Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dorothy George Kilave (6 total)

MHE. DOROTHY G. KILAVE Aliuliza:-

Serikali ilitenga eneo la Kurasini EPZ tangu mwaka 2014 kwa ajili ya uwekezaji lakini hadi sasa eneo hilo halijaendelezwa kama ilivyokusudiwa.

Je, kwa nini Serikali isirejeshe eneo hilo kwa Halmashauri ya Temeke ili lipangiwe shughuli za maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy Kilave, Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Serikali kupitia Mamlaka ya EPZ ilianza mchakato wa kutwaa ardhi eneo la Kurasini mwaka 2014 kwa madhumuni ya kujenga Kituo cha Biashara na Ugavi wa Vifaa. Hatua mbalimbali za kuendeleza eneo hilo zimefanyika zikiwemo ulipaji wa fidia, kusafisha eneo kwa kubomoa majengo yaliyokuwepo, kufanyika kwa upembuzi yakinifu wa awali na kupatikana kwa hatimiliki. Hatua inayoendelea sasa ni tathmini ya mazingira na maandalizi ya mpango kabambe (conceptual master plan) inayofanywa kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa.

MheshimiwaNaibu Spika, Wizara katika Bajeti yake ya mwaka 2020/2021 imetenga fedha kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu ya mradi awamu ya kwanza ikiwemo ujenzi wa uzio kuzunguka eneo la mradi. Tayari Mamlaka ya EPZ imeingia mkataba na Kitengo cha Ujenzi cha Jeshi la Kujenga Taifa kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa nia ya Serikali katika kutekeleza mradi huu wa kielelezo kwa mujibu wa Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa iko pale pale na pia nitumie fursa hii kuomba ushirikiano wake na Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kwa ujumla ili kufikia azma ya Serikali kupitia uendelezaji wa mradi huu kwa malengo yaliyokusudiwa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dorothy Kilave swali la nyongeza.

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Waziri, lakini naomba sasa niseme kwamba sasa ni miaka karibu saba tangu mmelitwaa hili eneo.

Je, haiwezekani kwamba mtachukua tena miaka saba kwa ajili ya kulirekebisha na kuweka mpango huo? Niombe basi kama nilivyosema kwamba wananchi wa Temeke tunatamani kujenga shule za sekondari na msingi kwa sababu tunazaliana sana na maeneo mijini sasa hivi hakuna. Niseme tu kwamba tuombe sasa Wizara yako itupe eneo hili ili sisi katika miaka hii ambayo tumeambiwa tujenge shule za sekondari pamoja na msingi basi tuyapate kwa sababu naona mtakwenda tena miaka saba ijayo katika kutengeneza hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; je, Serikali yetu sasa ina mpango gani wa kumalizia fidia kwa wananchi wa maeneo ya jirani karibu na pale ambapo mmetwaa lile eneo lakini yapo maeneo Shimo la Udongo ambapo mlitakiwa kuyatwaa lakini bado hamjalipa fidia. Naomba maswali yangu haya mawili tuweze kujibiwa. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE Aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Buza/Nzasa – Kilungule pamoja na daraja litamalizika hasa ikizingatiwa kuwa barabara hiyo inawaunganisha wananchi wa Temeke na Mbagala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave Mbunge wa Jimbo la Temeke kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mradi unatekelezwa kupitia DMDP, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke inatekeleza Mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Nzasa – Kilungule – Buza yenye urefu wa kilometa 7.6. Kati ya hizo kilometa 5.4 zinajengwa kwa kiwango cha lami na kilometa 2.2 kwa kiwango cha zege; na ujenzi wa stendi ya mabasi Buza fungu namba 14 wenye thamani ya shilingi bilioni 19.13 bila VAT, chini ya Mkandarasi Mjenzi Group Six International Ltd. Fedha hizi ni Mkopo wa Serikali kutoka Benki ya Dunia na unaotekelezwa kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa mradi huu ulianza kutekelezwa tarehe 01 Aprili, 2020 na unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Oktoba, 2021. Mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 69 na fedha kiasi cha shilingi bilioni 8.05 zimelipwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kufanya matengenezo ya miundombinu ya barabara za Jimbo la Temeke kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaajiri Walimu wa Sayansi katika Shule za Sekondari za Kata Wilaya ya Temeke pamoja na kumaliza tatizo la uhaba wa Vifaa vya Maabara kwenye shule hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Temeke, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 iliajiri Walimu 6,949 ambapo kati yao asilimia 79 walikuwa Walimu wa sayansi ambao walipangiwa vituo katika Shule za Sekondari za Serikali, kipaumbele kikiwa ni shule zenye upungufu mkubwa kulingana na mahitaji ya wakati huo. Serikali imefanya tathmini ya mahitaji ya Walimu wa sayansi katika shule za sekondari na kubaini kuwa Manispaa ya Temeke ina upungufu wa Walimu wa Sayansi 631, sawa na asilimia 71.05 ya mahitaji. Serikali itaendelea kuajiri Walimu wa fani zote na kuwapangia vituo kulingana na mahitaji ya shule za sekondari zote nchini, zikiwemo Shule za Sekondari za Manispaa ya Temeke.

(b) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/ 2021, Serikali ilinunua na kusambaza vifaa vya maabara katika Shule za Sekondari za Kata zipatazo 1,258 nchini zikiwemo shule 14 Manispaa ya Temeke ili kuwafanya wanafunzi waweze kujifunza kwa vitendo masomo ya Sayansi. Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ya Elimu nchini itaendelea kununua na kusambaza shuleni vifaa vya maabara katika shule za sekondari nchini, zikiwemo Shule za Sekondari za Manispaa ya Temeke. Ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -

Je ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa Ardhi kati ya Wananchi na Serikali katika Kata ya Yombo Vituka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na Serikali ili kupisha ujenzi na upanuzi wa Shule ya Msingi Uwanja wa Ndege, ulihitimishwa tarehe 26 Septemba, 2022 baada Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali Shauri la Rufaa Na. 116/2019 lililofunguliwa na walalamikaji 56 ambao walishindwa kuthibitisha madai yao.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari Bingwa na Wataalam wa Vifaa Tiba katika Hospitali ya Malawi ambayo ipo Kata ya Buza Temeke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kituo cha kutolea huduma za Afya cha Malawi bado hakijapandishwa hadhi kuwa Hospitali. Kwa sasa Kituo hicho kinatambulika kama Kituo cha Afya - Malawi ambacho hakijakidhi vigezo vya hitaji la kupelekewa Madaktari Bingwa kwa kuzingatia mwongozo wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa sasa inaendelea na taratibu za kuongeza Vifaa Tiba kwenye Kituo hicho. Aidha, Halmashari inaelekezwa kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu inayohitajika ili kiendane na hadhi ya Hospitali na kuombewa kupandishwa hadhi.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza gharama za malipo kwa Akinamama wanaojifungua kawaida na wale wa operesheni?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya inaendelea kutekeleza Sera ya Afya ya mwaka 2007 inayoelekeza kutoa huduma za matibabu bure kwa makundi maalum, ikiwemo akinamama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano. (Kipengere 5.3.4 chenye Tamko linalosema “Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inayotoa huduma bila faida na mashirika ya Kimataifa itaendelea kutoa huduma bila malipo kwa wanawake wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano”).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vituo vya binafsi visivyo na ubia na Serikali ukamilishaji wa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote utakapopitishwa utakuwa suluhisho la tatizo hili.