Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ally Mohamed Kassinge (3 total)

MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea katika Mji wa Kilwa Masoko kitakachotumia malighafi inayotokana na gesi asilia ya Songosongo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mpango wa Matumizi ya Gesi Asilia kwa maana Gas Utilization Master Plan imepanga kutumia kiasi cha futi za ujazo trilioni 0.7 za gesi asilia kwa uzalishaji wa Mbolea. Utafiti unaonesha kuwa Tanzania ina kiasi cha akiba ya gesi asilia kilichogunduliwa na kuthibitishwa takribani futi za ujazo trilioni 57. Hazina hii ya gesi tuliyonayo kwa sasa katika visima vyetu vya gesi asilia inatosha kwa matumizi ya viwanda vya mbolea.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na kiwanda cha mbolea kwa kutumia malighafi ya Gesi Asilia. Hivyo, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) na TPDC, Tume imeendelea na juhudi za kupata wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea. Hapo awali Serikali iliwahi kufanya majadiliano na kampuni ya Ferrostaal na Helm kutoka Ujerumani. Serikali imeendelea kufanya majadiliano na wawekezaji wengine akiwemo Dangote, Elsewedy kutoka Misri na Minjingu Mines Limited ambao wameonesha nia ya kufanya uwekezaji huo.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC), TPDC, PURA, EWURA na Wizara inaharakisha kukamilisha majadiliano hayo na hatimaye kupata wawekezaji wenye uwezo wa kujenga viwanda vya mbolea kwa lengo la kumaliza tatizo kubwa la uagizaji mbolea nje ya nchi. Pindi majadiliano hayo yatakapokamilika ni imani ya Serikali kuwa ujenzi wa kiwanda hicho utaanza mara moja. Nakushukuru.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza mradi wa maji kutoka Mto Mavuji kwa ajili ya wakazi wa Miji Midogo ya Kilwa Kivinje na Kilwa Masoko?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilipata mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India jumla ya Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika Miji 28. Mji Mdogo wa Kilwa Kivinje na Kilwa Masoko ni miongoni mwa Miji itakayonufaika. Utekelezaji unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Aprili, 2021 na unatarajiwa kuchukua miezi 24 kukamilika.
MHE. ZUBERI M. KACHAUKA K.n.y. MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:-

Je, Serikali iko tayari kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kata ya Makata - Liwale ambao wameanzisha ujenzi wa Chuo cha VETA na madarasa mawili yamekamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kachauka, Mbunge Liwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na wananchi za kuona umuhimu wa kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi katika maeneo yao wakiwemo wananchi wa Kata ya Makata - Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, azma ya Serikali ni kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Wilaya nchini. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali inaendelea na ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 29 nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inaendelea na mpango huu kwa awamu, nashauri wananchi wa Kata ya Makata waendelee na juhudi hizo wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha. Aidha, niombe uongozi wa Wilaya ya Liwale uwasiliane na uongozi wa VETA kuweza kuona namna ya kupata msaada wa kitaalam kuhusu ujenzi wa majengo ya Vyuo vya Ufundi Stadi. Ahsante.