Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe (32 total)

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru japo sijaridhishwa hata kidogo na majibu ya Serikali kwa sababu malalamiko ya wananchi kwenye vyama hivi ni makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize swali la kwanza la nyongeza; kwa kuwa kumekuwa na malalamiko makubwa ya ubadhirifu wa Vyama hivi vya Ushirika, Bodi hizi kuwa wababe, kutoshirikisha wananchi, lakini pia mashamba haya kukodishwa pasipo tija kwa wananchi. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa wa kuunda Tume Maalum itakayoshirikisha vyombo vyote vya dola kwenda kufanya uhakiki wa mashamba haya yote 17?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa tunaona Sheria ya Ushirika ya mwaka 2013 haitoi fursa kwa viongozi wa ngazi ya mkoa kushuka chini kuweza kuona kinachoendelea kwenye vyama hivi vya ushirika. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka wa kufanya mabadiliko ya sheria, ili sasa viongozi wa ngazi ya mkoa waweze kushiriki na kuona nini kinaendelea kwenye vyama hivi vya ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saashisha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna changamoto za baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Ushirika kuhusishwa na ubadhirifu na Serikali imekuwa ikichukua hatua mara kwa mara. Tumeona hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali katika Vyama vya Ushirika vya Tumbaku, tumeona hatua ambazo Serikali imechukua katika Vyama vya Ushirika vya Pamba, tumeona hatua ambayo Serikali imechukua katika Vyama vya Ushirika vya Mkonge.Hatua hizi zote zimechukuliwa na Serikali kuhakikisha kwamba kwanza mali zilizoibiwa za vyama vya ushirika zinarudishwa kwa wanachama, lakini mbili kuwachukulia hatua viongozi wote waliohusika na kuwapeleka katika vyombo vya sheria.

Suala ambalo analisema la uwepo wa Tume, ipo Timu Maalum chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inafanyakazi hii na imekuwa ikiendelea kufanyakazi hii katika maeneo yote yanayohusu vyama vya ushirika na kama kuna specific case inayohusu Wilaya ya Hai namkaribisha Mheshimiwa Mbunge aje atueleze Wizarani na tutashirikiana naye kuhakikisha kwamba ubadhirifu kama upo katika maeneo ya Hai ya Vyama vya Ushirika vya Wilaya ya Hai, au Mkoa wa Kilimanjaro tutaweza kuchukua hatua kama ambavyo tumechukua hatua katika masuala yanayohusu mali za KNCU.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mabadiliko ya sheria kwanza ni vizuri Waheshimiwa Wabunge tukaelewa dhana ya ushirika ni dhana ya hiyari. Ushirika siyo mali ya Serikali ni mali ya washirika, lakini Serikali inaingilia kwenye masuala ya ushirika kwasababu ya public interest kwasababu ile inakuwa ni mali ya umma ndiyo maana tunayo Tume ya Ushirika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la upungufu wa kisheria Wizara ya Kilimo sasa hivi inaipitia sheria na mwaka jana ilikuwa tuilete ndani ya Bunge ili kuweza kuihuisha iweze kuendana na mahitaji ya sasa, badala ya kuwa ushirika wa huduma uwe ushirika wa kibiashara kwa maslahi ya wanaushirika. Kwahiyo suala la kisheria tunaliangalia na ni suala genuine ambalo Mheshimiwa Mbunge amelisema na muda ukifika tutaileta sheria ndani ya Bunge ili iweze kwenda na wakati, lakini siyo kuifanya Serikali i-control ushirika bali tunatengeneza sheria kuufanya ushirika ujiendeshe wenyewe kwa maslahi ya washirika na kutengeneza governing bodies ambazo zitausimamia ushirika kwa maslahi ya wanaushirika.
MHE. SAASISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, majibu ambayo kimsingi yatapunguza maumivu makubwa waliyopata wananchi wa Hai tarehe mbili kutokana na majibu ya swali lao kuhusu suala la ushirika. Niwaambie wananchi wa Hai watulie Serikali yao inawapenda sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niulize swali la nyongeza la kwanza; kwa kuwa hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na kwa kuwa wananchi wa Hai tarehe 28 walifanya jambo lao kwa asilimia kubwa sana na kuleta utulivu humu Bungeni na huko nje; je, ni lini sasa Serikali itatekeleza kwa kiwango angalau cha asilimia 50 ya ahadi ya Mheshimiwa Rais?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, ni lini Serikali italipa madeni ya watumishi wa afya na Walimu ambao ni wastaafu, deni ambalo mimi mwenyewe nimeshaliwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri la milioni 171 ili watumishi wa afya waendelee kufanya kazi yao kwa uaminifu? Ikizingatiwa miongoni...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa umeshauliza swali.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saasisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi ya kuajiri watumishi wa afya japo kwa asilimia 50. Bunge lako Tukufu na Wabunge wote humu ni mashuhuda wa jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali katika kujenga Hospitali za Wilaya, kuongeza vituo vya afya na zahanati. Hivyo basi, pale ambapo bajeti itaruhusu, tutaendelea kuajiri watumishi katika Idara ya Afya; na hawa 75 wanaokwenda Hai, ni sawa na asilimia 18.6 ya watumishi wote ambao wameajiriwa hivi sasa. Kwa hiyo, kadri uwezo utakavyoruhusu, tutaendelea kuleta watumishi katika Wilaya ya Hai.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili juu ya madeni ya watumishi, Mheshimiwa Mbunge kwanza amekuwa mstari wa mbele kupigania haki za hawa watumishi na ili jambo amenieleza mimi mwenyewe zaidi ya mara mbili. Tayari tunashughulikia, ukiacha deni ambalo alikuwa analizungumzia la shilingi milioni 171, tayari yalikuja maombi 137 katika Ofisi ya Rais Utumishi yenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 246 ili yaweze kushughulikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa madeni yaliyolipwa ni Sh.50,690,000/= na madeni yenye thamani ya shilingi milioni 148 ambayo ni sawa na watu 88, yamerudishwa kwa mwajiri ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hai kwa sababu yalikuwa na dosari mbalimbali. Pale ambapo Mkurugenzi wa Hai atarekebisha dosari zile na kuzileta katika Ofisi ya Rais Utumishi, basi nasi tutazifanyia uhakiki tuweze kulipa madeni hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna madeni ya watu 27, sawa na shilingi milioni 33 na kitu hivi, tayari yameshafanyiwa uhakiki na yametolewa katika Ofisi ya Rais, Utumishi na sasa yapo Wizara ya Fedha, tayari kwa malipo muda wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nilikuwa naomba kuuliza; je, Serikali ina mpango gani ya kufufua Kiwanda cha Machine Tools, kiwanda ambacho kinatengeneza vipuri kwa ajili ya viwanda vingine na pia vinatengeneza na kuunda mashine za kusaidia viwanda vingine vidogo na vikubwa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo mnajua, Serikali sasa ina mpango wa kuendeleza uchumi wa viwanda. Kiwanda cha (Kilimanjaro Machine Tools – KMTC) ni moja ya viwanda muhimu sana kwa maana ya basic industries katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaamua kufufua kiwanda hicho. Katika bajeti ya mwaka huu tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kujenga kinu cha kuyeyushia chuma (foundry).

