Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Francis Kumba Ndulane (6 total)

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Wilaya ya Kilwa kuna changamoto inayofanana na Wilaya ya Mtwara katika huduma hii ya maji:-

Je, Serikali ni lini itatekeleza mradi wa maji kutoka Mto Rufiji ili kuwaondolea changamoto ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Kilwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali ina mipango mikakati ya kuona kwamba Mto Rufiji iwe ni sehemu ya miradi mikubwa ya kutoka maziwa makuu na mito, kuona kwamba maji yale sasa yanakwenda kunufaisha wananchi. Hivyo, kwa watu wa Kilwa pia tunaendelea kuwasihi waendelee kutuvumilia kidogo, huenda mwaka 2021/2022 kadiri tutakavyokuwa tunapata fedha, watu wa Kilwa pia watapata maji kupitia Mto Rufiji. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza. Kwa sasa Barabara ya Tingi – Kipatimu ina maeneo mengi ambayo hayapitiki na mengine yanapitika kwa shida sambamba na Barabara ya Nangurukuru – Liwale.

Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuweza kurekebisha barabara hizo mbili ili ziweze kutengenezwa na hatimaye wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, barabara hizi mbili za Nangurukuru – Liwale kilometa 258 na hiyo ya Tingi – Kipatimu katika miaka ya karibuni zilipanuliwa upana wake, lile eneo la hifadhi ya barabara kutoka mita 30 hadi kufikia mita 45. Na hii Hali ilisababisha wananchi kuweza kuvunjiwa nyumba zao na kuondolewa mazao yao. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa wananchi ambao hawajalipwa hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Tingi – Kipatimu ina vilima, na katika swali lake la msingi nimejibu kwamba, tayari TANROADS Mkoa wa Lindi umeainisha maeneo yote korofi ambayo yana vilima na yatawekewa lami. Na hivi tunavyoongea mwaka huu itawekwa walao mita 500 na mwaka wa fedha kama bajeti itapita pia, maeneo yameainishwa ambayo tunategemea kuongeza kiwango cha lami maeneo ambayo barabara inakuwa ina milima na inateleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Barabara ya Nangurukuru – Liwale, yako maeneo ambayo inapita kwenye bonde na maji huwa yanajaa. Na tunategemea kwenye bajeti ya mwaka huu tunayoiendea kama itapitishwa litajengwa tuta kubwa ambapo maji sasa yatakuwa hayana uwezo wa kufurika na kuziba njia hiyo ya Barabara ya Nangurukuru – Liwale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia, ni kweli kwamba, baada ya sheria kupitishwa barabara zetu zimetanuliwa kutoka mita 30 hadi 45, lakini 45 hadi 60. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mita hizi ambazo zimeongezeka saba na nusu, sab ana nusu kwa upande, pale ambapo ujenzi utaanza basi wananchi hawa ambao watakuwa ni wathirika watapata fidia wakati mradi huu utakapoanza kutekelezwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Hospitali ya Kipatimu ambayo imekuwa ikiendeshwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi ya Kanisa Katoliki imekuwa na changamoto kubwa ya mtaalam wa mashine ya x-ray. Itakumbukwa kwamba mwaka 2017 Serikali ilitumia jumla ya shilingi milioni 60 kuleta mashine ya x-ray katika hospitali ile lakini mpaka leo hatujawa na mtumishi wa kitengo hicho.

Je, katika hizi ajira chache 2,726 ambazo zimetangazwa hivi karibuni, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kunihakikishia kwamba moja kati ya watumishi hao atapelekwa katika Hospitali ya Kipatimu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, Mheshimiwa Naibu Waziri au Waziri wa TAMISEMI lini atakuwa tayari kutembelea Wilaya ya Kilwa ili kutambua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa? Ahsante.
(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, mwaka 2017 ilipeleka mashine ya x-ray na mpaka sasa utaratibu wa kumpata mtumishi kwa maana ya mtaalam wa x-ray upo hatua za mwisho na naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ajira hizi ambazo tumezitangaza, tutakwenda kuhakikisha tunapata mtaalam wa x-ray kwa ajili ya kwenda kutoa huduma katika Hospitali ya Kipatimo.

