Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Festo John Dugange (103 total)

MHE. COSATO D. CHUMI Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza Ujenzi wa Barabara za lami na kufunga taa za barabarani katika Mji wa Mafinga chini ya Mpango wa Uendelezaji Miji nchini?
NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia mimi na Waheshimiwa Wabunge wote afya njema na kutuwezesha kuwa wawakilishi wa wananchi kupitia Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa imani kubwa aliyonipa kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Wanging’ombe kwa kunichagua na kuchagua mafiga matatu ya Chama cha Mapinduzi na niwahakishie utumishi uliotukuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nijibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi,Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Miji ya Kimkakati (Tanzania Strategic Cities Projects -TSCP) umetekelezwa katika Halmashauri za Majiji ya Tanga, Dodoma, Mbeya, Arusha na Mwanza na Halmashauri za Manispaa za Mtwara- Mikindani, Ilemela na Kigoma-Ujiji kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 355.5 sawa na shilingi bilioni 799.52.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Kuendeleza Miundombinu katika Miji 18 (Urban Local Government Strengthening Programme - ULGSP) umetekelezwa katika Halmashauri za Manispaa za Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Iringa, Mpanda, Lindi, Singida, Musoma na Bukoba na Halmashauri za Miji Kibaha, Babati, Geita, Korogwe, Bariadi na Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Miji ya Kimkakati (TSCP) pamoja na Mradi wa Kuendeleza Miundombinu katika Miji 18 (ULGSP) ilimalizika muda wake Mwezi Desemba, 2020. Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuanza kutekeleza Programu nyingine ya kuendeleza miundombinu itakayohusisha Halmashauri26 zilizokuwepo kwenye Programu zilizomalizika pamoja na Halmashauri nyingine 19 za Miji ikiwemo Mafinga.
MHE.DKT. PINDI H. CHANA Aliuliza:-

Serikali imekuwa ikisaidia sana vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu nchini kupitia Halmashauri za Wilaya:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha Mifuko hiyo ili kutoa viwango vikubwa zaidi vya mikopo?
NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI,naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato kutokana na vyanzo vya ndani vya halmashauri inatolewa na halmashauri zote nchini kutokana na fedha zilizokusanywa na halmashauri kwa kipindi husika baada ya kutoa vyanzo lindwa kama vile fedha za uchangiaji wa Huduma za Afya, ada za taka na ada za Shule za Sekondari Kidato cha Tano na Sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha kiwango cha mikopo inayotolewa na halmashauri Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuzisimamia halmashauri kutekeleza Sheria ya Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, kuzijengea uwezo Kamati za Huduma za Mikopo za Kata na Halmashauri ili ziwe na ujuzi wa kutosha wa kuanzisha na kuendeleza vikundi vya wajasiriamali pamoja na ujuzi wa kusimamia utoaji na urejeshwaji wa mikopo, kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanufaika wa mikopo kabla ya utoaji wa mikopo kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na kuzielekeza halmashauri kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato.
MHE. ANNA R. LUPEMBE Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara za Kata ya Katumba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 420.97 ambazo tayari zimeingizwa katika mfumo wa barabara za Wilaya (DROMAS). Aidha, Kata ya Katumba ina mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa 185.88 ambazo ni sawa na asilimia 44 ya mtandao wote.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2017/ 2018 hadi 2019/2020 Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Nsimbo umetumia kiasi cha shilingi milioni
246.08 kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Msaginya – Kanoge na Ikondamoyo – Kalungu. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 81.2 imetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Msaginya – Kanoge na barabara ya Kituo cha Afya Katumba – Mto Kalungu.

MheshimiwaSpika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara kote nchini kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE (K.n.y. MHE. ALMAS A. MAIGE) Aliuliza: -

Wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini wamejitolea kujenga Vituo vya Afya katika Kata za llolangulu, Mabama, Shitagena na Usagari katika Kijiji cha Migungumalo: -

Je, Serikali ipo tayari kuanza kuchangia miradi hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mchango mkubwa wa wananchi katika ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini. Hivyo, Serikali ina dhamira ya dhati ya kuchangia nguvu hizo za wananchi katika kukamilishaji vituo hivyo ili vianze kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa ukarabati na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini ikiwemo kukamilisha maboma ya majengo ya kutolea huduma za afya yaliyojengwa na wananchi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambapo ujenzi wake ulisimama kwa kukosa fedha. Hadi kufikia Septemba 2020 jumla ya shilingi bilioni 315.31 zimetumika kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Mheshmiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 27.75 kwa ajili ya kukamilisha maboma 555 ya zahanati nchini yakiwemo maboma manne (04) katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora ili kuunga mkono jitihada za wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua na kuthamini michango na nguvu za wananchi na itaendelea kuchangia nguvu za wananchi katika kujenga na kukarabati miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. NAPE M. NNAUYE (K.n.y. MHE. GODWIN E. KUNAMBI) aliuliza: -

Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba ni Halmashauri mpya iliyotoka Wilaya ya Kilombero: -

(a) Je, ni lini Serikali itaipa Mlimba hadhi ya kuwa Wilaya hasa ikizingatiwa umbali mrefu wa takriban Km 200 ambao Wananchi wanatembea kufuata huduma Makao Makuu ya Wilaya?

(b) Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa majengo ya Halmashauri na kuboresha miundombinu ya barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa miongozo na taratibu, uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala unahusisha uhitaji wa wananchi, Viongozi wa Wilaya na Mkoa ambao huwasilisha maombi ya mapendekezo yao kwenye vikao vya Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na kisha kuwasilishwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa hatua zaidi. Ofisi ya Rais-TAMISEMI, haijapokea maombi rasmi ya Mkoa wa Morogoro kuomba Mlimba kuwa Wilaya. Serikali inashauri utaratibu huu uliowekwa ufuatwe.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba. Mwezi Januari mwaka huu, Serikali imekwisha peleka kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuanza shughuli za ujenzi wa jengo hilo la utawala.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa miundombinu ya barabara, katika mwaka wa fedha 2019/ 2020, Serikali imefanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 54, imejenga kalvati 22 na madaraja manne (4) kwa gharama ya shilingi milioni 545.87. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali kupitia TARURA imetenga kiasi cha shilingi milioni 517.56 kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA) Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatengeneza eneo la Katokoro linalounganisha Kata za Katoro na Kyamulaile katika Jimbo la Bukoba Vijijini ili kuondoa adha ya usafiri inayowakabili wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

MheshimiwaSpika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo korofi la Katokoro ambalo limejaa maji lina urefu wa kilomita 5 ambayo ni sehemu ya barabara ya Katoro – Kyamulaile – Kashaba yenye jumla yakilomita 15.7 inayounganisha Kata za Katoro, Kyamulaile na Ruhunga. Aidha, barabara hiyo pia inaunganisha maeneo mbalimbali ya Halmashauriya Wilaya ya Bukoba na Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imefanya usanifu kwa ajili ya kuboresha eneo hilo korofi ambapo kiasi cha fedha shilingi milioni 572 kinahitajika kunyanyua tuta la barabara na kujenga makalvati.

Mheshimiwa Spika, ili kupata ufumbuzi kwa sasa katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 87 kwa ajili ya kurekebisha eneo korofi katika barabara hiyo. Hata hivyo, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkandarasi aliyekuwa anafanya kazi hiyo alisimamishwa kutokana na eneo hilo kujaa maji.

Mheshimiwa Spika, wakati jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa barabara hiyo zikiendelea, mara maji yatakapopungua, mara moja Serikali itamrejesha kazini mkandarasi huyo ili kurejesha mawasiliano katika eneo hilo.
MHE. BENAYA L. KAPINGA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha kuanzia Novemba, 2015 hadi Septemba, 2020, Serikali imejenga Hospitali 101 za Halmashauri na kuongeza idadi ya Hospitali za Halmashauri kutoka Hospitali 77 zilizokuwepo mwaka 2015 hadi Hospitali 178 Septemba, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya kigezo muhimu kwa Halmashauri kupata fedha za ujenzi ilikuwa ni kuandaa eneo la ujenzi. Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ilikosa fedha za ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri kwa kuwa hadi wakati wa tathimini ya Halmashauri zilizotenga maeneo ya ujenzi, Hospitali ya Halmashauri ya Mbinga ilikuwa haijapata eneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 27 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 27 mpya nchini. Aidha, kwa kuwa sasa tayari Halmshauri ya Wilaya ya Mbinga imebainisha eneo la ujenzi, Serikali itaipa kipaumbele sambamba na Halmashauri nyingine ambazo hazina Hospitali za Halmashauri kwenye awamu zinazofuata kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA Aliuliza:-

Je ni lini Serikali itajenga chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2019/2020, Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya halmashauri. Majengo yaliyohusika katika awamu ya kwanza ni jengo la wagonjwa wa nje na maabara. Ujenzi wa majengo hayo upo katika hatua ya ukamilishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 60.5 ambapo kiasi cha shilingi 33.5 ni kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali za halmashauri 67 nchini na kiasi cha shilingi bilioni 27 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za halmashauri 27 mpya ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe iliyotengewa kiasi cha shilingi bilioni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe inaelekezwa pamoja na majengo mengine, kujenga jengo la kuhifadhia maiti pindi itakapopokea fedha za ujenzi kwa kuwa tayari ina majengo mawili kati ya majengo saba yanayotakiwa kujengwa na hivyo fedha iliyotengwa kwenye bajeti ya mwaka 2020/2021 itakuwa sehemu ya fedha ya kujenga jengo la kuhifadhia maiti.
MHE. JAFARI W. CHEGE Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Daraja la Mto Mori kwani mto huo umekuwa ukisomba watu na kusababisha vifo kwa wananchi wanaofuata huduma upande wa pili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Mori unakatisha katika barabara ya Kirogo-Nyamaguku yenye urefu wa kilomita 15, ikiunganisha Tarafa za Luo-imbo, Suba na Nyancha katika Wilaya ya Rorya. Barabara hii ilifunguliwa mwaka 2008 kwa nguvu za wananchi kupitia Mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto huu umegawanyika katika matawi mawili ambayo ni Mto Mori Mkuu wenye upana wa mita 43 na Wamala wenye upana wa mita 16 ambapo madaraja mawili (2) yanahitajika kujengwa. Hivyo, kwa sasa, barabara hii haipitiki kutokana na kutokuwepo kwa madaraja hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa barabara hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya imewasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI, maombi maalum ya Shilingi bilioni 1.54 ambayo ni makisio kwa ajili ya ujenzi wa daraja katika Mto Mori na matengenezo ya kawaida katika Barabara ya Nyamaguku- Kirogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali itatenga fedha kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ajili ya usanifu wa madaraja mawili ya Mto Mori ili kufahamu mahitaji na gharama halisi za ujenzi wa madaraja hayo na kisha kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi. Aidha, ujenzi wa madaraja na miundombinu ya barabara hizi utatekelezwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ASIA A. HALAMGA Aliuliza:-

Ni Halmashauri ngapi nchi zimetekeleza kwa asilimia 100 sheria ya utoaji mikopo asilimia 10 ya makusanyo ya ndani kwa makundi ya vijana, akinamama na watu wenye mahitaji maalum?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarim Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimwa Naibu Spika, kwa mujibu wa takwimu zilizopo hali ya utoaji wa mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu katika Halmashauri nchini imeimarika hasa baada ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 yaliyofanyika Julai, 2018 kwa kuongeza Kifungu cha 37A kuhusu Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

Mheshimwa Naibu Spika, tangu kuanza kutumika kwa Sheria hii mwaka wa fedha 2018/2019 na 2019/2020 Halmashauri 79 zimetoa mikopo kwa asilimia 100 na Halmashauri 54 zimetekeleza kwa asilimia zaidi ya 85.

Mheshimwa Naibu Spika, utekelezaji wa shughuli hizi za mikopo umewezesha kuongezeka kwa mikopo inayotolewa na halmashauri nchini ikilinganishwa na kipindi kabla ya kufanya marekebisho ya sheria. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 (kabla ya marekebisho ya sheria) shilingi bilioni 26.1 zilitolewa; mwaka wa fedha 2018/2019 (baada ya marekebisho ya sheria) shilingi bilioni 42.06 zilitolewa; na mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya mikopo iliyotolewa ilikuwa ni shilingi bilioni 40.7 zilitolewa.

Mheshimwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kifungu namba cha 24(2) cha Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za mwaka 2019, Mkurugenzi yeyote ambaye atashindwa kusimamia utekelezaji wa Kanuni hizi atakuwa ametenda kosa la kinidhamu na mamlaka yake ya nidhamu inaweza, kwa kadri itakavyoona inafaa, kumchukulia hatua za kinidhamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba kutoa rai kwa Wakurugenzi wote nchini kote kuhakikisha kwamba wanazingatia takwa hilo la kisheria.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE (K.n.y. MHE. SILVESTRY F. KOKA) Aliuliza:-

Miundombinu ya maji katika Shirika la Elimu Kibaha ilijengwa miaka 50 iliyopita kwa kutumia mabomba ya Asbestos ambayo siyo rafiki kwa afya za binadamu, lakini pia ni chakavu sana:-

(a) Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya maji katika shirika hilo?

