kwenye nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wataalamu wa Wizara ya Kilimo wa Tume ya Umwagiliaji wana review stand zote zilizofanywa zamani ili kuangalia namna gani tunaweza kuziboresha na kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wengine wote kwamba maeneo yote potation yatafanyiwa kazi katika kipindi cha miaka hii mitano Inshallah!
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni barabara muhimu sana kwa ulinzi wa nchi yetu hasa kwa upande wa Tanzania na Malawi, pamoja na hayo kuna barabara muhimu sana ambayo kwa uchumi wa Kyela inafaa ijengwe mara moja.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini barabara ya Ibanda – Itungi – Poti itaanza kujengwa rasmi?

Swali la pili, wakati wa ujenzi wa barabara ya Kikusya – Matema kuna madaraja ya chuma yaliyokuwepo kwenye Mto Lufilyo Nambaka yalitolewa. Je, Mheshimiwa Waziri, kwa sababu ya uhaba wa madaraja na watu wanaotembea kilometa nyingi kufuata daraja lilipo, Serikali haioni kwamba ni muhimu sasa madaraja yale yarudishwe Kyela ili yapelekwe sehemu zenye uhitaji za Ilondo, Ipande na sehemu za pale Ngorwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Anyigulile Mlaghila, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ibanda – Itungi – Poti imetengewa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami na naamimi tayari maandalizi yako ili iweze kutangazwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Kyela waiamini Serikali na hata akienda kwenye vitabu vyetu vya bajeti tumeonesha fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili haya madaraja ambayo anayasema. Madaraja haya ya chuma ni madaraja ambayo yanatumika kwa ajili ya kutumika pale panapotokea dharura. Kwa hiyo, madaraja anayoyasema ni kweli yalikuwepo lakini yalishapelekwa Katavi kwa ajili ya koa changamoto ambayo ilitokea. Kwa hiyo, kupitia Bunge lako Tukufu nimuagize Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya aende akafanye tathmini halafu tuone kama tutapata madaraja sehemu nyingine tuweze kurejesha mawasiliano ili kuwapunguzia adha wananchi ambao wanakwenda mbali kwa ajili ya kupata huduma ya usafiri. Ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Swali langu pia lililenga hili ambalo limeulizwa na Mbunge wa Rungwe, lakini pia naomba basi niulize kwamba, kwa kuwa imekuwa ni tabia ya wakandarasi kuruka baadhi ya vitongoji, halafu wanapeleka sehemu ya mbele na vitongoji vingine ambavyo vimekatiwa miti yake havipewi. Je Serikali inasemaje kuhusu hili?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mlaghila kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na tumeshaongea naye kuhusu vijiji na vitongoji vilivyorukwa. Naomba pia nitumie nafasi kupitia Bunge lako Tukufu kuwakumbusha tu wakandarasi na tumetoa maelekezo haya mara kwa mara, kwamba mradi wa vijiji ambavyo tunakwenda kuutekeleza sasa ambao pia una miradi ya vitongoji na mitaa, hauzingatii na hautarajii kuruka kitongoji chochote.

Kwa hiyo niwakumbushe wakandarasi kutoruka sio kitongoji tu kutoruka kijiji, kitongoji, kaya na nyumba, haitegemei ni aina gani ya nyumba. Nashukuru.
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa sera yetu sasa itachukua muda kuihuisha mpaka mwaka 2022; na kwa kuwa mpaka sasa kuna miradi mingi sana ya maji inaendelea na kwa kuwa pamoja na Sera hii kuna uhitaji wa maji wa kila mwananchi anahitaji kiasi gani kwa siku. Je, miradi inayofuata kwa sasa, Serikali imejipangaje kuhakikisha inakuwa endelevu?

