Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Exaud Silaoneka Kigahe (44 total)

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa ni zaidi ya miaka 30 sasa tangu wakulima wa chai wa Kilolo wapande chai yao na kujengewa kiwanda ambacho hakijawahi kufanya kazi; na kwa kuwa katika muda huo wako Mawaziri kadhaa na Manaibu wameenda kule wakapiga picha kwenye mandhari nzuri za mashamba yale na kuahidi wananchi wale kwamba shughuli hiyo itakamilika mapema iwezekanavyo na hawakurejea tena. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa wananchi wa Kilolo kwamba sasa kiwanda kile kilichojengwa na hakikuwahi kufanya kazi, kitafanya kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa michakato mingi imepita ya kumpata mwekezaji na mchakato wa mwisho ulikuwa mwaka 2019 na wawekezaji walijitokeza na wakapatikana na wako tayari, na kwa kuwa uwekezaji huu haukukamilika kutokana na urasimu wa Serikali. Je, Serikali iko tayari kuwawezesha wale wawekezaji kwenda kuwekeza badala ya kuanza mchakato mwingine ambao unaweza ukachukua miaka mingine 30?Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, Serikali imefanya jitihada nyingi sana kuhakikisha kiwanda hicho kinafanya kazi. Kwa taarifa tu ni kwamba katika miaka ya nyuma tayari kuna wawekezaji walikuwa wamejitokeza kwa ajili ya kuwekeza katika kiwanda hicho na mmojawapo ni Mufindi Tea and Coffee Company chini ya DL Group. Hata hivyo, baada ya kupitia mchakato wa upatikanaji wa mwekezaji huyo ilionekana kwamba kuna baadhi ya vipengele vilirukwa lakini pia baada ya kuwa na due diligence ya kutosha ilionekana kwamba mwekezaji huyo alikuwa hana uwezo wa kuwekeza katika kiwanda hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, juhudi hizo bado zinaendelea na kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba sasa tunaandaa andiko maalum ambalo litaangalia namna bora ya uendeshaji wa kiwanda/shamba lile likihusisha ushirikishwaji wa wadau wote kwa maana ya wakulima wadogo, halmashauri ya Kilolo lakini pia na Msajili wa Hazina ambaye ndiye anasimamia kiwanda hicho. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kama ilivyo kwa wananchi wa Kilolo, ni lini Serikali itakiamuru Kiwanda cha Chai cha Katumba kuongeza bei ya chai kwa wakulima wadogo wadogo katika Wilaya ya Rungwe?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya chai katika soko la dunia hivi karibuni iliyumba kidogo. Kwa hiyo, kampuni nyingi za chai zimekuwa na changamoto ya soko katika kuuza chai zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bei kwa wakulima wadogo wadogo naamini baada ya kutengemaa kwa soko la chai duniani sasa hivi ni dhahiri shairi kwamba kampuni nyingi za chai ikiwemo hiyo ya Katumba, Mbeya na nyingine zitaweza kuwaongezea bei wakulima kwa sababu sasa kuna uhakika wa soko katika soko la dunia.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwanza napenda kusema kwamba Serikali imepotosha Bunge lako Tukufu kwa kusema uongo ambao haukubaliki. Je, Waziri anajua kwamba TAMISEMI chini ya Waziri Jafo waliunda Kamati ya Uchunguzi (fraud) mwaka 2018 na Kamati hii ilitoa mapendekezo kuonesha jinsi SIDO ilivyowaibia wakulima pamoja na Halmashauri ambayo haikufanya kazi yake vizuri kuwasahauri wakulima na michango ambayo ilitolewa na Rais wakati huo Kikwete, karibu shilingi milioni 300 haikutumika vizuri na akaomba hatua madhubuti zichukuliwe na SIDO ilipe hela zile za wakulima?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri ana habari kwamba kutokana na kutofanya kazi kwa mitambo ile ndiyo maana sasa hivi PSSF imenunua mitambo mipya na inaifunga kwa kuona kwamba mitambo ile iliyofungwa ilikuwa batili? Inakuwaje Waziri…

NAIBU SPIKA: Umeshauliza maswali mawili tayari.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kaboyoka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme hakuna uongo ambao umesemwa katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba SIDO baada ya kuingia mkataba ule na kuweza kufunga mtambo ule kulikuwa na changamoto mbalimbali na hasa kwenye upande wa ukaushaji katika mchakato ule. Baada ya kujadiliana na Halmashauri ya Same ikaonekana kwamba wakulima wale walikuwa hawaridhishwi na utendaji wa mitambo ile kwa hiyo SIDO ilishirikiana na mradi wa Market Infrastructure, Value Addition And Rural Finance - MIVARF kuagiza mtambo mpya ambao ulikuwa na gharama ya shilingi milioni 29 na SIDO walichangia katika mtambo huo mpya shilingi milioni 9 na ukafungwa kama nilivyosema tarehe 27/02/2015 na ukaendelea kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hasara au gharama ambazo zilikuwa zimeingiwa na wakulima wale baada ya kuwa mtambo ule haufanyi kazi vizuri, kama nilivyosema tunaielekeza SIDO waweze kufanya mashauriano na Halmashauri ili waone namna gani ya kuwafidia wakulima wale ambao walipoteza mazao yao kipindi kile ambapo mtambo ule ulikuwa haufanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtambo uliopo sasa hivi unafanya kazi vizuri na yeye atakuwa ni shahidi. Wakulima wale wameridhika na wanaendelea kufanya kazi zao za kuchakata zao la tangawizi.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba viwanda hivyo viwili anavyovisema, kimoja kinabangua tani 2,000 badala ya tani 5,000 na kingine hakibangui kabisa, kinafanya kufunga. Swali la kwanza; je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha viwanda hivi vinabangua kwa ule uwezo wake? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; katika Manispaa ya Mtwara Mikindani kuna kiwanda kikubwa cha kubangua korosho kinachomilikiwa na Kampuni ya OLAM. Kiwanda hicho kimefungwa. Kiwanda kile kilikuwa kinaajiri wafanyakazi wasiopungua 6,000 wakiwemo wanawake karibu 5,000. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wanakaa na mwekezaji yule, kiwanda kile kiweze kufanya kazi ili wanawake wa Jimbo la Mtwara Mjini waweze kupata ajira wajikwamue kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kabisa kwamba, kama nilivyosema katika jibu la msingi, kuna changamoto ya malighali kwa maana ya korosho ambazo zinahitajika katika viwanda vyetu mbalimbali vya kubangua korosho hapa nchini. Hivyo, kutokana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Bodi ya Korosho, tumeandaa mwongozo ambao kwanza tunawapa kipaumbele wabanguaji wa korosho hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuanzia msimu wa 2021 mwongozo huo unataka malighafi zinazopatikana katika mnada wa awali kupitia soko la awali la korosho, viwanda vyote vya ndani ambavyo vinabangua korosho, kwanza vipate korosho, vikishajitosheleza ndiyo sasa tunafungua ule mnada wa pili ambao sasa utahusisha wafanyabiashara wote ambao wako katika soko la korosho. Hii itapelekea kuhakikisha kwamba viwanda vyote vinavyobangua korosho vinapata malighafi kulingana na mahitaji yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusu Kiwanda cha OLAM, ni kweli kiwanda hiki ambacho kilikuwa ni sehemu ya uwekezaji katika Manispaa ya Mikindani, changamoto kubwa iliyosababisha kufungwa kiwanda kile ilikuwa ni kutokana na kukosa malighafi ambazo zilitokana na ushindani wa wanunuzi wa korosho katika minada ambayo inafanyika kwenye maeneo hayo. Ndiyo maana tunapeleka mwongozo huu ambao sasa utahakikisha kwamba viwanda vya kubangua korosho vinapata malighafi kwanza, halafu sasa zile zinazobaki ndiyo zitaingizwa kwenye mnada ambao utajumuisha wafanyabiashara wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali tayari imeshaanza mawasiliano na Kampuni ya OLAM ambao waling’oa mitambo ile na kuipeleka nchi jirani Msumbiji ambako wao walikuwa na utaratibu mzuri wa kuhakikisha viwanda vinapata malighafi. Kwa hiyo, sasa tunataka warudi nyumbani kwa sababu nasi tayari tumeshaweka mwongozo huo ambao unawahakikishia malighafi viwanda vyote ambavyo vinabangua korosho hapa nchini. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tunduru tuna Kiwanda cha Kubangua Korosho kilichojengwa miaka ya 1980 ambacho alipewa mwekezaji kwa muda mrefu na mwekezaji yule alikuwa anaendelea kubangua korosho bila kufikisha lengo la makubaliano na Serikali. Kufikia mwezi Agosti, 2020, kubangua korosho wamesimama kabisa na korosho za Tunduru zinalazimika kununuliwa na kupelekwa nje. Je, kwa nini Serikali haioni haja ya kumnyang’anya mwekezaji yule Kiwanda cha Tunduru cha Korosho na kupewa mtu mwingine ili uzalishaji wa korosho uendelee? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mpakate kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni kuhamasisha uwekezaji wa viwanda mbalimbali hapa nchini ikiwemo viwanda vya kubangua korosho. Ni kweli kiwanda cha kubangua korosho cha Tunduru (Tunduru Cashew Factory) ambacho kilinunuliwa na Kampuni ya Micronics ambaye amewekeza katika maeneo mengi, bado kuna changamoto kidogo katika ufanyaji wake wa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, lengo la Serikali ni kuona tunaendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mpakate kwamba tutakaa na mwekezaji huyu, tuweze kujadiliana naye, tuone ni changamoto gani ambazo alizipata katika uendeshaji wa kiwanda hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, suala la kumnyang’anya kiwanda litakuwa baada ya kujihakikishia kwamba kweli ameshindwa kutekeleza kuwekeza katika kiwanda hicho halafu tuweze kuona namna bora ya kupata mwekezaji mwingine. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza sina budi kuishukuru Wizara kwa jawabu zuri lenye mantiki ambalo linaeleweka na linalofahamika. Itakuwa ni hasa Watanzania wengi watalifurahia jawabu hilo kutokana na maelezo yake aliyojipanga.

