Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Alfred James Kimea (1 total)

MHE. ALFRED J. KIMEA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Old Korogwe kwenda Kwamndolwa - Magoma - Mashewa - Bombomtoni - Maramba hadi Mabokweni yenye urefu wa kilomita 127.54 kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri Mkuu kwa wananchi wa Korogwe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Old Korogwe – Kwamndolwa – Magoma – Mashewa – Bongomtoni – Maramba hadi Mabokweni yenye urefu wa kilometa 127.69 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi kwa wananchi wanaoishi maeneo inayopita barabara kama ilivyotajwa hapo juu. Ili kuweza kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 1,450.78 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali.