Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dorothy George Kilave (19 total)

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza niishukuru sana Wizara ya Maji kwa sababu Jimbo letu la Temeke maji yamefika karibu kila kata. Tatizo letu kubwa ni kwamba bomba lile kubwa limepita katika barabara kubwa lakini kuvuta maji kwenda ndani ya nyumba zetu ambapo miundombinu siyo mizuri sana kwenye Kata za Buza na Kilakala na nyumba ziko mbali. Niombe Wizara ya Maji tunapoomba kuvutiwa maji ndani ya nyumba zetu, fedha ile ambayo tunatakiwa kuilipa kidogo ni kubwa, sasa mfikirie tuweze kuvuta kwa nusu ya bei halafu muendelee kutudai ndani ya malipo ya kila mwezi kama vile tunavyofanya luku ili tuweze kuona kila mmoja sasa anapata maji ndani ya nyumba yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU SPIKA: Hilo ni ombi, nadhani utakuwa umeliandika Mheshimiwa Waziri.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Waziri, lakini naomba sasa niseme kwamba sasa ni miaka karibu saba tangu mmelitwaa hili eneo.

Je, haiwezekani kwamba mtachukua tena miaka saba kwa ajili ya kulirekebisha na kuweka mpango huo? Niombe basi kama nilivyosema kwamba wananchi wa Temeke tunatamani kujenga shule za sekondari na msingi kwa sababu tunazaliana sana na maeneo mijini sasa hivi hakuna. Niseme tu kwamba tuombe sasa Wizara yako itupe eneo hili ili sisi katika miaka hii ambayo tumeambiwa tujenge shule za sekondari pamoja na msingi basi tuyapate kwa sababu naona mtakwenda tena miaka saba ijayo katika kutengeneza hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; je, Serikali yetu sasa ina mpango gani wa kumalizia fidia kwa wananchi wa maeneo ya jirani karibu na pale ambapo mmetwaa lile eneo lakini yapo maeneo Shimo la Udongo ambapo mlitakiwa kuyatwaa lakini bado hamjalipa fidia. Naomba maswali yangu haya mawili tuweze kujibiwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nomba kujibu maswali mawili ya ziada ya Mheshimiwa Dorothy kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie hatutachukua miaka saba tena. La pili ni kwamba eneo lile ni karibu kabisa na Bandari ya Dar es Salaam na sisi kama Taifa tumekuwa mara nyingi tukijadiliana namna gani kuifanya bandari yetu kuwa effective na efficient na ili iweze kuhudumia waagizaji na wasafirishaji wa bidhaa. Itakuwa ni makosa ya kimkakati tukiligeuza eneo ambalo halizidi mita 500 au 1,000 kuligeuza kuwa eneo la shule. Nataka tu nimshauri yeye na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Meya wake wa zamani yumo ndani ya Bunge hili ujenzi wa sekondari sio lazima tujenge kwenda…, tuna uwezo wa kujenga maghorofa kwa hiyo nawashauri Manispaa ya Temeke mjenge shule kwa mfumo wa maghorofa na ninyi mna mapato mengi kuliko Manispaa nyingi katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kuhusu fidia katika eneo lile tumebaki nadhani kaya kama mbili au tatu ambazo hazijamaliziwa fidia katika eneo la Kurasini na wale wananchi hawakuwa tayari, lakini wako katika hatua za mwisho kumalizana nao na watalipwa haki yao. Mpango wa Serikali katika lile eneo, eneo la ukubwa wa ekari 20 tunajenga The First Agricultural One Stop Centre ili mazo yetu ya kilimo hasa ya mbogamboga na matunda yaweze kusafiri kupitia Bandari ya Dar es Salaam badala ya sasa yanavyotumika kupitia bandari za nchi zinazotuzunguka.

