Contributions by Hon. Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya (3 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kutoa hitimisho la hoja ya Mpango na Makadirio ya Matumizi ya fedha ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka huu wa 2021/2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru sana Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Mhandisi Dkt. Leonard Madaraka Chamuriho kwa ushirikiano mkubwa anaonipa ambao umeniwezesha kutekeleza majukumu yangu ya Unaibu kwa urahisi. Pia namshukuru Naibu mwenzangu hapa kwa jinsi tunavyoweza kushirikiana katika kumsaidia Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi niweze kujibu hoja mbalimbali ambazo zimejitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge kwenye eneo la barabara wameongea kwa hisia kali sana. Ni kweli mahitaji ya barabara na hasa kwa kiwango cha lami, ni makubwa sana. Tukirudi nyuma miaka michache tu, miaka sita, tutakumbuka miundombinu ya barabara ilivyokuwa. Hivyo, tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali kwa awamu zote kwa jinsi ambavyo imekuwa ikifanya vizuri katika sekta ya miundombinu. Kikubwa tu ni kwamba barabara hizi ni nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge watakubaliana nami kwamba moja ya kigezo kikubwa sana ambacho kimeiingiza Serikali ya Awamu ya Tano na Wabunge wengi kupata kura nyingi sana za kishindo kilichangiwa sana na eneo hili la jinsi Serikali ilivyofanya vizuri katika sekta ya miundombinu ikiwa ni barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niende kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, imesema nini? Ni kweli kwamba tuna ilani ambayo tunatekeleza, lakini ilani hii inatekelezwa kwa miaka mitano. Katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 - 2025, kilometa ambazo zimeainishwa zitajengwa kwa kiwango cha lami, kwanza zinakamilishwa 1,716, zinazojengwa ni 6,006 kwa kipindi hiki cha miaka mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha inayohitajika kukamilisha barabara hizi ni takribani shilingi trilioni 11. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge isingekuwa rahisi barabara zote hizi ambazo zimeainishwa zikapata nafasi kwa kipindi hiki, lakini tukubali kwamba tunatekeleza barabara hizi kwa miaka mitano. Barabara ambazo zitafanyiwa upembuzi yakinifu zina kilometa 7,500; zinahitaji karibu shilingi trilioni 11.5. Kwa hiyo, ukiangalia unaweza ukaona hiyo bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu hoja ya mchangiaji mmoja na hasa Mkoa wa Kigoma. Mkoa wa Kigoma sasa hivi wana barabara tatu zinazoingia makao makuu. Barabara ya Kigoma – Nyakanazi wakandarasi wote wako site. Barabara inayounga Tabora na Kigoma imebaki kipande cha Malagarasi – Uvinza ambacho muda wowote kinaanza kutengenezwa. Pia Mpanda kwenda Kigoma, wakandarasi wapo wanapunguza barabara ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa nadhani ni Mkoa wa Katavi tu na Kigoma ambao wanafika Makao Makuu bila kupita kwenye lami, lakini wakandarasi wako site. Angalau mikoa yote mtu ana uwezo wa kufika Makao Makuu kupitia kwenye lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala lilijitokeza la muda wa barabara. Nitolee mfano barabara ya Dodoma – Iringa; tatizo kubwa ilikuwa, barabara hii ni traffic projection ambayo hatukutegemea kama barabara itakuwa na mzigo mkubwa na wingi wa magari kama hayo ambayo yamejitokeza hapo katikati, lakini ndiyo maana umepunguziwa muda ule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la matuta lilijitokeza. Iko sheria ambayo imetoka, miongozo ambayo pia tunayo ya SADC ambao tunashirikiana nao, niwahakikishie Wabunge kwamba tumeendelea kutoa matuta yale ambayo hayakindi vigezo ama hayaendani na huo mwongozo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niwape comfort Waheshimiwa Wabunge kwamba barabara zote ambazo zimeathirika kutokana na mafuriko, tumejipanga; yako