Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Abdallah Jafari Chaurembo (7 total)

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga chuo cha VETA katika Kata ya Chamazi eneo ambalo limetolewa bure na UVIKYUTA zaidi ya ekari 30 ili kuwawezesha vijana wengi wa Kitanzania kuweza kujiajiri na kuweza kupata ajira katika fani mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi Serikali ina mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba katika kila mkoa na katika kila wilaya tunakuwa na Chuo cha VETA. Katika awamu ya kwanza tumefanya ujenzi ambao mpaka hivi ssa unaendelea katika wilaya 29, lakini katika awamu ijayo tunatarajia katika kila wilaya kupeleka vyuo hivyo. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika kila wilaya tutafikia kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni nini kauli ya Serikali kwa kumalizia kipande cha Mbande – Kisewe ambacho kimekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa Kata ya Chamazi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, barabara ya Zakhem – Mbagala Kuu imepata fedha za Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar-Es-Salaam na imeshindwa kujengwa kwa sababu ya uwepo wa bomba la mafuta la TAZAMA. Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia walao corridor ya mita saba ili barabara hiyo ambayo tayari inayo fedha iweze kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi tunavyoongea sasa hivi, Mheshimiwa Chaurembo ni shahidi, tulikuwa na kilometa 6.05; kilometa moja imeshakamilika zimebaki kilometa 5.06. Nimhakikishie Mheshimiwa Chaurembo katika mwaka huu wa bajeti, kupitia fedha ya matengenezo, sasa tutaanza barabara ya kutoka Mbande kuja Msongola ambapo tunajenga kilometa 1.5 kwa kiwango cha lami. Pia kwa fedha ya maendeleo tutaendelea kutoka Msongola kwenda Mbande kilometa 1. Kwa hiyo, tutabakiwa kama na kilometa 2.5 ambazo zitakuwa bado hazijakamilika na fedha itakapopatikana tutaendelea kukamilisha barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kuhamisha bomba ama barabara Serikali imelipokea na itakwenda kulifanyia kazi tuone kama tutahamisha kwa sababu inapita karibu na bomba. Tutaangalia namna ya kufanya ili barabara ile muhimu sana iweze kuanza kujengwa. Pia kwa sababu suala hili siyo la Idara yangu pekee kwa maana ya Wizara ya Ujenzi ni Wizara nyingi, kwa hiyo, tumelipokea na tutakwenda kulifanyia kazi kuona ni namna gani tufanye kuhamisha barabara hiyo. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa umeme unaozalishwa katika Sub-station ya Mbagala ni chini ya asilimia 20 tu unaotumika Mbagala na asilimia zaidi ya 80 unaenda kutumika Mkuranga. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga sub-station kule Mkuranga ili kuwapoza watu wa Mbagala waendelee kutumia umeme wao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Jimbo la Mbagala ndiyo Jimbo ambalo lina watumiaji wengi wa umeme ukilinganisha na mikoa mingine ya Ki-TANESCO, je, Serikali ina mpango gani wa kulifanya Jimbo la Mbagala kuwa mkoa wa Ki-TANESCO?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Mbagala tunayo Sub- station inayozalisha Megawatts 48 na Megawatts 40 zinakwenda Mkuranga kama alivyosema kwa sababu kuna viwanda vingi sana pale zinabaki Megawatts 8 tu. Tunapata umeme wa Mbagala kutoka Ubungo kupitia Gongolamboto lakini tunapata umeme mwingine kutoka Kurasini. Pale Kurasini tunapata Megawatts kama 26 hivi, zinazoenda kujazia pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba umeme unapungua katika eneo la Mbagala kwa sababu mahitaji yamekuwa makubwa. Hata hivyo, kama tulivyosema kwenye swali la msingi, tunaongeza uwezo wa kituo hicho cha Mbagala kwa kuweka MVA 50 lakini pia cha Kinyerezi ambacho pia kitaleta umeme pale Mbagala.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali hilohilo ni kwamba tayari Serikali inafanya feasibility study ya kujenga sub-station nyingine kumi na kuziboresha nyingine kadhaa katika maeneo yetu ya Tanzania. Mkuranga kwa sababu ya umuhimu wake wa kuwa na viwanda vingi sana ni eneo mojawapo ambalo litapelekewa sub-station katika siku za hivi karibuni ili kupunguza mzigo mkubwa ambao vituo vyetu vya Mbagala na Kinyerezi vinaupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, Mkoa wa Dar es Salaam mpaka sasa unayo mikoa ya ki-TANESCO minne na hivi karibuni yamekuja maombi ya Kigamboni kuwa ni Mkoa wa ki-TANESCO na bado yanafanyiwa kazi. Niombe kwamba kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge amelisema, tutaenda kuangalia vigezo kwa sababu kuna kuangalia idadi ya wateja, makusanyo, line ya umeme mkubwa na mdogo katika eneo husika, vigezo vikikidhi basi, mamlaka husika zitaamua na huduma zitapelekwa karibu zaidi na wananchi.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo yanatia moyo, sasa nataka kujua; kwa kuwa Sera ya Serikali ni kuwa na Sekondari katika kila Kata: Je, ni lini sasa Serikali itajenga Shule za Sekondari katika Kata ya Mbagala, Kilungule na Kibonde Maji ambapo Kata hizo hazina Sekondari kabisa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuongozana nami kwenda katika Jimbo la Mbagala kujionea hali ya msongamano wa wanafunzi darasani katika Shule ya Mbande, Chamazi, Mianzini, Kilamba, Nzasa, Mbagala, Rangi Tatu, Mbagala Kuu, Mzinga, Kilungule na Kijichi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameainisha baadhi ya Kata hususan Kata ya Mbagala, Kilungule pamoja na Kibonde Maji ambazo mpaka sasa hivi hazina Sekondari; na Sera ya Serikali ni kwamba kila Kata lazima iwe na Sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Jimbo la Mbagala ambako anawapigania kwamba hizo Kata zote zitapata Sekondari za Kata ambazo zipo katika mpango wetu. Kwa sababu sasa hivi Serikali tuna mpango wa kujenga sekondari 1,000 nchi nzima katika zile Kata zote ambazo hazina sekondari. Kwa hiyo, miongoni mwa Kata tutapeleka Shule za Sekondari ni pamoja na Kata alizoziainisha; Kata ya Mbagala, Kilungule pamoja na Kiponde Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Mbunge alikuwa anaomba tuongozane tukaone msongamano katika shule ambazo ameziainisha hapa ikiwemo Mbande, Chamazi, Rangi Tatu, Mbagala Kuu, Mzinga, Kijichi na Kilungule; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, nipo tayari, hata akisema baada ya maswali na majibu twende, mimi nitakwenda kwa ajili ya hiyo kazi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mchakato wa kuhakiki mali za wananchi pamoja na majedwali haya ya fidia ulianza toka mwaka 2018, je, wananchi wa Kokoto hadi Kongowe wanataka kujua wavumilie mpaka lini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, ni nini hatma ya wananchi wa Mbagala Rangitatu eneo la Charambe hadi kule Mbande ambao wamewekewa mawe ya hifadhi ya barabara toka mwaka 2010 na bila kupewa maelezo yoyote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaurembo, Mbunge wa Mbagala kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Mbunge wa Mbagala ambaye ni Meya Mstaafu wa Manispaa ya Temeke kilio chako kimesikika Mheshimiwa Mbunge na ndio maana Mheshimiwa Rais alitembelea katika eneo lako na ametoa maelekezo. Kiongozi Mkuu wa nchi akitembelea nchi hayo ni maelekezo sisi ni watekelezaji.