Mheshimiwa Spika, lakini nina maswala mawili ya nyongeza. Kwa kweli matunda kama mananasi, matikiti, machungwa, embe n.k huwa yanazaliwa kwa wingi na yanakosa soko na yanaharibika mitaani. Je? Serikali inawaambia nini wananchi wa mikoa hiyo wanaozalisha matunda kwa wingi mbinu ya kunusuru matunda hayo ili yaweze kukaa kwa muda mrefu? (makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tunazungumza Tanzania ya viwanda na ninakubaliana na maelezo yako, lakini ningeiomba Serikali ikawahamasisha wazawa wa Tanzania wa kila mkoa wakaweza kuanzisha viwanda ili kila mkoa ukawa na viwanda vya kusindika au cha kufanya juhudi yoyote ili mikoa inayozalisha matunda kwa wingi iweze kuyanusuru matunda yao na iweze kufanikiwa na wanachokilima kiwape faida yao? Naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunajua changamoto ya upotevu wa mazao yaani (post harass losses) kwa ujumla wake na hasa katika msimu ambao kunakuwa na mavuno mengi, kwa maana ya matunda mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango Madhubuti, kwanza wa kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vidogo vidogo ambavyo Waheshimiwa Wabunge kila mmoja maeneo yake anaweza kuwa na viwanda hivyo ambavyo vinaweza kuchakata mazao haya au matunda hayo kwa muda ambao yanakuwa yamezalishwa kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, lakini pili kupitia SIDO tuna teknolojia na viwanda vidogo vidogo vingi ambavyo vinachakata mazao ya matunda lakini pia teknolojia ya kukausha ili kuyatunza matunda hayo yasiweze kuharibika, yaweze kutunzwa ili yasiweze kupotea kabla ya kutumika.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo nashukuru kwa ushauri wa Mheshimiwa Mbunge; kwamba Serikali tunaendelea kuhamasisha kweli uanzishaji wa viwanda lakini pia na teknolojia nyingine ikiwemo kuwa na vyumba maalum cold rooms ambazo ni facility za kutunza matunda kabla ya kuuza yaweze kukaa kwa muda mrefu ili angalau yaweze kudumu yasiharibike haraka.

Mheshimiwa Spika, tunachukua ushauri wake lakini tunaendelea kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vidogo vidogo, lakini pia kupitia masharika yetu tuna teknolojia mbalimbali ambazo tunawakaribisha Waheshimiwa Wabunge kupitia SIDO na taasisi zetu nyingine waweze kupata teknolojia hizi ili ziweze kuwasaidia katika kutunza matunda ili yasiweze kupotea wakati wa mavuno mengi.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Ni kwamba, Serikali yetu sasa hivi imeingia kwenye mfumo wa Serikali ya viwanda na uhamasishaji huu umekuwa mkubwa sana. Katika Wilaya ya Liwale viko viwanda vidogo vidogo kazi yake ni kusindika korosho, lakini wananchi wale wanashindwa kupata mali ghafi kwa sababu ya kuwa na mitaji midogo. Tunafahamu kwamba korosho, zinazalishwa, zinauzwa kwenye minada; na kwa sababu wale wawekezaji ni wadogo wadogo hawawezi kuingia kwenye mnada matokeo yake anapoingia kwa wananchi kwenda kununua korosho anaoneka wananunua kangomba.

Mheshimiwa Spika, je, sasa Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wale wadogo wadogo kupata mali ghafi hii ya korosho ili vile vikundi vyao vya kubangua korosho viweze kubangua kwa msimu mzima au kwa mwaka mzima?
NAIBU WAZIRI VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kutoka Liwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli usindikaji wa zao la korosho angalau sasa unaimarika kwa sababu sasa tumehamasisha uanzishaji na kufufua viwanda vingi vya kusindika korosho.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaweka utaratibu maalum baada ya kuona changamoto hiyo inayowapata wazalishaji au wabanguaji wa korosho wa viwanda vya ndani kutokana na ile changamoto ya kuweza kutokununua kwenye minada.

Mheshimiwa Spika, utaratibu uliopo ni kwamba wale wote wenye viwanda vya kuchakata au kubangua korosho ambao wanazalisha kwanza kabla ya kufungua msimu wa mnada huwa tunawapa kipaumbele wao kwanza, wanunue waweze kutosheleza mahitaji yao halafu zile korosho zinazobaki ndizo zitaingizwa kwenye mnada wa jumla. Lengo ni hilohilo kuwalinda, kulinda viwanda vyetu vya ndani ili viweze kupata raw material au malighafi ya kutosha kabla ya kuingia kwenye ile competition ya mnada mkubwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge wa Liwale kwamba hilo tutalichukulia kwa umakini sana kuhakikisha viwanda vyetu vya ndani vinapata malighafi za kutosha ili waweze kuzalisha kadri ya uweze ambao viwanda hivyo vimesimikwa.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninalo swali moja ambalo kwa kuwa NHIF na WCF walishaomba kibali hususani kwa ujenzi wa kiwanda hiki.

Ni lini sasa Serikali itatoa kibali cha ujenzi wa kiwanda hicho cha vifaa tiba Mkoani Simiyu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Lucy John Sabu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyosema tayari mkakati huu wa kujenga kiwanda hicho upo na kweli WCF na NHIF ndiyo walikuwa wamepewa kazi hiyo kujenga kiwanda hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kamati Maalum ambayo inaratibu au inashughulikia sekta ya viwanda vya dawa na vifaa tiba ambao wanaendelea kuchanganua namna bora kama nilivyosema ya kutekeleza mradi huu. Kwa hiyo, kama nilivyosema tukishakamilisha taratibu hizo kiwanda hicho kitaanza kujengwa mara moja kupitia mifuko hii, lakini pia na MSD nao watashiriki kuhakikisha tunakidhi vigezo vya kutengeneza dawa zenye ubora unaotakiwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kuwashukuru Serikali kwa majibu yao mazuri, lakini je, Serikali imejipangaje hasa kuwachukulia hatua hawa wawekezaji ambao wanapewa hivi viwanda na wanavitelekeza na wanaenda mbali zaidi wanavichukulia mikopo na kuviacha hapo? Serikali imejipangaje kisheria kuwabana aina hii ya wawekezaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Didas Masaburi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza kuchukua hatua na ndiyo maana tumeona katika viwanda vile 68 ambavyo vilikuwa haviendelezwi tayari hivi 20 vimesharejeshwa Serikalini. Lakini pia tunaendelea kuvitathimini na hivyo vingine.

Kwa hiyo niwahakikishie watanzania na Mheshimiwa Juliana Masaburi na Wabunge wote kwamba Serikali ipo makini kuona sasa wawekezaji wote watakaoingia mikataba ya kuviendeleza viwanda katika sekta zote pale ambapo watakiuka masharti ya mikataba tutakayoingia nayo sheria zitachukuliwa na hatua mahsusi ikiwemo kuwanyang’anya viwanda hivyo vitachukuliwa ili kuhakikisha sasa tunapata wawekezaji makini ambao kweli wataleta tija katika uendelezaji wa sekta ya viwanda nchini. Ahsante sana.
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kile Kiwanda cha MUTEX, Mheshimiwa Naibu Waziri amekubali kwamba aliyekuwa anakiendesha alinyang’anywa kwa sababu alikuwa hakiendeshi kwa tija na sasa yapata ni miaka mitatu kile kiwanda kimesimama.

Je, ni kwanini basi hata huyo, huyo asingepewa akakiendeleza kuliko ambavyo sasa kile kiwanda kimesimama na watu wanakosa ajira?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa ubinafsishaji wa viwanda hivi kulikuwa na mikataba na katika mikataba hiyo kulikuwa na vigezo maalum na ndiyo maana tuliona sasa katika kuvunjwa kwa mikataba hiyo ndiyo maana imechukua muda mrefu ili kujihakikishia, ilikuwa mojawapo ni kumshawishi yule aliyepo kuona kama anaweza kuendeleza, lakini baada ya kujiridhisha kwamba ameshindwa ndiyo maana vimerejeshwa Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kupata wawekezaji mahiri ambao kweli wapo makini na watawekeza kwa tija. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Vedastus Manyinyi, kwanza tuna dhamira ya dhati ya kupata wawekezaji sasa mahiri ambao watawekeza katika viwanda hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tusingependa kuwaonea au kumpa mtu kwa upendeleo. Kwa hiyo tufuate utaratibu ambao utatangazwa na baadaye wawekezaji wengi watapatikana ambao watawekeza kwa tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala hili la viwanda tutakumbuka pia kulikuwa na viwanda vingi vya korosho vilivyopo maeneo ya kusini, Mtwara, Lindi, Masasi, Nachingwea na maeneo mengi. Serikali imesema imeamua kubinafsisha na kuna vingine vilikuwa vinatumika kama maghala ya kuhifadhia mazao badala ya kuviendeleza kuwa viwanda vya korosho ili kuweza kutoa ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka tusikie commitment ya Serikali, ni lini zoezi hili wanalolifanya litakamilika ili kuweza kuvirejesha hivi viwanda, watu muda sahihi wa kukamilisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil David Mwambe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi ni kweli kuna viwanda vingi ambavyo vimekuwa havifanyi kazi baada ya wawekezaji wengi kuvitelekeza au kutokuviendeleza au kuendeleza kwa kusuasua au kubadilisha matumizi ya viwanda hivyo ikiwemo wengine waling’oa hata mitambo ya viwanda hivyo na kubadilisha kuwa ma-godown.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge watuelewe kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kuona sasa tunapata wawekezaji mahiri. Kwa hiyo hata viwanda vya korosho ambavyo vilikuwa vimetelekezwa kama nilivyosema tunaenda kutangaza utaratibu maalum wa kuweza kuwapata wawekezaji kwa njia ya wazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baada ya hapo naamini wengi ambao wana nia ya kuwekeza katika viwanda hivi watapatikana na hakika tunaamini viwanda hivi vitaenda kufanya kazi kwa tija kama ambavyo Serikali imekusudia. Nakushukuru sana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kipekee nimshukuru Mkuu wa Wilaya mpya aliyekuja katika Wilaya ya Rungwe, jana ameweza kuwaita wadau wanaonunua zao la maziwa na kuhakikisha wanapatikana wengi na wala siyo mmoja tena.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza; Serikali haioni kuna haja ya kuleta Sheria Namba 3 ya mwaka 1977 ambayo ilikuwa inataka wakulima wote wanakaa katika mfumo wa kijiji. Sasa inawafanya Bodi ya Chai ambao ndiyo watoaji wa leseni hawawapi wakulima mmoja, mmoja kwa maana mkulima wa chai aweze kwenda kukopa benki, aweze kujua ni chai yake amuuzie nani na amkatae nani, sheria hii inawabana. Sasa kwa nini Serikali isilete marekebisho ya Sheria hiyo?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Mrajisi wa Ushirika Wilaya ya Rungwe na sijui wilaya zingine alianzisha ushirika mpya na kuondoa ushirika wa kwanza bila kuwahusisha wakulima. Serikali inasemaje kwa hilo japokuwa jibu la msingi amesema ameweka, anasimamia na anafuatilia. Serikali ifuatilie kwa kina juu ya wakulima hawa ambao wao wanajua wapo RSTGA, lakini leo kuna kitu kinaitwa RUBUTUKOJE, wakulima wameachwa njia panda. Naomba Serikali ifuatilie kwa ukaribu suala hili. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana dada yangu kwa ufuatiliaji wa karibu kuhusiana na maendeleo ya wakulima wa chai na maziwa katika Wilaya ya Rungwe.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyosema kama kuna maendeleo ambayo anayaona kupitia Mkuu wa Wilaya kama tulivyosema tayari tumeshaanza kulishughulikia hili, ili kupata taarifa maalum kama nivyosema kwenye jibu la msingi kupitia Tume yetu ya Ushindani (FCC). Kwa hiyo hilo analolisema kuhusiana na Sheria Na.3 ya mwaka 1977, basi tutaangalia hilo pia, lakini tukipata taarifa maalum kulingana na ambavyo tumeomba kwa maana ya utaratibu wa ununuzi, namna bei zinavyopangwa katika soko, lakini pia na majina ya wanunuzi ambao wanashiriki katika ununuzi wa chai na maziwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Mrajisi katika Vyama vya Ushirika, naomba nalo tulichukue kama Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, tutafuatilia ili tuone ni namna gani tutatatua changamoto ambayo inawakabili wakulima wa chai na maziwa katika Wilaya ya Rungwe. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, gesi asilia ninayozungumzia kwenye swali langu la msingi ni ile gesi ya Songosongo na eneo mahsusi ambalo nimeulizia ujenzi wa kiwanda ni katika Mji wa Kilwa Masoko, ambapo kimsingi tayari eneo la kutosha lipatalo ekari 400 lilishatengwa tangu mwaka 1989, lakini pia TPDC ilishalipa fidia ya eneo hili na ni eneo ambalo lipo huru na lina hati. Je, Serikali inathibitisha kupitia Bunge lako Tukufu kwamba kiwanda hiki cha mbolea kitajengwa mahsusi Kilwa Masoko na si kwingineko? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kwa ridhaa yako kuambatana nami baada ya Bunge hili kwenda Kilwa ili akajionee maendeleo na maandalizi ya eneo la kutosha la kiwanda hiki? Ikiwa ni pamoja na uwepo wa bandari, uwepo wa eneo la kutosha kwa ajili ya upanuzi wa bandari, lakini pia uwepo wa eneo la kutosha kwa ajili ya kutolewa malighafi hii, lakini pia atapata fursa ya kujionea Kiwanda cha Maji cha Swahili Water pale Nangurukuru. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nipo tayari.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi ni kwamba tunataka kuona tunatumia malighafi iliyopo ya gesi asilia na kimsingi kama alivyosema TPDC tayari walishakuwa na eneo na hata wawekezaji hawa tunaojadiliana nao wengi tunataka waeleke kujenga katika Mji huu wa Kilwa Masoko ambapo ndipo malighafi inatoka.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana kwa juhudi zake za kufuatilia suala hili na kama nilivyosema mwanzoni nitaambatana naye katika maombi yake ili tuweze kupitia kuona namna gani tunajionea, lakini pia kuona na viwanda vingine ambavyo vimewekeza katika Mkoa wa Lindi hususani Kilwa Masoko.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Pamoja na uwepo wa viwanda hivyo 14 alivyovitaja, lakini bado Serikali inaagiza dawa na vifaa tiba kwa asilimia 80 kutoka nje. Je, tatizo ni ubora wa dawa zinazotolewa nchini ama ushindani wa kibiashara?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali imesema ifikapo mwaka 2025 itafikia asilimia 60, napenda kujua tu, sasa hivi tuko asilimia ngapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, Tanzania bado hatujajitosheleza katika uzalishaji wa dawa kwa maana ya kuwa na viwanda vichache ambavyo vinazalisha dawa na vifaa tiba kwa ajili ya matumizi hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala siyo ubora, ni uwezo wetu ambao bado haujakidhi mahitaji ya ndani. Suala la ushindani ni suala lingine kwa sababu ushindani upo hata katika bidhaa ambazo tumejitosheleza, lakini specifically kwenye hili bado uwezo wetu wa kuzalisha ndani ni mdogo, ndiyo maana tumelenga kuhamasisha kupitia vivutio mbalimbali ili tuwe na wawekezaji wengi zaidi wanaowekeza katika viwanda vya kutengeneza dawa na vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kiasi ambacho kinaagizwa sasa, ni kweli hatujafikia uwezo wa kutengeneza asilimia zote za dawa kwa maana ya asilimia 100, bado tunaagiza zaidi ya asilimia 80 kutoka nje. Kwa hiyo, bado lengo letu kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, ni kufikia asilimia ya uzalishaji ifikapo mwaka 2025.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nilikuwa naomba kuuliza; je, Serikali ina mpango gani ya kufufua Kiwanda cha Machine Tools, kiwanda ambacho kinatengeneza vipuri kwa ajili ya viwanda vingine na pia vinatengeneza na kuunda mashine za kusaidia viwanda vingine vidogo na vikubwa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo mnajua, Serikali sasa ina mpango wa kuendeleza uchumi wa viwanda. Kiwanda cha (Kilimanjaro Machine Tools – KMTC) ni moja ya viwanda muhimu sana kwa maana ya basic industries katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaamua kufufua kiwanda hicho. Katika bajeti ya mwaka huu tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kujenga kinu cha kuyeyushia chuma (foundry).