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Saasisha Mafuwe kwamba kiwanda hicho sasa kinaenda kufanya kazi kwa sababu tutakuwa na uwezo wa kuyeyusha chuma na kuzalisha vipuri ambavyo vinahitajika katika viwanda vingine kwa ajili ya maendeleo ya Sekta ya Viwanda hapa nchini. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Hai. Mgogoro huu umekuwa wa muda mrefu sana, jambo linalosababisha wananchi kukosa maeneo ya malisho na kuishi kwa wasiwasi kwenye maeneo yao ambayo wanaishi pale tangu mwaka 1975. Wananchi wote wa vijiji hivi vyote vinne vinavyotajwa, wana usajili wa vijiji vyao, nikimaanisha Kijiji cha Sanya station, Tindigani, Mtakuja na Chemka.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ukizingatia eneo lililopo kwenye uwanja huo ni kubwa sana; kwenye list ya Viwanja vya Ndege tulivyonavyo hapa Tanzania, Kiwanja cha Kilimanjaro Airport kinaongoza kikifuatiwa na Kiwanja cha Dodoma na Songwe, halafu kiwanja cha nne ni Dar es Salaam.

Je, Serikali haioni kwa ukubwa ulioko pale, iko haja ya baadhi ya maeneo yarudi kwa wananchi ili waweze kuendelea na maeneo yanayobaki, yabaki kwenye Uwanja huu wa Ndege jambo ambalo tayari mimi mwenyewe nilishakutana na Management na wakaonyesha utayari wa kukubaliana na jambo hili?

Swali la pili: Je, Kwa kuwa mgogoro huu umekuwa wa muda mrefu, Serikali haioni iko haja sasa wa kufikia mwisho na Mheshimiwa Naibu Waziri sasa tuambatane tukakae na wananchi wale tumalize mgogoro huu ili kesi hii iishe na wananchi waendelee na maisha yao; na kwa kuzingatia kwamba wananchi hawa ni wema sana, walitupa kura nyingi za Chama cha Mapinduzi na pia Diwani aliyeko pale alipita bila kupingwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mgogoro huu umekuwa ni wa muda mrefu na hapo nyuma kulikuwa kuna changamoto kwamba vijiji vilipima maeneo yao yakaingia katikati ya uwanja ambao tayari ulikuwa una hati. Changamoto hiyo tayari tulishairekebisha na zile ramani za vijiji vile zilifutwa ili ramani ya uwanja wa ndege ibaki na ndivyo ilivyo.

Mheshimiwa Spika, sasa ni kweli kwamba uwanja ule ni mkubwa lakini uwanja ule ulitolewa vile na muasisi wa Taifa baba yetu Julius Kambarage Nyerere na kile kiwanja kina mipango mahsusi ya kuweka viwanda vya kitalii na viwanda vinavyohusiana na viwanja vya ndege. Biashara zote za viwanda vya ndege, sasa hivi pale kuna mpango wa kuanzisha aviation school ambapo Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kimekwishajidhatiti na vile vile tuna mpango na hawa watu wa TAA ili kuweka majengo ya kuhifadhi mipango ambayo imepangwa pale. Kwa hiyo ningependa kumshauri Mheshimiwa Mbunge pamoja na wale wananchi wa Hai wajipange kuanzisha biashara zinazohusiana na viwanja vya ndege kuliko kupanga kuugawa uwanja wa ndege ule kwenda katika vijiji.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kweli kwamba Wizara yangu iko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda pale kuongea na kumaliza suala hilo kwani tumejipanga mwaka huu tuweze kufika pale kufanya tathmini na kumaliza suala hilo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba Serikali inisaidie kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na ikasababisha mafuriko makubwa ndani ya Jimbo la Hai na kuharibu skimu nyingi sana zilizoko ndani ya Jimbo la Hai, ikiongozwa na skimu kubwa iliyojengwa na fedha nyingi za Serikali inaitwa Skimu ya Kikafu Chini pamoja na Skimu ya Johari, Mwasha na skimu nyingine ndani ya kata tisa zote zimeharibika pamoja na mifereji. Je, ni lini sasa Serikali itafanya ukarabati wa skimu hizi ikizingatiwa ni kipindi cha kilimo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Saashisha is very committed na kazi kubwa anayofanya kwa ajili ya wananchi wake inaonekana. Jana tumekuwa naye pamoja na Mbunge wa Moshi Vijijini kwa ajili ya kuongelea madhara waliyoyapata wananchi na wakiomba msaada wa chakula na niji-commit kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo tunaifanyia kazi issue ya chakula na maafa waliyopata wananchi hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu skimu hizi, hivi tunavyoongea sasa hivi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Prof. Tumbo, yuko Mkoa wa Kilimanjaro, Wilaya ya Hai na maeneo yote yaliyoathirika pamoja na Moshi Vijijini, wakifanya tathmini ya athari ya mafuriko hayo ili tuwe na comprehensive plan. Hatuwezi kusema lini kabla ya technical team yetu kurudi na taarifa ya kuweza kuifanyia kazi lakini tuwaahidi tunaifanyia kazi.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante. Naomba sasa kwa kuwa bei ya kahawa kwenye soko la dunia kwa kilo moja inaenda takribani shilingi 9,660 lakini mkulima ambaye anakwenda kuuza kahawa yake kupitia Vyama vya Ushirika kilo moja ananunua kwa shilingi 2,000 bila bakaa.

