Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava (4 total)

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA Aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa wodi ya wazazi utaanza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa Hospitali za Rufaa za Mikoa zinazoboreshwa. Napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba Mshauri Elekezi wa Ujenzi wa Wodi ya Wazazi ameshapatikana, ambaye ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, hatua inayoendelea hivi sasa, ni mchakato wa zabuni ya kupata mkandarasi atakayefanya kazi ya ujenzi, ambapo ujenzi huo unategemewa kuanza mwezi Machi, 2021. Mradi huu utatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza:-

(a) Je, Serikali inawatumia vipi wanafunzi wanaohitimu Shahada ya Science in Industrial Engineering Management katika Uchumi huu wa kati wa Viwanda?

(b) Je, ni wanafunzi wangapi waliohitimu katika fani hiyo wameajiriwa Serikalini tangu mwaka 2019 hadi 2020?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Shahada ya Sayansi katika Menejimenti ya Uhandisi wa Viwanda (Bachelor of Science in Industrial Engineering Management), ilianzishwa mwaka 2015/2016 katika Chuo Kikuu cha Mzumbe. Shahada hiyo ilianzishwa ikilenga kuzalisha wataalam wa kusimamia shughuli za uzalishaji katika viwanda ambavyo vinamilikiwa na Serikali na vile vya mashirika na makampuni binafsi.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2019/2020, wahitimu wengi katika fani hiyo wameajiriwa katika sekta binafsi hususan katika viwanda vya kuzalisha bidhaa kama vile viwanda vya saruji, vinywaji, nguo, sukari, vyakula, mbao, vifungashio, mafuta na kadhalika na katika uchimbaji wa madini. Pia, wahitimu hao wameajiriwa katika taasisi za Serikali zinazoshughulikia masuala ya ubora kwa mfano Shirika la Viwango Tanzania - TBS, Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda-TIRDO, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Taasisi ya Uhandisi na Usanifu wa Mitambo -TEMDO, huduma za viwanda vidogo Vidogo-SIDO na mengineyo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali yetu inatekeleza azma ya ujenzi wa viwanda, yaani uchumi unaoongozwa na viwanda, wahitimu katika fani hiyo walioajiriwa wanatumika katika usimamizi wa shughuli mbalimbali za viwanda vilivyopo katika sekta ya umma na sekta binafsi na hivyo kuleta tija katika uzalishaji na uendeshaji wa taasisi za umma na za binafsi.

(b) Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2019/2020 jumla ya wahitimu wa shahada hiyo walikuwa 228. Kati ya hao, wahitimu 55 walipata ajira. Aidha, kati ya hao 55 waliopata ajira, katika mashirika na taasisi za Serikali ni wahitimu saba.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itazirejesha fedha za ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Msalala zilizorudishwa na mfumo baada ya mwaka wa fedha 2019/2020 kuisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ilipatiwa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Hadi Juni 30 mwaka 2020, Halmashauri hiyo ilikuwa imetumia shilingi milioni 22.4 pekee na hivyo shilingi milioni 477.59 zilirejeshwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti Namba 11 ya Mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2015. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Msalala shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa awamu hadi ujenzi wa hospitali hiyo utakapokamilika.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Kata za Mwamala, Samuye, Busanda, Usule, Bukene na Imesela?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji katika Kata ya Mwamala, Samuye, Busanda, Usule, Bukene na Imesela kupitia mpango wa muda wa kati na muda mrefu. Kwa mwaka wa 2020/2021, kazi zilizofanyika ni pamoja na kufanya usanifu wa matanki mawili yenye lita 100,000 na lita 200,000, mtandao wa kusambaza maji wa urefu wa kilometa 44.8 na vituo vya kuchotea maji 39.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022, ujenzi wa miundombinu ambayo itatumia maji kutoka mradi wa maji wa Masangwa, Ilobashi, Bubale utafanyika ili kuongeza upatikanaji wa maji katika Kata za Mwamala na Samuye.

Aidha, kwa mpango wa muda mrefu ni kutumia maji ya bomba kuu la kutoka Ziwa Victoria kupeleka maji Tinde, Shelui, ambapo kata zote sita zitapata huduma ya maji kwa zaidi ya asilimia 85 ifikapo mwezi Desemba, 2022.