Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage (4 total)

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa ili muundo fulani wa utumishi wa kada fulani uhuishwe lazima kwanza kada husika maombi yapelekwe Serikalini ndipo ifanyiwe kazi, kwa hiyo kama ikikwama kwenye meza fulani ya kamishna ina maana huo uhuishwaji unakwama. Kwa kuzingatia hivyo, je, Serikali haioni vema sasa kuwa na utaratibu wa kuwa na kipindi maalum cha kufanya uhakiki wa kada zote za Utumishi wa Umma na pia kufanya uhakiki wa Utumishi wa Umma pamoja na takwimu za Utumishi, hii yote kuleta usawa katika Utumishi wa Umma na pia kuboresha na kupandisha morale ya kazi ya watumishi? Mfano mzuri ni kada ya uhuishaji wa muundo wa kada ya maafisa kazi hawa Labour Officers.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa stahiki, stahili kwa watumishi pamoja na mafao yao hukokotolewa kuzingatia kiwango cha mshahara anacholipwa mtumishi. Kwa kuona umuhimu huu, je, Serikali sasa italipa kipaumbele suala zima la kuhakiki kada za kiutumishi kwa wakati? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kweye swali la msingi kwamba Serikali itaendelea kuhuisha miundo ya maendeleo ya utumishi kwa kadri ambavyo inaletwa kwenye Wizara yetu. Nitoe kumbukumbu tu kwa Mheshimiwa Mbunge aweze kufahamu kwamba kuanzia mwaka 2011 Serikali imekuwa ikihuisha miundo ya maendeleo ya utumishi hasa kwa kada hii ya ualimu, ambapo ilifanya nyongeza ya madaraja kutokana na nafasi zao za walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia mwaka 2014 Wizara iliendelea kufanya namna hiyo na mwaka 2015 Wizara ya Fedha pia Wizara yetu iliendelea kuhuisha miundo hasa kwenye kada mbalimbali ikizingatiwa baadhi ya watendaji kwenye kada hizo maafisa mipango, manunuzi, maaafisa ugavi, wahasibu na wakaguzi. Nitoe rai tu kwa Mheshimiwa Mbunge afahamu kwamba Wizara yetu itaendelea kuhuisha miundo mbalimbali ya maendeleo ya utumishi kwa kadri itakavyoona inafaa. Kwa hiyo nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba asiwe na hofu.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa swali la pili, kuhusu stahiki za mafao za watumishi kama ambavyo nimeulizwa. Katika utumishi wa umma stahiki na stahili za utumishi zimeanisha katika miongozo na nyaraka mbalimbali zinazotolewa kuhuishwa mara kwa mara na Serikali. Nyaraka hizo huainisha makundi mbalimbali ya utumishi na stahiki wanazotakiwa kupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, kwa mujibu wa kanuni ile ile Kanuni D. 6(2) za Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, Kanuni hii iliwahi kutolewa mwaka 2009; watumishi wa Umma kuajiriwa na kupandishwa vyeo na kubadilishwa kada (Recategorization) kwa kuzingatia sifa walizonazo na zinazooneshwa katika Miundo ya Maendeleo ya Utumishi katika kada mbalimbali zilizoainishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Miundo ya Maendeleo ya Utumishi wa kada mbalimbali katika Utumishi wa Umma imeainisha ngazi za mishahara, kuanzia cheo cha kuingilia katika Utumishi wa Umma (entry point) hadi cheo cha mwisho kwa kila kada kulingana na kiwango cha elimu na kwa kuzingatia uzito wa majukumu ya kada husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuliarifu Bunge lako hili Tukufu kuwa Serikali itaendelea kuhuisha stahiki na stahili mbalimbali za watumishi wa umma pamoja na viwango vya mishahara ya kada mbalimbali kwa kuzingatia sera za kibajeti na uzito wa majukumu ya kada husika ili viweze kutumika kukokotoa mafao mbalimbali ya umma. (Makofi)
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kwanza nisahihishe majibu ya Mheshimiwa Waziri. Jina langu siitwi Alice Kapungi, naitwa Alice Karungi. Baada ya hapo nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kutokana na umuhimu wa Sera hii ya Taifa ya Tija: Je, ni lini sera hii itakuwa tayari ili iweze kutumika tena kukuza tija? (Makofi)

Swali la pili, kutokana na marekebisho ya sera, sheria na kanuni ndogo ndogo za uwekezaji kwa nia ya kukuza uwekezaji: Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kukishika kikamilifu kitengo hiki katika marekebisho haya ya sheria ili mwisho wa siku sheria hizi ziwe zenye kuleta tija? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, kwa kipindi chote amekuwa akitupa ushirikiano mzuri sana katika kuhakikisha tunafanya maboresho kwenye maeneo mbalimbali hasa kwenye maeneo ya kazi, vijana na pia kwenye masuala mtambuka kama ya UKIMWI.

