Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Hamad Hassan Chande (16 total)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushuru Mheshimwa Spika, kwa kunipa nafasi ya kuuliza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa chande kwa kuteuliwa kupata nafasi hiyo, tunakuombea kwa Mungu akusaidie ili uweze kuona mbele zaidi, kwake nina swali moja tu. Kwa kuwa humu ndani ameandika sheria nyingi za mazingira, sasa swali ni lini atafika kwenye Jimbo la Bunda kwenye Vijiji vya Nyabuzume, Jabulundu na maeneo yaliyoharibiwa na barabara inayojengwa ya lami kutoka Butiama -Nyamswa na Sanzati ili kuangalia athari za mazingira katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Getere, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, siku za karibuni mara tu baada ya Bunge kumalizika tutafuatana mguu kwa mguu mimi na yeye twende kuangalia hali hiyo na insha Allah tutekeleza. (Makofi)
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa mabadiliko ya tabia ya nchi yanaendelea kuathiri vyanzo na miundombinu ya maji kule kijijini Nungwi jambo ambalo limepelekea kuwa na kero kubwa kwa Watanzania wanaoishi maeneo yale. Napenda kusikia kauli ya Serikali ni lini mradi huo unaozungumziwa hapa unatarajiwa kuanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Mheshimiwa Waziri ni lini atakuwa tayari kuongozana na mimi kwenda kuangalia moja kwa moja uhalisia wa athari ya mabadiliko ya tabia nchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kwa idhini yako nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Simai kwa juhudi yake ya kufuatilia miradi mbalimbali katika Jimbo lake ikiwepo miradi ya maji kwa kweli ni mwanaharakati mkubwa kufatilia maendeleo ya maslahi ya jimbo lake na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara tu baada ya utaratibu wa kifedha utakapokamilika mradi huu utaenda kutekelezwa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tupo katika harakati za kufatilia taratibu hizi za kifedha zikamilike ili kusudi kwenda kutekeleza mradi huo katika eneo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili mara tu baada ya kumaliza kikao hiki mwishoni mwa mwezi huu tutafuatana mimi na yeye twende tukaone athari hiyo ambayo inajitokeza ndani ya jimbo lake, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri bado nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tumeona jitihada mbalimbali za wananchi wakizichukua kwa makusudi katika kupanda mikoko kwa lengo na madhumuni ya kuhifadhi mazingira, kuongeza mazalia ya samaki lakini kuzuia maji ya bahari kupanda nchi kavu. Mfano mzuri ni wananchi wa Kijiji cha Mjini Wingwi na Sizini Wilaya ya Micheweni. Swali la kwanza, je, Serikali inawapa matumaini gani wananchi hawa wa Mjini Wingwi na Sizini kwa kuwapatia misaada ya kifedha na vifaa kama boti kwa ajili ya patrol kama sehemu ya kuhamasisha na kuwapa moyo kuendelea na jitihada hizo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufuatana nami baada ya Bunge hili mpaka kwenye Kijiji cha Mjini Wingwi na Sizini kwa lengo la kwenda kuona jitihada za wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu maswali haya, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Omar Issa kwa juhudi yake ya kutunza mazingira katika maeneo yake.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anauliza Serikali itawapa matumaini gani wananchi? Serikali kwa sababu inasikiliza na inathamini juhudi za wananchi, naomba hili tulichukue na baadaye tutakaa pamoja naye na wataalamu wetu tuone namna gani tunawapatia motisha wananchi ambao wanajitahidi kutunza mazingira.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili mimi niko tayari kabisa kufuatana naye baada ya Bunge hili kwenda kuona na kutafuta njia sahihi ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali na pia niishukuru Serikali kwa kupeleka fedha katika maeneo hayo ya ujenzi wat uta hilo. Na nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa, miradi hii inagharimu fedha nyingi katika utekelezaji wake, lakini katika utekelezaji huo Serikali haikutumia mafundi wazuri na hatukupata matokeo mazuri katika ujenzi wa tuta hilo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia mafundi bobezi ili wananchi waweze kunufaika na ujenzi huo wa tuta?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, Naibu Waziri atakuwa yuko tayari kufuatana nami ili kwa macho yake aende kushuhudia ujenzi wat uta uliofanyika katika phase II ya TASAF Awamu ya Pili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali haifanyi shughuli zake kwa kubahatisha upo utaratibu maalum ambao umeandaliwa wa kutumia wataalamu bobezi. Wataalam ambao wana uwezo mkubwa wa kujenga miradi hiyo, ili ufanisi uweze kupatikana.

