Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Juliana Didas Masaburi (1 total)

MHE. JULIANA D. MASABURI Aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Kiwanda cha MUTEX kilichopo Wilaya ya Musoma Mjini kinafunguliwa na kurudisha ajira kwa vijana wa Mkoa wa Mara?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Didas Masaburi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina jumla ya viwanda 12 vya nguo na mavazi na viwanda vitatu kati ya viwanda hivyo havifanyi kazi ikiwemo Kiwanda cha Musoma Textiles.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha MUTEX ni moja kati ya viwanda vilivyobinafsishwa na Serikali kwa wawekezaji kwa lengo la kuviendeleleza ili viweze kukuza sekta ndogo ya nguo na mavazi, kutoa ajira kwa wananchi, kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuleta ustawi kwa jamii. Kiwanda hiki kimekuwa kinafanya kazi kwa kusuasua na mara kadhaa kimesimamisha uzalishaji. Kiwanda cha MUTEX ni moja kati ya viwanda 20 ambavyo vimerejeshwa Serikalini baada ya wawekezaji wa awali kushindwa kuviendeleza na kukiuka masharti ya mkataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, dhamira ya dhati ya Serikali ni kuona viwanda hivyo vinafanya kazi kwa tija na ufanisi mkubwa ili kuongeza ajira kwa ajili ya maendeleo ya watu, kuchochea shughuli za kiuchumi, na kuongeza mapato ya ndani ya nchi. Serikali imeshatoa Tamko la kuvitafutia wawekezaji wapya wa kuviendeleza kwa tija viwanda vyote vilivyorejeshwa Serikalini ili vilete manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla. Ni matumaini ya Serikali, kuona kuwa wawekezaji makini watajitokeza kwa lengo la kutumia fursa hii adhimu kuwekeza katika viwanda hivi. Serikali inaandaa utaratibu maalum utakaowezesha kupatikana wawekezaji wapya kwa njia ya zabuni ya kiushindani na wazi kwa kuzingatia vigezo vitakavyowekwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha wawekezaji wenye nia na uwezo wa kuwekeza katika Kiwanda cha MUTEX na viwanda vingine vilivyorejeshwa Serikalini kuwasilisha maombi yao mara baada ya utaratibu utakapotangazwa rasmi. Nashukuru.