Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava (6 total)

MHE. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu yenye matumaini kutoka kwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kabla sijauliza, napenda kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Shinyanga hasa wanawake walioweza kunichagua na chama changu kuniteua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza la nyongeza; kwa kuwa ili hospitali iweze kukamilika na kuanza kufanya kazi ni lazima miundombinu yote iwepo kama maabara, X-Ray na mortuary. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba majengo mengine na miundombinu mingine inakamilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa tumeanza kuona jitihada nzuri za Wizara ya Afya katika kudhibiti wizi wa madawa na ubadhirifu wa madawa: Je, nini mkakati endelevu wa Serikali kuhakikisha kwamba wizi wa dawa unadhibitiwa na dawa zinapatikana muda wote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, Mheshimiwa Mnzava ameuliza kuhusu majengo mengine. Kwa bajeti ya mwaka huu 2021 Serikali imetenga shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya majengo mengine ambayo ameyataja.

Vilevile imetenga shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya magonjwa ya mlipuko. Kwa maana kwa bajeti mwaka huu tunaokwenda kuanza, kuna shilingi bilioni 6.4 ambazo zinaenda kuelekezwa kwenye hospitali husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ameuliza ni kwa namna gani tunaenda kudhibiti wizi wa madawa kwenye hospitali zetu. Kwanza, niseme tu kwamba tumepita na tumegundua kwamba watumishi wengi wa Wizara ya Afya wanafanya kazi nzuri sana lakini kuna wachache ambao wanafanya haya mambo ya ubadhirifu. Vile vile tumegundua kwamba wabadhirifu wamekuwa wakienda Mahakamani aidha, wanaishinda Serikali au kesi zinachukua muda mrefu. Kwa hiyo, tunaenda kimkakati sana kuhakikisha kwamba yeyote atakayepatikana hachomoki, ni lazima awajibike.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baada ya miezi miwili, mtaanza kuona mkakati wa Wizara wa kuhakikisha moja kwa moja hayo mambo yamefutika, kwa sababu watu wako chini kuhakikisha kwamba tukianza kufanya hiyo kazi hakuna atakayechomoka na tunamaliza hilo tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Viwanda. Tunazungumzia uchumi wa kati ikiwemo kuondeleza viwanda vyetu, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, ni nini mpango wa Serikali katika kuongeza viwanda vingi ili hawa vijana wanaohitimu mafunzo haya waweze kupata ajira kwa sababu naona ni vijana saba tu ambao wameajiriwa na Serikali?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, ni nini mpango mkakati wa Serikali kufufua viwanda vyote ambavyo vilijengwa enzi za Mwalimu ili hawa vijana wetu akribani 228 waliohitimu mafunzo haya ambao hawajapata ajira waweze kuajiriwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Christina Mnzava, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Tanzania tupo katika mkakati wa kuwa na uchumi unaoendeshwa na viwanda na hasa tukiwa sasa tumefika katika uchumi wa kati. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha tunaongeza viwanda vingi kwa kuhamasisha sekta binafsi kupitia kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya wadau wa viwanda kuwekeza katika viwanda vingi ambavyo hatimaye vinatumia vijana wetu wanaohitimu katika vyuo vingi ambavyo vinatoa elimu hususan inayolenga katika kuongeza ubora wa bidhaa zetu zinazozalishwa katika viwanda lakini pia lengo ni kuona sasa tunakuwa na viwanda ambavyo vitakuwa vinapata wataalam walio na utaalam mahsusi katika mahitaji wa viwanda hivyo. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi lakini pia mashirika na watu mbalimbali na wawekezaji kutoka nje ambao wanaweza kuwekeza katika viwanda hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, katika swali la pili ni kweli viwanda vingi vilivyokuwa vimejengwa wakati wa enzi za Nyerere lakini pia viwanda vingi ambavyo vilikuwa vimebinafsishwa havifanyi kazi. Serikali ina mkakati maalum kwanza kupitia viwanda vyote ambavyo havifanyi kazi, lakini hasa vile ambavyo vilikuwa vimebinafsishwa kwa watu ambao hawaviendelezi ili tuweze kuvifufua. Lengo ni kuona sekta ya viwanda inaendelea lakini wa kutumia miundombinu ya viwanda iliyokuwepo hapo kabla ili viweze sasa kuchukua wataalam wengi ambao wanasoma katika vyuo vyetu vingi ili waweze kuajiriwa katika viwanda hivyo.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa changamoto ya Barabara ya Kairuki ni sawa kabisa na changamoto iliyopo katika barabara ya kutoka Ndala kwenda Mwawaza kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Je, ni lini Serikali itatoa fedha kukamilisha barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Christina Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameainisha Barabara ya Ndala – Mwawaza kuelekea Hospitali ya Shinyanga. Ameuliza ni lini Serikali itaikamilisha. Niseme tu kwamba, tutaikamilisha kwa kadri ya upatikanaji wa fedha na tathmini ambazo zinaendelea kufanyika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na subira, hiyo barabara itajengwa kwa kadri tutakavyopata fedha. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa ajili ya majibu ya Naibu Waziri. Maswali mawili ya nyongeza; nini commitment ya Serikali kuhusu tabia ya kuzichelewesha fedha na baada ya muda mfupi kuzirejesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili…

SPIKA: Rudia la kwanza.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Nini commitment ya Serikali kuzichelewesha fedha kuzipeleka Halmashauri na baada ya muda mfupi kuzirejesha?

SPIKA: Swali lako halisomeki, la pili na la mwisho.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Je, halmashauri itakuwa…

SPIKA: Aah! Umechelewesha unarejeshaje tena ulichokichelewesha.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: mfumo unazichukua zile fedha…

SPIKA: Naam.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Kwamba inachelewesha kutuma fedha mpaka mwezi wa tano au wa nne lakini baada ya muda mfupi tu mfumo unazirejesha kwenda Hazina kabla zile fedha hazijatumika.

