Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon Abubakar Damian Asenga (12 total)

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naomba kuuliza Wizara ya Mawasiliano swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa vijiji vitatu katika Kata ya Ziginali, Kisawasawa na Kiberege havina mawasiliano ya simu kabisa. Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi hawa huduma ya mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilijibu katika majibu yangu ya msingi, ni kwamba Serikali iko katika mpango wa kufanya tathmini katika Kata nyingine 1,392 ambazo zimebaki Tanzania Bara ili tuweze kuona namna gani tutaziingiza katika Mpango wa Utekelezaji katika Bajeti ya 2020/2021. Hivyo namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, sambamba na hilo tutahakikisha kwamba tunawasiliana naye kwa ukaribu sana ili kujua changamoto ziko katika maeneo gani ili tuhakikishe kwamba mawasiliano katika Kata hizo yanafika kwa ukamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa wewe ni miongoni mwa watu waliofika Jimboni kwetu na kuona namna ambavyo tunalima miwa kwa bidii kwa kufuata kauli ya Mheshimiwa Rais ya nchi kujitegemea katika suala zima la sukari; na kwa kuwa hao wenye viwanda ndio waliopewa vibali vya kuingiza sukari inayopungua katika nchi yetu, je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka mwekezaji mwingine wa kiwanda ili kuondoa monopolism ya kiwanda ambacho kipo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri na Mawaziri husika katika sekta hii ya kilimo na viwanda na biashara, watakuwa tayari kuambatana nami baada ya Bunge hili, kwenda kuwasikiliza wananchi hasa wakulima wa miwa Jimboni kwangu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, Serikali inaona umuhimu wa kuongeza uwekezaji wa viwanda vya sukari nchini hasa katika Kiwanda cha Kilombero ili kuongeza uzalishaji wa sukari nchini. Kwa upande wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, Serikali na mbia mwenza, iko katika majadiliano ya kupanua kiwanda hiki na hatimaye kuongeza uzalishaji wa sukari ili miwa yote inayolimwa iweze kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, napenda kumwahidi Mheshimiwa Abubakari kwamba niko tayari kuongozana naye pamoja na wataalam wangu kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kujionea hali halisi ya uzalishaji katika kiwanda hicho, pale tutakapopata nafasi mara baada ya mkutano huu wa Bunge kuahirishwa. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kuongezea majibu kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Serikali iko kwenye mazungumzo na wawekezaji kadhaa angalau watatu ambao wana nia ya kuwekeza katika kujenga viwanda vipya vya sukari. Naamini kwa mazungumzo hayo, tukiwapata tutapunguza sana tatizo la sukari na nia ya Serikali ni kuona kwamba katika mwaka mmoja ujao tunajitosheleza kwa mahitaji ya sukari hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ni kwamba, wiki ijayo baada ya Bunge hili mimi na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tuna ziara katika Mkoa wa Morogoro na tutajitahidi tufike pia jimboni kwa Mheshimiwa ili kuweza kuona changamoto. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini bado specifically ninataka kusikia angalau kwenye takwimu jinsi ambavyo Serikali inawekeza haraka kutumia pumba hizi kwa sababu zinaharibu mazingira na hivi ninavyozungumza na wewe zimesababisha Mto Kilombero kujaa maji na kusababisha mafuriko kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza ni kwamba ni kiasi gani Serikali inawekeza haraka iwezekanavyo kutumia pumba hizi ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amesema ni tani 11,000; zinakwenda wapi pumba hizi? Ni kwamba uwekezaji wa haraka unatakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; hawa wakulima wadogo wadogo wa kilimo cha uyoga tayari Halmashauri yetu imewakopesha katika vikundi na wanaendelea kulima, changamoto kubwa wanayoipata ni katika vifungashio, mifuko ile ya kupandia.

Je, Serikali haiwezi kutafuta wawekezaji watakaoruhusu mifuko hii ya kupandia ipatikane kama ambavyo imefanyika kwa wauza mikate kwa sababu sasa hivi kuna katazo la Serikali la mifuko ya nylon?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kwamba kwa nini Serikali haijawekeza; naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba zao la uyoga ni zao ambalo ni kama ndiyo linaanza. Kwa hiyo, bado tunahitaji kufanya utafiti na kutoa hamasa kubwa ili wananchi waweze kufahamu umuhimu wa kulima hilo zao, lakini pia tuweze kuwa na elimu basi hata ya namna ya kulipanda na kulihudumia.