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Saasisha Mafuwe kwamba kiwanda hicho sasa kinaenda kufanya kazi kwa sababu tutakuwa na uwezo wa kuyeyusha chuma na kuzalisha vipuri ambavyo vinahitajika katika viwanda vingine kwa ajili ya maendeleo ya Sekta ya Viwanda hapa nchini. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa kuzungumza kitu kimoja:-

Mheshimiwa Spika, sasa hivi ni mwaka wa 12 toka fidia ya mwanzo ilipofanyika na wengine mpaka sasa bado hawajafanyiwa fidia. Na lile eneo Serikali ilishatengeneza GN tayari kiasi kwamba, wananchi wanashindwa kufanya tena chochote katika maeneo yale. Na maeneo yamekuwa mapori, yamekuwa usumbufu, wafugaji wameingia pale inakuwa mgogoro kati ya wakulima na wafugaji. Je, Serikali inaweza ikafanya mpango wowote kuwarudishia maeneo yao hawa wahusika kama hawatakuwa tayari?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, kwa haya majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari mimi na yeye tuongozane bagamoyo tukafanye mkutano wa hadhara Mlingotini, ili awaridhishe wananchi wa kule kwa hili janga ambalo lilewapata kwa miaka 12 sasa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwanza fidia ya mwisho iliyolipwa kwa wananchi hao ilikuwa ni mwaka wa fedha 2017/2018 kwa hiyo, sio kweli kwamba, ni zaidi ya miaka 12 katika malipo ya mwisho yaliyolipwa fidia kwa wananchi hao.

Mheshimiwa Spika, maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya maendelezo, hasa kwa sekta ya viwanda na uwekezaji mwingine ni muhimu sana. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa mkenge kwamba, si vema maeneo ambayo yameashaainishwa kwa ajili ya maendeleo ya viwanda na uwekezaji mwingine kurudishwa kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali inaendelea kuona umuhimu wa kulipa fidia hizo haraka iwezekanavyo, ili uendelezwaji wa maeneo hayo uweze kufanyika. Lakini pili tunaendelea kushauri Serikali za Mikoa na halmashauri kuona namna bora ya kuyamiliki maeneo ambayo Serikali Kuu kwa maana ya kupitia EPZA tutakuwa bado tunashindwa kuyalipa, ili nia ya Serikali ya kuwa na maeneo maalum ya uwekezaji na hasa kwa ajili ya maendeleo ya viwanda yaendelee kuwepo kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mheshimiwa Mkenge niko tayari, tutaongozana na wewe na wataalamu wetu kutoka EPZA ili kuweza kuongea na wananchi wa Mlingotini kwa ajili ya kuona namna bora ya kuendeleza, hasa kulipa fidia maeneo haya ambayo yametwaliwa.
MHE. IRENE A. NDYAMKAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, ni lini Serikali inawahakikishia wananchi wa Mkoa wa Rukwa itawatafutia wawekezaji na kuwekeza kiwanda hicho cha sukari mkoani hapo?

Mheshimiwa Spika, swali jingine, kwa kuwa, Mkoa wa Rukwa ni tatu bora kwa kilimo nchini Tanzania. Ni lini Serikali itaangalia tena mkoa huu kwa kuwekeza viwanda vingine?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunaendelea na kuhamasisha uwekezaji au viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mpango wa miaka mitano ambao umeuona moja ya maeneo muhimu sana ambayo tumeainisha ni kuhakikisha tunatafuta wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, ikiwemo miwa na mazao mengine ambayo yanalimwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Rukwa.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, na yeye ni mmoja wa wadau muhimu sana ambao tunaweza tukashirikiana ili kuhakikisha tunawekeza viwanda vidogovidogo vya kati na vikubwa kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa wa Rukwa. Lakini pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, muda wowote Wizara iko tayari kushirikiana na kukushauri na kushauriana na wawekezaji wengine, lakini pia kuangalia vivutio maalum ambavyo vitasababisha wawekezaji wengi kuwekeza katika mikoa yetu ikiwemo Mkoa wa Rukwa.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa kuwa Serikali inakiri kwamba, uwezo wetu wa kuzalisha sukari ndani hautoshelezi mahitaji ya ndani na tunaagiza kiasi cha takribani tani tani zaidi ya laki moja za sukari kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, na kwa kuwa, miwa ya wakulima katika Jimbo la Mikumi ni zaidi ya tani laki nne zinateketea mashambani. Na kwa kuwa, kiwanda cha Ilovo wakati wanauziwa walikuwa na masharti ya kuongeza upanuzi wa kiwanda hicho na Serikali inasuasua. Je, ni lini Serikali inaenda kuhakikisha kwamba, upanuzi wa kiwanda hicho unakamilika na mazao ya wakulima ya miwa yanaenda kupata soko la uhakika?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyosema mahitaji ya sukari hapa nchini ni makubwa ukilinganisha na uwezo wetu wa uzalishaji wa ndani. Suala la wananchi kukosa soko katika Wilaya ya Kilombero ni moja ya maeneo muhimu sana ambayo sisi kama Wizara ya Viwanda na Biashara tumeshayaona. Na moja ya mikakati ya Wizara ya Viwanda ni kuona namna gani sasa tunaongeza uchakataji wa miwa ambayo inakosa soko katika viwanda vilivyopo.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo (TEMDO), tunaenda kuleta mitambo midogo ambayo itaweza kusaidia kuchakata miwa kwa wakulima wadogowadogo ambao wanakosa soko katika viwanda vikubwa kwa sasa, ikiwemo maeneo ya Kilombero.

Mheshimiwa Spika, kuhisiana na viwanda vilivyopo tayari kuna mipango maalum, kwanza kuhamasisha kuongeza uwekezaji kwa kuongeza uzalishaji katika viwanda hivyo, lakini pia kuhakikisha na wao wanaingia sasa, kuna kitu tunaita quail farming, ili waweze kusaidiana na wakulima wadogowadogo kuzalisha miwa mingi, lakini pia na wao wenye viwanda kuwa na mashamba mengine ambayo yatatosheleza mahitaji ya uzalishaji katika viwanda vilivyopo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza tutahakikisha miwa ambayo inakosa soko tunaleta hiyo mitambo midogo ambayo itachakata miwa hiyo, ili angalao wakulima wale waweze kupata soko la uhakika.

