Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Eng. Kundo Andrea Mathew (35 total)

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mbulu Vijijini tumepata minara sita ambayo imejengwa. Mwingine umejengwa 2017, mingine inayofuata imejengwa mpaka juzi hapa lakini sasa minara hii sita haifanyi kazi.

Je, Mheshimiwa Waziri ana mpango kuwafuata au kuwaona wakandarasi ili wawashe minara hii sita ambayo sasa wananchi wanaisubiri mpaka leo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa amesema kata hizi atazipelekea mawasiliano na kujenga minara; je, kata zilizobaki lini zinakwenda kupata hiyo minara ambayo amekwishaisema?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kulingana na changamoto ambayo ilikuwepo ya masuala ya ujenzi, kata hizo zilikuwa zimechelewa kukamilishiwa miradi hiyo. Hata hivyo, hivi navyoongea wataalam wetu tayari wameshaanza kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naomba kutumia fursa hii kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna hatua mbili katika ujenzi wa minara; kuna hatua ambayo inatokana na ujenzi wa mnara wenyewe ambao tunaita passive equipment na hatua ya pili ambayo sasa ni kuweka vile vifaa ambavyo tunaita kwamba ndiyo active equipment.

Mheshimiwa Naibu Spika, vifaa hivi tumekutana na changamoto ya wakandarasi wetu ambao walikuwa wamepewa majukumu ya kukamilisha miradi hii kwa sababu wanatumia sana vifaa kutoka nje na mwaka jana tulikumbana na changamoto ya Corona, hivyo tukaona kwamba tuwaongezee muda ili waweze kukamilisha ujenzi wa minara hii. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, suala hili tayari tunalifanyia kazi na hizi kata ambazo amezisema tayari wataalam wetu wameshafika site kwa ajili ya kujua nini kinafanyika ndani ya muda ambao unatakiwa. Ahsante sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naomba kuuliza Wizara ya Mawasiliano swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa vijiji vitatu katika Kata ya Ziginali, Kisawasawa na Kiberege havina mawasiliano ya simu kabisa. Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi hawa huduma ya mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilijibu katika majibu yangu ya msingi, ni kwamba Serikali iko katika mpango wa kufanya tathmini katika Kata nyingine 1,392 ambazo zimebaki Tanzania Bara ili tuweze kuona namna gani tutaziingiza katika Mpango wa Utekelezaji katika Bajeti ya 2020/2021. Hivyo namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, sambamba na hilo tutahakikisha kwamba tunawasiliana naye kwa ukaribu sana ili kujua changamoto ziko katika maeneo gani ili tuhakikishe kwamba mawasiliano katika Kata hizo yanafika kwa ukamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Tatizo lililopo katika Jimbo la Mbulu Vijijini ni sawa kabisa na changamoto iliyoko katika Jimbo la Kalenga. Kata ya Kihanga, Ulanga, Ifunda katika Vijiji vya Mibikimitali na Kata ya Mgama iliyoko katika Vijiji vya Lupembewasenga, kuna changamoto ya mawasiliano.

Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha wananchi hao wanapata huduma hiyo ya mawasiliano ili waweze kufanya shughuli zao za kawaida?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto tuliyonayo kwa sasa, labda nitoe maelezo kidogo. Ni kwamba kuna baadhi ya sehemu ambazo mawasiliano au minara ilipelekwa ambapo uhitaji wake inawezekana walikuwa watu 5,000 ambao walikuwa wanaweza kutumia huduma hiyo. Kwa sababu ya ongezeko la watu katika eneo husika, kwa hiyo, ile minara yetu inashindwa kuwa na uwezo wa kuhudumia watu wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, kwa kugundua hilo, tumeagiza mobile operator wote wafanye tathmini, wafanye research za kutosha ili waongeze uwekezaji katika maeneo hayo, aidha kwa kuongeza minara au kwa kuongeza capacity katika minara ambayo tayari ipo katika maeneo husika ili kuhakikisha kwamba wananchi wote wanafikiwa na mawasiliano hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina swali la nyongeza ambalo lina vipengele viwili.

Mheshimiwa Spika, kwanza, katika Kata ya Uru Shimbwe kuna shida kubwa sana ya huduma ya mawasiliano ya Radio hasa kwa Redio yetu ya Tanzania na Television yetu ya Taifa. Pili, kuna shida ya huduma ya internet na imesababisha Kata ya Uru Shimbwe ishindwe kutuma taarifa kupitia kwenye zahanati yetu kwenye Shirika la Bima la Afya. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba huduma hizi zinaboreshwa kwenye eneo la Uru Shimbwe?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Patrick Alois Ndakidemi Mbunge wa Moshi Vijijini kwa sababu masuala haya tumekuwa tukiwasiliana na jiografia ya eneo husika tayari ameshanieleza jinsi ilivyo. Hata hivyo, kupitia mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma za mawasiliano vijijini zikiambatana na usikivu wa redio katika maeneo husika tayari Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeshaanza kufanya tathmini katika maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, vilevile katika eneo ambalo ameongelea kuhusu upatikanaji wa data, Serikali tayari imeshatoa maelekezo kwa watoa huduma wote, sehemu yoyote ambapo tutapeleka mradi wowote ule, lazima mradi huo ukajengwe wa kutoa huduma ya kuanzia 3G maana yake ni kwamba, ni lazima sasa Tanzania tutakuwa na miradi au minara ambayo itakuwa inatoa huduma ya internet. Nasema hivyo kwa sababu hapo kabla tulikuwa tunaangalia tu angalau kila Mtanzania aweze kupata mawasiliano, lakini kwa sasa tunalazimika kwa sababu ya mahitaji ya kuelekea kwenye digital transformation maana yake kwamba mahitaji ya internet ni makubwa zaidi ikiambata na eneo la Mheshimiwa Patrick, Moshi Vijijjini. Nashukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote una jukumu kubwa la kuboresha mawasiliano hususan kwenye sehemu za vijijini ambazo hazina mawasiliano ya simu ya kutosha, lakini juzi juzi tumeshuhudia hapa Mfuko huu ukizindua studio za kisasa za TBC wakati bado kuna sehemu hususan za vijijini hazina mawasiliano ya simu ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, nataka kujua ni nini hasa vipaumbele vya Mfuko wa huu wa Mawasiliano kwa Wote?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa ni jukumu la Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kuhakikisha kwamba tunafikisha mawasiliano maeneo ya vijijini, lakini sio maeneo ya vijijini peke yake maeneo yote ambayo hayana mvuto wa kibiashara, kwa sababu kuna maeneo ambayo watoa huduma wengine hawawezi kwenda kuwekeza kwa sababu zao za kibiashara.