Je, Serikali haioni iko haja ya kutoa au kuondosha au kupunguza tozo zinazotokana na zao la kahawa ili mwananchi yule ambaye ni mkulima aweze kunufanika na bei hii ya kahawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini swali la pili, kwa kuwa sasa wananchi wa Jimbo la Hai wako tayari kulima kahawa. Je, Serikali ipo tayari kusambaza pembejeo kwa bei ambayo ni Rafiki kwa wakulima? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ni kweli leo katika soko la dunia kwa bei ya mpaka jana wastani wa Arabica ilikuwa ni Dola 3 wakati wastani wa Robusta ilikuwa Dola 1.5. Na sisi kama wizara na Serikali tumeanza kupitia mjengeko wa bei ambao unahusisha tozo mbalimbali na leo mimi binafsi nitaongoza kikao kitakachohusisha Vyama vya Ushirika hasa vya Mkoa wa Kagera ndio tunaanza navyo. Kwa hiyo, hili la kwamba kuangalia suala la tozo wanazotozwa wakulima katika bei tutalipitia ili wakulima waweze ku-benefits na bei na zao lao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu pembejeo, Serikali sasa hivi inachukua hatua njia pekee ya kuwasaidia wakulima wadogo wadogo ni kupitia ushirika. Tumefanya majaribio katika sekta ya pamba tumeona wakulima wamepata pembejeo za kutosha katika msimu uliopita kupitia Vyama vya Ushirika. Tumefanya majaribio katika tumbaku, wakulima wamepunguza gharama za pembejeo kwa zaidi ya asilimia 40 kwasababu zinanunuliwa in bulk badala ya mkulima mmoja mmoja kwenda sokoni kununua. Kwa hiyo tunajenga Vyama vya Ushirika na nimuahidi Mheshimiwa Mbunge na niwaahidi Waheshimiwa Wabunge wote kwamba tutaangalia njia bora ya wakulima wa zao la Kahawai li Ushirika wao uweze kuwa imara waweze kupata pembejeo katika mfumo wa bulk na waweze kuzinunua kwa bei competitive ya soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakiri mkulima mmoja mmoja kwenda dukani kununua pembejeo moja moja gharama yake inakuwa ni kubwa na wengi wanashindwa kuhudumia mazao. Kwa hiyo, tupokee wazo la Mheshimiwa Mbunge tutatafuta mechanism sahihi ya kuwahudumia wakuliwa wa Kilimanjaro kupitia ushirika wao waweze kununua pembejeo kwa pamoja na hiyo itawapunguzia gharama.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; nilikuwa naomba kuuliza ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa Mradi wa Maji ya Kikafu ambao unalenga kuhudumia Kata ya Masama Kusini, Muungano, Bomang’ombe na KIA? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Hai, kiukweli amekuwa mfuatiliaji mkubwa sana, ni mradi ambao amekuwa akiupigia kelele.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa tumekwishatoa kibali na tumetoa maelekezo kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira - MUWSA, Moshi kuhakikisha kwamba anatangaza kazi hiyo na mkandarasi apatikane mara moja kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize Hospitali ya Wilaya ya Hai imekuwa na changamoto kubwa sana ya majengo mpaka ninivyozungumza hatuna jengo la mama na mtoto, hatuna jengo la pharmacy, hatuja jengo la maabara kakini pia work way za kuwasiliana kwenye majengo haya hatuna.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutujengea majengo haya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze kaka yangu Saashisha Mafuwe kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwenye Wilaya ya Hai hasa kwenye kufuatilia miundombinu tu sio tu ya Hospitali ya Wilaya, lakini zahanati zake lakini vituo vya afya na Hospitali ya Machame ambayo ni DDH, ni ya kanisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kuna kazi kubwa sana inafanywa na Waziri wa Afya Mheshimiwa Dorothy Gwajima pamoja na Waziri wa TAMISEMI dada yetu Ummy Mwalimu ya kuhakikisha tunapata resources kupita sources zingine ili tuweze kukamilisha miradi kama hiyo ambayo anaisema ambayo inawezekana haijaingia kwenye bajeti kubwa ambayo sasa tumeipitisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Saashisha tukitoka hapa twende pamoja, tuangalie mkakati huo wa Mawaziri wetu wawili tuone ni namna gani inaweza kufanyika kupitia Global Fund, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kipande cha barabara ya Mashua – Jiweni ni kipande muhimu sana kwa sababu kinahudumia Kata tatu; Kata za Masama Kusini, Romu na Masama Magharibi lakini Vijiji vikubwa vya Lukani, Kiu, Lwasaa na Jiweni. Barabara hii kwa sasa haipitiki, je, Serikali haioni ipo haja ya kupeleka fedha za dharura ili barabara hii ambayo inatuletea mazao huku Dodoma, iweze kupitika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tangia tumepata Uhuru, Jimbo la Hai hatujawahi kupata taa za barabarani, ni lini sasa Serikali itatuletea taa za barabarani kwenye Mji mkubwa unaokua wa Boma Ng’ombe, Maili Sita na Njia Panda ya kwenda Machame? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Jimbo la Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza hapa kwamba barabara ya Mashua mpaka Jiweni ambayo inahudumia Kata kubwa tatu haipitiki na ameomba fedha za dharura. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge tumelipokea ombi lake na tutakachokifanya sasa hivi tutatuma wataalam wakafanye tathmini na baada ya hapo tutatafuta fedha ili barabara hiyo iweze kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni lini sasa Serikali itapeleka taa za barabarani katika Miji Mikubwa ya Boma Ng’ombe, Njia Sita pamoja na Kata nyingine ambazo ameanisha hapa. Niseme tu najua jitihada kubwa za Mheshimiwa Mbunge kwa Jimbo la Hai na najua ana dhamira ya kweli ya kuwasaidia wananchi wake, kwa sababu ameleta ombi hili niseme na lenyewe tunalipokea kwa ajili ya kulifanyia kazi. Naamini kabisa kwa ufuatiliaji wake mzuri na fedha ikipatikana basi taa zitaletwa na Serikali kwa wakati kulingana na bajeti itakavyopatikana. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo nami nilikuwa nauliza kuhusu vanilla, amenijibu vizuri mno na kutambua Wilaya yetu inalima zao hili.