Kwa hiyo, tunawaombeni sana watu wa Temeke mtuunge mkono kufikia azma hii ili eneo lile liweze kutusaidia kutatua changamoto ya usafirishaji wa mazao na kugeuza kuwa ni export hub eneo lile. Nashukuru.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nawapongeza kwa jinsi ambavyo wameweza kutujengea vituo vya afya viwili; cha Buza pamoja na Malawi na vyote vimemalizika katika Halmashauri yetu ya Temeke. Sasa nauliza:-

Je, vifaa tiba vitaingia lini; kwa sababu sasa ni muda mrefu hatujapata vifaa hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba vituo vya afya vikiwemo vya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke vimekamilika na kuna changamoto ya vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha ujao tutakwenda kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha vituo hivi vya afya vinapelekewa vifaa tiba. Katika swali langu la msingi nimesema, katika mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi bilioni 26 zimeshatolewa tayari; na shilingi bilioni 15 vifaa tiba vimeshapelekwa kwenye vituo vya afya vilivyojengwa kwenye awamu ya kwanza na ya pili; na shilingi bilioni 11 zipo katika hatua za manunuzi kwa ajili ya kupeleka vifaa tiba katika vituo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vituo vya Afya hivi vya Temeke vilijengwa awamu ya tatu na awamu ya nne, kwa hiyo, vitakuwa katika mpango wa bajeti wa mwaka 2021/ 2022. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo litaendelea kufanyiwa kazi. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami siko mbali sana. Madhara yaliyopo katika Jimbo la Mbagala ni sawa sawa na Jimbo langu la Temeke.

Nimeona hapa Shule nyingi za Sekondari zimeenda kujengwa Mbagala, lakini Temeke bado tuna kiu; kama nilivyosema siku zote, Temeke tunazaliana sana na sasa tuna watoto wengi wa Darasa la Kwanza. Tutakapofika mbali, naamini kabisa sekondari hizi zilizopo haziwezi kutosha hasa kule Vituka, Tandika, Kurasini, Mtoni, Temeke 14, kote tunatamani sekondari hizi ziwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kwamba kama atakwenda naye Mbagala, basi twende pamoja na Temeke tufike. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, namuahidi Mheshimiwa Mbunge naye kwamba tutakavyopanga safari ya Pamoja, Mbunge wa Mbagala pamoja na Mbunge wa Temeke tutakwenda. Niliainisha Kata za Mbunge wa Mbagala na wewe tutakwenda wote katika maeneo ya Vituka, Tandika, Kurasini, Temeke 14, kuhakikisha tunafanya kazi ya wananchi. Nanyi wote mnafahamu, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuondoa tatizo la Madarasa nchi nzima, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza, je, ni lini Serikali itaweza kutuongezea transformer nyingine kwenye Jimbo la Temeke kwani tuna mahitaji ya megawatt 117, lakini sasa hivi tunatumia megawatt 32. Je, tutapata lini transformer hii nyingine? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilave, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Jimbo la Temeke pamoja na Mbagala na Mkuranga tumelazimika kuongeza vituo vitatu katika kila wilaya kwa ajili ya kuongeza transformer za megawatt 48 kila mahali, kwa hiyo Temeke, Mbagala pamoja na Mkuranga tunaongezea transformer ya megawatt 48 kila eneo. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Temeke, hasa Jimbo la Temeke, naomba kuuliza: Je, ni lini sasa umeme utakamilika kwenye Jimbo letu la Temeke? Kwani hata kabla ya mgawo tulikuwa hatupati umeme; na sasa pia hatupati umeme kwa masaa mengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Temeke wanataka kujua; je, ni lini sasa kutakuwa na ukamilifu wa umeme kwenye Jimbo letu la Temeke? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy Kilave, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwa kuna outage kadhaa ndani ya Jimbo la Temeke. Sababu ya kukatika kwa umeme mojawapo ilikuwa inasababishwa na ujenzi wa barabara ya BRT ambapo tumekuwa tuna schedule ya kukata umeme katika siku ya Jumanne na Alhamisi kwa ajili ya kupisha uhamishaji wa nguzo kwa ajili ya utengenezaji wa barabara hii. Pia zoezi hilo limekuwa likiendana pamoja na kuhamisha ile miundombinu ya umeme kuipitisha chini ya ile barabara na kuweza kuweka mazingira mazuri ambayo yatakuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo linakwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya umeme katika Jimbo la Temeke na mkoa mzima wa Dar es Salaam kwa kujenga vituo vya kupoozea umeme na kuviongeza nguvu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika muda mfupi ujao kama nilivyojibu juzi, kwamba tutakuwa tumeweka vizuri mazingira ya umeme kwenye Mkoa wetu wa Dar es Salaam na katika maeneo mengine kwa kurekebisha miundombinu mbalimbali. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini naomba niongeze maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imefanya jitihada kuweza kuleta Walimu, lakini utaona kwamba, asilimia 71 ni kubwa sana kwa jimbo letu la Temeke au Wilaya nzima ya Temeke. Sasa je, Serikali haioni kwamba, inaweza kufanya jitihada za ziada ili kuweza kupata vibali kwa halmashauri zetu kuweza kuajiri Walimu kwa mikataba, hao wa sayansi ili tuone kwamba, elimu sasa inaendelea mpaka hapo Wizara itakapokuwa imepata namna ya kuweza kuajiri?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuhusiana na vifaa katika sekondari zetu, je, bado haionekani ya kwamba, tunaweza tukapata vibali hivyo tukaweza kununua vifaa hivi kwa ajili ya maabara zetu, badala ya kusubiria wadau na sisi tuna fedha katika manispaa zetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, Serikali imeendelea kufanya jitihada za makusudi, ili kupunguza pengo la upungufu wa Walimu wa sayansi katika shule zetu za sekondari, lakini mikataba ya ajira kwa watumishi wa umma; tayari Serikali ilishaandaa modal ya mikataba kwa halmashauri zetu kuajiri watumishi kwa mkataba kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri.

