Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Hamad Hassan Chande (12 total)

MHE. BONIPHACE M. GETERE Aliuza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kufukia mashimo makubwa yaliyosababishwa na ulimaji wa barabara na uchimbaji wa madini hasa katika Mikoa ya Mara, Geita na Shinyanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004 inaelekeza maeneo yaliyoharibiwa kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini kurejeshwa katika hali yake awali ikiwemo kufukia mashimo, kupanda miti na kudhibiti taka. Aidha, wamiliki wa migodi yote wanatakiwa kuweka Hati Fungani (Environmental Performance Bonds) kama dhamana ya Usimamizi wa Mazingira katika migodi husika.

Aidha, Sheria ya Madini, Sura ya 123 inawataka wamiliki wote wa leseni za uchimbaji madini kuhakikisha uzingatiaji wa utunzaji wa mazingira katika maeneo ya uchimbaji wa madini ikiwemo ufukiaji wa mashimo yatokanayo na shughuli hizo.

Mheshimiwa Spika, Mikakati mbalimbali imewekwa ili kuzingatia utekelezwaji wa Sheria hizi ikiwemo:-

(i) Serikali kupitia Kamati ya Kitaifa ya Kufuatilia Utekelezaji wa Mipango ya Ufungaji Migodi inahakikisha hatua zote za urejeshwaji wa maeneo ya uchimbaji ikiwemo kufukia mashimo yaliyotokana na shughuli za uchimbaji zinazingatiwa ipasavyo; na

(ii) Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika migodi husika mara kwa mara imekuwa ikifanya ufuatiliaji na ukaguzi wa uzingatiaji wa matakwa haya ya kisheria.

Mheshimiwa Spika, mashimo makubwa yote yaliyotokana na uchimbaji wa madini katika Mikoa ya Mara, Geita na Shinyanga yanapaswa kufukiwa. Serikali inaendelea kufuatilia na kuhakikisha kuwa matakwa haya ya kisheria yanazingatiwa. Aidha, kwa upande wa mashimo makubwa yanayotokana na ulimaji wa barabara, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeendelea kuhimiza uzingatiaji wa masuala ya hifadhi ya mazingira wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI Aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kufanya mapitio kuimarisha miundombinu ya miradi ya maji ya African Adaptation Program (AAP) iliyojengwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi ili kuondokana na mahitaji makubwa ya maji kutokana na ongezeko la watu katika Jimbo la Nungwi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya ufadhili wa Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la UNDP ilitekeleza mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kupitia African Adaptation Program (AAP) mwaka 2011 katika eneo la Nungwi, Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja na kufaidisha jumla ya watu 11,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa ipo haja ya kufanya mapitio ya kuimarisha miundombinu ya miradi ya maji kupitia mpango wa African Adaptation Program (AAP) ili kukabiliana na mahitaji makubwa ya maji kutokana na ongezeko la watu katika Jimbo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaandaa mpango wa kuimarisha miondombinu ya maji katika maeneo mbalimbali Unguja ikiwemo eneo la Nungwi kupitia Mradi wa Uimarishaji wa Usambazaji Maji Safi na Salama na Misingi ya Maji Machafu Zanzibar chini ya mkopo wa Benki ya Exim ya India. Katika mpango huo, matenki mawili ya zege yatajengwa, moja la lita 500,000 na lingine la lita 300,000 ambapo mtandao wa maji utakuwa na urefu wa kilometa
14. Ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaweka matumbawe bandia na kupanda mikoko katika bahari ili kurejesha mazalia na makulia ya samaki yaliyoharibika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kuweka matumbawe bandia katika maeneo kadhaa ya mwambao wa Dar es Salaam, Unguja na Pemba. Katika eneo la Sinda Pwani ya Dar es Salaam eneo la mita za mraba 2000 limepandikizwa matumbawe bandia. Vilevile, kwa upande wa Unguja na Pemba jumla ya matumbawe bandia 90 aina ya reef ball yalipandikizwa katika Kijiji cha Jambiani; na matumbawe bandia 46 na mapande maalum 6 katika Kijiji cha Kukuu. Matumbawe hayo yalifuatiliwa ukuaji wake kitaalam na matokeo yameonyesha mafanikio makubwa kwa kuimarika kwa mazalia ya samaki na hivyo kuongezeka kwa kiwango cha samaki katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na upandaji wa mikoko, Serikali imekuwa ikiongeza jitihada zaidi katika upandaji wa mikoko katika fukwe mbalimbali nchi nzima kwa kushirikiana na asasi binafsi na washirika wa maendeleo. Takribani hekta 7 za mikoko zilipandwa Unguja na hekta 10 zilipandwa Pemba kwa mwaka 2020/2021. Upandaji wa hekta 13.5 unaendelea mpaka sasa na matarajio ni kupanda hekta 15 kwa mwaka huu. Aidha, kwa upande wa Tanzania Bara, hekta 105 zimepandwa katika Delta ya Rufiji na matarajio ni kupanda hekta 2000 kwa pwani yote ya Tanzania Bara ifikapo mwishoni mwa mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunatunza, tunahifadhi na kusimamia matumbawe na mikoko pamoja na mifumo ya ikolojia inayopatikana ndani ya bahari zetu. Ahsante.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga tuta kuzuia maji ya Bahari ya Hindi yasiathiri mashamba na mazao ya Wakulima wa Vijiji vya Nanguji, Jundamiti, Mwambe na Kiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Abdalla Rashid, Mbunge wa Jimbo la Kiwani, kutoa maelezo mafupi yafuatayo kuhusu ongezeko la kina cha maji bahari (Sea Level Rise):-