(b) Je, ni lini Serikali itakarabati majengo ya Chuo cha FDC katika Shirika hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya maji katika Shirika la Elimu Kibaha inayotokana na miundombinu mibovu na ya muda mrefu ambayo ni kutokana na uwepo wa mabomba ya maji ya kipenyo cha milimita 200 yenye urefu wa kilomita nne na kipenyo cha milimita 150 yenye urefu wa kilomita mbili yaliyojengwa kwa asbestos tangu kuanzishwa kwa Shirika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali ilikwishabadilisha bomba la asbestos lenye urefu wa kilomita 0.75 la kipenyo cha milimita 200 na bomba lenye urefu wa kilomita moja na kipenyo cha milimita 150 kuwa PVC. Serikali itaendelea kubadilisha mabomba hayo kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Shirika linaendelea kufanya matengenezo madogo madogo kwa kutumia mapato ya ndani pindi uharibifu unapotokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa shirika hili, imekamilisha ukarabati wa Shule ya Sekondari Kibaha kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.6. Vilevile katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya tathmini ya ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Shirika la Elimu Kibaha ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.48 kinahitajika ili kufanya matengenezo. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati. Hata hivyo, Shirika la Elimu Kibaha lilifanya ukarabati mdogo wa madarasa na jengo la utawala kwa kutumia mapato ya ndani ambao uligharimu shilingi milioni 25.73.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID Aliuliza:-

Je, ni lini utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne ya kujenga Daraja la Mto Pangani mpakani mwa Wilaya za Same na Simanjiro utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Pangani umekatisha kwenye kipande cha barabara ya Same – Ruvu – Mferejini chenye urefu wa kilomita 34.2. Barabara hiyo inaunganisha Kata za Same na Ruvu katika Wilaya ya Same na sehemu ya mto inayopendekezwa kujengwa daraja ina upana wa mita 70. Sehemu hii haipitiki kwa sasa kutokana na kukosekana kwa daraja la kuunganisha Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais-TAMISEMI kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekuwa ikikihudumia kipande cha barabara hiyo kwa kufanya matengenezo kwenye maeneo korofi ambapo katika mwaka wa fedha 2018/2019 kiasi cha shilingi milioni 48 kilitumika. Aidha, katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 kiasi cha shilingi milioni 63 kimetengwa kwa ajili ya matengenezo ambapo kwa sasa mkandarasi anaendelea na matengenezo ya kipande cha kilomita 7.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umepanga kufanya usanifu wa daraja ikiwa ni pamoja na kipande cha barabara yenye urefu wa kilomita 34.2 kwa upande wa Same hadi kufikia eneo la Mto Pangani panapohitajika kujengwa daraja ili kuunganisha Wilaya za Same na Simanjiro. Serikali itatoa kipaumbele cha ujenzi wa daraja na miundombinu ya barabara hiyo muhimu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA Aliuliza:-

Halmashauri ya Wilaya ya Newala ina Kata 22 na Vijiji 107, lakini ina Vituo vya Afya vitatu tu, kati ya 22 vinavyohitajika.

Je, Serikali haioni haja ya kujenga Vituo vipya vya Afya katika Halmashauri ya Newala ili kuboresha huduma za Afya kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM) kwa kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Kuanzia mwaka 2015 hadi Septemba 2020, Serikali imejenga Zahanati 1,198; imejenga na kukarabati Vituo vya Afya 487 na imejenga Hospitali za Halmashauri102.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 na 2019/2020, Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Newala kiasi cha Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri na Shilingi milioni 400 kwa ajili kufanya ukarabati wa Kituo cha Afya Kitangari. Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni moja (1) kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri na Shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya Zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa awamu kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. GRACE V. TENDEGA Aliuliza:-

Akina mama wajawazito wamekuwa wakitozwa fedha kuanzia shilingi 50,000/= hadi 70,000/= wasipojifungulia katika Vituo vya Afya hasa katika Jimbo la Kalenga; huku vituo hivyo vikiwa mbali na maeneo wanayoishi.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga maeneo ya kusubiri kujifungua katika Vituo vya Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, majengo ya wajawazito kujisubiria yanalenga kupunguza umbali kwa wajawazito kufika kwenye vituo vya huduma za afya pindi wanapokaribia kujifungua. Lengo likiwa ni kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga vinavyosababishwa na umbali kutoka katika vituo vya kutolea huduma.

Meshimiwa Spika, katika kutatua changamoto hii, Serikali imeendelea kujenga vituo vya huduma za afya kote nchini na kujenga Hospitali za Halmashauri 102, Vituo vya Afya 487 na Zahanati 1,198 katika kipindi cha Novemba, 2015 hadi Septemba, 2020. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 33.5 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 67; shilingi bilioni 33.5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali 67 za Halmashauri na shilingi bilioni 27 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya za Halmashauri. Kiasi cha shilingi bilioni 27.5 pia kimetengwa kwa ajili ya kukamilisha maboma ya Zahanati 555.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya nchini kote, umepunguza umbali kwa wananchi kuvifikia vituo vya huduma za afya na hivyo viashiria vya huduma na vifo vya wajawazito vimepungua kutoka 11,000 mwaka 2015 hadi 3,000 mwaka 2020. Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya huduma za afya kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ESTHER L. MIDIMU K.n.y. MHE. SIMON S. LUSENGEKILE Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa katika Hospitali ya Wilaya ya Busega ili huduma bora za afya ziendelee kutolewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Busega kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega ni miongoni mwa hospitali 67 za Halmashauri zilizoanza kujengwa mwaka 2018/2019 kwa kupewa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba ambayo ni jengo la utawala, jengo la wagonjwa wa nje, jengo la maabara, jengo la mionzi, jengo la wazazi, jengo la kufulia na jengo la kuhifadhia dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 33.5 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali 67 za Halmashauri ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega ambayo imetengewa shilingi milioni 500.

Vilevile katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 33.5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba katika hospitali 67 za Halmashauri ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Busega ambayo imetengewa shilingi milioni 500.
MHE. ZAYTUN S. SWAI Aliuliza:-

Kutokana na changamoto za vyanzo vya mapato hususan katika Halmashauri zilizo nje ya miji kumekuwa na uwiano usio sawa wa utoaji wa mikopo.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutafuta njia ya kuweka uwiano sawa wa mikopo hiyo bila kujali mapato ya Halmashauri husika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri hutolewa kwa kuzingatia kifungu cha 37A cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 na Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za mwaka 2019. Halmashauri inatakiwa kutenga na kutoa asilimia 10 ya fedha za makusanyo ya ndani katika kipindi husika kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu baada ya kuondoa vyanzo lindwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa sheria hii ni asilimia 10 ya mapato yanayokusanywa kwenye Halmashauri husika ambayo yanatofautiana kati ya halmashauri moja na nyingine kutokana na fursa zilizopo. Hivyo, kiwango cha mikopo inayotolewa kinategemea uwezo wa makusanyo wa Halmashauri husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka hususan baada ya kuwepo kwa sheria ambapo mikopo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 26.1 mwaka 2017/2018 hadi shilingi bilioni 42.06 mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio hayo Serikali inatambua changamoto zinazotokana na utaratibu huu na itaendelea kuuboresha ili kuongeza tija na kufikia malengo ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo hii.
MHE. FLATEI G. MASSAY (K.n.y. MHE. ZACHARIA P. ISSAAY) Aliuliza:-

Mwaka 2015 Serikali ilitangaza kugawa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na kupitia vikao vya Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri za Mbulu Wilaya na Mbulu Mji walipitisha rasmi mgawanyo wa rasilimali na madeni.

Je, ni lini Serikali itarejesha tamko la mapendekezo hayo ili kufanikisha maendeleo ya mambo yaliyopendekezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kupitia vikao vya Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Halmashauri ya Mji Mbulu waliridhia na kupitisha mgawanyo wa rasilimali na madeni na kuwasilisha mgawanyo huo Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Tarehe 9 Novemba, 2018 mgawanyo wa mali na madeni ya Halmashauri hizo ulitolewa na Waziri mwenye dhamana na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Toleo Namba 45 la mwaka 2018 pamoja na mgawanyo wa mali na madeni wa Halmashauri nyingine 42 kupitia Tangazo la Serikali Namba 696 la mwaka 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, mgawanyo wa rasilimali watu, magari, pikipiki, rasilimali na madeni umefanyika kwa asilimia 100 kwa kuzingatia Mwongozo wa Ugawaji wa Mali na Madeni ulioandaliwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI wa mwaka 2014. Katika mgawanyo huo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu (Halmashauri mama) ilipata asilimia 60 na Halmashauri ya Mji wa Mbulu ilipata asilimia 40.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Magu kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali imeendelea na ujenzi wa majengo ya utawala katika Halmashauri 100 ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Magu ambazo kwa ujumla zimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 147.33.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Magu ambalo litagharimu shilingi bilioni tano hadi kukamilika. Hadi mwezi Februari 2021, Serikali ilikuwa imekwishatoa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo ambalo tayari limeezekwa. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 750 kwa ajili ya kuendelea na hatua ya ukamilishaji wa jengo hilo.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Hospitali ya kisasa Mkoani Morogoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na mpango wa kujenga Hospitali za kisasa za Halmashauri na za Rufaa za Mikoa ili kuboresha huduma za afya za rufaa katika ngazi hizo. Kupitia mpango huo, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro itakarabatiwa na kupanuliwa. Mpango huo utahusika ujenzi wa jengo la kisasa la wagonjwa wa nje, jengo la kutolea huduma za dharura, jengo la huduma za uchunguzi wa mionzi na maabara, matibabu ya viungo, huduma za famasia, utawala pamoja na Wodi Maalum (Private Wards).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa eneo ilipo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa sasa ni dogo, Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro inakamilisha taratibu za umiliki wa eneo lenye ukubwa wa ekari 100 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kuboresha huduma za afya ngazi ya msingi katika Mkoa wa Morogoro, Serikali imejenga Hospitali tano za Halmashauri ya Malinyi, Gairo, Morogoro, Mvomero na Kilombero kwa gharama ya shilingi bilioni 7.5 katika kipindi cha Juni, 2016 hadi Juni, 2020. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali za Halmashauri ya Mlimba na Mvomero. Aidha, shilingi bilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa wodi tatu katika Halmashauri za Wilaya za Malinyi, Gairo na Morogoro.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaboresha Hospitali ya Wilaya ya Olturumet katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kwa kuipatia jengo la OPD, Wodi ya kulaza Wagonjwa, Jengo la X-Ray na mashine ya X-Ray ili Hospitali hiyo iweze kutoa huduma kwa wananchi ipasavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemberis Saputu Mollel, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa Hospitali kongwe 43 za Halmashauri nchini ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Olturumet Arusha, ambazo zinahitaji ukarabati na upanuzi wa miundombinu ili kuendana na mahitaji ya sasa ya utoaji wa huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Ukarabati wa Hospitali kongwe 43 nchini ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali itaomba kutengewa kiasi cha shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kuanza ukarabati wa Hospitali 21 za Halmashauri nchini. Mpango huo utaendelea kutekelezwa kwa awamu hadi ukarabati na upanuzi wa hospitali kongwe zote nchini utakapokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge Noah kuwa Hospitali ya Wilaya ya Olturumet Arusha ni miongoni mwa hospitali ambazo zitafanyiwa ukarabati na upanuzi.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA Aliuliza: -

(a) Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi na vifaa muhimu kwenye hospitali inayojengwa katika Mji wa Tunduma ili ianze kufanya kazi mapema?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza madaktari na wakunga pamoja na kuongeza bajeti katika Kituo cha Afya cha Tunduma ili kukidhi mahitaji ya kituo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa tangu Mheshimiwa Rais aliponipa dhamana ya kumsaidia kama Naibu Waziri, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, lakini nimuahidi kwamba nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Tunduma ambayo ilianza kujengwa katika mwaka wa fedha 2016/2017. Ujenzi wa awamu ya kwanza unahusisha jengo la ghorofa moja lenye sehemu tisa za huduma mbalimbali za OPD ambalo limetumia shilingi bilioni nne ambalo hadi Machi, 2021 ujenzi wake umefikia asilimia 82.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali itaomba kuidhinishiwa shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Baada ya kukamilisha ujenzi huo Serikali itapeleka watumishi na huduma za OPD zitaanza kutolewa. Serikali imeshawapanga madaktari wawili katika hospitali hii ambao kwa sasa wanaendelea kutoa huduma kwenye Kituo cha Afya Tunduma wakisubiri kukamilika kwa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Tunduma kina jumla ya watumishi 74 kati ya watumishi 52 wanaohitajika katika ngazi ya kituo cha afya na hivyo kuwa na ziada ya watumishi 22. Idadi ya watumishi waliozidi inatokana na kituo hiki kutumika kama Hospitali ya Mji wa Tunduma. Hivyo, watumishi hawa watahamishiwa katika hospitali mpya ya mji mara itakapokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali itaomba kuindhinishiwa shilingi milioni 409 kwa ajili ya dawa na vifaa tiba katika Kituo cha Afya cha Tunduma ambalo ni ongezeko la shilingi milioni 84 ikilinganishwa na bajeti ya shilingi milioni 325 iliyoidhinishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa mradi wa kimkakakti wa machinjio Iringa Ngelewala ili kuwekezaji huo uanze kuleta tija kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ilianza ujenzi wa machinjio ya Ngelewala katika mwaka wa fedha 2008/2009. Hadi Juni, 2018 kiasi cha shilingi milioni 928.99 kilikuwa kimetumika ikiwemo shilingi milioni 550 kutoka Serikali Kuu, shilingi milioni 108 mapato ya ndani ya Halmashauri, shilingi milioni 101 kupitia programu ya kuendeleza kilimo nchini ASDP na shilingi milioni 169 kutoka UNIDO.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 mradi huu ulijumuishwa kwenye miradi ya kimkakati ya Halmashauri inayotekelezwa ili kuziongezea Halmashauri uwezo wa kutoa huduma na kukusanya mapato. Miundombinu ambayo tayari imejengwa ni pamoja na mabwawa ya maji machafu (oxidation ponds), zizi la kuhifadhia mifugo kabla ya kuchinjwa, shimo la kutupa nyama isiyofaa kuliwa na binadamu, jengo la utawala, uzio eneo la shughuli za dobi, kichomea taka, maabara na jengo la kubadilishia mavazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi mradi kukamilika kwa kujenga miundombinu yote, utagharimu shilingi bilioni 1.147. Mkandarasi anaendelea na ujenzi na anatarajiwa kukamilisha mradi ifikapo tarehe 1 Agosti, 2021.
MHE. KENNETH E. NOLLO Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mfumo wa ukusanyaji mapato wa GoTHOMIS kwenye zahanati kama ilivyo kwenye vituo vya afya ili kuondoa mwanya wa upotevu wa mapato?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Jimbo la Bahi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Kieletroniki wa Uendeshaji wa Huduma za Afya (Government of Tanzania Health Operations Management Information System - (GoTHOMIS) ni mfumo wa usimamizi wa uendeshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya, ikiwa ni pamoja na kukusanya taarifa za wagonjwa na magonjwa, taarifa za malipo ya matibabu, taarifa za madawa na vifaa tiba na taarifa za huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu ulianzishwa mwaka 2016 na kuanza kusimikwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi zote. Mfumo umeboreshwa na kuunganishwa na mifumo mingine kama Mfumo wa Malipo ya Serikali (GePG), mfumo wa NHIF kwa ajili ya usimamizi wa madai na mfumo wa Kuomba Madawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa (ELMIS).