Mheshimiwa Spika, la pili. Tunaendelea kushirikiana na viwanda vilivyopo ili kuhakikisha wanahamasisha wakulima wadogowadogo kwa maana ya kuingia quail farming katika viwanda vyao.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla kwa majibu mazuri na ya kina kuhusiana na swali hilo ambalo tumeuliza, lakini naomba niulize maswali mawili za ziada madogo. Swali la kwanza; kwa vile SIDO inalenga watu wa chini watu ambao wapo kwenye vijiji na kadhalika na hawa watu ni vigumu sana waweze kuelewa hivi vitu alivyovieleza kwa sababu hata mimi nilikuwa sivijui. Je, wana mpango gani wa kuiongezea SIDO uwezo wa kujitangaza na kutekeleza maonesho kwenye miji midogo midogo kama Mji wa Himo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusiana na mabanda ya viwanda au majengo ya viwanda. Kasi ya ujengaji wa majengo haya ni ndogo sana pengine tunaenda na too much sophistication, lakini tukienda kwa mtindo mwingine naamini tutaweza tukaharakisha sana ujenzi wa haya mabanda. Je, kama wakienda na kasi hii kweli ni lini wanafikiria watatufikia sisi kule kwenye Mji wa Himo, Uchira na miji midogo midogo kwenye mikoa yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei, Mbunge wa Vunjo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli uelewa wa wajasiriamali wengi kuhusu huduma zinazotolewa na Shirika letu la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (SIDO) bado si wa kuridhisha sana kwa sababu taarifa nyingi haziwafikii wale wajasiriamali wadogo. Namshukuru Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei kwa mawazo mazuri kwamba sasa tuone namna ya pekee ya kuliwezesha shirika letu la SIDO kujitangaza zaidi kwa wajasiriamali wadogo ili waweze kutambua fursa na teknolojia ambazo zinatolewa na shirika letu la SIDO.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Kimei kwamba tunaenda kuwezesha SIDO na tunaenda kuwatengea fedha zaidi kwa maana ya mwaka ujao wa fedha 2021/2022 kuwatengea fedha zaidi ikiwemo kwa ajili ya kujitangaza ili angalau wajasiriamali wengi waweze kujua fursa na huduma za teknolojia ambazo zinazotolewa na shirika letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu majengo ya viwanda, naomba niwahakikishie Wabunge na Watanzania wote hasa wajasiriamali ambao wanataka kuwekeza katika viwanda kwa maana ya viwanda vidogo vidogo kwamba, tunakwenda kuwaongezea SIDO uwezo ili waweze kujenga majengo mengi zaidi ambapo humo wajasiriamali wetu wataweka viwanda vyao vidogo vidogo au mashine zao ambazo wataweza kuchakata mazao ya kilimo mbalimbali kulingana na mikoa au mahitaji ya sehemu mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaenda kuwaongezea uwezo SIDO ili angalau waendelee kujenga majengo mengi zaidi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wajasiriamali. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza. Uhitaji wa viwanda kwa ajili ya kuchakata muhogo katika Jimbo la Vunjo unafanana sana na uhitaji wa huduma hiyo katika Jimbo la Buyungu. Jimbo la Buyungu na Wilaya ya Kakonko kwa ujumla ni wakulima wazuri sana wa zao la Muhogo. Tatizo letu ni upatikanaji wa mashine hizo za kuchakata na kuweza kupata unga na kuboresha thamani ya zao hilo, lakini pia ni bei…

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali, je, ni lini tutapata mashine hizo za kuchakata unga wa Muhogo katika Wilaya yetu ya Buyungu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aloyce Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba kupitia shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo SIDO tayari tuna teknolojia mbalimbali na hasa za kuchakata mazao mbalimbali ikiwemo kuchakata muhogo. SIDO tayari kupitia ofisi za mikoa na hasa katika Mkoa wa Kigoma tayari tuna mashine hizo za kuchakata muhogo katika ofisi za Kibondo DC, Kakonko, Kasulu na Uvinza. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge kupitia Ofisi zetu za SIDO, Mkoa wa Kigoma aweze kuwasiliana nao ili kuona kama atapata mashine kulingana na mahitaji yake ambayo yeye anaomba katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee kama katika mashine hizo ambazo zipo katika Mkoa wa Kigoma itakuwa kwamba hazitoshelezi mahitaji yake basi nimhakikishie SIDO tupo tayari kuwasiliana nae ili tuweze kutengeneza mashine zinazokidhi mahitaji ya Mheshimiwa Mbunge na wajasiriamali katika Jimbo lake la Buyungu. (Makofi)
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa taasisi za SIDO na TEMDO zilizopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara zimeonesha ufanisi mkubwa kwenye kutengeneza mtambo wa destemming na crushing ya zabibu ambayo inapelekea kutengeneza mchuzi wa zabibu ambao umeonekana una tija kubwa sana kwa wakulima. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuziwezesha taasisi hizi mbili ili zitengeneze mashine nyingi zaidi za kuchakata mchuzi wa zabibu ili wakulima waondokane na kuuza zabibu na badala yake wauze mchuzi wa zabibu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anthony Mavunde, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali kupitia taasisi za SIDO na TEMDO tumekuwa tukiwawezesha ili waweze kubuni na kutengeneza teknolojia mbalimbali ambazo zinachakata mazao ya kilimo ikiwemo zao la zabibu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali sasa imeamua kwa dhati, kwanza kuziwezesha taasisi hizi kifedha, lakini pia na kuongeza uwezo kwa maana ya Rasilimali watu ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha 2020/2021, tayari tumeshawezesha SIDO kama nilivyosema zaidi ya bilioni nne lakini pia TEMDO zaidi ya milioni mia tano ili waweze kusanifu na kutengeneza teknolojia mbalimbali ikiwemo za kuchakata zabibu.

Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyosema kwa wengine kwamba kwa wale ambao wana hitaji teknolojia maalum kulingana na mahitaji ya mazao yao kama hili la zabibu, basi naomba nimkaribishe Mheshimiwa ndugu yangu Anthony Mavunde, katika ofisi zetu za SIDO ili tuweze kuona namna ya kukamilisha mahitaji yake ambayo yatafaa kwa ajili ya kukamua zabibu.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Viwanda. Tunazungumzia uchumi wa kati ikiwemo kuondeleza viwanda vyetu, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, ni nini mpango wa Serikali katika kuongeza viwanda vingi ili hawa vijana wanaohitimu mafunzo haya waweze kupata ajira kwa sababu naona ni vijana saba tu ambao wameajiriwa na Serikali?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, ni nini mpango mkakati wa Serikali kufufua viwanda vyote ambavyo vilijengwa enzi za Mwalimu ili hawa vijana wetu akribani 228 waliohitimu mafunzo haya ambao hawajapata ajira waweze kuajiriwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Christina Mnzava, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Tanzania tupo katika mkakati wa kuwa na uchumi unaoendeshwa na viwanda na hasa tukiwa sasa tumefika katika uchumi wa kati. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha tunaongeza viwanda vingi kwa kuhamasisha sekta binafsi kupitia kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya wadau wa viwanda kuwekeza katika viwanda vingi ambavyo hatimaye vinatumia vijana wetu wanaohitimu katika vyuo vingi ambavyo vinatoa elimu hususan inayolenga katika kuongeza ubora wa bidhaa zetu zinazozalishwa katika viwanda lakini pia lengo ni kuona sasa tunakuwa na viwanda ambavyo vitakuwa vinapata wataalam walio na utaalam mahsusi katika mahitaji wa viwanda hivyo. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi lakini pia mashirika na watu mbalimbali na wawekezaji kutoka nje ambao wanaweza kuwekeza katika viwanda hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, katika swali la pili ni kweli viwanda vingi vilivyokuwa vimejengwa wakati wa enzi za Nyerere lakini pia viwanda vingi ambavyo vilikuwa vimebinafsishwa havifanyi kazi. Serikali ina mkakati maalum kwanza kupitia viwanda vyote ambavyo havifanyi kazi, lakini hasa vile ambavyo vilikuwa vimebinafsishwa kwa watu ambao hawaviendelezi ili tuweze kuvifufua. Lengo ni kuona sekta ya viwanda inaendelea lakini wa kutumia miundombinu ya viwanda iliyokuwepo hapo kabla ili viweze sasa kuchukua wataalam wengi ambao wanasoma katika vyuo vyetu vingi ili waweze kuajiriwa katika viwanda hivyo.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri kwa niaba ya Serikali na ambayo yananipeleka kwenye maswali mawili ya nyongeza. Miongoni mwa matatizo makubwa ya kilimo na biashara ya viungo Wilayani Muheza ni kukosekana kwa ardhi kubwa ya kulimia mazao hayo kule ambako yanastawi. Pia na viwanda vya kuyachakata kulekule kwenye Tarafa ya Amani, ili kuyaongezea thamani kwa vile kule hakuna kiwanda hata kimoja. Sasa kuna ekari 35,063 ambazo ziko chini ya Kampuni ya East Usambara Tea Company ambazo zilikuwa na viwanda viwili ambavyo kwa sasa ni magofu na zinazotumika ni ekari 4,909 tu kwa miaka mingi na viwanda hivi vimegeuka magofu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali haioni hivi sasa ni wakati wa kuvirudisha viwanda hivi kwenye umiliki wake, ili kuwasaidia wananchi ikiwa ni kwa kuwekeza yenyewe ama kwa kushirikiana na wawekezaji wapya serious ili wananchi wa Amani wapate kupata viwanda vya kuongeza thamani mazao yao ya viungo kule? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tatizo la aina hii, Waheshimiwa Wabunge wanaweza kuwa mashahidi, limekuwa likitokea sehemu nyingi ambapo wawekezaji wamekuwa wakiomba kumilikishwa viwanda hivi kwa ahadi ya kuvifufua na kuzalisha ajira pamoja na kuliongezea pato Taifa, lakini badala yake wamekuwa wanaviuwa na kuvigeuza kuwa magofu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuwa aidha na sheria kali zaidi ama kutunga sheria mpya ili tusiendelee kuchezewa na viwanda vyetu vifanye makusudio yaliyokuwepo wakati vinaanzishwa? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma, Mbunge wa Jimbo la Muheza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Hamis Mwinjuma kwa kufuatilia sana maendeleo, hasa sekta ya viwanda katika jimbo lake. Amenifuata mara nyingi kuhusiana na viwanda hivi, hasa vya chai hivi vya East Usambara Tea Company Limited, ambavyo viko pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu suala la ardhi. East Usambara Tea Company Limited ina ekari 35,000 kama alivyosema na katika ekari hizo ni ekari 2,027 tu ndio zimepandwa chai na ekari 600 zimepandwa miti, kwa maana ya miti ile inayotumika kama nishati, kuni kwa ajili ya kutumika katika viwanda hivyo. Pia eneo lingine maeneo yaliyobakia ambayo yanamilikiwa na kampuni hii yanatumika kwanza katika sehemu nyingine ni vyanzo vya maji, lakini maeneo mengine ni natural reserve kulingana na utaratibu wa UNESCO kwamba, huwezi kutumia mazingira yote kulima, kwa hiyo, maeneo mengine makubwa yako katika mazingira ya reserve.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na uhitaji wa wakulima katika Jimbo la Muheza, tutaona namna gani kushirikiana na wenye kampuni, ili tuone kama wanaweza kutoa sehemu kidogo ambayo inaweza kutumika na wakulima wadogowadogo kwa ajili ya kuzalisha viungo ambavyo vitatumika katika viwanda vya kuchakata viungo kama alivyoomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwekezaji katika viwanda hivyo. Nimjulishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na ufuatiliaji huo wote, lakini viwanda hivi sasa vinafanya kazi vizuri. Uwezo uliosimikwa kwa viwanda vile viwili ambavyo vinafanya kazi vya Bukwa na Kwamkoro vina uwezo wa kuchakata kilo 120 kwa siku, lakini sasa hivi vinaweza kupata raw material kwa maana ya malighafi zaidi ya kilo 90,000. Kwa hiyo, maana yake viwanda hivi vinafanya kazi vizuri, lakini kuna viwanda vile viwili ambavyo kutokana na mahitaji haya wenye viwanda, Kampuni ya East Usambara Tea Company Limited, walivigeuza kama ma-godown, ambavyo vilikuwa Viwanda vya Munga na Nderema, lakini pia baadaye, nimjulishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kampuni hii ina mpango sasa wa kuanza ku-pack kwa maana ya blending ya ile chai wanayozalisha pale badala ya kwenda kuuza kwenye minada ya Mombasa na kwingine, wataanza kufanya blending pale. Kwa hiyo, tuna mpango wa kuwasaidia ili wafufue viwanda hivi viwili viweze sasa kufanya blending badala ya kuwa store au magofu kama yalivyo sasa.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Niseme tu kwa majibu pia ya Serikali ambayo ni fifty fifty hivi, wakulima hawa wameanza kusumbuliwa sana na TAKUKURU. Wanakamatwa kila mahali na sijui kwa nini? Kwa sababu ni mkataba; sijui kosa la TAKUKURU linakujaje hapo! Niseme tu Mheshimiwa Rais wetu hapendi sana wakulima waonewe. Kwa kuwa, sasa Serikali imesema ilipata mkopo wa miaka 30, kwa nini wakulima hawa msiwape muda wa miaka 15 ili waweze kurejesha mikopo hii? Kwa sababu naamini ilikuwa ni nia njema sana, nami nimefanya vikao na watu wangu tarehe 10 Januari, 2021 na watu wa URSUS na kuna Wabunge wengi sana hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Wizara hii, Waziri na Naibu Waziri ni wapya, kwa nini wasitengeze kikao cha pamoja na Wabunge na watu wote wenye matrekta ili tuanze kujadili namna bora ya kuwasaidia wakulima hawa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa ufuatiliaji ambao anafanya ndugu yangu Mheshimiwa Olelekaita kuhusiana na wakulima wa Jimbo la Kiteto. Nachukua maoni yake mazuri, lakini kwanza kuhusu TAKUKURU kuwasumbua hawa wakulima waliokopa, naomba Serikali tuchukue nafasi hii kusema kuwa tutawasiliana kwanza na wenzetu kupitia NDC tuone ni nini kilikuwa kinatokea mpaka TAKUKURU wakaingizwa kwenye utaratibu wa kufuatilia mikopo hii ambayo iliingiwa na wakulima wale waliokopa matrekta na NDC?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ulipaji wa mikopo hii kwa kuongezewa muda, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nalo hili tutalijadili kwa sababu ni mikataba ambayo iliingiwa na wakulima na walitoa wao wenyewe nafasi ya kulipa kulingana na uwezo wao. Kwa sababu ni nia njema ya Serikali kuhakikisha wakulima wanawezeshwa ili tuweze kupata mazao na malighafi za viwandani, basi tutakaa pia kupitia ili tuweze kuona namna gani tunawawezesha walipe kwa unafuu zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kikao cha pamoja, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tutakuja, tutakaa na ninyi, tutajadiliana na viongozi wote na hasa wakulima ambao wanatakiwa kusaidiwa kwa namna yoyote ile ili waweze kufanya kazi zao kilimo kiwe na tija.
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa, swali la msingi nami pia nina wakulima kwenye jimbo langu la Hanang wanasumbuliwa vivyo hivyo; na malalamiko makubwa ya wakulima hawa ni ubora wa matrekta ambayo wamepewa na pia kukosa usaidizi pale ambapo matrekta haya yanaharibika, kwa maana ya matengenezo na matengenezo kinga na vipuri:-

