Contributions by Hon. Stephen Lujwahuka Byabato (3 total)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia hoja hii ya Mpango. Niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara ya Nishati maoni yao na mapendekezo tumeyachukua na tutayafanyia kazi kwa upana wake. Niongelee tu kwenye maeneo machache mengine ni ya kuweka taarifa sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza kwenye gesi asilia. Kama tulivyosema juzi Serikali imeipa mtaji TPDC wa dola bilioni 1.193. Kwa kubadilisha deni la bomba la gesi kuwa sasa pesa ambayo TPDC inaweza ikaitumia. Kwa hiyo hatuna wasiwasi na tunakoelekea kwamba TPDC itaweza kukopesheka na kufanya biashara katika mazingira ambayo itakuwa na bargaining power za kuweza kupata mikopo yenye riba nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili tayari mikataba ya interest MOU zimesainiwa kati ya Tanzania na Uganda, Tanzania na Kenya, wenzetu wa Malawi na Rwanda wameonesha interest, kwa hiyo tukitoa gesi hii Dar es Salaam na Mtwara kupeleka Uganda hii Mikoa yote ya katikati itapata tukipeleka Kenya Mikoa ya katikati itapata kwa hiyo humu ndani tutaisambaza vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine ambalo nimeona nilisemee kidogo ni eneo la idadi ya vijiji vyenye umeme na visivyokuwa na umeme. Ukurasa wa 32 wa Mpango umeeleza taarifa na ni taarifa sahihi na naomba niseme kwa sasa. Vijiji tulivyonavyo kwa mujibu wa takwimu za TAMISEMI ni 12,345, kwa mujibu wa taarifa za TAMISEMI na kwenye mpango imeandikwa hivyo. Vijiji vyenye umeme mpaka kufikia Tarehe 31/10/2022 ni 9,163, Vijiji ambavyo bado ambavyo vyote viko kwenye REA III round II ni Vijiji 3,182 ambavyo mikataba yake inaendelea kwenye maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya takwimu ilitokea kwenye mazingira tuliyokuwa tunafanyia kazi. Huko nyuma kuna vitongoji vikubwa ambavyo vilipewa umeme na wenzetu wakavihesabu kama vijiji. Sasa vimeondolewa kwenye idadi ili tubakie na vijiji halisia na Waheshimiwa Wabunge tunafahamu kwenye maeneo yetu, maeneo ambayo tumeweka umeme kwenye vitongoji lakini vilihesabiwa kama vijiji. Sasa taarifa sahihi ni hii Vijiji 12,345, Vijiji 9163 tayari umeme na Vijiji 3182 umeme bado lakini vina mikataba vyote na vinafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Tatu ni kwenye uhakika wa umeme na wenye gharama nafuu. Mpango wetu umeelaza vizuri kabisa kwenye ukurasa wa 18, ukurasa 32 na kiambatisho C ukurasa wa 1- 3, umeeleza miradi mingi sana ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mchangiaji alisema hata mpango wa kutoa umeme Mwalimu Nyerere kuuleta Chalinze haupo. Ukurasa wa 33 umeeleza vizuri kabisa kwamba tunatoa umeme Mwalimu Nyerere na tutauleta Chalinze na kazi inaendelea tunatarajia ikamilike mwaka unaokuja na miradi ya kutoka Chalinze kuja Dodoma, kutoka Chalinze kwenda Mwalimu Nyerere yote imeelezwa kwenye mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye miradi ya uzalishaji kuna mwenzetu mmoja alichangia kwamba…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri hapo ndiyo ambapo kidogo huwa tunachanganyikiwa, mwaka ujao kwa maana ya 2023 au mwaka 2024 maana unasema mnatarajia ikamilike mwaka ujao, wakati taarifa tulizonazo ni 2024.
NAIBU WAZIRI WA NSHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kutoa umeme Mwalimu Nyerere kuuleta Chalinze unakamilika mwaka wa fedha huu. Nina maana ya Januari kuelekea Juni, mwaka wa fedha huu. Kwa hiyo, kwa program tuliyokuwa nayo itakamilika kabla ya Bwawa la Mwalimu Nyerere kukamlika ambalo kwa mujibu wa mkataba wa extension nitakaousema baadae inatakuwa kuwa Oktoba mwakani. Kwa hiyo, ni mwaka wa fedha huu tuliopo sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ambayo mpango umeitaja kwa ajili ya uzalishaji. Tunao Mwalimu Nyerere, megawatt 2115, tunayo Rusumo unakamilika muda siyo mrefu megawatt 80, tunayo Ruhuji inakuja megawatt 358, tunayo Rumakali megawatt 222, tunayo Kikonge megawatt 300 tuna miradi ya upepo na jua megawatt 300, tunayo Kinyerezi One Extension megawatt 185, zote hizo tunatarajia kwamba zitatupatia umeme kwa mujibu inavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unipe nafasi kidogo ya kueleza mambo mawili kwenye mradi wa Mwalimu Nyerere.