Mheshimiwa Spika, swali lake la nyongeza, napenda kujibu kuhusu lini sera hii itakuwa tayari? Kwa hatua ya sasa tayari tumeshaanza kuchukua maoni kwa wadau. Bahati nzuri sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ameliuliza swali hili, kuna uwezekano mkubwa kwamba ana ufahamu na uelewa mpana juu ya jambo hili. Namwomba pia awe sehemu ya hao wadau ambao tutawafikia kwa ajili ya kukusanya maoni hayo tukiwa tunaenda kukamilisha sera.

Mheshimiwa Spika, baada ya bajeti hii nina imani kwamba kwa mwaka huu 2021 tunaweza kwenda kukamilisha sasa uwepo wa sera na pia kuangalia mabadiliko ambayo tutayafanya katika sheria. Hili litatusaidia sana kwa sababu tumeliona kama Ofisi ya Waziri Mkuu litatusaidia kukuza tija na ubunifu katika maeneo mbalimbali. Kwa mfano, kwenye maeneo ya Agro-industry, automobile industry, airspace industry, mechanical industry, petro-mechanical industry na kwenye maeneo mbalimbali ambayo ni mtambuka.

Mheshimiwa Spika, viwanda vyetu na maeneo mengine hata ya kazi yamekuwa yakitengeneza bidhaa ambazo mwisho wa siku kunakuwa na uzalishaji mkubwa, lakini ubora unakuwa chini. Kwa hiyo, hili ni eneo muhimu sana ambalo Serikali tumeona tuliangazie pia.

Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Dkt. Alice kuhusu kukamilisha utaratibu wote wa mchakato wa kisheria kuweza kuhakikisha suala hili nalo linakuwa na nguvu ya kisheria ukiacha hivi hivi; hilo litaenda sambamba pamoja na hatua ya sasa ya kukusanya maoni ambayo tumekwisha kuianza na tuna imani kubwa kwamba kufikia mwaka huu tutakuwa tumekamilisha zoezi hilo na kuweza kurasimisha ili kuleta mapendekezo ya mabadiliko ya sheria, sambamba na kuwa na sheria ambayo inaweza ikasimama hapo.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru sana Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina swali moja la nyongeza. Kutokana na uhitaji mkubwa na ukuaji wa tatizo hili la stroke, kwa maana ya kupooza na uhitaji wa mazoezi tiba na utengamao: -

Je, Serikali sasa ina mpango gani kuhakikisha kwamba inaboresha vitita vya Bima ya Afya ya Taifa na Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa ili tiba hii iwe jumuishi katika bima hizi kwa ajili ya ustawi wa wananchi wetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, kumekuwa na ongezeko kubwa sana la magonjwa yasiyoambukiza ambalo linasababisha uhitaji mkubwa sana wa tiba mazoezi pamoja na huduma za utengemao. Serikali inaendelea kuboresha mpango mkakati ambao utakuja na mbinu; kwanza za kuhakikisha tunaweka mipango madhubuti ya kuzuia magonjwa yasiyoambukiza; pili, kuwa na vifaa tiba vya kutosha na wataalam katika maeneo ya magonjwa yasiyoambukiza na pia utengamao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tutakwenda kuona wazo zuri la Mheshimiwa Mbunge tuone namna gani tunakwenda kuboresha eneo la bima ya afya, lakini na CHF na huduma nyingine kuweza ku-cover huduma hizi za mazoezi tiba na utengamao. Kwa hiyo, tumelichukua wazo hilo, ni zuri sana na kwa kipindi hiki ni wakati muafaka, tutakwenda kuoifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; nafahamu kwamba utaratibu wa kuomba fedha kwa awamu ya kwanza ya ukarabati umeshakamilika. Swali langu langu kwa Serikali: Je, ni lini fedha hizo zitatolewa ili ukarabati uanze?

Swali la pili: Je, Serikali ina mpango gani wa ziada kuhakikisha kwamba ukarabati wa majengo haya chakavu ya Milembe unakamilika katika awamu hii na awamu ijayo ya mwaka wa fedha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O MOLLEL): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo amesema Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kwamba kuna utaratibu ambao tayari umefanyika, lakini wakati utaratibu huo umefanyika imeonekana kwamba kwa kweli unahitajika ukarabati mkubwa sana na vile vile baadhi ya majengo kubomolewa na kujengwa upya, kwa hiyo, ikahitajika kufanyika tathmini kwa sababu fedha nyingi zitahitajika zaidi.

Mheshimiwa Spika, mara tu baada ya huu upembuzi kufanyika, kwanza kazi ambayo ilikuwa inaendelea itaendelea kufanyika, lakini tunahitaji ifanyike kazi kubwa zaidi kwa maana ya kuingia kwenye bajeti ya mwaka kesho 2022 ili ujenzi mkubwa ufanyike na ukitambua kwamba pale Mirembe inaenda kuwa taasisi kamili, sasa iko kwenye wakati wa kuunda muundo. Maa yake kutakuwa na ongezeko la kibajeti na wataweza sasa kuandika proposal zao binafsi ili kufanya research na pengine ile taasisi kuwa kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. Ahsante.