Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Salma Rashid Kikwete (46 total)

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza, lakini kabla ya kuuliza swali la nyongeza, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na nimshukuru Mheshimiwa Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniteua kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza ni kuhusu huduma ya TASAF. Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuongeza huduma hii hasa kwa watu wetu maskini kutoka katika Mkoa wetu wa Lindi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia maendeleo ya jamii, lakini zaidi kwa siku ya kwanza tu ameweza kuuliza swali hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika Mkoa wa Lindi nikitolea tu mfano kwa sasa tuko Lindi DC, Lindi Manispaa, Nachingwea, Ruangwa pamoja na maeneo mengine. Niseme tu kwamba tumepokea hoja hii, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa tumefikia asilimia
70 tumebakiza asilimia 30 yenye vijiji 5,690 na tumepanga katika mwaka huu wa fedha unaokuja wa 2017/2018 tutaweza kutambua na kuandikisha kaya zilizobakia 355,000
na naamini Lindi pia itakuwa ni mojawapo.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Sambamba na hilo, tunajua walimu ni changamoto pamoja na kwamba Serikali imefanya kazi kubwa na nzuri katika jambo hili. Kwenye eneo la shule ya Kimambi; na shule ya Kimambi iko kwenye mpaka wa Liwale na Kilwa. Shule hii ina upungufu sana na walimu na sasa hivi kuna walimu wasiozidi watatu. Hata hivyo walimu wakipangiwa ndani ya Mkoa wa Lindi hasa kwenye vile vijiji wengi hawaripoti na hata wanaporipoti kinachojitokeza ni kutorudi kwenye maeneo yao. Serikali inasemaje juu ya jambo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli shule anayozungumza mama yangu ni kweli shule ambayo kwa kweli ipo mpakani. Na mimi nilipokuwa nikisafiri, nikienda Liwale, nikizunguka Mkoa wa Lindi, ukiangalia kijiografia ni shule ambayo ipo mbali zaidi. Kama taarifa ya sasa, shule ya Kimambi ambayo inaonekana ina walimu watatu, naomba tulichukue hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo naomba niseme kwamba Afisa Elimu wa eneo hili sasa kupitia chombo hiki, leo tuko live, nimwelekeze kuhakikisha kwamba shule ile anaitembelea na by Ijumaa tupate status kwamba amefanya nini kuhakikisha shule hiyo inakuwa na walimu kama katika maeneo mengine yalivyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuondoe sana suala la uonevu katika maeneo mengine, wengine wanaonekana kama hawana thamani kuliko sehemu nyingine, sasa wale tuliowapa dhamana katika Wilaya zetu wahakikishe wanafanya kazi hiyo kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma inayostahiki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, niwie radhi sana, nilitaka kuongezea kwenye jibu la Naibu Waziri kwamba ni kweli walimu hawa au watumishi hawa tunapowapangia wanakutana pia na changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli pia kwamba mazingira ya nchi yetu hayako sawa yote. Yako maeneo yana hali mbaya sana kimazingira, kimiundombinu na huduma nyingine; lakini kubwa ni nyumba za watumishi. Kusema ukweli ni jukumu la mamlaka hizi za Serikali za Mitaa kuangalia mazingira hayo na hata watumishi hao wanaporipoti kuwasaidia kwa kiasi kinachotosheleza ili waweze kukubali kwenda kukaa maeneo yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunaweza kuwapangia; lakini unampangia mtu anafika toka siku kwanza mtoto wa kike analia tu mpaka unashangaa amekonda, amepunguza, hata yaani alivyokuja ni tofauti na hawa ni watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuwe wakweli, Wakurugenzi wetu wakati mwingine wanayoyafanya siyo sawa. Hivi kumpatia usafiri binti mdogo au kijana mdogo anayeanza kazi na Halmashuri ina rasilimali ikampeleka na gari mpaka kile kituo wakampokea vizuri, lakini sehemu nyingine wanafanya na sehemu hawafanyi. Hili jambo ndilo linalopelekea kuwa na upungufu katika baadhi ya maeneo.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nisisitize na niseme hapa, sisi Wabunge ndio walezi, ndio viongozi kwenye maeneo husika. Tuwe karibu sana; tunaposikia watumishi wamepangwa, tujue hatma yao na mpaka siku watakapokwenda kuripoti kwenye vituo kama jukumu letu kama walezi lakini pia kama tunawajibisha mamlaka husika ili zitekeleze wajibu wao. