Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Eng. Kundo Andrea Mathew (18 total)

MHE. FLATEI G. MASSAY Aliuliza:-

Je, ni lini minara ya simu itajengwa katika Kata za Endahagichen – Ndamilay, Mewadan – Magong na Endaghadat – Qamtananat katika Jimbo la Mbulu Vijijini ambazo hazina mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ni siku yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa katika Bunge lako hili tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniamini ili nikatetee na kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika Jimbo la Bariadi. Pia naomba niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Bariadi kwa kunichagua kwa kishindo na hakika hawajapoteza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kuniamini na kuniteua kuwa msaidizi wake katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote pamoja na wadau wengine wa sekta ya mawasiliano ina jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yote ya vijijini na mijini yasiyo na mvuto wa kibiashara. Mpaka sasa jumla ya kata 633 zimekwishapata huduma za mawasiliano nchi nzima ambapo ujenzi unaendelea katika kata zingine 361 kupitia ruzuku ya Serikali. Watoa huduma kwa uwekezaji wao wamefikisha huduma za mawasiliano katika kata 1,692.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tarehe 25 Januari, 2021 tuliwekeana sahihi ya mikataba ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 59 zenye vijiji 166 katika zabuni ya awamu ya tano. Vilevile mwezi huu tunatarajia kutangaza zabuni nyingine ya awamu ya sita ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 74 zenye vijiji 206.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) una miradi 15 katika Jimbo la Mbulu Vijijini katika kata 13. Kata zenye miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano ni pamoja na Yaeda Ampa, Yaeda Chini, Maghang, Masieda, Bashay, Eshkesh, Geterer, Gidihim, Hayderer, Maretadu, Masqaroda, Endamilay, na Tumati. Jumla ya minara 14 imekamilika kujengwa katika kata 12 kati ya minara 15 inayopaswa kujengwa, hii ni sawa na asilimia 87.5 (87.5%) ya utekelezaji wa miradi hiyo. Bado mnara mmoja ambao unatarajiwa kujengwa na Shirika letu la Mawasiliano Tamnzania (TTCL) ambao utakamilika kabla ya mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizo za Serikali, bado kuna takribani kata 1,365 kati ya Kata 3,956 zilizopo Tanzania Bara zikiwemo kata za Jimbo la Mbulu Vijijini na wadi 16 kati ya wadi 111 zilizopo Zanzibar ambazo bado zina changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inavifanyia tathmini vijiji vingine vyote Tanzania Bara na Visiwani vikiwemo Vijiji ambavyo viko katika Jimbo la Mbulu Vijijini ambavyo ni Endahagichen – Ndamilay, Mewadan – Magong na Endaghadat – Qamtananat, na hatimaye vijiji husika vitaingizwa katika orodha ya vijiji ambavyo vitajumuishwa katika kutangaza zabuni katika mwaka wa fedha 2020/2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano ya simu katika Kata ya Uru Shimbwe Jimbo la Moshi Vijijini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote inatambua changamoto ya ukosefu wa huduma za mawasiliano katika Kata ya Uru Shimbwe yenye Vijiji vya Shimbwe Chini na Shimbwe Juu. Tathmini katika Kata hii ilifanyika mwezi Machi mwaka 2021 na kubainika kuwa vijiji hivi vina changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano. Hivyo, Vijiji hivi vya Kata ya Uru Shimbwe vitaingizwa katika zabuni zijazo za kupata mtoa huduma wa kuvifikishia huduma za mawasiliano. Nashukuru.
MHE. AMINA ALI MZEE Aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kuhamasisha vijana nchini kujiunga na biashara mtandao?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbali mbali katika kuweka mazingira wezeshi nchini ya kuvutia wananchi wengi kujiunga na biashara mtandao hususan vijana. Mwaka 2015 Serikali ilitunga Sheria ya Miamala ya Kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala ya kielektroniki inayofanyika kimtandao.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa inapitia Sheria na tozo mbalimbali ambazo ni kikwazo kwa vijana, wabunifu wa TEHAMA na wale wanaochipukia (start-ups) ili kuweka mazingira wezeshi ya vijana kushiriki kwenye biashara mtandao. Hii hatua inakwenda sambamba na maboresho yanayoendelea ya kupunguza tozo za leseni za maudhui mtandaoni, kazi ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2021.