Mheshimiwa Spika, mojawapo ya athari ya mabadiliko ya tabianchi katika dunia yetu ni kuongezeka kwa ujazo wa maji ya bahari (Sea Level Rise). Kwa mujibu wa takwimu za kisayansi zilizopo, kina cha maji ya bahari kimeongezeka kwa wastani wa sentimeta 21. Ili kutimiza lengo la kupambana na mabadiliko ya tabianchi, nchi wanachama wa mkataba zilianzisha mifuko ya fedha kama vile Least Developed Coutries Fund, Adaptation Fund, Green Climate Funds na Global Environment Facility. Nchi zilizoendelea ziliahidi kuchanga fedha na kuziweka kwenye mifuko hiyo. Hata hivyo, kuna changamoto ya urasimu ndani ya sekretarieti ya mifuko ambayo husababisha uidhinishaji wa miradi kuchukua muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdalla Rashid, Mbunge wa Jimbo la Kiwani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ujenzi wa kuta za bahari hugharimu fedha nyingi, ambazo ni vigumu kuzipata kutokana na ufinyu wa bajeti, Serikali itaendelea kuandaa miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na kuendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kupata fedha kupitia mifuko hiyo na kuwezesha Serikali kujenga kuta hizo mara fedha zitakapopatikana. Aidha, wakazi wa maeneo ya Nanguji, Jundamiti, Mwambe na Kiwani kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge wanahimizwa kuibua miradi ya ujenzi wa matuta wakati wa TASAF ya III Awamu ya Pili ambayo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwezi Septemba, 2021.
MHE. MWANAHAMIS KASSIM SAID aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa waliokuwa Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano waliostaafishwa kwa maslahi ya Umma tarehe 30 Juni, 1996?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. HAMAD HASSAN CHANDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu ya Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said wa Jimbo la Magomeni, Zanzibar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais ilipokea malalamiko ya wastaafu saba waliopunguzwa kazini kwa manufaa ya Umma mwaka 1996. Baada ya uchambuzi wa suala hili na kuwasiliana na Wizara ya Fedha na Mipango, ilibainika kwamba stahili zao zote zilishalipwa kipindi walipostaafishwa. Hivyo, hawastahili kulipwa pensheni kutokana na masharti yao ya ajira, bali walilipwa kiinua mgongo cha mkupuo ambacho ni stahili ya watumishi walioajiriwa chini ya masharti ya “Operational Services.” Hii ni kwa mujibu wa Kanuni Na. 6 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi Serikalini za Mwaka 1994 na Sheria Na. 36 ya Mwaka 1964 (The National Provident Fund Act).
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mto Msimbazi ambao umeainishwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira; kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas Mbunge Jimbo la Kinondoni naomba kutoa maelezo yafuatayo kuhusu Mto Msimbazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inatekeleza mradi wa kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project) kwa mkopo nafuu wa Dola za Marekani milioni 300 kutoka Benki ya Dunia.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza DFID, inatekeleza programu ya Tanzania Urban Resilience Programme ambayo imelenga kuzisaidia halmashauri na Serikali Kuu katika kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi. Kwa kuanzia, programu itaanza kutatua changamoto zinazolikabili Bonde la Mto Msimbazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari DFID imeshatenga kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 20 kwa ajili ya Bonde la Mto Msimbazi. Pia Benki ya Dunia, kupitia mradi wa DMDP, imekubali mkopo wa nyongeza wa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 100 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za Bonde la Mto Msimbazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Abbas Tarimba Gulam Mbunge wa Kinondoni:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kubadili eneo la bonde la Mto Msimbazi kuwa eneo la uwekezaji na fursa mbalimbali. Ili kufikia azma hiyo, usanifu wa mradi huo umekamilika. Utekelezaji wa mradi utaanza baada ya kupata idhini ya Serikali kuhusu matumizi ya fedha hizo za mkopo kupitia Wizara ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ili kupunguza athari za mafuriko kwa sasa, kipande cha Mto Msimbazi cha daraja la Jangwani kinafanyiwa usafi wa mara kwa mara na wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
MHE. GEORGE N. MALIMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza kingo za korongo linalopita katikati ya Mji wa Mpwapwa lisiendelee kutanuka ili kunusuru maisha na makazi ya wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa naomba kutoa maelezo yafuatayo kuhusu Korongo lililoko katikati ya Mji wa Mpwapwa:-

