Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Agnesta Lambert Kaiza (6 total)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi hii ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu na takwimu zilizotolewa na Serikali, ukweli ni kwamba kutoka ngazi ya Mkaguzi Msaidizi kwenda Mkaguzi kamili inapaswa kufanyika ndani ya mwaka mmoja mpaka miaka miwili. Je, Mheshimiwa Waziri anayo taarifa kwamba kuanzia mwaka 2015 mpaka muda huu ambapo nimesimama mbele ya Bunge hili Tukufu kuna Wakaguzi Wasaidizi ambao hawajapandishwa madaraja?

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Mheshimiwa Waziri atueleze hapa ikiwa anazo hizo taarifa ni kwa nini basi hao Wakaguzi hawajapandishwa madaraja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, si kweli kwamba tangu 2015 mpaka hapa tulipo watu hawajapandishwa madaraja. Kama ataangalia kwenye jibu langu la msingi nilitoa takwimu ambazo zinaonyesha kwamba kuna watu walipandishwa madaraja.

Mheshimiwa Spika, kingine nimfahamishe tu Mheshimiwa kwamba ni vizuri wakapata nafasi wakaipitia hii PGO (Police General Order) itawasaidia kujua baadhi ya taratibu ambazo zinatumika kupandisha madaraja. Kuna mambo ya msingi huwa yanaangaliwa, siyo kwamba watu wanapandishwa tu kwa sababu hawajapandishwa muda mrefu. Kwanza, lazima kipatikane kibali cha kupandisha majaraja. Pili, tunaangalia pia uwezo wa kiuongozi wa yule ambaye anatakiwa kupandishwa daraja. Tatu, tunazingatia zaidi vigezo vya kimaadili kwamba tunayekwenda kumpandisha cheo ana maadili gani katika kutumikia Taifa hili. Nne, tunaangalia kama hana mashtaka mengine. Tano, huwa tunaangalia na bajeti maana tukimpandisha cheo lazima tumpandishie na mshahara wake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa afahamu kwamba utaratibu ndiyo huo lakini tumeanza na tumepandisha madaraja mbalimbali kwa watumishi wa Jeshi la Polisi kama ambavyo taratibu zimeeleza.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa ajili ya nafasi hii ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri kwamba, hayaleti matumaini ya moja kwa moja kwa wakazi wa Butiama naomba nijielekeze kwenye maswali kama ifuatavyo; Swali la kwanza; kwa kuwa, miradi hii ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja hapa utekelezaji wake umekuwa ni wa kusuasua sana kwa lugha nyingine umekuwa na mwendo wa kinyonga. Je, nini kauli ya Serikali basi kuhusiana na bili zinazotolewa kwa wakazi wa Butiama bila kupatiwa huduma?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kumtua mwanamke ndoo kichwani. Swali langu ni kwamba, ni lini basi Serikali itatekeleza kauli mbiu hii kwa matendo kukamilisha miradi yote ya Serikali nchi nzima ambayo imeonekana kusuasua mpaka sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na masuala ya bills, maeneo mengi yalikuwa na tatizo hili, lakini tayari Wizara tunashughulikia kwa karibu kuona kwamba, mtu anakwenda kulipa bili kulingana na matumizi yake. Tunaendelea kuweka mbinu mbalimbali kama kumhusisha moja kwa moja mtumiaji maji kwa kushirikiana na msomaji mita wataangalia kwa Pamoja, watasaini kadi na hapo sasa yule mlipaji atakwenda kulipa bili kulingana na matumizi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na kumtua mwanamke ndoo kichwani; hili suala sasa hivi ni tayari linatekelezeka. Maeneo mengi ya Tanzania sasa hivi akinamama wameshakiri hawabebi tena maji vichwani na tayari Wizara tunaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha maeneo yote ya pembezoni mwa miji kwa maana ya vijijini nao wanakwenda kukamilika katika mpango huu na kazi zinaendelea. Tayari tuna ari kubwa sana kama Wizara na watendaji wetu wametuelewa mwendo wetu ni mwendo wa kasi ya mwanga. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Changamoto ya kujaa kwa maji yanayotokana na mvua iliyoko Mkoa wa Mtwara haina tofauti kabisa na changamoto iliyopo Mkoa wa Dar es Salaam hususan eneo la Jangwani. Kujaa kwa maji katika eneo la Jangwani imekuwa ni changamoto ya muda mrefu na haijawahi kupatiwa tiba ya kutosha. (Makofi)