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Posta Tanzania imeanzisha jukwaa la kutangaza na kuuza bidhaa na huduma kwa njia ya mtandao ambapo maduka 270 ya kuuza na kununua bidhaa yamesajiliwa na jukwaa hili ambalo linapatikana kupitia tovuti https://www.postashoptz.post. Jukwaa hili limeunganishwa na mtandao wa vituo 670,000 duniani. Jukwaa hili linatoa fursa kwa wafanyabishara ikiwemo vijana kutumia mtandao huo kufanya biashara mtandao kwa kuunganisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa na huduma ulimwenguni. Ahsante.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu kwenye maeneo ambayo hayana mawasiliano ya simu katika Jimbo la Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imetekeleza miradi ya ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu katika maeneo mbalimbali Wilaya ya Lushoto. Mpaka sasa kuna miradi 16 ya ujenzi wa minara katika Wilaya ya Lushoto katika kata 15 ambapo tayari miradi 8 imekamilika na miradi mingine 8 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Miradi hiyo iko katika Kata za Baga, Kwai, Kwekanga, Malibwi, Malindi, Manolo, Mayo, Mbaramo, Mgwashi, Mlola, Mponde, Rangwi, Shume, Ubiri na Vuga. Miradi ya ujenzi wa minara katika Kata za Kwekanga, Kwai, Malindi, Manolo, Mbaramo, Mayo, Mponde na Mlola imekamilika na tayari inatoa huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa minara ya mawasiliano unaendelea katika Kata za Shume, Ubiri, Rangwi, Mgwashi, Vuga, Baga, Kwai na Malibwi. Ujenzi wa minara hii utakamilika mwezi Disemba 2021. Aidha, Kata zilizobaki Mfuko utazifanyia tathmini na zitaingizwa katika zabuni zijazo.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu katika Kata za Masisiwe, Nyanzwa, Irole na Ibumu ambazo zina shida kubwa ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI, alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Serikali ya Awamu ya Sita, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Rais wa Awamu ya Sita katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania. Sambamba na hilo, naomba niwapongeze wanawake wote wa Tanzania, kwa sababu wameendelea kuonesha mfano wa kuigwa, tukishuhudia katika Awamu ya Nne, mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Katika Awamu ya Tano, alikuwa mwanamke wa kwanza Tanzania kuwa Makamu wa Rais na katika Awamu ya Sita, amekuwa mwanamke wa kwanza katika Nchi yetu ya Tanzania kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kuendelea kuniamini kumsaidia katika nafasi ya Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Lazaro Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kilolo lina Kata 24 ambapo Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeishakamilisha utekelezaji wa miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata tatu ambazo ni Lugalo ambapo ina mnara wa Halotel, Udekwa ambapo kuna mnara Vodacom na Ukwega ambapo kuna minara miwili ya Tigo na Halotel.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizi za Serikali baadhi ya kata za jimbo hili zinachangamoto za upatikanaji wa huduma ya mawasiliano kama vile Kata za Masisiwe, Nyanzwa, Ibumu na baadhi ya maeneo ya Kata ya Irole. Jiografia ya jimbo hili ni ya milima na miti mirefu ambapo kwa kiasi kikubwa sana inaathiri upatikanaji wa huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Irole kuna baadhi ya maeneo yanapatikana huduma za mawasiliano kupitia mnara wa mawasiliano wa HTT, uliobeba watoa huduma watatu ambao ni Airtel ambayo inatoa teknolojia ya 2G, Vodacom ambapo wanatoa teknolojia ya 2G na 3G na Tigo ambao wanatoa 2G na 3G. Pamoja na uwepo wa huduma za mawasiliano kutoka kwa watoa huduma niliotaja, bado kuna maeneo ndani ya Kata ya Irole yana changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) iliifanyia tathmini Kata ya Ibumu na hatimaye kukijumuisha Kijiji cha Ilambo katika zabuni ya awamu ya tano ya mradi wa kufikisha mawasiliano mipakani na kanda maalum. Mradi huu unatekelezwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ambapo mikataba ya utekelezaji wa mradi huo ilitiwa saini tarehe 6 Julai, 2020. Mradi huu utakapokamilika utaweza kuhudumia Vijiji vya Ibumu, Kilala, Kidewa, Ilambo na Kilumbwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote UCSAF itavifanyia tathmini vijiji vya Kata za Masisiwe, Nyanzwa na baadhi ya vijiji vya Kata ya Irole ambavyo huduma ya mawasiliano imekuwa changamoto kwa kiasi kikubwa sana. Huduma inatolewa na mnara wa HTT uliopo na hatimaye vijiji husika vitaingizwa katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-

