Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Maimuna Salum Mtanda (9 total)

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Jimbo la Newala Vijijini linakabiliwa na uhaba mkubwa wa upatikanaji wa dawa kwa wananchi wake. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na suala hili? Uhaba ule unachangia kwa kiasi kikubwa sana wananchi kushindwa kujiunga na mpango wa CHF iliyoboreshwa kwa sababu wamekatishwa tamaa na mpango wa awali, wakienda vituoni hawapati dawa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Jimbo la Newala Vijijini linakabilishwa na uhaba mkubwa pia wa watumishi, hali ambayo inazorotesha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi. Ni lini Serikali itapeleka watumishi wa afya katika Jimbo la Newala Vijijini ili wananchi wale wapate huduma inayostahili kama wananchi wengine? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imeweka kipaumbele kuhakikisha vituo vyetu vya huduma kote nchini vinakuwa na dawa za kutosha. Ndiyo maana katika kipindi cha miaka mitano, bajeti ya dawa ya Serikali imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 271 mwaka 2020. Hii ni jitihada kubwa sana ya Serikali kuhakikisha wananchi wanapata dawa za kutosha vituoni.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusisitiza, kwanza kuhakikisha Halmashauri zinasimamia ipasavyo mapato ya uchangiaji wa huduma za afya katika vituo vyetu. Nasi Waheshimiwa Wabunge ni sehemu ya Madiwani katika Halmashauri zetu, kumekuwa na changamoto ya usimamizi wa makusanyo ya fedha za uchangiaji ili ziweze kuongeza mapato ya vituo na kuboresha dawa katika vituo vyetu. Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu na kuboresha upatikanaji wa dawa nchini kote lakini katika Halmashauri ya Newala Vijijini.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na uhaba wa watumishi, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele cha hali ya juu sana katika kuboresha upatikanaji wa watumishi katika vituo vyetu. Mipango iliyopo ni pamoja na kuendelea kuajiri na ushahidi unaonekana. Katika kipindi cha miaka mitano, zaidi ya watumishi 14,000 na mwaka jana madaktari 1,000 wameajiriwa katika vituo vyetu mbalimbali. Zoezi hili la kuajiri watumishi wa afya ni endelevu na Serikali itaendelea kuajiri ili kuboresha huduma za afya katika nchi yetu.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Jimbo la Tandahimba pamoja na Newala Vijijini lina changamoto ya upatikanji wa vifaatiba pamoja na vitenganishi hali ambayo wakati mwingine inasababisha akinamama wanaojifungua kwenda kutafuta kadi za kliniki mitaani. Je, upi mpango wa dharura wa Serikali wa kunusuru hali hiyo ya upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na vitendanishi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Jimbo la Newala Vijijini lenye Kata 22 lina vituo vitatu tu vya kutolea huduma za afya hali ambayo inaleta changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wake. Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya katika Jimbo la Newala Vijijini ili wananchi wale wapate huduma za afya kama ambavyo inahitajika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya utoaji huduma za afya katika vituo vya afya kwanza kwa kutenga fedha kwa ajili ya kununua vifaatiba, vitendanishi lakini pia ununuzi wa dawa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha huu tunaoendelea nao Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 26 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba na tayari shilingi bilioni 15 zimekwishanunua vifaatiba na vimekwishapelekwa kwenye vituo vya afya vya awamu ya kwanza na awamu ya pili. Kiasi cha shilingi bilioni 11 kiko katika hatua za manunuzi na mara moja vifaa hivyo vitanunuliwa na kupelekwa kwenye vituo hivyo.