Mhesimiwa Spika, swali langu ni kwamba, je, Serikali ina mkakati gani au inatueleza nini kuhusiana na changamoto hii ya kujaa maji pale Jangwani hasa ikizingatiwa kwamba Jangwani ni kiunganishi kikubwa sana cha wafanyabiashara wanaoelekea Kariakoo eneo ambao limebeba uchumi mkubwa sana wa nchi? Naomba Serikali basi itoe majibu ni lini itaweza kukomesha changamoto hii ya kujaa maji Jangwani. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Agnesta Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amejaribu kuoanisha eneo la Jangwani na maeneo yaliyoko kule Mtwara katika Manispaa ya Mikindani kwamba na lenyewe linajaa sana maji na anataka kufahamu mkakati gani ambao Serikali inao kuhakikisha tunatatua tatizo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, cha kwanza nimhakikishie kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tuna mradi mkubwa wa DMDP ambao unajenga miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam. Sehemu ya miundombinu hiyo ambayo tumekuwa tukiijenga ni pamoja na mifereji mikubwa ambayo imekuwa ikihamisha maji kutoka katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kupeleka baharini.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili, sasa hivi tuna Mradi mkubwa wa Mabasi Yaendayo Kasi na moja ya jukumu lao kubwa ni kuhakikisha lile eneo la Jangwani linapandishwa tuta kubwa ambalo litahakikisha ile kero ambayo inawapata wananchi inaondolewa. Kwa hiyo, nimhakikishie kabisa Serikali ipo kazini na ile kazi itakamilika na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam hawatajutia kuichagua Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Tume ya Umwagiliaji imekuwa ikipata shida kubwa sana ya bajeti ili kuweza kuteleza majukumu yake yanayohusiana na skimu za umwagiliaji. Je, Serikali ina mkakati gani endelevu wa kuhakikisha Tume hii ya Umwagiliaji nchini inapata bajeti endelevu na si ya kusuasua kama ilivyo sasa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, soko la ndani pekee haliwezi kuwanufaisha wakulima wa mazao katika skimu ya umwagiliaji. Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kuhakikisha mazao haya sasa yanayopatikana kwenye hizi skimu za umwagiliaji yanapata masoko nje ya nchi kuliko ilivyo sasa?

Mheshimiwa Spika, nakushuru sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnesta, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kumekuwa na upungufu wa rasilimali fedha katika maeneo mbalimbali lakini mkakati ambao Serikali unao na hili lilikuwa ni agizo la Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alilolitoa mwaka jana akiwa Makamu wa Rais katika Mkoa wa Simiyu ni kuzifanya subsector zilizoko ndani ya sekta ya kilimo kujiendesha. Wizara ya Kilimo hatua ya kwanza ambayo tumechukua na Bunge hili likituidhinishia bajeti, katika mwaka wa fedha ujao tunaanzisha kitu tunaita Irrigation Development Fund (Mfuko wa Kuendeleza Umwagiliaji).