Mheshimiwa Spika, la pili, mradi mmojawapo ambao umeathirika sana kwa Wilaya ya Kyela na hii Sera ya Maji ya watu 250 kuchota kwenye kituo kimoja ni Mradi wa Ngana group. Serikali imejipangaje sasa kuhakikisha mradi huu unafufuliwa na unakuwa katika viwango vya sasa ili kukidhi matarajio ya wana Kyela? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Mlaghila, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa miradi ambayo inaendelea sasa hivi ni miradi endelevu na tayari tunajitahidi kuhakikisha kuona kwamba tunapata vifaa vya kufanya uchunguzi kabla ya kuingia kwenye miradi na tumshukuru kabisa kwa kipekee Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan, kwa kupitia fedha ambazo tumepewa tayari tumeagiza mitambo saba kwa ajili ya kuchunguza maeneo ambayo yatatuletea vyanzo endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa Mradi wa Ngana Group tayari umeshafufuliwa, wiki hii fedha zaidi ya shilingi milioni 500 tunaelekeza huko, ili kuona kwamba shughuli za awali zinaanza kutekelezwa. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimwulize swali la nyongeza Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amefanya kazi kubwa sana, lakini ameendelea kutoa hadithi zile zile. Sasa naomba tujue, ni lini mgodi huu utaanza kuzalisha ile mass production? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge. Bahati njema yeye mwenyewe katika kipindi kilichopita alitupa hati ya mashaka. Sasa hivi nataka nimwambie hati ile aiondoe kwa sababu tayari uzalishaji umeshaanza.

Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa, itakapofika mwezi Machi mwaka huu 2022 uzalishaji wa mass production wa tani 50,000 kwa mwezi utaanza mara moja.

Mheshimiwa Spika, vile vile underground mining kama nilivyokukwa nikijibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda, tayari tumeshaijenga na kiberenge kinapita na uzalishaji unaanza. Ndani ya mwezi huu tunaanza kuzalisha kwenye mradi wa Kiwira tani 5,000.

Mheshimiwa Spika, Block E na yenyewe tumeanza kuanzisha open pit kwa ajili ya kuchimba. Mgodi huu ulisimama kwa muda mrefu toka mwaka 2008. Ni Awamu ya Sita ya mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeweka msukumo mkubwa ili mgodi huu uanze na wateja wako wengi, tayari wanapita. Hata barabara ile Mheshimiwa Mbunge alikuwa analalamikia tayari tumeshaijenga. Sasa hivi tunakamilisha lile Daraja la Mwalisi watu waanze kupita pale; na wananchi wa maeneo yale wananufaika na uwepo wa mradi huu. Ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa Mto Kiwira unapita maene mengi sana ya Wilaya ya Kyela ikiwemo Vijiji vya Lema, Mwalisi, mpaka Bujonde. Na kwa kuwa mto huo umelalamikiwa na wananchi wa maeneo hayo kuwa na uchafuzi mkubwa ambapo inafikia hatua mto unanuka na unakuwa na rangi ya damu.

Je, ni lini Serikali itaunda Tume Maalum kufanya utafiti wa nini kinasababisha maji hayo yawe machafu?