madaraja ya muda ambayo tumeyaagiza, tutahakikisha kwamba tunafanya tathmini na kurudishia maeneo yote ambayo yamekatika ikiwa ni pamoja na kuinua matuta sehemu ambazo zimeathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la vigezo vinavyotumika kutengeneza barabara za lami, barabara ili iweze kutengenezwa kwa kiwango cha lami lazima iwe ni barabara ya ukanda, yaani barabara ambazo zinaunga kwenye ushoroba, ziwe zinaunga mikoa, barabara iwe ni ahadi ya viongozi wa kitaifa kwa maana ya Mheshimiwa Rais, Makamu ama Waziri Mkuu, iwe ipo kwenye Ilani ya Chama Tawala, iwe ni kutekeleza Mipango ya Maendeleo ya Miaka Mitano. Pia barabara zinazoenda kwenye eneo la kuchochea uchumi ambalo ni kama utalii, uzalishaji mali na vitu kama hivyo na vile vile liwe ni eneo la ulinzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba tu, niwaombe Waheshimiwa Wabunge watupitishie bajeti ili twende tukatekeleze hiyo mipango ambayo wananchi wanahitaji sana barabara zao zikatengenezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Waheshimiwa Wabunge sasa nimwite Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mheshimiwa Engineer Dkt. Leonard Madaraka Chamuriho aje ahitimishe hoja yake.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia hoja ya Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Bunge, hasa ya Miundombinu.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Kamati ya Miundombinu wakiongozwa na Mheshimiwa Selemani Kakoso na Makamu wake Mheshimiwa Anne Kilango na Wajumbe wote kwa jinsi ambavyo wanatushauri sisi kama Wizara na kutoa maelekezo.
Mheshimiwa Spika, bila kupoteza muda, naomba sasa nijielekeze kwenye mchango wangu hasa kutokana na maoni ya Kamati. Nilisikia Kamati kwamba karibu mambo yote ambayo walikuwa wametuelekeza tunaendelea kuyatekeleza, nami nataka nitoe mchango kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kuhusu muundo wa TBA ili iweze kufanya na sekta binasfi; Machi, 2022 wakati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anazindua Mogomeni Quarter, moja ya jambo ambalo analieleza, ni kueleza Wizara na TBA kwamba waangalie uwezekano wa TBA kufanya kazi na sekta binafsi. Hivi ninavyoongea, tayari muundo wa TBA umeshakuwa reviewed kwa maana ya establishment order, pamoja na majukumu yake yote ambayo ilikuwa inayafanya, lakini pia sasa itaanza kufanya na sekta binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sasa hivi kwa maana ya taratibu zote tunasubiri tu baraka za mamlaka ambayo ndiyo ilitoa hayo maelekezo pamoja na Kamati ya Miundombinu. Hivyo, tuna uhakika suala hili liko mwishoni na itakuwa hivyo, kufanya kazi na sekta binafsi ikiwa ni pamoja na majukumu yake yote iliyokuwa inayatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, limejitokeza pia suala la TANROADS kuachia kazi kwenda TAA. Nataka kulijulisha Bunge hili kwamba hilo suala pia wataalam wameshashauri. Ni kweli kwamba TANROADS itaachia shughuli zote kwenda TAA lakini kwa hatua. Kwa sababu gani? Kwa sababu shughuli zote ambazo zilikuwa zimeingiwa mikataba na TANROADS, zitaendelea kufanyika kwa sababu ya mikataba yake, huku kama walivyoshauri wataalam, TAA ikianza kuchukua kazi.
Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara, kwa sababu taasisi zote ziko chini ya Wizara, hilo tumeshalikubali na litakwenda kutekelezwa hivyo, lakini kwa muda ili tusije tukaathiri miradi ambayo inaendelea ambapo tayari TANROADS walishaingia mikataba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu TEMESA, tayari Kamati ilishashauri kwamba Serikali iangalie muundo na utendaji kazi wa TEMESA na Serikali inaendelea kulifanyia kazi hilo. Kwa hiyo, nataka nilihakikishie Bunge hili kwamba tunaendelea kulifanyia kazi kama alivyoshauri Mheshimiwa Dkt. Ndugulile. Tayari Serikali ilishaliona na Kamati ilishashauri na tayari kazi inaendelea kuunda upya majukumu yake na muundo wake ili kuleta tija.