Mheshimiwa Spika, lakini swali lake la pili, niko tayari kwa sababu ya juhudi zake ambazo nimeziona katika jimbo lake kufuatananaye bega kwa bega, hatua kwa hatua mpaka katika jimbo hilo kuona sehemu husika.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tatizo linalowaathiri wananchi wa Nanguji na Kiwani linafanana kabisa na tatizo linalowaathiri wakazi wa Kijiji cha Kojani. Na kwa kuwa, wananchi wa Kijiji cha Kojani wamekuwa wakilalamika muda mrefu kuhusiana na suala la maji ya bahari kuwaathiri katika makazi yao ya kudumu. Je, Serikali ina mpango gani au inaweza kuweka mkakati gani ili kuweka ukuta, pamoja na alama, lakini ili kunusuru makazi ya wananchi wa Kijiji cha Kojani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kojani ni ndani ya jimbo lang na Kojani ni sehemu yangu nitashawishi Serikali na kuandika miradi tofauti kwa ajili ya kuhami kisiwa hicho cha Kojani. (Makofi)
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa wazee hawa walifanya kazi kwenye Serikali hii, walitumia vigezo gani kuwa walipwe kiinua mgongo na wasilipwe pensheni yao ya kila mwezi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Je, Waziri yuko tayari kwa ruhusa yako kuungana nami kwenda kuwaona wazee hawa kuwapa maneno mazima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. HAMAD HASSAN CHANDE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said wa Jimbo la Magomeni kwa juhudi yake ya kufuatilia wazee kupata stahiki zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo ambavyo tumetumia ni Kanuni, Taratibu na Sheria ambazo zimewekwa na kama hatukutumia vigezo hivyo, basi ingekuwa ni kinyume na taratibu. Hivyo basi, Serikali bado iko na usikivu. Serikali yetu ni sikivu, Mheshimiwa Mbunge anao uwezo wa kupeleka malalamiko tena na tutayazingia kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, Swali la pili, niko tayari kabisa mimi na Waziri wangu kufuatana naye kwenda kushuhudia jambo hilo, Inshaallah. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze Serikali kwa juhudi wanazozifanya katika kutafuta majawabu ya eneo hili. Lakini vilevile nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya matumaini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Msimbazi sasa hivi umepoteza kina kutokana na kujaa michanga mingi sana kiasi kwamba tupo katika kipindi cha mvua, kipindi ambacho maji hutapakaa na wananchi wa maeneo ya Kigogo Jaba, Kigogo Kati, Kata ya Mzimuni, Daraja la Magomeni na hata Kata ya Magomeni yenyewe, pale wanapata athari kubwa sana ya mafuriko.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba commitment ya Serikali kwamba wasaidie juhudi za wananchi katika maeneo hayo, juhudi ambazo zinaongozwa na Madiwani wangu Mheshimiwa Richard Mgana, Mheshimiwa Loto na Mheshimiwa Nurdin katika kuondoa mchanga katika maeneo yale ili mvua hizi zisilete athari tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, changamoto hii pia…