Serikali kwa kuwa sasa imeona zao hili ambalo lina bei nzuri sana sokoni, mwanzoni ilikuwa ni 120,000 sasa hivi limeshuka kwa sababu ya kukosa watu wa kuwaunganisha, kilo inauzwa 20,000.

Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha inatuletea wataalam sambamba na hili ambalo ametuambia la kutafutia masoko? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Bunge lako Tukufu hili mlitupitishia ongezeko la bajeti ya Wizara ya Kilimo kwenye utafiti zaidi ya asilimia 90. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge moja ya eneo ambalo tunaenda kuwekeza sana ni kwenye utafiti na training ya Wataalam hasa wanaoshiriki katika shughuli za uzalishaji kwa maana ya Wagani.

Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba, mwaka huu tunaanza program ya training na Waziri wa kilimo wiki iliyopita amezindua training ya kwanza katika Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma na zoezi hili linaendelea nchi nzima tutakuwa tuna-train kutokana na ikolojia na mazao husika ya eneo husika ya eneo husika ili kuwafanya wataalam waweze kufanana na mazao yaliyoko eneo hilo. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza naipongeza Serikali kwa nia hiyo njema ya kutamani kuboresha stahiki za watumishi, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa sasa tathmini imeshafanyika tangu mwaka 2015/2017 ya kufanya marekebisho ya muundo na mishahara ya watumishi: Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza jambo hili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa sana wa mafao ya watumishi wanapostahili: Ni nini kauli thabiti ya Serikali kuwahakikishia watumishi wanapostahili watapata stahiki zao/mafao yao kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe Mbunge wa Hai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nitoe pongezi zangu kwa Mbunge wa Hai, Mheshimiwa Saashisha kwa kuwa anafuatilia sana masuala ya kiutumishi hasa yale ya watumishi katika jimbo lake na yale ambayo yanahusu wastaafu wanaotoka katika Wilaya ile ya Hai na jimboni kwake.

Mheshimiwa Spika, sasa nikienda kwenye kujibu swali lake la kwanza, Serikali tayari ilishaanza mpango wa kuweza kufanyia kazi ile tathmini iliyofanyika 2015/2017. Tayari kuna kada ambazo zilishafanyiwa kazi ambapo kwa zoezi lililofanyika mwaka 2015, kada ya Wahasibu, Internal Auditors na hawa washika fedha; kada hizo zilikuwa zinatofautiana sana katika ngazi ya mshahara, lakini ukiangalia elimu wanayosoma, ilikuwa ni moja. Kwa hiyo, tayari Serikali imeanza kufanyia mpango huo.

Mheshimiwa Spika, vile vile mwaka 2017 ilifanyika tathmini ya Watumishi wa Umma wote, kuangalia ulinganifu ikiwemo kwenye ma-engneer ukiangalia katika wanasheria na kadhalika. Sasa katika utekelezaji kama unavyofahamu Serikali itatekeleza pale tu kwa uwezo wa kibajeti katika kulipa mishahara. Kama tunavyoona jitihada zinazofanyika na Serikali za kuboresha uchumi wetu chini wa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, uchumi wetu ukiboreka, basi tutafanyia kazi na kuboresha maslahi ya watumishi wetu.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, Watumishi wa Umma inatakiwa inapofika mienzi sita kabla ya kustaafu, tayari waanze na kujiandaa na nyaraka mbalimbali. Sasa changamoto imekuwa ikijitokeza unakuta mtu ajira yake ya kwanza alianzia Halmashauri ya Kongwa, lakini anapokuja kustaafu, anastaafia Ukerewe, tatizo linakuwa kwenye documentation. Halafu mtu anakuja kukumbushwa suala hili la Maafisa Utumishi limebaki mwezi mmoja, anapoanza kufuatilia barua yake ya ajira, iko Kongwa. Sijui alipata uhamisho kwenda Songea; akatoka akaenda kustaafia Ukerewe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utakuta changamoto kwenye documentation na mtu huyu hana nauli, ndiyo maana mafao yanachelewa, lakini tayari tumeanzisha mfumo wa HCMIS ambao utahakikisha taarifa zote za mtumishi zipo na zinaanza kutoa notification walau miezi sita kabla.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali tunafanyia kazi mfumo huu, nawaasa Maafisa Utumishi wote nchi nzima kuhakikisha wanaangalia records za watumishi wao wanaokaribia kustaafu wawape taarifa walau mienzi sita kabla, ili isije ikafika nauli imekwisha, anakaribia kustaafu kesho, ndiyo anakumbushwa aanze kutafuta taarifa zake. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana, Wilaya ya Hai inawafugaji wengi sana wa ng’ombe wa kisasa, ng’ombe walionenepeshwa lakini pia ng’ombe wale wa kienyeji pia tuna Uwanja wa Ndege wa Kimataifa na tuko tayari kufanya biashara ya Kimataifa ya kuuza nyama.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza machinjio ya kisasa katika eneo la KIA ili na sisi tuweze kufungua milango ya kibiashara ya kuuza nyama?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mafuwe Mbunge wa Hai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wafugaji wa Hai ni wafugaji wa ng’ombe wa kisasa wanafuga katika utaratibu ule wa zero grazing, ni katika maeneo yanayofuga vizuri sana na viwanda vidogo vidogo vya maziwa viko pale Hai. Lakini vile vile Hai wanavyo viwanda vya chakula vya mifugo, hongera sana Mheshimiwa Mafuwe na wananchi wote wa Hai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini tutajenga machinjio ya kisasa, ninaomba Mheshimiwa Mafuwe wewe na waheshimiwa madiwani wenzako katika Halmashauri ya Hai muanzishe mpango huu, na sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tutakuwa tayari kushirikiana nanyi katika kuwapa utaalam na mchango mwengine wowote wa kuhakikisha jambo na wazo hili zuri linatimia pale Hai, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nikiri kabisa kwamba, Wizara ya Afya kwa kweli, kwa upande wetu Jimbo la Hai wanatutendea haki, lakini naomba niulize swali. Hospitali yetu ya Wilaya ya Hai ni chakavu sana na watumishi wanapata tabu kweli kutoa huduma pale. Walk ways zimekuwa chakavu, hatuna jengo la mama na mtoto, hatuna jengo la pharmacy, kiufupi hospitali hii ni chakavu na Naibu Waziri anaifahamu vizuri. Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati katika hospitali yetu ya Wilaya ya Hai?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Hai kwa jinsi ambavyo anapambana na matatizo ya watu wa Hai. Kwenye hospitali hiyo ya Hai Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan amepeleka milioni 220, amepeleka 300, akapeleka tena milioni 90 kwa ajili ya kujenga nyumba ya watumishi, hata hivyo, nakubaliana na yeye kwamba, kwa kweli hospitali hiyo ni chakavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipita mimi na yeye na kikubwa tuliongea na DMO pale kwamba, sasa waanze kuweka kwenye mchakato wa bajeti ya mwaka huu ili itakapofika fedha zimepatikana basi liweze kutekelezeka kulingana na taratibu za fedha.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Hai kwa asilimia 78 tunategemea kilimo cha umwagiliaji, lakini pia tunazo skimu
25 za kimkakati ambazo tukizitumia tutabadilisha kabisa maisha ya watu na sisi kushiriki katika pato la Taifa. Tarehe 21Januari, 2022 Mheshimiwa Rais akiwa anaelekea Moshi Mjini alisimama pale Bomang’ombe, nami nilipata nafasi ya kumwomba atujengee skimu hizi. Alituahidi atatujengea kwa kutambua umuhimu mkubwa wa skimu hizi.