Mheshimiwa Spika, mbili, kwa kuwa wananchi wengi wa eneo hilo baada ya kukosa maji ya Ngana wanatumia kwa ajili ya kunywa na kuoga. Je, ni lini Serikali sasa itaanza ujenzi wa mradi wa Ngana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Ally amekuwa mfuatiliaji mzuri, amekuwa anakwenda zaidi ya uhitaji wa kupata maji yakiwa bombani lakini pia amekuwa akizingatia suala la usalama.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na bonde hili maji haya yanapochafuka, Mto Kiwira ni Mto ambao tunautumia kwa miradi mingi, naomba kutumia Bunge lako Tukufu kuagiza Bonde husika lifanye kazi kadri ambavyo inatakiwa kisheria. Vilevile Wizara tutaendelea kusimamia. Tayari Mheshimiwa Waziri amekuwa akitoa maagizo kadhaa kwa Mabonde yote kuhakikisha shughuli za maji kuwa salama yafanye usimamizi unaotakiwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la lini ujenzi wa Ngana utaanza, kwa furaha kubwa ninapenda kukuarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu tayari tumeshatangaza na hivi karibuni kabla yam waka huu wa fedha kuisha tutapata Mkandarasi na lazima kasi zije zianze kwa kasi kwa sababu tunafahamu umuhimu wake kulingana na jiografia ya eneo hilo. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, ni lini Mkandarasi wa kujenga Skimu ya Umwagiliaji ya Makwale Wilayani Kyela kutumia Mto Rufilio ataanza kazi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Jumbe, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, maelekezo ambayo tuliyatoa kwa Wakandarasi wote wale ambao walisaini mikataba wakati wa sherehe ya Nanenane pale Mbeya ni kwamba wanapaswa kuwa site kuanzia tarehe 15. Lakini tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa hoja yake mahsusi, basi tutahakikisha kwamba tunamharakisha Mkandarasi huyo aende kuanza kazi mapema kama ambavyo maelekezo yalitoka Wizarani.
MHE. ALLY M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ni miezi mitatu sasa katika Wilaya ya Kyela, umeme haupatikani mchana. Je, ni lini wananchi wa Kyela watajisikia kwamba nao wana haki ya kupata umeme asubuhi na mchana?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Jumbe, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba baada ya hapa nikafuatilie ili kufahamu kwa nini Mheshimiwa Mbunge katika jimbo lake kwa miezi mitatu hakupatikani umeme mchana. Ninachofahamu ni kwamba kwa sababu ya upungufu wa umeme kumekuwa na kupungua kwa umeme kwenye baadhi ya maeneo, lakini jambo la kwamba miezi mitatu mchana wote hakuna, hilo ni jambo la kufuatilia, halafu tutashirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kutatua changamoto hiyo.
MHE. ALLY A. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii. Swali la kwanza; kwa kuwa Kyela ni sehemu ambayo ina mvua nyingi sana na huwa inakumbwa na mafuriko kwa kipindi kila mwaka. Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta fedha ambazo zimekosekana kwa muda mrefu kwa maendeleo ya barabara Wilayani Kyela?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa inajulikana barabara haziwezi kudumu kwenye mafuriko hasa hizi za changarawe na udongo. Je, Serikali imewahi kufanya utafiti wa kutafuta namna nyingine ya ujenzi wa barabara kwa mfano, kutumia enzymes katika kitengo chake cha utafiti hapo TARURA?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kupeleka fedha kwa ajili ya barabara na nimwondoe shaka tu. Bahati nzuri Serikali sasa hivi imeongeza bajeti yake na sisi tumekuwa tukitekeleza vya kutosha. Kwa hiyo, hilo aondoe shaka kabisa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu tafiti katika maeneo ambayo barabara hazidumu kutokana na mvua nyingi kama ilivyo Kyela, utafiti huo umefanyika na moja ya mipango yetu ni kuja na majibu ambayo yatasaidia barabara za maeneo hayo ziweze kupitika muda wote. Kwa hiyo, Serikali ipo kazini na inafanya hii kazi kwa umakini kabisa ili kuwasaidia wananchi wake.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwenye Mradi wa Songwe River Basin kuna package inayounganisha eneo la umwagiliaji la hekta zaidi ya 3,500 pale Kyela.

Je, Serikali imefikia wapi kuungana na Malawi kuanza kutekeleza mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema muuliza swali, Mheshimiwa Mbunge, amelitaja Bonde la Mto Songwe ambalo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huu. Kazi ambayo Wizara inafanya hivi sasa ni kuhakikisha tunaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu wa haya mambonde yote, lengo letu kubwa ni kuwa na miradi mikubwa ambayo itahusisha miradi ambayo pia Mheshimiwa Mbunge ameitaja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mwaka huu wa fedha tayari tumeshawapa kazi washauri elekezi kwa ajili ya kuanza kazi hii na tunategemea kwamba mabonde yote yale 22 kuanzia Bonde la Ziwa Victoria, Malagarasi, Manonga, Wembele, Bonde la Ruvuma, Bonde la Rufiji, Bonde la Mto Songwe, Ifakara Idete, Kilombero, Mkomazi, haya yote yapo katika mpango na yatakwenda kukata kiu ya wakulima wa Tanzania. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuuliza ni lini uwanja wa Mbeya utaanza kutumika usiku na mchana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyoongea uwekaji wa taa kwa uwanja wa Mbeya ambao ni Songwe airport upo pengine kwenye asilimia 95 uwekaji wa taa, runway imeshakamilika zaidi ya mita 3000, uzio na sasa hivi tunakamilisha pia jengo la kisasa la abiria. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba uwanja huu utaanza kutumika, taa zimeshajengwa na utaanza kupokea ndege usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba uwanja huo unatumika kwa asilimia 100, ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, je ni lini Serikali itaanza rasmi ujenzi wa barabara ya Katumba - Songwe – Kasumuru – Ngana - Ileje?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara hiyo ilishatangazwa na tender zimeshafunguliwa, kwa hiyo muda wowote itaanza kujengwa baada ya kumpata mkandarasi, ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Ikombe, tangu kuumbwa kwa dunia hii hawajawahi kuona gari. Zimebaki kilomita moja na nusu, ili barabara ifunguke mpaka Kijiji cha Ikombe, na mwezi wa kumi tuliambiwa kwamba mkandarasi yuko tayari, amepatikana.