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Februari 2021, Mfumo wa GoTHOMIS umesimikwa katika vituo vya kutolea huduma 921, ikiwa ni hospitali 21 za mikoa, hospitali 82 za halmashauri, hospitali teule za wilaya 22, vituo vya afya 385 na zahanati 411. Kazi ya kusimika mfumo huu katika vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi zote nchini inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri zimekuwa zikitumia vyanzo vyake vya ndani kusimika mtandao kiwambo na kununua vifaa vingine zikiwemo kompyuta na wataalam wa halmashauri kushirikiana na wataalam wa mikoa katika kusimika mifumo hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya vituo vilivyofungiwa Mfumo wa GoTHOMIS na ambavyo vina miundombinu wezeshi kama mawasiliano ya internet vinatumia moja kwa moja Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (GePG) na hivyo kuwezesha wapewa huduma kulipa moja kwa moja benki au kupitia mitandao ya simu na hivyo kuwezesha makusanyo ya vituo kuongezeka na kutumika ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ufungaji wa mifumo huu utaendelea kutekelezwa.
MHE. CECILIA D. PARESSO K.n.y. MHE. ALLY J. MAKOA Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakarabati au kujenga Hospitali mpya ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa kwa kuwa Hospitali iliyopo ni ya muda mrefu na miundombinu yake ni chakavu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa hospitali kongwe na chakavu katika baadhi ya Halmashauri nchini ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 102 ambazo zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Kwa kuwa, bado kuna Halmashauri 28 zisizo na Hospitali ya Halmashauri, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 14 ili kuanza ujenzi katika Halmashauri hizo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka kipaumbele kwa kuanza ujenzi katika Halmashauri hizo na baada ya hapo ukarabati wa Hospitali chakavu ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa utafanyika. Ahsante sana.
MHE. BAHATI K. NDINGO Aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha uanzishwaji wa hati fungani za Serikali za Mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wakati wa kuwasilisha hotuba ya bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2021/22 Waziri wa Fedha na Mipango aliwasilisha kuhusu kuanzisha hati fungani za Halmashauri. Kifungu cha 92 ya hotuba yake ilieleza, katika jitihada za kupanua wigo wa vyanzo vya mapato rasilimali fedha Serikali itaangalia uwezekano wa kutumia hati fungani zitakazotolewa na Halmashauri za Manispaa na Majiji kama njia mbadala ya kupata rasilimali fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati.

Mheshimiwa Spika, hatua hii itapunguza mzigo kwenye mfuko mkuu wa Hazina ya Serikali hasa kwa Halmashauri zenye miradi ambayo imefanyiwa upembuzi yakinifu na kuwa na uhakika wa uwezo wa miradi hii kurejesha kwa faida kwa maana ya bankable projects.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (United Nations Capital Development Fund – UNCDF) na Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji (Capital Markets and Securities Authority- CMSA) imeanza mchakato wa kupitia miradi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhakikisha Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji yatakayokidhi vigezo na masharti ya matumizi ya hati fungani yanaanza kutumia utaratibu huu katika mwaka huu wa fedha 2021/2022. Ahsante sana.
MHE. ANTON A. MWANTONA Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapima maeneo yote ya umma ikiwemo Shule, Vituo vya Afya na Zahanati kwa kutumia Sheria Na. 4 na Na. 5 ili kuondokana na matatizo ya migogoro ya mipaka kwa Wananchi, lakini pia kuondokana na hoja za ukaguzi ambazo zaidi ya asilimia 90 ya Halmashauri wanazipata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ninaomba kujibu Swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa baadhi ya maeneo ya umma yaliyoainishwa na kutengwa kwa ajili ya utoaji wa huduma mbalimbali za umma zinazotolewa na Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa hayajapimwa na kuwekewa alama zinazoonekana kwa urahisi. Hali hii husababisha migogoro ya mara kwa mara ya ardhi na uvamizi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo Serikali imezielekeza halmashauri zote nchini kutenga fedha kila mwaka katika bajeti zao kwa ajili ya kupima maeneo yote ya taasisi za umma zilizo chini ya mamlaka hizo; ikiwa ni pamoja na kuweka alama zinazoonekana kwa urahisi ili kuepusha migogoro ya ardhi na kuzuia uvamizi unaofanywa na baadhi ya wananchi. Serikali ilishatoa maelekezo haya kwa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; hivyo nitumie fursa hii kuzisisitiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinatenga fedha na kutekeleza maelekezo hayo. Ahsante sana.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kutatua migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji katika kilimo na wananchi wa Kata za Kapele, Ndalamo, Ikama, Nzoka, Msanyani na Kamsamba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba kumekuwa na migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji katika kilimo na wananchi katika Kata za Kapele, Ndalamo, Ikama, Nzoka, Msanyani na Kamsamba. Migogoro hii imetokana na uuzaji holela wa ardhi uliokuwa unafanywa na baadhi ya viongozi wa vijiji katika kata hizo.

Mheshimiwa Spika, ili kutatua migogoro hiyo, Serikali kupitia Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Momba imefanya uhakiki na kubaini jumla ya migogoro 38. Kati ya migogoro hiyo, migogoro 34 tayari imetatuliwa na migogoro minne ipo katika hatua mbalimbali za utatuzi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka utaratibu rasmi wa kisheria katika uuzaji na ukodishaji ardhi ili kuepusha migogoro kati ya wawekezaji na wananchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU Aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itapeleka Watumishi na Vitendea kazi vya kutosha katika Zahanati mpya 24 zilizojengwa ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita?

(b) Je, ni lini Serikali itadhibiti upotevu wa mapato katika Zahanati, Vituo vya Afya hadi Hospitali za Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu Mbunge wa Geita Mjini lenye sehemu (a) and (b) kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Geita ina jumla ya watumishi 162 wa kada mbalimbali ya afya na upungufu wa watumishi 469. Mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali iliajiri watumishi 2,726 na kupanga katika vituo vilivyokuwa na upungufu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 halmashauri imeomba jumla ya watumishi 126. Aidha, Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya katika kuendelea kupunguza changamoto ya upungufu wa watumishi, ikiwemo watumishi kwenye Halmashauri ya Mji Geita.

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kudhibiti upotevu wa mapato kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini ambapo hadi Februari 2021, mfumo wa GoTHOMIS umesimikwa katika hospitali 21 za Mikoa, Hospitali 82 za halmashauri, hospitali teule za Wilaya 22, Vituo vya Afya 385 na zahanati 411. Aidha hatua za kinidhamu na kisheria zinaendelea kuchukuliwa kwa watumishi wanaothibitika kuhusika na upotevu wa mapato.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji Geita inaendelea kufunga mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za Afya na fedha ili kuboresha ukusanyaji wa mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 shilingi milioni 28.2 zimetengwa kwa ajili ya ukamilishaji wa Mfumo wa ukusanyaji wa mapato (GoTHoMIS) katika Zahanati 11 kati ya Zahanati 13 zilizopo ambazo hazina Mfumo wa GOT- HOMIS. Hospitali ya Geita pamoja na Vituo viwili vya Afya vilivyopo tayari vimefungwa mfumo wa GoTHOMIS. Ahsante sana.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Hayati Dkt. John Magufuli, Makamu wa Rais wa sasa na Waziri Mkuu ya kujenga Kituo cha Afya Kata ya Murungu katika Wilaya ya Kibondo ili kusogeza huduma na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi Mbunge wa Jimbo la Muhambwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujenga na kukarabati Vituo vya Kutolea huduma za Afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuboresha utoaji wa Huduma za Afya ya Msingi kwa wananchi ikiwemo upatikanaji wa huduma za upasuaji. Ujenzi na ukarabati wa huo unahusisha pia utekelezaji wa ahadi za Viongozi Wakuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza mkakati huu, Serikali imepeleka fedha shilingi bilioni 25.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Tarafa 90 zisizo na Vituo vya Afya ikiwemo Tarafa ya Kibondo Mjini inayoundwa na Kata tisa za Murungu, Bunyambo, Kibondo Mjini, Biturana, Kumwambu, Kitahana, Rusohoko, Misezero na Bitare ambapo kiasi cha shilingi milioni 250 kimepelekwa kwa jili ya ujenzi wa Kituo cha Afya kwenye Kata ya Bunyambo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na utekelezaji wa mkakati huu, Serikali, itaendelea kutoa fedha kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi zote za Viongozi.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa Jengo la Manispaa ya Tabora ambao umesimama kwa muda mrefu sasa huku shughuli za Manispaa zikiendelea kufanyika kwenye majengo ya zamani yaliyochakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mhesimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa baadhi ya halmashauri nchini ambazo hazina majengo ya utawala na uwepo wa majengo chakavu. Serikali kwa kutambua hilo, inaendelea na ujenzi wa majengo ya utawala ya Halmashauri 100 nchini kote ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa Tabora kwa kutumia mapato ya ndani, mwaka 2015 ilianza kujenga jengo la utawala la ghorofa nne ambalo lilikadiriwa kugharimu kiasi cha shilling bilioni 5.7 mpaka litakapokamilika. Ujenzi wa awamu ya kwanza unaohusisha boma la jengo hilo umekamilika.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo, katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja ili kuendeleza ujenzi wa jengo hilo ambapo ujenzi wa awamu ya pili utatumia utaratibu wa force account ili kupunguza gharama za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, imeelekezwa kukamilisha taratibu za kuwasilisha maombi ya fedha za ujenzi huo Wizara ya fedha na Mipango ili ujenzi uanze mara moja.

Mheshimiwa Spika, aidha, halmasahuri imeelekezwa kuanza ukamilishaji wa baadhi ya maeneo ya jengo hilo ili watumishi waweze kupata ofisi wakati ukamilishaji ukiendelea.
MHE. FATMA H. TOUFIQ K.n.y. MHE. MOHAMED L. MONNI Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga stendi katika Mji wa Chemba ambao unakuwa kwa kasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Wilaya ya Chemba kuwa na kituo cha kisasa cha mabasi. Kwa umuhimu huo Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Chemba imetenga eneo la ekari 22 kwa ajili ya ujenzi wa stendi kuu ya mabasi katika Mji wa Chemba ambayo imekadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 643.8 mpaka kukamilika kwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri ilitenga kiasi cha shilingi milioni 37 kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi hiyo ambapo ujenzi wa vyoo na ofisi za muda umekamilika kwa gharama ya shilingi milioni saba ili kuwezesha wananchi kuanza kupata huduma za stendi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri imetenga kiasi cha shilingi milioni 16 ili kuendeleza ujenzi wa stendi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati unahusisha andiko maalum la mradi linaloandaliwa na Halmashauri na kuwasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango, naishauri Halmashauri ya Wilaya ya Chemba kufuata utaratibu huo ili Serikali itafute fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo. Ahsante sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI Aliuliza: -

Serikali ilichukua eneo la Mlima Nkongore ambao ndani yake kulikuwa na makazi ya wananchi na kuliwekea beacon na kusababisha kaya zaidi ya 10 zilizochukuliwa maeneo hayo kuishi kwa hofu.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzilipa fidia Kaya hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mlima Nkongore uliopo katika Halmashauri ya Mji Tarime una eneo lenye ukubwa wa ekari 266.65. Wananchi wanaozunguka eneo hilo walikuwa wakiutumia Mlima Nkongore kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ukataji kuni, uchomaji mkaa na kilimo kinyume na taratibu za Mamlaka ya Upangaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Mlima Nkongore ni moja ya eneo lililokuwa limekithiri kwa shughuli haramu ikiwemo kilimo cha bangi. Hivyo, mwezi Novemba, 2017 Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime ilikabidhi eneo hilo kwa Jeshi la Magereza ili kuhakikisha kuwa eneo hilo linalindwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004 kifungu cha 58(1) na (2) ambacho kinazuia kufanya shughuli zozote zinazoweza kusababisha hifadhi ya mlima kuharibiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira inakamilisha taratibu za kulifanya eneo la Mlima Nkongore kuwa hifadhi. Hivyo, eneo la Mlima Nkongore litaendelea kuwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Magereza hadi taratibu zitakapokamilika na kulitangaza kuwa eneo la hifadhi, ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI K.n.y. MOSHI S. KAKOSO Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya shilingi milioni 400 aliyoahidi Waziri Mkuu kuchangia katika ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kasekese kinachojengwa na wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuboresha utoaji wa huduma za afya ya msingi kwa wananchi ikiwemo upatikanaji wa huduma za upasuaji. Ujenzi na ukarabati huo unahusisha pia utekelezaji wa ahadi za Viongozi Wakuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya Serikali kuchangia shilingi milioni 400 ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kasekese imetekelezwa, ambapo fedha hizo zimepelekwa kwenye Kata ya Kasekese tarehe 25/8/2021 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo hicho.

Mheshimiwa Spika, majengo manne yanatarajiwa kujengwa, ambayo ni jengo la wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la kufulia nguo na nyumba ya mtumishi. Aidha, ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje la Kituo cha Afya Kasekese umekamilika kwa gharama ya shilingi 164.9 kupitia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri. Ahsante sana.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia Wananchi wenye Viwanja eneo la Miganga West na East, Kata ya Mkonze katika Manispaa ya Jiji la Dodoma kwa kuwa uthamini ulishafanywa na baadhi ya Wananchi bado hawajalipwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifauatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo la Miganga West na East katika Kata ya Mkonze ni miongoni mwa maeneo ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambayo yamepangwa, kupimwa viwanja na kumilikishwa kwa wananchi ili waviendeleze kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Mji Mkuu (Master Plan).

Mheshimiwa Spika, kufuatia uwepo wa miradi ya kimkakati wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa 400KV kutoka Chalinze hadi Zuzu inayotekelezwa na Serikali kupita katika eneo hili na kuathiri viwanja vilivyomilikishwa, imelazimu eneo hilo kutwaliwa chini ya Sheria ya Utwaaji Ardhi Na. 47 ya Mwaka 1967, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya Mwaka 1999, Kanuni za Ardhi za Mwaka 2001, Miongozo ya Uthamini na Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini Na. 7 ya Mwaka 2016.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya uthamini kwenye jumla ya viwanja 309 vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.77 vilivyoathiriwa na mradi wa reli ya kisasa ambapo kiasi cha shilingi milioni 576.5 imeshalipwa kwa wananchi ikiwa ni fidia ya viwanja 231. Viwaja 78 vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 vinaendelea kuhakikiwa na Ofisi ya Mthamini Mkuu ili kukamilisha taratibu za fidia zao kwa mujibu wa sheria. Aidha, Serikali imeshafanya uthamini kwenye viwanja 123 na makaburi manne vyenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 1.1 vilivyoathiriwa na mradi wa ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa 400KV.