Je, ni lini changamoto ya mawasiliano ya simu Wilayani Nanyumbu itamalizika katika Kata za Likokona, Mkonona, Nangomba, Nandete, Napacho, Lumesure, Michiga na Chipuputa?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Ally Mhata, Mbunge wa Nanyumbu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ina jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yote ya vijijini na mijini yasiyo na mvuto wa kibiashara. Mpaka sasa kupitia tumeshafikisha miradi 1,057 ambapo miradi 686 imeshakamilika na miradi 371 inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizo za Serikali bado kuna maeneo mengi yakiwemo maeneo ya Jimbo la Nanyumbu ambayo hayana huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, umevifanyia tathmini vijiji vya Kata ya Likokona, Mkonona, Nangomba, Nandete, Napacho, Lumesure, Michiga na Chipuputa katika Jimbo la Nanyumbu. Vijiji vya Kata hizi vimeingizwa katika Mradi wa Mpakani na Kanda Maalum awamu ya sita ambapo zabuni tarajiwa kutangazwa kabla ya kwisha kwa mwaka wa fedha 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Jimbo la Nanyumbu vilivyoingizwa katika zabuni hiyo inayotarajiwa kutangazwa ni kama ifuatavyo:-

1. Kata ya Likokona Vijiji vya Misawaji, Namaka, Msinyasi, na Likokona;

2. Kata ya Mkonona Vijiji vya Nambundu, Waniku and Namaromba;

3. Kata ya Nandete Vijiji vya Chivikikiti na Nakole;

4. Kata ya Lumesure Kijiji cha Lumesure;

5. Kata ya Michiga Kijiji cha Makong’ondera; na

6. Kata ya Chipuputa Vijiji vya Mpwachia, Nakatete na Ngalinje.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Vijiji vya Kata za Nangomba na Napacho vitaingizwa kwenye awamu nyingine ya miradi ya kufikishiwa huduma za mawasiliano kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mawasiliano ya simu kwenye Vijiji vya Igalula ambavyo havina mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daud Protas Venant, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ina jukumu la kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini ambayo hayana mvuto wa kibiashara. Mpaka sasa Mfuko wa Mawasiliano umeshatekeleza miradi 686 na bado kuna miradi katika kata 371 ikiwa inaendelea na utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Igalula lina kata 11 ambapo Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imetekeleza miradi sita ya mawasiliano katika Jimbo la Igalula ambapo imejengwa minara sita ambayo imetolewa na watoa huduma katika Kata tano ambazo ni Kizengi, Loya ambayo ina Miradi miwili, Lutende, Miswaki pamoja na Tura.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata zenye watoa huduma wa mawasiliano katika Jimbo la Igalula ni 10 ambazo ni Igalula yenyewe, Kigwa, Loya, Lutende, Miswaki, Kizengi, Miyenze, Tura, Goweko pamoja na Nsololo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada za Serikali, Kata ya Mmale na baadhi ya maeneo ya Jimbo la Igalula bado yana changamoto ya mawasiliano na kupitia Mfuko wetu wa Mawasiliano tunaendelea kufanya tathmini, ili tujiridhishe specifically kwamba kuna changamoto katika maeneo yapi ili yaingizwe katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni zitakazotangazwa katika siku za usoni kadri upatikanaji wa fedha utakapokuwa unaruhusu. (Makofi)
MHE. YAHYA ABDULWAKIL AHMED aliuliza: -

Je, Shirika la Posta Zanzibar halioni umuhimu wa kuchimba kisima katika Jimbo la Kwahani katika Kitongoji kilichopo karibu na Ofisi hiyo ili kukuza ujirani mwema?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Abdul Wakil Ahmed Mbunge wa Kwohani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Shirika la Posta Tanzania ni taasisi ya Kimuungano ambapo kwa upande wa Zanzibar ina jumla ya Ofisi tisa, kati ya Ofisi hizo, Unguja kuna Ofisi tano ambazo zipo Kijangwani, Shangani, Mahonda, Jambiani na Makunduchi; na Pemba kuna Ofisi nne zilizopo Chakechake, Wete, Mkoani na Kengeja.