MWENYEKITI: Sasa kila Waziri anaomba apewe nafasi kidogo tu sijui nimkate mmoja ili ndiyo niwe nimezigawanya hizo? Haya dakika moja malizia.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa sababu ya muda nizungumzie vitu viwili tu. Kimoja muda tuliouongeza kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere ni mwaka kwa mujibu wa mkataba, tumeongeza mwaka mmoja na muda huo utakapoisha ndiyo tutaanza kugombana kuhusu nani kachelewesha mradi.
MWENYEKITI: Mwaka mmoja ndiyo mpaka lini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Oktoba mwakani kwa mujibu wa mkataba tuliosaini. Iko taarifa na mpango kazi wake aliouleta anapoomba miaka miwili sisi tulimwambia tunampa mwaka mmoja na wenzetu wataalam wanaendelea kuchanganua ule mpangokazi wa utekelezaji ili u-fit mwaka mmoja lakini mkataba wa nyongeza extension of time ni mwaka mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo kuhusu hii habari inayosemwa ya liquidated damages, taarifa sahihi ni kwamba liquidated damage kwenye mkataba wa Mwalimu Nyerere ni 0.1% kwa kila siku kwa maximum ya asilimia Tano siyo asilimia Kumi siyo zaidi ya hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kwenye CSR tunaambiwa tunatoa taarifa kwamba tungezikata hizi pesa. Mkataba unatueleza kwamba tumpe Mkandarasi atekeleze CSR, tulikuwa hatujakubaliana miradi ya kutekeleza sasa tumekubaliana Mkandarasi ataanza kutekeleza CSR za bilioni 263 na tuko ndani ya muda na tutakamilisha kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kwanza kuunga mkono hoja ili lolote likitokea huko mbele basi niwe kwenye safe side. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa muda huu mfupi ili na mimi niweze kusema kidogo tu wakati huo nikimuachia Mheshimiwa Waziri nafasi ya kueleza na kuweka commitment za Serikali kwenye maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge wamechangia.
Mheshimiwa Spika, nianze kwa shukrani, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai, afya na nimshukuru Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuniona mimi kijana na akaamua kunipa majukumu haya makubwa. Nimhakikishie tu kwamba kwa niaba ya vijana wenzangu ambao tunaendelea kutumika katika nafasi hizi hatutamuangusha yeye wala Watanzania katika utekelezaji wa majukumu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini niwashukuru viongozi wa Kitaifa, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Kipekee kabisa nikushukuru wewe kwa jinsi unavyotuongoza na kutujenga sisi Wabunge na hasa sisi Wabunge vijana na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wapo humu kwa ushirikiano mkubwa ambao wanatupatia kama Wabunge, lakini mimi kwa nafasi yangu kama kiongozi kwenye nafasi ya Uwaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimshukuru pia Mheshimiwa Waziri wa Wizara yetu ya Nishati kwa kuendelea kuwa kiongozi, jemedari shupavu na aliyekakamaa kabisa na kutufikisha hapa ambapo wengi tunaogopa tunadhani hatutafika, lakini kwa maelekezo ya wakubwa wetu na yeye Wizara yetu imeendelea kufanya kazi ambazo Watanzania wanazitegemea. Pia niwashukuru watendaji wengine wote wa Wizara yetu ambao kwa kweli mengi tunayoyasema na kuyafanya hapa ni yale ambayo wao wametushauri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitakuwa mnyimi wa fadhila nisipowashukuru wananchi wa Jimbo la Bukoba Mjini walioamua kukichagua Chama cha Mapinduzi kwa kunipa mimi kura za kutosha na kunituma kijana wao kuja kutumikia Taifa katika maeneo haya. Nimshukuru pia mke wangu kwa kuendelea kunivumilia na kunipa nafasi ya kufanya majukumu haya, lakini na familia kwa ujumla na maisha yanaendelea vema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nitazungumzia maeneo matatu tu, kwa haraka haraka, maeneo mawili ni ya ufafanuzi mdogo na Mheshimiwa Waziri atakuja kumalizia. Eneo la kwanza Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamezungumzia kuhusu kukatika kwa umeme. Sababu za kukatika kwa umeme zitaelezwa, lakini mimi niseme tumejipanga kupitia bajeti tunayoomba mbele yenu lakini tumejipanga kufanya yafuatayo kwa uchache wake ili kuhakikisha basi umeme unakuwa haukatiki mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika, cha kwanza tutarekebisha miundombinu kama ambavyo tumekuwa tukifanya, tutaendelea kupanua wigo wa kurekebisha miundombinu. Pia tutasogeza vituo vya kupoza umeme karibia na watumiaji ili kupunguza ule wigo wa umeme kupotea na vimetajwa kwenye bajeti yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tutafunga vifaa mbalimbali vya kitaalam vya kuhimili vitishio vya kiasili kama radi, mvua na vitu kama hivyo nitavitaja baadaye kitaalam. Pia tunaweka njia ile ya kupitisha umeme salama kwa kuendelea kufyekea yale maeneo ili yasipate madhara ya miti kuangukia nguzo na nyaya za umeme.