Mheshimiwa Spika, wananchi ambao viwanja vyao vimeathirika na mradi huo, watalipwa fidia mara baada ya Mthamini Mkuu kukamilisha taratibu za kisheria. Ahsante sana.
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Stendi ya Mabasi Makete Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Festo Richard Sanga Mbunge wa Jimbo la Makete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Makete katika Mwaka wa Fedha 2013/2014 ilitenga eneo lenye ukubwa wa ekari 3.1 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2014/ 2015 Halmashauri ilianza ujenzi kwa gharama ya shilingi milioni 40; na katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Halmashauri imepanga kutenga fedha kwenye mapato ya ndani ili kuendelea na ujenzi wa kituo hicho

Mheshimiwa Spika, Serikali inaishauri Halmashauri ya Wilaya ya Makete kufanya tathimini ya ujenzi wa kituo cha mabasi na kuandaa andiko ili kutafuta vyanzo vya fedha kwa ajili ya ujenzi. Ahsante sana.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatafuta mkakati wa kudumu wa kutatua tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo ya Mkoa wa Lindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Lindi kumekuwa na ongezeko la migogoro ya wakulima na wafugaji, hususan katika Wilaya za Kilwa, Nachingwea na Liwale. Migogoro hii imetokana na ongezeko la mifugo ambapo kumeongeza uhitaji wa nyanda za malisho na maji.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi pamoja na Halmashauri ya Wilaya za Kilwa, Nachingwea na Liwale imefanya uhakiki na kubaini jumla ya migogoro 19, ambapo jumla ya migogoro 12 imetatuliwa na migogoro saba iko katika hatua mbalimbali za utatuzi.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Sekretariati ya Mkoa wa Lindi imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 81, na kuunda kamati ya utatuzi wa migogoro kwa kila halmashauri ili kuwahamasisha wafugaji kufuga kibiashara kwa kuendeleza ranch ndogondogo, na kila halmashauri kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji vitano kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Halmashuri za Mkoa wa Lindi na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kutumia kiasi cha shilingi milioni 279.22 kwa ajili ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 15, ikiwa ni hatua za utatuzi wa migogoro hiyo. Ahsante.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Jimbo la Lushoto lina Kituo kimoja cha Afya na sasa wananchi wameanza kujenga Vituo vya Afya viwili vya Gare na Ngwelo.

Je, Serikali ipo tayari sasa kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia vituo hivyo na ni lini itafanya hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa za Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha huduma za afya katika Wilaya ya Lushoto kuanzia mwaka wa fedha 2017/ 2018 - 2019/2020, Serikali imetoa shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto pamoja na ukarabati na upanuzi wa Vituo vya Afya vya Mlola, Kangagai na Mnazi ili kuviwezesha kutoa huduma za dharura za upasuaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Machi 2021, Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma matatu ya zahanati. Serikali inatambua na kuthamini juhudi za wananchi wa Jimbo la Lushoto katika ujenzi wa Vituo vya Afya. Serikali itaendelea kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya nchini, vikiwemo vituo vya afya vilivyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi Jimboni Lushoto kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga stendi ya kisasa Jijini Arusha ili kukidhi mahitaji ya Wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Jiji la Arusha imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 30 katika eneo la Bondeni City kwa ajili ya ujenzi wa stendi mpya ya kisasa. Stendi mpya itakayojengwa itazingatia pia mahitaji ya wafanyabiashara wadogo kama Machinga, stendi ya teksi, pikipiki, bajaji, Ofisi za Polisi wa Usalama Barabarani na maeneo ya huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi inayoendelea sasa ni taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu wa mradi huo. Mradi huu wa ujenzi wa Stendi ya Kisasa Jiji la Arusha utajumuishwa kwenye Mradi wa Uboreshaji Miundombinu yaani Tanzania Cities Transforming Infrastructures and Competitiveness - TACTIC utakaotekelezwa kwenye Halmashauri 45 za Majiji, Manispaa na Miji nchini ambapo Serikali inaendelea na majadiliano na Benki ya Dunia.
MHE. VICENT P. MBOGO aliuliza:-

Jimbo la Nkasi Kusini lina Kata 11 na Kituo cha Afya kimoja pekee:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Vituo vya Afya hasa katika Tarafa ya Chala, Kate, Myula, Sintali na Ninde?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, ambapo katika mwaka wa fedha 2017/2018 hadi mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imejenga na kukarabati Vituo vya Afya vya Nkomolo na Kirando kwa gharama ya shilingi milioni 900. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tatu na shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi. Vilevile, Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma matatu ya zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kusogeza zaidi huduma za afya kwa wananchi, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi inakamilisha utaratibu wa kuingia makubaliano ya utoaji wa huduma za afya (service agreement) na Kituo cha Afya cha Mzimwa kinachomilikiwa na Taasisi ya Kikatoliki Abei kwa ajili ya wananchi kupata huduma za afya ikiwemo upasuaji wa dharura ambapo wananchi kutoka Tarafa za Myula na Sintali ni miongoni mwa watakaonufaika na mpango huo. Aidha, Halmashauri imetenga eneo katika Tarafa ya Chala kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya kupitia fedha za mapato ya ndani katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kujenga na kupanua vituo vya kutolea huduma za afya katika Jimbo la Nkasi na nchini kote kwa awamu kwa kuwa shughuli hizi ni endelevu.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ununuzi wa Vifaa Tiba ikiwemo vya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Mwabayanda Wilayani Maswa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Kituo cha Afya Mwabayanda kilipatiwa shilingi milioni 400 kwa ajili ya upanuzi kwa kuwa awali ilikuwa ni zahanati. Ujenzi na ukarabati wa Kituo cha Afya Mwabayanda umekamilika na kituo kimeanza kutoa huduma za dharura za upasuaji kwa akina mama wajawazito kuanzia mwezi Oktoba 2020 baada ya kupatiwa vifaa tiba kutoka kwenye vituo vingine vilivyopo katika Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021, Serikali imetoa shilingi bilioni 26 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika vituo vya afya vilivyojengwa awamu ya kwanza na ya pili na vifaa vya shilingi bilioni 15 tayari vimeshapokelewa na taratibu za kupeleka vifaa vya shilingi bilioni 11 zinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Mwabayanda kilijengwa katika awamu ya nne; na hivyo vituo vyote vya afya vilivyojengwa awamu ya tatu na ya nne vitatengewa fedha ya ununuzi wa vifaa tiba katika bajeti ya mwaka 2021/2022. Aidha, naishauri Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kupitia mapato yake ya ndani itoe kipaumbele cha ununuzi wa vifaa tiba kwa awamu ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha za ununuzi wa vifaa tiba.
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Sera ya Matibabu Bure kwa Wazee wenye umri kuanzia miaka 60 katika Halmashauri za Mkoa wa Mara inatekelezeka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inatekeleza Sera ya Afya ya Mwaka 2007 na Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003, inayoelekeza kutoa matibabu bila malipo kwa wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wasio na uwezo kwa kuwatambua na kuwapatia huduma mbalimbali za afya. Hadi Desemba, 2020 jumla ya wazee 2,344,747 wametambuliwa sawa na asimilia ya 87 ya makadirio ya wazee wote nchini. Kati yao wanaume ni 1,092,310 na wanawake 1,252,437. Aidha, wazee wasiokuwa na uwezo 1,087,008 wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bure na wazee 856,052 wamepatiwa kadi za matibabu ya Afya ya Jamii (ICHF).

Mheshimiwa Spika, hadi Februari, 2021 Halmashauri za Mkoa wa Mara zimefanya utambuzi wa wazee 70,170 kati ya lengo la kuwatambua wazee 196,000. Kati ya wazee waliotambuliwa, wanaume ni 32,900 na wanawake ni 37,270. Wazee 39,664 wamepewa vitambulisho vya matibabu kati ya wazee 70,170 waliotambuliwa.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mara na Mikoa mingine inaendelea kufanya utambuzi kwa wazee na kuhakikisha wazee wote wanaotambuliwa wanapewa vitambulisho vya matibabu bila malipo. Aidha, Serikali itaendelea kuwatambua wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wasio na uwezo ili waweze kunufaika na Sera ya Matibabu Bila Malipo.
MHE. CHARLES M. KAJEGE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itazikarabati barabara za Jimbo la Mwibara ambazo zimeharibika sana ili kuruhusu mawasiliano kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles Mugeta Kajege, Mbunge wa Jimbo la Mwibara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ina majimbo mawili ya Uchaguzi ambayo ni Bunda Vijijiini na Mwibara yenye mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 527.55. Serikali imekuwa ikitenga fedha za matengenezo ya barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambapo katika mwaka wa fedha 2019/20 shilingi milioni 546.87 zilitumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara na shilingi bilioni 708.56 zimeidhinishwa katika mwaka wa fedha 2020/21 kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha miundombinu ya barabara katika jimbo la Mwibara katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imefanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 28.2 na makalvati 11 kwa gharama ya shilingi milioni 237. 43. Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/ 21 shilingi milioni 460.44 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu kilomita 54.5 na makalvati 29 ambapo utekelezaji unaendelea.

Mheshimwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha za ujenzi na matengenezo ya barabara za Wilaya ya Bunda na nchini kote kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA K.n.y. MHE. KATANI A. KATANI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi wa Kata za Mnyawa, Nanhyanga, Nambahu, Kitama na Nguja ambao wameanza kujenga vituo vya afya kwa nguvu zao wenyewe kwa kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmad Katani, Mbunge wa Tandahimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kupitia mpango wa uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya ya msingi ulioanza katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Kituo cha Afya Mahuta, ambapo ujenzi na upanuzi umekamilika na kituo kinatoa huduma ikiwemo ya upasuaji wa dharura.

Mheshimiwa Spika, mwezi Machi, 2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Tandahimba shilingi milioni 150 kwa ajili ya kumalizia maboma ya zahanati nne za Miuta, Chikongo, Mnazi Mmoja na Mabamba. Vilevile, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali imepanga kutumia shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya zahanati na shilingi milioni 500 zitatengwa katika mapato ya ndani kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya cha Kitama.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wananchi kwa kutenga fedha za kukamilisha maboma ya zahanati, vituo vya afya na hospitali kwa awamu vikiwemo vituo vya afya katika Kata za Nanhyanga, Nambahu, Kitama na Nguja.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza:-

Serikali ilitoa shilingi 500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo, lakini kiasi cha shilingi 204,000,000 kilirejeshwa baada ya kufunga mwaka Julai, 2020.

(a) Je, ni lini fedha hizo zitarejeshwa ili ujenzi uendelee?

(b) Gharama ya ujenzi ni shilingi 1,500,000,000; je, ni lini kiasi cha shilingi 1,000,000,000 kitatolewa ili kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ilipatiwa shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali mpya ya Halmashauri ambapo majengo yaliyojengwa ni Jengo la Wagonjwa wa Nje na Maabara na majengo yote mawili yamefikia asilimia 80 ya ukamilishaji. Aidha, kati ya fedha hizo zilizotolewa shilingi milioni 204 zilirejeshwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali baada ya kuvuka mwaka wa fedha 2019/2020 kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya fedha ya mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2016.

(b) Mheshimiwa Spika, mwezi Januari 2021 Serikali imetoa shilingi bilioni 1 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ili kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Majengo yatakayojengwa ni Jengo la Utawala na Jengo la Wazazi ambayo yamefikia asilimia 40 ya ukamilishaji, Jengo la kuhifadhia dawa na Jengo la kufulia ambayo yamefikia asilimia 60 ya ukamilishaji. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Hospitali hiyo imetengewa shilingi milioni 300.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga na kukarabati majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Mbinga kutokana na kukosa baadhi ya majengo na yaliyopo kuchakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga ina majengo saba ambayo ni jengo la akinamama, jengo la huduma za Bima, jengo la upasuaji, jengo la maabara, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la mionzi na jengo la wagonjwa wa nje. Baadhi ya majengo hayo yana uchakavu wa wastani na mengine yana uchakavu wa hali ya juu. Jengo muhimu linalokosekana katika hospitali hiyo ni jengo la wodi ya watoto. Serikali imefanya tathmini ya hali ya uchakavu wa miundombinu ya hospitali hiyo ili kuona namna bora ya kufanya ukarabati au ujenzi wa hospitali mpya ya halmashauri. Kuanzia Mwaka wa Fedha 2017/2018 hadi 2019/2020, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri imefanya ukarabati wa jengo la wodi maalum na jengo la wagonjwa wa nje kwa gharama ya shilingi milioni 45.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga na katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeipatia Halmashauri ya Mji wa Mbinga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Kituo cha Afya, Kalembo ambacho ukarabati wake umekamilika na huduma zinatolewa ikiwemo huduma za upasuaji. Aidha, mwaka 2021 Serikali imeipatia shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya Zahanati za Kagugu, Iringa na Ruwaita. Vile vile katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali imeomba kuidhinishiwa shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya zahanati katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa awamu itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini kote ikiwemo katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:-

Je, ni lini Kituo cha Afya Kinesi kitapandishwa hadhi na kuwa Hospitali kamili kutokana na kituo hicho kuhudumia wananchi zaidi ya vijiji 27 katika Jimbo la Rorya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, na kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya katika Wilaya ya Rorya katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilipatia Halmashauri ya Wilaya ya Rorya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ambapo tayari ujenzi wa majengo saba ya awali umekamilika na huduma za wagonjwa wa nje zinatolewa.

Mheshimiwa Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tatu ambapo tayari Halmashauri imeshazipokea fedha hizo na fedha shilingi milioni 500 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba. Vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya Rorya. Hivyo, Serikali haikusudii kupandisha hadhi Kituo cha Afya Kinesi kuwa Hospitali ya Halmashauri kwa kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Rorya shilingi milioni 900 kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Afya Utegi kilichopewa shilingi milioni 500 na Kituo cha Afya Kinesi kilichopewa shilingi milioni 400 ambapo ujenzi na ukarabati wa vituo hivyo umekamilika na huduma za upasuaji zimeanza kutolewa. Aidha, Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.