Mheshimiwa Spika, Mji wa Mpwapwa umejengwa pembezoni mwa mto ambao ni maarufu kwa jina la Mto Shaaban Robert, ambao sasa unaonekana kama Korongo linalopita katikati ya Mji. Kutokana na wananchi kufanya shughuli zao mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwenye kingo za mto huo, kumekuwa na kubomoka kwa kingo hizo. Hali ambayo imeleta athari kubwa kwenye miundombinu na makazi ya watu walioko karibu na kingo za mto huo.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na uharibifu huo wa mazingira, Serikali imefanya upembuzi wa awali kwenye mto kiasi cha urefu upatao kilometa mbili ambazo ziko jirani na makazi ya watu ili kufahamu gharama za kudhibiti kingo zake. Katika upembuzi huo, inakadiriwa kwamba zinahitajika kiasi cha shilingi bilioni 2,170 kwa ajili ya ukarabati huo. Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kufanya yafuatayo:-

(i) Kuweka gabioni kiasi cha mita za ujazo 8,870;

(ii) Kujenga vizuri mmomonyoko kwa zege kiasi cha mita za ujazo 52;

(iii) Kujaza udongo maeneo yote yaliyoporomoka kiasi cha mita za ujazo 9,000; na

(iv) Kurudisha mto kwenye mkondo wake wa asili ambapo kinahitajika kifusi kiasi cha meta za ujazo 6,000. Serikali imetenga fedha ili kuweza kutekeleza mradi huo.

Mheshimiwa Spika, pia, napenda kuchukua fursa hii kuwasihi wananchi kuacha shughuli zinazosababisha uharibifu wa mazingira katika kingo za mito na badala yake wajitahidi kupanda miti, kupanda majani ambayo yatazuia mmomonyoko wa kingo hizo. Ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-

(a) Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na wizi wa vyuma unaosababishwa na kushamiri kwa biashara ya chuma chakavu nchini?