NAIBU SPIKA: Hilo swali la pili nenda moja kwa moja kwenye swali.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ningemuomba Mheshimiwa Waziri aambatane nami kutembelea Kata za Tandale, Magomeni, Ndugumbi, Makumbusho, Kijitonyama, Mwananyamala na Hananasif ili kwenda kuona athari za mto Ng’ombe kutokana na mafuriko vilevile ili aweze kusaidia juhudi za Serikali ambazo zimeshaanza kuujenga mto huo. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Abbas Tarimba Gulam kwa juhudi yake ambayo anaifanya katika jimbo lake la Kinondoni. Lakini pili kuwa ni Mwenyekiti wa Bunge Sports Club kwa awamu ya pili nadhani. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tarimba. Swali la kwanza, kwa kuwa juhudi imeshafanyika kwa wananchi wa Jimbo la Kinondoni katika kuhami, kuokoa mafuriko ambayo yanatokea katika Mto Msimbazi, basi Serikali ipo tayari kushirikiana nao kwa ajili ya kuondoa mchanga huo kuongeza kina cha maji, kuongeza kina cha mto ili maji yaweze kupita kwa usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lake la pili, niko tayari Mheshimiwa Abbas kufuatana na wewe kwenda katika sehemu inayohusika. Ahsante sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, Mkoa wa Arusha una mito mingi ambayo ni vyanzo vizuri vya maji na vilevile ni vivutio vya utalii. Kama vile Mto Temi, Mto Nduruma na n.k. Lakini mito hii mingi imetekelezwa na kupelekea kukauka maji kutokana na shughuli nyingi za kibanadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu kwa Serikali, Je, Serikali inampango gani wa kuirudisha mito hii katika hali yake ya asili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo katika harakati ya upandaji wa miti kuimarisha mazingira ili kuhami mito hiyo iweze kuwa salama na kurudi katika hali ya kawaida.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuuliza swali ambalo linafanana na ambalo muuliza swali wa kwanza alivyouliza.

Swali langu ni kwamba katika Mji wetu wa Tarime Mjini lipo korongo maarufu kama korongo la starehe, na korongo hili limekuwa hasa wakati wa mvua linaleta madhara makubwa maana linapitisha maji mengi na hatimaye linahatarisha nyumba za wakazi ambao wanaishi kandokando ya korongo hili.

Je, Serikali ni lini litajenga Korongo hili ili at least wakazi ambao wapo katika mtaa huu waweze kuwa na uhakika wa makazi yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tutatuma wataalam wetu kwenda kuangalia na kufanya tathmini katika Korongo hilo ili kusudi wataalam hao walete tathmini ambayo ni sahihi kwa ajili ya kufanyia kazi ndani ya mwaka wa fedha ujao. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa changamoto zilizopo ndani ya Jimbo la Kinondoni kuhusiana na Mto Msimbazi ni sawa kabisa na changamoto zilizopo katika Mto Mbezi na Mto Mpiji ndani ya Jimbo la Kibamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ni lini sasa itaanza kutengeneza kingo za mto Mbezi ili kuokoa taasisi za Serikali mashule lakini vile vile na nyumba za wananchi, kuondolewa na maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kwa juhudi yake ya kupitia na kufanya mambo yaliyomengi ndani ya Jimbo la Kibamba. Kwa hakika Serikali ipo tayari kufanya tathimini ama inafanya tathmini juu ya jambo hilo mara tu mwaka wa fedha tutakapopata idhini ya fedha za kutosha basi tutapita ndani ya Jimbo hilo na kutatua changamoto ambazo zinazikabili Jimbo la Kibamba.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa Korongo hili kwa msimu wa mvua wa mwaka 2020 na mwaka 2021, nyumba 29 za wananchi zimechukuliwa na maji.

Je, Serikali ina mpango gani kupitia Mfuko wa Maafa kuwasaidia wananchi hawa ambao wameathirika kwa kuchukuliwa na nyumba zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ili kuona ukubwa wa tatizo hili, ni muhimu sana Waziri na timu yake ya wataalam wa mazingira kutembelea eneo hili ili kuona wenyewe uharibifu ambao umetokea pale: Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana nami katika eneo lile ambalo imetokea shida hii ajionee mwenyewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Malima kwa juhudi yake ya ufuatiliaji katika mto huo na Jimbo lake kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, pili, nampa pole Mheshimiwa Mbunge kwa maafa ambayo yametokea katika mvua zilizopita. Ni kawaida ya Serikali, inapotokea maafa katika sehemu yoyote kufuatilia, kufanya tathmini na kuwafariji watu hao ambao wamepata maafa katika sehemu mbalimbali. Kwa hiyo, nimtoe shaka kwamba, Serikali itafuatilia na itakwenda kuwafariji watu waliopata maafa katika sehemu hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili. Mimi pamoja na timu yangu ya wataalam, niko tayari kabisa kufuatana na yeye baada ya Eid El-Fitr twende wote kuona hali ilivyo Inshallah. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwanza nimshukuru Naibu Waziri kwa kunijibu vizuri na Watanzania wamesikia jinsi gani vyuma chakavu vilivyokuwa vinafanya kazi ya kusaidia jamii, lakini hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa suala la vyuma chakavu limekuwa sugu ingawa mazingira wameiwekea kanuni na kwa kuwa suala hili la mazingira limeshamiri la watu kuiba vyuma chakavu kwamba imekuwa kama ni mtaji wao na inaipa taabu Serikali katika kudhibiti ambavyo vyuma kama alivyozungumza Mheshimiwa Waziri.