Mheshimiwa Spika, vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo kimoja cha afya wilayani Rorya na shilingi milioni 150 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma matatu ya zahanati.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka vitendea kazi Kituo cha Afya Kata ya Mtii, Jimbo la Same Mashariki baada ya kukamilika kwa vyumba 12 vya Jengo la OPD?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuweka kumbukumbu sahihi kwanza naomba nianze kwa ufafanuzi kwamba jengo linalojengwa eneo la Mtii ni zahanati na si kituo cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati ya mpya inayojengwa kwa nguvu za wananchi, fedha za Mfuko wa Jimbo, wadau wa maendeelo pamoja na fedha za Halmashauri. Majengo yanayojengwa ni pamoja na Jengo la Wagonjwa wa Nje na Jengo la Huduma ya Kliniki ya Afya ya Mama na Mtoto ambayo tayari yamekamilika na ujenzi wa Jengo la Huduma za Uzazi unaendelea. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Same imepokea fedha shilingi milioni 150 iliyotengwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo Zahanati ya Mtii imepokea shilingi milioni 50 itakayotumika kukamilisha Jengo la Wazazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Zahanati ya Mtii itakapokamilika itapatiwa usajili na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kuwekewa utaratibu wa kupatiwa vitendea kazi.

Aidha, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele cha ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali za Halmashauri na Vituo vya Afya vilivyojengwa na kukarabatiwa na kote nchini, vikiwemo Vituo vya Afya vya Ndungu, Shengena na Kisiwani ambavyo vimepokea shilingi milioni 400 kila kimoja na Zahanati ya Kasapo iliyopokea shilingi milioni 154 vilivyoko kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Same ambavyo tayari vimepokea fedha hizo na shughuli za ujenzi zinaendelea ujenzi na ukarabati wa vituo hivyo umekamilika na huduma sasa zinatolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Halmashauri ya Wilaya ya Same iweke kipaumbele kwa kutenga bajeti kwa kupitia mapato yake ya ndani kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya zahanati mpya ya Mtii pindi itakapokamailika na kupatiwa usajili.
MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itaongeza Vituo vya Afya katika Kata za Jimbo la Segerea Pamoja na kupandisha hadhi Zahanati za Kinyerezi, Segerea, Kipawa na Yombo Kiwalani ili kuondoa adha kwa wananchi wa Kata 13 wanaotegemea Kituo kimoja cha Afya?

(b) Je, ni lini Kata za Minazi Mirefu, Buguruni, Kimanga na Kisukuru zitapatiwa Zahanati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Ladislaus Kamoli, Mbunge wa Segerea, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali iliipatia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam; iliyokuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Mwezi Februari 2021, Serikali imeipatia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tatu kwenye Hospitali ya Halmashauri na imeitenga shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2020/ 2021 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 na 2019/2020, Serikali iliipatia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Guluka Kwalala na upanuzi wa Kituo cha Afya Buguruni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia mapato yake ya ndani, imetenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitatu vya afya na shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya kuongeza miundombinu katika zahati tano ili ziweze kupandishwa hadhi kuwa vituo vya afya zikiwemo Zahanati za Kinyerezi na Kiwalani katika Jimbo la Segerea.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi milioni 250 kwa ajili ya kukamilisha maboma matano ya zahanati katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zikiwemo Zahanati za Bonyokwa na Tabata zilizopo katika Jimbo la Segerea. Aidha, kupitia mapato ya ndani, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetenga shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kulipa fidia kwenye maeneo ambayo yatachukuliwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa vituo vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya huduma za afya katika Jimbo la Segerea na nchini kote ili kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi. (Makofi)
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE aliuliza:-

Wananchi wa Kata ya Imalamate Wilayani Busega wamejenga zahanati na kumaliza maboma manne kwa maana ya zahanati moja kila kijiji:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi hao kuezeka maboma hayo ili waweze kupata huduma za afya kwenye zahanati hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya huduma za afya katika Wilaya ya Busega, ambapo katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Busega shilingi milioni 250 kwa ajili ya ukarabati wa Kituo cha Afya Nasa na kukiwezesha kuanza kutoa huduma za dharura za upasuaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 Serikali iliipatia halmashauri hiyo shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Vilevile, mwezi Februari, mwaka 2021 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Busega shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tati katika Hospitali ya Halmashauri na imetenga shilingi milioni 500 katika bajeti ya mwaka 2020/2021 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Februari, 2021, Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Busega shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma ya Zahanati za Ng’wang’wenge, Sanga na Mkula. Vilevile, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma ya Zahanati ya Imalamate, Ijutu na Busami katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya huduma za afya katika Jimbo la Busega na nchini kote ili kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza:-

Je, ni lini watumishi waliohamishiwa Halmashauri ya Uvinza kutoka Halmashauri ya Kigoma Vijijini watalipwa stahiki zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya Uvinza ina watumishi 99 wanaostahili kulipwa stahiki za uhamisho kufuatia kuhamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza katika mwaka wa fedha 2013/2014. Kiasi cha shilingi milioni 319.89 kinahitajika ili kulipa madeni hayo ya watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imezielekeza Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza kuanza kutenga fedha kupitia mapato yake ya ndani kwa ajili ya kulipa madeni na stahili za watumishi. Aidha, Serikali itaendelea kuhakiki madeni ya watumishi na kuyalipa kwa kadri wa upatikanaji wa fedha.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa maboma ya vituo vya afya yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika Kata za Makuro na Ngimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Singida shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, hospitali hiyo imetengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wa wodi tatu na shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma ya Zahanati Minyeye, Mnung’una na Msikii katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi milioni 250 kwa ajili ya kukamilisha maboma matano ya zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wananchi katika kujenga na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya huduma za afya katika Jimbo la Singida Kaskazini zikiwemo Kata za Makuro, Ngimu na nchini kote ili kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itarekebisha tatizo la Hospitali ya Frelimo ambayo inapata mgao kama Kituo cha Afya wakati ni Hospitali ya Wilaya ya Iringa tangu mwaka 2013?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, vituo vya kutolea huduma za afya nchini ikiwemo Hospitali za Halmasahuri hupatiwa mgao wa fedha za ruzuku kwa ajili ya uendeshaji na ununuzi wa dawa na vitendanishi na vifaa tiba kwa kuzingatia vigezo maalum vilivyowekwa. Vigezo hivyo ni pamoja na idadi ya watu wanaopata huduma katika eneo husika, umbali kilipo kituo, pamoja na idadi ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano katika Halmashauri husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, utofauti wa mgao baina ya vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo Hospitali ya Frelimo na Hospitali nyingine za Halmashauri hutokana na vigezo hivyo. Hospitali ya Manispaa ya Iringa Frelimo ilisajiliwa tarehe 25 Julai, 2013 kama Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na ilianza kupokea mgao wa ruzuku ya fedha za uendeshaji kama Hospitali kuanzia Agosti, 2013 ambapo kwa mwaka huu wa fedha mpaka Machi imepokea kiasi cha shilingi 53,32.

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu iliyopo katika Hospitali ya Frelimo ni pamoja na jengo la Utawala, jengo la Huduma za Wagonjwa wa Nje, jengo la huduma za Maabara, jengo la huduma za Mionzi, jengo la Ufuaji na jengo la Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto. Miundombinu inayokosekana katika Hospitali hii ni pamoja na jengo la upasuaji, Wodi za kulaza wagonjwa, jengo la kuhifadhia maiti, na jengo la kutunzia dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuongeza majengo kwenye Hospitali hii ili kuboresha huduma zinazotolewa. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya upungufu wa watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe hasa kwenye Idara za Afya, Elimu na Kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Ikama ya mwaka 2020/2021, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe inapaswa kuwa na watumishi 2,630. Hadi Machi 2021 Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ilikuwa na watumishi 2,294 hivyo ina upungufu wa watumishi 336 sawa na asilimia 12.8.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Ikama Idara ya Afya katika Halmashauri ya Wlaya ya Korogwe inapaswa kuwa na watumishi 392, na hadi Machi 2021 Idara ya Afya ilikuwa na watumishi 263 hivyo ina upungufu wa watumishi 129 sawa na asilimia 32.9. Idara za Elimu msingi na sekondari zinapaswa kuwa na watumishi 1891 lakini zina watumishi 1604 hivyo zina upungufu wa watumishi 287 sawa na asilimia 15.2. Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika inapaswa kuwa na watumishi 55 na ina watumishi 45 hivyo ina upungufu wa watumishi 10 sawa na asilimia 18.2.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeendelea kuajiri na kuwapnaga watumishi wa kada mbalimbali katika halmashauri nchini ambapo katika mwaka wa fedha 2020/21 watumishi 81 wapya waliajiriwa na kupangwa katika Halamshauri ya Wilaya ya Korogwe. Kati ya hao, watumishi 22 ni walimu wa sekondari, 35 shule za msingi, 6 watumishi wa kada za afya na Afisa Ugani 1 pamoja na 17 wa kada mbalimbali. Pamoja na jitihada hizo, katika Ikama ya mwaka 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya imetenga nafasi za ajira mpya 150 ambao watapangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-

Je, Serikai haioni umuhimu wa kuajiri Wafamasia angalau katika kila Kituo cha Afya nchini ili kuimarisha usimamizi na mtiririko wa upatikanaji dawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Jimbo la Bukene, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ikama wa watumishi wa afya, Mfamasia anapaswa kuwepo katika ngazi ya Hospitali. Kwenye ngazi ya Vituo vya Afya na Zahanati, ikama inaelekeza kuwepo kwa Mteknolojia wa Dawa au Mteknolojia Msaidizi wa Dawa. Kada hizi ni muhimu kuwepo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuimarisha uratibu na usimamizi wa bidhaa za afya.

Mheshimiwa Spika, kuanzia Mei, 2017 hadi Februari, 2021 Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeajiri Wafamasia 79, Wateknolojia wa Dawa 313 na Wateknolojia wa Dawa Wasaidizi 160. Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa Wataalam hawa, ambapo katika mwaka wa fedha 2021/ 2022 imepanga kuajiri watumishi 10,467 wakiwemo Wafamasia na Wateknolojia wa Dawa watakaopelekwa kwenye Hospitali za Halmashauri, Vituo vya Afya pamoja na zahanati kote nchini.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-

Kumekuwa na changamoto ya huduma za Afya katika Zahanati zetu hasa ukosefu wa dawa pamoja na huduma bure kwa wazee, watoto na akinamama wajawazito.

Je, ni lini Serikali itahakikisha Sera ya Afya inatekelezwa bila tatizo lolote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa kuongeza bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba kutoka shilingi bilioni 31 katika mwaka wa fedha 2015/2016 hadi shilingi bilioni 270 katika mwaka wa fedha 2020/2021. Ongezeko hilo la fedha limewezesha kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu (tracer medicine) kutoka wastani wa asilimia 31 mwaka 2015/2016 hadi asilimia 90 kufikia Aprili 30, 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Mei, 2021 Serikali imetoa huduma ya matibabu bila malipo yenye gharama ya shilingi bilioni 30.1 kwa wananchi wa makundi maalum milioni 12 ikijumlisha wazee, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizi, bado kuna changamoto ya upatikanaji wa baadhi ya dawa za makundi maalum kama wazee, wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, mwezi Novemba, 2020 Serikali ilitoa shilingi bilioni 41.2, mwezi Februari, 2021 Serikali ilipeleka shilingi bilioni
18.2 katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa na mwezi Mei, 2021 Serikali imepeleka shilingi bilioni 80 na kufanya jumla ya fedha zote zilizopelekwa kwa ajili ya dawa kufikia shilingi bilioni 140.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa dawa na bidhaa nyingine za afya ili kuboresha huduma kwa makundi maalum na wananchi kwa ujumla.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wanaume, akina mama na watoto katika Hospitali ya Wilaya ya Frelimo katika Manispaa ya Iringa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa (Frelimo) imeanza kufanya kazi kama Hospitali ya Halmashauri mwezi Februari, 2012 na kusajiliwa rasmi mwaka 2013. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliipatia Halmashauri ya Manispaa ya Iringa shilingi milioni 400 kwa ajili ya upanuzi wa hospitali ambapo jengo la maabara na jengo la mionzi yalijengwa na kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu iliyopo katika Hospitali ya Frelimo ni pamoja na jengo la utawala, jengo la huduma za wagonjwa wa nje (OPD), jengo la huduma za maabara, jengo la huduma za mionzi, jengo la kufualia na jengo la huduma za afya ya uzazi na mtoto. Miundombinu inayokosekana katika hospitali hii ni pamoja na jengo la upasuaji, wodi za kulaza wagonjwa, jengo la kuhifadhi maiti na jengo la kutunzia dawa. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya watoto, wodi ya wanaume na wodi ya wanawake magonjwa mchanganyiko (medical ward).
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-

Je, ni kwa nini Hospitali ya Mji Tarime isipandishwe hadhi na kuwa Hospitali ya Kanda Maalum ya Tarime na Rorya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Mji Tarime ina Wodi nane na vitengo mbalimbali vya huduma ikiwemo maabara, jengo la mionzi, chumba cha upasuaji, huduma za mama na mtoto, chumba cha dawa, chumba cha magonjwa ya akili, macho, duka la dawa lakini pia miundombinu mingine. Hospitali hii inahudumia wastani wa wagonjwa 140 wa nje (OPD), lakini inahudumia wagonjwa 70 wanaolazwa kwa siku. Hospitali ina jumla ya vitanda 180.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kanda ya Ziwa tayari ina Hospitali ya Rufaa ambayo ni Hospitali ya Bugando iliyopo Mkoa wa Mwanza. Hivyo, Serikali haikusudii kuipandisha hadhi Hospitali ya Mji Tarime kuwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Maalum ya Tarime na Rorya. (Makofi)
MHE. NICHOLAS G. NGASSA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaipatia Hospitali ya Wilaya ya Igunga gari la kubebea wagonjwa kwa kuwa lililopo limechakaa sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholas George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, gari la wagonjwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ni chakavu na halifai kuendelea kutumika. Kwa sasa Hospitali ya Halmashauri ya Igunga imepatiwa gari la Kituo cha Afya kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kutoka katika Kituo cha Afya cha Choma ambalo linatoa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto za uchakavu wa magari ya kubebea wagonjwa katika Hospitali na Vituo vya Afya nchini. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kununua magari ya kubebea wagonjwa na itatoa kipaumbele kwa Hospitali na Vituo vya Afya vyenye uhitaji mkubwa wa magari ya kubebea wagonjwa.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakipatia Kituo cha Afya cha Muyama Wilayani Buhigwe vifaa vya Ultrasound na X-ray?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Muyama katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe hakitoi huduma ya uchunguzi wa Ultrasound na X-ray kutokana na ukosefu wa majengo lakini na vifaa hivyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inamuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buhigwe kupanga kununua Ultrasound kupitia mapato ya ndani wakati Serikali Kuu inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kununua X-ray. Aidha, ikiwa mapato ya ndani ya Halmashauri hayatoshelezi, Serikali inamshauri Mkurugenzi kukopa kupitia NHIF na kununua mashine ya Ultrasound wakati Serikali inapanga kununua X- ray.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-

Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Vituo vya Afya vya Mwangozo na Uyowa katika Jimbo la Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2020/2021 imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kiasi cha Shilingi milioni 600 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Uyowa na ujenzi unaendelea. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wananchi inaendelea na ujenzi wa Kituo cha Afya Mwangozo. Hadi Aprili 2021, shilingi milioni 158.69 zinazotokana na michango ya wananchi na mapato ya ndani ya halmashauri zimetumika kujenga jengo la wagonjwa wa nje na wodi ya wazazi ambapo ujenzi unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, halmashauri imetenga shilingi milioni 25 na katika mwaka wa fedha 2021/2022, Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua imetenga shilingi milioni 140 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Je, ni nini mpango wa Serikali kuwawezesha akina baba kiuchumi baada ya mpango wa Halmashauri wa kuwawezesha akina mama, vijana na watu wenye ulemavu kuwa na mafanikio makubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeendelea kuwezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Mikopo hiyo hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 kifungu cha 37A inayoelekeza kutenga 10% ya mapato yanayokusanywa na Halmashauri kwa ajili ya mikopo ya 4% kwa wanawake, 4% kwa vijana na 2% kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, lengo la mikopo hii ni kusaidia makundi maalum katika jamii ambayo hayawezi kupata mikopo katika mabenki ya biashara na taasisi za fedha kwa sababu ya masharti magumu ikiwemo dhamana na riba kubwa. Hivyo, Serikali ilitoa kipaumbele kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa kuwa wengi wao hawakopesheki katika mabenki na taasisi za fedha. Kwa sasa Serikali haikusudii kuanzisha mpango wa kuwawezesha wanaume au akina baba katika mikopo hii.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kwa sababu Hospitali iliyopo haikidhi mahitaji kutokana na uchakavu na ongezeko la watu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa hospitali 43 kongwe na chakavu za Halmashauri ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni. Serikali inaendelea kufanya tathmini ya miundombinu ya hospitali hizo ili kuona namna bora ya kuziboresha ikiwemo kuzikarabati au kujenga hospitali mpya kulingana na matokeo ya tathmini.

Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kukamilisha kwanza ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 28 na hivyo baada ya ujenzi huo kisha hospitali chakavu zitawekewa mpango.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itazirejesha fedha za ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Msalala zilizorudishwa na mfumo baada ya mwaka wa fedha 2019/2020 kuisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ilipatiwa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Hadi Juni 30 mwaka 2020, Halmashauri hiyo ilikuwa imetumia shilingi milioni 22.4 pekee na hivyo shilingi milioni 477.59 zilirejeshwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti Namba 11 ya Mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2015. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Msalala shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa awamu hadi ujenzi wa hospitali hiyo utakapokamilika.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italeta gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Mgololo?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Mgololo kilipatiwa gari la kubeba wagonjwa mwaka 2018 ambalo linalotumika kwa sasa kuhudumia wagonjwa wa dharura kwenye kituo hicho. Hata hivyo, kutokana na udogo wa gari hilo na ugumu wa jiografia ya eneo husika, gari la kubebea wagonjwa lililopo Kituo cha Afya Kasanga hutumika kuhudumia wagonjwa wa dharura inapohitajika.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa magari ya kubebea wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na kwa kulizingatia hilo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri imenunua gari ya wagonjwa kwa kutumia mapato yake ya ndani lenye thamani ya shilingi milioni 174.

Aidha, Halmashauri imefanya matengenezo ya magari mawili ya wagonjwa ambayo yalikuwa mabovu kwa muda mrefu na kufanya Halmashauri kuwa na jumla ya magari matano ya kubebea wagonjwa. Magari haya yanatumika kubeba wagonjwa mara tu dharura zinapotokea katika vituo vya afya vilivyopo Wilayani Mufindi.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ya wagonjwa ili kuboresha huduma za rufaa Wilayani Mufindi na nchini kwa ujumla, ahsante.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati barabara zilizoharibika hasa barabara za vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua adha kubwa inayotokana na kuharibika kwa miundombinu ya barabara uliosababishwa na mvua nyingi zilizonyesha msimu wa mwaka 2019/2020 na msimu wa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza bajeti ya matengenezo ya barabara ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kutoka shilingi bilioni 275.03 iliyotengwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 hadi shilingi bilioni 400 iliyotengwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 ambalo ni ongezeko la Shilingi bilioni 124.97 sawa na aslimia 45.4. Ongezeko hili litaiwezesha TARURA kufanya matengenezo ya miundombinu ilyoharibika kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti ya ujenzi na matengenezo ya barabara kadri ya upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya Igunga – Miswaki – Loya – Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida yenye urefu wa kilometa 89?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daudi Protas Venant, Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Igunga – Miswaki –Loya – Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida ni barabara inayouganisha Wilaya za Igunga na Uyui. Kwa upande wa Wilaya ya Igunga, barabara hii inajulikana kama barabara ya Igunga – Itumba – Buhekela – Simbo na ina urefu wa kilometa 107. Kwa upande wa Wilaya ya Uyui barabra hii inaunganisha barabara tatu ambazo ni Simbo - Miswaki - Loya – Migongwa – Magulyati yenye urefu wa kilometa 72.8, hivyo kufanya urefu wa barabara ya Igunga – Miswaki – Loya –Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida kuwa na urefu wa kilometa 179.8.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 TARURA Halmashauri za Wilaya ya Igunga na Uyui zimetenga jumla ya shilingi milioni 361.99 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida, kilometa 27, maeneo korofi kilometa 8.7 na matengenezo maalumu kilometa tano na ujenzi unaendelea. Aidha, katika mwaka 2021/2022 TARURA Halmashauri za Wilaya ya Igunga na Uyui zimetenga jumla ya shilingi milioni 235 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kilometa 35 na ujenzi wa daraja dogo (box culvert) mawili, makalvati mistari minne ili kuimarisha maeneo korofi ya barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kuzifanyia matengenezo barabara katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na upatikanaji wa fedha, nashukuru sana.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, ni lini Hospitali ya Wilaya ya Rorya itaanza kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Jimbo la Rorya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ambapo kati ya mwaka wa fedha 2018/2019 hadi 2020/2021 Serikali imeipatia shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tisa na shughuli za ujenzi zinaendelea ambapo ujenzi wa majengo saba ya awali umekamilika na tangu Juni 2020 inatoa huduma ya wagonjwa wa nje (OPD). Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Rorya.

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya inatarajiwa kuanza kutoa huduma za upasuaji wa dharula na kulaza wagonjwa ifikapo Disemba, 2021.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Afya Bashnet baada ya Serikali ya Kijiji kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na mpango wa kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kuendelea na ujenzi wa vituo vya afya nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Babati. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya ya Babati kupitia mapato yake ya ndani imetenga shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya Bashnet katika eneo lenye ukubwa wa ekari 12.6 lililotengwa na Serikali ya Kijiji.

Mhjeshimiwa Spika, Ujenzi huo utaanza katika mwaka wa fedha 2021/2022 kama ilivyopangwa.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kupeleka watumishi wa Idara ya Afya katika Jimbo la Kilwa Kaskazini ambalo lina uhaba mkubwa wa watumishi kiasi cha kufanya baadhi ya zahanati kutoa huduma duni na nyingine kuchelewa kufunguliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 60 zikiwemo hospitali mbili, vituo vya afya vitano na zahanati 53. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017 hadi Desemba, 2020, Serikali imeajiri na kuwapanga watumishi 108 wa kada mbalimbali za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Aidha, mwezi Mei, 2021 Ofisi ya Rais-TAMISEMI imetangaza nafasi 2,726 za ajira za kada mbalimbali za afya. Watumishi hao watapangwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini kwa kutoa kipaumbele kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vyenye upungufu mkubwa wa watumishi ikiwemo baadhi ya vituo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya na kuwapangia katika vituo Wilayani Kilwa na kote nchini kwa ujumla, ahsante sana.
MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka na kuongeza vifaa tiba na wataalam katika vituo vya afya ilivyojenga vikiwemo vifaa tiba maalum kama vile “incubator beds” na taa maalum kwa ajili ya kukabiliana na homa ya manjano kwa watoto njiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika,utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa vituo vya afya unaenda sambamba na mpango wa ununuzi wa vifaa tiba. Kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2020/2021 Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 68.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika vituo vya afya vilivyojengwa na kukarabatiwa ili kuwezesha utoaji wa huduma za dharura na upasuaji kwa akinamama wajawazito na wananchi kwa ujumla. Vifaa vilivyonunuliwa vinajumuisha vifaa kwa ajili ya kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya muda (Infant Radiant Warmers).

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imetoa shilingi bilioni 34 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali mpya 67 za Halmashauri zilizojengwa kuanzia mwaka wa fedha 2017/ 2018.

Mheshimiwa Spika, kuanzia Mei, 2017 hadi Mei, 2020 Serikali imeajiri na kuwapanga watumishi 9,531 wa kada mbalimbali za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Aidha, mwezi Mei 2021 Ofisi ya Rais - TAMISEMI imetangaza nafasi 2,726 za kada mbalimbali za afya. Wataalam hao watapangwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini na kipaumbele kitakuwa kwenye vituo vyenye uhitaji mkubwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya nchini kwa kuboresha miundombinu, kununua vifaa tiba na kuajiri wataalam wa kada mbalimbali za afya kwa kadri ya upatikanaji wa fedha, ahsante sana.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italeta gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Mgololo?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Mgololo kilipatiwa gari la kubeba wagonjwa mwaka 2018 ambalo linalotumika kwa sasa kuhudumia wagonjwa wa dharura kwenye kituo hicho. Hata hivyo, kutokana na udogo wa gari hilo na ugumu wa jiografia ya eneo husika, gari la kubebea wagonjwa lililopo Kituo cha Afya Kasanga hutumika kuhudumia wagonjwa wa dharura inapohitajika.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa magari ya kubebea wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na kwa kulizingatia hilo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri imenunua gari ya wagonjwa kwa kutumia mapato yake ya ndani lenye thamani ya shilingi milioni 174.

Aidha, Halmashauri imefanya matengenezo ya magari mawili ya wagonjwa ambayo yalikuwa mabovu kwa muda mrefu na kufanya Halmashauri kuwa na jumla ya magari matano ya kubebea wagonjwa. Magari haya yanatumika kubeba wagonjwa mara tu dharura zinapotokea katika vituo vya afya vilivyopo Wilayani Mufindi.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ya wagonjwa ili kuboresha huduma za rufaa Wilayani Mufindi na nchini kwa ujumla, ahsante.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati barabara zilizoharibika hasa barabara za vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua adha kubwa inayotokana na kuharibika kwa miundombinu ya barabara uliosababishwa na mvua nyingi zilizonyesha msimu wa mwaka 2019/2020 na msimu wa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza bajeti ya matengenezo ya barabara ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kutoka shilingi bilioni 275.03 iliyotengwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 hadi shilingi bilioni 400 iliyotengwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 ambalo ni ongezeko la Shilingi bilioni 124.97 sawa na aslimia 45.4. Ongezeko hili litaiwezesha TARURA kufanya matengenezo ya miundombinu ilyoharibika kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti ya ujenzi na matengenezo ya barabara kadri ya upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya Igunga – Miswaki – Loya – Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida yenye urefu wa kilometa 89?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daudi Protas Venant, Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Igunga – Miswaki –Loya – Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida ni barabara inayouganisha Wilaya za Igunga na Uyui. Kwa upande wa Wilaya ya Igunga, barabara hii inajulikana kama barabara ya Igunga – Itumba – Buhekela – Simbo na ina urefu wa kilometa 107. Kwa upande wa Wilaya ya Uyui barabra hii inaunganisha barabara tatu ambazo ni Simbo - Miswaki - Loya – Migongwa – Magulyati yenye urefu wa kilometa 72.8, hivyo kufanya urefu wa barabara ya Igunga – Miswaki – Loya –Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida kuwa na urefu wa kilometa 179.8.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 TARURA Halmashauri za Wilaya ya Igunga na Uyui zimetenga jumla ya shilingi milioni 361.99 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida, kilometa 27, maeneo korofi kilometa 8.7 na matengenezo maalumu kilometa tano na ujenzi unaendelea. Aidha, katika mwaka 2021/2022 TARURA Halmashauri za Wilaya ya Igunga na Uyui zimetenga jumla ya shilingi milioni 235 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kilometa 35 na ujenzi wa daraja dogo (box culvert) mawili, makalvati mistari minne ili kuimarisha maeneo korofi ya barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kuzifanyia matengenezo barabara katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na upatikanaji wa fedha, nashukuru sana.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je ni lini Serikali itaainisha mpaka kati ya Wilaya ya Mkalama na Hanang’ eneo la Singa na Limbadau ili kuondoa taaruki kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kuna mgogoro wa mipaka ya Vijiji kati ya Wilaya za Mkalama na Hanang ambao umekuwepo kwa muda mrefu licha ya jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ikwemo vikao vya ujirani mwema baina ya wahusika wa mgogoro, Serikali ilitekeleza uwekaji wa alama za mipaka iliyotangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 266 la tarehe 14 Desemba 1973 lililotangaza Wilaya ya Mbulu na Hanang’. Chanzo kikubwa cha mgogoro huo ni baaadhi ya wananchi kutokukubaliana na alama za mipaka zilizopo kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 266 la uanzishwaji wa Wilaya ya Mbulu na Wilaya ya Hanang’.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri za Wilaya ya Hanang na Mkalama zimetenga jumla ya shilingi milioni 40 kwa ajili ya kupima Vijiji vya Singa na Limbadau ambavyo ndio vipo kwenye eneo la mgogoro. Serikali inatarajia mgogoro huo utamalizika, ahsante sana.
MHE. MWANTUMU M. ZODO K.n.y. MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mtwara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2018/2019 hadi Mei, 2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Hospitali hiyo inajengwa katika Kituo cha Afya Nanguruwe ambacho kitapandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Halmashauri baada ya kuongeza miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Mei, 2021 ujenzi wa majengo matano umekamilika. Ujenzi wa wodi tatu za kulaza wagonjwa unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2021. Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba katika Hospitali ya Halmashauri. Vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua migogoro ya mipaka kati ya Vijiji vya Mwanholo na Nyenze dhidi ya Mwekezaji na Mchimbaji Madini Eli Hilal Wilayani Kishapu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nyangindu Boniphace Butondo, Mbunge wa Jimbo la Kishapu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mgogoro wa mipaka kati ya Vijiji vya Mwanholo na Nyenze dhidi ya Mwekezaji na Mchimbaji wa Madini aitwaye Eli Hilal Wilayani Kishapu unaohusisha eneo lenye ukubwa wa hekta 2,872.4. Eneo hilo awali lililkuwa linamilikiwa na Mgodi wa Wiliamson Diamond Limited, kabla ya kugawiwa kwa Mchimbaji Eli Hilal ambaye alimilikishwa na Serikali. Baadhi ya wanakijiji wa Mwanholo na Nyenze hawaitambui mipaka ya eneo la mwekezaji wa uchimbaji wa madini na wengine wanalalamikia maeneo yao kutwaliwa na mwekezaji wa uchimbaji bila kulipa fidia.