Mheshimiwa Spika, vilevile tunapoongelea kufikisha mawasiliano ni pamoja katika maeneo ambayo ni ya mipakani. Pamoja na maeneo ya mipakani, kuna maeneo ya hifadhi, kuna maeneo ambayo kwa kweli ukiangalia katika ramani vizuri ni kwamba hakuna wakazi wengi, lakini hao wakazi waliopo pale wana haki ya kupata huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo, kwa sababu huduma ya mawasiliano tunaichukulia kama ni sehemu ya usalama, sehemu ya huduma ya msingi ya kila Mtanzania na kubwa zaidi ni uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu mawasiliano yanaenda kuwa moja ya njia kuu ya uchumi wa nchi yetu. Hivyo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote utaendelea kufanya tathmini katika maeneo yote ambayo bado yamebaki nyuma kimawasiliano ili yaweze kufikishiwa mawasiliano. Nakushukuru sana.
MHE. AMINA ALI MZEE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, hatua zipi zinachukuliwa na Serikali kuwawezesha vijana wanaofanya biashara mtandao ili kuwezesha mapato ya Taifa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu na mikopo ili kuwezesha upatikanaji wa ajira ya ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali kazi yake ni kuhakikisha kwamba inaweka mazingira wezeshi kwa vijana ili waweze kufanya biashara hiyo. Sambamba na hilo kupitia biashara zozote za kimtandao Serikali imeweza kurasimisha shughuli hizo kwa kuanzisha sheria ya makosa ya kimtandao maana yake kwamba kijana ili aweze kujua mipaka ya namna gani biashara yake akaifanye.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta ya Mwaka 2010, hii yote inatoa guidelines za namna gani kijana anaweza kuingia katika biashara hiyo.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kwa sababu unapofanya biashara lazima kuna transactions zitakuwa zinafanyika, ili sasa kumlinda katika zile transactions Serikali pia ilichukua jukumu la kuanzisha Sheria ya Miamala ya Kieletroniki ambayo sasa transaction yoyote inakuwa inatambulika, anapokuwa anafanya hizi biashara.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kupitia Wizara yetu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia vijana hawa, Serikali ina mpango mzuri wa kutoa elimu ambapo vijana watakuwa wanajua namna gani na sehemu zipi wanaweza kuwa wanapata mikopo kwa ajili ya kujiongezea kipato na hatimaye tunaongeza pato la Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza, nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri, kwa kweli nimehakikisha mwenyewe kwamba kazi inaendelea.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kama unavyojua jiografia ya Wilaya ya Lushoto ni ya milima na mabonde ambayo husababisha kutopata huduma katika maeneo mbalimbali hasa Makanya, Mavului, Mbwei na maeneo mengine ya Mazumbai. Je, ni lini sasa Serikali itaenda kujenga minara ile ili kuondoa kadhia wanayoipata wananchi wa Wilaya ya Lushoto?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Wilaya ya Lushoto ina changamoto ya usikivu wa Radio ya Taifa yaani TBC na hili suala nilikuwa naliongelea mara kwa mara lakini mpaka leo hii hakuna majibu yoyote wala hakuna mnara wowote uliojengwa. Je, ni lini Serikali itaenda kujenga minara ya habari ndani ya Wilaya ya Lushoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hatua ambazo Serikali inazichukua kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwanza kabisa ni kujiridhisha na ukubwa wa tatizo wa eneo husika. Ukubwa huo unaweza ukategemea na tatizo lenyewe, inawezekana katika maeneo fulani mawasiliano hakuna kabisa; maeneo mengine mawasiliano ni hafifu; lakini kuna maeneo mengine ambapo unakuta kwamba mawasiliano yako hapa hayako hapa; kunakuwa na dark sport za kutosha. Sasa Serikali inapofanya tathmini ni kujiridhisha pia na ukubwa wa tatizo ili kujua teknolojia gani ambayo tunaweza kwenda kuitumia pale ili kutatua tatizo la eneo husika kulingana na tathmini iliyofanyika.

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri tumekuwa na mawasiliano mazuri na amekuwa akiwapambania kweli wananchi wa Jimbo lake na sisi kama Serikali kwa sababu ndio jukumu letu na kupitia Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, ibara ya 61(f) na (g) inaeleza kabisa kwamba ni jukumu la Serikali kwenda kufikisha mawasiliano kwa wananchi wote, kwa hiyo, suala lake litaangaliwa baada ya tathmini kufanyika.

Mheshimiwa Spika, vilevile suala la usikivu ni jambo lilelile ambalo pia kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wanaendelea na kufanya tathmini katika maeneo yote pamoja na maeneo ya mipakani kuhakikisha kwamba palipo na changamoto ya usikivu basi Serikali inafikisha mawasiliano katika maeneo husika.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru sana kwa majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri ambayo yanatoa matumaini kwenye maeneo yale ambayo kumewekwa ahadi za kuweka minara. Hata hivyo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Kata ya Masisiwe na Kata ya Udekwa hakuna mawasiliano kabisa na tayari watu wawili wameanguka kutoka kwenye miti wakijaribu kutafuta mtandao na kuumia na kulazwa katika Hospitali ya Ilula mmoja na ya Kilolo mmoja.

