Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ally Anyigulile Jumbe (6 total)

MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. ALLY A. MLAGHILA aliuliza: -

Suluhisho la tatizo la maji katika Wilaya ya Kyela ni kutumia chanzo cha Ziwa Nyasa kama ilivyoelezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020.

Je, ni lini sasa mradi huo utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Mlaghila, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua tatizo la huduma ya maji linaloikabili Wilaya ya Kyela. Katika kuhakikisha wananchi wa Wilaya hiyo wanapata huduma ya majisafi, salama na ya kutosha, Serikali ina mpango wa muda mfupi na wa muda mrefu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango wa muda mfupi Serikali imeendelea na ukarabati wa miradi ambapo baadhi ya miradi iliyokarabatiwa tayari inatoa huduma ya maji ukiwemo mradi wa maji wa Makwale Group ambao unahudumia vijiji viwili vya Ibale na Makwale, Mradi wa maji wa Matema unaohudumia kijiji cha Matema (kitongoji cha Ibungu) na Kijiji cha Ikombe (Kitongoji cha Lyulilo) na mradi wa maji wa Lubaga ulioharibika muda mrefu umekarabatiwa na wananchi wanapata maji kwenye vituo 15 vya kuchotea maji. Aidha, kupitia bajeti ya mwaka 2020/ 2021 Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji wa Mababu, Kisyosyo, Katumbasongwe, mradi wa Kapapa kwenda kijiji cha Mwaigoga na mradi wa Sinyanga Group.

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za muda mrefu, Serikali imepanga kutumia Ziwa Nyasa kama chanzo cha kudumu cha kusambaza maji kwa wananchi waliopo Wilayani Kyela pamoja na maeneo ya jirani. Hadi sasa timu ya kitaifa ya wataalam imefanya upembuzi wa awali kwa kufika Kyela na kubaini eneo la kijiji cha Ikombe kilichopo katika mwambao wa Ziwa Nyasa kuwa linafaa kujengwa chanzo cha maji. Mradi huu unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2021/2022.
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA Aliuliza:-

Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa zao la kokoa haujamnufaisha mkulima:-

Je, ni lini sasa mfumo huo utabadilishwa ili kukidhi lengo la ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Mlaghila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani ni utaratibu unaowezesha biashara kufanyika kwa kutumia bidhaa ambazo zinakuwa zimehifadhiwa katika ghala lililopewa leseni kwa mujibu wa sheria kifungu cha 5(a) cha sheria ya mwaka 2005 na marekebisho ya mwaka 2015.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mfumo huu, mmiliki wa bidhaa anapewa stakabadhi ambayo inathibitisha ubora, uzito, idadi ya vifungashio na umiliki mahsusi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani kwa zao la kokoa umesaidia kuimarisha bei ya zao la kokoa kutoka wastani wa Sh.3,000 kwa kilo katika msimu wa 2017 hadi kufikia Sh.5,011 katika msimu wa 2019/ 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani umesaidia kuimarisha na kuweza kugundua bei halisi na hivyo kumpa mkulima bei nzuri za zao hilo. Pia mfumo huu umeimarisha upatikanaji wa takwimu za uzalishaji na umesaidia ukusanyaji wa ushuru halali kwa Halmashauri za Kyela, Rungwe na Busokelo unaotokana na zao la kokoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika msimu wa 2018/2019 jumla ya tani 7,532 ziliuzwa ambapo jumla ya Sh.33,697,643,289.75 zilipatikana na kulipwa kwa wakulima na Sh.1,033,098,535.20 zilipatikana ikiwa ni ushuru kwa Halmashauri zote tatu. Katika msimu 2019/2020 jumla ya tani 9,483 ziliuzwa na wakulima kupata jumla ya Sh.45.721 na Halmashauri kujipatia jumla ya shilingi bilioni 1.367. Hadi kufikia tarehe 21 Januari 2021, jumla ya kokoa zilizouzwa ni tani 7,000 na kiasi cha shilingi bilioni 33 zimelipwa kwa wakulima na Halmashauri ya Rungwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kusimamia ubora wa kokoa kupitia Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani na hivyo ubora wa zao la kokoa umeongezeka kwa kuwa katika mfumo huu kokoa inaandaliwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na matakwa ya walaji.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itaufufua Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira?

(b) Je, ni lini baadhi ya waliokuwa wafanyakazi wa Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira watalipwa stahiki zao baada ya mgodi huo kufungwa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu maswali ya Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Jimbo la Kyela, yenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, mgodi wa makaa ya Mawe wa Kiwira ulikabidhiwa Serikalini kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mwaka 2013 kwa lengo la kuuendeleza. STAMICO kwa kushirikiana na TANESCO wanaendelea na mpango wa pamoja wa muda mrefu wa kuanzisha mradi wa kuzalisha umeme zaidi ya megawatt 200 utakaotumia makaa ya mawe yatakayozalishwa katika mgodi huo. Makubaliano ya ushirikiano baina ya STAMICO na TANESCO yako hatua za mwisho kabla ya kuwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kisha kusainiwa.

