Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jacquline Andrew Kainja (4 total)

MHE. JACKLINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii niweze kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na kwamba tunajua Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inajitahidi kupunguza ajali za bodaboda, tukiangalia kwa mwaka 2019 tulikuwa na ajali 567 lakini mwaka 2020 tuna 240. Je, Jeshi la Polisi lina mpango gani wa kuhakikisha ajali hizi zinapungua zaidi? Tukiangalia wahanga wakubwa ni vijana na wanawake ndiyo wanaopata shida ya kupoteza vijana ambao ni nguvukazi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; utafiti unaonyesha askari wastaafu wanachelewa kupata mafao yao, je, Wizara husika ina mpango gani wa kuhakikisha askari hawa baada ya kustaafu wanapatiwa mafao yao kwa haraka ili kuepusha wanapokuwa kazini kuchukua rushwa ili kujilimbikizia akiba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika jibu la msingi inaonekana Mheshimiwa tumempa sababu moja au njia moja ambayo tunaweza tukaitumia katika kuepuka hizi ajali. Zipo njia ambazo tumeshazichukua kama Serikali na nyingine tuko mbioni kuzichukua kwa kushirikiana na Wizara nyingine au kushirikiana na taasisi nyingine kuhakikisha kwamba hizi ajali za barabarani zinapungua. Cha kwanza tumefikiria kuendelea kuwafundisha zaidi hasa vijana wa bodaboda namna ya kutumia alama za barabarani ambazo zina uwezo mzuri wa kuwaeleza kwamba wanakoelekea wanaweza wakapata ajali.

Mheshimiwa Spika, lingine tuna mpango sasa wa kutengeneza mfumo wa kufunga au ku-control ajali kwa kutumia vidhibiti mwendo, ambapo tunahisi hivi vinaweza kupunguza ajali. Pia tuna mpango wa kufanya marekebisho ya sheria ambayo yanakwenda moja kwa moja kwenye masuala ya faini na adhabu katika mambo haya ya usalama barabarani.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge atusaidie pia kuwaelimisha vijana kwa sababu naamini katika mkoa wake vijana wa bodaboda wapo, basi azidi kuwaelimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kujibu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kuhusu mafao ya Askari. Kwa kweli Wizara inajitahidi sana kuhakikisha kwamba tunawalipa wastaafu posho zao mara tu baada ya wao kustaafu. Katika kipindi cha 2018/2019 tumejitahidi kati ya wastaafu 591; jumla ya wastaafu 479 tayari tulishawapatia mafao yao na sasa hivi wengi wanaishi maisha mazuri.

Mheshimiwa Spika, kikubwa kinachokuwa kinatukabili kama sehemu ya changamoto, inafika wakati inakuwa OC nazo na bajeti nayo inakuwa mtihani, kwa hiyo, ndiyo maana kuna wakati wanachelewa kidogo kulipwa. Hata hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kama itakuwa kuna mtu ambaye hajapata mafao yake na amestaafu, basi tukitoka hapa tuonane, tuone tunamsaidia vipi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na jitihada nzuri za Wizara inavyofanya kuzitangaza zao la asali nchini, lakini bado hatujafanya vizuri kwa masoko ya nje ambayo inapelekea wafanyabiashara wengi wa nchini wanashindwa kufanya vizuri kwa masoko ya nje hususan ni Mkoa wa Tabora na tukiangalia kinamama wengi wa Mkoa wa Tabora wamejikita kwenye uvunaji wa asali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Wizara inakuja na mkakati upi kuhakikisha soko la nje la zao la asali linafanya vizuri kama ambavyo zao la asali linafanya vizuri ndani ya nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, pamoja na jitihada nzuri zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuhakikisha zao la asali linaendelea kuwa na thamani, mpaka kupata wafadhili kutoka Umoja wa Ulaya.

Je, Wizara imeweka mikakati ipi na mipango madhubuti ya kutenga pesa kwa ajili ya kuhakikisha mradi huu walioweka kusaidiwa na Umoja wa Ulaya unaweza kuendelea hata kama mradi ule, hata kama wafadhali watachelewesha pesa au hawatoleta pesa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jacqueline, Mbunge wa Viti Maalum Tabora kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tabora Mheshimiwa Jacqueline kwa kuona umuhimu wa zao hili la asali. Ni kweli Tanzania tunafaidika kwa asilimia kubwa kwa soko hili la asali kuuza ndani na nje ya nchi. Mkakakati wa Wizara na Serikali kwa ujumla ni kuhakikisha kwamba asali yetu inakuwa na ubora zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba kwa sasa hivi wizara inashikirikiana na Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani kupeleka sampuli za kemikali za asali ambazo huwa zinachakatwa na kuangalia ubora wa asali ya Tanzania. Na kwa asilimia 90 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 tulipeleka asali yetu ya Tanzania na ikaonekana kwa asilimia 90 ni nzuri na inafaa kuuzwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Tanzania sasa itaanza kupeleka asali kwenye nchi za Ulaya na Marekani kwa kuwa tumekidhi vigezo vya viwango vya ubora wa asali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwenye mikakati ya kutenga fedha nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa sasa tuna mkakati wa kuanzisha viwanda vitano. Viwanda vitatu tayari vimeshajengwa na viwili tunakarabati. Lakini pia hii ni mwanzo wa kuhakikisha kwamba tayari tuna vyanzo vyetu sisi wenyewe bila kutegemea misaada mingine ambavyo vitaweza kukusanya asali yote nchini na itachakatwa kwenye viwanda hivi na kuhakikisha soko la ubora wa asali linapatikana na tunaweza kuuza nje na ndani ya nchi. Ahsante. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Kutokana na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri yanayowapa matumaini wafanyabiashara wa usindikaji wa mbogamboga hasa kwa Mkoa wa Tabora hususan kinamama.

