Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mwanakhamis Kassim Said (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia Wizara hii ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye mchango wangu. Leo tunazungumza ni mwaka 57 wa Muungano wetu na tunasema Muungano huu tutaulinda na tutautetea na ndipo tunapozungumza tunasema mbili zatosha, tatu za nini. Leo toka tulivyoanza kuchangia Muungano huu Wazanzibar ndiyo tumepangwa kuchangia. Kwa kweli inasikitisha na inaumiza kwa sababu huu Muungano siyo wa Wazanzibar peke yetu ni Muungano wa Tanzania nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ukizungumza hapa ukisema leo ni miaka 57 Muungano huu asilimia kubwa sisi viongozi wenyewe hatuujui na tunashindwa kuuzungumzia, zaidi tukizungumzia Muungano tutauzungumzia kisiasa, kumbe Muungano huu ni tunu ya nchi yetu; ni moyo wa nchi yetu; ni mishipa ya nchi yetu. Sisi tunasema tunatoka Zanzibar lakini na sisi vitovu vyetu vipo huku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi baba ni Mpemba, mama ni Mzaramo. Tunapouzungumzia Muungano lazima tuuzungumzie Muungano wa Watanzania; tuzungumzie Muungano wa wanyonge na tumzungumzie mtu wa chini.

Leo unapokwenda mikoani; utamkuta mwananchi kutoka Mtambwe lakini yupo Shinyanga na Shinyanga kule amewekeza kiwanda cha mchele lakini kuuzungumza Muungano kusema hajui, kwa sababu gani? Ni kwa sababu hatupewi elimu, wala wananchi hawapewi elimu kuhusu Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo unapokwenda mikoani, utamkuta mwananchi kutoka Mtambwe, lakini yupo Shinyanga; na kule amewekeza kiwanda cha mchele, lakini kuuzungumza Muungano, kuusemea hajui. Kwa sababu gani? Kwa sababu hatupewi elimu, wala wananchi hawapewi elimu ya Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwenye utalii tunapeperusha vipeperushi vya utalii. Kwa nini na Muungano tusipeleke vipeperushi wananchi wakaufahamu Muungano huu? Tumenyamaza zaidi! Leo tunanyanyuka kuzungumza Habari za Muungano, tunashindwa. Tunazungumza zaidi kisiasa, lakini kuuzungumza ile ilivyo, tunashindwa. Wapi tunafaidika, hatupajui; wapi tunakosea, hatujui; wapi tunapokwenda, hatujui. Tutayazungumza yale madogo madogo, lakini na makubwa yapo yanaumiza.

