Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ally Mohamed Kassinge (5 total)

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Umuhimu wa reli ya kutoka Tunduma kwenda Kasanga ni sawa kabisa na umuhimu wa reli ambayo ilishakuwepo kabla ya Tanganyika kupata uhuru ya kutoka Mtwara – Nachingwea kwa Mikoa ya Kusini. Je, ni nini mpango wa Serikali wa kufufua reli ya Mtwara – Nachingwea mpaka Nyasa kwa manufaa ya kiuchumi na shughuli za kijamii kwa Mikoa ya Kusini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Kasinge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge atakubaliana nami kwamba, Serikali ina mpango wa kujenga reli ya Mtwara hadi Mbamba Bay kwa kiwango cha SGR ambapo tayari upembuzi yakinifu umeshakamilika na usanifu wa awali umeshafanyika. Serikali imeshatafuta tayari transaction adviser kwa ajili ya kuandaa andiko ili kutafuta mbia ambapo reli hiyo tunategemea itajengwa kwa mfumo wa PPP. Kwa hiyo, itategemea na kama mbia huyo atapatikana haraka, basi hiyo reli itajengwa. Reli hiyo itahudumia corridor ya Mtwara kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay, lakini pia itakuwa na branch kwenda Liganga na Mchuchuma kwa ajili ya kusafirisha madini ambayo tunategemea yatazalishwa katika migodi hiyo. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, gesi asilia ninayozungumzia kwenye swali langu la msingi ni ile gesi ya Songosongo na eneo mahsusi ambalo nimeulizia ujenzi wa kiwanda ni katika Mji wa Kilwa Masoko, ambapo kimsingi tayari eneo la kutosha lipatalo ekari 400 lilishatengwa tangu mwaka 1989, lakini pia TPDC ilishalipa fidia ya eneo hili na ni eneo ambalo lipo huru na lina hati. Je, Serikali inathibitisha kupitia Bunge lako Tukufu kwamba kiwanda hiki cha mbolea kitajengwa mahsusi Kilwa Masoko na si kwingineko? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kwa ridhaa yako kuambatana nami baada ya Bunge hili kwenda Kilwa ili akajionee maendeleo na maandalizi ya eneo la kutosha la kiwanda hiki? Ikiwa ni pamoja na uwepo wa bandari, uwepo wa eneo la kutosha kwa ajili ya upanuzi wa bandari, lakini pia uwepo wa eneo la kutosha kwa ajili ya kutolewa malighafi hii, lakini pia atapata fursa ya kujionea Kiwanda cha Maji cha Swahili Water pale Nangurukuru. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nipo tayari.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi ni kwamba tunataka kuona tunatumia malighafi iliyopo ya gesi asilia na kimsingi kama alivyosema TPDC tayari walishakuwa na eneo na hata wawekezaji hawa tunaojadiliana nao wengi tunataka waeleke kujenga katika Mji huu wa Kilwa Masoko ambapo ndipo malighafi inatoka.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana kwa juhudi zake za kufuatilia suala hili na kama nilivyosema mwanzoni nitaambatana naye katika maombi yake ili tuweze kupitia kuona namna gani tunajionea, lakini pia kuona na viwanda vingine ambavyo vimewekeza katika Mkoa wa Lindi hususani Kilwa Masoko.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Umuhimu wa barabara ya Kenyatta katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza ni sawa kabisa na umuhimu wa barabara ya kutoka Kiranjeranje - Nanjilinji mpaka Ruangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Jimbo la Kilwa Kusini. Lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, barabara hii ni kati ya barabara ambazo zimeainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na ni barabara ambayo pia imeahidiwa na viongozi wa Kitaifa. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kadri fedha itakapopatikana barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami mara baada ya kukamilisha usanifu wa kina wa barabara hii. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri na ufuatiliaji na usimamizi madhubuti wa mradi huu, lakini nina swali la nyongeza. Mosi, kwa kuwa mradi huu utachukua miezi 24 tangu kuanza kwa utekelezaji wake maana yake ni miaka miwili, lakini pia utakuwa ni mradi wa kutoka katika chanzo cha maji kuelekea katika miji hii miwili niliyoitaja ya Kilwa Masoko na Kilwa Kivinje, lakini viko vijiji ambavyo vitakuwa mbali na mradi huu. Je, Serikali itakuwa tayari kwa upendeleo wa kipekee kutenga bajeti kwa mwaka huu kwa ajili ya vijiji angalau vitatu vya Nainokwe, Limalyao pamoja na Mandawa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mohammed Kassinge kutoka Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunapoongelea miezi 24 wakati fulani kwa sababu ya changamoto kubwa ya maji ni muda mrefu, lakini naendelea kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo ameendelea kuwa karibu na sisi na kwa hakika namna ambavyo anafuatilia tutahakikisha tunakamilisha vile vijiji sio vitatu, ila kwa sasa hivi kwa mwaka huu wa fedha tutajitahidi tumchimbie kisima kimoja cha maji, lakini hivi vingine vitaingia kwenye Mpango wa Mwaka ujao wa Fedha. Haya maeneo ya vijiji vyake vitatu ambavyo viko mbali na mtandao wetu wa mabomba tutahakikisha tunakuja kuwahudumia wananchi kwa mtandao wa visima.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante pamoja na majibu haya ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Zuberi Kuchauka, Mbunge wa Liwale. Swali la kwanza, je, Serikali inatuahidi nini katika bajeti ijayo?

Lakini swali la pili; je, Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri atakuwa tayari kwenda kuona juhudi za wananchi Liwale lakini wakati wa kwenda au wa kurudi apitie Kilwa Masoko kwa ajili ya kuona changamoto zilizopo katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kassinge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ijayo kwasababu tuna ujenzi wa vyuo hivi 29 katika Wilaya 29 nchini. Katika bajeti ijayo tumepanga kununua vifaa ambavyo vitakavyowezesha sasa vyuo hivi ifikapo Januari, 2022 viweze kuanza kutoa huduma kwa maana kwamba vianze kutoa huduma ya kufundisha wanafunzi katika maeneo hayo. Hilo ndio lengo letu katika bajeti ijayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hili suala la pili la kuweza kwenda kuona maeneo haya nipo tayari, baada ya Bunge hili la Bajeti tutapanga ziara na hata jana tulikuwa na uwekeaji wa jiwe la msingi katika chuo chetu cha VETA pale katika Wilaya ya Ruangwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pamoja na maeneo mengine na dhamira ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba nafika Liwale, lakini nitafika Ruangwa, lakini vilevile nitafika kwa ndugu yangu Kassinge pale Kilwa Kusini kuweza kuona changamoto zilizopo na kwa namna gani ya kuweza kuzitatua. Ahsante. (Makofi)