Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Zuena Athumani Bushiri (3 total)

MHE. ZUENA A. BUSHIRI Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza umeme katika Vijiji na Vitongoji kupitia REA III hasa katika maeneo ambayo nguzo zimetelekezwa barabarani zaidi ya miaka miwili?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini - REA na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), inaendelea kutekeleza mpango wake wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu, mzunguko wa pili katika vijiji vyote nchini. Utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Machi, 2021 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Disemba, 2022.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mradi huu unalenga kufikisha umeme katika vijiji 1,956 kati ya vijiji 12,268 ambavyo havijafikiwa na umeme. Kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji ni endelevu inayoendelea kutekelezwa kupitia TANESCO na REA ikiwa ni kazi ya kuendelea kuunganisha huduma ya umeme kwa wananchi.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:-

Je, lini Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Mawenzi litakamilika na kuanza kutoa huduma stahiki?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbuge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea na ujenzi wa jengo la kuwahudumia mama na mtoto ambalo kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 70. Mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni 10.5 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 5.3 kimetolewa na kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha dhilingi bilioni 57 kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya Hospitali za Rufaa za Mikoa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ambayo imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya vifaa na vifaatiba. Aidha, huduma zitaanza kutolewa baada ya kukamilika kwa ujenzi na ukamilishaji usimikaji wa vifaa ifikapo Januari, 2022.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Makanya kwenda kwenye Machimbo ya Jasi Wilayani Same?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Makanya hadi kwenye Machimbo ya Jasi Wilayani Same ina urefu wa kilometa 40.9. Kipande cha kilometa 4.5 cha barabara hii kimeinuliwa kwa kujengwa tuta kati ya kilometa 14.5 zinazotakiwa kujengewa tuta kwa kiwango cha changarawe. Kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha kuwa barabara hii inapitika muda wote na ndiyo maana imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya mara kwa mara.

Katika mwaka wa fedha 20219/2020, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Same umefanya matengenezo ya barabara ya Makanya hadi kwenye Machimbo ya Jasi maeneo korofi yenye urefu wa kilometa 3.54 kwa gharama ya shilingi milioni 77.36.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Same imefanya matengenezo ya barabara hiyo kipande chenye urefu wa kilometa mbili kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya shilingi milioni 49.4. Vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 61.25 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilomita moja pamoja na ujenzi wa makalavati 14.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya Makanya hadi kwenye Machimbo ya Jasi na itaendelea kuifanyia matengenezo ili kuhakikisha inapitika. Serikali itatoa kipaumbele cha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami katika bajeti zijazo ili kuiboresha na kurahisisha usafirishaji wa Jasi.