Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Abubakar Damian Asenga (6 total)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI (K.n.y MHE. ABUBAKAR D. ASENGA) Aliuliza: -

Je, ni lini Ujenzi wa Barabara ya Kidatu hadi Ifakara utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshmiwa Abubakar Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Kidatu – Ifakara ni sehemu ya Barabara Kuu ya Mikumi - Kidatu - Ifakara - Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo – Lumecha yenye urefu wa jumla ya kilometa 547. Barabara hii ni miongoni mwa barabara muhimu katika Taifa kwa kuwa inaunganisha Mkoa wa Morogoro na mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara ya Njombe, Ruvuma na Lindi kupitia Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara kati ya Kidatu hadi Ifakara yenye urefu wa kilometa. 66.9 pamoja na Daraja la Ruaha Mkuu vinajengwa na Mkandarasi M/S Reynolds Construction Company Limited (Nigeria).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii kwa gharama ya Euro 40,441,890.81 takribani sawa na shilingi bilioni 113.13 bila VAT. Mradi ulitegemea kukamilika tangu tarehe 29 Septemba, 2020. Mradi huu umechelewa kukamilika kwa sababu za kimenejimenti kwa upande wa Mkandarasi. Hata hivyo, Serikali inaendelea kumsimamia Mkandarasi kwa karibu ili akamilishe mradi kama ilivyopangwa. Mradi huu umepangwa kukamilika mwezi Oktoba, 2021.
MHE. ABUBAKAR D. ASENGA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaongeza uwekezaji wa Kiwanda cha Sukari Kilombero ili kunusuru miwa ambayo haijavunwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaona kuna umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa sukari nchini ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa sukari ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara. Kwa msingi huo, hoja ya kuongeza uwekezaji katika Kiwanda cha Sukari cha Kilombero ni ya msingi sana.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikisimamia utendaji kazi wa Kiwanda hiki cha Sukari cha Kilombero kwa ukaribu kama inavyosimamia kampuni nyingine ambazo Serikali ina hisa chache kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina, Sura 370. Serikali pamoja na Mbia Mwenza (Kilombero Holding Limited) imekuwa kwenye majadiliano ya kina kuhusu kuongeza uzalishaji wa kiwanda hiki kwa kufanya upanuzi wa kiwanda ambapo imekubaliana kupitia gharama za upanuzi wa kiwanda, kufanya upembuzi yakinifu na namna ya ugharamiaji wa mradi. Mara baada ya zoezi hili kukamilika uwekezaji katika kiwanda hiki utafanyika haraka iwezekanavyo. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvutia wawekezaji hasa katika kutumia pumba za mpunga ambazo hutumika katika uzalishaji wa uyoga hasa katika Jimbo la Kilombero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI) Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza baada ya uteuzi uliofanywa na Mheshimiwa Rais, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru kwanza Mungu kwa kutuweka hai, lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini katika nafasi mpya ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji. Ahadi yangu kwake ni kwamba nitatumikia nafasi niliyopelekwa kwa uadilifu, uaminifu na kwa kufanya kazi kwa bidii kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ya mwanzo, naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, nijibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inavutia uwekezaji wa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo kuandaa miongozo ya uwekezaji ya mikoa ili kubainisha fursa za uwekezaji za mikoa husika, kuandaa makongamano ya uwekezaji ya ndani na nje na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Kilombero wanayo fursa kubwa ya kuingia kwenye kilimo cha uyoga kwa kutumia pumba za mpunga kwa kuwa wilaya hiyo ni kati ya maeneo yanayoongoza kwa kilimo cha mpunga nchini. Kwa mfano, Halmashauri ya Mji wa Ifakara inazalisha tani 11,125 za pumba za mpunga kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa uyoga una soko kubwa nchini, Serikali imeanza uhamasishaji na kufanya tafiti mbalimbali kuhusu uzalishaji wake. Kwa mfano, Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) lilianza utafiti na uhamasishaji wa zao la uyoga mwaka 2001 kwa kutumia masalia ya uzalishaji wa kilimo cha viwanda ambapo jumla ya wajasiriamali 1,823 wamefundishwa uzalishaji uyoga ikiwemo uyoga wa dawa aina ya gonagema na shitake kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, TIRDO kwa kushirikiana na taasisi za utafiti inaendelea kufanya tafiti zaidi ambapo mwezi Machi, 2021, imeanza utafiti wa kujua uwezo wa vimeng’enya aina tofauti katika kuongeza uzalishaji wa uyoga na ubora wa uyoga unaozalishwa kilishe (yield and nutritive value).
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kiburubutu katika Jimbo la Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilipata mkopo kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India jumla ya dola za Marekani millioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika miji 28 nchini ukiwemo Mji wa Ifakara ambao utapata maji kupitia chanzo cha Lumemo. Mradi utahudumia jumla ya Kata tisa na vijiji tisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za kupatikana kwa wakandarasi watakaotekeleza mradi huu zimeshakamilika na unatarajiwa kuanza wakati wowote katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 na ujenzi wa mradi umepangwa kutekelezwa kwa miezi 24.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mikakati gani ya kuanza uzalishaji katika Kiwanda cha Chuma Mang’ula?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa uchumi wa viwanda hapa nchini, pamoja na mambo mengine unalenga kufufua na kuendeleza viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo havifanyi kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mang’ula Mechanical Workshop ni karakana iliyoanzishwa kwa msaada wa Serikali ya China mwaka 1969. Karakana hiyo ilianzishwa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa vipuri mbalimbali ya mitambo iliyokuwa inatumika wakati wa ujenzi wa Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA), pamoja na utengenezaji wa vipuri sehemu ya eneo la karakana hiyo ilitumika kujenga kiwanga cha Pre-Fabricated Concrete Manufacturing kwa ajili ya kutengeneza mataruma ya zege kwa maana ya concrete slippers na nguzo za zege.

Mheshimiwa Naibu Spika, karakana ya Mang’ula Mechanical and Machine Tools Company Limited ilirejeshwa Serikalini mwaka 2019 kutokana na mwekezaji wake kushindwa kuendeleza kiwanda hicho kwa mujibu wa mkataba wa mauziano. Kufuatia urejeshwaji huo Wizara ya Viwanda na Biashara na Ofisi ya Msajili wa Hazina imeandaa utaratibu wa kutafuta wawekezaji wapya watakaoviendesha viwanda hivyo kikiwemo kiwanda cha Mang’ula Machine and Mechanical Tools Limited.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mhe. Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2018 ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilombero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa Hospitali za Halmashauri nchini kote. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali 102 na kuanza ujenzi wa hospitali mpya kwenye halmashauri 28 zikiwemo hospitali zilizoahidiwa na viongozi wa kitaifa.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Ifakara ni miongoni mwa halmashauri 28 zisizo na Hospitali za Halmashauri, ambayo imetengewa fedha shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo matatu ya awali. Ahsante.