Sasa, je, Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi katika kata hizi, kwanza ili kutoa pole kwa watu hao, lakini pili ili kuweza kuona yeye mwenyewe na nafahamu yeye ni mtu ambaye ametembelea maeneo mengi ili aweze kujionea hali halisi na kuweka msisitizo wa kuweka minara katika maeneo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, maeneo yenye mitandao, yenye wananchi wenye matumiani makubwa sana yakutumia vifurushi vya bei ndogo, yalikatishwa tamaa na ongezeko la bei ya vifurushi ambapo ilitarajiwa vishuke. Tunaishukuru Serikali kwamba imerudisha katika ile hali ya kawaida, lakini matumaini ya wananchi ilikuwa ni kushushwa. Sasa je, ni lini Serikali itarudia ule mpango wake wa awali wa kushusha vifurushi, ili Watanzania wakiwemo wananchi wa Kilolo ambao wanataka sana kutumia vifurushi hivi katika shughuli zao za kibiashara, waweze kufurahia bei nafuu ya vifurushi?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba maswali yangu hayo mawili madogo yajibiwe.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Justin Nyamoga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, nimesema kwamba Serikali tayari imeshaanza kufanya tathmini katika Kata ya Irole pamoja na Masisiwe ili tuweze kuingiza katika mpango wa awamu ya tano na ya sita katika mwaka wa fedha wa 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika suala la pili, nafahamu kabisa hili ni swali ambalo Waheshimiwa Wabunge wote wangeweza kuliuliza. Naweza kusema kwamba kazi ya Serikali ya kwanza ni kuhakikisha kwamba ina-stabilize bei iliyopo na hilo ndilo ambalo tumelifanya kwa sasa. Naona kwamba kulikuwa na changamoto ambapo makampuni yaliweza kuwa na bei tofauti tofauti ambazo ziliwaumiza sana wananchi, lakini Serikali ikatoa maelekezo ya kuhakikisha kwamba bei ya hapo awali inarejea kama ambavyo Watanzania walikuwa wanakusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunafahamu kwamba, katika kurejesha hizi gharama za vifurushi, kuna changamoto yake. Kupandisha kifurushi ni mchakato ambao unahusisha ujenzi wa mifumo ambayo itaweza ku-support hicho kifurushi kipya ambacho utakiingiza sokoni. Vile vile unaposema kwamba urudishe maana yake kwamba unaaanza kufanya reverse engineering maana yake unaanza kurudisha kwenye mfumo ule ulioko zamani, kama ulikuwa umeshautoa maana yake sasa inabidi uanze kuusuka tena ili uanze kutoa bei ambazo zilikuwa zinatolewa hapo kabla.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge pia ameongelea namna gani Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba bei hizi, zinashuka zaidi ya sasa ambavyo Watanzania wangetarajia. Changamoto ya biashara ya mawasiliano, kitu ambacho tunakiangalia Serikali ni kwamba hapa tunatakiwa kuangalia tuna-balance namna gani kati ya consumer, watumiaji wa huduma, Serikali pamoja na mtoa huduma. Ni lazima tuangalie ile production cost yake, ni lazima aweze kufanya biashara katika kiwango ambacho anaweza akapata faida ili Serikali pia iendelee kupata kodi lakini kodi hizohizo ziweze kurudi kujenga barabara na zahanati na hatimaye Wabunge katika Majimbo yao wanayotoka tuweze kushuhudia kuna mabadiliko ya barabara na zahanati ambazo zitakuwa zinajengwa. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza nafasi ya swali la nyongeza. Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unalenga kupeleka mawasiliano katika maeneo yote ya nchi yetu. Je, ni lini sasa Mfuko utawezesha upatikanaji wa mawasiliano katika kata na maeneo yasiyo na mawasiliano katika Mkoa wa Manyara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rahhi, kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote jukumu lake la msingi ni kuhakikisha kwamba tunafikisha mawasiliano kwa Watanzania wote, hasa katika maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara. Maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara maana yake watoa huduma wengine hawatoweza kupeleka huduma hiyo kwa sababu wanaongozwa zaidi na business plan zao, business case zao na ndio maana kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, sasa Serikali inafanya tathmini katika maeneo yote ambayo yana changamoto ya mawasiliano katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie kwamba, tumeshaanza kufanya tathmini mipakani pamoja na maeneo maalum ambayo yalikuwa na changamoto kubwa sana ambapo Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakilalamika mara kwa mara, lakini mpaka sasa tathmini hiyo imeshakamilika. Kuanzia mwaka huu wa fedha, tayari tunatarajia kuanza kutangaza zabuni kwa ajili ya kupeleka mawasiliano katika maeneo hayo. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia swali la nyongeza. Changamoto iliyoko Jimbo la Kilolo ni sawa na changamoto iliyoko katika Hifadhi ya Same ambayo katika hifadhi hiyo barabara kuu inapita kuelekea katika Jimbo la Same Mashariki. Katikati ya Hifadhi hiyo, hakuna mawasiliano ya simu, jambo ambalo linapelekea vijana wengi kwenda kufanya mambo ya kiukorofi, kuteka baadhi ya magari na kuwapora wananchi mali zao. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha kwamba inajenga minara ya simu maeneo hayo ili endapo ukorofi kama huo vijana wataufanya, waweze kutoa mawasiliano kwa ajili ya kutetea haki yao? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Zuena Bushiri, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari ina mpango wa kuhakikisha kwamba tunapeleka mawasiliano katika maeneo ya mbuga na hifadhi ili kuhakikisha kwamba maeneo haya yasiwe na changamoto tena kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema. (Makofi)
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana. Pamoja na kwamba kuna changamoto ya mitandao kupitia maeneo mbalimbali ya Tanzania, lakini halikadhalika kuna changamoto pia ya wizi wa kimitandao, tumekuwa tukipoteza fedha nyingi sana kupitia hii mitandao. Swali langu, je,ni lini Serikali itaweza kudhibiti wizi huu wa kimtandao unafanywa na simu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utapeli wa kimtandao viko chini ya makosa ya kimtandao na Sheria ya Makosa ya Kimtandao ya mwaka 2015. Hata hivyo watekelezaji wa sheria hii ni pamoja na vyombo vingine vya dola, ikiwemo na Jeshi la Polishi. Tunafanya juhudi za kutosha kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwa umma, kwa sababu ndicho kitu ambacho ni cha msingi sana kwa Watanzania kuelewa namna gani wanaweza wakatumia simu zao za mkononi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia changamoto ambayo ilikuwepo ni pamoja na wale waliokuwa wanapewa majukumu ya kuandikisha au kuuza zile lines za simu, ambao walionekana kutokuwa na uaminifu na hatimaye kuwa wanawatapeli Watanzania badala ya kusajili line moja kwa mtu mmoja, matokeo yake anajikuta kwamba Mtanzania amesajili line tano kabla ya kuondoka katika kituo cha kusajili lines hizo. Matokeo yake hizi lines zitakapochukuliwa na watu ambao wanania ovu matokeo yake ndio zitakuja kutumika kwa ajili ya matatizo kama hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwa umma lakini pia tunatumia teknolojia ambayo itaanza kudhibiti, matatizo ambayo yangesababishwa na watu ambao wamepewa majukumu ya kuuza hizi lines. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wengine, Serikali bado inayafanyia kazi na kufanya uchambuzi wa kutosha ili kujiridhisha kwamba tunatumia njia gani ambayo itakuwa rafiki zaidi kwa Watanzania bila kuwabugudhi katika maisha yao ya kila siku. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali moja la nyongeza. Changamoto ya mawasiliano iliyopo katika Jimbo la Kilolo inafanana kabisa na changamoto ya mawasiliano ambayo tunayo katika Jimbo la Handeni Mjini, hasa maeneo ya Kwa Magome, Malezi, Mlimani, Konje, Kwediyamba, Kwenjugo, Msasa, Kideleko na Mabanda. Je, ni lini, Serikali itapeleka mawasiliano katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema Serikali inabidi ifanye tathmini, ni kwa sababu tumekuwa na uelewa ambao unatofautiana kidogo. Kuna maeneo ambayo tayari unakuta kwamba kuna mnara mmoja, kuna minara miwili, lakini wananchi wetu wanatamani kuona kila kijiji kina minara mitatu au minne. Kazi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kupitia Serikali yetu, ni kuhakikisha pale ambapo hakuna kabisa mawasiliano na ndipo Serikali inapokwenda kufikisha mawasiliano kwa wananchi. Ndio maana tunasisitiza sana, Serikali tutaendelea kuhakikisha kwamba tunafika katika maeneo husika na kufanya tathmini na kujiridhisha kama tatizo ni kwamba hakuna mawasiliano ama mawasiliano yaliyopo hayana ubora unaotakiwa na kama hayana ubora unaotakiwa basi tutaelekeza TCRA kuhakikisha kwamba inawawajibisha watoa huduma katika maeneo husika kulingana na makubaliano ya utoaji wa huduma nchini. (Makofi)
