Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ahmed Yahya Abdulwakil (2 total)

MHE. AHMED YAHYA ABULWAKIL aliuza:-

Je, ni lini Serikali itawaunga mkono wananchi wa Chukwani waliojitolea kujenga Kituo cha Polisi cha ghorofa moja kwa kumalizia ujenzi wa kituo hicho?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Yahya Abdulwakil Mbunge wa Kwahani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Kituo cha Polisi Chukwani ulianza mwaka 2015 na unatekelezwa kwa mchango wa nguvu za wananchi na wadau werevu wa Ulinzi na Usalama huku Jeshi la Polisi likitoa wataalam wa ushauri na usimamizi kwa mafundi wake. Gharama ya ujenzi inatarajia kufikia kiasi cha shilingi 98,000,000/= hadi kukamilika kwake. Kwa sasa ujenzi umefikia hatua ya kumalizia (finishing) na gharama za kumalizia zinahitajika shilingi 40,000,000/=.

Mheshimiwa Spika, Serikali inafanya utaratibu wa kutumia fedha za mfuko wa Tuzo na Tozo ili kumalizia ujenzi wa vituo mbalimbali vilivyosimama katika ujenzi kutokana na kukosa fedha kikiwemo Kituo cha Polisi Chukwani. Hata hivyo, kwa kushirikiana na wananchi na wadau werevu, Kituo hiki kitaendelea kukamilishwa ili kianze kazi ya kuwahudumia wananchi wa eneo hili na maeneo jirani. (Makofi)
MHE. YAHYA ABDULWAKIL AHMED aliuliza: -

Je, Shirika la Posta Zanzibar halioni umuhimu wa kuchimba kisima katika Jimbo la Kwahani katika Kitongoji kilichopo karibu na Ofisi hiyo ili kukuza ujirani mwema?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Abdul Wakil Ahmed Mbunge wa Kwohani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Shirika la Posta Tanzania ni taasisi ya Kimuungano ambapo kwa upande wa Zanzibar ina jumla ya Ofisi tisa, kati ya Ofisi hizo, Unguja kuna Ofisi tano ambazo zipo Kijangwani, Shangani, Mahonda, Jambiani na Makunduchi; na Pemba kuna Ofisi nne zilizopo Chakechake, Wete, Mkoani na Kengeja.

Mheshimiwa Spika, Shirika limekuwa na utaratibu kila mwaka wa kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii kwa kuzingatia mtiririko wa fedha na bajeti ya mwaka husika. Kwa kipindi cha miaka mitatu yaani 2018 hadi 2020 Shirika katika kuchangia huduma za kijamii kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar – SMZ imefanya yafuatayo: -

(i) Mwaka 2018, Shirika lilitoa vifaa mbalimbali katika Kituo cha wazee cha Amani ili kusaidia matunzo ya wazee katika kituo hicho.

(ii) Mwaka 2019, Shirika lilitoa vifaa mbalimbali katika Hospitali ya Mnazi Mmoja ili kusaidia akinamama wanaojifungua.

(iii) Mwaka 2020, Shirika lilitoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kusaidia wazee wanaotunzwa katika kituo cha kulelea Wazee cha Welezo kilichopo Unguja.

Mheshimiwa Spika, Shirika linaendelea na utaratibu wake wa huduma kwa jamii kulingana na bajeti. Shirika litaangalia uwezekano wa kuchangia uchimbaji wa kisima katika kitongoji kilichopo karibu na ofisi katika kuendeleza ujirani mwema kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu, ahsante.