Mheshimiwa Spika, Shirika limekuwa na utaratibu kila mwaka wa kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii kwa kuzingatia mtiririko wa fedha na bajeti ya mwaka husika. Kwa kipindi cha miaka mitatu yaani 2018 hadi 2020 Shirika katika kuchangia huduma za kijamii kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar – SMZ imefanya yafuatayo: -

(i) Mwaka 2018, Shirika lilitoa vifaa mbalimbali katika Kituo cha wazee cha Amani ili kusaidia matunzo ya wazee katika kituo hicho.

(ii) Mwaka 2019, Shirika lilitoa vifaa mbalimbali katika Hospitali ya Mnazi Mmoja ili kusaidia akinamama wanaojifungua.

(iii) Mwaka 2020, Shirika lilitoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kusaidia wazee wanaotunzwa katika kituo cha kulelea Wazee cha Welezo kilichopo Unguja.

Mheshimiwa Spika, Shirika linaendelea na utaratibu wake wa huduma kwa jamii kulingana na bajeti. Shirika litaangalia uwezekano wa kuchangia uchimbaji wa kisima katika kitongoji kilichopo karibu na ofisi katika kuendeleza ujirani mwema kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu, ahsante.
MHE. KATANI A. KATANI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka Mawasiliano ya Simu yenye usikivu katika Kata ya Litehu, Ngunja na Mkwiti Wilayani Tandahimba?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmed Katani Mbunge wa Tandahimba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unatekeleza miradi saba katika kata sita za Jimbo la Tandahimba kupitia Mradi wa Awamu ya nne na tano . Miradi hiyo inatekelezwa katika Kata za Chaume, Mdimba Mnyoma, Mkoreha katika Kijiji cha Chikongo, Ngunja. Kuna miradi miwili mmoja uko Kijiji cha Ngunja na mwingine Namindondi Juu, lakini katika Kata ya Mihambwe, na Namikupa utekelezaji wa mradi uliopo katika hizo Kata unaendelea.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na jitihada hizo za Serikali, bado kuna maeneo mengi ya Jimbo la Tandahimba ambayo yana changamoto za mawasiliano. Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano imevifanyia tathmini vijiji vya Kata za Litehu, Ngunja na Mkwiti katika Jimbo hilo.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba zinaingizwa katikazabuni ya mradi wa mipakani na kanda maalumu ya Kanda Maaalum awamu ya sita yaani Border and Special Zone Phase six Mradi huu unatarajiwa kutangazwa kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mawasiliano katika Kijiji cha Matinje Ikombandulu ambalo ni eneo la machimbo na lina idadi kubwa ya watu ili kurahisisha biashara katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unatekeleza miradi mitatu katika Jimbo la Manonga. Miradi hiyo inatekelezwa katika Kata za Igoweko; mnara huu unahudumia pia Kata ya Uswaya, Sungwizi pamoja na Ngulu. Utekelezaji wa miradi katika Kata hizi umekamilika.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itakifanyia tathmini Kijiji cha Matinje Ikombandulu na hatimaye kijiji hiki kitaingizwa katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni zitakazotangazwa katika mwaka wa fedha 2021/22, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi wa Kijiji cha Kintanula Kata ya Mwamagembe katika Jimbo la Manyoni Magharibi mawasiliano ya uhakika ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unatekeleza miradi minne katika Kata mbili za Jimbo la Manyoni Magharibi. Miradi hiyo inatekelezwa katika Kata za Mgandu ambapo kuna miradi miwili na Idodyandole miradi miwili. Utekelezaji wa miradi yote miwili katika Kata ya Mgandu na mradi mmoja katika Kata ya Idodyandole umekamilika. Utekelezaji wa mradi mmoja katika Kata ya Idodyandole katika Kijiji cha Mbugani bado unaendelea.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itakifanyia tathmini Kijiji cha Kintanula Kata ya Mwamagembe na hatimaye kijiji hiki kitaingizwa katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni zitakazotangazwa katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-

Je, ni lini Kata 16 zisizo na mawasiliano ya simu katika Wilaya ya Urambo zitapatiwa mawasiliano ya simu na kuwaondolea wananchi adha ya kutokuwa na mawasiliano kwa muda mrefu?