Mheshimiwa Spika, tayari timu ya wataalam wa STAMICO na TANESCO imetembelea eneo la mradi kwa lengo la kutambua mahitaji halisi ya uendelezaji wa mradi huo na STAMICO imeanza kufanya ukarabati wa miundombinu ya mgodi wa chini ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uzalishaji mkubwa kwa ajili ya mahitaji ya mitambo ya kuzalisha umeme. Aidha, kutokana na ukubwa wa mradi, Mashirika haya yanaendelea na jitihada za kutafuta fedha na uwekezaji kupitia wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na kuihusisha Serikali yenyewe kuona uwezekano wa kutengewa sehemu ya bajeti kwa ajili ya uwekezaji huo.

(b) Mheshimiwa Spika, kipindi ambacho mgodi unakabidhiwa kwa STAMICO kulikuwa na malimbikizo ya madeni yanayofikia shilingi bilioni 1.02 ikiwa ni stahiki na mapunjo ya wafanyakazi takriban 893 waliopunguzwa. Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na shirika tayari imehakiki deni hilo kwa mara nyingine mwezi Juni, 2019 na taratibu za ulipwaji wa madeni hayo zinaratibiwa na Hazina. Nakushukuru.
MHE. ALLY A. MLAGHILA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia Mto Songwe, Kiwira, Mbaka na Lufilyo ili kuongeza uzalishaji wa mpunga na kukuza uchumi wa nchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Mlaghila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji pamoja na fursa zilizopo katika Bonde la Mto Songwe pamoja na mabonde ya Mito Kiwira, Mbaka na Lufilyo, Serikali ilitekeleza miradi mbalimbali katika mabonde hayo. Katika Wilaya ya Kyela, kupitia Mpango wa Kilimo awamu ya kwanza (ASDP I), Serikali ilijenga Maghala mawili ya kuhifadhia mpunga katika skimu za Makwale na Ngana. Aidha, wakulima walipata mafunzo ya uendeshaji wa skimu, kilimo chenye tija na masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imekamilisha ujenzi wa Skimu ya Mbaka iliyogharimu Sh.358,877,336.48. Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na Uchimbaji wa mfereji mkuu mita 1,900; Ujenzi wa tuta la bwawa (formation of embarkment) urefu wa mita 450 na usakafiaji wa mfereji mkuu kwa zege mita 1,355.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina Mpango wa kuendeleza hekta 3,005 za umwagiliaji katika Bonde la Mto Songwe kwa ubia baina ya Serikali ya Tanzania na Malawi chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bonde la Mto Songwe. Aidha, Serikali itaendelea na juhudi za kutafuta fedha ili kuendelea na uendelezaji wa mabonde hayo pamoja na mabonde mengine nchini kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza: -

Je, ni lini barabara ya kutoka Katumbasongwe hadi Ileje kilometa 90.7 itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Mlaghila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Katumbasongwe – Ileje ni barabara ya Mkoa yenye urefu wa kilometa 114.51 inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Songwe kupitia Wilaya ya Kyela na Wilaya ya Ileje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Katumbasongwe - Kasumulu – Ngana – Ileje ipo katika taratibu za kumpata Mhandisi Mshauri kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina taratibu za ujenzi zitaanza. Aidha, Serikali inaendelea kuihudumia barabara hii kwa kuifanyia matengenezo mbalimbali ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka wakati taratibu za ujenzi wa kiwango cha lami zikiendelea. Katika mwaka wa fedha huu wa 2021/ 22 barabara hii imetengewa Shilingi milioni 141.45 za matengenezo. Ahsante.
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itahuisha Sera ya Maji ili iendane na wakati kwa kukidhi mahitaji halisi kwani kwa sasa haiendani na viwango vya kimataifa na imepitwa na wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Maji ndiyo mwongozo unaotumika katika kutekeleza jukumu la Serikali la kuhifadhi na kutunza vyanzo vya maji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. Lengo la Sera ya Maji ya mwaka 2002, ilikuwa ni kuweka mfumo madhubuti na endelevu wa kuendeleza na kusimamia kikamilifu rasilimali za maji. Kupitia Sera hii, umekuwepo ushirikishwaji wa walengwa wa huduma ya maji katika hatua zote za utekelezaji, uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/ 2021, Serikali ilianza utaratibu wa kuhuisha Sera ya Maji hiyo ambayo imetekelezwa kwa takribani miaka 19 ili iweze kukidhi mahitaji ya Mipango iliyopo ambayo ni; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Awamu ya Tatu 2021 – 2026; Malengo ya Maendeleo Endelevu 2015 – 2030; na Mageuzi ya Viwanda Awamu Nne (Fourth Industrial Revolution).

Mheshimiwa Spika, matarajio ni kukamilisha hatua zote ifikapo mwezi Juni, 2022 na Sera mpya ya Maji ianze kutumika ikianzia mahitaji halisi na kufikia malengo ya Uchumi wa Kati na Maendeleo ya nchi yetu kwa ujumla.