Mheshimiwa Spika, la mwisho siyo kwa umuhimu kuendelea kuwasimamia watumishi tunaofanya nao kazi na hasa wale wachache ambao ni wazembe, wanaosababisha upotevu wa umeme na kuonekana kwamba umeme unakatika pengine bila sababu za msingi. Hivi juzi mmeona hatua ambazo Mheshimiwa Waziri Mkuu alizichukua pamoja na Mheshimiwa Waziri wetu katika kuhakikisha kwamba watumishi wanakuwa waadilifu na wanatumika vizuri kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo nataka nizungumzie kidogo tu ni kuhusu miradi ya REA. Kwa nini miradi ya REA mingine imekuwa ikichelewa kukamilika? Sababu zipo nyingi lakini mimi nitaje kidogo tu, mojawapo ni ile kuongezeka kwa wigo wa kazi ambayo mkandarasi amekuwa amepewa mara ya kwanza. Alipewa vijiji sita lakini tumefika site tumekuta vijiji vinavyohitaji umeme zaidi ni kama tisa au kumi kwa vyovyote vile ule muda wa awali tunajikuta tunatakiwa kuongeza ili kukamilisha yale ambayo yanatakiwa kufanyika.
Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili ambalo ni la kuelezeka ni pale ambapo baadhi ya maeneo yanakuwa hayafikiki labda ni kwenye mapori, hifadhi au hali ya hewa ya mvua basi hapapitiki kwa sababu ya miundombinu kuchukuliwa na maji tunajikuta tunachelewa katika maeneo hayo. La tatu ambalo pia linatokea ni mkandarasi kujikuta ana kazi nyingi na mwisho wa siku ikawa ni ngumu kuzimaliza kwa wakati aliopewa kwa sababu pengine ya usimamizi kuwa mgumu kidogo na hilo pia tutalizungumza kwamba tumechukua hatua.
Mheshimiwa Spika, lakini niseme kama alivyosema mwenzangu mmoja lakini kama alivyowahi kusema kiongozi wetu mstaafu wa Mkoa wa Kagera Mama yetu Prof. Tibaijuka kwamba kadri unavyopanua zaidi ndivyo watu wanavyokuwa na hamu zaidi. Sasa Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita zimeendelea kupanua wigo wa kupata umeme. Katika kupanua wigo wa kupata umeme wananchi wamekuwa wakiuhitaji sana na matumizi yamekuwa ni makubwa na hiyo sasa inapelekea pengine umeme usionekane wa kutosha lakini jitihada za Serikali ni wazi kabisa mambo yataendelea kuwa mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho ambalo naomba nilizungumzie, mimi kwa nafasi yangu ya Unaibu Waziri na kwa jinsi tunavyofanya kazi katika michango mbalimbali iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge nimeona tunayo mambo kama 15 ambayo tunatakiwa kujivunia lakini pia yatakuwa ni chachu ya sisi kuendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha Watanzania wanapata nishati ya umeme katika maeneo yaliyopo na umeme wa uhakika, sahihi, kila wakati na kwa gharama nafuu. Mambo hayo nikiyataja kwa haraka haraka tu, naamini dakika zilizobaki zitanitosha kuyajata hayo mambo 15; la kwanza ni bajeti ya Wizara ya Nishati kuwa na fedha ya maendeleo asilimia 98.9, hii fedha nyingine ni asilimia moja tu. Kwa hiyo, Wizara ya Nishati tumejipanga mkitupitishia kama ambavyo nitaomba mwishoni kufanya kazi kwa fedha tuliyopewa asilimia 98, tunaamini tutafika mbali kabisa.
