Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa (8 total)

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa sababu amenihakikishia kwamba mradi unakamilika Machi mwaka huu, napenda sasa kupata kauli ya Serikali kwa sababu bado tuna vijiji takribani 25 pale Biharamulo ambavyo havina umeme, kwa hiyo, labda ningehakikishiwa na Serikali sasa kwamba wakazi wa Biharamulo wajipange kwa ajili ya kusambaziwa umeme kwa sababu jibu ilikuwa tuko low voltage ndio maana hatukusambaziwa umeme katika vijiji vingine. Kwa hiyo, labda nipate kauli ya Serikali kutuhakikishia kwamba vijiji vilivyobaki baada ya kukamilika mradi huu vitaweza kupata umeme pia? Ahsante sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, uniwie radhi sana ili niweze kusimama kwa ajili ya kuongeza majibu na nimesimama kwa sababu hivi karibuni nilitembelea Biharamulo.

Mheshimiwa Spika, Biharamulo wana vijiji takribani 79 na bado vijiji 27. Hivi karibuni pamoja na Mheshimiwa Mbunge nilitembelea vijiji hivyo, tumeshakamilisha matayarisho yote na si kwa Biharamulo peke yake.

Napenda nitoe taarifa mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba vijiji vyote ambavyo havijapata umeme 2,159 kati ya vijiji 12,268 tunaanza kuvipelekea umeme kuanzia tarehe 15 mwezi huu ndani ya miezi 18, nimeona nianze na taarifa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa Biharamulo umeme ambao tunajenga ambao kwenye jibu la msingi umeelezwa wa kutoka Geita-Nyakanazi, Nyakanazi-Rusumo na Nyakanazi- Kigoma ni mwarobani kwa kuwapatia umeme wananchi wa Biharamulo na Mkoa wa Kagera na mikoa ya Geita pamoja na Kigoma. Mradi wenyewe peke yake kabla ya kupeleka umeme kwenye mpango wa REA utapeleka vijiji 32 na katika vijiji 32 vijiji saba ni vya Biharamulo, ikiwemo Nyakafundwa, Kalenge, Kasonta pamoja na Nyanyantakala, Mavota mpaka Nakahanyia vyote vitapelekewa umeme.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Nitoe shukrani kwa Serikali kwa majibu mazuri kabisa ya kuridhisha kwa ajili ya wananchi wa Biharamulo lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Miji ya Nyakanazi, Nyakahura na Nyanza ni miongoni mwa sehemu ambazo zinapanuka kwa kasi katika Wilaya ya Biharamulo lakini bado zina ukosefu wa maji. Naomba kujua au kusikia kauli ya Serikali jinsi gani hawa wananchi wataweza kupatiwa huduma ya maji katika mwaka huu wa fedha au mwaka ujao ili tuweze kuondoa kero hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kata ya Kaniha na Nyantakala zinabeba shule mbili kubwa za boarding pale Biharamulo na shule zile zina uhaba mkubwa wa maji. Naomba kupata kauli ya Serikali ni lini wataweza hata kuchimbiwa visima viwili virefu katika shule zile ili watoto hao waweze kuondokana na adha ya kupata maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua vema tatizo la maji lililopo pale Biharamulo. Hivi karibuni Mheshimiwa Waziri alikuwa katika Kata ya Nyakahura kwenye ziara yake ya kikazi. Kwa sasa maji toka Bwawa la Nyakahura ambapo vijiji vinne vinapata maji, tunatambua utekelezaji wake unakwenda vizuri kwa vijiji vile vinne.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tunafahamu kuna ushirikiano mzuri kati ya RUWASA pamoja na BWSSA. Tayari Serikali inafahamu chanzo kile bado hakitoshelezi kwa sababu ya ongezeko la watu. Tayari Serikali kupitia EWURA imeshatenga fedha za usanifu wa maji kutoka kwenye Mto Myovozi. Lengo ni kuona kwamba eneo lote la Nyakahura linakwenda kupata maji safi na salama ya kutosheleza hivi karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye kwenye Kata ya Nyanza usanifu unaendelea. Pia tutahakikisha maji ya kutosha yanakwenda kupatikana. Tayari kuna chanzo chenye uwezo wa lita 50,000 kwa saa ambapo maji haya yatasaidia sana mpaka kwenye Kata ya Nyanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali inatambua umuhimu wa maji mashuleni. Tayari kwenye Shule ya Mbaba kuna kisima kirefu pale kimechimbwa na maji yanapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Nyantakara, mradi umetekelezwa. Pale tuna mradi mkubwa tu ambapo fedha zaidi ya shilingi milioni 300 zimeelekezwa na maji yatafika mabombani muda sio mrefu, haitazidi wiki tatu.