Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Agnesta Lambert Kaiza (4 total)

MHE. AGNESTA L. KAIZA Aliuliza:-

Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu ucheleweshaji wa kupandisha vyeo kwa Askari wa Jeshi la Polisi katika ngazi ya Wakaguzi Wasaidizi na kwa Wakaguzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi ni Taasisi ya Serikali ambayo mfumo wake wa upandishwaji wa vyeo huzingatia sheria na kanuni za utumishi. Askari, Wakaguzi na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi hupandishwa vyeo pamoja na watendaji wengine wa Jeshi la Polisi kwa kuzingatia ikama na bajeti ya mwaka husika.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 mpaka 2018 jumla ya askari 2,354 walipandishwa vyeo kuwa Wakaguzi Wasaidizi na kwa kipindi cha kuanzia 2015 mpaka 2020 jumla ya Wakaguzi Wasaidizi 1,163 walipandishwa vyeo kuwa Wakaguzi wa Polisi. Serikali itaendelea kuwapandisha vyeo Askari Wakaguzi na Maofisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi kulingana na taratibu zilizoelezwa hapo awali. Ahsante.
MHE. AGNESTA L. KAIZA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka maji safi na salama Butiama ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa Baba wa Taifa katika Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambart Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji wa maji safi na salama katika Wilaya ya Butiama ni 61.18%. Katika kuhakikisha wananchi wa Butiama wanapata huduma ya maji safi Serikali kupitia RUWASA imekamilisha miradi ya maji katika Vijiji vya Nyabanje, Magunga, Kongoto, Bukwaba, Kamgendi na Masurura, vinavyohudumia wananchi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lengo la kutatua tatizo la maji katika muda mrefu Butiama, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa Mugango – Kiabakari – Butiama mwezi Disemba, 2020 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2022. Kazi zilizoanza kutekelezwa ni upimaji wa maeneo ya ujenzi wa matenki, mtambo wa kusafisha maji, njia kuu ya bomba na uletaji wa vifaa katika eneo la mradi. Mradi huu unatarajiwa kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji kwa asilimia 100 katika eneo la mradi pamoja na vijiji vilivyoko ndani ya kilometa 12 kutoka bomba kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huo utatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (Saudi Fund for Development – SFD) kwa gharama ya dola za Marekani milioni 30.69 sawa na takribani shilingi bilioni 70.
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji katika Mikoa ya Kigoma, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma na Morogoro ili kuongeza mazao ya kilimo yatakayosafirishwa kupitia SGR?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambart Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kutekeleza na kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji katika mikoa inayopitiwa na reli ya kisasa ya mwendokasi kuanzia Mkoa wa Pwani na kufanya kutathmini maeneo yote yenye sifa ya kufanya uzalishaji kwa kutumia njia ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 na 2020/2021 eneo linalomwagiliwa limeongezeka hadi kufikia hekta 695,045 na hivyo kufikia asilimia 58 ya lengo la kufikia hekta milioni 1.2 ifikapo 2025. Ongezeko hilo limetokana na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu za umwagiliaji za Kilangali Seed Farm (Kilosa) kupitia mradi wa ERPP na akimu 13 za SSIDP kupitia mradi wa SSIDP. Serikali inakamilisha ujenzi wa awali kwa skimu za umwagiliaji katika Mikoa ya Shinyanga, Tabora, Kigoma, Singida, Morogoro, Dodoma na Kagera. Aidha, Serikali itaendelea na ukamilishaji wa skimu hizo hili ziweze kutumiwa ipasavyo na wakulima.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inakamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa Mradi mkubwa wa Umwagiliaji katika Mkoa wa Kigoma wenye hekta 3,000 ambapo ujenzi wa mradi huo wa Luiche unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Aidha, miradi mingine ya umwagiliaji inayopitiwa na reli ya SGR itakayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2021 ni pamoja na Skimu za Ngomai (Kongwa), Idudumo (Tabora) na Msufini pamoja na Shamba la Mbegu la Msimba (Morogoro).
MHE. OMAR ALI OMAR K.n.y. MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:-

Je ni kwa nini askari polisi wasiwekewe utaratibu wa kusamehewa kodi katika vifaa vya ujenzi na kupewa viwanja kwa bei elekezi ili wawe na moyo wa kulitumikia Taifa bila kujiingiza katika njia za udanganyifu kwa lengo la kujiandaa na maisha baada ya kustaafu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa utoaji wa msamaha wa kodi kwa bidhaa mbalimbali vikiwemo vifaa vya ujenzi kwa askari wa Jeshi la Polisi ulikuwa unatekelezwa kupitia Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), na kutokana na changamoto za kimuundo na mfumo uliosababisha uvujaji wa mapato na utozaji kodi usio na usawa, Serikali ilifanya marekebisho yaliyopelekea kufutwa kwa baadhi ya misamaha ya kodi ikiwemo ya vifaa vya ujenzi kwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua kazi kubwa na nzuri katika kulitumikia Taifa letu inayofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Polisi, ilianzisha utaratibu mwingine wa kibajeti wa kutoa nyongeza ya posho maalum kwa kila Askari ili kufidia gharama za kodi pale wanapofanya manunuzi ya vifaa vya ujenzi pamoja na mahitaji yao mengine. Nakushukuru.