Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa (6 total)

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza:-

Je, ni lini mradi wa kujenga Sub-station ya Nyakanazi (KV 220) toka Rusumo na Geita utakamilika ili kuondoa tatizo la kukatikakatika kwa umeme Biharamulo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovolti 220 kutoka Geita hadi Nyakanazi. Mradi huu unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Geita - Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 144 ambapo Mkandarasi Kampuni ya M/S Kalpataru Power Transmission Ltd kutoka nchini India anaendelea na kazi za mradi. Hadi sasa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme pamoja na kituo cha kupoza umeme umefikia asilimia 60.

Mheshimiwa Spika, gharama ya mradi ni EURO milioni 45 sawa na takriban shilingi bilioni 117.79. Mradi huu unatarajiwa kukamilika Machi, 2021. Ni mategemeo ya Serikali kuwa mradi utakapokamilika utaimarisha na kuboresha hali ya upatikanaji umeme katika maeneo ya Wilaya ya Biharamuro na maeneo mengine ya jirani.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa mradi wa kutoa maji toka Ziwa Victoria kuyapeleka Biharamulo kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi hapo tarehe 16/09/2020 alipokuwa Biharamulo katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu, 2020?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto za upatikanaji huduma ya maji katika Wilaya ya Biharamulo. Hivyo, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali inatekeleza mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji wenye urefu wa km 10.9 katika maeneo ya Ng’ambo, Kalebezo, Nyakatuntu, Rubondo Chuoni na Rukaragata na kuchimba kisima katika eneo la Rukagarata. Thamani ya mradi huu ni shilingi milioni 178.9 na utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 70.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto ya uhaba wa maji katika Mji wa Biharamulo, Serikali iliamua chanzo cha uhakika cha maji kiwe Ziwa Victoria badala ya bwawa na chemichemi vinavyotumika kwa sasa. Hivyo mradi wa usambazaji maji katika Mji wa Biharamulo ambao utatoa maji katika Ziwa Victoria umefikia katika hatua ya kuandaa makabrasha ya zabuni (tender documents). Utekelezaji utaanza katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Aidha, kupitia Mradi wa Maziwa Makuu, Wilaya ya Biharamulo itanufaika kupitia chanzo cha Ziwa Victoria ambapo jumla ya vijiji 12 vya Rwekubo, Rusese, Kabindi, Runazi, Rukora, Kikomakoma, Kagoma, Songambele, Kasozibakaya, Nyamigogo, Chebitoke na Nyabusozi vitapata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza:-

Serikali ilitoa shilingi 500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo, lakini kiasi cha shilingi 204,000,000 kilirejeshwa baada ya kufunga mwaka Julai, 2020.

(a) Je, ni lini fedha hizo zitarejeshwa ili ujenzi uendelee?

(b) Gharama ya ujenzi ni shilingi 1,500,000,000; je, ni lini kiasi cha shilingi 1,000,000,000 kitatolewa ili kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ilipatiwa shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali mpya ya Halmashauri ambapo majengo yaliyojengwa ni Jengo la Wagonjwa wa Nje na Maabara na majengo yote mawili yamefikia asilimia 80 ya ukamilishaji. Aidha, kati ya fedha hizo zilizotolewa shilingi milioni 204 zilirejeshwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali baada ya kuvuka mwaka wa fedha 2019/2020 kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya fedha ya mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2016.

(b) Mheshimiwa Spika, mwezi Januari 2021 Serikali imetoa shilingi bilioni 1 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ili kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Majengo yatakayojengwa ni Jengo la Utawala na Jengo la Wazazi ambayo yamefikia asilimia 40 ya ukamilishaji, Jengo la kuhifadhia dawa na Jengo la kufulia ambayo yamefikia asilimia 60 ya ukamilishaji. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Hospitali hiyo imetengewa shilingi milioni 300.
MHE. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Nyamirembe – Chato mpaka Katoke Biharamulo ya kilomita 50 kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Nyamirembe Port – Katoke yenye urefu wa kilometa 50 ni barabara ya Mkoa inayounganisha Bandari ya Nyamirembe ambayo ipo Mkoa wa Geita na Mji Mdogo wa Katoke ambao upo Mkoa wa Kagera kupitia vijiji mbalimbali na Hifadhi ya Burigi Chato. Barabara hii inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza taratibu za kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa gharama ya Shilingi milioni 861.046 kwa kutumia fedha za ndani. Katika mwaka wa fedha ujao 2021/2022, fedha zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa Nyamirembe Port – Katoke, urefu wa kilomita 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii inaendelea kuiimarisha kwa kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali kila mwaka kabla ya ujenzi kwa kiwango cha lami kuanza ili barabara hiyo ipitike katika vipindi vyote vya mwaka. Katika mwaka huu wa fedha 2020/2021, jumla ya Shilingi milioni 447.771 zilitengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali na kwa sasa barabara hiyo ipo katika hali nzuri. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Soko la Kimkakati la Rusahunga Wilayani Biharamulo litakalogharimu shilingi bilioni 3.5 kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri Mkuu Bungeni?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na masoko nchini kwa ajili ya kukuza biashara na mauzo ndani na nje ya nchi kwa maendeleo na ustawi wa wananchi wake. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha masoko yanaanzishwa, kuboreshwa na kuendelezwa ili kutoa fursa kwa wakulima wadogo pamoja na wafanyabishara kuuza mazao na bidhaa zao katika masoko hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kipindi cha mwaka 2017/2018, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ilitenga eneo la uwekezaji katika Kata ya Lusahunga lenye ukubwa wa ekari 65 ambalo lina thamani ya shilingi bilioni 3.5. Eneo hili limetengwa kwa ajili ya kujenga viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, kujenga maghala ya kuhifadhia mazao, miundombinu ya majengo ya kibiashara kama mahoteli, ujenzi wa soko la kimkakati, kituo cha afya, viwanja vya makazi, na kituo cha mafunzo ya wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) imeendelea kusisitiza Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo kutenga fedha katika bajeti yake ili kufanikisha ujenzi wa soko hilo. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta wadau mbalimbali ikiwemo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili iweze kufanikisha ujenzi wa soko hilo.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Burigi – Chato ili waache kuingiza Mifugo ndani ya Hifadhi na kumaliza mgogoro kati ya wananchi hao na Hifadhi hiyo?
NAIBU WAZIRI, MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TANAPA imeendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Burigi - Chato. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi 20,836,200 zilitumika kutoa elimu ya uhifadhi katika vijiji 37, ambapo katika Wilaya ya Biharamulo elimu hiyo ilitolewa kwa vijiji sita vya Kiruruma, Nyabugombe, Ngararambe, Kabukome, Katerela na vya Kitwechembogo.

Aidha, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga jumla ya Shilingi Milioni 96.7 kwa ajili ya utoaji wa elimu ya uhifadhi katika maeneo ya vijiji 38 vinavyopakana na hifadhi hiyo vikiwemo vijiji 10 vya Wilaya ya Biharamulo.

Mheshimiwa Spika, sambamba na utoaji wa elimu kwa vijiji, Serikali imejipanga kutumia makundi maalum wakiwemo viongozi wa dini, wanasiasa na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili waweze kusaidia katika kuelimisha faida za uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)