Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Alfred James Kimea (4 total)

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya maji ya Busanda inafanana kabisa na changamoto ya maji iliyoko Korogwe Mjini. Nimekuwa nikifuatilia kwa Mheshimiwa Waziri na ameniahidi tatizo la Korogwe litatatuliwa na mradi wa miji 28 ambao Korogwe ni sehemu ya mradi huo.

Je, Serikali inawaahidi vipi wananchi wa Korogwe kwamba lini mradi huu utatekelezwa ili kuweza kutatua changamoto ya maji ambayo inawakabili wananchi wa Korogwe Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred Kimea, Mbunge wa Korogwe Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa ni mfuatiliaji mzuri na nimeshaweza kuongea naye mara kadhaa na kumhakikishia eneo lake kupata maji na uzuri Korogwe Mjini ipo ndani ya ile miji 28 ambayo fedha tayari zipo na muendelezo wa maandalizi unaendelea na hivi karibuni kuanzia mwezi Aprili miji ile 28 shughuli za kupeleka maji zinakwenda kuanza mara moja.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri na Naibu Waziri, pia tunashukuru kwa ajili ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya matengenezo madogomadogo lakini matengenezo haya madogomadogo hayakidhi haja ya barabara hii kwani wakati wa mvua inaharibika kabisa na tunakosa mawasiliano kati ya mji mmoja hadi mwingine. Je, Serikali haioni kuna haja ya kutupa commitment ni wakati gani barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami ili tutatue changamoto hii kabisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara zote za changarawe ama za udongo na hasa maeneo ya mwinuko inaponyesha mvua huwa zinakuwa na changamoto ya kuondoka udongo ama changarawe. Commitment ya Serikali pamoja kutekeleza ahadi ya Rais na Waziri Mkuu tayari Serikali inatafuta fedha ili tuweze kufanya usanifu wa kina ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, Serikali inatafuta fedha na fedha ikipatikana barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona nami niulize swali dogo la nyongeza. Napenda kuipongeza Serikali kwani ndani ya Kata zangu zote 11 kwenye Jimbo la Korogwe Mjini umeme umefika, lakini changamoto ni kwamba ndani ya Kata hizo ipo Mitaa mingi ambayo umeme haujafika kabisa. Je, Serikali inawaahidi nini wananchi wa Korogwe katika kutatua changamoto hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kimea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, TANESCO inapeleka umeme katika maeneo mbalimbali kwa program za kila siku za kawaida, kwenye Mitaa, Vijiji na Vitongoji. Pia zipo program nyingine ambazo zinapeleka umeme kwenye Mitaa na Vijiji vyetu ikiwemo REA yenyewe, densification na peri-urban.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mheshimiwa Dkt. Alfred ambapo tayari Kata zake zote na vijiji vyake vyote vina umeme, yale maeneo machache ambayo hayana umeme, mradi wetu wa densification utapelekea umeme katika maeneo hayo kuanzia mwezi Saba. Pia tunavyo Vitongoji na Mitaa takribani kama 3,000 ambavyo vitapelekewa umeme, kwa hiyo, Vitongoji vyake na Mitaa yake Mheshimiwa Mbunge pia ni sehemu ya maeneo hayo yatakayopelekewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pale ambao densification tu itaanza mwezi wa Saba, Mheshimiwa ataweza kupata umeme katika eneo lake kwa sababu amekuwa akifuatilia sana ofisini kwetu na ni mfuataliaji mzuri wa maendeleo ya wananchi. Kwa hiyo, nawapongeza wananchi kwa kupata Mbunge mfuatiliaji kama wa aina yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Spika, Nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tuna Barabara yetu ya Korogwe Mjini ambayo inatokea Old Korogwe, Kwamndolwa, Magoma, Mashewa, Bombo Mtoni mpaka Mabokweni, ambayo ni ahadi ya Marehemu Rais Magufuli, Mama Samia na Waziri Mkuu. Je, ni lini Serikali itatekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kutimiza ahadi ya viongozi wetu wa kitaifa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara alizozitaja Mheshimiwa Mbunge wa Korogwe zipo kwenye ahadi ya Rais na zipo kwenye Ilani na ni kati ya barabara ambazo zinakamilisha kilomita 6,006 ambazo zimeahidiwa kujengwa katika kipindi hiki cha miaka mitano. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kadri fedha itakapopatikana barabara hizi ikiwemo na hii zitajengwa kwa awamu. Ahsante.