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba tufanye masahisho katika majina ya vijiji. Kata ya Mkonona ni Nambunda siyo Nambundu na siyo Waniku.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya masahisho hayo, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa dhumuni la uanzishaji Mfuko huu pamoja na madhumuni mengine ni kuziwezesha vile vijiji vya mpakani kuweza kupata mawasiliano ya simu hasa kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchi yetu unakuwepo. Mfuko huu ulianzishwa mwaka 2007, vijiji vile bado vina matatizo makubwa ya mawasiliano. Hivi ninavyoongea hatuna mawasiliano ya simu ya Airtel wala mitandao mingine. Je, wakati mchakato huu wa kutangaza tenda unaandaliwa ni hatua gani za dharura zinachukuliwa hili kuhakikisha vijiji vile vinapata mawasiliano hasa kwa kipindi hiki kigumu ambacho usalama wetu na nchi ya Msumbiji ni mbaya? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tatizo hili la mawasiliano linakwenda sambamba na usikuvu wa redio yetu ya TBC. Katika Wilaya yangu hatuna kabisa mawasiliano ya TBC. Je, ni hatua gani za dharura Mfuko huu unaweza kuisadia TBC ikasikika ndani ya Jimbo langu?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuonyesha ukaribu na Wizara yetu kwa kuhakikisha kwamba anatupatia taarifa sahihi ili na sisi tuweze kuzifanyia kazi kadri inavyowezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ameongelea vijiji ambavyo viko mipakani, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tayari imeshafanya utafiti na tathmini ya vijiji vyote Tanzania nzima siyo Nanyumbu peke yake ambapo maeneo yote ya mipakani tunatarajia kuutangaza tenda kwa ajili ya ujenzi na kuhakikisha kwamba tunalinda mipaka yetu yote. Mipaka ya Mtwara, Namanga, Sirari pamoja na maeneo mengine Serikali tunafahamu kabisa kwamba mawasiliano ni jukumu letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilisema katika jibu la msingi maeneo haya ni yale ambayo mara nyingine hayana mvuto wa kibishara. Ndio maana kupitia Mfuko huu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema ulianzishwa mwaka 2007 kazi yake mahsusi ni kuhakikisha tunafikisha mawasiliano katika maeneo ambayo watoa huduma wengine hawawezi kufikisha mawasiliano, hilo ni jukumu la Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Sasa hivi Ku-migrate kutoka 4G kwenda 5G service providers wengi duniani wamegundulika wanatumia multivendor badala ya kutumia system ambayo imewekwa. Multivendor inaongeza risk ya complicity ya 5G. Wanafanya hivyo kupunguza gharama zao na mteja anapoingia kwenye 5G anataka apate speed anayolipia. 5G inaweza ika-download kitabu cha kurasa 1,000 for 3 to 5 seconds. Serikali imejiandaa vipi ili risk hii ya complicity ya 5G isitokee Tanzania kama ilivyoanza kutoa kwenye nchi nyingine?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, teknolojia ya 5G na 4G vyote hivi vinaendana na uwekezaji. Tunaposema uwekezaji wa 3G, 4G na 5G kwanza lazima Serikali ijiridhishe watoa huduma waliopo wanapotumia hizi spectrum ambazo tumewapitia kwa ajili ya 3G na 4G wameweza ku-deploy vizuri kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoondoka kutoka teknolojia moja kwenda teknolojia nyingine pia inaathari ya moja kwa moja kwa watumiaji wa huduma hii. Kwa hiyo, ni lazima sasa tutengeneze mazingira ili pindi tutakoporuhusu sasa spectrum ya 5G kutumika basi watoa huduma pamoja na watumiaji wa huduma hii wawe tayari kwa ajili ya mabadiliko hayo. Nashukuru.
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nitoe taarifa, katika Jimbo la Igalula kuna watoa huduma wamekwishafika baadhi ya maeneo ambayo wamekwishasainiana mikataba ikiwemo Maguliathi, Migongwa, Makoyesengi na Mbulumbulu lakini wameondoka mpaka sasa hivi hawajui nini hatima ya maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niulize maswali mawili ya nyongeza, Jimbo la Igalula ni miongoni mwa majimbo yenye changamoto kubwa ya mawasiliano na vijiji vingi vimekua, wananchi wana simu lakini hawana mawasiliano hasa katika Vijiji vya Songambele, Kawekapina, Nyauwanga na Simbozamalu. Sasa ni lini Serikali itaiwekea mpango wa kupelekea minara hasa vijiji hivi vilivyokuwa katika Jimbo la Igalula? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; tuna huduma ya mawasiliano katika kata alizozitoa katika jibu la msingi lakini, huduma hizi zimekuja miaka mingi iliyopita, sasa mitandao imekuwa ikisumbua na wananchi hawapati huduma. Je, ni lini Serikali itakwenda kwa watoa huduma kukagua kwa sababu idadi ya watu imekuwa kubwa, wananchi ikifika jioni haipatikani simu na huduma haipatikani. Serikali ina kauli gani kwa watoa huduma ili waweze kwenda kuipitia minara hii ili iweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Protas Daudi, Mbunge wa Igalula kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwanza ameongelea kuhusu watoa huduma ambao wamefika na kuanza kufanya utafiti ili waweze kuweka minara. Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi ambayo anaifanya kwa niaba ya wananchi wake wa Jimbo la Igalula. Mheshimiwa Mbunge alishafika katika ofisi zetu na akatuomba tuweze kuhakikisha kwamba mawasiliano katika Jimbo lake yanapatikana na ndio maana mpaka sasa amesema kwamba, kuna watoa huduma tayari wameshafika katika eneo lake. Hii ni kwa sababu, Serikali imeenda kutekeleza ombi la Mheshimiwa Mbunge. Pia tufahamu kwamba, mikataba tunayowapatia watoa huduma ni mikataba ambayo inachukua takribani miezi tisa katika utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kama ambavyo amesema hatua ya kwanza watoa huduma wanayoifanya, ni kwenda kupata ile lease agreement pale ambapo mnara unatakiwa kwenda kujengwa. Hatua ya pili mtoa huduma anatakiwa kwenda kutafuta aviation permit ili aweze kuruhusiwa kujenga mnara. Hatua ya tatu ni kwenda kutafuta environmental impact assessment permit ili aweze kuruhusiwa na ndugu zetu wa mazingira. Baada ya hapo ndipo sasa apate building permit.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi process zote ni sequential process ambazo hatua moja ikitokea ndio inatoa nafasi ya hatua ya pili kufanyika. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge baada ya kukamilika kwa huu mchakato mzima wa kupata hivi vibali, basi utekelezaji wa ujenzi wa minara hii katika Jimbo lake utatekelezwa bila kuwa na changamoto yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la pili ambalo ameongelea kwamba, kuna minara ambayo ipo lakini haitoi huduma stahiki. Ni kweli kabisa tunatambua kwamba kuna minara mingine ambayo ilijengwa miaka ya nyuma ambapo population ya eneo husika ilikuwa kidogo, iliweza kuhudumia wananchi waliokuwepo kwa kipindi hicho, lakini kwa sababu wananchi wanaendelea kuongezeka maana yake sasa minara hii inaanza kuzidiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo tumeshaelekeza watoa huduma wetu waende kufanya tathmini, ili wajiridhishe tatizo halisi ni lipi, kwa sababu kuna matatizo mengine ambayo yatahitaji kufanya treating tu ya antenna. Mengine itabidi kuongeza capacity, tatizo lingine itabidi kuongeza nguvu ya transmitter na tatizo lingine ambalo litatufanya tukaongeze antenna zingine ili ziweze kuhudumia wananchi wa eneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote ni lazima tathmini ifanyike kwa kina na kuna mengine ambayo yana budget implication, lakini kuna mengine ambayo ni matatizo ya kiufundi peke yake, tayari watoa huduma tumeshawaelekeza na tayari wameshaanza kufanya tathmini katika maeneo yote nchini ili kujiridhisha kwamba tatizo linalolalamikiwa linahusiana na nini hasa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Matatizo yanayowapata wananchi wa Igunga ni sawasawa kabisa na matatizo yanayowapata wananchi wa Jimbo la Buchosa hasa katika Visiwa vya Kome na Maisome. Naomba Mheshimiwa Waziri anieleze kwamba ni lini watajenga minara katika maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Eric Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Buchosa yameshaingizwa tayari kwenye mpango wa utekelezaji katika zabuni itakayotangazwa ya awamu ya sita ili eneo hilo sasa lipate mawasiliano kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Buchosa. Ahsante.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa mujibu wa taarifa ya TCRA asilimia 68 ya Watanzania wako kwenye maeneo yenye mtandao wa kuweza kutoa huduma ya internet, lakini ni asilimia 26 tu wenye simu janja ama vifaa vingine vyovyote vinavyoweza kuwapa access ya internet. Sasa na changamoto kubwa ni kwa sababu ya kodi na vitu vinavyofanania hivyo, sasa kwa kuzingatia kwamba Wizara inataka kuifanya Tanzania iwe katika utaratibu wa kidijitali, wana mkakati gani basi wa kuhakikisha huduma hizi zinapatikana kwa gharama nafuu, ili Watanzania wengi waweze na kuwa na hivi vifaa na hatimaye kuweza kushiriki katika dunia ya TEHAMA na kidijitali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima Mdee kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge alivyosema tuna changamoto hiyo kwa sasa, lakini sasa Serikali tunafahamu kwamba tunaenda kwenye uchumi wa kidijitali, lakini tunapoenda kwenye mfumo wa kidijitali maana yake ni kwamba tunahitaji kuwa na internet penetration na mpaka 2025 tufikie tuwe tumeshafikia asilimia 80 kutoka asilimia 43 ya sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, maendeleo ya dijitali yoyote yanaendana na vifaa ambavyo vita-support matumizi halisi ya teknolojia husika. Mheshimiwa Mbunge pia anafahamu kwamba, tuko kwenye mchakato wa kuangalia namna bora ambayo itasababisha vifaa hivi vitakapokuwa vinaingia nchini, basi viwe vina bei ambazo zitawavutia Watanzania wengi kununua hizi simu ili waweze kutumia teknolojia ambayo itakuwa inatumika. Ahsante. (Makofi)
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, Kata ya Michenjele ambayo iko mpakani na Msumbiji nako kuna tatizo kubwa la usikivu wa mawasiliano ya simu hakuna hata mnara wa aina moja ambao unapatikana kule Michenjele: -