Mheshimiwa Spika, lakini pili niko tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge kufanya ziara katika Jimbo la Kilwa mara baada ya kumaliza session hizi za Bunge Juni 30, 2021. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu namba moja la nyongeza ningependa kufahamu, kwa kuwa katika Mikoa ya Kusini kumekuwa na vyanzo vingi vya maji vinavyotokana na mito mikubwa kama ule wa Rufiji, Ruvuma, Mavuji, Lukuledi, Luhuhu pamoja na Ketewaka kule Njombe. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inamaliza tatizo la maji kwa asilimia 100 kama ilivyofanyika Kanda ya Ziwa kupitia vyanzo hivi vya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Ndulane kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji mzuri. Nipende tu kumjibu swali lake la nyongeza la matumizi ya maji yote yanayopatikana kwenye mito na vyanzo vyote vikubwa vyenye uhakika kwa miradi endelevu. Sisi kama Wizara, mikakati yetu katika mwaka ujao wa fedha na kuendelea, ni kujenga miradi mikubwa inayofanana na mradi huu wa Ziwa Viktoria. Mikakati imekamilika na kwa Kusini pia tumepanga kutumia Mto Ruvuma, Mto Rufiji na Ziwa Tanganyika. Hii yote tutakuja kuitekeleza kadri tutakavyokuwa tukipata fedha. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza, napenda kumwuliza Waziri wa Ujenzi kwamba, kwa kuwa katika mwaka 2019, Serikali ilichepusha katika Kijiji cha Njinjo, barabara ya Nangurukuru – Liwale na hivyo ililazimu kulipa fidia kwa baadhi ya wananchi ambao walikuwa na mali zao katika lile eneo ambalo limechepushwa barabara; lakini kuna wananchi wawili hadi kufikia sasa hawajalipwa fidia ya mali zao; nao ni Mama Mary Mahmoud Kiroboto pamoja na Ndugu Said Salum Karanje, ambao wanadai jumla ya shilingi 13,264,180/ =. Napenda kujua: Je, Serikali ni lini itawalipa wananchi hawa wawili haki yao ya fidia kwa ajili ya kuchepusha kipande kile cha barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, napenda kumwuliza Waziri kwamba, kwa kuwa wakati wa maadhimisho ya Kumbukizi za Vita vya Majimaji ilipotimiza miaka 100 mwaka 2010, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati ule, aliwaelekeza Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Lindi…

NAIBU SPIKA: Uliza swali lako, Mheshimiwa Ndulane.

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nashukuru. Alitoa maelekezo wafungue barabara kati ya Nandete na Nyamwage: Je, mpango huu umefikia wapi wa kufungua barabara ile ya kipande cha Nyamwage kwenda Nandete? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa, Francis Ndulane Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake amesema kwamba, kulitolewa ahadi na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tatu. Napenda tu nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa hii barabara ilitakiwa ifunguliwe maana yake haipo kwenye mtandao wa barabara za TANROAD wala za TARURA. Hivyo napenda nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imelichukua na tutawasiliana na Meneja wa TANROAD Mkoa wa Lindi ili tuweze kupata taarifa sahihi na ahadi hii ili tuweze kuanza kuitekeleza ama kama ilikwama tujue ni kwa nini ilikwama wakati ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili, kama ulivyotoa maelekezo, ni swali ambalo lipo very specific na kama watu hao wapo ni bora wakaandika barua rasmi kwa TANROAD Mkoa wa Lindi, wakupe copy na sisi watupe copy ili tuweze kuliangalia, kwa sababu ni suala la watu wawili, tuweze kuliangalia kama lina changamoto gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa kwa muda mrefu wavuvi wadogo wadogo kutoka katika Wilaya ya Kilwa na maeneo mengine ya nchi yetu ya Tanzania wamekuwa hawapati mikopo kutoka kwenye mabenki kwa ajili ya kufanyia shughuli zao mbalimbali za kuboresha shughuli za uvuvi.

Je, Serikali haioni sasa wakati umefika wa kuweza kuwaundia hawa wavuvi wadogo wadogo mfuko maalum ambao wataweza kukopa kwa riba ndogo na hatimae hiyo mikopo iweze kuwanufaisha katika kufanya shughuli zao za uvuvi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Wilaya ya Kilwa kumekuwa na wimbi kubwa la uingiaji wa wafugaji wenye mifugo mingi sana hasa katika Kata za Somanga, Tingi, Kandawale, Njinjo, Mitole, Likawage, Nanjilinji pamoja na Kikole.

Je, Mheshimiwa Waziri ni lini atafika katika Wilaya ya Kilwa ili kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Kilwa kwenda kutatua changamoto mbalimbali zinazotokana na uingiaji wa mifugo mingi katika Wilaya ya Kilwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ndulane Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Uvuvi kwa ajili ya kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo waweze kupata mikopo ya bei nafuu na yenye riba ndogo. Ninaungana na yeye na ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya Wabunge wote ambao wanasimamia wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa miaka mitano tulionao Wizarani mwaka 2021-2016 wa kuhakikisha tunaupa nguvu uchumi wa blue, jambo hili la kuanzishwa kwa Fisheries Development Fund (Mfuko wa Maendeleo ya Uvuvi) ni miongoni mwa jambo lililopewa kipaumbele. Kwa hivyo, Mheshimiwa Mbunge nikupongeze kwamba umelileta jambo ambalo tayari Serikali imeshaliona na kwa hivyo tunakwenda kulianzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili la kuingia kwa mifugo. Tayari tumekwenda kufanya ziara na nimpe pole sana yeye na wananchi wote, lakini tumekwenda na tumezungumza na makundi mbalimbali, katika Wilaya ya Kilwa nilifika katika Kata ya Nanjilinji kwenda kuzungumza na wananchi pale lakini niko tayari kurejea tena ili kusudi tuweze kufika kule kote alipotaja Mitole, Njinjo, Likawage, Kandawale na hata kule Miguruwe na Zinga Kibaoni, ili kuweza kwenda kuzungumza na wananchi kwa niaba ya maombi haya ya Mheshimiwa Mbunge na hatimaye kuweza kupata suluhu ya tatizo hili kubwa ambalo linawasumbua wananchi wa Kilwa Kaskazini. Ahsante sana. (Makofi)