Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Anton Albert Mwantona (3 total)

MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii. Kabla ya yote nipongeze sana Wizara ya Maji. Napongeza Wizara ya Maji, Naibu Waziri alikuja kwetu Rungwe Jimboni, ametembelea miradi, ameona matatizo ya maji kwa wananchi wa Rungwe. Naomba sasa niulize swali langu; je, ni lini mradi wa maji wa Mji Mdogo wa Tukuyu utaanza kutekelezwa hasa baada ya Naibu Spika kutembelea na kutuahidi pale. Lakini pia upembuzi yakinifu ulishafanyika…

NAIBU SPIKA: Umeshauliza swali.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantona Mbunge wa Rungwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji mdogo wa Tukuyu tunafahamu kabisa miundombinu yake ni chakavu na idadi ya watu imeongezeka, tayari maelekezo yapo kwa Meneja wa Maji Mkoa wa Mbeya na ameshaanza manunuzi ya vifaa vya kazi na kufikia mwezi Machi kazi zitaanza kufanyika pale Tukuyu na upatikanaji wa maji unakwenda kuboreshwa. (Makofi)
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Wizara ya Maji. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwenye Mradi wa Maji Tukuyu nimeridhika, lakini kuna mradi mwingine ambao unaendelea katika Mji wa Ushirika, Kata ya Mpuguso. Tenki tayari limeshajengwa, mabomba tayari yameshafika kwenye tenki, usambazaji wa maji bado kwa wananchi kwa muda mrefu. Naomba Wizara ituambie wananchi wa Rungwe lini itaanza kusambaza maji kwa wananchi wa Rungwe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tuna Kituo cha Afya cha Ikuti ambacho kina matatizo makubwa sana ya maji. Nilikuwa naomba Wizara iwaambie wananchi wa Ikuti, Jimbo la Rungwe, ni lini maji yatasambazwa hasa baada ya upembuzi yakinifu wa mradi ule kuonekana kwamba, ni milioni 100 tu ambayo itapeleka maji kutoka kwenye chanzo cha maji mpaka kwenye Kituo cha Afya cha Ikuti? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unaoendelea pale miundombinu yake imeshakamilika, imebaki tu usambazaji wa maji. Mheshimiwa Mbunge mradi ule unakwenda kukamilika wiki chache zijazo na maji yatafika mabombani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Kituo cha Afya cha Ikuti kupata maji, Mheshimiwa Mbunge Serikali tutalifanyia kazi na namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, ndani ya muda mfupi utekelezaji wake utakuja kufanyika.
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nilikuwa naomba Serikali itoe kauli, hasa kwa kutumia Sheria Na. 5 ambako halmashauri nyingi zipo huko kupima ardhi kwa kutumia hati za kimila; kwa sababu ukiangalia kwenye statement nyingi za halmashauri zetu inaonekana hoja kubwa ya migogoro ni kutokuwa na hati za kumiliki ardhi.

Je, Serikali ina mpango gani kwa kutumia hati miliki za kimila kuhakikisha maeneo yote ya umma, shule na vituo vya afya yanapimwa kama inavyotakiwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa; ya kwamba hoja yake ni ya msingi na ni nzuri, lakini, shule ambazo zinamilikiwa na halmashauri haziwezi kupimwa kwa hati ya kimila, zile zinapimwa chini ya Sheria Na. 4; kwa maana ya kwenda kwenye general land. Kwa hiyo kama hitaji hilo lipo ni kwamba ni halmashauri pia, tuone namna ya kuhakikisha, na Wizara ilishaelekeza, kwamba taasisi zote za umma zipimwe. Huwezi kuipima kwa kutumia Sheria Na. 4.

Mheshimiwa Spika, niombe tu kwamba halmashauri zijipange katika kutumia Sheria Na. 5 kwasababu ile imeshaingia kwenye general land na haiwezekani tena kukaribisha kwenye umiliki wa kijiji. (Makofi)

SPIKA: Kwa hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri zikishapimwa zitapewa hati each na hati ile inalipiwa kodi ya ardhi, au inakuwaje?

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, watapewa, na kodi inayolipwa sasa hivi; tulibadilisha sheria hapa mwaka 2019, wanalipa token tu, shilingi 5,000 kwa mwaka badala ya kutumia ukubwa wa eneo. (Makofi)