Kwa hiyo, kibali kilishatolewa na watumishi wote wa sekta ya afya, sekta ya elimu na wengine ambao halmashauri kwa uwezo wa mapato ya ndani wana uwezo wa kuwalipa mishahara kwa mikataba, kibali kilishatolewa na tunatia shime kwamba, waendelee kutumia fedha za mapato ya ndani kuajiri watumishi kwa ajili ya kupunguza pengo la upungufu wa watumishi hao.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na vifaa vya sayansi kwa shule za sekondari, nalo linafanana na jibu langu la kwanza kwamba, mapato ya ndani ni sehemu ya fedha za Serikali kwa hiyo, kazi yake ni pamoja na kutatua changamoto zikiwemo za upungufu wa vifaa vya sayansi katika shule zetu. Kwa hiyo, lazima halmashauri zitenge fedha hizo ili kupunguza mapengo ya vifaa hivyo. Nakushukuru.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, swali langu mimi ni, kule Temeke Kata ya Sandali, kuna jengo kubwa sana ambalo mmelijenga la zimamoto, lakini mpaka sasa halijamaliziwa wala hakuna vifaa vyovyote ambavyo vimeingizwa kwa ajili ya zimamoto.

Je, ni lini sasa vifaa hivi pamoja na jingo lile litamalizika kwa ajili ye Serikali yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nalifahamu amelizungumzia suala hilo la eneo la Mchicha majuzi, tutalipa kipaumbele kwa interest ya watu wa Dar es Salaam, uchumi wao na shughuli nyingi za kiviwanda zinazotekelezwa ili kuwawezesha Fire kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nina swali dogo la nyongeza kuhusiana na barabara inayotoka Mbagala kuelekea Temeke kutokea Kilungule - Mbagala kupitia Buza Kwa Mpalange; ni lini sasa itakamilisha ile lami? Kwa sababu wananchi wanapiga kelele sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara zetu nyingi za TANROADS na TARURA zinaingiliana. Lakini nitumie tu nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba azma ya Serikali ni kuzijenga barabara zote kwa kiwango cha lami na kwa kuwa barabara zimeshaanza kujengwa, tunamhakikishia kwamba Serikali itazikamilisha hizo barabara, ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itarekebisha au kupunguza bei ya huduma ya upasuaji hasa ya uzazi katika hospitali za rufaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha inatoa huduma ambazo zinaendana na gharama kwa maana ya kupunguza gharama za matibabu na hasa eneo la upasuaji. Katika hospitali za Rufaa za Mikoa, bado gharama za upasuaji ni changamoto na tumekubaliana na Wizara ya Afya, pia katika maeneo ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Vituo vya Afya na hospitali za Halmashauri, bado gharama za upasuaji ni kubwa. Kwa hiyo, tunapitia lakini baada ya muda tutatoa gharama ambazo zitakuwa zinafikika kirahisi kwa wananchi wetu. Ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Ili kuepusha hii migogoro: Je, ni lini sasa Serikali itaweza kwenda kuweka mipaka halisi ya ile sehemu ili tuendelee na shule kwa sababu mgogoro huu umekuwa ukijirudia mara kwa mara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nawaagiza Halmashauri ya Temeke kwamba baada ya rufaa hii kwisha, mara moja waanze mchakato wa kuweka mipaka halisi ili watu wasiende kuvamia hilo eneo. Kwa hiyo, mchakato uanze mara moja kuanzia sasa.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana swali langu dogo tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na magari mengi ambayo mmeyatuma yatakuja kwa awamu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutenga fedha za kutengeneza magari yaliyopo ambayo ni mengi tunayaona yapo katika vituo vingi vya Polisi ni mabovu. Sasa ni wakati mzuri labda muweze kutenga fedha ili tuweze kutengeneza haya yaliyopo tukisubiri hayo mageni, nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilave Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hoja yake ni ya msingi lakini nimhakikishie kwamba tumekuwa tukifanya hivyo na hata ndani ya Jeshi la Polisi tuna kitengo maalum kwa ajili ya matengenezo ya magari ya Polisi yale ambayo yanaweza kutengenezeka tunafanya hivyo na tutaendelea kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo tunafikiria kuja na mpango mwingine ambao utasaidia sana kuweza kutatua changamoto ya ubovu wa magari, nadhani wakati tutakapokuja kuwasilisha bajeti yetu hapa tutakuwa na nafasi pana zaidi ya kuweza kufafanua, lakini nimpongeze kwa wazo lake ni zuri na tunaendelea kulifanyia kazi na tutazidi kuliboresha zaidi.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali langu, ni lini sasa kituo cha afya kinachoitwa Malawi kilichopo Yombo Vituka kitapata maji? Tumepata vifaa vizuri sana vya ndani ya hospitali lakini maji tunayotumia ni ya visima, leo na tuko mjini.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kilave, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kutoa huduma ya maji katika maeneo kama ya hospitali, shule ni moja ya vipaumbele vyetu.

