Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Miraji Jumanne Mtaturu (8 total)

MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya ujenzi wa barabara ya urefu wa kilomita tano kwa kiwango cha lami Wilayani Ikungi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imepanga kufanya usanifu na tathmini ya gharama za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Ikungi. Utambuzi wa barabara hizi umekuwa shirikishi ili kutoa kipaumbele kwenye barabara zenye umuhimu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, hadi Machi, 2021, TARURA imetoa shilingi milioni 598.22, kati ya shilingi milioni 890.89 zilizotengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 97.92 katika ya Wilaya ya Ikungi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali itaomba kuidhinishiwa shilingi milioni 925.08 kwa ajili ya matengenezo yenye urefu wa kilomita 92.6. Vilevile Shilingi bilioni 1.4 zitatengwa kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mihyuge Wilayani Ikungi.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kufanya usanifu na kujenga barabara kwa kiwango cha lami kwenye maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Ikungi kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itafikisha umeme katika vijiji 28 ambavyo bado havijapata umeme kati ya vijiji 50 vya Jimbo la Singida Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Singida Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kupeleka umeme vijijini na kuufikisha katika vijiji vyote vya Tanzania Bara ifikapo mwezi Desemba, 2022.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Singida Mashariki lina jumla ya vijiji 50. Vijiji 22 tayari vina umeme; vijiji 12 vinapatiwa umeme sasa kupitia Mradi wa Ujazilizi (Densification) ulioanza kutekelezwa katika Mkoa wa Singida mwezi Novemba, 2020 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2021.

Mheshimiwa Spika, vijiji 16 vilivyobakia vinaendelea kupatiwa umeme kupitia utekelezaji wa Mradi wa REA wa kusambaza umeme vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ulioanza kutekelezwa mwezi Machi, 2021 na utakaokamilika mwezi Desemba, 2022. Gharama ya mradi ni bilioni 8.47.
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: -

(a) Je, ni lini Serikali itajenga Vituo vya Afya vya Issuna, Ikungi, Makiungu, Ntuntu na Misughaa ili kurahisisha huduma za dharura Wilayani Ikungi kwa kuwa Wilaya hii inapitiwa na Barabara ya Dodoma – Mwanza ambayo imekuwa na ajali za mara kwa mara?

(b) Je, ni lini Serikali itapeleka Gari la Wagonjwa ili kuwahisha majeruhi na wagonjwa katika Hospitali za Rufaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshmiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi iliyoanza kujengwa mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo hadi mwezi Mei 2021 ilikuwa imepatiwa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali hiyo. Hospitali hiyo itasaidia kuokoa maisha ya majeruhi wa ajali zitakazotokea eneo la Ikungi katika barabara ya Dodoma hadi Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi Mei 2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi shilingi milioni 900 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya Ihanja na Sepuka. Ujenzi wa Vituo hivyo umekamilika na vinatoa huduma ikiwemo huduma za dharura za upasuaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapitia Sera ya Zahanati katika kila Kijiji na Kituo cha Afya katika kila Kata na itafanyiwa maboresho yenye tija zaidi ili ili ujenzi uwe wa kimkakati badala ya kila Kijiji au kila Kata.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya Ikungi ina magari matatu ya kubebea wagonjwa ambayo yapo katika Vituo vya Afya Ikungi, Sepuka na Ihanja ambayo yote yanaendelea kutoa huduma za rufaa za dharura ndani na nje ya wilaya ya Ikungi. Ahsante.
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Shule ya Sekondari ya Kidato cha Tano na Sita Mungaa ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kipindi cha Kampeni mwaka 2020 alipopita Jimbo la Singida Mashariki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa ujenzi wa shule 26 za wasichana, moja katika kila Mkoa na ujenzi wa shule 1,000 za sekondari kwenye kata zisizo na shule za sekondari ili kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na vikwazo hususani kwa watoto wa kike kutembea umbali mrefu. Vilevile, Serikali itafanya upanuzi wa shule za sekondari 100 kuweza kupokea wanafunzi zaidi wa kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa shule zote mpya za sekondari na upanuzi wa sekondari za kidato cha tano utafanyika kwa awamu. Awamu ya kwanza ya ujenzi itaanza mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 220. Kabla ya kuanza ujenzi, Serikali itafanya tathmini ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari na mahitaji ya upanuzi wa sekondari za kidato cha tano na sita ikiwa ni pamoja na Shule ya Sekondari Mungaa.
MHE. MIRAJI J. MTATURU Aliuliza: -

Je, Serikali ina Mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Mang’onyi ili kuongeza tija ya kilimo cha mbogamboga kwenye Kata za Mang’onyi na Makiungu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu leo ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa, napenda nichukue fursa hii kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyeniwezesha kufika siku ya leo na kwa Ukuu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kubwa kwangu na kuahidi kwamba nitailinda imani hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Singida Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya Mang’onyi ambayo ipo Mkoani Singida imeendelezwa kwa kujengewa banio linalopokea maji kutoka Bwawa la Mwiyanji na takribani hekta 50 kati ya hekta 450 zimeendelezwa kwa kujengewa miundombinu ya umwagiliaji na sehemu ya shamba lililobaki hufikiwa na maji kwa njia ya asili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kukamilisha ujenzi wa Skimu ya Mang’onyi.
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itarudisha huduma ya treni Manyoni – Singida?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Singida Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TRC katika bajeti ya mwaka 2022/2023 imetenga fedha kwa ajili ya kufanya tathmini na maadalizi ya awali ya kufufua njia ya Manyoni – Singida yenye urefu wa kilometa 115 ambayo ilifungwa takribani miaka 30 iliyopita. Lengo la kufufua njia hii ni kuboresha usafirishaji wa mizigo na abiria pamoja na kukuza uchumi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) inaendelea na mchakato wa ununuzi wa wakandarasi watakaofanya tathmini ya mahitaji na maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi huo. Ahsante.
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga nyumba za Walimu katika Halmashauri ya Ikungi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA(MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Tais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu Mbunge wa singida Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya mahitaji ya Nyumba za Walimu Nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya Ikungi.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Ikungi ina mahitaji ya nyumba 454 na nyumba zilizopo ni 172, ili kukabiliana na upungufu uliopo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Wilaya Ikungi imetenga Shilingi Milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nne za Walimu katika shule za Mandigu Kata ya Munga, Nali - Kata ya Siuyu, Mankumbi - Kata ya Kikio na Mau - Kata ya Ikungi.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu kwa Halmashauri ikiwemo na Halmashauri ya Ikungi kadri fedha zitakavyopatikana.
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga stendi ya kisasa Ikungi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ina uhitaji wa stendi ya mabasi yenye ubora itakayowezesha huduma bora za usafiri.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri imekwishalipa fidia ya eneo la ukubwa wa hekari tano kiasi cha shilingi milioni 36 lililopo katika Kijiji cha Muungano Kata ya Unyahati ili kupisha ujenzi wa stendi hiyo.

Mheshimiwa Spika; katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023, Halmashauri imetenga kiasi cha shilingi milioni 110 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi hiyo.