Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Justin Lazaro Nyamoga (13 total)

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa kumpata mwekezaji katika Shamba la Chai la Kidabaga?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile nami ni mara ya kwanza leo kusimama katika Bunge lako Tukufu, naomba kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema ambaye ametujalia mema mengi. Pili, nakishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuniamini na kunipa nafasi kuwakilisha katika Jimbo la Mufindi Kaskazini. Tatu, nawashukuru wananchi wenzangu wa Jimbo la Mufindi Kaskazini ambao waliniamini na kunipa kura nyingi ili niweze kuwa mtumishi wao. Mwisho, kwa niaba ya familia yangu, nawashukuru sana, lakini kwa namna ya pekee mke wangu kwa kunipa ushirikiano ili niweze kuendelea kutekeleza majukumu yangu ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kumpata mwekezaji mahiri katika Kiwanda cha Chai cha Kidabaga. Maandalizi ya kumpata mwekezaji huyo yameanza ikiwa ni pamoja na kukamilishwa kwa Andiko linalohusu Viwanda 17 vilivyokuwa vimebinafsishwa lakini baadaye kurejeshwa Serikalini, kikiwemo Kiwanda cha Kidabaga.

Mheshimiwa Naibu Spika, andiko hilo kwa namna ya pekee kuhusu Kidabaga linajumuisha mapendekezo ya muundo mpya wa uendeshaji wa kampuni utakaozingatia maslahi ya wakulima wa chai wa Kidabaga na kwa Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara inaandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri kwa ajili ya viwanda vilivyorejeshwa Serikalini ikiwa ni pamoja na Kiwanda cha Chai cha Kidabaga. Hivyo, Serikali itakamilisha mchakato huo mapema iwezekanavyo ili mwekezaji mahiri aweze kupatikana kwa ajili ya kuwekeza katika shamba hilo la Kidabaga.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu katika Kata za Masisiwe, Nyanzwa, Irole na Ibumu ambazo zina shida kubwa ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI, alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Serikali ya Awamu ya Sita, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Rais wa Awamu ya Sita katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania. Sambamba na hilo, naomba niwapongeze wanawake wote wa Tanzania, kwa sababu wameendelea kuonesha mfano wa kuigwa, tukishuhudia katika Awamu ya Nne, mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Katika Awamu ya Tano, alikuwa mwanamke wa kwanza Tanzania kuwa Makamu wa Rais na katika Awamu ya Sita, amekuwa mwanamke wa kwanza katika Nchi yetu ya Tanzania kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kuendelea kuniamini kumsaidia katika nafasi ya Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Lazaro Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kilolo lina Kata 24 ambapo Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeishakamilisha utekelezaji wa miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata tatu ambazo ni Lugalo ambapo ina mnara wa Halotel, Udekwa ambapo kuna mnara Vodacom na Ukwega ambapo kuna minara miwili ya Tigo na Halotel.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizi za Serikali baadhi ya kata za jimbo hili zinachangamoto za upatikanaji wa huduma ya mawasiliano kama vile Kata za Masisiwe, Nyanzwa, Ibumu na baadhi ya maeneo ya Kata ya Irole. Jiografia ya jimbo hili ni ya milima na miti mirefu ambapo kwa kiasi kikubwa sana inaathiri upatikanaji wa huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Irole kuna baadhi ya maeneo yanapatikana huduma za mawasiliano kupitia mnara wa mawasiliano wa HTT, uliobeba watoa huduma watatu ambao ni Airtel ambayo inatoa teknolojia ya 2G, Vodacom ambapo wanatoa teknolojia ya 2G na 3G na Tigo ambao wanatoa 2G na 3G. Pamoja na uwepo wa huduma za mawasiliano kutoka kwa watoa huduma niliotaja, bado kuna maeneo ndani ya Kata ya Irole yana changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) iliifanyia tathmini Kata ya Ibumu na hatimaye kukijumuisha Kijiji cha Ilambo katika zabuni ya awamu ya tano ya mradi wa kufikisha mawasiliano mipakani na kanda maalum. Mradi huu unatekelezwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ambapo mikataba ya utekelezaji wa mradi huo ilitiwa saini tarehe 6 Julai, 2020. Mradi huu utakapokamilika utaweza kuhudumia Vijiji vya Ibumu, Kilala, Kidewa, Ilambo na Kilumbwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote UCSAF itavifanyia tathmini vijiji vya Kata za Masisiwe, Nyanzwa na baadhi ya vijiji vya Kata ya Irole ambavyo huduma ya mawasiliano imekuwa changamoto kwa kiasi kikubwa sana. Huduma inatolewa na mnara wa HTT uliopo na hatimaye vijiji husika vitaingizwa katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022.