Mheshimiwa Spika, kituo cha afya katika Jimbo la Newala ni moja ya vituo vya afya vilivyojengwa katika awamu ya tatu na ya nne na hivyo vituo hivi vitakwenda kutengewa fedha za ununuzi wa vifaatiba katika mwaka wa fedha 2021/ 2022. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Maimuna Mtanda kwamba vituo vyake hivi vya afya vitawekewa mpango wa kununuliwa vifaatiba ili viendelee kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na idadi ya vitu vya afya katika kata za Jimbo la Newala Vijijini, ni kweli Serikali inatambua kwamba bado kuna uhitaji mkubwa wa vituo vya afya katika kata za Jimbo la Newala Vijijini na nchini kote kwa ujumla na ndiyo maana katika mwaka wa fedha ujao ambapo Mheshimiwa Waziri atawasilisha Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tunatarajia kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kujenga vituo vya afya katika kata za Jimbo hili la Newala na nchini kote kwa ujumla. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, suala hili litaendelea kufanyiwa kazi.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Wazir nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipande cha barabara Miyuyu - Ndanda kimekuwa kimetengewa fedha mara kwa mara za matengenezo ya kawaida, lakini fedha hizo hazitibu shida iliyoko kwenye mlima pale na barabara ile ni barabara ambayo inatumika kwa wagonjwa kutoka Wilaya za Newala na Tandahimba wanaopata rufaa kwenda Hospitali ya Ndanda. Hali ya pale ni mbaya, ni mlima kumbwa na korongo kubwa kiasi kwamba inahatarisha usalama kwa watumiaji wa barabara ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupata kauli ya Serikali. Ni lini itajenga kwa kiwango cha lami barabara ile hasa kipande kile ili wananchi wanaotumia hospitali ya Ndanda kama hospitali ya Rufaa waweze kupata urahisi wa kufika hospitalini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Jimbo la Newala Vijijini, zimesababisha athari kubwa sana ya barabara kukatika magari hayapiti, hata pikipiki zinapita kwa shida, kwa mfano barabara kutoka Malatu Shuleni - Namkonda hadi Chitekete, barabara ya Maputi - Meta, barabara ya Likwaya Nambali, barabara ya Mtikwichini - Chikalule, barabara ya Mtikwichini - Lochino na Chikalule.

Mheshsimiwa Naibu Spika, upi mpango wa Serikali wa kupeleka fedha kwa ajili ya dharura ya kutengeneza barabara hizo ambazo kwa sasa hazipitiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge aliuliza eneo korofi la Mlima Miyuyu mpaka Ndanda na amesema kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha, lakini bahati mbaya tatizo hilo limekuwa halitatuliki, kwa hiyo, alikuwa anaiomba Serikali ni lini itajenga lami katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jibu peke ninachoweza kumuhakikishia ni kwamba kutokana na ombi alilolileta na sisi Ofisi ya Rais - TAMISEMI tutakwenda tufanye tathimini na baada ya hapo tutaleta majibu ya eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sehemu ya pili barabara ambazo amejaribu kuzitaja Mheshimiwa Mbunge ambaye ninaamini anafanya kazi hii kwa nia njema ya kusaidia wananchi wake wa Jimbo la Newala, ameainisha maeneo mengi sana na kutaka mpango wa dharura na lenyewe nimuhakikishie kwamba Serikali tumesikia na kwa sababu katika mwaka huu wa fedha tumetenga fedha yakiwemo hayo maeneo ambayo ameyaainisha, lakini Serikali inaendelea na mchakato wa kutafuta vyanzo vingine.

Kwa hiyo kulingana na bajeti itakavyopatikana na sisi tutaakikisha kabisa kwamba tunatatua matatizo ya wananchi wa Newala na maeneo mengine ya Tanzania. Kwa hiyo, ahsante sana Mheshimiwa Mbunge tumepokea maombi yako na nikupongeze kwa kazi nzuri kwa wananchi wako, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza; kwanza nishukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nataka kujua namna ambavyo Wizara ya Mambo ya Ndani inashirikiana na Wizara ya TAMISEMI wenye shule kuhakikisha kwamba matukio haya sasa yanakoma kwa sababu, yamekuwa yakisumbua mara kwa mara katika shule zetu hasa za mabweni. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimtoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunao ushirikiano wa karibu baina ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na TAMISEMI na hata hawa watu wa Wizara ya Elimu katika kuhakikisha kwamba tunapunguza idadi kubwa ya majanga ya moto na majanga mengine hasa katika maeneo ya shule na maeneo mengine. Tayari tumeshakuwa tunakaa vikao mbalimbali, tumeshapanga mipango mbalimbali ambayo ni mikakati ya kuhakikisha kwamba tunapunguza haya majanga.

