Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo (10 total)

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Wizara, ninayo maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, wakati wananchi wa Muleba wakisubiria hizi hatua ambazo Wizara inazichukua, je, Serikali iko tayari kuiongezea nguvu Ofisi ya TANESCO iliyopo kwa sasa kwa kuiongezea wafanyakazi na vitendea kazi ili wakati tunaendelea kusubiria iendelee kutoa huduma stahiki kwa wananchi wa Wilaya ya Muleba? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wilaya ya Muleba inavyo visiwa 39 na kati ya hivyo, visiwa 25 vinakaliwa na wavuvi ambao wanachangia pato la taifa. Je, Wizara na Serikali ni lini itavipelekea umeme wa uhakika na wa bei nafuu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TANESCO imeendelea kutoa huduma kwa wananchi na kuhakikisha kwamba huduma ya umeme inapatikana kwa uhakika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini kwamba tutaendelea kupeleka huduma ya umeme kwa wananchi na kuhakikisha kwamba ofisi ya TANESCO Muleba lakini na maeneo mengine yote nchini zinafanya kazi vizuri kabisa. Serikali tayari imeshaongeza nguvu kazi katika maeneo mbalimbali kwa kupeleka watumishi na vifaa mbalimbali ikiwemo vitendea kazi na magari. Tunaahidi kwamba tutaendelea kuboresha utendaji katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, kama nilivyokuwa nimetangulia kusema kwamba miradi inayopeleka umeme visiwani ni miradi inayoitwa off grid, maeneo ambapo Gridi ya Taifa haijafika na Muleba ni mojawapo ya maeneo ambayo ina visiwa vingi vinavyokaliwa na watu vinavyohitaji kupata huduma ya umeme. Tayari wako watu ambao walikuwa wanapeleka umeme huko ikiwemo kampuni ya JUMEME lakini gharama yake ilikuwa ni kubwa na Serikali ilitoa maelekezo kwamba gharama hiyo ya unit 1 kwa Sh.3,500 ishuke na kufikia shilingi
100. Maelekezo hayo tayari yameshaanza kutekelezwa. Kama bado kuna tatizo katika maeneo hayo basi tunaomba taarifa hiyo itolewa ofisini ili tuendelee kusimamia vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Serikali inao mpango wa kufikisha umeme wa TANESCO katika maeneo hayo kwa kadri bajeti itakavyoruhusu au kuweza kusimamia ile miradi ili iweze kutoa umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu kwa wananchi wote wanaoishi visiwani.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi wa maji wa Wilaya ya Muleba ambao unalenga kusaidia kata sita ambao umefanyiwa usanifu tangu mwaka 2018. Je, Wizara itaujenga lini na utakamilika lini kwa ajili ya kuwahudumia wakazi wa Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daktari, Mbunge kutoka Muleba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ambao usanifu wake umekamilika nao tayari Wizara tunaendelea na michakato kuona kwamba mradi huu tunakuja kuutekeleza ndani ya wakati.

Waheshimiwa Wabunge pale tunaposema kwamba, maji ni uhai, Wizara tunasimamia kuhakikisha kuona kwamba, wananchi wote wanaenda kupata maji safi na salama ya kutosheleza kwa lengo la kulinda uhai wa wananchi. Hivyo, Mheshimiwa Daktari nikuhakikishie kwamba, namna usanifu umekwenda vizuri na utekelezaji wake nao unakuja vizuri namna hiyo.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa lengo la Serikali ni kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 561,383 ya mwaka 2020 hadi kufikia hekta 1,200,000. Je, Serikali haioni busara kuhakikisha kwamba hii miradi ambayo imeshaanza badala ya kukimbilia kuanzisha miradi mipya tuhakikishe inakamilishwa ili wananchi waweze kuzalisha kwa wingi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mkoa wa Kagera kwa historia yake na jiografia yake ni Mkoa pekee ambao unapakana na nchi nne na nchi hizo nne zina uhaba mkubwa wa ardhi na hivyo uhaba mkubwa wa chakula. Je, Serikali haioni busara kuendeleza hili bonde kuhakikisha kwamba Mkoa wa Kagera sasa unakuwa soko la chakula kwa hizi nchi ambazo zinapakana na Mkoa huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Kikoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kama Wizara priority yetu ya kwanza sasa hivi tunachokifanya na Waheshimiwa Wabunge tutakapokuja kwenye bajeti wataona, ni kufanya tathmini na kukamilisha miradi ya umwagiliaji na tathmini tunazofanya ni za aina mbili; moja kuangalia efficiency ya miradi ya umwagiliaji iliyopo sasa hivi kama inafanya kazi kwa kiwango ambacho kinatarajiwa na kufanya marekebisho pale ambapo tunahitaji kufanya marekebisho. Pia kukamilisha miradi ya umwagiliaji ambayo tumeshaianza. Hatutakuja na mradi mpya wa umwagiliaji isipokuwa kukamilisha miradi tuliyoianza.