MHE. LAZARO J. NYAMOGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Makao Makuu ya Polisi ya Wilaya ya Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lazaro Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua hitaji la ofisi ya Makao Makuu ya Polisi Wilaya ya Kilolo na eneo linalohitajika kujengwa ofisi limeshapatikana na ni eneo la Luganga na lina ukubwa wa hekari 16. Zoezi la kufanya tathmini ili kulipa fidia wananchi limeshafanyika tangu mwezi Julai 2020 kupitia wataalam toka Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo na kupata makadirio ya shilingi 110,092,554.00 zinazohitajika kulipa fidia wananchi hao.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatafuta fedha kwa ajili ya kulipa fidia wananchi na mara baada ya kuwalipa wananchi fidia kwa mujibu wa sheria na taratibu ujenzi utaanza mara moja.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Iringa Mjini hadi Kilolo ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Iringa Mjini hadi Kilolo yenye urefu wa kilometa 33.6 ni sehemu ya barabara ya Iringa iliyoanzia Ipogolo – Idete yenye urefu wa kilometa 67.7 ambayo ni barabara ya Mkoa inayosimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS). Kilometa 9.9 za barabara hiyo ni za lami na kilometa 23.7 nyingine ni za changarawe.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara ya Iringa Mjini hadi Kilolo, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) ilikamilisha Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo mwaka 2009. Kwa sasa ujenzi wa kilometa 10 kwa kiwango cha lami kati ya kilometa 23.7 za changarawe unaendelea huku marejeo ya usanifu wa mwaka 2009 yakiendelea.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa kilometa 13.7 zilizosalia kadri ya upatikanaji wa fedha. Aidha, Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara yote kutoka Iringa Mjini hadi Idete kuhakikisha kuwa inapitika vipindi vyote vya mwaka, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafikisha umeme katika Kata za Nyanzwa, Udekwa na Ukwega Wilayani Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lazaro Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kilolo ina kata 21, kati yake kata tatu tu hazijapata umeme na vijiji 94, kati yake vijiji 23 tu havijapata umeme. Vijiji vyote 23 ambavyo havina umeme vikiwemo Vijiji vya Kata za Nyanzwa, Udekwa na Ukwega ambavyo ni Nyanzwa, Mgowelo, Igunda, Udekwa, Wotalisoli, Ifuwa, Ukwega, Ipalamwa, Makungu na Mkalanga vinapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambao utekelezaji wake ulianza mwezi Machi, 2021 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2022.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kuigawa Wilaya ya Kilolo kuwa na Halmashauri mbili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa kuanzisha eneo la utawala la wilaya unafanyika kwa Mujibu wa Sheria, Kanuni na kwa kuzingatia mwongozo wa kuanzishwa maeneo mapya ya utawala wa mwaka 2014. Aidha, maombi ya kuanzisha wilaya mpya yanatakiwa kujadiliwa na kupitishwa kwenye Vikao vya Kisheria ngazi ya Vijiji, Kata, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Kamati ya Ushauri ya Mkoa. Maombi hayo yanawasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya uchambuzi na uhakiki na baadaye kuishauri mamlaka ipasavyo juu ya suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Iringa haujawasilisha mapendekezo yanayohusu kugawa Wilaya ya Kilolo ili kuwe na Halmashauri mbili. Napenda kumshauri Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Kilolo kufuata utaratibu uliolekezwa hapo juu, ahsante.
MHE. JUSTINE L. NYAMOGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga bwawa la maji katika Kata ya Nyanzwa kwa ajili ya skimu ya umwagiliaji?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justine Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa bwawa na Skimu ya Umwagiliaji Nyanzwa. Aidha, mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatenga fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa bwawa na Skimu ya Umwagiliaji Nyanzwa.