Je, Mheshimiwa Waziri anajua kwamba mkandarasi mpaka sasa hivi hayuko site?

Mheshimiwa Spika, mbili, barabara ya Ngamanga – Lusungo Matema inaenda moja kwa moja Ikombe, pale kuna daraja la bilioni 4.50 lakini eneo la Ngolwa halina daraja. Je, unaonaje sasa ni wakati sahihi wa kujenga daraja la Ngorwa, ili barabara ipitike kirahisi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFRY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya mheshimiwa Ally Anyingulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi ambao hawajaona gari nimuhakikishie kwamba barabara hiyo tunaifikisha kwenye hicho kijiji ili wananchi hao waweze kuiona gari katika maisha yao.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba nichukue nafasi hii kumuagiza Meneja wa Mkoa wa Mbeya, ahakikishe kwamba mkandarasi anarudi site na anafanya kazi ambayo anatakiwa kuifanya. Lakini kuhusu daraja hili ambalo amelisema, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali italijenga hili daraja ili paweze kuwa na mawasiliano ambayo yamekosekana kwa sasa. Ahsante.
MHE. ALLY A. J. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ETBICO ni Kampuni ambayo inasambaza umeme Mkoani Mbeya, wanaenda vijijini, kwa mfano Kijiji cha Bukunelo, Kijiji cha Ikama wanasema wamewasha umeme na taarifa Serikalini ni kwamba imewasha umeme, wakati huo wamewasha transformer zinaunguruma na umeme wenyewe kwa wananchi haujafika, je hiyo ni sahihi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Ally Jumbe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuwasha umeme kwa mwananchi ni kumwashia katika nyumba yake na eneo lake analohitaji umeme. Kwa hiyo, kama wanasema wamewasha kwenye transformer hiyo sio sawa na tutalifuatilia kuhakikisha kwamba umeme unawafikia wananchi kwa sababu ndio wanaouhitaji. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Ikombe ni kijiji ambacho kiko pembezoni sana na ni kisiwa ambacho hakifikiwi kirahisi. Leo hii tunapouliza hili swali wananchi wa Ikombe wamewatuma viongozi wao waje washuhudie majibu haya ya Serikali, wako hapa leo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ETDCO ambao wanasambaza umeme wa REA walianza kazi hii Agosti, 2021 na wamefikia vijiji 21 tu na vijiji vilivyobaki ni 14. Na katika vijiji hivyo 14 bado hata nyaya hazijavutwa wala hakujatokea uwezekano wa kupeleka nguzo na mkataba unaisha ndani ya siku kumi zijazo, swali la kwanza: -

Je, sasa Serikali haioni umuhimu mkubwa wa kushirikiana na TANESCO ili kwa Kyela vijiji hivyo viishe mapema?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni maajabu gani yatatokea kufanikisha ndani ya siku kumi mkataba huu uendelee ufike mpaka watakapofikisha hapo Juni pale Ikombe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa spirit ya kutotaja kumuwakilisha Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya muda naomba niendelee.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu mawali ya nyongeza la Mheshimiwa Ally Anyigulile kwa ujumla wake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna mikataba ambayo muda wake utaisha kabla kazi hazijakamilika, lakini nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba vijiji vyote vinapata umeme. Na tunachokifanya ni kukabana na wakandarasi wote wanaopeleka miradi yetu ya umeme kwenye maeneo mbalimbali kuhakikisha wanamaliza kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, lakini sababu nyingine moja inayofanya kazi izidi muda wa mkataba wa awali ni kuongezeka kwa hizo kilometa mbili ambazo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa pesa ya nyongeza kwa ajili ya kuongeza scope. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Ally kwamba kama tulivyosema kabla ya mwezi Juni hicho kijiji kitakuwa kimepata umeme na wananchi wataweza kuutumia katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, na kwa mkandarasi ETDCO yupo zaidi ya asilimia 60 na vijiji 14 vilivyobaki vitakamilika katika huu muda ambao tumejipangia kwa spidi mpya ambayo tuko nayo kwa sasa. Ahsante.

Whoops, looks like something went wrong.