Kwa hiyo, Serikali imeanza kwa kutoa uhamasishaji na kufanya tafiti mbalimbali. Sasa huko mbele ya safari tunaamini kwamba taarifa ambayo itatokana na tafiti hizo, na wananchi wakihamasika basi inakuwa ni rahisi kuvutia wawekezaji wengine na hata kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na upatikanaji wa vifungashio; ni swali zuri na sishangai kwa sababu ni Mbunge makini, namfahamu tokea siku nyingi. Lakini naomba nilibebe ili tushirikiane na Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira pamoja na wenzetu wa Wizara ya Kilimo, tuangalie ni namna gani tunaweza tukapata vifungashio vizuri zaidi kwa ajili ya kuzalisha vimeng’enya kwa ajili ya uzalishaji wa uyoga.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi, japokuwa ntaendelea kubakia kuwa mwananchi mtiifu wa Jangwani, na chini ya GSM naamini kwamba tutavuka salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja katika Jimbo la Kilombero na Mheshimiwa Job Ndugai akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu alipokuja katika Jimbo la Kilombero, waliwaahidi wananchi wa Jimbo la Kilombero juu ya ujenzi wa Hospitali ya Jimbo la Kilombero. Namshukuru Mheshimiwa Waziri, dada yangu, Mheshimiwa Ummy, ametuahidi kwamba tutapata milioni 500 za kuanza ujenzi huu.

Mheshimiwa Spika, swali langu; je, ni lini ujenzi huu utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kabisa katika bajeti inayokuja ya mwaka 2021/ 2022, Serikali imehakikisha kuanza hospitali mpya katika halmashauri zote nchini ambazo hazina hospitali za wilaya.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, na kwa niaba ya Mbunge wa Ulanga Mheshimiwa Salim, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa lazima ukitaka kwenda Ulanga upite Jimbo la Kilombero na kwa kuwa Wilaya ya Malinyi, Ulanga, Jimbo la Mlimba na Jimbo la Kilombero ni ukanda mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba ni muhimu kuwa na timu ya dharura ya TARURA ikaenda kwenye eneo hilo kwa sababu Wilaya ya Kilombero, Jimbo la Mlimba, Ulanga na Malinyi hakuendeki?

Mheshimiwa Naibu Spika, pili: Je, Mheshimiwa Waziri pia haoni kwa udharura huo akatafuta haraka iwezekanavyo gari la kuwapelekea wananchi wa Wilaya ya Ulanga kwa maana ya timu ya TARURA ikapata gari la dharura wakati huu wa mvua ambapo njia hazipitiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Jambo la kwanza ameiomba Serikali kupeleka timu ya dharura kwa ajili ya kwenda kupitia zile barabara ambazo zimebadilika na kufanya tathmini. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hivi ninavyozungumza sasa hivi kuna timu zipo huko kwa ajili ya kuangalia zile barabara zote mbovu ambazo zilipitiwa na hili janga la mvua yakiwemo maeneo ya kule Malinyi. Kwa hiyo, watu wapo kazini na hiyo timu inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu katika Bunge hili wengi huwa wanatusikiliza sasa hivi, ninaagiza wapitie tena upya waangalie hiyo tathmini ya barabara ya Kilombero kupitia Ulanga inafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ameomba kwamba tuwe na gari la dharura kwa ajili ya Ulanga. Kama nilivyoeleza katika jibu la msingi kwamba, tumeshatengewa fedha na katika hizo fedha tutanunua magari 30 na miongoni mwa maeneo ambayo tumeyapa kipaumbele, tutapeleka gari kwa ajili ya TARURA ni katika Jimbo la Ulanga. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshmiwa Mbunge, Ulanga watapata hilo gari.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kilombero, napenda kushukuru kwa majibu mazuri ya Wizara na tunaombea kweli huu mkopo upatikane na mradi huu ufanyike.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutembelea Jimbo la Kilombero ili apite angalau kuzungumza na wananchi wa Zinginai, Magombera, Kanyenja, Mpanga na Muhelule ambao wana shida kubwa ya maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutokana na hali ya udharura wakati tukisubiri mradi huu wa maji tayari Serikali ilishachimba kisima kikubwa katika Kata ya Lumemo ambapo kinatoa lita 30,000 kwa saa. Changamoto ni tenki la kuhifadhi maji yale kuwasambazia wananchi. Katika hali hii ya udharura, je, Serikali haiwezi kutujengea tenki wakati tunasubiri mradi wa maji wa Kiburubutu - Ifakara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la kwenda Kilombero ni moja ya majukumu yangu. Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili tutaweka utaratibu mzuri ili niweze kufika hapo. Naamini mpaka mwisho wa Bunge hili hata mradi huu utekelezaji utakuwa umeanza, kwa hiyo, nitakuja nikiwa na bashasha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ujenzi wa tenki kwa kisima kile ambacho tumekichimba, nia na dhamira kabisa ya Wizara ni kuona wananchi wanapata maji kwa umbali mfupi. Tumeshaweza kutoa fedha ya kuchimba kisima ni dhahiri lazima tutoe fedha ya ujenzi wa tenki. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge, kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha, ujenzi wa tenki utaanza kufanyika. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana, Kituo cha Afya cha Kidatu Nyandeo kina uhaba mkubwa sana wa jokofu la kuhifadhia miili ya marehemu na mara ya mwisho tuliwasiliana na MSD wakasema kwamba wangepeleka jokofu hilo lakini mpaka sasa hawajapeleka.