MHE. NANCY H. NYALUSI K.n.y. MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itarudisha Shamba la Kijiji cha Ng’ang’ange kwa wananchi kufuatia mauziano kati ya EFATHA na Kijiji kutofuata sheria?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2003 Taasisi ya Efatha Ministry iliomba eneo lenye ukubwa wa ekari 200 katika Kijiji cha Ng'anga'nge kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi, Kilimo na Mifugo. Taratibu zote za utoaji eneo husika zilifuatwa ikiwemo Kikao cha Halmashauri ya Kijiji, Mkutano Mkuu wa Kijiji na Kamati ya kugawa ardhi ya Wilaya pamoja na fidia za mali zililipwa.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mgambalenga Wilayani Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Justine Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/ 2023, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya Mgambalenga yenye hekta 3,000 Wilayani Kilolo. Ujenzi huo utahusisha ukamilishaji wa mfereji mkuu wenye urefu wa kilometa 14 pamoja na maumbo yake.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kufuta Hati ya Umiliki wa Shamba la Mwekezaji katika Kijiji cha Mawalla - Kilolo ambalo limetelekezwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, shamba lililotelekezwa katika Kijiji cha Mawalla, ni shamba lenye Hati Na.16633 lenye ukubwa wa ekari 639 ambalo linamilikiwa na Ndugu Mbaraka Mazrui. Mmiliki wa shamba hili alitelekeza shamba tangu mwaka 1980. Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, imelitambua shamba hili kama shamba lililotelekezwa.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo, Serikali imeanza hatua za awali za ubatilishaji wa shamba husika na pindi hatua hizo zitakapokamilika, mapendekezo yatawasilishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya ubatilishaji.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE K.n.y. MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa mradi wa maji wa Kihesa Mgagao, Masege hadi Masalali - Kilolo?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi wa maji katika vijiji vya Kihesa Mgagao, Masege hadi Masalali upo kwenye hatua za mwisho za kumwajiri Mkandarasi. Utekelezaji wa mradi utaanza Mwezi Mei, 2023 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei, 2024. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa matenki matatu (3) yenye jumla ya ujazo wa lita 250,000, ujenzi wa mtandao wa mabomba ya maji yenye urefu wa kilometa 25.4 na ujenzi wa vituo 25 vya kuchotea maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha wananchi wapatao 9,006 waishio kwenye vijiji hivyo.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA K.n.y. MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la Pareto Wilayani Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbuge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tija ya sasa ni kati ya kilo 280 hadi 300 ya pareto kavu kwa ekari. Hata hivyo, tija inayoweza kufikiwa na wakulima wengi ni kati ya kilo 400 hadi 500 kwa ekari moja. Pamoja na mambo mengine tija ndogo inasababishwa na wakulima wengi kwa muda mrefu kuendelea kutumia mbegu ambazo zina tija ndogo na wakulima walio wengi kutopendelea kutumia mbolea katika uzalishaji wa zao la pareto.

Mheshimiwa Spika, aidha, kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo katika mwaka wa fedha 2022/2023 ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 200 ambazo zilipelekwa TARI kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora na zenye tija. Upatikanaji na usambazaji wa mbegu bora hizo unatarajiwa kuanza msimu 2023/2024. Mbegu hizo ambazo zitakuwa na tija kuanzia kilo 400 na zaidi kwa ekari zitasambazwa kwa wakulima wote wa pareto nchini ikiwa ni pamoja Wilaya ya Kilolo. Usambazaji huo utaenda sambamba na utoaji elimu ya mbinu bora za kilimo cha pareto kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kuendesha tafiti za matumizi ya mbolea kwa zao la pareto. Utoaji wa elimu utafanywa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi hususan Wanunuzi na Wasindikaji wa zao katika Wilaya ya Kilolo.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga minara ya simu katika Kata za Masisiwe, Udwekwa na Nyanzwa Wilayani Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la Kilolo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ilibaini changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Kata za Udekwa, Nyanzwa na Masisiwe ambapo tayari imekwishawapata watoa huduma wa kufikisha huduma za mawasiliano katika kata za Masisiwe na Nyanzwa wakati Kata ya Udekwa itaingizwa katika orodha ya miradi itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.