(b) Je, Serikali haioni kwamba biashara ya vyuma chakavu ni hatarishi hata kwa usalama wa raia na mali zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kupitia vifungu vya 133 hadi139, Serikali imeweka kanuni za udhibiti wa taka hatarishi ikihusisha ukusanyaji, usafirishaji na uhifadhi wa taka hizo. Sambamba na uwepo wa kanuni, Serikali imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali pamoja na elimu kwa jamii katika ulinzi wa miundombinu. Aidha, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na jeshi la polisi imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika viwanda ili kudhibiti suala la uhujumu wa miundombinu ya Serikali na watu binafsi.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya vyuma chakavu imesaidia kuziondoa taka hizi katika mazingira na hivyo kutengeneza mazingira safi na salama kwa afya ya binadamu. Aidha, vyuma chakavu ni malighafi ya viwanda hasa viwanda vya nondo na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali imekuwa ikifanya ufuatiliaji ili kudhibiti hujuma ya miundombinu ya Serikali na watu binafsi. Aidha, wananchi na vyombo mbalimbali vinaombwa kushiriki kwa pamoja katika kulinda miundombinu dhidi ya watu waovu na wale watu wasio na uzalendo, ahsante.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, Taasisis ngapi zimeweza kujisajili hadi sasa na Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) nchini, na miradi mingapi imeshaombewa kupitiwa mfuko huo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira). Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge Jimbo la Donge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) ulianzishwa mwaka 2010 na kuanza kufanya kazi mwaka 2015. Taasisi inayotaka kuomba fedha kutoka katika Mfuko huu, ni lazima iwe imesajiliwa au kupata ithibati chini ya Mfuko huu. Ithibati au usajili hutolewa baada ya taasisi husika kutimiza vigezo stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko wa mabadiliko ya Tabianchi unaruhusu taasisi za kitaifa, kikanda na kimataifa, kusajiliwa ili kuweza kuomba fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya mabadiliko ya tabianchi. Hadi kufikia mwezi Machi 2021, mfuko huu ulikuwa umesajili jumla ya taaisis 74 ulimwenguni kote. Hapa nchini, taasisi iliyopata usajili ni moja tu, ambayo ni Benki ya CRDB. Tunaipongeza Benki ya CRDB kwa kuweza kupata ithibati ya mfuko huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa usajili wa taasisi katika mfuko huu wa mabadiliko ya Tabianchi hauna ukomo. Serikali inaendelea kuhamasisha taasisi nyingine za hapa nchini kujisajili na mfuko huu, ili kuwa na uwezo wa kupata fedha na kutekeleza miradi mbalimbali ya mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi, hadi sasa jumla ya miradi sita imeombewa fedha kutoka Mfuko huu kupitia taasisi mbalimbali. Hata hivyo, ni miradi miwili tu ambayo fedha yake imeidhinishwa. Miradi hiyo ni Pamoja na mradi wa Maji kwa Kuwezesha uhimili katika Mkoa wa Simiyu (Dola za Marekani millioni 120), na mradi wa pili, ni mradi wa kuandaa Uwezo wa CRDB (Dola za Marekani 560,000) ahsante.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mashindano ya michezo mbalimbali kwa kila mwaka wakati wa sherehe za Muungano ili kudumisha hamasa za Muungano kwa vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninakubaliana na Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, kuwa mashindano ya michezo kuelekea maadhimisho ya Muungano yalikuwa yanaleta hamasa kubwa kwa wananchi kila ifikapo Aprili kila mwaka. Kwa kutambua hilo, Serikali italifanyia kazi suala hili na Ofisi ya Makamu wa Rais itaratibu utekelezaji wake kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwani ni ukweli usiopingika kuwa michezo ina umuhimu mkubwa sana katika kudumisha Muungano wetu huu adimu na adhimu. Baada ya utekelezaji huo, Serikali itatoa taarifa, ahsante.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha vikundi vya wananchi ili kuhamasisha uhifadhi wa mazingira hasa katika fukwe za Bahari ya Hindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali tayari ina mpango wa kushirikisha wananchi kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais. Pia Serikali imeandaa mkakati wa kuhifadhi mazingira ya Bahari, Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa. Aidha, kufuatia utekelezaji wa mkakati huu na kwa kutambua umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika kuhifadhi mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanzisha vikundi vya usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi vinavyofahamika kwa jina la “Beach Management Units” – BMUs. Vikundi hivi vimeanzishwa katika ngazi ya Kijiji/Mtaa kwa mujibu wa Kifungu cha 18 cha Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003. Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi una jumla ya vikundi 157 ambapo Tanga ina vikundi (31), Pwani (46), Dar es Salaam (23), Lindi (46) na Mtwara (11). Ahsante. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvisaidia vikundi vya BMU ili kuendeleza kasi ya upandaji mikoko na kusafisha fukwe kuanzia Pwani ya Bagamoyo, Pangani hadi Tanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari ina mipango ya kuvijengea uwezo wa uelewa ili kujisimamia vikundi vyote vya BMUs katika kuendeleza kasi ya upandaji mikoko na kusafisha fukwe za bahari yetu. Jumla ya vikundi 18 vya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti vimepatiwa mafunzo ya kupanda, kuhifadhi na kusimamia mikoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, vikundi vya BMUs vya Mlingotini Bagamoyo vimewezeshwa kupanda miche 7,000 ya mikoko. Vilevile, vikundi vya BMUs vya vijiji vya Moa, Ndumbani na Mahandakini Wilayani Mkinga vimepatiwa mafunzo ya usimamizi wa mazingira ikiwemo upandaji wa mikoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kupitia mradi wa South West Indian Ocean Fisheries (SWIOfish) unaoratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Vikundi vya BMUs vya Bagamoyo na Pangani wamepata uelewa wa kukusanya maduhuli ambapo kiasi cha fedha kinachokusanywa kitatumika katika kuendeleza shughuli za upandaji wa mikoko na usafi wa mazingira. Ahsante.