Mheshimiwa Spika, lakini tumejipanga kuendelea kusimamia bora rasilimaliwatu na rasilimali fedha kama ambavyo imekuwa ikifanyika. Pia tunahakikisha kwamba tunafikisha ile adhma ya kuwa na umeme unaotosha kwa Watanzania wote. Kwa sasa tunao uwezo wa kuzalisha megawatt karibu 1,602, lakini jana usiku ndio tumekuwa na matumizi ya juu megawatt 1,201, kwa hiyo bado tuna kama megawatt 400. Sasa miundombinu ya kuzifikisha hizo zote kwa Watanzania ndiyo ambayo tunaomba sasa mtusaidie ili tuweze kuendelea.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoomba kwamba naomba…
SPIKA: Bado dakika tano.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, eneo la nne ni kuendelea kuzalisha umeme katika miradi mbalimbali mkubwa sana ukiwa wa Mwalimu Nyerere, lakini pia tunayo Rusumo, tumesaini mkataba mwingine wa Malagarasi na tunaamini kwamba tutakuwa katika nafasi nzuri na miradi mingine. Pia tunahakikisha tutapeleka umeme katika vijiji vyote vilivyobakia takribani kama 1,500 kabla ya mwezi Disemba 2022. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuboresha miundombinu yetu ya umeme kwa kufunga vifaa mbalimbali nilivyokuwa navisema, tunafunga surge arrester, combi unit, auto recloser socket breaker, AVR wameitaja hapa asubuhi na vitu vingine kama lightning arrester, tunahakikisha kwamba sasa umeme ukishakuwepo unaweza kuhimili hayo mambo ambayo ni ya kina naturally yanayoweza kuja kuzuia umeme wetu usiwe wa uhakika.
Pia tumejitahidi kutoa kazi nyingi kwa wakandarasi kidogo kidogo ili mkandarasi awe na wigo mdogo wa kufanya kazi na kumaliza, lakini tukiwa tunajenga uwezo wa watu wetu wa ndani kuweza kila mmoja kupata kazi na kumaliza kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tunahakikisha kwamba hakuna anayeuziwa nguzo, Mheshimiwa Waziri atakuja kulisisitiza na kuliweka vizuri. Pia tunaunganisha wateja kwa gharama ya shilingi 27,000 peke yake, Mheshimiwa Waziri atakuja kulisema.
Mheshimiwa Spika, lakini tutahakikisha kwamba katika hiki kipindi cha kupeleka umeme kwenye awamu ya tatu, mzunguko wa pili, tunafungua madawati ya malipo katika maeneo ya wananchi wenyewe. Mtu asifunge safari kufuata sehemu ya kwenda kulipia kilometa 20, 30; madawati ya wenzetu wa TANESCO yatakuwa katika Kijiji au kitongoji ambapo mradi unafanyika. Ilishaelezwa Mheshimiwa Waziri naamini atakumbushia kwamba tutaruhusu hata kulipa kidogo kidogo kwa utaratibu ambao mwananchi atakuwa anaweza ili mwisho wa siku ile shilingi 27,000 iweze kufikia hatua ambayo sasa anaweza kila mmoja akaimudu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini tunafurahi kwamba TPDC imefanya kazi kubwa, asilimia 60 ya umeme tunaouzalisha unatokana na gesi yetu tunayozalisha ambayo inasimamiwa na TPDC. Hilo ni jambo la kujivunia sana.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki tunalo bomba la mafuta limezungumzwa hapa, tunazo fursa kedekede zitakazo kuja. Pia tunafikisha Gridi ya Taifa katika maeneo ambayo hayakuwa na grid, Mkoa wa Kagera ikiwemo, imeshafika Nyakanazi, Mkoa wa Kigoma tutakwenda mpaka Katavi na ni katika muda mfupi sana tutakuwa tumekamilisha yote hayo.