Mheshimiwa Spika, mwezi Februari, 2021, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga iliunda Timu ya Wataalam kwa ajili kufanya uchunguzi wa mgogoro huo. Timu iliyoundwa imewasilisha taarifa yake na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga inaendelea kuifanyia kazi taarifa iliyowasilishwa ili kubaini masuala yanayoweza kushughulikiwa na Mkoa na yale yanayohitaji uamuzi wa ngazi za juu. Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga itashirikiana na wananchi na wadau wote muhimu katika kutatua mgogoro huu na kuhakikisha haki inatendeka.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-

Halmasauri ya Wilaya ya Lushoto ina upungufu wa walimu wa shule za msingi takribani 1,270 kwa mujibu wa ikama: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka walimu katika Halmashauri hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, – TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Jimbo la Mlalo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2019/2020 Serikali imeajiri na kuwapanga walimu 148 wa shule za msingi na walimu 118 wa shule za sekondari katika Halmashauri ya Lushoto kati ya walimu 26,181 wa shule za msingi na sekondari walioajiriwa katika kipindi hicho. Aidha, Serikali inaendelea kuratibu zoezi la kuajiri walimu 6,949 kwa nafasi za ajira zilizotangazwa mwezi Mei, 2021 ambao watapangwa kwenye shule mbalimbali zikiwemo za Wilaya ya Lushoto, ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO K.n.y. MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake na vijana katika Halmashauri wanapewa mikopo ya asilimia tano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni ya 23 ya Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo ya asimilia 10 kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za mwaka 2019, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinapaswa kutoa mafunzo kwa vikundi vilivyokubaliwa kupata mikopo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia Kanuni hiyo Serikali ilikwishaanza kutoa elimu ya ujasiriamali na katika mwaka wa fedha 2019/2020 Mamlaka za Serikali za Mitaa zimetoa mafunzo kwa vikundi 11,915 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambavyo vilipewa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zote nchini. Mafunzo yaliyotolewa ni pamoja na mafunzo ya ujasiriamali, utunzaji fedha, uendeshaji na usimamizi wa miradi, utoaji taarifa na usimamizi wa marejesho ya mikopo. Serikali kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa itaendelea kutoa elimu kwa vikundi hivyo ili kuvijengea uwezo wa kuendelea kukua na kutumia ipasavyo fursa mbalimbali za kiuchumi katika maeneo yao, ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza:-

Kituo cha Afya Upuge kinahitaji jengo kwa ajili ya mashine za mionzi yaani x-ray na ultra sound: -

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya mashine hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athumani Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Uyui shilingi milioni 500 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Kituo cha Afya Upuge. Ujenzi wa majengo manne ulifanyika na majengo yote yanatumika. Serikali inatambua uhitaji wa jengo la x-ray na ultra sound katika kituo hicho. Serikali imekwishatoa ramani za majengo ya mionzi kwa Halmashauri zote nchini ikwemo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, Serikali inaielekeza Halmashauri kutenga fedha za mapato ya ndani ili kuanza ujenzi huo kwa awamu kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023. Serikali itaendelea kuboresha majengo ya x-ray na ultra sound kote nchini.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-

Kituo cha Afya Msindo kilichopo Wilayani Namtumbo kinapata mgao mdogo wa dawa usiokidhi mahitaji: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza mgao wa dawa katika Kituo cha Afya Msindo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Msindo kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kilipandishwa hadhi kutoka Zahanati na kuwa Kituo cha Afya tarehe 26 Machi, 2014. Kituo hiki kimekuwa kikipokea mgao wa dawa kama Zahanati badala ya Kituo cha Afya kwa kuwa Halmashauri haikuwasilisha maombi husika kadri ya utaratibu. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kutumia fedha za makusanyo zinazotokana na uchangiaji wa huduma za afya kwa ajili ya ununuzi wa dawa. Wastani wa upatikanaji wa dawa muhimu katika kituo hiki ni asilimia 87.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kuwasilisha rasmi maombi ya mgao wa fedha za dawa za Kituo cha Afya Msindo kupitia ruzuku ya Serikali Kuu ili mgao huo urekebishwe na kukiwezesha kituo hicho kupatiwa mgao wa dawa wenye hadhi ya Kituo cha Afya, ahsante.
MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: -

Sekta ya Afya nchini ina upungufu wa Watumishi wapatao 16,000:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na changamoto hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA(MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Mzamili Zodo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Sekta ya Afya nchini ina upungufu wa watumishi ambapo hadi mwezi Mei 2021 watumishi waliokuwepo ni asilimia 41 ya mahitaji halisi. Upungufu huo unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kustaafu kazi, kufariki na kuongezeka kwa idadi ya Vituo vya kutolea huduma za afya nchini kutokana na utekelezaji wa Programu ya Ujenzi na Ukarabati wa Vituo vya kutolea huduma za Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 2017 hadi 2020 Serikali kwa kushirikiana na wadau imeajiri watumishi 12,868 wa Sekta ya Afya ambao wamepangwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Adha, Serikali inakamilisha taratibu za ajira 2,726 za watumishi wa kada mbalimbali za afya zilizotangazwa Mwezi Mei 2021. Watumishi hao watapangwa kwenye Vituo vya kutolea huduma za afya vyenye uhitaji mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ili kukabiliana na changamoto hii, mpango wa Serikali ni kuendelea kuajiri watumishi wa kada za afya kwa awamu, nashukuru.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutekeleza Sera ya Afya ya kuwa na Kituo cha Afya kwa kila Kata ili kupunguza vifo vya Mama na Mtoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutekeleza Sera ya Afya ya kuwa na Zahanati kwa kila Kijiji na Kituo cha Afya kwa kila Kata kwa awamu ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2020/2021 Serikali imejenga Zahanati 1,281, Vituo vya Afya 488 na Hospitali za Halmashauri 102. Mpango huu umewezesha kuongeza Vituo vya Afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa vyenye uwezo wa kutoa huduma za dharula za upasuaji kutoka Vituo 115 Disemba 2015 hadi Vituo 352 Juni 2021 na hivyo kuchangia katika kupunguza vifo vya mama wajawazito na Watoto. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali itaendelea na ujenzi wa vituo vya afya 121 na kiasi cha shilingi billioni 27.75 kimetengwa kwa ajili ya umaliziaji wa maboma 768 ya zahanati kote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali ni kuendelea kutenga fedha za ujenzi wa vituo vya afya kwa awamu. Nakushukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka uwiano sawa wa mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani bila kujali mapato ya halmashauri husika ili kusaidia wanufaika wa mikopo wanaoishi nje ya miji wapate fursa sawa na wanufaika wa mijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura ya 290 kifungu cha 37(a) na Kanuni zake za mwaka 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa Sheria ya mikopo ya asilimia 10 ya wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu ni asilimia 10 ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri baada ya kuondoa mapato lindwa. Hivyo kiwango cha mikopo kinatokana na uwezo wa makusanyo ya halmashauri husika. Halmashauri zimeelekezwa kutoa fursa sawa za mikopo kwa vikundi vyote vilivyokidhi vigezo vilivyopo ndani ya halmashauri husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo hii ni sehemu tu ya mifuko mbalimbali ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi iliyopo nchini, na Serikali itaendelea kuiboresha kadri itakavyohitajika.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Halmashauri ya Sumbawanga katika Mji wa Laela baada ya agizo la Serikali la kuhamisha Makao Makuu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ni miongoni mwa Halmashauri 30 zilizohamia kwenye maeneo mapya ya utawala mwaka 2019.

Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha Halmashauri kutoa huduma bora kwa wananchi, Serikali imeweka mpango wa ujenzi wa jengo la utawala utakaogharimu shilingi bilioni 2.7.

Mheshimiwa Spika, mwezi Mei, 2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuendelea na ujenzi huo. Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga imesaini mkataba wa ufundi na Chuo cha Sayansi Mbeya kwa ajili ya ujenzi utakaoanza tarehe 22 Juni, 2021.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha za ukamilishaji wa jengo hilo, ahsante sana.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kurasimisha vitambulisho vya wajasiriamali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwezi Machi 2018, Serikali kwa kuwathamini na kuwajali wajasiriamali na watoa huduma wadogo ilianzisha utaratibu wa vitambulisho ili kuwawezesha kufanya biashara katika mazingira bora na tulivu zaidi. Vitambulisho hivi vilirasimishwa kutumiwa na wajasiriamali wenye mitaji yao na mauzo ghafi yasiyozidi shilingi milioni nne kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2021 vitambulisho vya wajasiriamali wadogo vimefanyiwa maboresho kadhaa ikiwemo kuwekwa picha na jina la mjasiriamali mdogo aliyepatiwa kitambulisho hicho pamoja na ukomo wa muda wa kutumia kitambulisho hicho. Muda wa matumizi ni mwaka mmoja tangu tarehe ya kupatiwa kitambulisho badala ya mwaka wa kalenda kama ilivyokuwa awali.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha vitambulisho vya wajasiriamali wadogo kadri itakavyohitajika, ahsante.
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Afya Ikuwo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Festo Richard Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha huduma za afya katika Wilaya ya Makete, Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Makete shilingi milioni 400 katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Ipelele. Ujenzi wa Kituo hicho umekamilika na kinatoa huduma zikiwemo huduma za dharura za upasuaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Makete shilingi milioni 150 kwa ajili ya ukamilishaji wa Zahanati za Usungilo, Nungu na Matenga. Vilevile, Mei 2021, Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Makete shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kitulo. Aidha, ombi la Kituo cha Afya Ikuwo limepokelewa na linafanyiwa tathimini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaipitia na kuiboresha Sera ya Ujenzi wa Zahanati kila Kijiji na Kituo cha Afya kila Kata ili ujenzi ufanyike kimkakati na kwa tija zaidi badala ya kila Kijiji na kila Kata. Ahsante.
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: -

(a) Je, ni lini Serikali itajenga Vituo vya Afya vya Issuna, Ikungi, Makiungu, Ntuntu na Misughaa ili kurahisisha huduma za dharura Wilayani Ikungi kwa kuwa Wilaya hii inapitiwa na Barabara ya Dodoma – Mwanza ambayo imekuwa na ajali za mara kwa mara?

(b) Je, ni lini Serikali itapeleka Gari la Wagonjwa ili kuwahisha majeruhi na wagonjwa katika Hospitali za Rufaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshmiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi iliyoanza kujengwa mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo hadi mwezi Mei 2021 ilikuwa imepatiwa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali hiyo. Hospitali hiyo itasaidia kuokoa maisha ya majeruhi wa ajali zitakazotokea eneo la Ikungi katika barabara ya Dodoma hadi Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi Mei 2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi shilingi milioni 900 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya Ihanja na Sepuka. Ujenzi wa Vituo hivyo umekamilika na vinatoa huduma ikiwemo huduma za dharura za upasuaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapitia Sera ya Zahanati katika kila Kijiji na Kituo cha Afya katika kila Kata na itafanyiwa maboresho yenye tija zaidi ili ili ujenzi uwe wa kimkakati badala ya kila Kijiji au kila Kata.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya Ikungi ina magari matatu ya kubebea wagonjwa ambayo yapo katika Vituo vya Afya Ikungi, Sepuka na Ihanja ambayo yote yanaendelea kutoa huduma za rufaa za dharura ndani na nje ya wilaya ya Ikungi. Ahsante.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kutatua changamoto iliyopo katika vituo vya kutolea huduma za afya ya kukosekana kwa Idara ya Huduma ya Mazoezi Tiba na Utengamao ukilinganisha na ongezeko la wagonjwa wanaohitaji aina hiyo ya tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa kuna ongezeko kubwa la uhitaji wa huduma ya mazoezi tiba na utengamao kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, huku kukiwa na changamoto ya uwepo wa miundombinu stahiki, vifaa na wataalam kwenye vituo vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefanya tathmini ya mahitaji wa huduma ya mazoezi tiba na utengamao kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na inaendelea kukamilisha mpango mkakati ambao utatoa mwongozo katika kutatua uhitaji wa huduma hizo. Ofisi ya Rais, TAMISEMI itatekeleza kikamilifu mpango utakaotolewa ili kuboresha huduma ya mazoezi tiba na utengamao katika vituo vya afya. Ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, ni lini Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio itatambuliwa rasmi na kuanza kuwahudumia wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tangazo la kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio lilitolewa tarehe 1/10/2007 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa, Mamlaka za Wilaya Sheria Na. 7 ya mwaka 1982 kifungu cha 16 na 17.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013 Serikali iliunda timu ya wataalam kwa ajili ya kuchukua maoni ya wananchi kuufanya Mji Mdogo wa Nansio kuwa Halmashauri ya Mji. Wananchi wa kata kumi zilizopendekezwa kuunda Halmashauri ya Mji Nansio waliridhia Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio kupandishwa hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji na mapendekezo hayo yaliwasilishwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mwaka 2014.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilipokea mapendekezo hayo na kutuma timu ya wataalam kwenda katika Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio ili kujiridhisha kama vigezo muhimu vinavyotakiwa ili kupandisha hadhi Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio vimefikiwa. Timu ilibaini kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio bado haikidhi vigezo vya kupandishwa hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji.

