Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Zuena Athumani Bushiri (4 total)

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ya mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto ya miradi kutokukamilika kwa wakati. Nini kauli ya Serikali kwa wakandarasi ambao hawamalizi miradi yao kwa wakati na kuchelewesha huduma kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kumekuwa na wimbi kubwa sana la wizi wa miundombinu ya umeme, mfano kule Moshi Manispaa, katika Kata za Soweto, Boma Ng’ombe, Barabara ya Bonite pamekuwa na wimbi la vijana ambao wanaiba miundombinu hii. Je, Serikali hii inachukua hatua gani kudhibiti uharibifu huu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali kuhusiana na miradi ambayo haijakamilika ni kwamba, kwanza ifikapo Disemba mwaka huu 2021 miradi yote ambayo siyo ya REA III round II itakuwa imekamilika kwa maana ya REA II na REA III round I itakuwa imekamilika.

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na changamoto kidogo zilizopelekea miradi hii kuchelewa, sababu mojawapo ikiwa ni kwamba ni vile vifaa ambavyo vilikuwa vinaagizwa nje ya nchi vilichelewa kufika kwa sababu ya lockdown za wenzetu kule kushindwa kuleta vile vifaa kwa wakati. Shida nyingine ilikuwa ni maeneo mengine miundombinu kuharibiwa na mvua kali na hivyo watu wakashindwa kukamilisha kazi zao kwa wakati. Hata hivyo, tumejiwekea utaratibu na tunawaahidi Watanzania kwamba ifikapo Disemba mwaka huu hakutakuwa kuna mradi wowote wa REA III round I au REA II ambayo inaendelea, itakuwa yote imekwisha. Miradi ambayo itakayokuwa inaendelea ni ya REA III round II ambayo nayo Disemba mwakani itakamilika.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha mambo haya hayajitokezi tena, Serikali ilielekeza kwamba vifaa vyote vipatikane hapa nchini na kweli vinapatikana. Hiyo inatuongezea speed ya kufanya kazi hizi na kuzimaliza mapema.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo Serikali imelifanya ni kuhakikisha sasa inatoka kwenye kufanya kazi hizi kwa mtindo wa goods na kuziweka kwenye works, kwamba mtu atalipwa baada kukamilisha kipande fulani cha kazi ambacho anatakiwa kukifanya na hiyo inatusaidia kusimamia vizuri maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo Serikali imelifanya, tumehakikisha sasa tunakwenda kila kanda na kila mkoa kuweka msimamizi wa miradi yetu ya REA, akae kule masaa 24 akimsimamia mkandarasi anayefanya kazi kuhakikisha kwamba kazi inakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, jambo la nne, tumehakikisha kwamba, wale wakandarasi wanaokwenda kwenye maeneo yetu tumewakabidhi kwa Waheshimiwa Wabunge ili na wenyewe wawe wasimamizi namba moja wa kuhakikisha kila siku wanawaona site na pale ambapo panatokea hitilafu ya kuwa mzembe mzembe, basi taarifa hizo zinatufikia mara moja. Tunaamini njia hizo zitatusaidia.

Mheshimiwa Spika kwenye jambo la pili; jambo la wizi siyo la mtu mmoja kulikemea, tunawaomba wenzetu tuendelee kushirikiana, sisi kama Wizara tunawapa support kubwa sana wakandarasi wanapotoa taarifa za kuibiwa, tunasaidiana nao moja kwa moja kuhakikisha kwamba tunafuatilia, kuhakikisha tunawachukulia hatua wale walioiba miundombinu. Pia tunaweka mikakati mingine ya ziada ya kuwasaidia wale wakandarasi kuweka vifaa vyao katika godown za TANESCO ili angalau viwe katika usalama zaidi.

Mheshimiwa Spika, vile vile tumewaelekeza, wao ndiyo wenye wajibu wa kuhakikisha mali hizo haziibiwi ili wafikishe mizigo ile na kazi ifanyike kwa wakati. Tunaamini kufikia Disemba mwakani, jambo la kupeleka umeme REA III round II litakamilika kwa muda uliopangwa kwa mujibu maelekezo ya Serikali. Nashukuru.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia swali la nyongeza. Changamoto iliyoko Jimbo la Kilolo ni sawa na changamoto iliyoko katika Hifadhi ya Same ambayo katika hifadhi hiyo barabara kuu inapita kuelekea katika Jimbo la Same Mashariki. Katikati ya Hifadhi hiyo, hakuna mawasiliano ya simu, jambo ambalo linapelekea vijana wengi kwenda kufanya mambo ya kiukorofi, kuteka baadhi ya magari na kuwapora wananchi mali zao. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha kwamba inajenga minara ya simu maeneo hayo ili endapo ukorofi kama huo vijana wataufanya, waweze kutoa mawasiliano kwa ajili ya kutetea haki yao? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Zuena Bushiri, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari ina mpango wa kuhakikisha kwamba tunapeleka mawasiliano katika maeneo ya mbuga na hifadhi ili kuhakikisha kwamba maeneo haya yasiwe na changamoto tena kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ilianza kama zahanati mnamo mwaka 1920 ikapandishwa daraja ikawa Kituo cha Afya mwaka 1922, ikapandishwa daraja ikawa Hospitali ya Mkoa mwaka 1956, mwaka 2011 ikapanda daraja kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Hospitali hii inahudumia Wilaya zote saba za Mkoa wa Kilimanjaro, lakini ina upungufu wa Madaktari Bingwa hususani upande wa wanawake.

