Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Maimuna Salum Mtanda (5 total)

MHE. MAIMUNA S. MTANDA Aliuliza:-

Halmashauri ya Wilaya ya Newala ina Kata 22 na Vijiji 107, lakini ina Vituo vya Afya vitatu tu, kati ya 22 vinavyohitajika.

Je, Serikali haioni haja ya kujenga Vituo vipya vya Afya katika Halmashauri ya Newala ili kuboresha huduma za Afya kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM) kwa kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Kuanzia mwaka 2015 hadi Septemba 2020, Serikali imejenga Zahanati 1,198; imejenga na kukarabati Vituo vya Afya 487 na imejenga Hospitali za Halmashauri102.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 na 2019/2020, Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Newala kiasi cha Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri na Shilingi milioni 400 kwa ajili kufanya ukarabati wa Kituo cha Afya Kitangari. Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni moja (1) kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri na Shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya Zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa awamu kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itaongeza bajeti ya barabara za Newala Vijijini ambayo imetengewa fedha za kilometa 340 wakati zina mtandao wa barabara wa kilometa 960?

(b) Je, Serikali inatoa msaada gani wa dharula kwenye matengenezo ya barabara za vijijini vinavyozungukwa na milima au mito kama vile Mkongi – Nanganga, Mikumbi – Mpanyani, Namdimba – Chiwata, Mkoma – Chimenena na Miyuyu – Ndanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Newala ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 960.04. Serikali imekuwa ikiongeza fedha za bajeti ya matengenezo ya barabara katika Halmashauri ya Newala mwaka hadi mwaka. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, shilingi milioni 939.27 zilitengwa kwa ajili ya kuzifanyia matengenezo barabara zenye urefu wa kilometa 343.86, mwaka wa fedha 2020/2021, shilingi milioni 976.88 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 320.38.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.056 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 277.35 na ujenzi wa mifereji yenye urefu wa kilometa 1.37.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 barabara ya Mkwiti - Lochino - Nyangao yenye urefu wa kilometa 11.1 imefanyiwa matengenezo kwa gharama ya shilingi milioni 84.78. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 barabara hii imetengewa shilingi milioni 56.32. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi milioni 87 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Maputi – Mikumbi – Miyuyu – Ndanda Kibaoni yenye urefu wa kilometa 17.5 ikiwa sehemu ya kipande cha Mlima Miyuyu – Ndanda na shilingi milioni 56 kwa ajili ya matengenezo ya maeneo korofi yenye urefu wa kilometa 3.5 ili iweze kupitika hadi Kijiji cha Lochino.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itaimarisha na kuboresha miundombinu ya maji ya Mamlaka ya Maji Makonde ili Wananchi waweze kupata maji ya uhakika?

(b) Je, Serikali inachukua hatua gani za dharura kuboresha upatikanaji wa maji Newala Vijijini ambapo kwa sasa uzalishaji ni ujazo wa lita 6,700 tu kwa siku badala ya lita 23,741?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya maji ya Mamlaka ya Maji Makonde inayohudumiwa Wilaya za Newala, Tandahimba na Nanyamba.

Katika kutatua changamoto hiyo, Serikali imeendelea na ukarabati wa miundombinu ambapo katika mwaka huu wa fedha 2020/2021 kazi zinazofanyika ni kukarabati mitambo na mfumo wa umeme katika vituo vya kuzalishia na kusukuma maji. Utekelezaji wa kazi hizi unalenga kuongeza uzalishaji wa maji kutoka meta za ujazo 6,700 kwa siku hadi meta za ujazo 11,116 kwa siku, kazi inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupata suluhisho la kudumu la tatizo la maji katika maeneo hayo, Serikali kuanzia mwaka 2021/2022 imepanga kutekeleza kazi mbalimbali ikiwemo kuongeza idadi ya visima vya kuzalisha maji kutoka 6 hadi 12 kwenye Bonde la Mitema pamoja na kupanua miundombinu ya kusafirisha maji uchimbaji wa visima utaongeza uzalishaji wa maji kutoka meta za ujazo 11,116 hadi Meta za ujazo 23,741 kwa siku. Kukamilika kwa kazi hizo kutaboresha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 58 za sasa hadi asilimia 95.

Vilevile Wizara ya maji kupitia RUWASA katika mwaka wa fedha 2020/2021, imeendelea na utekelezaji wa miradi ya maji Mchemo na Chiule iliyotarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2021 na miradi ya maji Mtongwele, Miyuyu na Mnima inayotarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2021. Katika mwaka 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni
1.95 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali katika Wilaya Newala Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katika mpango wa muda mrefu, Serikali ilipata mkopo kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India jumla ya dola za Marekani Milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa Miji 28 ukiwemo mradi wa Makonde; ambapo maeneo yatakayonufaika ni vijiji 155 vya Wilaya ya Newala. Ujenzi unatarajiwa kuanza wakati wowote katika mwaka wa fedha 2020/2021.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mkwiti – Amkeni inayounganisha Mkoa wa Lindi na Mtwara kupitia Mtama?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mkwiti – Amkeni yenye urefu wa kilometa 74.23 inayounganisha Wilaya ya Tandahimba na Newala katika Mkoa wa Mtwara na Wilaya ya Lindi Vijijini mkoa wa Lindi unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, jumla ya shilingi milioni 1,807.00 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa kilometa tatu ambapo jumla ya kilometa 2.8 zimekamilika kujengwa na kazi za ujenzi zinaendelea kwenye kipande chenye urefu wa mita 200. Wakati ujenzi kwa kiwango cha lami ukiendelea kutekelezwa kwa awamu, Wizara yangu itaendelea kuifanyia matengenezo barabara hiyo ili iweze kupitika majira yote ahsante.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya ujenzi wa mnara wa mawasiliano wa Halotel katika Kata ya Chilangala ambapo mkataba ulisainiwa mwaka 2020 lakini mpaka Septemba, 2021 mradi huo haujaanza?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARl alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) katika zabuni ya awamu ya nne ya kufikisha mawasiliano maeneo ya vijijini, iliingia mkataba wa kufikisha huduma ya mawasiliano ya simu katika Kata 114 ikiwemo Kata ya Chilangala na Kampuni ya Halotel (Viettel) mnamo tarehe 24 Januari 2020. Utekelezaji wa mkataba huo ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi tisa yaani tarehe 23 Oktoba 2020. Lakini kutokana na changamoto ya UVIKO-19 utekelezaji wa mradi huo ulichelewa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kutokana na ucheleweshaji wa utekelezaji wa mradi huo ulipelekea watoa huduma wengine kuboresha huduma za mawasiliano katika kata hiyo ambapo Kata ya Chilangala ina mawasiliano ya Mtandao wa Tigo ambao wana minara miwili katika Vijiji vya Chilangala na Namdimba. Hivyo basi, Serikali haitojenga mnara huo katika Kata ya Chilangala, na hivyo kuzielekeza fedha hizo katika maeneo mengine yenye changamoto zaidi za mawasiliano. Ahsante.