Je, sasa Serikali iko tayari kuwasimamia hawa NDC pamoja na URSUS, kampuni iliyouza matrekta kuhakikisha kwamba matrekta haya yanahudumiwa kadri ya mikataba ya wakulima?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto kidogo kwa baadhi ya wakopaji kwa wakulima ambao walikopa matrekta haya ya URSUS katika suala la ubora. Kweli suala la teknolojia ambayo ilikuja na matrekta haya kulikuwa kidogo kuna changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara kupitia NDC tulishaligundua hilo na hivyo tumeshaanza kulifanyia kazi kuona namna gani tunaweza kuwa na utaratibu mzuri wa kuwasaidia ili matrekta hayo yanayopata changamoto ya ubora kwa maana ya utekelezaji wa dhana nzima ya kuhakikisha trekta lile linafanya kazi, tumeshaanza kuainisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba wenzetu wa NDC wameshaweka utaratibu mzuri wa kuwa na mafundi maalum ambao watapita kuwasaidia wakulima wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na vipuri, ni kweli matrekta haya kidogo yalikuwa na changamoto ya vipuri kwa sababu ni mapya na ile kampuni ya URSUS ilikuwa bado inaendelea kuleta baadhi ya spare. Kwa hiyo, hili nalo tunalifuatilia kuhakikisha kwamba matrekta haya yanaendelea kuwa na vipuri ili pale ambapo yanapata hitilafu au yanaharibika, basi angalau vipuri vya kurekebisha hitilafu hizo vinapatikana.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi. Swali la kwanza; uthamini wa mali na fidia ulifanyika tangu mwaka 2015, takribani miaka sita sasa wananchi wa Kata ya Mkoma Ng’ombe, Lwilo, Iwela pamoja na Mundindi hawajalipwa fidia hii ya bilioni 11.

Je, Serikali haioni kwamba, kuchelewesha kulipa fidia kwa wananchi hawa kutaiingizia Serikali gharama kubwa kwa sababu, nina wasiwasi isije tathmini hii ikaja kushuka thamani kipindi hicho wao watakachokuwa wanataka kuwalipa wananchi hawa fidia hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa kumekuwa na uhitaji mkubwa sana wa makaa ya mawe na NDC wamechukua vitalu vyote vya makaa ya mawe. Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa baadhi ya vitalu kwa wananchi wachimbaji wadogowadogo wazawa ili waweze kuchimba na kuweza ku-stimulate uchumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Mgaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, uthamini wa mali kwa ajili ya kulipa fidia ili kupisha kuendelea kutekeleza mradi huo ulifanyika mwaka 2015 na kweli wakati ule thamani ya fidia iliyokuwa imeainishwa ni bilioni 11.03.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi ni kwamba, utekelezaji wa mradi huu bado uko kwenye majadiliano. Moja ya vipengele ambavyo viko kwenye majadiliano ni kuona namna gani mwekezaji ambaye atapatikana ataweza kulipa fidia ambayo iliainishwa, lakini pia baada ya kupitiwa kutokana na hali halisi ya sasa itabainika. Kwa hiyo, ulipaji wa fidia huu nao ni sehemu ya majadiliano ambayo tunaona kwamba, mwekezaji ambaye atapata nafasi sasa kuwekeza katika eneo hili yeye pia atahusika katika kulipa fidia ambayo ilibainishwa kwa ajili ya wananchi kupisha mradi ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vitalu vya makaa ya mawe ambavyo vinasimiwa na NDC; naomba niwahakikishie kuwa ni kweli vitalu hivi kwa ajili ya maendeleo ya nchi NDC ndio inasimamia uendelezwaji wa uchimbaji katika maeneo hayo, lakini kwa ajili ya maendeleo endelevu mambo haya au biashara hizi za uchimbaji zinakwenda kibiashara zaidi. Kwa hiyo, wananchi au ambao wana uwezo kama wafanyabiashara au wawekezaji ikiwemo wananchi wa maeneo hayo wanaweza kwenda kuomba nafasi ya kushiriki katika maendeleo au uendelezaji wa uchimbaji wa makaa ya mawe katika vitalu hivi kwa kushirikiana au kupata vibali kutoka Shirika letu la Maendeleo la Taifa (NDC).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunawakaribisha na kama watakidhi vigezo na kuweza kuwa na mitaji stahiki ya kuwekeza katika maeneo haya, nadhani hakutakuwa na shida, tunawakaribisha na shirika letu liko kwa ajili ya kusaidia Watanzania.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa fursa hii. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza, moja hilo ambalo umelileta la TAKUKURU na hili la Mheshimiwa Kamonga ambalo ameliuliza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimepanga kutembelea mradi huu mara baada ya bajeti yetu, Ijumaa. Katika ratiba zangu moja ya weekend nitatembelea mradi huu na tutazungumza na wananchi kwa ajili ya kuwapa maendeleo. Kwa kweli, katika bajeti yetu ambayo tutaitoa wiki hii tutaeleza kwa kina zaidi hatua ambazo zimefikiwa katika utekelezaji wa mradi huu na lini hasa utaanza. Kwa hiyo, nitafurahi sana Mheshimiwa Mbunge tukifuatana tukaenda kuzungumza na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili la TAKUKURU. Naomba nilichukue hilo, tulifanyie kazi, tupate details hasa TAKUKURU wanafuatilia nini na katika mazingira yapi, ili tuweze kutoa jibu ambalo linaeleweka. Kwa sababu, kwa kweli, sina details za kutosha kuhusu TAKUKURU wanawakamata wananchi na kuwahoji katika masuala yapi hasa. Kwa hiyo, tunaomba tupate nafasi tulifuatilie tupate details, ili tukitoa jibu hapa tutoe jibu ambalo linaeleweka. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa haya masoko yamesimama muda mrefu, kuanzia mwaka 2013 na maelezo ya Serikali kila siku ni wanatenga bajeti: Sasa swali, Kwa kuwa haya masoko ni strategic, Serikali haioni ni umuhimu wa kushirikisha wadau binafsi katika kuendeleza haya masoko? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali imesema tangu mwaka 2019/2020 kwamba itatenga shilingi bilioni 2.9 kujenga hayo masoko, nataka commitment ya haya masoko kuanza kujengwa.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, ni kweli ujenzi wa masoko haya umesimama kwa muda mrefu tangu mwaka 2013/2014 wa mwaka wa fedha huo, kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba ilitokana na changamoto za ufinyu wa bajeti.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Mheshimiwa Innocent Bilakwate, ambaye amekuwa akiendelea kufuatia sana ujenzi wa masoko haya kwa muda mrefu na ndiyo maana tumesema tunatafuta wadau wengine ikiwemo na benki, lakini na wadau wengine ambao tulikuwa tunashirikiana nao katika kujenga masoko hayo na ndiyo maana mwaka wa fedha huu 2021/2022 unaokuja Serikali imetenga angalau shilingi milioni 500. Lengo ni kukamilisha ujenzi wa masoko hayo.