Mheshimiwa Spika, jimboni kwangu, Jimbo la Magomeni kuna wanawake hawana uwezo wa kwenda China, China yao ni Kariakoo, wanakwenda kuchukua madera, khanga, viatu wanaleta Zanzibar. Utakuta amekwenda na mwananchi kutoka Mwanza, atachuka mzigo wake ule atakwenda kuuza Mwanza, lakini mwanamke anayetoka Zanzibar Magomeni, anateseka akifika bandarini. Muungano huo, miaka 57, tunaomba mambo haya mdogo madogo yaondolewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi sisi ni wamoja, ni ndugu, ni wazaliwa wa damu moja na tumbo moja, wa baba mmoja. Wameshapita viongozi wengi katika nchi hii, lakini bado wanasema wataulinda na watautetea kwa nguvu zote. Nasi tunasema tutaulinda na tutautetea kwa nguvu zote. Tunasema mbili zatosha, tatu za nini? Hatuoni haya, hatuoni aibu wala hatujuti, tunasema Muungano utaendelea kwa yeyote atakayekuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, Mheshimiwa Marehemu Dkt. Omary Ali Juma alikuwa ni Makamu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alikuwa Waziri Kiongozi miaka minane, akawa Makamu wa Rais miaka saba. Alizikwa vizuri, kwa heshima zote, tunashukuru; lakini leo ukienda kwenye kaburi la Marehemu Dkt. Omary, inauma sana. Kwa kweli inatusikitisha. Mheshimiwa Dkt. Omary aliitumikia nchi hii kwa nguvu zake zote, hakuna ambalo hakujua. Alikuwa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, leo Mheshimiwa Dkt. Omary kaburi lake lina uzio wa waya toka laipozikwa hadi leo. Maana kaburi lile utasema siyo Makamu wa Rais, kama nililozikwa mie tu, nikaenda nikazikwa, nikawekewa kuti, watu wakaondoka. Kwa kweli inauma. Viongozi wetu waliopita tunawaacha. Tunawadhalilisha. Hii inauma, inakera. Wao wameanza, imefikia hivyo, wengine itakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sina zaidi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Mimi leo sitawapongeza, nitawaombea, namuombea Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri Mwenyezi Mungu awape nguvu na afya kwa kuwatetea wananchi wa Tanzania. Pia nichukue nafasi hii kumuombea Mheshimiwa Sirro na Kamishna wa Zanzibar kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kuwatetea wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, askari wetu wanafanya kazi ngumu sana, kwa kweli ni kazi ya kusikitisha. Asilimia kubwa ya Askari wa Jeshi la Polisi wanaostaafu ni nadra kuwakuta ni wazima. Askari wetu hawa wanafanya kazi ngumu wakistaafu wengi wana- paralyze. Hawa watu wanafanya kazi kubwa sana na ngumu na maeneo yao ya kazi siyo rafiki.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye vituo vya polisi Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza vipo kwenye hali ngumu lakini hata mazingira yao ya kazi wanapokuwa barabarani ni magumu. Wewe ni shuhuda leo ukiondoka kuanzia Dodoma kufika Dar es Salaam ni askari lakini jua, mvua wanapigwa askari wetu. Kazi yao ni ngumu sana, tutakaa tutawalaumu lakini askari wetu wanafanya kazi ngumu na kipato chao ni kigumu sana. Wapo askari siyo wazuri lakini kuna askari ni wazuri sana akiwemo Kamanda Sirro na Kamishna wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushahidi tosha ni wakati tunapofanya chaguzi. Askari wetu wanafanya kazi ngumu sana ya kudhalilishwa, kutukanwa, ni nusu kujuta kufanya kazi hii lakini hawana lingine la kufanya kwa sababu waliiomba kazi hii. Namuomba Mheshimiwa Waziri wawaone askari wetu kwa posho zao lakini na vitendea kazi. Sasa hivi unakwenda kwenye vituo kuripoti kesi ya ubakaji lakini unaambiwa hakuna gari wala hakuna askari kutoka pale kwenye kituo akamfuata mtuhumiwa, unaambiwa wewe kama unayo pesa utoe mafuta upeleke kule akachukuliwe mtuhumiwa. Mimi nahisi yote haya ni kwa sababu bajeti ni ndogo. Sababu ya vituo vyetu kuwa chakavu bajeti ni ndogo kwa sababu polisi si maskini wa wafanyakazi; wana wajenzi, watu wa umeme, nafikiri wana kila design ya mafundi, kwa nini wasipewe bajeti kubwa ya kufanya kazi zao wanakuwa ni watu wanyonge sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, turudi katika wale wanaostaafu, askari wetu wengi wanastaafu hawapati haki zao mapema. Unakuta askari kastaafu kama mwaka au miezi sita unamkuta ni omba omba. Haipendezi, inakera, inauma na wao ni binadamu kama sisi na wao ni wafanyakazi kama sisi, lazima askari wetu watunzwe wana kazi ngumu kutulinda sisi na mali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bora aombe kuliko kuiba. Wengi tunasema askari wanapenda rushwa lakini mimi nasema wasiombe rushwa ila kuomba ni haki kwa sababu hawaibi. Wanaomba kwa sababu wapo kwenye hali ngumu lazima tuungane bajeti ya watu hawa iwe kubwa, ni haki yao. Mimi nasema pesa hizi angekuwa nazo Sirro angewapa askari wote wakaneemeka au angekuwa Kamishna wa Zanzibar anazo pesa hizi angewapa askari wake wote wakaneemeka kwa sababu hataki waombeombe wala waombe rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini leo unawakuta askari wapo kwenye …

T A A R I F A

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, taarifa

SPIKA: Taarifa, endelea

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mchangiaji anayeendelea kuchangia kwamba kuomba ama kutoa rushwa ni mwiko na ni kinyume kabisa cha sheria bila kujali mazingira uliyopo. Naomba Mheshimiwa mzungumzaji awatetee askari lakini asitee rushwa. (Makofi)

SPIKA: Pokea hiyo taarifa Mheshimiwa Mwanakhamis.