Kwa hiyo maeneo haya ambayo bado yanatumia maji ya visima tunatoa kipaumbele na tutahakikisha kwenye kituo cha afya tutapeleka maji safi na salama bombani kwa lengo la kuona kwamba wanaendelea kuishi kwenye karne ya mama Samia kwa sababu Serikali ya Mama Samia imeweza kutoa fedha nyingi kwenye miradi ya maji.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza swali, ni lini sasa barabara inayotoka Chang’ombe kupitia DUCE mpaka Mgulani mtamalizia, kwa sababu sasa hivi malori ni mengi sana ambayo yanapeleka vifaa viwandani na njia haipitiki sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, labda tu nichukue nafasi hii kumuhimiza mkandarisi lakini pia na Meneja wa TANROADS kuhakikisha kwamba barabara hii inakamilishwa haraka. Mheshimiwa Mbunge kama kutakuwa na changamoto ya ziada naomba tuonane nae ili tuweze kutatua hiyo changamoto kama ipo kwa upande usimamizi ama kwa mkandarasi mwenyewe. Ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali, pamoja na yote hayo utaona kwamba Hospitali ya Temeke sasa hivi ni hospitali ya Kimkoa. Kwa nini, sasa basi isiwe muhimu kituo hiki cha afya cha Malawi kipandishwe nakuwa Hospitali ya Temeke kwa sababu ile ya Temeke ni ya Kimkoa sasa hivi?

Swali la pili; Je, ni lini sasa Serikali itatutengea fedha ili tuweze kujenga mochwari katika kituo hiki cha Malawi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dorothy Kilave Mbunge wa Jimbo la Temeke kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Dorothy Kilave kwa namna ambavyo anawasemea kwa dhati kabisa wananchi wa Jimbo la Temeke, nimhakikishie kwamba katika utaratibu ambao Serikali inaendelea kuufanya kila Halmashauri lazima iwe na hospitali ya Halmashauri, ni kweli kwamba hospitali ya Temeke ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa hiyo taratibu zitafanyika kufanya tathmini ya kituo cha afya cha Malawi kama eneo linatosheleza ili miuondombinu iongezwe ili baadaye iweze kupandishwa hadhi kuwa hospitali ya Halmashauri ya Temeke.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na jengo la mochwari tumeelekeza Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ianze kutenga fedha kwenye mapato ya ndani, ili ijenge jengo la kuhifadhia maiti na huduma hiyo iweze kuwa bora kwa wananchi wa Temeke.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, siko mbali sana na swali alilouliza mtu wa Mbagala kwa sababu kata ulizozitaja ndiyo mtandao huo huo wa Kata ya Buza, Makangarawe, Sandali na Vituka. Tunaomba na sisi maji haya yaweze kusambazwa kule kwetu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba niseme nimepopkea, maji yatafika.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini nilitaka kujua ni mpango upi wa kupunguza kabisa gharama hasa za mama mjamzito anapojifungua kwa operesheni, ambapo Temeke tunalipa laki mbili kwa operesheni na Vituo vya Afya ni shilingi laki moja; je, mpango huo ukoje wa kupunguza kabisa gharama hii?