Je, ni lini Serikali kushirikiana na FAO inaweza kuanza mradi huu wa kuwawezesha kina mama kuweza kufanya biashara ya Kitaifa na Kimataifa?

Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi kuwezesha mazao haya ya usindikaji wa mbogamboga ambayo wakinamama wengi wa Mkoa wa Tabora wamejikita katika biashara hiyo kuhakikisha kwamba yanakuwa yana masoko ndani ya nchi na ukizingatia unaweza ukaenda kwenye hoteli nyingi hatuna mboga za asili, tunatumia mboga ambazo ni roast na zilizoungwa ungwa zaidi. Naomba kupata jibu, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naoba kumjibu Mheshimiwa Jacqueline maswali yake ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, lini tunaanza mradi wa FAO, tunaaza mwaka wa fedha unaokuja; ni mradi wa miaka mitano, tunaanzia majaribio katika Wilaya ya Kaliua ndipo tutakapoanzia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kuwasaidia wakinamama wa Mkoa wa Tabora na Watanzania wote kuweza kuingia katika masoko. Sasa hivi tunapata project pamoja na wenzetu wa SIDO ili waweze kukidhi vigezo vya viwango vinavyoweza kuwasaidia kuingia katika masoko ndio maana mmesikia katika Mkoa wa Tabora tumesema kwamba Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Umoja wa Wanyabiashara sasa hivi pamoja na SIDO inatafutwa eneo moja ambalo litakuwa ni center ya kina mama kwa ajili ya kukaushia na hapo kuweza kufanya packaging waweze ku- meet standard za masoko. Kwa hiyo, ni hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo la msingi sio tu kuzalisha, je tunachokizalisha kinaweza kukidhi vigezo vinavyotakiwa vya sokoni, hiyo ndio kazi tunayoifanya katika sekta ya mbogamboga na matunda.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwamba na wewe umeweza kuona hili swali halijajibiwa na mimi nimegundua hivyo, lakini nimpongeze Waziri kwa majibu mazuri yanayoonyesha namna gani Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan imeendelea kupanga bajeti kuendelea kuhakikisha maboma ambayo yanatakiwa kukamilishwa yakamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tu nipatiwe majibu mazuri, ambayo yanaendana na swali langu ili niweze kuridhika sasa kwamba ni lini Serikali inaweza ikaona kuna mpango mzuri kwenye hizi Kata ambazo ni kubwa hazina zahanati ili wananchi hawa waweze kupata zahanati na siyo kwamba kuna maboma hakuna hata hayo maboma ambayo yanatakiwa kukamilishwa yaani ni ujenzi mpya, Serikali ina mpango gani na njia ipi madhubuti kuhakikisha kwamba Kata ambazo ni kubwa mfano, Kata hii ya Ng’ambo ambayo iko Tabora Mjini na zingine nyingi ambazo sijaziainisha zinaweza kupata ufumbuzi huo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa sasa Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwanza tunamaliza ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Tarafa zote nchini. Tangu uhuru tulikuwa tuna Tarafa 570 na tulikuwa na Tarafa 363 tu pekee ambazo zilikuwa na Vituo vya Afya na katika Awamu ya sasa hivi tulikuwa na Vituo vya Afya kama 207 ambavyo Serikali tayari imeshapeleka fedha kwa awamu mbili ambazo nafikiri kila Mbunge anazo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tukija kwenye level ya zahanati kwa kila Kijiji lengo la Serikali ambalo tumeliweka na ndiyo maana nimejaribu kuelezea hapa fedha ambazo tumezitenga ni kwa ajili ya kwenda kumalizia zahanati ambazo zimeanzishwa na nguvu za wananchi na nyingine zimeanzishwa na mapato ya ndani ya Halmashauri na ndiyo maana kwenye swali hili la msingi lilipokuwa linaulizwa, tumemshauri Mbunge wa Jimbo na Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Tabora kwamba, hamasisheni wananchi mkishirikiana na vyanzo vya ndani muanze ujenzi ili sisi kutoka Serikali Kuu tulete fedha kwa ajili ya kumalizia hiyo zahanati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukisema kwamba tutajenga zahanati vijiji 12,000 kwa wakati mmoja kwa sasa hivi hatuwezi kudanganya kwenye hilo, ukweli wetu ni kwamba tunamaliza Vituo vya Afya Tarafa zote, tunamaliza Hospitali katika Halmashauri zote halafu kwenye ngazi ya vijiji tutapeleka fedha, kwenye vijiji vyote ambavyo zahanati wananchi wamepeleka nguvu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hilo ndiyo jibu letu, ahsante. (Makofi)