Swali langu, ni lini sasa Serikali itatekeleza agizo la Mheshimiwa Rais? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Mafue, Mbunge wa Hai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya Mheshimiwa Rais ni maelekezo kwetu na tumeipokea na tutaitekeleza kwa kadri ambavyo fedha zitaruhusu, kuanzia mwaka ujao wa fedha. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumepokea ahadi ya Mheshimiwa Rais na tutaitekeleza kadri ambavyo fedha zitakuwa zinapatikana ndani ya Wizara.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mgogoro wa muda mrefu sana kati ya wananchi wa Kata ya KIA kwa maana ya vijiji saba na Kata ya Rundugai na kule Arumeru dhidi ya Uwanja wa Ndege wa KIA. Mgogoro huu Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba ataumaliza, lakini humu ndani nimekuwa nikiahidiwa na Serikali kila mara kwamba tutaenda kuumaliza. Hivi ninavyozungumza Mheshimiwa Diwani wa Kata ya KIA muda si mrefu amenipigia simu akiniambia kwamba wameanza kuweka alama ya X nyumba za watu bila kushirikisha wananchi na viongozi wa wananchi. Naomba majibu ya Serikali yaliyo thabiti, je, ni lini Serikali itamaliza mgogoro huu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saasisha Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na mgogoro kati ya wananchi na Serikali kwenye uwanja wa KIA. Mbunge amekuwa akilifuatilia mara kwa mara, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ameshaunda timu ambayo imekwenda kufanya tathmini na kufanya utafiti na mara watakapoleta taarifa tunategemea kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha Mheshimiwa Mbunge atapewa hiyo taarifa na tuna uhakika baadaye tutakwenda kwenye eneo la tukio lenyewe na yeye pamoja na wananchi ili suala hili liweze kufika mwisho. Ahsante. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali: -

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na uchakavu wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Hai, lakini Wilaya ya Hai ina watumishi 149, hakuna nyumba hata moja ya watumishi hawa, kiasi kwamba, OCD, OC-CID na Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Hai anakaa mbali sana kwa hiyo, wanashindwa kutoa huduma pale. Ni lini sasa Serikali itajenga walao hata nyumba moja tu ya Mkuu wa Kituo Wilaya ya Hai?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni nia ya Serikali kuweka mazingira bora ya utendaji wa kazi wa vyombo vyetu vya ulinzi, hasa vya usalama, ikiwemo Polisi, Zimamoto, Magereza,
n.k. Kama nilivyosema katika jibu nililotoa juzi, tunaendelea kutenga fedha na mwaka huu zipo fedha zimetengwa kwa ajili hiyo. Lengo ni kuhakikisha kwamba, maeneo yote ambayo hayana nyumba yanapewa kipaumbele ikiwemo wilaya yako ya Hai. Ahsante sana
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; kwa kweli majibu haya sioni kama yatatusaidia kuinua michezo nchini, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.

Kwanza, Jimbo la Hai tayari pale Half London tayari tumetenga eneo kwa ajili ya kujenga kiwanja cha michezo.

Je, Serikali ipo tayari sasa kufanya mabadiliko kwenye Sera ya Michezo ili jukumu la kujenga uwanja liwe ni la Serikali Kuu na siyo Halmashauri? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili; Jimbo la Hai tuna vikundi vya sanaa vingi, tuna wasanii wazuri wengi na tayari tumeshaunda jukwaa la wasanii Jimbo la Hai na walezi wetu Mheshimiwa Taletale na Mheshimiwa MwanaFA.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri upo tayari kuambatana na mimi kwenda Hai kukaa na jukwaa la wasanii wa Hai ili kusikiliza changamoto walizonazo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mafuwe, Mbunge wa Hai.

Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Saasisha amehitaji kubadilishwa kwa sera hii ili jukumu la kujenga viwanja liwe ni jukumu la Serikali Kuu na si vinginevyo kama ambavyo sera imesema.

Mheshimiwa Spika, Niliarifu Bunge lako tukufu kwamba sera hii imeshawahi kupelekwa kwenye Kamati yetu ya Huduma za Jamii ikidhaniwa kwamba Sera hii imepitwa na wakati na mara nyingi tumekuwa tukiangalia miaka ya sera imetungwa lini lakini siyo validity ya sera hiyo.