Je, ni kwa nini kuna maeneo yenye minara ya mawasiliano ya simu lakini kuna matatizo ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Urambo lina jumla ya Kata 18 ambapo Kata zote zina huduma ya mawasiliano isipokuwa vijiji baadhi katika Kata Tisa za Kiloleni, Itundu, Imalamakoye, Ugalla, Vumilia, Nsondo na Uyogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Utundu na Ukondamoyo zitafikishiwa huduma za mawasiliano na kampuni ya simu ya Vodacom ifikapo Oktoba, 2021, Kata za Nsondo na Uyogo zitafikishiwa huduma za mawasiliano na kampuni ya Airtel ifikapo Oktoba, 2021, Kata ya Vumilia itafikishiwa huduma za mawasiliano kupitia kampuni ya simu ya Halotel ifikapo Septemba, 2021 pamoja na Kata ya Ugala itakayofikishiwa huduma na kampuni ya simu ya TTCL ifikapo Septemba, 2021. Aidha Kata za Kiloleni na Imalamakoye zitaingizwa kwenye miradi ya mfuko itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sababu mbalimbali zinazoweza kusababisha kukosekana huduma ya mawasiliano kwenye maeneo yenye minara ya simu ikiwa ni pamoja na hali ya kijiografia ya eneo husika kama vile uwepo wa milima, mabonde na uoto wa asili wenye miti mirefu ambayo huzuia huduma za mawasiliano. Hali ya kukosekana kwa nishati ya umeme wa uhakika pia inaweza kusababisha minara kushindwa kutoa huduma za mawasiliano. Ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, Serikali haioni uamuzi wa kutaka ifikapo tarehe 1 Mei, 2021 wasajili wa namba za simu za mkononi mitaani (freelancers) wawe katika maduka unaweza kufuta ajira zaidi ya 40,000 na kudhoofisha lengo lake la ajira milioni nane ifikapo mwaka 2025?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Kalanga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tarehe 16 Februari, 2021 Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliwaelekeza watoa huduma kutekeleza takwa la kikanuni la usajili wa laini za simu kibayometria kwa kuwatumia mawakala wanaokidhi vigezo kwa mujibu wa Kanuni ya 10 ya Kanuni za Usajili wa Laini za Simu ya 2020 (The Electronic and Postal Communications (SIM Card Registration) Regulations, 2020 GN No. 112 ya 2020.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa freelancers kwenye sekta, kiuchumi na katika kulinda ajira zao, tarehe 14 Aprili, 2021 Serikali ilisitisha zuio kwa watoa huduma kutowatumia freelancers katika usajili wa laini za simu kibayometria, kwa kutoa taarifa kwa umma na kwa kuwaandikia watoa huduma barua ya kuondoa zuio hilo.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma imetengeneza rasimu ya mwongozo wa kuwatambua na kuratibu kazi za freelancers ili kuondoa mapungufu yaliyojitokeza na kuweka bayana uhusiano kati ya watoa huduma na freelancers, ahsante.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mikakati gani ya ziada ya kudhibiti tatizo la utapeli na wizi wa kimtandao kupitia simu za mkononi?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imechukua hatua za kuweka mazingira salama kwa wananchi hususan kwenye mitandao kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 Serikali ilitunga Sheria ya Makosa ya Mitandao kwa lengo la kutambua kisheria makosa yanayofanyika kwenye mitandao ili kuweza kuchukua hatua stahiki yanapobainika makosa hayo; na vile vile, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala inayofanyika kimtandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilianzisha Kitengo cha Uhalifu wa Mitandao chini ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa makosa ya kimitandao ikiwemo wizi wa aina yoyote kwenye mtandao na kuandaa majalada ya kufungulia mashtaka kwa kusaidiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. Watuhumiwa wanaokamatwa kutokana na matumizi mabaya ya mitandao huchukuliwa hatua stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Februari, 2021 Serikali imeunda Kamati ya Taifa ya Kusimamia Utatuzi wa Matumizi Mabaya ya Huduma na Bidhaa za Mawasiliano ambayo inahusisha Wizara na taasisi zote zinazohusika katika kushughulikia makosa ya mtandao. Kamati hiyo ni Kamati ya kudumu na inaishauri Serikali namna ya kutatua changamoto za mitandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Watoa Huduma wa Simu za Mkononi imeanzisha mfumo kupitia namba 15040 wa kupokea na kuzifungia namba ambazo zimeripotiwa na kuthibitika kutuma ujumbe au kupiga simu za utapeli. Baada ya kuthibitisha namba hizo kufanya vitendo hivyo, namba husika hufungiwa na kitambulisho cha NIDA kilichotumika kusajili namba hiyo kufungiwa pia, lakini vile vile hata kifaa ambacho kimetumika pia(simu) kinafungiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali itaendelea kuongeza jitihada za kuelimisha Umma matumizi mazuri na sahihi ya TEHAMA kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Ahsante. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu katika Kata ya Litapunga?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kufatia mabadiliko aliyoyafanya katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na baadaye kuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuniteua na kuniapisha kuendelea kuwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Taknolojia ya Habari.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe Mbunge wa Nsimbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kata ya Litapunga ina jumla ya vijiji nane ambavyo ni Kaburonge “A”, Kaburonge “B”, Kambuzi “A”, Kambuzi “B”, Kambuzi Halt, Bulembo, Lukama pamoja na Litapunga.