Mheshimiwa Spika, mawili ya mwisho, Wizara imehakikisha inaweka utaratibu mzuri kabisa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Waziri kuhakikisha mkandarasi anampata Mbunge na Mbunge anampata mkandarasi. Tunaamini hilo ni sehemu kubwa ambayo itatuwezesha kujadiliana, kushauriana na kusimamiana vizuri kabisa ili muda utakapofika basi yale tunayo yaahidi yaweze kuwa yamefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho japo siyo kwa umuhimu ninashukuru kwamba wakati haya yote ninayoyasema yanatokea, mimi ni Naibu Waziri kwa hiyo nitakuwa na mimi ninajivunia na historia itakuwa imeandikwa kwangu mimi, kwa familia, lakini na kwa Watanzania wenzangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo mafupi, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzetu mtupitishie bajeti yetu, siyo ndogo ni kubwa, lakini itaweza kufanya yale ambayo mtatuagiza kuyafanya kwa moyo thabiti kama ambavyo mmetusifia na kutusemea vizuri tangu mnaanza na kwa kuendelea kutumwa bila kuchoka kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Watanzania basi wanakipata kile ambacho wanakitarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
WABUNGE FULANI: Kazi Iendelee.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia nafasi ya kujadiliana na kutoa maoni yetu mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, nimesikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge inaonesha nia njema ya kuisukuma nchi kuweza kusogea mbele kwa niaba ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, nilipata maneno, nimeambiwa ni ya kiarabu, yanayosema: “Yashukurunasu lashukurullah.” Nirudie tena kwa ambao hawakusikia, Yashukurunasu lashukurullah, yaani maana yake, asiyemshukuru binadamu mwenzake kwa wema aliomtendea, hawezi hata kumshukuru Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwatendea mema sana Watanzania na kuhakikisha kwamba wanafikia katika ile nchi ya ahadi. Pili, nakushukuru na kukupongeza wewe kwa jinsi ambavyo unaliendesha Bunge letu, nasi wanafunzi wako na Wanasheria wenzako tunajivunia na kuona tulipita kwenye mikono salama kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nawashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa michango yao ambayo nimesema inaonesha kabisa kuwa objective na progressive kwa nia ya kuijenga nchi. Niongeze shukurani na pongezi nyingine kwa wale ambao pengine hawakusemwa hapa; hoja zilizopo hapa zinaihusu Serikali na Serikali inayo watendaji. Siyo watendaji wote wameoza, wameharibika, hawana weledi, ni wezi. Wapo ambao ni wazuri na wanafanya yale mazuri ambayo humu tumekuwa tukimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutufanyia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wangu niwashukuru na niwapongeze watumishi safi wa Umma na tuendelee kuwatia moyo ili wao sasa wasihamie kwenye lile kundi la wengine ambao tunakubaliana hapa kwamba mwisho wa siku tushughulike nao kisawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kwenye maeneo matatu yaliyosemwa kwenye Wizara ya Nishati, nikikubaliana na hoja na ushauri wa maeneo mengine ambao umetolewa kwenye taarifa ya CAG na kwenye Taarifa za Kamati. Yale ambayo sitayasema kwa taarifa zilivyo, tunakubaliana na tunachukua ushauri na maoni na maelekezo yaliyotolewa kwenye taarifa hizo.
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye eneo la kwanza la Symbion. Sitakuwa na mengi sana ya kusema hapa kwenye eneo hili. Mkaguzi amekagua objectively na ametoa maoni yake na yalikuwa matatu. Ameshauri mikataba isimamiwe vyema kwa kuwashirikisha wanasheria; pia ameshauri kabla ya kuivunja, basi tuhakikishe kwamba tunaangalia mapato na hasara za sasa na za baadaye; na pia ameshauri kwamba zile pesa ambazo zimelipwa na Serikali zitizamwe namna bora ya kuziweka kwenye vitabu na hesabu za Serikali ili mikeka ikae vizuri. Hayo ndiyo maoni ya CAG, nasi tunakubaliananayo na tunayafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kwenye eneo la mazuri yaliyotokana na malipo yaliyofanywa baina ya Serikali na huyo aliyekuwa Symbion. Nadhani huko panaweza pakawa panafaa zaidi. Wakati kesi inapelekwa Mahakamani, ilipelekwa ikiwa inadaiwa jumla ya kama Dola bilioni moja na milioni mia tano na zaidi kidogo. Kwa
majadiliano yaliyofanyika nje ya Mahakama, imelipwa kama ilivyosemwa, milioni 153 ambazo zinakwenda kwenye bilioni karibia mia tatu na zaidi kidogo. Kwa hiyo, kwa upande wangu naweza kusema pesa nyingi iliokolewa tofauti na kama tungeendelea Mahakamani na kuwa na mafanikio yasiyokuwa chanya, yaani mafanikio hasi, kwa maana ya kushindwa katika kesi hiyo.
Mheshimiwa Spika, ule mtambo ambao umelipiwa zile fedha, sitaki kusema tumeununua; ule mtambo ambao umelipiwa fedha ikiwa ni maelekezo ya makubaliano, thamani yake kwa wataalamu walioifanya ni karibia Dola 120. Kwa hiyo, kwa kulipa milioni 153, maana yake ni kama tumenunua mtambo. Hizo 153 ndani yake kulikuwa kuna deni la bili za kuuziwa umeme, kuna faini ya kuchelewesha yale malipo ya kulipia umeme na gharama za uwekezaji. Kwa hiyo, ukifanya hesabu ya kawaida, inaonekana kama tulichokifanya kilikuwa ni kitu ambacho ni kizuri kwa maana ya kuokoa pesa ya Serikali, ni kama tumenunua mtambo kwa gharama ambazo zilikuwa zina uhalisia.