Mheshimiwa Spika, sera hii imepitiwa na imeonekana kwamba inashirikisha wadau wote. Serikali Kuu ina jukumu lake, Serikali za Mitaa ina jukumu lake, wadau wana majukumu yao; kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba tushirikiane. Kwa upande wa Serikali Kuu tuna-deal na viwanja vikubwa ambavyo timu zetu za Kitaifa na kimataisa wanaweza wakafika. Lakini Halmashauri zetu zikitenga fedha, Mheshimiwa Mbunge tukishirikiana katika Halmashauri zetu kwa own source zetu, nina hakika kwamba viwanja vitajengwa na wananchi wetu watashiriki katika michezo. Lakini sisi hatukatai kushirikiana na Serikali za Mitaa na nishukuru Bunge mlitupatia shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Michezo, kama bajeti itaendelea kuongezeka sisi tutaendelea ku-support pia huko chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameomba tuambatane kwenda Hai kwa ajili ya jukwaa la wasanii, ninakuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaambatana kwa sababu ndiyo maelekezo tuliyopewa tuwahudumie wasanii na mimi nipo tayari tutakwenda tarehe ambazo utakuwa tayari tutafika tutawasikiliza wasanii. Ahsante. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la uhalifu na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye mabasi yanayobeba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Je, Serikali haioni ni wakati sahihi sasa kutoa maagizo kwamba mabasi haya yaendeshwe na madereva wanawake na makondakta wawe wanawake ili tunusuru ukatili wa kijinsia unaoendelea?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, inawezekana ikawa ushauri wake ni moja kati ya mambo yanayoweza kusaidia, kwa hiyo tunauchukua. Hata hivyo, ziko na hatua zingine ambazo Serikali inazifanyia kazi, kwa pamoja tutajumuisha na ushauri wake ili tuweze kufanyia kazi ili matatizo kama haya yasijitokeze tena.
MHE. SAASISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza sana Serikali kwa kupokea ushauri na kuanza kuufanyia kazi, lakini naipongeza kwa kununua ndege za mizigo. Swali la kwanza; kwa kuwa sasa Serikali imekubali kupokea ushauri, je, Serikali iko tayari kutangaza Uwanja wa Kimataifa wa KIA kuwa uwanja wa kimkakati wa kusafirisha mazao ya kilimo na mifugo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tayari Serikali imeshatenga fedha na utaratibu wa kuanza kujenga common use facility ndani ya Jimbo la Hai. Je, Serikali haioni iko haja sasa ya kujenga kiwanda cha kutengeneza maboksi kwa ajili ya kusafirishia bidhaa zinazotokana na mifugo na kilimo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza Mheshimiwa Saasisha Elinikiyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia suala hili la ndege za mizigo. Katika maswali yake mawili ya kwanza anasema je, Serikali tuko tayari kutangaza uwanja huu kuwa ni wa kimkakati. Sisi Serikali kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri tunatangaza rasmi uwanja wa KIA kuwa ni uwanja wa kimkakati kwa mazao, hususan maua, matunda, mboga mboga pamoja na nyama pamoja na viwanja vingine kama cha Songwe International Airport kilichopo Mkoani Mbeya pamoja na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, anataka kufahamu ni kwa namna gani tunaweza tukashirikiana pia na wenzetu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara katika kukuza eneo hili na kujenga viwanda vidogo.

Mheshimiwa Spika, uwanja wa KIA tayari tumeshatenga hekari ama hekta 711 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogovidogo, lakini pia kwa kushirikiana na wawekezaji na tayari tumeshaanza kufanya hiyo hatua. Ahsante.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kuna mradi mpya unaojengwa wa visima kutoa maji Hai kwenda Arusha, lakini kwenye vile vyanzo ambavyo maji yanapita kama kanuni na sheria zinavyotaka kwamba, maeneo ambayo yanaptikana vyanzo vya maji watu wapate. Sasa nauliza swali langu; je, ni lini Serikali itatengeneza miundombinu maeneo ya Hai kwenye mradi mkubwa unaoenda Arusha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Sera ya Maji inataka maeneo yote ya vyanzo vya maji, wale wanaozunguka makazi yale wananchi wawe wanufaika namba moja. Katika visima hivi anavyoviongelea tayari sisi kama Wizara tuna utaratibu ambao tunaendelea nao, pesa itakapokamilika tutakuja kuendelea kuhakikisha wananchi wote wale wanaokaa kuzunguka vile visima wanaendelea kupatiwa huduma ya maji.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Hai maeneo mengi yamekuwa na miundombinu ya umeme ambayo ni chakavu sana, jambo ambalo ni hatari. Katika Kata ya Uroki, Masama Kusini, Machame na maeneo mengi yamekuwa na miundombinu ambayo kwa kweli ni chakavu sana. Tuliwasilisha maombi maalum ya kupewa vifaa kwa ajili ya kufanya marekebisho.

Je, ni lini Serikali itatuletea vifaa hivi ili kutuondoa kwenye hatari ya miundombinu ambayo imekuwa chakavu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kurasimisha na kurekebisha miundombinu yake ya umeme inayowapelekea wananchi nishati hiyo. Katika Mwaka huu wa Fedha, Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 500 kwa ajili ya kurekebisha Gridi ya Taifa katika maeneo ya umeme mkubwa pia imetenga Bilioni 300 kwa ajili ya kurekebisha miundombinu ya umeme kwenye maeneo madogo madogo ambayo tunaziita ni project mapato.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba na yeye atapata mgao huo kwa ajili ya kurekebisha miundombinu yake chakavu ili huduma hii iweze kuendelea kupatikana katika eneo lake la Hai. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kwanza naishukuru sana Serikali kwa namna ambayo kwa kweli wameweza kudhibiti moto uliokuwa unawaka ndani ya Mlima Kilimanjaro. Katika dhana hiyo hiyo ya kudhibiti, je, Serikali haioni iko haja ya kufanya mabadiliko ya sheria ili wananchi wanaozunguka Mlima Kilimanjaro waweze kupata service levy kama ilivyo kwenye maeneo mengine yenye mgodi ili kuongeza sense of ownership ya wananchi wanaozunguka kuona mlima ule ni mali yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunapokea mawazo yake, lakini bado tunatambua kwamba wananchi wanaozunguka maeneo ya Mlima Kilimanjaro, ni sehemu ya hifadhi na mara nyingi tumekuwa tukihamasisha upandaji wa miti ili kulinda hifadhi hii ili iweze kutunzwa vizuri. Kwa hiyo, tunalipokea hili pia la sheria ili tuweze kuangalia utaratibu mwingine kuhakikisha mlima huu tunautunza vizuri.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, asante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza, nikiwa na hakika kabisa kwenye magari na Wilaya ya Hai itapata.

Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza ni lini Serikali sasa itatuletea vifaa tiba kwenye kituo chetu cha afya cha Longoi ambacho kimekamilika, ili kiweze kuanza kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe Mbunge wa Hai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali yetu imeendelea kutenga fedha za ununuzi wa vifaa tiba kwa awamu. Kwa sasa tayari imeshatenga kwa ajili ya Hospitali zile 67 za awamu ya kwanza lakini tutakwenda Hospitali zile 28 za awamu ya pili na vituo vya afya vitatengewa fedha baada ya kukamilika kwa hizi 67 na 28 kikiwemo Kituo hiki cha Afya katika Halmashauri ya Hai. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hicho ni kipaumbele cha Serikali na kadri ya upatikanaji wa fedha tutapeleka fedha na vifaa tiba katika Kituo cha Afya cha Hai.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kwasadala - Kware - Lemira Kati, kilometa 15.2 ni barabara muhimu sana inayoshusha mazao kwenye soko la Kwasadala na hatimae kuja huku Dodoma na sisi kuweza kuitumia.

Je, Serikali ni lini itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saasisha Mafuwe, Mbunge wa Hai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja ya Kware - Lemira ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa Hai. Hivi tunavyoongea ni kwamba Serikali inatafuta fedha ili fedha ikipatikana barabara hii ambayo siyo ndefu iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara Serikali itakapopata fedha barabara hii ambayo inasimamiwa na TANROADS itajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kumekuwa na uonevu mkubwa sana na wizi mkubwa wa wananchi wanapoenda kuuza mazao yao sokoni, kuna watu wanaitwa madalali hawa watu ndio wanao panga bei ya mazao na kuondoa fursa ya wakulima kupanga bei ya mazao yao. Je, Serikali ina mpango gani wa kisheria wa kuondoa tatizo hili na kuweza kumlinda mkulima aweze kuuza kwa bei anayotaka yeye?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kumekuwa na changamoto ya uuzaji wa mazao kwa kulazimishwa kuuza kwa rumbesa wakulima wetu. Je, Serikali ni lini itapeleka maagizo maalum kwenye halmashauri zetu za kuzuia uuzaji huu wa rumbesa mazao ya wananchi?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Saashisha, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la rumbesa kama alivyojibu Naibu Waziri wa Viwanda hapa mbele ya Bunge lako tukufu vilevile Wizara ya Kilimo tukishirikiana na Wizara ya Viwanda tumeshakuwa na mwongozo rasmi ambao tutaupeleka katika halmashauri zote nchini ili halmashauri waweze kusimamia mwongozo huo kuanzia suala la ununuzi, suala la uwekaji kwenye vifungashio na namna ambavyo mazao yanasafirishwa kwa hiyo hili ni jambo ambalo tutashirikiana pamoja na Serikali za Mitaa kuhakikisha tunalitatua hili tatizo ni kweli lipo na ni tatizo kubwa lakini naamini litakwisha.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hili la madalali walioko masokoni. Kwanza uwepo wa middle man katika biashara ni jamba ambalo limekuwepo toka historia ya Dunia inaumbwa na ni jambo ambalo halikwepeki lakini kuwa na watu wakati ambao hawako regulated hili ndio tatizo ambalo linatukabili kwa hiyo Serikali kupitia Sheria iliyoianzisha Mamlaka ya COPRA hivi karibuni tumeshapeleka mapendekezo atateuliwa Mkurugenzi Mkuu wa COPRA ambaye atakuwa na jukumu la kudhibiti wauzaji na wanunuzi wanaosimamia uuzaji na ununuzi wa mazao katika masoko makuu na masoko ya awali. Kwa hiyo tutaweka utaratibu wa wazi wa kikanuni kwa kufuatana na Sheria ya COPRA ili kuweza kudhibiti na kuhakikisha kwamba mkulima anafaidika na jasho lake.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Kunambi, swali lake hapa linauliza ni lini Serikali itatatua mgogoro huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ili kupunguza migogoro na kuimarisha sense of ownership kati ya Mlima Kilimanjaro na Vijiji vya Foo, Mkuu, Ndoo, Kilanya, Sawe, Ng’uni na kule Kieli, Serikali ilituahidi kutuletea fedha za CSR ili tujenge madarasa; nawe Mheshimiwa Naibu Waziri uliahidi hapa Bungeni kwamba mtatupa fedha hizo: Je, ni lini Serikali itatuletea fedha hizo za CSR? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saashisha kwa niaba ya Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nifafanue kwenye suala la lini Serikali itatatua mgogoro? Kwenye jibu langu la msingi nimeeleza kwamba, kwa sasa hivi Kamati ya Mawaziri nane imeshapita maeneo takribani yote hapa nchini, na imeacha kila mkoa kamati inayofanya tathmini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya maeneo tayari uthamini umeshaanza, lakini kuna maeneo ambayo tayari wananchi walikuwa wameshavamia kwenye maeneo kama hilo la kilombero. Tunafanya tathmini kuangalia eneo lipi ambalo litakuwa ni la muhimu kuokoa kile kiini ambacho kitatunza haya maji kwa ajili ya kuyapeleka katika Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini hii iko uwandani inafanyika na inashirikisha wananchi wa Mlimba hatua kwa hatua ili kuangalia nini kilicho sahihi ili kusije kukaleta mkanganyiko tena kwamba kamati hii haikushirikisha wananchi. Kwa hiyo, ni lini? Ni pale ambapo tu kamati hii itakapokamilisha uthamini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la CSR, naomba tu tena niendelee kuelekeza TANAPA; nakumbuka tulifanya ziara na Mheshimiwa Saashisha katika maeneo ya hai, lakini tukaangalia, kweli kulikuwa kuna uhitaji wa wananchi katika eneo hilo ambalo wanatakiwa wapate CSR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nielekeze TANAPA tukamilishe ahadi hii kwa wananchi ili tuweze kuwa na ushirikiano mzuri na wananchi waweze kuwa ni sehemu ya uhifadhi kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye, ahsante.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naishukuru Serikali kwa kutujengea vituo vya afya ndani ya Jimbo la Hai.