Mheshimiwa Spika, suala la ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ni wajibu wa Serikali. Serikali inaenda kujenga miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya wananchi wa kawaida. Hivi karibuni tumefanya mradi kwenye skimu tano kwa zaidi ya dola milioni 22 katika Mkoa wa Morogoro, tunatengeneza utaratibu ambao umo kwenye sheria kwamba tunapowekeza katika eneo la umwagiliaji kunakuwa kuna kuzizungusha zile fedha ili zirudi katika Mfuko na ziweze kutumika katika eneo lingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika bajeti ijayo mtaona tunaanzisha Mfuko wa Umwagiliaji ambao utakuwa sustainable na revolving ambao utawezesha sekta ya umwagiliaji kuwa na uhakika wa fedha. Tunawashukuru wenzetu wa Wizara ya Fedha wameturuhusu part of that fund ziweze kuwa retained na Mfuko na hazitaenda katika Mfuko Mkuu wa Hazina ili tuwe na uhakika wa kuweza kujiendesha.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili katika eneo la umwagiliaji badala ya miradi mingi kuendesha katika mfumo ambao tumekuwa tukiendesha sasa hivi, tunafanya miradi mipya kuanzia mwaka kesho kwa kutumia mfumo wa design and build na kutumia force account kama tunavyojenga shule, zahanati na vituo vya afya katika Halmashauri. Pia tutaiwezesha Tume ya Umwagiliaji kwa kuipatia vifaa ili iweze kufanya miradi yenyewe moja kwa moja badala ya kutegemea njia zingine. Kwa hiyo, hii nadhani itatusaidia sana kupunguza gharama za miradi lakini kuifanya Tume kuwa na uhakika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu soko la mazao, siyo tu mazao yanayotokana na skimu za umwagiliaji, dhana yetu ya umwagiliaji mara nyingi tunaitazama katika mpunga tu, kila ukimsikiliza Mbunge au mtu yeyote anaitazama dhana ya umwagiliaji katika suala la mpunga. Sisi tunafanya jitihada ya kufungua masoko ya mazao yote, sasa hivi tunatumia Balozi zetu na hasa mazao ya nafaka, tunaanza communication na nchi ambazo zina masoko tuweze kujenga bonded warehouses kulekule ili wafanyabishara wetu waweze kupeleka mazao na kuyauzia sokoni badala ya kumsubiri mnunuzi atoke Kongo kuja Dar es Salaam au kuja Tanzania kununua. Kwa hiyo, hii ni njia nyingine ambayo tunaitumia, tunaamini kwa kutumia Mabalozi; kupunguza ukiritimba katika biashara ya mazao; kufungua mipaka; kupunguza gharama za biashara na kuongeza tija mazao yetu yatapata masoko ya uhakika.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na utoaji na usambazwaji wa maji mijini na vijijini bado kuna malalamiko makubwa sana ya ankara za maji kutokuwa na uhalisia. Je, Serikali ina nini la kusema au kuna tamko gani la Serikali ili kuondoa mkanganyiko huu ambapo wananchi wanabambikwa ankara ambazo hazina uhalisia? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mheshimiwa Mbunge lakini niseme tu wazi ni haki ya mwananchi kupatiwa huduma ya maji na mwananchi ana wajibu wa kulipia bili za maji, lakini wajibu huo wa kulipia bili za maji zisiwe bambikizi. Kwa hiyo, maelekezo ya Wizara yetu ya Maji kwa Mamlaka zote za Maji nchini watoe bili halisia ambazo zimeidhinishwa na EWURA. Ikiwa kuna Mkurugenzi au msoma mita kwa makusudi anambakizia mwananchi bili ya maji tutashughulika naye.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukosefu wa dawa na vifaatiba imekuwa ni changamoto karibia nchi nzima. Je, ni kwa nini Serikali basi isihamasishe uwekezaji mdogo na mkubwa wa viwanda vya dawa na vifaa tiba ikiwa ni pamoja na kuondoa Kodi ya Forodha pamoja na masharti mengine ili basi viwepo viwanda vingi ambapo mwisho wa siku dawa hizi zitakwenda kuwasaidia Watanzania na hususani walio wengi huko vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Agnesta Lambert ameleta pendekezo kwamba ni kwa nini sasa Serikali isione haja ya kuongeza uwekezaji kwenye viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba nchini ili kupunguza hii adha? Jambo hili ni jema, ndiyo maana sasa hivi sera ya Serikali ni kuhimiza watu wote wanaotaka kuwekeza nchini waje, ikiwemo kwenye sekta hii ya dawa na vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi tunawaruhusu watu wote na katika kipindi sahihi kabisa cha kuwekeza ni
sasa, kwa sababu Serikali imeboresha mazingira bora ya kufanya biashara nchini ambayo yanaruhusu wawekezaji wote kuwekeza ndani ya nchi. Ninaamini hao watakaokuja kuwekeza kwenye maeneo ya dawa na vifaa tiba wanapewa kipaumbele zaidi. Kwa hiyo, mazingira ya Serikali yako sahihi na tunawaruhusu na Serikali itaendelea kuwekeza zaidi. Ahsante.