Mheshimiwa Spika, mtambo huu wataalamu wameuhakiki na kuukagua kuona unaweza kufanya kazi kwa miaka 15 ijayo mpaka 30 bila kuhitaji matengenezo makubwa. Kwa hiyo, bado ni mtambo ambao uko vizuri na unaweza ukatusaidia kwenye kazi zetu za kuzalisha umeme.
Mheshimiwa Spika, tangu ulipoanza kufanya kazi mwezi wa pili baada ya kuwa umelipiwa mpaka huu mwezi Oktoba mwishoni umeshaizalishia Serikali jumla ya Shilingi bilioni 73 kwa kufanya kazi za kuuza umeme katika muda mfupi huu ambao umefanya kazi. Kwa hiyo kwa hesabu hizo ndani ya miaka kama minne kuanzia tulipolipa ile pesa bilioni 153 za dollar ambazo zimelipwa juzi zitakuwa zimerudi kwenye Serikali na Serikali itaendelea kutumia mtambo huu kwa faida zake.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa tunayo chaangamoto ya upungufu wa maji kwenye vyanzo vyetu vya maji mtambo huu wa Symbion unatumia gesi na hivyo sisi kama Serikali kwa kutumia gesi tuliyokuwa nayo na mtambo wetu tuliyoupata baada ya kumaliza ile kesi nje ya mahakama, tunautumia kupunguza gap la upatikanaji umeme kwa takriban megawatt 112 ambazo zinatoka kwenye mtambo huu. Kwa hiyo kwa ushauri wangu na kwa mchango wangu, nadhani yapo mazuri mengi ambayo mtambo huu unatupatia sisi kama Serikali na ni wa kwetu tunaumiliki sisi wenyewe. Kwa maoni na hoja ya CAG nadhani sasa itoshe tuachane na hii habari tuannze kusonga mbele kwa yale mazuri ambayo yamepatikana kwenye hili eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nijielekeze kwenye eneo lingine la Mradi wa Mwalimu Nyerere. Kwa Nchi yetu ya Tanzania katika miradi mikubwa ambayo tunayo na tuliwahi kuwa nayo mmojawapo ni huu wa trilioni sita na bilioni 500 na zaidi. Ni faraja kubwa sana kwa nchi kuwa na mradi kama huu tunaoutekeleza kwa pesa zetu za ndani. Katika hili lazima tuipongeze Serikali.
Mheshimiwa Spika, pesa hizi zinapatikana kwa wakati katika yale maeneo ambapo Serikali ya Awamu ya Sita imehakikisha inalipa pesa kwa wakati bila kuchelewa hata siku moja madai yanapokuwa yamehakikiwa ni katika eneo hili la Mradi wa Mwalimu Nyerere. CAG alipokagua ameona mambo ya kushauri na kusonga mbele na tunayachukua kwa sababu ni ya kuboresha. Nisemee mambo mawili tu kwa haraka haraka kwa sababu naona kengele ya kwanza tayari imegonga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mambo mawili makubwa ambayo naona nichangie kidogo ni kuhusu muda wa kukamilisha mradi. Ni kweli mradi ulianza 2018 na ulitakiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu ambayo ilikuwa ni Juni mwaka jana. Juni ilipofika mradi ulikuwa haujakamilika kwa sababu ambazo zinafahamika na zinavutana kati ya pande mbili ya Serikali na mtekelezaji wa mradi. Tulikuwa na options mbili sisi kama wasimamizi, tu-abandon mradi kwa sababu muda umeisha au tuwe weledi na wazalendo tuendelee na mradi kwa ku-extend muda huku tukiendelea kuvutana na kubishana kuhusiana na nani mwenye haki, kwenye nini nani kamchelewesha nani na nani kafanya nini? Busara zilituonyesha tutoe kitu kinachoitwa ex-gratia grants of extra time ya kufanya kazi extension of time wakati tukiendelea na majadiliano mengine, nani amechelewesha nini? Nani anamdai nani nini? Nani anatakiwa kumlipa nani?
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.
