Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Ummy Hamisi Nderiananga (3 total)

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba kutoa maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jamii iliyo kuwa inawaona watu wenye ulemavu hawawezi kufanya kazi ikiwemo ujasiriamali. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha watu wenye ulemavu nao wajaikwamue kimaisha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kwenda Zanzibar kwenda kuwaona watu wenye ulemavu jinsi wanavyojikita kuhusu suala la ujasiriamali? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji. Amekuwa akifuatilia kwa ukaribu sana masuala yetu ya watu wenye ulemavu.

Niseme kwamba suala hili la watu kuwaona watu wenye ulemavu kama wanabaguliwa na hawawezi kufanya shughuli, nataka nimwambie tutaendelea kutoa elimu lakini kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tutaendelea kuwasaka wale wote wanaowanyanyapaa na kuwatumikisha watu wenye ulemavu ili kuchukua hatua stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tutaendelea kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu wao wenyewe waweze kujiamini na waone wana mchango katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari tuambatane naye baada ya kukamilika kwa bajeti hii na twende Zanzibar tukafanye kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia hapo Mheshimiwa Naibu Waziri ameweza kuonesha programu mbalimbali na nyingi ambazo Serikali inaendelea kuzifanya kwa ajili ya kuwasaidia vijana. Sasa wanasema wakati mwingine kuona ni kuamini. Hebu anieleze sasa: Ni lini Serikali walau itaanzisha hata programu moja katika Jimbo langu ili vijana wangu nao waweze kuona haya mengi ambayo Serikali imeweza kuyazungumza? (Makofi)

Swali la pili; kwa kuwa vijana wanaopata umri wa miaka 18 kwenda juu wapo wengi; na mojawapo ya jukumu kubwa la Serikali ni kuhakikisha kwamba vijana wanapata ajira: Je, ni kwa nini sasa Serikali isiwe na ule utaratibu kama iliyokuwa nao wa JKT wa crash programe ya miaka miwili au mitatu huko huko wanajifunza ukakamavu, kilimo, ufugaji wa samaki na mafunzo mbalimbali ili baada ya hapo Serikali iwape mitaji waweze kuendelea na maisha yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge Vedastus Mathayo Manyinyi kwa namna anavyojitolea katika kuhakikisha vijana katika Jimbo lake na nchi yetu wananufaika na progamu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile napenda kumhakikishia na kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali kupitia bajeti ambayo mmetupitishia ambayo itaenda kutekelezwa kuanzia mwezi wa Saba mwaka huu tutapeleka programu ya greenhouse katika mikoa tisa iliyobakia ikiwemo Mkoa wa Mara na tutajenga greenhouse hizi katika kila Halmashauri. Kwa hiyo na Musoma Mjini ambapo anatoka kaka yangu Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi itapata greenhouse hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile programu hizo za uanagenzi tutafanya na vyuo mbalimbali vilivyopo Mkoa wa Mara ikiwemo Chuo kile cha Lake Victoria na vyuo vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu sana na wenzetu wa JKT. Utakumbuka pia katika wasilisho la bajeti la Wizara ambayo inahusika na masuala haya ya JKT, Waheshimiwa Wabunge tulipokea ushauri wenu kwa kuona namna ambavyo JKT inaweza ikatusaidia katika kuwajenga vijana na kuwaandaa kikamilifu ili waweze kujiajiri na kuajiriwa na hata kuajiri wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. Ahsante. (Makofi)
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mojawapo ya maeneo yanayoweza kuongeza ajira kwa vijana ni eneo la kuongeza thamani kwenye bidhaa. Je, Serikali inamkakati gani wa kuja na programu zinazoweza kuwasaidia vikundi vya vijana vinavyopata mikopo ya halmashauri kuweza kuongeza thamani kwenye bidhaa ambazo inazalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; ni kutokana na mabadiliko mbalimbali ikiwemo ya Sayansi na Teknolojia zipo ajira mbalimbali zinazoweza kuzalishwa kutokana na mabadiliko hayo. Je, Serikali inamkakati gani wa kufanya maboresho ya sera ya vijana ili vijana waweze kupata ajira kutokana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea hususani katika Sekta ya Sayansi na Teknolojia. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwanza kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Judith Kapinga amekuwa akifanya kazi kubwa ya kutushauri Serikali katika eneo hili hongera sana Mheshimiwa Judith. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali lake la kwanza anauliza kuhusu kuongeza thamani, Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tunaendelea kuhakikisha kwamba tunawaunganisha vijana na fursa hizi mbalimbali tunashirikiana na wenzetu wa SIDO na UNIDO tuna mfano hai wa vijana wetu wa Kampuni ya JATU wanafanya vizuri kuongeza thamani, mazao.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna vijana wa Kiwanda cha Chaki kule Maswa, tuna vijana pia wa Kiwanda cha Mabegi Mwanza na vijana wengine na tunaendelea bado kuhakikisha kwamba vijana wetu wanaongeza thamani vitu wanavyozalisha badala ya kuuza raw material na tutaendelea kuendelea kutilia mkazo katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anataka kufahamu ni lini tutaleta sera hii; tupo katika hatua nzuri na tayari kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tumeshakusanya maoni kwa wadau wote wanaohusika na masuala ya vijana na tumemaliza sasa tuna rasimu ya kwanza ambayo inafuata utaratibu wa kiserikali na baadaye tutaendelea kuwafahamisha kwamba tumefika hatua gani, lakini tunaweza kuahidi tu kwamba kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa fedha tutakuwa tayari tuna sera ya vijana. Naomba kuwasilisha. (Makofi)