Je, lini Serikali itapeleka Jokofu katika Kituo cha Afya cha Nyandeo Tarafa ya Kidatu Jimbo la Kilombero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abubakari Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka mipango ya kupata vifaa tiba na vifaa mbalimbali yakiwemo majokofu ya kuhifadhia maiti, lakini pamoja na jitihada za Serikali tumeendelea pia kuhakikisha tunawaelekeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali kuona umuhimu wa kutenga fedha katika mapato ya ndani kununua baadhi ya vifaa tiba na baadhi ya vitendea kazi katika hospitali zetu yakiwemo majokofu ya kuhifadhia maiti.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba nichukue nafasi hii kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kwa sababu majokofu haya ni kati ya Milioni 12 hadi Milioni 30; fedha hii ipo ndani ya uwezo wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilombero na hivyo ninamuelekeza katika mwaka ujao wa fedha wahakikishe wanaweka provision ya kununua jokofu la kuhifadhia maiti katika kituo cha afya. Nakushukuru sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana, Kituo cha Afya cha Kidatu Nyandeo kina uhaba mkubwa sana wa jokofu la kuhifadhia miili ya marehemu na mara ya mwisho tuliwasiliana na MSD wakasema kwamba wangepeleka jokofu hilo lakini mpaka sasa hawajapeleka.

Je, lini Serikali itapeleka Jokofu katika Kituo cha Afya cha Nyandeo Tarafa ya Kidatu Jimbo la Kilombero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abubakari Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka mipango ya kupata vifaa tiba na vifaa mbalimbali yakiwemo majokofu ya kuhifadhia maiti, lakini pamoja na jitihada za Serikali tumeendelea pia kuhakikisha tunawaelekeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali kuona umuhimu wa kutenga fedha katika mapato ya ndani kununua baadhi ya vifaa tiba na baadhi ya vitendea kazi katika hospitali zetu yakiwemo majokofu ya kuhifadhia maiti.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba nichukue nafasi hii kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kwa sababu majokofu haya ni kati ya Milioni 12 hadi Milioni 30; fedha hii ipo ndani ya uwezo wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilombero na hivyo ninamuelekeza katika mwaka ujao wa fedha wahakikishe wanaweka provision ya kununua jokofu la kuhifadhia maiti katika kituo cha afya. Nakushukuru sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Naibu wake, walipokuja jimboni kwetu walichukua hatua kuhusu askari wa TAWA, baadhi ambao walikuwa wakiwaonea wananchi wetu. Na kuwa Mheshimiwa Waziri aliahidi pale katika mkutano ule kwamba atatujengea soko la samaki, Ifakara, Kilombero. Naomba kuiuliza Serikali ni lini ahadi ile nzuri ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii itaanza?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Asenga kwa kuuliza swali hilo na kujali wananchi wake:-

Mheshimiwa Spika, mpango wa kujenga soko katika Daraja la Mto Kilombero upo katika bajeti ya Wizara katika mwaka huu 2021/2022. Kwa hiyo, mara baada ya bajeto hiyo kupitishwa mkakatin huo utaanza.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, japokuwa majibu ya Serikali zijaridhika nayo sana, lakini kwa kuzingatia kuwa Kassim Faya Nakapala Mwenyekiti wa Halmashauri na Ebeneza Emmanuel Katibu wa CCM wa Wilaya wako hapa kufuatilia miongoni mwa mambo mengine jambo hili na Diwani wa Kata husika Fatma Mahigi wa Mang’ula “B” kwamba eneo hili sasa limekuwa hatarishi sana ni eneo ambalo lina ekari takribani 250 na akina mama wameshaanza kubakwa. Naomba kuiuliza Serikali maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza Serikali ipo tayari kuweka ulinzi wakati huu inatafuta mwekezaji wa kuwekeza katika Kiwanda hiki cha Machine Tools?