T A A R I F A
MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na wachangiaji wengi hapa Wabunge ambao wamechangia, kuna suala ambalo tunaliona labda kama huyu mkandarasi alikuwa anamaliza Mwezi Juni na amechelewesha mradi na kimsingi yule anaye chelewesha mradi ndiye anaetakiwa kuomba Serikali au kuomba aongezewe muda. Sasa hoja iliyokuja ni kwamba mtu amechelewesha mradi halafu ameongezewa muda, ameongezewa na fedha na wataalam wetu mahiri kabisa waliofanya ule mkataba walikuwepo, Watanzania kabisa wazalendo wamefanya ile mikataba, wakakubaliana kwa ngazi yeyote kwamba mradi utaisha mwezi Juni, sasa hii ya kuongeza muda na kuongeza fedha ufafanuzi wake ukoje labda inakuaje hii? (Kicheko)
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati, unaipokea taarifa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, mchangiaji hajatoa taarifa, lakini katika mchango wangu sijasema tumeongeza gharama za mradi na nimesema kuhusu kuongezeka kwa muda wa utekelezaji. Kwa hiyo sijasemea kuhusu kuhusu kuongezeka kwa gharama za mradi.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, nadhani nia ni kwamba kwa sababu hii mikataba ambayo tunaingia kwa maana ya Serikali pamoja na hawa wenzetu ambao tunaingia nao mikataba kwa kutoa huduma mbalimbali, upande wa Serikali inaonekana kwenye mikataba pengine si yote, lakini mingi kuwa inalipa ile pesa ya riba kwa kuchelewesha malipo. Sasa huyu mwingine anapochelewesha yeye, Serikali kwa sababu wataalam wapo na mikataba ipo na yeye upande wake analipa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, mkandarasi ana madai yake kwa Serikali na Serikali ina madai yake kwa mkandarasi na kama tungekaa kwenye kuvutana na kubishana tu-establish nani mwenye haki gani kwanza ndio tuendelee na mradi mpaka sasa mradi ungekuwa umesimama. Kwa hiyo alipoomba extension of time kwa sababu alizozileta na akiomba kuongezewa pesa, tumekataa kumwongezea pesa, tumemwambia kwa sababu tuna madai yetu kwako na wewe una ya kwako kwetu hatuja-resolve. Sasa tutakuongezea muda usiokuwa na hayo masharti ya kuongezewa pesa au kuongezeka kwa kitu kingine, tuendelee kutekeleza mradi kwa sababu pesa tunazo na wakati huo tukiendelea kujadiliana nani mwenye haki ya kupata nini.? Kwa hiyo hakuna ambaye mpaka sasa amemdai na kufanikiwa kwa mwenzake kulipa hela ya ziada na sisi tunachokisema ni kwamba hatutalipa pesa ya ziada kwa sababu tunayo madai yetu kwake tukionyesha yeye ndiyo kachelewesha mradi. (Makofi)
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge wawili mmesimama, hiyo taarifa inahusu ufafanuzi aliotoa? Maana ndicho kinachoendelea sasa. Mheshimiwa Mpina.
T A A R I F A
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ndiyo. Mkataba wetu uko very clear, juu ya mkandarasi kuchelewesha mradi anatakiwa kufanya nini? La pili Waziri hapa anatueleza kwamba Mkandarasi ameomba extension of time na Serikali ika-grant extension of time, base ya extension of time waliipata wapi? Kama hawajafanya tathmini ya kazi iliyofanywa na changamoto zilizopo? Utaipata wapi base of extension of time kama ujafanya tathmini?
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, sasa nimeshawaanbia anayeruhusiwa kuuliza maswali ni mimi. Mheshimiwa Naibu Waziri hoja yako imeeleweka, sasa haya maswali ya Mheshimiwa Mbunge, ni maswali, kwa hivyo siyo taariafa. Kwa hiyo endelea na mchango wako wako.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna taarifa nyingine nyuma yako. Mheshimiwa Kigwangalla.
T A A R I F A
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, nilipenda kumpa taarifa mchangiaji anayezunguza kwamba wametoa extensions ya muda ex-gratia kwa favor, kwa huruma, lakini kule kucheleweshwa kwa utekelezaji wa Mradi kwa zaidi ya miaka miwili kumesababisha mazingira ya utekelezaji wa mradi huo yabadilike. Kwa mfano; kuchelesha tu tayari kunabadilisha exchange rate ya kati ya dollar na shilingi na hatimaye leo hii wanapomlipa pesa nyingine za kukamilisha huo mradi wanamlipa kwa exchange rate ya sasa na hasara ambayo imeingia ni zaidi ya bilioni 110 kwa kuchelewesha tu. (Makofi)
SPIKA: Haya, ahsante sana. Waheshimiwa Wabunge, hili jambo nilikuwa najaribu kuangalia hapa kwenye hivi vitabu vya Kamati wameandika azimio kwa namna gani, lakini hoja hii imeshawahi kufafanuliwa hapa na Mheshimiwa Waziri na kueleza ule mradi umechelewa kwa sababu zipi? Alitoa maelezo, lakini sasa kwa maelezo anayotoa hapa Mheshimiwa Naibu Waziri ni maelezo ambayo ni mahususi kwa zile hoja ambazo zimejitokeza hapa, lakini kwa maana ya yale maelezo ya jumla kukusu mradi Mheshimiwa Waziri wa Nishati alishawahi kusimama hapa Bungeni na akaeleza sababu.