Mheshimiwa Spika, kilichofanyika ni kwamba ni fidia imefanyika, mkandarasi yupo pale site ataleta taarifa, watu wa TANROADS Mkoa wa Dar es salaam watapitia taarifa hiyo, tutafanya joint verification kwa maana ya Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Fedha na Valuer wa Serikali baada ya hapo wananchi wale watalipwa fidia. Maelekezo ni kwamba ujenzi hautaanza mpaka tuondoe vikwazo vya kulalamikiwa na wananchi baada ya kulipwa haki zao. Kwa hiyo, naomba wavute subira katika jambo hilo tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili Mheshimiwa Mbunge anauliza habari ya mawe ambayo imewekwa pale katika road reserve ya Mbande kwenda Msongola mpaka Mvuti. Ni kweli kwamba wananchi baadhi walilipwa wakati huo, lakini tumekubaliana kwamba tukianza upanuzi wa barabara hiyo, yule mwananchi ambaye anafikiwa kwa wakati huo atakuwa analipwa fidia yake, hayo ndio majibu ya Serikali, ahsante sana.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa mgawanyo wa mali iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam haukuhusisha wadau wakiwepo Waheshimiwa Wabunge: -

Je, Serikali haioni sasa haja ya kuu-review ule mgao hasa katika ile mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu?