Mheshimiwa Naibu Spika, priority ya tatu ni kuwekeza umwagiliaji katika uzalishaji wa mbegu, Serikali ina mashamba 13 ambayo hayana mifumo ya umwagiliaji, mashamba haya 13 ndiyo tutakayoyapa kipaumbele katika bajeti ya mwaka kesho kuwekeza fedha ili yaweze kufanya kazi yote at optimal level ili kuweza kuzalisha mbegu bora na kwa wakati na kuondokana na tatizo la wakulima kutokupata mbegu za uhakika na kuyaacha mashamba idle ambayo hayatumiki. Kwa hiyo hivi ndiyo vipaumbele. Niseme tu ndani ya Bunge kwmaba kipaumbele chetu ni kukamilisha hiyo miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Mto Ngono na umuhimu wa Mkoa wa Kagera, kwetu sisi kama Wizara ya Kilimo na Serikali Mkoa wa Kagera ni moja kati ya mikoa ambayo tunaipa kipaumbele sana na ndiyo tutakapoelekeza nguvu zetu katika kipindi cha miaka mitano. Sababu ya kufanya hivi, mkoa huu strategically umeungana na nchi kama alivyozitaja nne, lakini vile vile ni lango kubwa la kuuza mazao katika nchi ya South Sudan. Kwa hiyo Mto Ngono tutaupa priority kama tulivyosema katika jibu letu la msingi kwamba tunatafuta fedha na tutawekeza katika hizo hekta 11,700 ili waweze kuzalisha mwaka mzima. (Makofi)
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Pamoja na nia njema ya Serikali yetu kutoa tiba bure kwa wazee wetu, lakini zoezi zima limegubikwa na ukiritimba wa kutoa tiba kwa wazee wetu.

Je, Serikali haioni busara kuoanisha vitambulisho hivi vinavyotolewa kwa wazee na Bima ya Afya ili wazee wetu wapate tiba stahiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme, Serikali imeendelea kuhakikisha inapunguza changamoto ambazo Mheshimiwa anaziita ukiritimba wa Matibabu kwa Wazee Bila Malipo na ndiyo maana tumeainisha utaratibu wa kuainisha, kuwatambua wazee wetu na kuwapa vitambulisho. Hiyo ni sehemu ya jitihada ya Serikali kuhakikisha ule ukiritimba unapungua na kuwawezesha wazee wetu kupata matibabu bila malipo na bila changamoto yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupokea wazo lake la kuunganisha vitambulisho pamoja na sehemu ya matibabu kwa wazee ili Serikali iweze kulifanyia tathmini na kuona uwezekano wa kufanya hivyo au uwezekano wa kuendelea kuboresha utaratibu uliopo ili tuweze kuboresha huduma.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nilitaka kuongeza kwenye swali la Dkt. Kikoyo kwenye suala la ku-link huduma za matibabu kwa wazee na Bima ya Afya. Jambo moja ambalo lilituchelewesha labda kuleta kwenye Bunge lako Muswada wa Bima ya Afya kwa wote ilikuwa ni kuweka utaratibu kama huo ambao ukishafanya Bima ya Afya ni compulsory, maana yake lazima Serikali ije na utaratibu wa kuona ni jinsi gani Bima za Afya zitapatikana kwa watu hao kama wazee, akina mama wajawazito pamoja na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, swali la Dkt. Kikoyo ni zuri. Pale ambapo Serikali italeta Muswaada wa Bima ya Afya, pia itaweka sasa utaratibu ambao utaondoa hizi changamoto za matibabu bure kwa wazee.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Dkt. Kikoyo kwamba tukimaliza, nadhani tutakuwa tumepata mwarobaini wa tatizo hili. (Makofi)
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Lakini ninalo swali moja tu la nyongeza. Kutokana na uhaba mkubwa wa maji katika Wilaya ya Muleba na jiografia ya Wilaya ya Muleba inapakana na Ziwa Victoria. Serikali inao mpango wowote wa kutumia Ziwa Victoria kuvuta maji kwa ajili ya Wilaya ya Muleba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mhehsmiwa Naibu Spika, Mradi wa Ziwa Victoria ni mradi wa kimkakati na ni mradi ambao tunautarajia uhudumie maeneo mengi sana kwasababu ni mradi unaopita katika majimbo mengi na mikoa mbalimbali. Hivyo niweze kumwambia Mhehimiwa Mbunge kwamba maeneo yake ambayo bomba hili kubwa litakuwa likipita basi na yeye atanufaika katika vijiji vile ambavyo viko kilometa 12 kutoka kwenye bomba kwa pande zote kulia na kushoto.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipatia nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Muleba iko pembezoni mwa Ziwa Victoria, lakini inalo tatizo kubwa la uhaba wa maji na tunao mradi mkubwa ambao usanifu na upembuzi yakinifu umekamilika.

Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwa ajili ya kata sita za Wilaya ya Muleba; Kata ya Gwanseri, Kata ya Muleba Mjini, Kata ya Magata Karutanga, Kikuku, Kagoma na Buleza?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Muleba kwa namna bora na nzuri ambayo kwa kufuatilia wananchi wake waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa ambalo sisi kama Wizara na Bunge lako tukufu, sisi kama Wizara ya Maji tumesema hatuna sababu tena ya Watanzania kulalamika suala la maji. Mwenyezi Mungu ametupa rasilimali toshelevu, tuna rasilimali ya maji mita za ujazo zaidi ya bilioni 126. Tuna mita za ujazo bilioni 105 juu ya ardhi ikiwemo mito pamoja na mabonde na bilioni 21 ambayo iliyokuwa chini ya ardhi.

Kwa hiyo, mkakati ambao tumeuweka sisi kama Wizara na katika bajeti yetu kutumia maziwa, rasilimali toshelevu, kuhakikisha kwamba tunatatua tatizo la maji na moja ya maeneo ambayo ya kipaumbele ni vijiji ambavyo vipo kandokando ya mito ama maziwa. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi ni Wizara ya Maji si Wizara ya ukame. Tunakwenda kutatua tatizo la maji kwa wananchi wako, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Mkoa wa Kagera kwa muda mrefu kumekuwa na uwanja wetu wa ndege wa kimataifa Omukajunguti.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua ni lini uwanja huu wa Omukajunguzi utajengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni kuboresha uwanja wa ndege wa Bukoba, uwanja wa kimataifa na kwenye bajeti ya mwaka ambayo imepitishwa mwezi uliopita tarehe 27 na tarehe 28. Uwanja ule tunatarajia kujenga jengo la abiria maarufu kama VIP, lakini pia na kuongeza runway ili ndege nyingi kubwa ziweze kutoa katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka huu wa fedha Mheshimiwa Mbunge watu wa Bukoba na maeneo ya jirani muwe na Amani tunajenga uwanja ule jengo la abiria maarufu lakini pia na run way utapata usafiri.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Tume ya Ushindani, kama zilivyo mamlaka zote za udhibiti hapa nchini, zina mamlaka ya kimahakama quasi- judicial organs. Je, Serikali haioni kuunganisha ushindani na kumlinda mtumiaji zinafifisha dhana nzima ya ushindani na inafifisha dhana nzima ya kumlinda mtumiaji wa Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Dhana ya mtumiaji hapa nchini inaakisiwa kwenye sheria mbalimbali ambazo hazina dhana nzima ya kumlinsda mtumiaji na kuakisi haki nane za mtumiaji kama zilizvyoainishwa na Umoja wa Mataifa. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kutunga sheria, a standalone law ya kumlinda mtumiaji wa Kitanzania?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli FCC au Tume ya Ushindani inasimama kama tume ambayo inahusika kama ya kimahakama, kwa maana ya quasi-judicial organ na ndiyo maana katika majukumu yake yale mawili ya kulinda ushindani pamoja na ya kumlinda mlaji tumeamua sasa ile National Consumer Advocacy Council ambayo ilikuwa ni sehemu, kama section katika taasisi hii ikae sasa independent ili sasa tuwe na uhakika kwamba, mlaji anasimamiwa ipasavyo badala ya kuwa chini ya Tume hii ya Ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, miongoni mwa majukumu ambayo tunaenda kufanya, sasa tunataka tuanze kutunga sera ya kumlinda mlaji; na ndani ya sera hiyo sasa tutatengeneza pia sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, kama nilivyosema, pia ili kumlinda mlaji maana yake sasa tunataka tuwe na sheria ambayo yenyewe moja kwa moja itahakikisha inasimamia kumlinda mlaji tu ikiwa nje ya FCC ambayo inafanya majukumu mawili ya kusimamia ushindani, lakini pia na kumlinda mlaji.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, matatizo ya zao la kahawa ya Mkoa wa Kilimanjaro yanafanana sana na matatizo ya kahawa ya Mkoa wa Kagera. Mavuno ya kahawa katika Mkoa wa Kagera huanza mwezi Aprili hadi Mei, lakini mpaka juzi Vyama vya Msingi vilikuwa havijafungua msimu wa kahawa.