Mheshimiwa Spika, suala la fidia ya Itoni – Lusitu – Mawenge – Ludewa hadi Manda; ninapoongea sasa hivi, ni mama mmoja ambaye hajapata ambaye hakuwepo, na mtu mmoja, nyumba Na. 45 Kijiji cha Mlangali ambaye baada ya realignment alisahaulika, lakini fedha yake ipo na atalipwa wakati wa kulipa watu wa kati ya Mradi wa Itoni kwenda Lusitu ambapo jedwali liko tayari. Kwa hiyo, tumetekeleza yale maagizo ya Kamati.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Hazina kuipatia fedha TBA; kwa kweli kwa sasa Hazina imeendelea kutoa fedha nyingi na ndiyo maana tunaona sasa hivi majengo mengi TBA yanajengwa, pamoja na ruzuku ambayo TBA wanaitoa ya kujenga majengo kwa ajili ya wafanyakazi na nyumba za Serikali.
Mheshimiwa Spika, mwisho, kuhusu bajeti…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Sekunde 30.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, utakubaliana nami kwamba katika kipindi ambacho Serikali inalipa wakandarasi, ni kipindi hiki. Ndiyo maana miradi mingi inakwenda. Hata ukiwauliza wakandarasi, kwa kweli ni tofauti na ilivyokuwa na ndiyo maana miradi mingi inalipwa. Kadri tunavyotengeneza certificate kwa kweli Wizara ya Fedha inalipa na ndiyo maana tumekuwa kati ya Taifa ambalo yanafanya vizuri sana katika miundombinu kwa Afrika Mashariki na hasa miundombinu ya barabara.
Mheshimiwa Spika, mwisho, kuhusu madeni ya TBA, tayari pia lipo kwenye ngazi za juu kwa maana ya kwamba wale wadaiwa sugu na hata taasisi ndani ya Serikali, mpango umeandaliwa kati ya Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuona namna bora ya madeni yote yaweze kulipwa. Kwa hiyo, nina hakika hili nalo litafanyika ili kuipa uwezo TBA kupata madeni yake kwa ajili ya kuiimarisha kuweza kutimiza majukumu yake.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. Ahsante. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana. Hebu tusaidie kufafanua moja lile la uwezo wa kampuni za hapa nchini kuweza kutengeneza meli na kutengeneza vivuko halafu zisiweze kukarabati. Au ni ule utaratibu wa sheria yetu kwamba mlifanya hiyo International Competitive Tendering, kwa hiyo, akashinda yule? Hebu tueleweshe vizuri hapo.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Moja ulilolisema ndiyo hilo kwamba mikataba mingi huwa inatangazwa kwa maana ya kwamba iko wazi Kimataifa na mtu yeyote anaweza aka-tender. Pia tuna kampuni za Tanzania ambazo kwa kweli siyo nyingi.
Mheshimiwa Spika, moja ya kampuni ambayo inafanya vizuri sana ni Songoro Marine, Iakini tunaona kazi nyingi ambazo anazifanya kwa sasa hivi ni nyingi sana.
Nasi ni kati ya watu ambao tunam-promote sana. Kwa hiyo, kutokana na hilo tukaona pengine atachelewa zaidi kwa sababu ya taasisi yake na watu alionao. Kwa hiyo, naamini kwamba kama tungempa hiyo kazi pengine angeweza kuchukua muda mrefu kuifanya. Ila ni tenda iliyotangazwa kwa maana ya kwamba iko wazi kwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hoja hii.