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana; na mimi kwa niaba ya wananchi wa Biharamuro ningependa niongezee swali la nyongeza. Wilaya ya Biharamuro ni miongoni mwa wilaya kongwe kabisa za nchi hii lakini ukiingia katika mazingira ya polisi wa Biharamuro wanapoishi, bado wanaishi kwenye nyumba zilizojengwa na Mkoloni pale. Lakini mazingira ya kazi ni magumu wote mnajua kumekuwa na majambazi kule lakini vijana wale wanajitahidi kupambana nao usiku na mchana na hali yetu ni shwari kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maswali niliyonayo ni mawili, ni lini tutajengewa kituo kipya cha Polisi, ikizingatiwa tayari hati iko pale na kiwanja kipo tayari? Lakini pili…

NAIBU SPIKA: Moja tu Mheshimiwa; moja tu.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa ruhusa yako, nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kukiri tena kwamba bado tuna changamoto hasa kwenye usafiri, makazi na Vituo vya Polisi. Kwa kuwa, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, tayari wana hati ambayo inawamilikisha wao waweze kujengewa eneo zuri waweze kupata jengo zuri ambalo litatoa huduma za ulinzi na usalama kwa wananchi, nimwambie tu kwamba aendelee kustahimili na mimi nalichukua hili tunakwenda kulifanyia kazi ili tuhakikishe kwamba katika eneo lake wanapata kituo kikubwa kizuri na cha kisasa ambacho kitaendelea kutoa huduma kwa wananchi na wananchi wakaendelea ku-enjoy hiyo huduma ya ulinzi na usalama katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na pesa ambayo tumeipata hiyo shilingi bilioni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa sababu majengo yanaelekea kukamilika na tumefikia mwisho sasa, ni nini mpango wa Serikali kutupatia vifaatiba ili majengo haya angalau yaweze kuanza kufanya kazi haraka iwezekanavyo kwenye robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2021/2022?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu hospitali hii bado ni sehemu ya kwanza itakuwa haiwezi kulaza wagonjwa, ni nini mpango wa Serikali kwenye kutupatia ambulance mpya na ya kisasa ili angalau wagonjwa wale ambao hawataweza kupata huduma kwenye Hospitali ya Wilaya waweze kukimbizwa na kupatiwa huduma sehemu nyingine kipindi tunaendelea na kukamilisha ujenzi wa awamu ya pili? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Eng. Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba majengo haya ya Hospitali ya Halmashauri ya Biharamulo yako katika hatua za mwisho za ukamilishaji. Katika mpango wa bajeti wa mwaka 2021/2022, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kwenda kununua vifaatiba kwa ajili ya hospitali hizi mpya ambazo zinaendelea na ujenzi. Kati ya hospitali hizo, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ni moja ya hospitali ambazo zitatengewa bajeti hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili tunahitaji kuwa na magari ya wagonjwa katika hospitali zetu za halmashauri na mipango ya Serikali inaendelea kufanyika ili kuona namna ambavyo tunaweza tukapata magari hayo na kuyafikisha katika halmashauri hizi. Kwa hivyo, Hospitali ya Halmashauri ya Biharamulo ni moja ya hospitali ambazo zitawekewa mpango wa kupata gari la wagonjwa ili tuweze kuboresha zaidi huduma za afya katika eneo hilo.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza ambayo ningependa kupata majibu yake. Swali la kwanza; kwa kuwa barabara hii ni kiunganishi muhimu ambacho kinaunga Chato na Biharamulo kuelekea katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato, ningependa kujua sasa kwamba construction period ya barabara hii itakuwa ni miezi mingapi ili nijue na wananchi wale waweze kujipanga kwa ajili ya kuchukua fursa za pale?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuzingatia umuhimu wa Hifadhi ya Chato Burigi na location ya Uwanja wa Ndege wa Geita Chato ulipo, sasa ningependa kujua je, Serikali haioni ni wakati muhimu sasa wa kuijenga barabara hii sambamba na barabara ya Mkingo – Chato kupitia Kaswezibakaya ili iweze kuunganisha Kabindi pale watu wanaokuja waweze kutoka vizuri? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ezra Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi ni kwamba barabara hii imetengewa fedha kwenye bajeti hii na yeye Mheshimiwa Mbunge ni shahidi. Kipindi cha matengenezo kitategemea na hali halisi, lakini cha msingi tu ni kwamba mara bajeti itakapoanza barabara hii itaanza kujengwa, lakini kipindi kitakachotumika itategemea na taratibu za manunuzi zitakavyokamilika, lakini pia na hali ya hewa itakayokuwepo. Kwa hiyo, ni ngumu kusema itachukua muda gani, lakini tutaanza kujenga mara tu bajeti itakavyoanza kutolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, barabara hii itaendelea kukarabatiwa katika kiwango cha changarawe. Hata hivyo, azma ya Serikali ni kuijenga kwa kiwango cha lami kadri fedha itakavyopatikana ili watalii na watu mbalimbali waweze kupita kwenye hizo mbuga za wanyama na kufika kwenye Uwanja wa Ndege wa Chato. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali, lakini pia labda nieleze kidogo; mnamo tarehe 1 mwezi wa Kumi mwaka jana 2020 tukiwa katika kampeni Waziri Mkuu aliahidi ujenzi wa soko hili pale Nyakanazi na tarehe 11 mwezi wa Pili wakati akijibu Maswali ya Papo kwa Papo, swali lililoulizwa na Mheshimiwa Neema Lugangira aliahidi pia ujenzi wa soko hili na akataja kabisa ni soko la kimkakati na akataja value yake kama ni 3.5 billion.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye majibu ya Serikali wanasema wanahamasisha Halmashauri ya Biharamulo ili iweze kufanya ujenzi wa soko hili; hili soko limetamkwa, ukisema 3.5 billion kwa Halmashauri ya Biharamulo wajenge soko hili, labda litakaa zaidi ya miaka kumi, kwa sababu uwezo huo hatuna; na ilitamkwa humu ndani ya Bunge: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate commitment ya Serikali kwanza nijue financing ya soko hili itafanyika vipi? Sisi uwezo huo hatuna. Kwa hiyo, nipate majibu ya Serikali kama Serikali kuu itafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu soko hili ni muhimu kwa ajili ya kufungua ukanda wetu na ni soko la kikanda litakalohudumia nchi za Kongo, Burundi, Rwanda na nchi nyingine zote za Jirani: nipate majibu ya Serikali, ni lini ujenzi wa soko hili utaanza? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali ina mkakati na mipango mbalimbali ya kuhakikisha inatekeleza ahadi ambazo viongozi wa Serikali wanaahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Chiwelesa kwa ufuatiliaji mkubwa anaofanya kwa ajili ya maendeleo katika Jimbo lake la Biharamulo Magharibi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli masoko haya ya kimkakati na hasa masoko ya pembezoni ambayo yako katika mipaka ya nchi za jirani na hasa hizi za Kongo, Rwanda na Burundi ni masoko ambayo yana umuhimu sana kuyaendeleza ili yaweze kuleta maendeleo ya nchi, lakini kuwapatia kipato wananchi wanaokaa katika maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kupitia programu ya ASDP II ambayo pia imeweka ule mfumo wa O and OD ambao ni fursa na vikwazo kupitia utaratibu huo, Halmashauri zinahamasishwa kuangalia vyanzo mbalimbali vya ku-finance mipango yao, mikakati yao katika kuendeleza sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na TAMISEMI tuna mikakati mbalimbali ambayo pia kupitia humo tunaweza kujenga masoko haya kulingana na fedha zinazvyopatikana. Nakushukuru sana.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi pia.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Biharamulo tuna vijiji 75. Kati ya vijiji 75 vijiji 25 havina mawasiliano kabisa, kabisa, na bado tuna shida, ukiachilia mbali vitongoji. Sasa ni nini hatua ambayo Serikali imachukua kwa ajili kuweza kuboresha mawasiliano? Ukizingatia watu hawa nao inabidi washiriki mchango wa maendeleo wa nchi hii lakini wameachwa mbali kwa sababu wako katika maeneo ambayo hayana mawasiliano kabisa. Nataka kusikia kauli ya Serikali kuhusu vijiji 25 vya Biharamulo.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ezra Mbunge wa Biharamulo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Kagera, Wilaya ambayo imebahatika na ambayo itanufaika katika mpango wa utekelezaji mradi wa mipakani basi na Biharamulo inaenda kupata miradi takribani sita.

Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana na kuhakikisha kwamba kipindi kitakapofikia tena cha kuleta bajeti ili tuweze kuhakikisha kwamba maeneo mengi yanapata mawasiliano basi aweze kutuunga mkono kuhakikisha kwamba bajeti hii iweze kwenda kujibu mahitaji ya Watanzania. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa na tatizo kubwa sana katika eneo hili la hifadhi hii ya Burigi Chato na tunashukuru kwa fedha ambazo zimetolewa na kutoa elimu kwa umma unaozunguka hifadhi ile. Kumekuwa na kesi kubwa sana pale za mifugo ya watu kukamatwa ndani ya hifadhi lakini baada ya kukamatwa zinapopelekwa kesi mahakamani, watu wale wamekuwa wanatozwa fine ya Shilingi 100,000/= kwa kila ng’ombe na wengi wanalipa baada ya kutozwa ile fine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa shida imekuja unatoza fine mahakamani ulikamatiwa ng’ombe 100 unapopewa barua ya mahakama, umeshalipa fedha ya Shilingi Milioni 10 ukarudishiwe ng’ombe wako unaenda unakuta ng’ombe wako 70, ng’ombe wako 80 badala ya ng’ombe waliokamatwa.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kusikia kauli ya Serikali juu ya vitendo hivi ambavyo vimesababisha wananchi wa Biharamulo kuteseka na hatimae kupoteza fedha zao na ng’ombe hao ambao wamekuwa wanapotea huko. Nisikie kauli ya Serikali juu ya hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kumekuwa na kesi pia wananchi wananifuata ninapokuwa Jimboni, saa nyingine wanapiga simu na kwa DC kesi zipo. Mwananchi anakuja analalamika kwamba, Mheshimiwa Mbunge nimekamatiwa ng’ombe wangu 50 bado tuna kesi mahakamani, lakini ng’ombe wangu nimewaona kwenye mnada wanauzwa. Sasa naomba kusikia kauli ya Serikali juu ya hili jambo ambalo limesababisha watu sasa wanaona taabu kabisa na wanatuchonganisha na wananchi. Tukisikia kauli ya Serikali juu ya hili pia hao ng’ombe ambao wamekuwa wanauzwa kwenye mnada je, hatuoni haja ya Serikali kuunda Tume Maalum, kwa ajili ya kwenda kuangalia hivi vitendo vya wananchi kulalamika? Kwamba, ng’ombe wao wanauzwa kwenye mnada na ilhali bado kesi zinaendelea mahakamani.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika,
ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niendelee kutoa pole kwa wale wananchi ambao wameendelea kukutana na kadhia hii, ya kudhulumiwa mifugo yao na kumekuwa ndiyo na malalamiko mengi na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walishawahi kunifuata kwamba, kuna baadhi ya wahifadhi wasio waaminifu ambao inapelekea mifugo yao kutotimia kama ambavyo imekamatwa awali.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tunafahamu Sheria za Utumishi wa Umma, watumishi hawa tumekuwa tukiwachukulia hatua wale ambao wanahusika na kadhia hii ikiwemo upotevu wa mifugo. Lakini pia kumekuwa na changamoto ya baadhi ya mifugo ambayo huwa inakufa wakati ikiwa inasubiri kupelekwa Mahakamani kwa maana ya kesi inapochukua muda mrefu Mahakamani inapelekea baadhi ya mifugo kupoteza maisha. Lakini kwa upande mwingine ambao amesema Mheshimiwa Mbunge kwamba mifugo mingine inaonekana iko minadani, basi Serikali itaendelea kufuatilia na wale watumishi ambao wanahusika na changamoto hizi tutawachukulia hatua. Na inapothibitika basi wengine tunawasimamisha kazi na hata kufukuzwa kazi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge ambao wana changamoto hii, niwaombe pale kuna mfugaji ambaye amekutana na changamoto hii basi watusaidie kutupa hizi taarifa. Lakini pia niwaombe Waheshimiwa tuendelee kuelimisha hawa wafugaji pia, wakifuga kwa kufuata Sheria na taratibu za nchi ninaamini kabisa kadhia hii tutaipunguza kabisa ama kuimaliza. Ahsante. (Makofi)