Mheshimiwa Spika, pili, ni kweli commitment ya Serikali ni kuhakikisha tunajenga masoko ya kimkakati ya mipakani kwa sababu tunajua lengo la Serikali sasa ni kuanza ku-access masoko ya nje baada ya bidhaa nyingi au mazao mengi ya kilimo Tanzania kuongezeka. Kwa hiyo, ni lazima tutafute masoko ya nje. Kwa hiyo, ni mpango mkakati wa Serikali kuhakikisha tunajenga masoko ya mpakani, lakini ku-access masoko ya nje kupitia fursa mbalimbali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; Tokyo International Conference on African Development (TICAD) pamoja na mambo mengine inahusisha nchi zote za Afrika kupeleka vijana kwenda kusoma katika vyuo nchini Japan na kupata uzoefu kwenye kampuni kubwa za nchini Japan kwa lengo kwamba wanapotoka huko waje kufanya uwekezaji hapa nchini kwa kushirikiana na kampuni hizo za Japan. (Makofi)

Kwa nini mpango huu kwa Tanzania umekoma ilhali nchi nyingine za Afrika zinzendelea kupeleka vijana Japan kujifunza? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; vijana hawa ambao tayari tumebahatika kuwapeleka Japan na wamesharejea. Serikali imewatumiaje kwa kushirikiana na kampuni sasa walikopata uzoefu huko Japan kwa ajili ya uwekezaji hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania na Japan bado wanaendelea na mipango ya kuwapa mafunzo na pia kupata uzoefu wa kazi mbalimbali kupitia taasisi zake nyingi ikiwemo JICA, lakini pia kuna utaratibu maalum baina ya Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa vijana kwenda kupata mafunzo Japan. Kwa hiyo, sio kweli kwamba tumekoma au utaratibu huo umesitishwa kwa sababu hata mwaka 2019 ambayo ni TICAD ya mwisho iliyofanyika nchini Japan baadhi ya maeneo ambayo yaliongelewa ni kuendeleza au kukuza ushirikiano wetu ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, alikuwepo kule Tokyo moja ya maeneo yaliyoongelewa ni kuona namna gani kutumia vijana wetu katika miradi mbalimbali ikiwemo kuvutia kampuni mbalimbali za uwekezaji nchini kama vile TOSHIBA, ambayo yanaweza kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kielektronic, lakini kuhusu kuwatumia vijana ambao wamepata mafunzo au uzoefu mbalimbali nchini Japan.

Mheshimiwa Spika, Tanzania bado inaendelea kuwatumia vijana hao wengi, lakini pia kwa Taarifa yako na mimi ni mmoja wa vijana hao ambao nimeweza kupata mafunzo Japan na ninaendelea kutumikia Serikali ya Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika sekta ya viwanda. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa katika majibu ya msingi Serikali imetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kujenga kongano ya kubangua korosho katika eneo la Masasi, je, ni lini ujenzi huo utaanza? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, baadhi ya viwanda vya kubangua korosho vimekuwa vikinunua korosho katika minada ya awali ili kuwezesha viwanda hivyo kubangua korosho na kuongeza thamani. Hata hivyo, imeonekana pia vimekuwa vikibangua korosho kiasi kidogo na nyingine kuuzwa ghafi. Serikali ina utaratibu gani wa kudhibiti jambo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnes Hokororo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa mfuatiliaji sana kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya korosho na hasa katika uwekezaji kwenye viwanda vya kubangua korosho.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema ni kweli Wizara na jukumu la Serikali ni kuhakikisha mazao ya kilimo ikiwemo korosho yanapata soko lakini pia yanaongezewa thamani kwa kuchakatwa katika viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto kubwa iliyokuwepo ni kuona korosho hizo zinapata wanunuzi na ndiyo maana tumeanzisha kongano au cluster ya korosho ili kuwahusisha pia na wajasiliamali wadogo waweze kushirikki katika kuongeza thamani ya zao la korosho.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilikuwa tumetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kongano hilo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka wa fedha ujao 2021/2022 kazi hii ya ujenzi itaanza kwa sababu tayari fedha hizo zimeshatengwa kwa ajili ya kujenga kongano hilo la wajasiliamali kwa ajili ya kubangua korosho kwenye maeneo ya Masasi na Mtwara.

Mheshimiwa Spika, kuhusu viwanda na kupata korosho katika minada ya awali, ni kweli ni utaratibu ambao Serikali imeuweka baada ya kuona viwanda vingi vinakosa malighafi ambayo ni korosho kwa ajili ya kubanguliwa katika viwanda hivyo. Kwa hiyo, utaratibu sasa kama alivyosema ni kweli kuna minada ya awali ili angalau viwanda hivi visikose kupata malighafi. Baada ya viwanda hivi kununua korosho hatua ya pili ni mnada ambao sasa unashirikisha na makampuni mengine.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kudhibiti viwanda hivi inategemea kwa sasabu kama kiwanda kimeshatosheka na malighafi inayohitajika katika kuchakata korosho basi wana uhuru wa kuuza nje. Kama tunavyojua Tanzania tuna competitive advantage kwa maana ya kuzalisha zaidi korosho kuliko maeneo mengine. Kwa hiyo, tukitosheka sasa katika viwanda vyetu then korosho inayobaki inaweza kuuzwa kwenye minada ya nje ambapo wanaweza kusafirisha nje kama ambavyo wanafanya sasa.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli ya uchimbaji chumvi kwenye kata ya Ilindi imekuwa ni ya muda mrefu na Halmashauri tumepanga mwaka ujao wa fedha tuweze kutenga fedha kwa ajili ya kujenga jengo ambalo sasa tutahitaji tupate mashine kwa ajili ya kiwanda kianze.

Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari aambatane na mimi baada ya Bunge hili ili kwanza akaone eneo lile na ikiwezekana kama alivyosema sasa SIDO waweze kutusaidia kiwanda kile kianze?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, Serikali imesema kwamba Kata ya Chali na Kata ya Ilindi ni kata ambazo zina chumvi pale, lakini pamoja na ile kumekuwa na tatizo la upatikanaji wa maji kwa sababu ya chumvi Kata ya Ilindi haina maji kabisa kila sehemu maji yana chumvi na Kata ya Chali nayo haina maji ina sehemu moja ambayo ina chanzo cha maji, lakini Serikali imekuwa inaahidi haijatekeleza mradi ule.

Je, Waziri wa Maji yuko tayari vilevile naye aweze kufanya ziara kwenye Kata ya Ilindi na Kata ya Chali ili aweze kuona shida inayowakabili wananchi wa kata hizi kutokana uwepo wa chumvi ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kenneth Nollo, Mbunge wa Bahi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema lengo la Serikali ni kuona tunahamamisha ujenzi wa viwanda vingi nchini ili kutumia malighafi tulizonazo, kwa hiyo, niko tayari kuambatana na Mheshimiwa Nollo ili twende kuangalia kwanza sehemu yenyewe ilivyo, lakini pia tuweze kupata taarifa sahihi na kuweza kuanza michakato ya kuona namna gani ya kuvutia wawekezaji katika kujenga kiwanda au viwanda katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la pili, ni kweli, kwa sababu kama alivyosema eneo lile lina chumvi kwa hiyo maana yake maji mengi yatakuwa ni ya chumvi. Serikali kupitia Wizara ya Maji najua wana mipango mingi, basi tutashirikiana na Wizara ya Maji ili kuhakikisha tunaona namna gani ya kuwasaidia ndugu zetu wa Bahi ili waweze kupata maji safi kwa ajili ya matumizi ya majumbani.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Manyoni Mashariki chumvi inapatikana katika Vijiji vya Mpandagani, Majiri na Mahaka.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa vijiji hivyo vitatu ili waweze kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sisi Tanzania tumebahatika kuwa na madini ya chumvi mengi kwa maana ya maeneo mengi, lakini uzalishaji wetu bado ni mdogo, ni wastani wa takribani tani 330,000 ambazo tunazalisha kwa mwaka. Kwa hiyo, kama nilivyosema, lengo la Serikali ni kuona sasa tunahamasisha viwanda vingi ili tuweze kuzalisha zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na takwimu zinatuonesha kwamba tunaweza kuzalisha mpaka uwezo wa tani milioni moja kwa mwaka. Kwa hiyo tani 330,000 ambazo zipo ni kidogo. Kwa hiyo, jimbo la Mheshimiwa Dkt. Chaya ambao nao pia wana deposit nyingi za chumvi, basi nako pia tutaona namna gani ya kuona sasa tunahamasisha viwanda vingi ili viweze kujengwa katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Chaya kwa kuwa amekuwa akifuatilia sana suala hili na mimi nimuahidi kwa niaba ya Serikali kwamba tunafanya kila liwezekanalo ili tuweze kuwa na viwanda katika Mkoa huu wa Singida, Jimboni kwa Mheshimiwa Chaya kule Manyoni Mashariki. Ahsante sana.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo Bahi linafanana kabisa na tatizo lililopo Mtwara; viwanda vingi vimekufa kikiwemo Kiwanda cha Kubangulia Korosho cha Olam ambacho kilikuwa kinatoa ajira kwa wnanachi wengi wa Mkoa wa Mtwara.

Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua viwanda hivyo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mkoa wa Mtwara ndiyo ambao unazalisha korosho nyingi hapa nchini kuliko mikoa mingine na pia kumekuwa na viwanda vingi sana vya kubangua korosho ambavyo kama nilivyosema kabla tulikuwa na viwanda 12 vya Serikali ambavyo baadaye vilibinafsishwa. Lakini kuna vingine ambavyo vimekuwa havifanyi vizuri sana na tumeweza kuvirejesha Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda hiki cha Olam anachokisema of course kimefungwa kutokana na changamoto mbalimbali, lakini moja ya changamoto kubwa ambazo zilikuwa zinakabili viwanda vyetu ilikuwa ni upatikanaji wa malighafi, kwa maana ya korosho ghafi kwa ajili ya kubanguliwa katika viwanda hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na moja ya mikakati ambayo Serikali sasa imefanya ni kuona sasa viwanda hivi vinapata malighafi katika mnada wa awali, kwamba viwanda vile vya kubangua korosho vipate malighafi zinazotakiwa, halafu baadaye sasa korosho zinazobakia ziende kwenye mnada wa kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mikakati inayowekwa na Serikali viwanda vingi sasa vitarudi kufanya kazi kwa sababu vitakuwa na uhakika wa malighafi, lakini pia na mazingira wezeshi ambayo Serikali imeanza kuyaweka ili kuvutia wawekezaji zaidi katika viwanda mbalimbali vikiwemo viwanda vya korosho katika Mkoa wa Mtwara.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Serikali iliahidi kujenga kiwanda cha kusindika chumvi Ziwa Eyasi, Nyalanja katika Jimbo la Meatu; je, ni lini Serikali itatekeleza hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba tunahamasisha ujenzi wa viwanda mbalimbali hapa nchini ikiwemo viwanda ambavyo vinachakata chumvi. Katika jimbo la Mheshimiwa Komanya katika Halmashauri ya Meatu Serikali iliahidi kujenga kiwanda kwa ajili ya kuchakata chumvi iliyopo katika Mkoa huo wa Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali kama Wizara tulipata andiko kutoka kwenye Halmashauri ya Meatu na andiko hilo tunalifanyia kazi. Lakini pia tunajua kwamba kuna taasisi moja ya Nutrition International ambayo yenyewe tayari imeshaanza kuongeza thamani chumvi inayochimbwa pale ambayo kweli soko lake lipo katika nchi za Rwanda na Burundi na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba sisi Tanzania ambao ndio tuko kwenye Ukanda huu wa Pwani pamoja na Kenya, ndio wenye deposit kubwa za chumvi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa hiyo, ni vyema sana na sisi kama Serikali tumelitambua hilo kutumia soko hili ili tuweze kuzalisha chumvi nyingi zaidi, tuweze kuuza katika masoko ambayo yanatuzunguka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutakamilisha hilo, na Serikali inaendelea kulitekeleza andiko hilo ili angalau tuweze kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho kwa kuwavutia wawekezaji wengi zaidi, lakini pia na taasisi za Serikali ambazo zinaweza zikafanya uwekezaji katika eneo la Meatu. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; wananchi wa Ludewa wangependa kufahamu kwa kuwa wamesubiria fidia hizi kwa muda mrefu. Je, kwa nini Serikali isitenganishe majadiliano na mwekezaji na suala la fidia ili wananchi wa Jimbo la Ludewa waweze kulipwa fidia mapema?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ningependa kufahamu ni lini Serikali itaanza kutoa elimu ya kuandaa wananchi wanaoathirika na miradi ili waweze kunufaika na miradi hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Jimbo la Ludewa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika mradi huu fidia kwa wananchi iliyothaminiwa jumla ya bilioni 11.037 katika majadiliano au katika mkataba ambao tuliingia na kampuni hii Situan Honda ilikuwa yeye kama mwekezaji atakuwa na wajibu wa kulipa fidia eneo hilo ambalo atakuwa analitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama nilivyosema baada ya majadiliano na mwekezaji huyu tutaangalia sasa kama tutafikia muafaka maana yake yeye atakubaliana kulipa fidia, lakini utekelezaji wa mradi huu lazima uanze mwaka 2021/2022, aidha tumekubaliana na mwekezaji huyu au hatujakubaliana lakini mradi huu lazima uanze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshaeleleza na ni utekelezaji ambao unaenda kufanyika katika mwaka wa fedha ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu katika eneo hili, ni kweli Serikali imekuwa ikiweka fedha kwa ajili ya kuelimisha wananchi namna ambavyo watashiriki katika ujenzi wa mradi huu kwa maana ya local content kwamba wao watafanya nini au watashiriki vipi katika mradi huu mkubwa wa Mchuchuma na Liganga. Kwa hiyo fedha zinatengwa kila mwaka na elimu inaendelea kutolewa kwamba sasa mradi huu ukianza naamini elimu zaidi itatolewa ili wananchi wa eneo hili waweze kushiriki katika utekelezaji wa mradi huu kikamilifu.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Tume ya Ushindani, kama zilivyo mamlaka zote za udhibiti hapa nchini, zina mamlaka ya kimahakama quasi- judicial organs. Je, Serikali haioni kuunganisha ushindani na kumlinda mtumiaji zinafifisha dhana nzima ya ushindani na inafifisha dhana nzima ya kumlinda mtumiaji wa Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Dhana ya mtumiaji hapa nchini inaakisiwa kwenye sheria mbalimbali ambazo hazina dhana nzima ya kumlinsda mtumiaji na kuakisi haki nane za mtumiaji kama zilizvyoainishwa na Umoja wa Mataifa. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kutunga sheria, a standalone law ya kumlinda mtumiaji wa Kitanzania?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli FCC au Tume ya Ushindani inasimama kama tume ambayo inahusika kama ya kimahakama, kwa maana ya quasi-judicial organ na ndiyo maana katika majukumu yake yale mawili ya kulinda ushindani pamoja na ya kumlinda mlaji tumeamua sasa ile National Consumer Advocacy Council ambayo ilikuwa ni sehemu, kama section katika taasisi hii ikae sasa independent ili sasa tuwe na uhakika kwamba, mlaji anasimamiwa ipasavyo badala ya kuwa chini ya Tume hii ya Ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, miongoni mwa majukumu ambayo tunaenda kufanya, sasa tunataka tuanze kutunga sera ya kumlinda mlaji; na ndani ya sera hiyo sasa tutatengeneza pia sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, kama nilivyosema, pia ili kumlinda mlaji maana yake sasa tunataka tuwe na sheria ambayo yenyewe moja kwa moja itahakikisha inasimamia kumlinda mlaji tu ikiwa nje ya FCC ambayo inafanya majukumu mawili ya kusimamia ushindani, lakini pia na kumlinda mlaji.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali, lakini pia labda nieleze kidogo; mnamo tarehe 1 mwezi wa Kumi mwaka jana 2020 tukiwa katika kampeni Waziri Mkuu aliahidi ujenzi wa soko hili pale Nyakanazi na tarehe 11 mwezi wa Pili wakati akijibu Maswali ya Papo kwa Papo, swali lililoulizwa na Mheshimiwa Neema Lugangira aliahidi pia ujenzi wa soko hili na akataja kabisa ni soko la kimkakati na akataja value yake kama ni 3.5 billion.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye majibu ya Serikali wanasema wanahamasisha Halmashauri ya Biharamulo ili iweze kufanya ujenzi wa soko hili; hili soko limetamkwa, ukisema 3.5 billion kwa Halmashauri ya Biharamulo wajenge soko hili, labda litakaa zaidi ya miaka kumi, kwa sababu uwezo huo hatuna; na ilitamkwa humu ndani ya Bunge: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate commitment ya Serikali kwanza nijue financing ya soko hili itafanyika vipi? Sisi uwezo huo hatuna. Kwa hiyo, nipate majibu ya Serikali kama Serikali kuu itafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu soko hili ni muhimu kwa ajili ya kufungua ukanda wetu na ni soko la kikanda litakalohudumia nchi za Kongo, Burundi, Rwanda na nchi nyingine zote za Jirani: nipate majibu ya Serikali, ni lini ujenzi wa soko hili utaanza? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali ina mkakati na mipango mbalimbali ya kuhakikisha inatekeleza ahadi ambazo viongozi wa Serikali wanaahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Chiwelesa kwa ufuatiliaji mkubwa anaofanya kwa ajili ya maendeleo katika Jimbo lake la Biharamulo Magharibi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli masoko haya ya kimkakati na hasa masoko ya pembezoni ambayo yako katika mipaka ya nchi za jirani na hasa hizi za Kongo, Rwanda na Burundi ni masoko ambayo yana umuhimu sana kuyaendeleza ili yaweze kuleta maendeleo ya nchi, lakini kuwapatia kipato wananchi wanaokaa katika maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kupitia programu ya ASDP II ambayo pia imeweka ule mfumo wa O and OD ambao ni fursa na vikwazo kupitia utaratibu huo, Halmashauri zinahamasishwa kuangalia vyanzo mbalimbali vya ku-finance mipango yao, mikakati yao katika kuendeleza sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na TAMISEMI tuna mikakati mbalimbali ambayo pia kupitia humo tunaweza kujenga masoko haya kulingana na fedha zinazvyopatikana. Nakushukuru sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, japokuwa majibu ya Serikali zijaridhika nayo sana, lakini kwa kuzingatia kuwa Kassim Faya Nakapala Mwenyekiti wa Halmashauri na Ebeneza Emmanuel Katibu wa CCM wa Wilaya wako hapa kufuatilia miongoni mwa mambo mengine jambo hili na Diwani wa Kata husika Fatma Mahigi wa Mang’ula “B” kwamba eneo hili sasa limekuwa hatarishi sana ni eneo ambalo lina ekari takribani 250 na akina mama wameshaanza kubakwa. Naomba kuiuliza Serikali maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza Serikali ipo tayari kuweka ulinzi wakati huu inatafuta mwekezaji wa kuwekeza katika Kiwanda hiki cha Machine Tools?

Lakini pili naomba kuiuliza Serikali sasa hivi tunajenga reli ya kisasa ya SGR na hii reli ya kisasa itahitaji mataruma na kadhalika, kwa nini wasikabidhi eneo hili na kiwanda hiki kwa SGR ili iendelee kutumia kuzalisha vifaa vya reli? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana ndugu yangu Asenga kwa ufuatiliaji kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo lake na hasa katika sekta ya viwanda na kwa ajili ya ufufuaji wa kiwanda hiki cha Mang’ula Machine Tools.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli eneo hili limekuwa kwa muda mrefu halitumiki kama nilivyosema kwa sababu mwekezaji aliyepewa eneo hili kuliendeleza hajaliendeleza kwa muda mrefu, nichukue nafasi hii kumuahidi kwamba tutashirikiana na Halmashauri kuona namna bora ya kuweka ulinzi ili eneo hili lisiwe hatarishi kwa sasa ambapo bado hatujapata mwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili kama nilivyosema tunaangalia matumizi bora ikiwa ni pamoja na kutafuta wawekezaji ambao wataweza kutumia eneo hili kwa ajili ya kuwekeza viwanda, tuchukue pia hoja ya Mheshimiwa Mbunge kwamba kama wenzetu wa reli ya kisasa watataka kutumia eneo hili kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kutumika katika SGR basi nao tutawakaribisha, ahsante sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniruhusu kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa kiwanda hiki kipo katika eneo la kimkakati kwa sababu kimezungukwa na mashamba ya miwa ama eneo ambalo linalima miwa kwa wingi, na kwa kuwa kulikuwa na mpango wa ku-transform kiwanda hiki kwenda kuzalisha sukari.