Mheshimiwa Spika, vigezo zilivyokosekana ni pamoja na kutokuwa na idadi ya watu angalau 150,000, kutokuwa na eneo lenye ukubwa wa walau kilomita za mraba 300, kutokuwa na kata walau 12 na mitaa 60. Hivyo, Ofisi ya Rais- TAMISEMI iliishauri Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kuendelea kuilea Mamlaka ya Mji Mdogo wa Nansio mpaka itakapokidhi vigezo. Ahsante sana.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -

Wananchi wa Wilaya ya Same bado wanaendelea kutaabika sana kwa kukosa huduma bora za afya kwenye Hospitali ya Wilaya licha ya ahadi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa ya ujenzi wa hospitali mpya ya Halmashauri ya Wilaya ya Same.

Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa ikizingatiwa kuwa eneo la ujenzi wa hospitali hiyo tayari limeshatengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya nchini zikiwemo Hospitali za Halmashauri. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni 55.7 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali 68 za Halmashauri zilizoanza kujengwa katika mwaka wa fedha 2018/2019. Pia Serikali imetenga shilingi bilioni 11.4 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali 27 za Halmashauri zilizoanza kujengwa katika mwaka wa fedha 2019/2020 na shilingi bilioni 14 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali 28 za Halmashauri katika Halmashauri 28 ambazo hazikuwa na Hospitali za Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa Hospitali kongwe 43 za Halmashauri ambazo zina uchakavu wa miundombinu ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Same. Kupitia Programu ya Ujenzi na Ukarabati wa Vituo vya Kutolea Huduma za Afya nchini; Hospitali hizo zitaanza kujengwa upya kwa awamu kuanzia mwaka wa fedha 2022/ 2023. Ahsante.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba ikiwemo x-ray pamoja na vifaa vingine vya kupima wagonjwa katika hospitali zilizojengwa hivi karibuni hasa katika Wilaya mpya ikwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetoa shilingi bilioni 34 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali 67 za Halmashauri zilizoanza kujengwa katika mwaka wa fedha 2018/2019. Fedha hizo zimepelekwa Bohari Kuu ya Dawa na utaratibu za kupeleka vifaa tiba katika Hospitali 67 zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali mpya ya Halmashauri.

Aidha, mwezi Mei, 2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ambapo majengo mapya matano yamejengwa na yameyakamilika. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali na shilingi milioni 487 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe. Ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, ni lini mradi wa ujenzi wa soko la kisasa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime wenye thamani ya shilingi bilioni 8.07 utakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime ilikidhi vigezo vya kupatiwa Shilingi bilioni 8.07 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa kupitia utaratibu wa Miradi ya Kimkakati mwezi Februari, 2019. Kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi ya kimakatati Serikali ilisitisha baadhi ya miradi ya kimkakati iliyoidhinishwa ukiwemo mradi wa ujenzi wa soko la kisasa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime. Hata hivyo, Serikali imetoa kibali kwa Halmashauri ya Mji Tarime kuendelea na ujenzi wa Soko na katika mwaka wa fedha 2021/2022, shilingi bilioni tatu zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa soko katika Mji wa Tarime.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji Tarime inatarajia kutangaza kazi ya ujenzi wa soko la kisasa mwezi Julai, 2021 na ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi Agosti, 2021 baada ya kumpata mkandarasi. Halmashauri imejipanga kukamilisha mradi huo ndani ya miezi 12 tangu tarehe ya kusaini mkataba.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itasaidia na kufanikisha kutoa namba kwa Vijiji vya Chipunda Kata ya Namatutwe, Mkalinga Kata ya Chikunja na Sululu ya Leo Kata ya Namatutwe vyenye Wakazi zaidi ya elfu kumi katika Jimbo la Ndanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, namba za usajili wa vijiji hutolewa kupitia Hati za Usajili wa Vijiji kwa kuzingatia matakwa ya Kifungu cha 22 na 26 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287. Aidha, Vijiji hivyo hupaswa kuwa vimetangazwa kupitia Gazeti la Serikali kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287.

Mheshimiwa Naibu Spika, Chipunda na Mkalinga ni Vitongoji katika Kijiji cha Namatutwe na Napata na Sululu ya Leo ni eneo ndani ya Kitongoji cha Maleta katika Kijiji cha Namatutwe, Kata ya Namatutwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, hivyo maeneo hayo hayatambuliki kama Vijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wakazi wa maeneo hayo wameonesha uhitaji wa kuanzisha Vijiji ni vema wakaanzisha kusudio la kuyafanya maeneo hayo kuwa vijiji kwa kuzingatia sheria pamoja na Mwongozo wa Uanzishaji Maeneo ya Utawala wa Mwaka 2014 kupitia mikutano na vikao kwenye ngazi ya vijiji, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya, Kamati ya Ushauri ya Mkoa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI. Ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA K.n.y. MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka Watumishi pamoja na vitendea kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi, mwezi Julai, 2021, Serikali ilipeleka watumishi 28 wakiwemo watumishi 19 wa Sekta ya Afya na watumishi tisa wa Sekta ya Elimu. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022, imepanga kuajiri jumla ya watumishi 477 ili kupunguza changamoto ya upungufu wa watumishi. Pamoja na jitihada hizo, Serikali itaendelea kufanya msawazo wa watumishi katika Halmashauri zote ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kwa kadri ya mahitaji.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vitendea kazi, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imetenga na kuidhinishiwa bajeti ya shilingi milioni 705.85 kwa ajili ya ununuzi wa vitendea kazi ikiwemo samani za ofisi pamoja na magari manne kwa gharama ya shilingi milioni 430.00. Mpaka sasa, Halmashauri ipo katika hatua za mwisho za ununuzi wa magari mawili ya awali kwa gharama ya shilingi milioni 220.00 yatakayosaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa magari. Kwa ujumla, Serikali itaendelea kununua vitendea kazi kwa ajili ya halmashauri hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante sana.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka Gari la Wagonjwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Jimbo la Kilindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali kupitia fedha za Mkopo wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) imetenga shilingi bilioni 46.94 kwa ajili ya ununuzi wa magari ya wagonjwa 253, ambapo magari 195 yenye thamani ya shilingi bilioni 35.1 yatanunuliwa kwa ajili ya halmashauri zote 184, ambapo kupitia magari hayo Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi itapatiwa gari moja la wagonjwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Jengo la Wodi za kulaza Wagonjwa pamoja na kupeleka mashine ya X-ray katika Kituo cha Afya Itobo kilichopo Jimbo la Bukene?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Jimbo la Bukene, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imepeleka shilingi milioni 250 katika Kata ya Itobo kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kituo hicho ili kiweze kuwa na uwezo wa kutoa huduma za upasuaji. Ujenzi wa majengo hayo umeanza na unatarajiwa kukamilika ifikapo 30 Aprili, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa vituo hivi vya afya unafanyika kwa awamu. Hivyo, baada ya awamu hii ya kwanza ya ujenzi kukamilika, Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo mengine ikiwemo wodi katika Kituo cha Afya cha Itobo. Aidha, mashine za X-ray zitaendelea kununuliwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. MRISHO S. GAMBO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wanapata malipo kama Madiwani na Wabunge kutokana na majukumu mazito wanayoyafanya ikiwemo ufuatiliaji wa malipo ya Kodi ya Majengo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kwa kuwa ndio wasimamizi wakuu wa shughuli zote za maendeleo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ngazi ya Vijiji na Mitaa za Mwaka 2014 chini ya Tangazo la Serikali Na. 322, miongoni mwa sifa zinazomwezesha mkazi wa Kijiji, Mtaa au Kitongoji kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti ni pamoja na kuwa na shughuli halali inayomwingizia kipato.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa mwongozo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu malipo ya posho ya viongozi hawa kwa kutumia mapato ya ndani kadri ya uwezo wa Halmashauri. Kwa ujumla, uwezo wa Halmashauri zilizo nyingi bado ni mdogo katika kutekeleza jukumu hili. Hivyo, Serikali imeichukua changamoto hii na itaendelea kufanya tathmini. Ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Zahanati na Vituo vya Afya katika Wilaya ya Kakonko?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati na Vituo vya vya Afya vya kimkakati nchini, ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni 38.15 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati 758 kote nchini. Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko imetengewa shilingi milioni 150 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati tatu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetoa fedha za makato ya tozo za miamala ya simu shilingi bilioni 55.25 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 221 kwenye Tarafa zisizo na Vituo vya Afya vyenye uwezo wa kutoa huduma ya upasuaji, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko imepokea shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika Tarafa ya Nyaronga kata ya Gwalama.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuendelea kujenga zahanati na vituo vya afya katika Wilaya ya Kakonko na nchini kote katika maeneo ya kimkakati kulingana na vigezo vilivyowekwa badala ya kila Kijiji na kila Kata. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro uliopo mpakani mwa Wilaya ya Kishapu Kata ya Mwamalasa Kijiji cha Magalata na Wilaya ya Iramba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Jimbo la Kishapu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa, upo mgogoro wa mipaka kati ya Wilaya ya Kishapu na Wilaya ya Iramba. Mgogoro huo upo katika eneo la Bonde la Mto Manonga katika Kijiji cha Magalata Wilaya ya Kishapu na Kijiji cha Mwasangata Wilaya ya Iramba.

Mheshimiwa Spika, Mgogoro huu unatokana na malisho ya mifugo na maji, ambapo kwa upande wa Wilaya ya Kishapu jamii ya wafugaji wanaoishi kijiji cha Magalata hutumia bonde la Mto Manonga kwa ajili ya malisho na maji na upande wa Wilaya ya Iramba jamii ya wafugaji wanaoishi kijiji cha Masangata hutumia pia bonde la mto Manonga kwa ajili ya malisho na maji. Mgogoro huu mara nyingi hutokea wakati wa kiangazi ambapo jamii za pande zote mbili hutafuta malisho na maji kwa ajili ya mifugo ambayo hupatikana kwa wingi katika Bonde hilo.

Mheshimiwa Spika, vikao mbalimbali vya usuluhishi vimefanyika vikihusisha viongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Uongozi wa Mikoa, Wilaya na Wananchi wa Vijiji vinavyohusika. Aidha, vikao hivyo vimesaidia kurejesha amani, utulivu na usalama kati ya vijiji hivyo hususan Magalata na Mwasangata.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na jitihada za kuutatua mgogoro huu kwa njia shirikishi ili kudumisha amani na utulivu katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Zahanati ya Ihalula kuwa Kituo cha Afya baada ya kukidhi vigezo vyote kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali iliipandisha hadhi zahanati ya Ihalula kuwa Kituo cha Afya mwaka 2018/2019 na kupewa namba ya utambulisho 101604-7. Aidha, Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 ilipeleka Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ukarabati wa majengo mengine likiwemo jengo la upasuaji ambalo sasa linatoa huduma.

Mheshimiwa Spika, Kituo hiki kimekuwa kikilipwa fedha za Mfuko wa Bima ya afya kama zahanati kutokana na baadhi ya taratibu ambazo zilikuwa hazijakamilika.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zimekwishalifanyia kazi na barua rasmi itapelekwa ndani ya mwezi huu. Ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuziwajibisha halmashauri nchini ambazo zinajiweza kimapato lakini hazipeleki asilimia 40 ya mapato ya ndani kwenye shughuli za maendeleo kama zinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria na badala yake zimekuwa zikiwalazimisha wananchi wake wachangie?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwongozo wa Uandaaji wa Bajeti unaotolewa kila mwaka na Serikali unatoa maelekezo kwa halmashauri zote nchini kutenga sehemu ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Halmashauri zenye mapato yasiyolindwa chini ya shilingi bilioni tano zinapaswa kutenga asilimia 40 ya mapato ya ndani na Halmashauri zenye mapato yasiyolindwa zaidi ya shilingi bilioni tano zinapaswa kutenga asilimia 60 ya mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 kiasi cha fedha shilingi bilioni 216.4 kimetumika kwenye shughuli za maendeleo sawa na asilimia 70.87 ya fedha zilizopaswa kutumika kwenye miradi ya Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021 kiasi cha shilingi bilioni 279.7 kimetumika kwenye miradi ya maendeleo sawa na asilimia 92 ya fedha zilizopaswa kupelekwa kwenye miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekwisha wachukulia hatua watumishi 63 wakiwemo Wakurugenzi na Wakuu wa Idara, kwa kushindwa kutekeleza maagizo haya na utaratibu huu ni endelevu.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa rai kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha Maelekezo haya yanatekelezwa kwa ufanisi. Ahsante.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza agizo la Rais wa Awamu ya Tatu la kuitambua Kizengi kuwa Tarafa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Protas Venant, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala hufanyika kwa mujibu wa mwongozo wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala wa mwaka 2004.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwongozo huu unaelekeza maombi ya kuanzisha maeneo hayo kujadiliwa na kupitishwa kwenye vikao vya kisheria ngazi za Vijiji, Kata (WDC), Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC) kisha kuwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI haijapokea maombi ya Kizengi kuwa Tarafa. Hivyo, naishauri Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kufuata mwongozo uliotolewa na kuwasilisha maombi hayo Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya tathmini na kufanya maamuzi kwa kadri ya taratibu. Ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mhe. Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2018 ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilombero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa Hospitali za Halmashauri nchini kote. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali 102 na kuanza ujenzi wa hospitali mpya kwenye halmashauri 28 zikiwemo hospitali zilizoahidiwa na viongozi wa kitaifa.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Ifakara ni miongoni mwa halmashauri 28 zisizo na Hospitali za Halmashauri, ambayo imetengewa fedha shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo matatu ya awali. Ahsante.