Swali langu, ni lini sasa Serikali itatuletea vifaa tiba kwenye Vituo vya Afya vya Kwansira, Chemka na pale Kisiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Jimbo la Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba Kituo cha Afya cha Kwansira ambako mimi na yeye tulifanya ziara na kazi ya ujenzi iko hatua za mwisho, ni sehemu ya vituo ambavyo vinahitaji vifaa tiba mara baada ya kukamilika, lakini pamoja na hivi vituo vya afya vingine ambavyo amevitaja. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kutenga fedha na kupeleka vifaa tiba kwenye vituo hivyo alivyovitaja ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wa Hai, ahsante.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, kwenye hayo magari 12 ambayo Serikali imenunua; je, Wilaya ya Hai imo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa sasa haimo, lakini mpango wa Serikali kadri utakavyoongeza uwezo wetu maeneo kama haya ambayo yamekuwa na usumbufu wa kuwaka moto msitu wetu unaozunguka Mlima Kilimanjaro kuwaka moto mara kwa mara yatazingatiwa katika bajeti zetu zijazo.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Hai, wamehamasika sana kulima zao hili la parachichi na zao la kahawa: Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku ili wakulima hawa waweze kufanya kazi hii kwa ufanisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, kutokana na umuhimu wa zao hilo la parachichi, Serikali tumedhamilia kuweka ruzuku ya kutosha ili kuwafanya wakulima waendelee kulima kwa tija na kupata miche hii kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mkoa wa Kilimanjaro, tunashirikiana pia na wadau kama Africado na wadau wengine kama vile KEDA kule Rombo ambao pia kwa pamoja tunafanya kazi ya uzalishaji wa parachichi. Tumesema katika bajeti ya mwaka 2022/2023, tutazungumza kuhusu ruzuku ambayo tumeitenga kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wakulima hawa wanapata miche kwa bei nafuu.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshiiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali.

Mheshimiwa Spika, swali hili niliwahi kuuliza likiwa linafanana hivi kwenye maswali ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Majibu yaliyotolewa na Serikali na haya yanayotolewa sasa hivi yanapishana. Sasa napenda kufahamu msimamo wa Serikali kuhusu shule hizi, kwa mfano shule ya Mshara, Sare na Mroma. Shule hizi zina majengo, vifaa na walimu: Je, Serikali inatoa msimamo gani kuhusiana na shule hizo?

Swali la pili; Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha Ufundi VETA ndani ya Jimbo la Hai ilhali tayari tumeshapanga eneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saashisha, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna shule za msingi 123 hapa nchini ambazo zilikuwa zinatakiwa zitoe mafunzo ya ufundi pamoja na elimu ya msingi, lakini shule zote hizo sasa hivi hazitoi mafunzo hayo kwa sababu ya uhaba wa walimu. Vyuo ambavyo vilikuwa vinatoa mafunzo kwa mfano Chuo cha Ualimu cha Mtwara ambacho kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwafundisha walimu elimu ya ufundi kwa ajili ya shule za msingi, imeacha kufanya kazi hiyo kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika kujibu swali la msingi, sasa hivi tunapitia mitaala yote ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya ufundi na lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba tunaingiza ufundi na ujuzi katika shule zote ikiwa ni pamoja na hizi shule 123 na hizi shule za Jimbo la Hai kama alivyoeleza Mheshimiwa Saashisha. Tunatarajia kwamba tutamaliza shule za mitaala mwisho wa mwaka huu, hivyo tutaweza kuanza sasa kuhakikisha kwamba tunafundisha wanafunzi katika ngazi zote hizo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu VETA, ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba tunajenga vyuo vya VETA kila Wilaya hapa nchini na juhudi hizo zinaendelea. Kwa yale maeneo ambayo tayari Wilaya zimeshatenga maeneo na hasa maeneo yale ambayo Wilaya na Halmashauri na Wabunge wameanza juhudi za kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi, tutajitahidi kuhakikisha kwamba tunaenda kuongeza nguvu za Serikali ili kukamilisha azma hii ya kuwa na VETA katika kila Wilaya ikiwa ni pamoja na Jimbo la Hai kwa Mheshimiwa Saashisha.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa Jimbo la Hai kuna changamoto kubwa sana ya uchakavu wa miundombinu, lakini kumekuwa na maombi ya muda mrefu sana ya wananchi tangia mwaka 2008 mpaka sasa hivi hawajaunganishiwa; na kwa kuwa tulikaa na Mheshimiwa Waziri na timu yake na wakapeleka wataalam kule Hai kwenda kubaini mahitaji ya wananchi. Je, ni lini Serikali itatuletea vifaa ili wananchi waweze kuunganishiwa umeme na kurekebisha miundombinu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Saashisha amefuatilia sana umeme katika jimbo lake na kama alivyosema Mheshimiwa Waziri alituma timu kwenda kufuatilia. Niombe kwamba baada ya hapa tukutane ili nipate taarifa ya hiyo Kamati na nitoe maelekezo ya kufanya kile ambacho kilibainika kinaweza kufanyika ili tatizo lake la muda mrefu ambalo amekuwa ukilifuatilia liweze kutatuliwa. Naomba baada ya hapa tuweze kuwasiliana.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, Wilaya ya Hai ina shule 13 chakavu sana na Mheshimiwa Rais alipotembelea Wilaya ya Hai, aliahidi kutupa fedha kwa ajili ya kujenga maboma ya shule hizi chakavu, lakini wewe mwenyewe Mheshimiwa Naibu Waziri pia ametembele Wilaya ya Hai na amejionea shule zilivyo chakavu. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Jimbo la Hai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuondoe wasiwasi, kwamba mpango wa Serikali wa marekebisho ya shule tutaanza katika mwaka wa fedha wa 2022/2023. Najua moja ya shule niliahidi ni Makeresho na ipo katika huo mpango, ahsante sana.