Mheshimiwa Spika, na tatizo kubwa lililopo hasa Wilaya ya Muleba, wananchi wanabugudhiwa na task force ambayo imeundwa ambayo inajumuisha watu wa PCCB, Usalama wa Taifa na watu wa Kilimo. Kila anayekutana naye anatoka shambani ana gunia moja anakamatwa na kupelekwa kituo cha polisi.

Naomba kauli ya Serikali, je, ni nini kauli ya Serikali kukomesha vitendo viovu hivi ambavyo vinawabugudhi wakulima kwa kisingizo kwamba wanalangua kahawa ilhali wako kwenye Wilaya yao, wako kwenye tarafa yao na vijiji vyao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Muleba Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza, niseme na nirudie tena, tumefanya vikao na viongozi wa Mkoa wa Kagera, tumefanya vikao na vyama vikuu vya ushirika vya Kagera, tumefanya vikao na wanunuzi binafsi; la kwanza, hatumzuii mkulima yeyote kupitia chama chake cha msingi kuuza mazao yake kwa mfanyabiashara katika level ya chama cha msingi. Hili ni jambo la kwanza, na tumeruhusu na tumetoa leseni. Na msimu umeshafunguliwa. Na wiki iliyopita tulikuwa na mkutano hapa Dodoma wa wadau wote wa kahawa.

Mheshimiwa Spika, la pili, tuwaombe viongozi katika ngazi za Halmashauri na Wilaya. Sekta ya kilimo haiwezi kusimamiwa kimabavu, sekta ya kilimo inasimamiwa kwa misingi ya win-win. Mkulima anayevuna mazao yake kutoka shambani kuyapeleka kwenye nyumba yake ama kuyapeleka kwenye chama chake cha msingi, naomba kupitia Bunge lako niwaombe viongozi walioko katika Halmashauri na Wilaya wasiwabughudhi.

Mheshimiwa Spika, lakini haturuhusu vilevile wafanyabiashara wanaowafuata wakulima mashambani kwenda kununua mazao chini ya bei ya soko, halafu wao kupeleka kwenye minada na Chama cha Msingi ili waweze ku-benefit na bei. Hilo hatutaruhusu na wala hatutaruhusu mfanyabiashara yeyote anayechepusha mazao kuvusha kwenye mpaka wa Tanzania na Uganda.

Mheshimiwa Spika, tunawataka na nitumie Bunge lako kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, kama mna wanunuzi kutoka Uganda ambao wana uwezo wa kutupa bei nzuri, waleteni Wizarani tutawapa leseni, watakwenda kununua katika mfumo rasmi bila kubugudhiwa na mtu yeyote.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii. Matatizo ya Ludewa yanafanana sana na matatizo ya Wilaya ya Muleba. Wilaya ya Muleba ni kubwa yenye watoto wengi wanaohitimu darasa la saba, form four na kidato cha sita.

Je, ni lini Serikali itatujengea Chuo cha VETA katika Wilaya ya Muleba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba sasa kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kikoyo, Mbunge wa Muleba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwa upande wa Kilolo, Serikali inaendelea kutafuta fedha baada ya ukamilishaji wa vyuo hivi 29 katika wilaya 29 ambayo tumeanza kwa awamu ya kwanza kuweza kuzifikia wilaya nyingine ikiwemo na Wilaya ya Muleba. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Kikoyo katika muda mfupi ujao baada ya Serikali kupata fedha tutahakikisha kwamba kila wilaya tunaifikia ikiwemo na wilaya ya Muleba. Ahsante sana.