Je, Serikali inatoa tamko gani ikizingatiwa kwamba sasa hivi kuna mpango wa kuboresha viwanda vidogo vidogo vya kuzalisha sukari?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ukanda huu wa Kilombero ni ukanda ambao tunaweza tukasema ni wa kimkakati kwa uzalishaji wa miwa na sukari kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya hapa nchini. Ni kweli ni moja ya azma ya Serikali kuhamasisha au kuvutia wawekezaji wengi katika kuchakata miwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi tunatafuta wawekezaji mahiri ambao watajitokeza kuwekeza katika eneo hili ikiwemo wale ambao watataka kuchakata miwa basi na sisi tutawakaribisha ili kutumia nafasi hiyo katika eneo hili la Machine Tools kama sehemu ya kuwekeza viwanda vya kuchakata miwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tupo tayari na tusaidiane na Wabunge ili tuweze kuwekeza katika maeneo haya kwa umahiri zaidi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kwenye jibu la msingi Naibu Waziri amesema kwamba magunia ya katani ni ya adimu na yanahitajika sana; na kwa kuwa Mkoani Kilimanjaro ikiwemo Same, Mwanga ni wakulima wazuri wa katani lakini katani hiyo haipati namna ya kuhifadhiwa. Je, ni kwa nini Serikali haioni uharaka sasa kuzungumza na Mohamed Enterprise ambaye pia alimiliki mashamba hayo na akamiliki kile kiwanda ili waweze kutengeneza magunia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ametutajia kuwa kuna viwanda nane na vitatu ndiyo vipo active lakini magunia haya yanatumika kwenye kuweka kahawa na Mkoa wa Kilimanjaro unalima kahawa na magunia wanaagiza kutoka nje. Je, Serikali inasema nini kuhusu hilo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema ni kweli kuna changamoto katika zao la mkonge kwa maana ya uchakataji. Sasa hivi Serikali inafanya juhudi kwanza kuongeza uzalishaji wa mkonge kwa maana ya malighafi, lakini pia kuhakikisha wazalishaji kwa maana ya wachakataji kwenye viwanda wanaendelea. Ndiyo maana tumesema moja ya kazi tunazozifanya ni kuwapa vivutio maalumu ikiwemo kuwalinda wazalishaji wa ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimueleze tu Mheshimiwa Shally Raymond kwamba huyu mwekezaji METL kwa maana Mohamed Enterprise tayari tumeshaanza kumpa baadhi ya mikataba kwa ajili ya kuzalisha vifungashio kwa maana ya magunia hayo katika zao la korosho. Hii ni mojawapo ya mipango ambayo tunadhani kwa sababu ana uhakika wa soko maana yake atapata mtaji na kuendelea kuzalisha kwenye viwanda hivyo vingine. Kiwanda cha Morogoro tayari kinazalisha tunaamini ataendelea kuzalisha pia katika kiwanda hicho cha Moshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, kama ambavyo nimesema tumeshaanza kuwapa vivutio maalum ikiwemo kuwapunguzia baadhi ya kodi kwa magunia haya ambayo yanaenda kufanya kazi kwenye vifungashio katika mazao ya kilimo. Kwa hiyo, ameanza na korosho tunaamini akiendelea kuzalisha sasa ataenda kwenye vifungashio kwa ajili ya zao la kahawa na mazao mengine. Nakushukuru.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kwenye Jimbo la Same Mashariki, Kata ya Ndungu pamoja na Kata ya Mahore kuna mashamba makubwa ya kilimo cha mkonge lakini anayemiliki mashamba hayo haonyeshi kujali zao lile.

Je, Serikali mnasema nini katika hilo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema moja ya mikakati ya Serikali ni kujihakikishia kuwa tuna malighafi za kutosha ambazo zitaenda kuchakatwa kwenye viwanda vyetu ambavyo tunavihamasisha kuanza kuvifufa sasa.

Kwa hiyo, moja ya mikakati ambayo tumeshaweka kupitia Wizara ya Kilimo ni kuwapa mikakati au kuhakikisha hawa wakulima wanaendeleza sasa haya mashamba ya mkonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hata hawa wa Same nakuahidi na Wabunge wapo hapa tunaendelea kujadiliana nao lakini kuhakikisha wanaenda kufufua mashamba hayo ili aweze kutoa raw material au malighafi kwenye viwanda ambavyo tunaendelea kuvifufua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru kwanza kwa majibu ya Serikali juu ya zao letu hili la mchikichi ambalo linazaa mafuta ya mawese. Kwa kweli mchikichi ni zao la kipekee sana Kitaifa na Kimataifa, na sisi pia tunategemea tukiona zao hili likiweza kuwanufaisha wananchi wa Kigoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 19 Desemba, 2020 Mheshimiwa Waziri Mkuu alikaa na wadau wa zao hili pale Kigoma ndani ya Ukumbi wa NSSF. Mojawapo ya mambo watu hawa waliomwambia wanahitaji kuona yakifanyiwa kazi ni Bodi ya Mawese na vifungashio maalum.

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa Makanika.

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua sasa ni nini mkakati wa Serikali ulipofikia katika kutekeleza mambo haya ambayo walimwomba Waziri Mkuu yafanyiwe kazi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Assa Nelson Makanika, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, moja ya mikakati ambayo tunatekeleza ni kuanza sasa kutatua changamoto hizo, lakini zaidi tumeshaunda timu ya wataalam baada ya maelekezo ya Waziri Mkuu, wakati huo tumeshaunda timu ya wataalam kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na Kilimo ambao sasa wataandaa guidelines kwa ajili ya vifungashio kwenye mazao haya ya kilimo na bidhaa zake, mazao yote ikiwemo ya mawese.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la bodi, nadhani hili tunalichukua kama moja ya vitu vya kufanyia kazi kama Serikali ili tuweze kuona kama kuwepo kwa Bodi ya Michikichi ni moja ya suluhisho, basi nalo tutalifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Changamoto ya vifungashio ambayo ipo kwenye mawese ni sawasawa na changamoto ambayo ipo kwenye zao la viazi kule Makete, Mbeya na sehemu nyingine na Serikali ilituahidi.

Je, ni lini vifungashio rasmi vya viazi vitapatikana kwa wananchi wa Makete, Mkoa wa Njombe, Mbeya na sehemu nyingine ili tuondokane na changamoto ya lumbesa ambayo imekuwa ikisumbua kwa muda mrefu hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Sanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema hiyo timu ambayo tumeiunda tumeshawapa deadline, kama ambavyo pia umesema, ndani ya mwezi mmoja waje na mkakati au mpango ambao utaweza kutatua changamoto hii. Kama nilivyosema, si kwa zao moja tu la viazi au michikichi na mazao mengine yote. Kwa sababu changamoto ya lumbesa iko katika mazao mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lumbesa ni tatizo pale ambapo inazidi vipimo ambavyo vimekubalika katika zao husika. Kwa mfano katika hali ya kawaida tunasema gunia moja liwe kati ya kilo 95 mpaka 105, kwa hiyo zaidi ya hapo inakuwa ni shida. Sasa inaweza kuwa kifungashio ni kidogo kiasi kwamba ikaonekana kama ni lumbesa lakini kiko ndani ya uzito unaokubalika. Hata hivyo, tunachukua changamoto hizi, kama nilivyosema, Kamati hii itakwenda kuweka sasa mkakati au guidelines maalum kwa ajili ya kupata vifungashio specific kwa mazao maalum likiwemo hili la viazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri, Tanzania Bureau of Standards na Bureau of Standards zote ulimwenguni kazi yake ni kulinda na kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingia nchini na zinazozalishwa ndani ya nchi.

Je, utakubaliana nami kwamba, TBS haipimwi kwa kiasi cha pesa inazoingiza nchini, kutokana na jibu lako ulilonijibu katika swali langu la msingi?

Swali la pili; kuna wale ambao wanashindwa kulipia yale magari, kwa kushindwa huko kulipia yale magari inabidi yale magari mtueleze mnapeleka wapi yale magari? Hamuoni kwamba, Tanzania mnataka kuigeuza kuwa dumping area? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Mgaya, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Neema kwa ufuatiliaji wa siku nyingi kuhusiana na ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini. Ni kweli, kazi ya msingi ya TBS ni kuhakikisha na kudhibiti ubora wa bidhaa zote zinazoingizwa nchini ndiyo maana tumeamua sasa ili kuwa na ufanisi katika hilo kukagua sisi wenyewe kwa sababu kama nilivyosema katika jibu la msingi, baadhi ya mawakala huko nje walikuwa hawafanyi kazi ipasavyo na malalamiko bado yalikuwa mengi sana kwamba kuna baadhi walikuwa wanaletewa bidhaa ambazo hazina ubora lakini kwa sababu tayari mawakala walikuwa wamethibitisha kwa hiyo maana yake TBS ilikuwa haina namna ya kufanya.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa sababu sasahivi tunathibitisha wenyewe, pia tumeshawaambia makampuni yanayoleta bidhaa nchini kuhakikisha wanaleta bidhaa ambazo zina ubora. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Neema kwamba kazi hiyo inafanyika na ndiyo maana tunaamua kujiimarisha sasa ili TBS waweze kufanya kazi hiyo kwa uthabiti.

Mheshimiwa Spika, pili, kuhusu ubovu wa bidhaa au magari yaliyotumika yanayoingizwa nchini, kama nilivyosema mpaka sasa zaidi ya wateja hao 13,968 ambao wameingiza magari nchini hakuna hata mteja mmoja ambaye amelalamika kuhusiana na ubovu wa magari au bidhaa zinazoingizwa. Kwa hiyo, tunaamini sasa mfumo huo utaenda kuboreshwa zaidi kwa maana ya kukagua kwa ubora zaidi na tunawaelekeza wateja wetu kuhakikisha wanaingiza bidhaa kupitia makampuni ambayo tumekubaliana ambayo yanatoa bidhaa hizo kutoka nje. Ninakushukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Naibu Waziri, sijaridhika na majibu yake. Kwa taarifa rasmi zilizopo ni kwamba, viwanda hivi pamoja na mashamba viko chini ya Msajili wa Hazina. Msajili wa Hazina pamoja na Wizara ya Fedha ndiyo wanaotakiwa kuwalipa wafanyakazi hawa.

Mheshimiwa Spika, naomba kusikia commitment ya Serikali. Je, ni lini wafanyakazi hawa 502 watalipwa na Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Viwanda hivi vinaenda sambamba na mashamba yale maua na mbogamboga. Mashamba haya na viwanda ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Arusha pamoja na sekta hii ya maua na mbogamboga.

Naomba kujua Serikali ina mikakati gani wa kuyafufua mashamba haya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kuongezea majibu mazuri ambayo amejibiwa na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, siyo sahihi kwamba Serikali ndiyo inapaswa kulipa madeni haya, kwa sababu kama ambavyo ameeleza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Viwanda kwamba TIB ilipewa dhamana ya kuhakikisha kwamba inarudisha fedha ambazo Kiliflora ilikuwa imekopeshwa. Fedha hii ilirudishwa kupitia mnada ambapo Serikali ilinunua mashamba yale kihalali, lakini hawa ambao wanadai wanadai vitu viwili vikubwa: Kwanza wanadai malimbikizo ya mishahara kwa kampuni ambayo ilikuwa imewaajiri pamoja na mafao.

Mheshimiwa Spika, haya ni madai ambayo yanapaswa kulipwa na mwajiri ndiyo maana hata katika kesi waliyofungua walimshitaki muajiri na Mahakama kupitia Tume ya Usuluhishi wakatoa maamuzi kwamba, hii kampuni iwalipe kwa hiyo, maamuzi tayari yalishatoka kwamba, kampuni hii ndiyo inapaswa kuwalipa hawa wadai.

Mheshimiwa Spika, nawashauri hawa wadai kwamba pengine wangeweza kuwasiliana na vyombo vya dola ili waweze kuwasaidia kuwatafuta hawa wanaowadai waweze kuwalipa mali yao.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na namna ambavyo mashamba haya yataendelezwa kwa sababu, mashamba haya sasa hivi yapo tayari kwa Serikali, kuna mikakati mikubwa ya kuhakikisha kwamba tunaimarisha sekta ya kilimo kupitia rasilimali mbalimbali ambazo zinamilikiwa na Serikali, yakiwepo mashamba haya, lakini kwa kuwa, sasa hivi muda ni mfupi siwezi kueleza mikakati hiyo ambayo iko chini ya benki ya TIB kwa kirefu.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo Mheshimiwa Mbunge nitakupatia baadae. (Makofi)