Swali la pili; je, kuna mkakakti gani wa kufanya ili sasa Serikali itoe vifaa vile ambavyo akina mama tunapokwenda kujifungua tunaambiwa tununue pamba viwembe vile na kadhalika.

Je, Serikali ina mpango mkakati gani sasa wa kuweka vile vifaa ndani ya hospitali zote ili tusiweze kununua. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza kwa jinsi ambavyo anafuatilia masuala haya kwa ukaribu kwenye Jimbo lake. Niseme tu kwamba suala ni la kisera kwamba mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano hawatakiwi kulipishwa. Ninaomba Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa tuweze kushirikiana pamoja kusimamia hili takwa la kisera.

Mheshimiwa Naibu Spika, Dar es salaam kwa kweli nilitembea kwenye baadhi ya vituo vya afya na hospitali za Wilaya nilichogundua ni kwamba, unaweza ukakuta Kituo cha Afya kinapata wagonjwa wengi kuliko hata baadhi ya hospitali za Wilaya. Kwa hiyo, wakati mwingine mgao wanaoupata MSD unakuwa mdogo kiasi kwamba wanaishiwa mapema kulingana na idadi ya watu, hata kwa mwaka ni zaidi ya 160,000 watoto wanazaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini? Kwamba mgao wanaoupata MSD ni mdogo ukilinganisha na idadi ya watu, kwa hiyo tutakwenda sisi kama MSD kufanya kuhakikisha inatolewa mgao wa dawa na vifaa kulingana na idadi ya watu na siyo kuangalia kituo, aidha ni kituo cha afya au na ku-generalize.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu mkakati ndiyo huo, kwamba tukiweza kwa Dar es Salaam ambapo unakuta kituo cha afya kinapata wagonjwa kuliko hata baadhi ya Hospitali za Wilaya sehemu nyingine, tukienda kuwapa vifaa kulingana na idadi ya wagonjwa badala ya kuangalia ni status gani hospitali inayo, maana yake hawatakuwa tena na huo upungufu na pale MSD zimenunuliwa kit za kutosha kwa ajili ya akina mama kujifungua. Hivyo hilo tatizo litaenda kuisha, nafikiri shida kwako ni idadi ya watu kwa hiyo kinachopelekwa kinakuwa kidogo sana. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, mimi nina swali moja tu; kuna upotevu mkubwa sana wa maji Mkoa wa Dar es Salaam hasa kwenye Jimbo la Temeke, nadhani mabomba yale ni chakavu na ya siku nyingi.

Je, mna mkakati gani sasa wa kubadilisha yale mabomba kuweka mabomba mapya ili tusipate taabu ya maji tena?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Temeke kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Ni kweli moja ya changamoto kubwa juu ya miradi ni upotevu wa maji na tumetoa maelekezo mahususi juu ya kuhakikisha kwamba tunakarabati na kujenga miundombinu mipya ili kuhakikisha upotevu huu unakuwa katika standard.

Kwa hiyo, nataka nimhakikishie na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na DAWASA katika kuhakikisha tunakarabati na kujenga miundombinu mipya ili upotevu huu usiendelee na wananchi wahakikishe wanapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, Ahsante. Sambamba na nyumba za Walimu Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga ofisi za Walimu au kukarabati ofisi zilizopo kwa ajili ya Walimu na kuweka samani zake ndani ya ofisi hizi, hasa katika Jimbo letu la Temeke? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy Kilave Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama tulivyojibu kwenye upande wa nyumba za Walimu sasa hivi moja ya mkakati wetu mkubwa ni kuhakikisha kila tunapokenga madarasa tunaweka na ofisi za Walimu, kwa hiyo huo ndio mkakati wa Serikali ili kuhakikisha kwamba walimu wanakuwa na maeneo mazuri ya kukaa ambayo yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi wa kila siku. Hivyo, hilo lipo na limezingatiwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Ahsante sana. (Makofi)