Mheshimiwa Spika, Kata hii imekuwa ikipokea huduma za mawasiliano kutoka kata Jirani za Katumba na Kanoge zenye huduma ya mawasiliano ya Mtandao wa Halotel na Vodacom.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itafanya tathmini ya kiufundi ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Kata ya Litapunga ili kupata uelewa wa pamoja na ukubwa halisi wa changamoto ili kuelekeza ufumbuzi unaoendana na changamoto zilizopo.

Mheshimiwa Spika, iwapo tathmini hiyo itabainisha kuwa utatuzi wa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano iliyopo unahitaji kuwa na mnara katika kata hiyo, basi Serikali itaingiza kata hii katika zabuni zitakazotangazwa katika siku za karibuni kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya ujenzi wa mnara wa mawasiliano wa Halotel katika Kata ya Chilangala ambapo mkataba ulisainiwa mwaka 2020 lakini mpaka Septemba, 2021 mradi huo haujaanza?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARl alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) katika zabuni ya awamu ya nne ya kufikisha mawasiliano maeneo ya vijijini, iliingia mkataba wa kufikisha huduma ya mawasiliano ya simu katika Kata 114 ikiwemo Kata ya Chilangala na Kampuni ya Halotel (Viettel) mnamo tarehe 24 Januari 2020. Utekelezaji wa mkataba huo ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi tisa yaani tarehe 23 Oktoba 2020. Lakini kutokana na changamoto ya UVIKO-19 utekelezaji wa mradi huo ulichelewa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kutokana na ucheleweshaji wa utekelezaji wa mradi huo ulipelekea watoa huduma wengine kuboresha huduma za mawasiliano katika kata hiyo ambapo Kata ya Chilangala ina mawasiliano ya Mtandao wa Tigo ambao wana minara miwili katika Vijiji vya Chilangala na Namdimba. Hivyo basi, Serikali haitojenga mnara huo katika Kata ya Chilangala, na hivyo kuzielekeza fedha hizo katika maeneo mengine yenye changamoto zaidi za mawasiliano. Ahsante.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha usikivu wa Radio ya Taifa (TBC) katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiboresha usikivu wa TBC kwa kutenga fedha katika bajeti ya maendeleo kila mwaka ili kuyafikia maeneo yasiyo na usikivu wa TBC kwa nchi nzima yakiwemo maeneo ya Zanzibar. Miradi iliyotekelezwa na TBC ni pamoja na kufunga mitambo ya kurushia matangazo ya redio katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

Mheshimiwa Spika, aidha, miradi ya upanuzi wa usikivu wa TBC inaendelea kutekelezwa katika Mikoa mipya ya Songwe, Njombe na Simiyu. Vilevile upanuzi huo unaendelea kwa upande wa Visiwa vya Unguja na Pemba. Miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo Machi, 2022.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuiwezesha TBC ili maeneo yote nchini ambayo hayana usikivu yakamilike ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoainishwa katika Ilani ya uchaguzi ya CCM (2020 – 2025) Ibara ya 125 (f). Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la mawasiliano ya simu katika maeneo ya Bukiko, Chabilungo, Kitale na maeneo mengine yenye tatizo hilo Visiwani Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, eneo la Bukiko lina mnara wa Halotel uliojengwa kwa ruzuku ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). Eneo la Chabilungo linapata huduma za mawasiliano kupitia watoa huduma ambao ni Tigo, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) pamoja na Vodacom.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itafanya tathmini kwa mara nyingine katika maeneo ya Chabilungo, Bukiko, Kitale na maeneo mengine katika Jimbo la Ukerewe ili kubaini mahitaji halisi ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo hayo, Ahsante.