NAIBU SPIKA: Nataka kuamini ukisema Wabunge, unamaanisha pia na Madiwani hawakushirikishwa. Kwa sababu kama walishirikishwa Madiwani halafu Wabunge ndio hamkuwepo, ni ninyi ambao hamkuwepo. Hebu fafanua kidogo.

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam hayakushirikishwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Jambo alilolita Mheshimiwa Abdallah Chaurembo ni kubwa sana ambalo linahitaji kwanza tufuatilie, tujiridhishe kwa sababu ninaamini kila jambo linapofanyika kunakuwa na muhtasari ambao huwa unaandikwa na vikao na idadi ya watu waliohudhuria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, endapo jambo hilo halikufanyika, basi ninaamini Ofisi ya Rais, TAMISEMI itazingatia namna bora kabisa ambayo itasaidia jambo hili liweze kufanyika kikamilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunalipokea na tutakwenda kulifanyia kazi, ahsante sana.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Halmashauri ndiyo Mamlaka za Upangaji: ni lini Wizara ya Ardhi itakabidhi viwanja vya mradi wa viwanja 20,000 kwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ili kuyapangia matumizi mengine maeneo yote ya Taasisi ambayo hayakuendelezwa katika Kata ya Tuangoma na Kibada hasa katika Kiwanja kilichopo Goroka Block D, Block 10 Kiwanja Na. 219, Changanyikeni Block 9 Kiwanja Na. 215, mashamba pori ya NSSF ya Mtaa wa Masuliza, Mwapemba, Vikunai na Changanyikeni? (Makofi)

Swali la pili: Je, ni lini Wizara ya Ardhi itaweka miundombinu ya barabara katika mradi wa viwanja 20,000 katika maeneo yote ya Kata ya Tuangoma. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula, nataka tu niwaeleze Waheshimiwa Wabunge, alichosema Mheshimiwa Chaurembo ni kweli kwamba kwa mujibu wa Sheria Mamlaka za Upangaji wa Ardhi ni Halmashauri. Kwa hiyo, sisi kama Madiwani ni sehemu ya Mamlaka ya Upangaji wa Ardhi. Kila Halmashauri inapanga yenyewe matumizi ya ardhi yake. Ingawa tunashirikiana katika kuthibitisha ule upangaji, lazima uthibitishwe na Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Dar es Salaam kuna mradi ulianzishwa miaka ya nyuma ya viwanja 20,000. Sasa leo nataka niseme hapa mbele ya Mheshimiwa Mbunge, viwanja 20,000 vilivyopimwa katika Wilaya ya Temeke, kwa mfano hivi vya Tuangoma iliyokuwa miradi 20,000 na Kibada, nimeshaagiza na ninarudia tena kuagiza, Wizara ya Ardhi ikabidhi michoro ya viwanja hivi 20,000 kwa Manispaa ya Temeke na wiki hii lazima makabidhiano yafanyike ili wananchi na Wilaya ya Kigamboni waweze kusimamia ipasavyo miradi hii ya viwanja 20,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, ulikuwa ni mradi ndani ya Wilaya ya Temeke, sasa michoro yote na taarifa zote za umiliki ziwe ni open space, maeneo ambayo hayajaendelezwa, Temeke liwe ni jukumu lao kufuatilia. Kama kuna watu hawajaendeleza Temeke ni Mamlaka halisi. Pekuweni tutoe notice kwa watu ambao hawajaendeleza tuchukue hatua mchukue ardhi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naagiza Kamishina wa Ardhi akabidhi michoro na taarifa zote. Kuanzia leo, eneo lote la Viwanja 20,000 la Kibada na Tuangoma lazima liwe chini ya Mamlaka ya Manispaa ya Temeke. Hayo mengine mtafanya wenyewe. (Makofi)