Je, wako tayari kutuletea sheria itakayokuwa kali inayohusu vyuma chakavu ili tuipitishe hapa Bungeni iweze kusaidia jamii?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa baadhi ya wezi wanaohujumu vyuma chakavu wengi wao wanatumia vilevi ambavyo havikubaliki na jamii ambao kama mfano wanaokula unga, hao ndio jamii kubwa inayofanya kazi hizo za kubeba vyuma chakavu ambavyo vimo katika mitaro ya maji.

Je, suala hili Serikali inalijua na kama inalijua imeliangaliaje…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Fakharia umeshauliza maswali mawili tayari.

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, Insha Allah nataka nijue hayo mawili ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli sheria zilizopo zinatosha kabisa, lakini ushauri unazingatiwa, kimsingi Mheshimiwa Mbunge tuondoe na tuache tu muhali wale watu ambao wamefanya makosa tuchukue hatua na kuwapeleka sehemu ambayo inayohusika. Ahsante. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo ameyaweka mbele ya Bunge lako Tukufu, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Fakharia, ni kweli kabisa wengi kati ya vijana ambao wamekuwa wakijihusisha na shughuli hiyo wamekuwa na dalili zote ambazo zinaviashiria vya matumizi ya dawa za kulevya za aina mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kulevya na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya inachokifanya kwa sasa ni kuanzisha klabu mbalimbali katika mitaa na shule na maeneo mbalimbali kwenye nchi yetu ili kuweza pia kuwabaini hata hao vijana wanaojihusisha na shughuli hizo na shughuli nyingine tu, lakini wanaendelea kutumia dawa za kulevya na lengo letu ni kuwasaidia kuwaondoa huko na kuwaleta katika biashara ambazo hatawajihusisha tena na matumizi ya dawa za kulevya. Kwa hiyo tutaendelea kufanya kazi hiyo nzuri, lengo la Serikali ni kuhakikisha Tanzania bila matumizi na biashara ya dawa za kulevya iwezekane na tuweze kusonga mbele. (Makofi)
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naishukuru Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Muungano kwa niaba ya Waziri wa Fedha kwa majibu mazuri ambayo nafikiri sasa yataielekeza nchi yetu kuwa shirika hili ni la Serikali kwa mujibu wa sheria.

Swali langu ni moja tu kwamba kwa vile Serikali imeelekeza taasisi za Muungano na taasisi zote za Serikali kutumia Shirika la Bima la Taifa sasa kwa nini Serikali hairudi na kuelekeza wananchi wake ili waelewe kwamba Shirika la Bima la Zanzibar ni Shirika la Kiserikali na wana wajibu pia wa kutumia kulingana na huduma zao wanakavyoona ni nzuri na mimi nikiwathibitishia wabunge kwamba huduma hizo ni nzuri? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Najma kwa juhudi yake ya ufuatiliaji wa kero za wananchi na kwa namna anavyopambana kwa wananchi wote, kwa kweli naomba hili tulichukue kama ni wazo, ni ushauri na tutalifanyia kazi. Tutashauriana na Serikali kulifanyia kazi jambo hili, ahsante.