Je ni lini Serikali itapeleka huduma hii kwenye maeneo yale ya mpakani?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Katani kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kata ya Michenjele ipo katika vijiji ambavyo vimeshafanyiwa tathmini kwa ajili ya Awamu ya Sita ya mipakani na border and special zone. Lakini kata hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja kwa mfano Kata ya Mihambwe tayari kuna mtoa huduma wa airtel ambao anaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa minara.

Mheshimiwa Spika, lakini pia Kata ya Mdimba kama ambavyo nilijibu katika swali langu la msingi kuna mtoa huduma tayari ambaye ni tigo ambaye anaendelea na utekelezaji lakini pia kina Kata ya Chaume ambapo tayari kuna mtoa huduma ambaye anaendelea na ujenzi wa mnara katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wilaya yetu ya Igunga hususan Jimbo la Manonga sisi ni wakulima wa pamba, mpunga, madini na mifugo kwa wingi. Katika vijiji kama hicho ambacho nimekitaja cha Ikombandulu, Mwakabuta, Ikungwi Ipina, Utuja na Shalamo ni katika maeneo yenye uzalishaji kwa wingi katika mazao niliyoyataja. Ipi mikakati ya Serikali kuhakikisha maeneo hayo yanapata mitandao ya simu kwa wakati?

Mheshimiwa Spika, maeneo ya Mwisi, Simbo, Choma, Ibologelo na Indembezi wanapata mawasiliano ya simu lakini mitandao hii ipo chini sana hasa kwenye internet. Je, Serikali kupitia wadau wanaotoa huduma katika maeneo hayo ipi mikakati yao na hasa ukitambua sasa hivi Tanzania tuna- launch 5G, nini mikakati ya Serikali kuhakikisha maeneo hayo niliyoyataja tunapata angalau 4G kwa ajili ya kusaidia wataalam, watafiti na waandishi wa Habari…

SPIKA: Ahsante sana umeeleweka Mheshimiwa.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Hususan kwenye vijiji vilivyopo nchini Tanzania, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilivyojibu katika majibu yangu ya msingi kwamba Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tupo katika mkakati wa kufanyia tathmini Kijiji hicho sambamba na vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameshavitaja ili kuhakikisha kwamba tujiridhishe ukubwa wa tatizo baada ya hapo vitaingizwa katika zabuni ya awamu zinazokuja katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, suala la pili kuhusu masuala ya internet. Tunafahamu kwamba kwa sasa hivi tunakoelekea katika uchumi wa kidigitali na tunaelewa kabisa kwamba internet coverage inahitajika ili Watanzania waweze kutumia vizuri katika shughuli zao za hapa na pale. Tumeshaelekeza watoa huduma wote wafanye tathmini katika minara ambayo bado inatumia teknolojia ya 2G ili waweze ku- upgrade na kuweza kutumia teknolojia ya 3G, 4G na hatimaye baada ya kujiridhisha kwamba tutakuwa tunahitaji 5G basi tutakuwa tumefikia huko.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, maeneo mengi ya Mkoani Songwe ikiwepo Kata Maalum ya Mbangala ambayo ni Kata maalum kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya dhahabu yanakabiriwa na changamoto kubwa sana ya mawasiliano. Nataka kufahamu nini mkakati wa Serikali katika kupeleka mawasiliano katika maeneo haya ya Wilaya nzima ya Songwe? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iko kwenye mchakato na katika hatua za awali kabisa katika kuhakikisha inafanyia tathmini Vijiji na Kata zote nchini ili kujiridhisha wapi tuna tatizo la mawasiliano ili tuhakikishe kwamba katika mwaka wa fedha ujao tuweze kuviingiza na kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata mawasiliano.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, changamoto ya wananchi wa Manonga inafanana sana na wananchi wa Jimbo la Kyerwa. Nimekuwa nikiongelea changamoto ya Kijiji cha Kitega, Kata ya Songambele ambacho kipo chini ya mlima na kipo karibu na Rwanda, hakuna mawasiliano ya Redio wala simu wala kitu chochote. Ni mpango gani wa Serikali na wa dharura kuhakikisha kile Kijiji tunakirudisha Tanzania kwa kukipa mawasiliano kwa sababu ni kama wapo gizani. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tayari Serikali kupitia Wizara yetu na kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote tayari tumeshafanya tathmini katika Vijiji na Kata zote zilizopo mipakani na katika maeneo ya mbuga na hifadhi. Tayari tunaenda kuviingiza katika mpango wa kuhakikisha kwamba mwaka huu tunaenda na utaratibu wa kuanza kwanza na maeneo ya mipakani.

Katika siku ambayo tunapitisha bajeti yetu tuliwaambia Waheshimiwa maeneo ya mipakani ndio ambayo tunaenda kuyapa kipaumbele yakiwepo maeneo ya Mheshimiwa Mbunge, ahsante sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi wa Kintanula ni walinzi shirikishi wa hifadhi kubwa kabisa ya Rungo Mhesi Kizigo ambayo ipo pale na wanasaidia kupambana na majangili kwa njia ya mawasiliano. Sasa kupitia mnara huu, wananchi hawana mawasiliano sasa. Ili kuepusha ajali nyingi ambazo zinatokea za watu kuanguka juu ya miti na kuvunjika mgongo na wakati mwingine viuno; je, Serikali inasemaje? Ni lini itakwenda kukamilisha mradi huu ili wananchi hao pia wanufaike na mradi huu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna mnara ambao unajengwa pale katika Kijiji cha Mhanga, ulisimama Kitongoji cha Jirimli, ulikuwa unajengwa na Halotel. Sasa Serikali ipo tayari kuzungumza na Halotel ambao walisimamisha ujenzi wa mnara huu ili waendelee? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, Kijiji hiki kitaingizwa katika utaratibu wa kufanyiwa tathmini ili tujiridhishe ukubwa wa tatizo na kujua kama tunahitaji kwenda kuweka mnara au tunaenda kuongeza tu nguvu ya mnara uliopo ili uweze kuhudumia wananchi wa pale.