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, sitetei rushwa, natetea askari wetu. Wengi tumezungumza hapa, wamesemwa wana vitendo vibaya, wanabaka, wanakera, wanaudhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nafikiri ni mwaka wa ishirini au na zaidi nipo kwenye siasa lakini sijawahi kukamatwa kupelekwa kituo cha polisi wala sijapelekwa magereza. Suala la magereza mimi sijui najua utendaji wa kazi wa askari wetu, kwa sababu sote humu tunapogombea anatulinda askari polisi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana muda umeisha.

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu chetu cha Quran mwanamke ametajwa mara tatu, mwanaume ametajwa mara moja, kwa nini sasa? Wengi tunamzungumza Mama Samia, tunampongeza kwa kazi nzuri alivyoanza, lakini mimi ninasema Mama Samia tumuombee dua usiku na mchana, huyu ni mama, huyu ni mwanamke. Nilisema Kitabu cha Quran mwanamke ametajwa mara tatu kwa sababu mama ndiye aliyebeba mimba, mama ni mlezi, mama ana upendo. Kwa hiyo, naomba Watanzania, Waheshimiwa Wabunge, tumuombee Mama Samia afanye kazi kwa kuwatendea haki Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumuombea dua Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri waliyoanza kufanya, Mwenyezi Mungu awape nguvu na afya kwa kuitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge niliyetokea Zanzibar. Bajeti imezungumza vizuri sana, lakini bado nitasema kuna mambo yanayotutanza Wabunge tunaotoka Zanzibar. Mimi leo nilileta gari langu karibuni na barua hii hapa. Barua hii nimepewa nije na gari langu kuishi nalo Tanzania Bara kwa mwaka mmoja, wakati mimi ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mkataba wangu nikiwa hai ni miaka mitano, leo nimepewa barua hii nikae na gari langu huku mwaka mmoja.

Je, tunamuuliza Mheshimiwa Waziri hii ni sheria au ni haki au ni nini? ama ni sisi tu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili niulizie kuhusu ma-agent kutoa gari Zanzibar kuja Tanzania Bara. Tuelezwe huyu agent ana mchango kwenye Serikali au ni nini? Tuelezwe kwa kweli imekuwa ni mateso ni maonevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa wafanyabiashara wadogo-wadogo. Tunapenda sana wafanyabisahara wadogo-wadogo, vijana, akina mama na wazee, lakini vijana na wazee sasa hivi biashara zao wanafanyia katikati ya barabara, kwa kweli hii ni hatari maana hata Serikali inakuwa mapato inapoteza. Unakuta leo sado za nyanya zimepangwa barabarani, pana ujororo tu wa barabara tunaopita na magari, kwa hivyo naomba suala hili lishughulikiwe. Kwa kweli, wapangiwe nafasi, sehemu nzuri ya kufanya biashara zao wao wapate, lakini na Serikali ikusanye mapato vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira. Ilipopita bajeti Wabunge wengi tulizungumza kuhusu maliasili, kama hatukulisimamia suala la maliasili basi maliasili nafikiri baada ya muda mdogo itakuwa wanyama wetu wengi watapotea. Leo Mheshimiwa Mbunge anasimama anasema yeye tembo hana faida nae, ng’ombe ndiyo wana faida nao. Mimi naiomba Serikali lazima Wabunge wale waliopo pembeni mwa hifadhi wapewe elimu pia na wafugaji wapewe elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema tembo hana faida kwa sababu tembo ni mnyama aliyeumbwa hifadhi yake ni kukaa kwenye hifadhi, hatembei, hata ukimfuata tembo unamfuata nyumbani kwake. Kwa hivyo, mtu yeyote anayemfuata mtu nyumbani kwake unakwenda kumtafuta ushari. Mimi nilikuwa naomba suala hili la hifadhi zetu lazima zilindwe, ziheshimiwe na sheria zifuatwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utalii. Tunasema sana utalii ni wa nje tulikuwa tunautangaza, lakini sasa tutangaze utalii wa ndani. Nani atatangaza utalii wa ndani? Kutangaza utalii wa ndani ni wananchi wenyewe wa ndani. Tuna wasanii wazuri, vijana, warembo, hawa tuwape ubalozi watangaze utalii wetu wasitafute watu wengine wa nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii. (Makofi)