MHE. AMOUR K. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza sijajua kwa nini mikoa ya Zanzibar haijaorodheshwa hapa, lakini pia sijajua Serikali inawezeshaje makundi haya 157 ili kumudu kazi hii ngumu sana?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Kwa kuwa zipo dini ambazo zinajinasibu na kujitahidi kusema kwamba kila kitu kitakachotokea duniani kwenye vitabu vyao wameeleza: Je, Serikali imeshaona umuhimu wa kuwashauri viongozi wa dini katika kuondoa tatizo hilo ambalo ni gumu sana hata pale Zanzibar ambapo visiwa ndiyo vinaondoka?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khamis Amour Mbarouk kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Amour kwa juhudi yake ya kufuatilia masuala ya mazingira kule visiwani Zanzibar. Suala lake la kwanza ni kweli kwamba ipo haja ya kuhamasisha vikundi mbalimbali katika sehemu zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na tayari tumewasiliana na wenzetu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kule Zanzibar kwa ajili ya kuhamasisha wananchi wa Kanda za Pwani ili kusudi kuanzisha vikundi kama hivi kwa lengo la kutunza mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kwa kweli tunachukua hoja yake hii kwamba upo umuhimu wa kushirikisha taasisi za dini. Tumeanza kuwaita viongozi wa dini na kuzungumza nao kuhusu suala la utunzaji wa mazingira. Kwa mwelekeo ambao tunakwenda nao sasa, ni lazima tuzishirikishe taasisi za dini kuhusu suala la utunzaji wa mazingira, kwa sababu wao kwa asilimia kubwa wanakaa na wananchi. Kwa hiyo, tutawaomba viongozi wa Makanisa ama Misikiti iwe ni sehemu ya mahubiri yao ya utunzaji wa mazingira ili mazingira yetu yawe salama kwa maslahi ya Taifa letu. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Huko nje hasa katika ukanda wa bahari, sisi tunatokea kwenye visiwa, hali ni mbaya sana kuhusu masuala mazima ya mazingira. Wakisema kwamba waanzishe vikundi, kwamba vikundi ndiyo viwe vinasimamia mazingira katika kukusanya taka, bado elimu haijafikiwa. Yaani wananchi walio wengi wanazalisha taka, lakini hawana taaluma ya utunzaji wa hizo taka hasa kwenye upande wa mazingira. Je, nini kauli ya Serikali juu ya usimamizi wa masuala mazima ya utoaji wa elimu ya usimamizi wa mazingira? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asya, ni kweli kabisa anachokisema Mheshimiwa Mbunge kwamba elimu bado ni ndogo, lakini tumieandaa programu maalumu za kutoa taaluma kwa wanavikundi na wananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Spika, jibu langu la pili la nyongeza nilisema kwamba tutaenda mpaka kwa taasisi za dini ili suala la taaluma liwe na wigo mpana. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba taaluma hiyo ya utunzaji wa mazingira itafika nchini kote.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, Waziri anaweza kutueleza ni mafanikio yapi yamepatikana katika mpango huo toka umeanza kutekelezwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Bagamoyo imekumbwa na changamoto kubwa sasa hivi ya kumegwa ardhi na maji ya bahari na hasa katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo na maeneo mengineyo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inadhibiti hali hiyo isiweze kuendelea.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Muharami kwa juhudi yake ya ufuatiliaji wa mazingira lakini na mabadiliko ya tabianchi katika Jimbo lake la Bagamoyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio ambayo yamepatikana katika miradi hii, moja; ofisi tano za BMUs tumejenga katika Wilaya za Bagamoyo na Pangani. Sehemu ambazo zimejengewa ofisi hizo na kuzipatia samani ni pamoja na Saadani, Chalinze; Zingibari, Mkinga; Kipumbwi, Pangani; Dunda, Bagamoyo; na Sudimtama na tumewanunulia viatu na makato kwa ajili ya kusimamia usafi huu wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ni kweli kwamba Bagamoyo ni moja ya kati ya sehemu ambazo zina changamoto kubwa za mabadiliko ya tabianchi, lakini tayari ofisi yetu imeshapeleka watalaam kufanya upembuzi yakinifu na kufanya survey ambayo ni sahihi na watalaam hawa wameshaleta majibu, siku za karibuni hivi basi mradi utaanza kutekelezwa katika eneo hilo. Ahsante.