Mheshimiwa Spika, pia lengo la Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ni kufikisha mawasiliano kwa wananchi wote. Kwa hiyo, hilo ni jukumu la Serikali, nasi Serikali tumejipanga kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vijiji ambavyo vinahitaji mawasiliano kikiwemo na Kijiji ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja, kitakuwepo ndani ya mkakati wa Kiserikali wa kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, pia kuhusu masuala ya Halotel; katika ujenzi wa minara, wakandarasi wengi ambao wanapewa tender za ujenzi wa minara hii ni kwamba wamekumbana na changamoto nyingi katika kipindi hiki ambacho tulikuwa tuna Covid 19, lakini pia katika baadhi ya vibali ambavyo walikuwa wanaomba, vingine vilichelewa kwa sababu ambazo zilikuwa nje ya uwezo wao. Sasa Serikali imejipanga kwamba katika vipengele ambavyo vinahusisha na vibali ambavyo Serikali moja kwa moja inahusika, tunaenda kuhakikisha kwamba tunashirikiana na wenzetu ambao wanatoa vibali ili vibali vile vinatoka kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake lakini bado ningeomba kwa kuwa maisha ya sasa yanategemea sana matumizi ya simu na wahusika wanaathirika kwa kiasi kikubwa naomba niyataje maeneo hasa ambayo yanahitaji kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo, Kata ya Itundu, hasa Katuli, Ilani, Kiloleni, Mwinyi, Kalembela, Jumbe na Kikwete Kata ya Muungano ni Muungano yenyewe, Magulungu, Isenda, Utenge na Kangeme, Kata ya Usisya ni Usisya Kati, Mabundulu, Katungulu na Majengo. Kata ya Uyogo ni Uyogo yenyewe, Igembesabo, Kasela, Igunguli na Mirambo, Kata ya Ugala ni Ugala yenyewe Izengamatogile na Isogwa, Songambele, Mlangale na Ukwanga na Kata ya Kapilula ni Kata yote, naomba lini wanapatiwa mawasiliano watu wa Urambo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya wananchi wa Urambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli alichokiongea Mheshimiwa Mbunge ni kweli kabisa, kwasababu tayari tarehe 16 Machi 2021 nilifanya ziara katika Jimbo lake la Urambo, na kweli nikagundua kuna maeneo ambayo bado yana changamoto ya mawasiliano. Lakini katika maeneo ambayo tuligundua yana changamoto ya mawasiliano, tulitoa maelekezo ili tathmini ifanyike na kuhakikisha kwamba wananchi wa Urambo hawapitwi mbali na huduma ya mawasiliano kwa ajili ya kujiletea maendeleo kupitia mtandao wa mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jimbo la Tabora Mjini lina kata 29 na
vijiji 41, na katika vijiji hivyo vingi havina mawasiliano ya simu na vijiji vingine vipo karibu kabisa, kilomita mbili tu kutoka mjini lakini bado ni vigumu kupata mawasiliano; mathalani kata ya Itetemya. Ninaomba kuuliza;

Je, ni lini Serikali itatufanyia mpango wa kuongeza angalau minara ili mawasiliano yaweze kuwa mazuri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA
HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakasaka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mawasiliano ni takriban nchi nzima ina changamoto mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ambazo zinatokana na teknolojia iliyowekwa katika eneo husika, lakini pia mnara uliowekwa pale inategemea kwamba uliwekwa katika wakati upi, kwamba iawezekana kulikuwa na population ya watu wachache na sasa wameongezeka sasa mnara unaweza ukazidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunafahamu kabisa kwamba kuna maeneo ambayo kutokana na sababu za kijiografia unakuta kwamba katika kata moja mawasiliano yapo katika vijiji sita lakini Kijiji kimoja kinakuwa kinakosa mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali kupitia Wizara yetu imeanza kufanya utafiti wa kujiridhisha ili tuweze kupata teknolojia ambayo tutakuwa tunafikisha huduma ya mawasiliano katika zile sports ambapo unakuta kwamba ni Kijiji kimoja tu ambacho kimekosa mawasiliano lakini tufikishe kwa teknolojia ambayo ni nafuu na yenye gharama nafuu. Waheshimiwa Wabunge pia tuweze kusaidiana kuhakikisha kwamba tunawaelewesha wananchi wetu kujua kwamba mawasiliano yatafika kwasababu bahati nzuri mmetusaidia kupitisha bajeti ambayo itatufikishia mawasiliano katika vijiji vyetu.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Waziri kwa majibu mazuri, pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza kwa kuwa asilimia 90 mpaka 95 ya wateja wapya kwenye mitandao ya simu wanapatikana kutokana na mfumo huu wa freelancer na Kampuni yetu ya TTCL imekuwa ikisuasua katika kuongeza wigo wake.

Je, lini sasa TTCL au Wizara itaagiza TTCL waweze kutumia mfumo huu ili waweze kuongeza wigo wao?

Swali langu la pili ni kwamba mfumo huu wa freelancer siyo ajira kamili, I mean vijana wamekuwa wakilipwa kwa njia ya commission na haya makampuni kwa mfano yana vijana kama laki moja hivi ambao wako kwenye mfumo huo. Sasa kutokana na kutokuwa na sheria inayotambua mfumo huu, hawa vijana wamekuwa wakitumia wakati mwingine loophole ya kuyashitaki haya makampuni kwamba wameajiriwa na hivyo kuleta hofu ya haya makampuni kuendelea kuajiri hawa vijana.

Je, Serikali italeta lini hapa sheria ili sasa itambue mfumo huu kwamba ni mfumo kamili ambao unasaidia kuajiri vijana wengi ambao hawana kazi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI MAWASILIANO TEKNOLOJIA NA HABARI:
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiswaga Gedion Mbunge wa Kalanga kama ifuatavyo: -

Kwanza kabisa naomba nimpongeze Mbunge wa Kalenga Mheshimiwa Kiswaga kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya Jimbo na wananchi wake wa Kalenga. Haya ni matakwa ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kupitia ukurasa wetu wa 96, 97, 98 na ukurasa wa 113 kuongeza wigo wa mawasiliano kufikia asilimia 94. Sasa kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, tayari imeshatoa maelekezo kwa TTCL kuanza kutumia mfumo huu na mpaka sasa wana-agrigator watano na freelancer takribani 3000. Kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha kwamba tunasimamia hili ili waendelee kuongeza wigo mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, lakini suala la kamisheni kati ya freelancer na watoa huduma ni suala ambalo Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba inaweka mfumo mzuri ambao utatumika katika kusimamia ili kuwepo na uwajibikaji kwa freelancer pamoja na watoa huduma ili kuhakikisha kwamba tunaondoa hili gap ambalo lilikuwa linasababisha na kutokana na uhalifu uliokuwa unatokea sababu ya freelancer kutumia hizi national ID kwa matakwa yao na si matakwa ambayo yamewekwa kisheria, ahsante.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Wizi wa kimtandao unaongezeka kila kukicha; kwa kuwa TCRA kwa maana ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania wana uwezo wa kujua namba fulani inayofanya wizi ipo mahali fulani: Je, kwa nini Serikali sasa haioni kwamba uwepo utaratibu maalumu wa Jeshi la Polisi pamoja na TCRA kuzuia watu kabla hawajaibiwa kwa sababu wana uwezo wa ku-trace hiyo namba? Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, pale namba inapotumika ambapo namba ile siyo ya kawaida kwa mfano hizi namba zinazoanzia 15000 na kuendelea ndiyo namba ambazo ni za mitandao yenyewe, unakuta zinatuma ujumbe kwa mfano umeshinda labda shilingi milioni 600, umeshinda shilingi milioni sita, umeshinda kiasi kadhaa; anatuma mtu anaendelea kukatwa fedha zake. Sasa nauliza je, pale mwananchi ambapo anakuwa hana kosa na kosa ni la hawa wenye mitandao wenyewe kwa mfano TiGO au Vodacom, kuna mkakati gani wa Serikali ili wananchi ambao hawakufanya makosa yoyote waweze kubanwa hizi kampuni za simu kulipa fedha zao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kwa kazi kubwa anayoifanya kwa maslahi ya wananchi wa Jimbo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, naomba niwashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya kwa kushiriki katika michakato mbalimbali ya kuishauri Serikali ili tuweze kuboresha huduma kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo Mheshimiwa Mwakasaka ameliongelea ni kwamba Serikali inamkakati gani wa kujaribu kuzuia wizi kabla hata haujatokea? Sheria ya makosa ya Kimatandao ya Mwaka 2015 ambayo ilianzishwa mahususi kwanza kutambua makosa yenyewe ya kimtandao ni yapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kikubwa ni kwamba kupitia Kamati ambayo imeshaundwa, kwa nafasi hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuisimamia vizuri Kamati hiyo, kazi yake kubwa ni kwenda kutoa elimu kwa Umma. Inapotoa elimu kwa Umma ni pale ambapo sasa Mtanzania anajua kabisa kwamba ni kosa lipi ambalo linahusika na sheria hii na kulihalalisha kwamba nikilifanya basi hatua za kisheria zitachukuliwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni kujenga uwezo kama ambavyo nimesema kwamba kuna kitengo maalum cha makosa ya kimtandao, ambayo ni Cybercrime Unit ambayo inashughulika na makosa haya. Lakini kuwajengea uwezo na kuleta vitendea kazi ambavyo…

NAIBU SPIKA: Elekea kwenye jibu la pili hilo ameshaelewa Mheshimiwa Mwakasaka. Jibu swali lake la pili. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali la pili anaongelea kuhusu message ambazo wanakuwa wanatumiwa. Nalo hili linaangukia katika makosa yale yale ya kimtandao tunasema unsolicited messages. Hili tayari tumeshakaa na watoa huduma tumeshaanza kuweka mkakati wa kuhakikisha kwamba, tunawasaidia na kuelewa kwamba namna gani message hizi hazitakiwi kutumwa kwa watanzania ambao hawajaziomba. Matokeo yake wanakuwa na makosa ambayo hawajahusika moja kwa moja. Ahsante. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyoneza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba kuuliza. Katika mkoa wetu wa Iringa bado kuna maeneo ambayo yanasuasua katika mawasiliano na hasa katika ya Nyazwa, pamoja na kuwa kuna mnara wa Halotel lakini bado kabisa maeneo mengi sana hakuna mawasiliano. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba Mkoa wote wa Iringa kata zote zinapatiwa mawasiliano ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ritta Kabati Mbunge wa Viti Maalum kutoka Iringa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba inafikisha mawasiliano kwa wananchi wote na kuhakikisha kwamba tunaimarisha upatikanaji wa mawasiliano. Lakini naomba kupokea changamoto hii ili tuweze kutuma wataalamu wetu wakafanya tathmini na ili wajiridhishe kchangamoto iko na ukubwa gani ili tuchukue hatua stahiki. Ahsante.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote nikupongeze kwa kazi kubwa na nzuri ambayo unaifanya katika Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. ((Makofi)

Mheshimiwa Spika, mawasiliano ni kila kitu katika maisha ya mwanadamu, bila mawsiliano kila kitu kinakuwa siyo sawasawa. Kwa muktadha huo; Jimbo la Mchinga lina tarafa nne ndani ya tarafa mbili angalau klidogo mawasiliano ya simu yanapatikana lakini ndani ya tarafa mbili nyingine, Tarafa ya Milola na Tarafa ya Mipingo hakuna kabisa mtandao. Kukosekana kwa mtandao unasababisha pale kuwa kama kisiwa.

Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itatuletea mtandao katika Tarafa ya Mpingo na Milola na hasa katika vijiji vya Mipingo, Namakwia, Namkongo, Matakwa na Kiwawa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete Mbunge wa Mchinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Salma Kikwete kwa kuendelea kuwapigania wananchi wake ili wapate huduma ya mawasiliano ili waweze kufanya shughuli zao za kibiashara kama ambavyo Watanzania wangetamani.

Mheshimiwa Spika, lakini kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba tunafiksiha mawasiliano kwa Watanzania wote. Hivyo basi changamoto kama hii inapotokea katika maeneo tofauti tofauti basi kama Serikali ni wajibu wetu kupokea changamoto hii ili tuhakikishe kwamba wataalamu wetu tuwatume katika maeneo specific ili wakapate ukubwa wa tatizo na namna ambavyo tutaenda kulishughulikia kulingana na eneo husika lenyewe. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge wa Mchinga amesema, yeye kwake ni tarafa mbili, mimi nina tarafa tano. Kati ya tarafa tano tarafa tatu hazina mawasiliano kabisa. Na utaona hapa sisi wa Lindi tunazungumzia Tarafa, siyo Kijiji, ni tarafa nzaima ambayo ina kata kadhaa na vijiji kadhaa.

Mheshimiwa Spika, swali langu kwa Serikali, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuja kukomboa Mkoa wa Lindi na suala la mawasiliano kwa sababu pamekuwa na ahadi za miaka nenda, miaka rudi kulimaliza hili jambo?

Hii habari ya kusema tutakuja kutembea ndio majibu yamekuwa haya kila siku. Nataka commitment ya Serikali kuja kutusaidia Mkoa wa Lindi tuondokane na tatizo hili.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Nnauye Mbunge wa Mtama kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Nape Nnauye kwa sababu amekuwa akitoa taarifa ya changamoto ya mawasiliano ya wananchi wake wa Jimbo la Mtama. Na kwa bahati nzuri nimekaa naye sana na tayari tumeshakubaliana mimi na yeye tutatoka hapa kwenda mpaka Mtama kwenda kujiridisha tukiwa na wataalamu wote kiasi kwamba sasa hili tatizo pindi ambapo tutajua kwamba tatizo lipo wapi ili tuweze sasa kuingiza katika mpango wa utekelezaji wa mwaka ujao. Ahsante sana.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa changamoto iliyopo Jimbo la Nsimbo linashabihiana kabisa na changamoto ya Jiji la Kitalii la Arusha; tunazo kata ambazo zilikuwa zamani Wilaya ya Arumeru kabla hatujawa jiji Kata kama ya Olmoti ambayo ina mitaa ya Nafco na Milongoine, Kata ya Terrat ambayo ina mitaa ya Ulepolosi, Masikilia na Engavunet na Kata ya Olasiti ambayo ina mtaa wa Oloesho bado zina changamoto kubwa ya mawasiliano ya simu.

Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu kwenye kata na mitaa hiyo ambayo nimeitaja?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mrisho Gambo Mbunge wa Arusha Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Mrisho Gambo kwa kazi nzuri anayoifanya katika Jimbo lake la Arusha.

Mheshimiwa Spika, nimeshafika Arusha, na maeneo ambayo ameyataja nayatambua kweli kabisa yana changamoto hiyo. Tayari tumeshaelekeza wataalamu wetu; kwa sababu changamoto ya Arusha si ujenzi wa mnara isipokuwa ni kuongeza nguvu katika minara iliyopo ili iweze kuhudumia wakazi wa Arusha kwa sababu wamekuwa wakiongezeka kwa kasi kubwa hivyo basi minara iliyokuwepo ilikuwa imeshazidiwa nguvu. Tayari wataalamu wetu wameshaanza kufanya kazi na pindi kazi hii itakapokamilika basi changamoto hii itakuwa imeweza kutatuliwa. Ahsante sana.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi pia.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Biharamulo tuna vijiji 75. Kati ya vijiji 75 vijiji 25 havina mawasiliano kabisa, kabisa, na bado tuna shida, ukiachilia mbali vitongoji. Sasa ni nini hatua ambayo Serikali imachukua kwa ajili kuweza kuboresha mawasiliano? Ukizingatia watu hawa nao inabidi washiriki mchango wa maendeleo wa nchi hii lakini wameachwa mbali kwa sababu wako katika maeneo ambayo hayana mawasiliano kabisa. Nataka kusikia kauli ya Serikali kuhusu vijiji 25 vya Biharamulo.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ezra Mbunge wa Biharamulo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Kagera, Wilaya ambayo imebahatika na ambayo itanufaika katika mpango wa utekelezaji mradi wa mipakani basi na Biharamulo inaenda kupata miradi takribani sita.

Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana na kuhakikisha kwamba kipindi kitakapofikia tena cha kuleta bajeti ili tuweze kuhakikisha kwamba maeneo mengi yanapata mawasiliano basi aweze kutuunga mkono kuhakikisha kwamba bajeti hii iweze kwenda kujibu mahitaji ya Watanzania. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza:

Mheshimiwa Spika, changamoto ya mawasiliano iliyopo Kata ya Chilangala inafanana na Kata za Kitaya, Mnongodi na Namtumbuka ambazo zipo mpakani na Msumbiji na ambako kama utakuwa unafahamu sasa hivi kuna changamoto ya kiusalama kule. Naomba mpango mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba Kata hizi kwa sasa zinakuwa na mawasiliano ya uhakika ili isaidie katika…

SPIKA: Zipo kwenye Wilaya gani hizi Kata.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, zipo Wilaya za Mtwara Vijijini na Tandahimba ambazo zinapakana na jirani zetu wa Msumbiji. Kwa hiyo naomba mpango wa haraka wa Serikali wa kuhakikisha kwamba Kata hizi zote zinapata mawasiliano ya uhakika.

Swali langu la pili ni kwamba minara ambayo inajengwa vijijini sasa hivi ni kwa ajili ya mawasiliano ya sauti tu, kwa ajili ya voice, lakini kuna mahitaji makubwa ya internet sasa hivi vijijini na hata Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi inasema tunataka kuboresha upatikanaji wa internet vijijini. Sasa Serikali ina mpango gani wa kuboresha au ku-upgrade minara hii ili iweze kuhakikisha kwamba hata data zinapatikana vijijini?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARl: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nitumie fursa hii kuwapongeza sana Wabunge wote wa Mtwara kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakitupatia tunapofika katika maeneo yao ya kazi. Maeneo haya ya Kitaya pamoja na maeneo mengine ya Lulindi, Tandahimba pamoja na Newala tulishafika na kupitia fedha ambayo Serikali ilipitishiwa hapa Bungeni tayari kuna miradi ambayo imepangwa kwenda kutekelezwa kupitia miradi ya mipakani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi kabisa, kwa sababu dhamira ya Serikali ni ileile ya kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanapata mawasiliano. Maeneo ya mipakani tunayaangalia kwa umuhimu wake kwa sababu ni masuala ya kiusalama.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika Kata ya Kitaya, Mbunge anafahamu, mimi na yeye tulikwenda mpaka katika Kata ya Kitaya ambapo kuna mradi wetu ambao umeshakamilika na tayari umeshawashwa na huduma ya mawasiliano tayari imeshafika katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo suala la uhitaji wa internet kwanza kabisa mpaka sasa Serikali inaboresha miundombinu ya Mkongo wa Taifa. Kwa upande wa Kusini mpaka sasa ukitoka pale Mangaka kwenda Mtambaswala takribani kilometa 72, tunajenga mkongo wa Taifa siku za hivi karibuni mradi huo utakamilika. Hivyo basi, hata ile miradi sasa ambayo itakuwa inahitaji data maana yake ni kwamba Serikali imeshaelekeza watoa huduma wote wahakikishe miradi yote ambayo itajengwa kuanzia sasa iwe inatoa huduma ya 3G na 4G na kuendelea. Ahsante. (Makofi)
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri na ya kuridhisha ya Serikali, nina swali fupi la nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, ili kuongeza wigo wa usikivu nchini, TBC haioni kwamba kuna haja ya kuwasiliana na redio za kijamii ili kuziwezesha kujiunga na TBC Taifa wakati wa matokeo makubwa kama vile taarifa ya habari na mengineyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Othman Hija kama ifuatavyo: -


Mheshimiwa Spika, ni mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba Shirika la Utangazaji TBC linafanya mahusiano mazuri na Shirika la Utangazaji la Zanzibar. Baada ya kukamilisha katika miradi yetu ya awali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, tuna mpango wa kuja kushirikisha na redio zingine ili pale ambapo Shirika la Utangazaji Tanzania linapokuwa na changamoto ya miundombinu basi iweze kushirikisha redio nyingine ambazo zitakuwa zinasaidiana. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwanza kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini eneo la Bukiko ni kweli kupitia UCSAF, ulijengwa mnara wa Halotel lakini kuna shida kubwa; ule mnara unategemea umeme jua, kiasi kwamba nguvu ya umeme inapopungua kunakuwa hakuna mawasiliano, lakini vile vile kuna shida kubwa ya Internet kwa sababu mtandao ulioko pale ni wa 2G; Sasa naiomba Serikali niweze kujua, ni lini sasa Serikali itapeleka jenereta kwenye eneo lile? Vile vile iwasiliane na watu Halotel ili kuweka mtandao wa zaidi ya 2G kwa maana ya 3G na vyovyote itakavyowezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema kwenye majibu, ni kweli kuna shida kubwa ya mawasiliano kwenye maeneo mengi, kwenye visiwa vya Ukerewe; na Serikali imejibu kwamba itaenda kupitia maeneo yote yenye shida: Ni lini sasa kazi hii itafanywa na Serikali ili timu iende kule, ifanye uchunguzi na hatimaye marekebisho yafanyike ili kuwe na mawasiliano mazuri kwenye eneo lile? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kuhusu jenereta; kwanza kabisa ile site ya mawasiliano iwe imekamilika, haijalishi kama ni umeme wa TANESCO au ni wa Solar, ni lazima site iwe na backup generator. Kwa vile Mheshimiwa Mbunge amelifikisha hili, basi Serikali inalipokea na tutalifanyia kazi ili kujiridhisha na changamoto ambayo ameiongea.

Mheshimiwa Spika, vilevile ni azma ya Serikali sasa kuhakikisha kwamba, maeneo mengi nchini yanapata huduma ya internet, yaani kutoka katika huduma ya zamani ya 2G kwenda 3G. Hapo kabla Wizara tayari ilishatoa maelekezo kwa watoa huduma ili kuhakikisha kwamba, minara inayojengwa kuanzia sasa basi iwe na huduma ya 3G.

Mheshimiwa Spika, tuna minara ya aina mbili; minara ambayo inatokana na ruzuku ya Serikali, lakini vilevile kuna minara ambayo inatokana na wawekezaji wenyewe. Ile ambayo inatokana na ruzuku ya Serikali tayari Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umeshaanzisha mchakato wa ku-up grade minara yote ambayo itakuwa ina 2G kwenda kwenye 3G. Pia Serikali imeelekeza kwa watoa huduma wengine katika minara ambayo sio ya Serikali, ihakikishe kwamba, inaona umuhimu sasa wa kuelewa kwamba, sasa teknolojia ya 3G inahitajika kwa Watanzania wote. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Hivi karibuni na katika Jimbo lote la Ndanda kuna matatizo sana ya network na hasa eneo la Ndanda ambako ndio Makao Makuu ya Jimbo na mtandao tunaotumia pale sana ni Vodacom pamoja na Airtel na Airtel kuna hisa za Serikali. Hata hivyo, wataalam walipopewa taarifa mpaka leo hawajaenda kufanya marekebisho. Sasa kwa nini Mheshimiwa Waziri asiwakumbushe watu wa Airtel kwenda kuufanyia marekebisho mnara ule ili mawasiliano yawe bora?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kimsingi ameomba Serikali tuongee na watu wa Airtel ili wakarekebishe changamoto iliyojitokeza. Tunaipokea changamoto hiyo na tutawasiliana na wenzetu wa Airtel ili kwenda kuifanyia kazi hiyo changamoto. Ahsante.