Kwa hiyo, hilo Mheshimiwa asiwe na wasiwasi juhudi zinaendelea kazi inaendelea na tutahakikisha kwamba tunapunguza haya majanga kwa kiasi kikubwa. Nakushukuru.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante. Naomba kuiuliza wizara maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Tatizo la maji kwenye Jimbo la Newala Vijijini limekuwa ni sugu, wananchi wa Newala Vijijini wanakunywa maji ya kuokota ambayo wanaokota kipindi cha mvua, maji ambayo huwa yanaoza na yanatoa harufu. Lakini tunacho chanzo kikubwa cha Bonde la Mitema ambalo Serikali ikiwekeza kwa kiasi kikubwa bonde lile litatua kabisa changamoto za maji kwa sababu maji yaliyopo katika bonde lile yana mita za ujazo zipatazo 31,200 lakini mahitaji ya wananchi wa Newala, Tandahimba pamoja na Nanyamba kwa siku ni mita za ujazo 23,441.

Je Serikali imejipangaje kuhakikisha inaweka fedha za kutosha katika bonde la Mitema ili tatizo la maji liweze kukoma na wananchi waweze kupata maji ya kutosha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika kituo cha Mto Ngwele kulikuwa na tatizo la pump house pamoja na transformer. Lakini bahati nzuri Januari mwaka huu pump house imerekebishwa na TANESCO wameshapelekwa pale transformer iko pale haijafungwa hadi leo hii ikaweza kusukuma maji. Nini kauli ya Serikali kwasababu wananchi wanaendelea kutaabika kupata maji wakati transformer iko pale wanashindwa kuifunga. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge kwanza nakupongeza sana wewe ni Mbunge wa Jimbo, mwana mama Hodari na umekuwa ukifuatilia kwa uchungu sana masuala la maji ili kuokoa kina mama wenzako kuhakikisha wanatuliwa ndoo kichwani kama ambavyo wizara tunakesha, tunafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba kina mama lazima tuwatue ndoo kichwani na maji yapatikane umbali mfupi kutoka kwenye makazi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake namba moja anauliza fedha za kutosha kuwezesha bonde la Mitema. Hii ni moja ya kazi ambazo tumeagiza RUWASA waweze kushughulikia, hii itafanyika ndani ya mwaka wa fedha ujao na kuona kwamba tuanze kuuona usanifu unakamilika na kila kitu kinakwenda vizuri ili maji yaweze kupatikana kwenye chanzo cha uhakika. Wakati tuna hitimisha bajeti yetu nimeongelea suala la Newala hata mimi ni mwana mama nisingependa kuona watu wanaendelea kutumia maji ya kuokota kwa karne hii na tumshukuru Mungu tumempata Rais mwana mama ambaye kiu yake kubwa ni kuona kina mama wanatuliwa ndoo kichwani. Mheshimiwa Mbunge Maimuna hili tutashirikiana kwa pamaja kuona kwamba tunakamilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusiana na transformer ambayo ipo pale. Sisi kwa upande wa wizara yetu tuliweza kushughulika na pump house na imeshakamilika. Kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Nishati kuona kwamba sasa ile transformer inakwenda kufungwa haraka iwezekanavyo ili matumizi ya umeme kwenye kusukuma maji yakaweze kufanyika na watu wakanufaike na mradi ambao umeshakamilika.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza kwamba, katika Jimbo la Newala Vijijini, kuna Mradi wa Maji wa Mnima Miuyu, mradi huu ulikuwa ni wa miezi tisa, ulikuwa ni mwaka 2018 na hadi leo hii haujakamilika. Je, ni lini mradi huu utakamilika ili wananchi wa Jimbo la Newala Vijijini waweze kupata maji ya uhakika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Naomba kujibu swali la Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote ambayo utekelezaji wake umeanza na ipo katika process, yote lazima itakamilika kadri fedha tunavyozipata na kadri ya muda ulivyopangwa. Hivyo nipende kumtoa hofu Mheshimiwa Mbunge, namna ambavyo amekuwa akizungumza nasi mara kwa mara, tuendelee kuwasiliana kwa karibu na tutakwenda pia kuona kazi imefikia wapi na kazi itakamilika kadiri inavyotakiwa.