Lakini pili naomba kuiuliza Serikali sasa hivi tunajenga reli ya kisasa ya SGR na hii reli ya kisasa itahitaji mataruma na kadhalika, kwa nini wasikabidhi eneo hili na kiwanda hiki kwa SGR ili iendelee kutumia kuzalisha vifaa vya reli? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana ndugu yangu Asenga kwa ufuatiliaji kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo lake na hasa katika sekta ya viwanda na kwa ajili ya ufufuaji wa kiwanda hiki cha Mang’ula Machine Tools.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli eneo hili limekuwa kwa muda mrefu halitumiki kama nilivyosema kwa sababu mwekezaji aliyepewa eneo hili kuliendeleza hajaliendeleza kwa muda mrefu, nichukue nafasi hii kumuahidi kwamba tutashirikiana na Halmashauri kuona namna bora ya kuweka ulinzi ili eneo hili lisiwe hatarishi kwa sasa ambapo bado hatujapata mwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili kama nilivyosema tunaangalia matumizi bora ikiwa ni pamoja na kutafuta wawekezaji ambao wataweza kutumia eneo hili kwa ajili ya kuwekeza viwanda, tuchukue pia hoja ya Mheshimiwa Mbunge kwamba kama wenzetu wa reli ya kisasa watataka kutumia eneo hili kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kutumika katika SGR basi nao tutawakaribisha, ahsante sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, pia Halmashauri ya Mji wa Ifakara Jimbo la Kilombero imekuwa ikikosa umeme kila Jumanne na Alhamis; na tunamradi mkubwa sana wa Serikali wa zaidi ya shilingi bilioni 20 wa kituo cha kukuzia umeme. Ujenzi huo wa mradi unasuasua kwa muda mrefu sana: -

Je, Naibu Waziri atakuwa tayari kutembelea pale kutazama changamoto za kusuasua za mradi ule?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako nipo tayari kwenda kuangalia changamoto hizo, lakini niseme kwamba kama anasema ni Jumanne na Alhamis, basi nitafanya mawasiliano na wenzangu tufahamu shida ni nini?

Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Watanzania kwamba hatuna mgao kwa nchi yetu ya Tanzania kwa sasa. Tunao umeme ambao unatosheleza mahitaji tuliyokuwa nayo kwa kile kiasi tunachoweza kupeleka, lakini tutaenda kuangalia tatizo ni nini ili tuweze kulitatua.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, napenda kuishukuru Serikali kwa majibu mazuri ya kutelekeza ahadi hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu maana Waziri Mkuu mwenyewe alilitembelea eneo hili na aliona ufinyu wa eneo hili. Napenda pia kuishukuru Serikali kwa Waziri wa Ardhi Mheshimiwa Lukuvi kutupatia ardhi Kata ya Kiberege kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali hii ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa sasa hivi wakati mchakato wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ukiendelea Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara wanategemea sana kituo cha afya cha Kibaoni, kituo hiki kinakabiliwa na upungufu mkubwa sana wa watumishi.

Je, Serikali haioni kuchukua hatua za haraka kuongeza watumishi katika kituo cha afya cha Kibaoni? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kutokana na ufinyu wa ardhi na eneo la ekari takribani kumi za kujenga Kituo cha Afya cha Kata ya Ifakara Mjini, Ifakara Mjini mpaka sasa hivi haina Kituo cha Afya eneo lililopo ni dogo. Je, Serikali ipo tayari kutupatia ramani maalumu ya ujenzi wa ghorofa ili tufanye mchakato wa kuanza Kituo cha Afya cha Kata ya Ifakara Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee shukrani zake nyingi kwa Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi ambayo imeendelea kuifanya ya kujenga vituo vya afya, hospitali na zahanati nchini kote na nimuhakikishie kwamba mpango huo ni endelevu tutaendelea kujenga vituo vya afya, zahanati, lakini na hospitali zetu za halmashauri kuhakikisha tunasogeza huduma za afya kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kituo cha afya cha Kibaoni kuwa na watumishi wachache nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ujenzi wa vituo hivi unakwenda sambamba na mipango ya kuajiri watumishi kwa awamu kwa kadri fedha zitakapopatikana, lakini pia kwa kadri ya vibali vya ajira vitakavyotolewa. Kwa hiyo, naomba nichukue suala hilo na tutakipa kipaumbele kituo cha afya cha Kibaoni ili kiweze kupata wahudumu kwenye awamu za ajira zinazofuata ili tutoe huduma bora kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kituo cha afya Ifakara Mjini utaratibu upo wazi kama tunahitaji kujenga jengo la kwenda juu kwa maana ya ghorofa. Tunaomba kibali rasmi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunawasilisha michoro na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia watalaamu tunapitia na kuwashauri namna ya kujenga. Kwa hiyo tunakukaribisha kuwasilisha maombi hayo ili tuweze kuona uwezekano wa kujenga kituo hicho. Ahsante. (Makofi)