Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Anton Albert Mwantona (2 total)

MHE. ANTON A. MWANTONA Aliuliza:-

Serikali ilifanya upembuzi yakinifu na kubaini kuwa jumla ya shilingi Bilioni 21 zinahitajika ili kukarabati miundombinu ya maji Mji wa Tukuyu:-

Je, ni lini Serikali itatenga fedha na kuanza ukarabati wa miundombinu hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Albert Anton Mwantona, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha wananchi wa Mji wa Tukuyu wanapata huduma ya maji safi na salama ya kutosha, Serikali imeendelea na mikakati ya muda mfupi na mrefu. Mkakati wa muda mfupi ulihusisha uboreshaji wa chanzo cha maji cha Masalala, ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 200,000 pamoja na ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa mita 750. Kazi hizo zimesaidia kuimarisha huduma ya maji kwa wakazi wa Mji wa Katumba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mkakati wa muda mrefu wa kuboresha hali ya upatikanaji wa maji safi katika Mji wa Tukuyu, Serikali kwa kutumia wataalam wa ndani wa Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira za Mbeya na Tukuyu inafanya mapitio ya usanifu wa mahitaji kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya maji katika Mji wa Tukuyu kwa kutumia chanzo cha Mto Mbaka. Kulingana na usanifu kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huu ni pamoja na ujenzi wa bomba kuu la kilometa 15.5, ujenzi wa bomba la usambazaji maji kilometa 20, ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 2,000,000. Mradi huu utatengewa fedha katika mwaka wa fedha 2021/2022 na utekelezaji wake unatarajia kuanza mwezi Julai, 2021.
MHE. ANTON A. MWANTONA Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapima maeneo yote ya umma ikiwemo Shule, Vituo vya Afya na Zahanati kwa kutumia Sheria Na. 4 na Na. 5 ili kuondokana na matatizo ya migogoro ya mipaka kwa Wananchi, lakini pia kuondokana na hoja za ukaguzi ambazo zaidi ya asilimia 90 ya Halmashauri wanazipata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ninaomba kujibu Swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa baadhi ya maeneo ya umma yaliyoainishwa na kutengwa kwa ajili ya utoaji wa huduma mbalimbali za umma zinazotolewa na Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa hayajapimwa na kuwekewa alama zinazoonekana kwa urahisi. Hali hii husababisha migogoro ya mara kwa mara ya ardhi na uvamizi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo Serikali imezielekeza halmashauri zote nchini kutenga fedha kila mwaka katika bajeti zao kwa ajili ya kupima maeneo yote ya taasisi za umma zilizo chini ya mamlaka hizo; ikiwa ni pamoja na kuweka alama zinazoonekana kwa urahisi ili kuepusha migogoro ya ardhi na kuzuia uvamizi unaofanywa na baadhi ya wananchi. Serikali ilishatoa maelekezo haya kwa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; hivyo nitumie fursa hii kuzisisitiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinatenga fedha na kutekeleza maelekezo hayo. Ahsante sana.