Kwanza nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wote wa Kamati zote tatu kwa taarifa zao. Niseme tu kwamba mapendekezo yote yanayohusu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tumeyapokea na tunaahidi kwamba tutayafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ufafanuzi kwa maeneo mawili ama matatu kulingana na muda na naomba nianze na eneo la kurejesha majukumu ya ukarabati, ujenzi na kazi zote za viwanja vya ndege kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwenda Mamlaka ya Viwanja vya Ndege.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikubaliane na Waheshimiwa Wabunge, CAG, Kamati ya Miundo Mbinu lakini pia na Kamati ya PAC. Niwajulishe Waheshimiwa Wabunge kwamba tayari kazi hiyo imeshaanza na niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba shughuli za TAA kwenda TANROADS zilikuwa ni presidential decree na hii ilikuwa ni baada ya kuona shughuli nyingi wakati ziko chini ya TAA zilikuwa haziendi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tayari wataalam wameshatoa mapendekezo ya namna ya kuhamisha majukumu kutoka TANROADS kwenda TAA kwa hatua kwa sababu ziko kazi ambazo tayari zinaendelea na hatuwezi leo tukaziondoa ghafla. Kitakachoweza kutokea kama tutakifanya hicho, ndio kama walivyosema baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kwamba kuna viwanja vilisimama kwa sababu wakati TAA inatekeleza hiyo miradi ama imeshaingia mikataba tukafanya mabadiliko. Kwa hiyo tutahakikisha hilo halifanyiki na wataalam wameshatoa mapendekezo yao, hatua za kuanza kuchukua, hatua baada ya hatua na tunategemea kwamba zile fedha ama zile kazi ambazo zitafanyika kwa fedha hasa ya Tanzania kwa maana haina wahisani, miradi yote tutakayoanza kutekeleza itaanza hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengine watakuwa mashahidi kwamba hata sasa hivi tumeanza, pale ambapo kunakuwa na kazi wote wanakuwepo kwa ajili ya kuanza taratibu ya kuwajengea uwezo na uzoefu. Hilo kwa upande wa Serikali halina tatizo, tumeshalifanyia kazi na tunaamini kadri tunavyokwenda shughuli zote zitahamia TAA.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu bado vile viwanja vyote tulivyovijenga kama Msalato, Songea vimejengwa na hawa TANROADS na wataalam kwa hiyo tunategemea baada ya hapo pia kutakuwa na kuhamisha wataalam ambao wamepata uzoefu kutoka TANROADS kwenda kule TAA ili kuwajengea uzoefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine ambalo kuna Mbunge amelichangia kwa nguvu kuhusu TEMESA. Tunatambua hii taasisi ni muhimu sana kwa sababu ndio inayoshughulikia magari ya Serikali ya Viongozi lakini pia na vivuko. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali inapitia hii Taasisi na majukumu yake ili iweze kufanya kazi vizuri zaidi. Kwa hiyo, tumelipokea Kamati ilishauri, lakini pia Wabunge wameshauri na wameendelea kushauri na sisi tunasema tumeshaona kwamba, kuna haja kubwa ya kuangalia muundo wake, majukumu yake na utendaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ilikuwa ni taarifa na mapendekezo ya kiufundi na ufanisi. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara tunaangalia na kuweka mifumo imara sasa hivi ya jinsi ya kuangalia upungufu unaojitokeza wa kiufundi na hasa ya kiuhandisi yanayosababisha baadhi ya kazi zetu kufanyika chini ya kiwango. Niwahakikshie Waheshimiwa Wabunge kwamba, tumeliona hilo, tumelichukua, lakini tumeshaanza kuweka mifumo ambayo itahakikisha kwamba tunazuia hilo lisitokee na pale ambapo linatokea, hatua kubwa sana zinachukuliwa za kisheria na kinidhamu kwa wale ambao watakuwa wamesababisha kufanyika kwa kazi za kiufundi chini ya kiwango kama ambavyo ripoti imesema na tarifa ya PAC imesema.
Mheshimiwa Naibu Spika, masuala mengine ambayo yameongelewa hasa ya ulipaji wa certificate, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameelezea vizuri, kwa hiyo hilo naomba nisilieleze tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja; ahsante sana. (Makofi)