Nini commitment ya Serikali… (Makofi)

SPIKA: Rudia mara ya mwisho.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Swali la mwisho je Halmashauri…

SPIKA: Hilohilo hujaeleweka

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Sijaeleweka, nasema hivi…

SPIKA: Unajua anatoka Shinyanga ni Msukuma huyu sasa inakuwa tabu kidogo.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Nini commitment ya Serikali kuhusu suala la kuchelewesha fedha kuzituma katika halmashauri husika na baada ya muda mfupi kuzirejesha kupitia huo mfumo?

SPIKA: Yaani anachosema hela inacheleweshwa kupelekwa kwenye halmashauri hadi kwenye mwezi wa nne/ tano si bajeti inaisha mwezi wa sita halafu wakishazituma kwenye halmashauri mwezi ule wa nne/tano baada ya wiki mbili/tatu wanazichukua tena fedha zilezile ndicho anachojaribu kukieleza. (Makofi)

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa elaboration.

SPIKA: La mwisho.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, la mwisho; je, halmashauri itakuwa inatenda kosa ikizikatalia zile fedha zisirejeshwe kwenye mfumo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Christina Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 inaeleza vizuri utaratibu wa fedha zinazopelekwa kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zimepangiwa majukumu mahususi lakini hazitatumika mpaka tarehe 30 Juni ya mwaka husika wa fedha.

Utaratibu uliolekezwa na sheria ni kwamba Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wakishaona fedha zimeingia kwa kuchelewa na kwa mazingira halisi hawawezi kuzitekelezea majukumu yake by tarehe 30 Juni ya mwaka husika wanatakiwa kuandika barua kwa Katibu Mkuu Hazina kupitia Katibu Mkuu TAMISEMI kuomba maombi maalum na kutoa sababu za msingi kwamba fedha zile hazitaweza kutumika kwa tarehe husika na hivyo wapewe kibali maalum cha kutumia fedha zile ndani ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha unaofuata kwa maana ya Julai, Agosti na Septemba ya mwaka wa fedha unaofuata.

Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo, Wakurugenzi wengi wamekuwa hawaitekelezi ipasavyo sheria hiyo na nichukue nafasi hii kutoa wito na maelekezo kwa Wakurugenzi wa halmashauri kwanza kuhakikisha wanaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mara wanapopokea fedha lakini pili kutekeleza sheria hiyo kwa kuomba kibali maalum cha matumizi ya fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, pili; mifumo ambayo kimsingi inatumika katika kupeleka hizi fedha na kutumia katika mazingira hayo zina changamoto zake lakini Serikali inaendelea kuboresha kuhakikisha karibu na mwisho wa mwaka mifumo hii inafanya kazi na kuwezesha miradi ya maendeleo kutekelezwa.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Kwa kuwa katika majibu yake ya msingi amesema kwamba mradi wa muda mrefu wa Shelui – Tinde utaweza kukidhi mahitaji ya wananchi wa Shinyanga: Je, ni lini sasa Mradi wa Shelui –Tinde utaanza kwa kuwa mkataba umeshasainiwa toka tarehe 25 mwezi wa Pili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa tunajua Sera ya Maji ni kuhakikisha kwamba inasambaza maji katika vijiji vyote ambavyo vinapitiwa na bomba kuu la Ziwa Victoria.

Je, ni lini Serikali itaanza kusambaza maji katika Kata za Lyabukande, Lyamidati, Nindo, Imesela na Didia?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mradi huu kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi tunatarajia kutoa maji Ziwa Victoria na Shelui – Tinde pia itakuwa ni moja ya wanufaika mwaka ujao wa fedha, kadiri fedha tunavyozipata.

Mheshimiwa Mwenyrkiti, napenda sana kumshukuru Mheshimiwa Rais, tumesikia jana wakati Bajeti ya Serikali Mheshimiwa Waziri akihitimisha pale, Mheshimiwa Rais ametuongezea fedha ambazo zitatusaidia kuongeza maeneo mengi katika nchi hii kuhakikisha maji ya uhakika yanakwenda kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile suala la usambazaji maji katika miradi yetu hii ni lazima ifanyike. Lengo ni kuona kwamba, wananchi wanapelekewa maji karibu na makazi yao na kupunguziwa umbali mrefu wa kutembea. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matumizi ya zebaki, hasa Kanda ya Ziwa, sehemu ambazo wanachimba madini imekuwa ikisababisha ongezeko la wagonjwa wa Kansa ya Shingo ya Uzazi: Je, Serikali imeshafanya utafiti kuthibitisha kwamba zebaki ndiyo chanzo cha ongezeko la magonjwa ya kansa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba hata ukienda Ocean Road imeonekana kwamba wagonjwa wengi wenye matatizo ya kansa wanatokea Kanda ya Ziwa. Hayati Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli aliwahi kuagiza ufanyike utafiti ambao bado majibu yake hayajaja ili kuthibitisha nini hasa chanzo cha tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachofanyika kwa sasa ni kwamba kwanza kuna sababu nyingi ambazo zinasababisha kansa ya kizazi. Kwa hiyo, hatuwezi kusema specifically ni hilo. Kikubwa, tunashirikina na Wizara ya Madini kupitia taasisi yake kuhakikisha sasa wanapochenjua madini, wale wachimbaji wadogo na wakubwa kunakuwepo na control ya kutosha kuhakikisha kwamba haiendi kwenye mazingira na vilevile haiendi kufika maeneo ambayo binadamu wanatumia maji na vitu vingine. Hilo ndiyo tunaendelea nalo kwa sasa.