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante barabara ya kutoka Amkeni – Kitangali hadi Mtama yenye kilomita 74 ndiyo barabara pekee inayofungua mji wa Newala na maeneo mengine kuelekea Dar es Salaam hadi kuja huku Dodoma. Nakubaliana na Mheshimiwa Waziri kwamba fedha zitatengwa kwa awamu lakini ikumbukwe kwamba wilaya hii ni ya muda mrefu tangu 1952 hadi leo haina barabara ya uhakika. Je, ni lini Serikali itatenga fedha za kutosha ili barabara hii iweze kukamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kutokana na changamoto za ubovu wa hii barabara wafanyabiashara wengi wa usafirishaji wanakwama kupeleka vyombo vyao vya usafiri kwa hofu ya uharibifu wa vyombo vyao na wananchi wanateseka na usafiri kwa sababu ya ubovu wa barabara. Je, Serikali haioni kwamba inarudisha nyuma jitihada zake za ajira kupitia sekta zisizo rasmi hasa usafirishaji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi barabara hii ni kweli ni ya muhimu sana kwa mkoa wa Mtwara ambayo inaunganisha mkoa wa Lindi. Lakini kwa kulitambua hilo Wizara ya Ujenzi kupitia TANROAD inajenga maeneo korofi yote kwa kiwango cha lami na Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba maeneo mengi korofi yamejengwa kwa kiwango cha lami na hata katika mwaka huu wa fedha tunaoendea kuna fedha imetengwa kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha lami yale maeneo yote korofi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili, ambalo linafanana hili jibu la kwanza kwa sababu ya kutambua ule ubovu kwenye hii barabara ndiyo maana sasa TANROADS Mkoa wa Mtwara unafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba barabara hii inapitika muda wote na kuhakikisha kwamba maeneo korofi yote yanawekewa lami ili barabara hii iweze kupitika muda wote wa mwaka ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii. Chanzo cha maji ya Mitema ambacho kipo katika Jimbo la Newala Vijijini kina maji ya kutosha kiasi kwamba kama uwekezaji wa fedha utakuwa wa kutosha, tatizo la maji katika Jimbo ya Newala Vijijini, Newala Mjini, Tandahimba na baadhi ya Kata za Nanyama zitaondokana na shida ya maji. Je, ni lini Serikali itawekeza fedha za kutosha katika chanzo cha maji cha Mitema ili kuondoa kadhia ya maji kwa wananchi wa maeneo tajwa? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Newala Vijijini. Lakini pia nimpongeze sana, juzi tuliweza kukutana pia na Mheshimiwa Mbunge wa Newala Mjini, baba yangu, mzee wangu, Mheshimiwa Kapteni Mkuchika, juu ya Mradi huu wa Makonde. Ni mradi wa muda mrefu sana ambao umekuwa na maneno mengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwahakikishie nikiwa mwenye dhamana ya Wizara ya Maji, Mheshimiwa Rais ametupa maelekezo mahususi kwa ajili ya Watanzania, waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Juzi tumekaa kikao baada ya mazungumzo yale, maelekezo ambayo tumeyatoa ni kwamba mradi ule tunakwenda kuuanza, iwe jua iwe mvua, ili wananchi wa Newala waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali kuhusiana na barabara ya kutoka Amkeni – Kitangali hadi Mtama yenye kilometa 74.23 ambayo imeshajengwa kwa lami kwa kilometa 22.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba commitment ya Serikali ni lini itatafuta fedha kutoka kwa wadau wengine wa maendeleo ili barabara kipande kilichobaki kiweze kukamilishwa kwa kiwango cha lami kwa sababu Serikali imekuwa ikitenga fedha kidogo, inajenga kilometa tatu tu kwa mwaka?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupata jibu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY
K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba hii barabara aliyoitaja ya Amkeni kwenda Kitangali, tumekuwa tukitenga fedha kidogo kwa ajili ya ujenzi, lakini yote hii ni kutokana na uwezo wa bajeti. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kutafuta vyanzo vingine vya fedha kwa ajili ya kujenga barabara, siyo hii tu bali ni barabara zote, kwamba kadri fedha inavyopatikana, basi Serikali itaongeza fedha. Ndiyo maana hata tukitangaza barabara pengine kilometa tatu, lakini fedha ikipatikana Serikali hatusiti kuongeza bajeti kwa ajili ya kuendeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na barabara hii, kadri fedha itakavyopatikana, Serikali itazidi kuongeza kiasi cha fedha. Ahsante.