Je, Serikali inasema nini kuhusu kuongeza madaktari bingwa wa Hospitali hii kwa sababu huduma stahiki wananchi wa Kilimanjaro hawazipati kutokana na ukosefu wa madaktari na madaktari bingwa?

Kutokana na miundombinu hii iliyoanza tangu mwaka 1920 ni kweli kabisa hospitali ile imechoka, mazingira…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa uliza swali.

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati na kujenga majengo ambayo yana hadhi ya kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake mzuri sana hasa kwenye eneo la hospitali hiyo, lakini kwa ufuatiliaji wake mzuri hasa kwenye huduma ya akina mama na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni kuhusu Madaktari Bingwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Mawenzi hospitali hiyo mpaka sasa ina ma-specialist, tisa lakini specifically idara anayoisema Mheshimiwa Mbunge ambayo inahitajika kuwa na Madaktari Bingwa wanne ina Daktari Bingwa mmoja. Kwa hiyo, ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge wakati tunajipanga kwa mwaka huu kwa maana ya ajira za mwaka huu Hospitali ya Mawenzi itakuwa mojawapo ya hospitali za kipumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sivyo tu kwamba kuna ma-specialist tisa, lakini kuna baadhi ya Idara kama Idara ya Mifupa ambayo haifanyi vizuri sana, tutaenda kufanya kazi kubwa kwenye kuboresha hasa kuweka kwenye vifaa, lakini kuelekeza utawala wa hospitali ili usimamie vizuri eneo hili liwe kufanya kupunguza rufaa kwenda KCMC.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pilli ni kuhusu miundombinu kwamba hospitali ni ya muda mrefu na kuna majengo ambayo yamechakaa na mengine kabisa hayafai kutumika. Ni kweli kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema na baada yeye kuja Wizarani, Mheshimiwa Waziri wa Afya alituma timu wiki mbili zilizopita, wameshakwenda Mawenzi na sasa wako kwenye hali ya kuangalia yale majengo ambayo hayafai kabisa na michoro imeanza kuchorwa ili kuja na mawazo ya namna gani tunaweza kuboresha hospitali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini kuna suala la ardhi pembeni ya Hospitali ya Mawenzi kuna ardhi ya Manispaa ambayo tunaweza tukafikiria namna ya kushirikiana na Manispaa kama inawezekana, lakini ukiangalia ramani yamwaka 1959 Hospitali ya Mawenzi na ukiangalia mabadiliko ya 2009 utaona kuna maeneo fulani ya hospitali hiyo ambayo vilevile hayaonekani kwenye ramani nayo yatashughulikiwa kuhakikisha sasa tunaenda kuja na mkakati ambao hospitali hiyo itaboreshwa vizuri sana, ahsante sana.
(Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni ukweli usiopingika kwamba ni barabara ambayo haipitiki kipindi chote cha mvua. Ni barabara ambayo inaleta manufaa sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa madini ya jasi ya Makanya yanalisha viwanda vya Tanga Cement, Twiga Cement, Moshi Cement, Doria Arusha na nchi za Rwanda na Burundi na kuiingizia Serikali mapato. Serikali haioni haja ya kuiboresha barabara kwa kuitengea fedha ili iweze kufanya kazi muda wote na kuongeza mapato ya Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, katika machimbo haya wako wanawake ambao wamewekeza kule ambao wamepata fursa ya kuendesha biashara ya mama lishe na biashara ndogondogo. Je, Serikali haioni kwamba kwa kusimama kwa machimbo haya kutokana na barabara korofi wanawake hawa wanadhoofika kiuchumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza maswali mawili ya msingi kabisa ambayo yana nia njema ya kuwasaidia wanawake wote wa Same mpaka Mkoa mzima wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza la msingi ambalo ameuliza hapa, amesema barabara hii haipitiki na ameomba Serikali tutenge fedha. Kwa kuwa maombi haya yametoka kwa mtu ambaye ameshakuwa kiongozi ndani ya chama na ni maombi muhimu sana,
nimwambie tu kwamba tutatuma wataalam wetu wa Ofisi ya Rais, TARURA, waende katika eneo hilo wakafanye tathmini ya kina na kuileta ofisini ili tuone namna ambavyo tunaweza tukasaidia barabara hii iweze kupitika wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, amesema kwamba kusimama kwa machimbo ya jasi kunasababisha uchumi kwa akina mama kuyumba na kuomba watu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kusaidia ili barabara hiyo iweze kujengwa. Kama nilivyojibu katika jibu la msingi kwamba tutahakikisha barabara hiyo inatengenezwa na inapitika kwa wakati wote kuhakikisha tunasaidia akina mama hao wanaoendesha biashara zao maeneo yale lakini vilevile tunawasaidia wananchi wa Same.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.