Sasa sisi sasa hivi ili tujielekeze vizuri tuko kwenye hoja hizi hapa za Kamati na tunataka tufike mahali ambapo mchango wa Serikali kwa sasa na wao wanachangia kama Wabunge, lakini utatusaidia Bunge kuazimia kwenye yale mambo ambayo Serikali hatujaweza kujiridhisha na kile ambacho wanasema. Kwa hiyo anachoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri ni kile ambacho kimeibuliwa kama hoja, lakini yale mengine ya jumla hayajaletwa bado na CAG na kwa sababu mradi unaendelea CAG atakuja atuambie tu, halafu kwenye ngazi hiyo ndiyo tutashughulika nayo kama haya tunayoshughulika nayo kwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Waziri, malizia mchango wako.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Eneo lingine ambalo naona nilisemee kidogo ni kwenye gharama za mradi zinazohusiana na mabadiliko ya fedha. Miradi mikubwa kama hii inapotengenezewa mikataba inawekewa component mbili, mara nyingi local component na foreign component kulingana na kile ambacho kitatekelezwa kitatumia gharama zipi kubwa? Kwa ilivyofanyika katika mkataba huu gharama kubwa ya utekelezaji wa mradi huu ni mambo yanayotoka nje ya nchi. Kwa hiyo ilikubaliwa kwamba itakuwa ni asilimia sabini ya malipo yatafanywa kwa dollar na asilimia thelathini yatafanywa kwa shilingi ya Kitanzania, kwa sababu supply na mambo makubwa yanapatikana nje ya nchi. Hivyo wataalam walitafuta njia nzuri na namna bora ya kufanya haya. Walijaribu kuhakikisha haifikii sabini ili tuweze kuokoa exchange rate, lakini kwa mazingira na uhalisia ulivyokuwa na wote mnaufahamu mradi huu hatuna haja ya kurudi huko sana ilionekana ibaki sabini kwa thelathini kwa sababu ya uhalisia.
Mheshimiwa Spika, suala pia la kufanya utaratibu wa aging ni kama ku-secure kufanya insurance ya malipo ya baadaye kwenye exchange rate yalitazamwa yote lakini hesabu hazikuleta faida. Kwa hiyo ilikubaliwa kwamba twende na utaratibu huu. Pia kipindi tunaingia mkataba exchange rate tuliyoi-commit ilikuwa na shilingi 2,224.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimwa kengele ya pili hiyo, dakika mbili malizia mchango wako.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniongezea muda. Ilikuwa ni shilingi 2,224 kwa dollar moja. Tangu tumeanza kazi dollar imekuwa ikipanda na kuna muda fulani imefikia mpaka shi2,310.93. Sasa hii pesa bilioni 113 iliyowekwa nilihakikishie Bunge lako na Watanzania haijaliwa wala haijapigwa mtu, ni gharama halisia za mabadiliko ya pesa ambayo hata kwenye biashara zetu za kawaida yanatokea.
Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho kwa haraka haraka, ukwasi wa taasisi zetu ya TPDC na TANESCO, naomba nipende kutoa mchango wangu katika hili.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kunti Majala.
T A A R I F A
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na yote anayotueleza, pamoja na ucheleweshaji, pamoja na hizo exchanging rate lakini ikumbukwe kuwa mradi huu ulitakiwa pia utoe CSSR kwa jamii inayozunguka ule mradi, lakini mpaka leo zaidi ya bilioni 190 na hazijalipwa mpaka leo. Kwa hiyo hilo nalo waweze kuliona kama Serikali kwa namna gani mradi huu unavyoendelea kudidimiza Taifa letu kwenye suala hilo la mradi na mradi kutokuwa na tija kwa Watanzania.
SPIKA: Ungelikuwa umeishia hapo kabla ya swali lako ungekuwa umetoa taarifa, sasa umeuliza swali. Haya mchangiaji malizia mchango wako.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kumalizia mchango wangu kwa kuzungumzia ukwasi wa TPDC na TANESCO. Kwa mara ya kwanza katika historia chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania TANESCO imepewa shilingi trilioni 2.4 kama mtaji na wenzetu wa TPDC wamepewa shilingi trilioni karibia 2.8 kama mtaji kwa ajili ya kuweza kujiendesha. Pesa hizi zimetoka wapi? Serikali imeamua kuchukua jitihada za makusudi za kubadilisha deni lake kwenye Taasisi hizi sasa ibadilike kuwa mitaji. Kwa hiyo yale madeni ambayo Serikali ilikuwa imezikopesha hizi taasisi, lakini inaendelea kulipa yenyewe imezibadilisha sasa ili ziweze kuwa mitaji katika taasisi hizi na hivyo zitakuwa na uwezo wa kujiendesha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.