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo amenipatia kutokana na swali langu ambalo nimeliuliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu yake mazuri ambayo umenipatia, amesema hakuna taarifa zozote za kitabibu ambazo zimekuja kwake kuhusiana na madhara yanayotokana na utumiaji wa hizo simu kwa kusikiliza masikioni. Mimi ninao ushahidi wa kutosha, je, yuko tayari nimletee mtu au watu kuhusiana na suala hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kuna baadhi ya madereva wa vyombo vya moto, nikisema vyombo vya moto mnajua ni nini, wanapoendesha huwa wanasikiliza simu na kutokana na kusikiliza huko wengi wao wameweza kupata madhara na hatimaye wengi wanapoteza maisha na hasa vijana ambao ndio nguvukazi kubwa. Je, Serikali itaanza lini, kwa sababu mmesema mtatoa elimu, Serikali itaanza lini kutoa elimu hiyo ili kunusuru maisha ya vijana hawa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mimi sio Daktari nakubaliana na Mheshimiwa Mama yangu ampeleke huyo mtu kwa wenye dhamana na afya ili wakamchunguze na taarifa ya kitabibu itakapotufikia tutachukua hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Madereva naomba nianze sasa kwa kuchukua fursa hii kuwaasa Madereva wote wanaoendesha vyombo vya moto kutosikiliza simu wakiwa katika mwendo. Kama ni lazima asikilize simu asimamishe chombo cha moto halafu ndipo asikilize simu. Kusikiliza simu huku unaendesha ni kuhatarisha maisha yake lakini vilevile ni kuhatarisha maisha ya abiria ambao wakati mwingine wamewabeba. Tutaendelea kutoa elimu hii na kuendelea kutoa makatazo haya mara kwa mara kila tunapopata fursa ili kuhakikisha tunaokoa maisha ya watu wetu. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, walimu wengi walipata fursa ya kwenda kujiendeleza na waliweza kujiendeleza, pale wanapokuwa wanafanya hayo masomo yao katika ngazi ya shahada wanapokwenda kwenye ile Block Teaching Practice walimu hawa wanapangiwa kwenye shule za sekondari na wanapomaliza bado walimu hawa wanarejeshwa kwenye shule za msingi. Wanaporejeshwa kwenye shule za msingi, yale waliyosomea hayapo kwenye shule za msingi bali yapo kwenye shule za sekondari.
Serikali hapa ina utaratibu gani wa kubadilisha au wa kutengeneza mitaala kuhusiana na shule za msingi ili wakitoka kule warudi kule kule walikotoka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Mama yangu Salma Kikwete anazungumzia changamoto za jinsi gani tuweze kuboresha elimu yetu kwa watu walioko katika vyuo wanapoenda kwenye katika zile field practical na wanapoenda kufundisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni wazo kwa sababu bahati nzuri Mheshimiwa ni mwalimu anajua changamoto gani zipo na vipi tuziboreshe. Mimi naomba tulichukue hili kama wazo jema, kwamba nini tufanye hasa katika suala zima la mitaala kiujumla wake, hata hivyo, tuangalie ni jinsi gani wanafunzi wetu wanapokuwa katika masomo, kile kitu ambacho anaenda kufanyia field practical na iwe best practice akienda kwenye kazi. Kwa hiyo, nasema huu ni ushauri mzuri, Serikali tumeuchukua, tunachukua mawazo mazuri, kwa sababu tuko katika mchakato wa kuboresha elimu yetu iwe elimu shindani tunachukua mawazo haya kwa ajili ya kuyafanyia kazi vizuri. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TAKNOLOJIA:
Mheshiwa Naibu Spika, ahsante sana. nampongeza Mheshimiwa kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongezea tu kwamba lengo la kufanya mafunzo kwa vitendo ni kutoa fursa kwa wanafunzi kuweza kufanya kwa vitendo kile ambacho wanajifunza. Katika teaching practice jambo kubwa ambalo linaangaliwa ni ule mfumo wa ufundishaji yaani kwa kingereza tunaita pedagogical skills, jinsi ambavyo mwalimu anaweza akalihimili darasa, anaweza akafanya yale ambayo yanatakiwa kumudu darasa lake. Kwa hiyo, mwalimu ambaye anajifunza mafunzo ya sekondari principal za darasani kwenda kujifunza, hata akienda kufanya katika shule za msingi hakuna jambo lolote ambalo linaharibika. Ndio maana wapo walimu wa sekondari wanapangiwa kwenda kufundisha shule za msingi kwa sababu kinachoangaliwa ni ule uwezo wa mwalimu kufanya ule ufundishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na nini anachokifundisha, ukiangalia maudhui ya mtaala katika elimu ya msingi ni ya kiwango cha chini kuliko ya sekondari. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba mwalimu ambaye ana uwezo wa kufundisha sekondari atakuwa ni mwalimu mzuri sana katika kufundisha shule za msingi. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Sambamba na swali la msingi la Mheshimiwa Bobali napenda niulize swali langu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tunafahamu kwamba kwenye ukanda wa Pwani wavuvi wake ni maskini sana hasa katika mikoa hiyo iliyotajwa na ninataka nizungumzie Mkoa wa Lindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Lindi hauna viwanda, rasilimali pekee iliyopo ni ya bahari na wavuvi wanategemea bahari hiyo ili kujipatia riziki zao. Wavuvi hao wote kule wanavua samaki wengi sana matokeo yake baada ya kuvua samaki wale kwa kuwa wanakosa soko kinachofanyika, samaki wale ni kuwakausha kwa mazingira ya kwetu tunaita ng’onda. Samaki wale wanafanywa kuwa ng’onda yaani samaki wakavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaamini kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ya viwanda. Je, Serikali ina mpango gani juu ya kutuletea au ya kuhakikisha kwamba wavuvi wale wanatengenezewa viwanda ili kuondokana na umaskini waliokuwa nao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Lindi sasa ni ya viwanda na ushahidi upo tayari wa kutosha kutokana na malighafi hiyo ya upatikanaji wa gesi. Lindi inanukia katika viwanda na tayari maeneo kama ya Kilwa yameonesha mfano, kuna kiwanda kikubwa sana cha mbolea ambacho kinaenda kujengwa pale. Nina imani kwa uwepo wa malighafi hii ya samaki na nina imani kwa kuwa Serikali yetu ya Awamu ya Tano ni Serikali ya viwanda na kwa kuwa Mheshimiwa Mwijage na Wizara yake wanafanya kazi kubwa sana ya kuhamasisha viwanda viweze kujengwa na sekta binafsi, ninaamini wawekezaji watavutika na wataenda kuweka kiwanda cha uchakataji wa samaki katika eneo la Lindi na kuondoa kilio hiki cha kukosekana kwa kiwanda cha samaki katika mwambao wetu huu wa Pwani. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeamua kuuliza swali hili kwa sababu ya msingi, kwanza, naomba nieleze, mimi ni Mwalimu kitaaluma na mada hii ya shilingi na senti inafundishwa katika shule zetu za msingi.
Kwa kuwa inafundishwa katika shule zetu za msingi, zana ni sehemu muhimu sana katika ufundishaji kwa mwalimu na ujifunzaji kwa mwanafunzi. Hii hupelekea kufanya somo lieleweke kwa ufasaha na kwa urahisi zaidi badala ya kutumia maneno mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuondoa hizi senti, ninaamini kwamba mtoto huyu wa Kitanzania ambaye hajui hizi senti ni kumwekea wakati mgumu sana na siyo kwa mwanafunzi tu bali hata kwa mwalimu.
Je, Serikali haioni kwamba mtoto huyu ananyimwa haki yake ya msingi ya kuzijua hizi senti? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, umesema kuondoa na kuweka sarafu zenye thamani kubwa kunaimarisha mfumuko wa bei, lakini naomba mtambue kwamba hakuna bilioni moja isiyoanzia na senti tano. Shilingi bilioni moja ni lazima ianzie na senti tano. Hata bajeti zinapokuja tunaambiwa kwamba bajeti hii ni ya Shilingi bilioni moja na senti kadhaa. Sasa tunapoondoa tunaweka uhalisia gani wa senti yetu hiyo ambayo ni senti tano? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua fika kwamba mtoto huyu wa Kitanzania anatakiwa kufundishwa na ndiyo maana mada hizi zipo katika shule zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu langu la msingi namba (b) nimesema kwamba, fedha hii bado ni halali kwa matumizi halali ndani ya nchi yetu na Serikali kupitia Benki Kuu haijaziondoa fedha hizi sokoni, bado fedha hizi zipo na zinapohitajika zinapatikana kwa matumizi husika.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali langu la nyongeza linaendana na swali la msingi namba 347.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara ya Kiguza kupitia Hoyoyo hadi Mvuti inaunganisha Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani na katika kipindi kilichopita mvua nyingi sana zimenyeesha na hatimaye kusababisha kukatika kwa daraja na kukata mawasiliano baina ya mikoa hii miwili.
Sasa Serikali inatusaidiaje juu ya barabara hii tukiamini kwamba ujenzi wa barabara hii utasaidia sana kupeleka malighafi au rasilimali nyingi tukiamini kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ya viwanda na kutakuwa na vigae vitakavyosafirishwa kupitia barabara hii. Naiomba Serikali itupe majibu kwamba inatusaidiaje juu ya suala hili kuhakikisha ile barabara inakamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete kwa kulikumbusha hili kwa sababu lilishaletwa kupitia Mkoa wa Pwani kupitia Mbunge wa Mkuranga pamoja na Wabunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Pwani na sasa kwa sababu mama naye ameshindilia hapa, mimi naomba tu nichukue fursa hii kuiagiza TANROADS kwanza ikaangalie hali ya hii barabara kwa sasa hasa pale ambapo pamekatika. Halafu tujadiliane na wenye barabara ambao ni Halmashauri juu ya tufanye nini kwa pamoja kati ya Serikali Kuu na Halmashauri kurekebisha barabara hii kwa sababu kwanza barabara hii ni muhimu sana kwani ni kiungo muhimu kati ya malighafi inayotoka nje ya Pwani na inayoingia Mkuranga. Kwa hiyo, ni barabara mojawapo ya kuwezesha viwanda kukua.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la nyongeza ni kama ifuatavyo; mwaka 2016 tulipata tatizo kule Lindi kwenye shule ya sekondari ambayo ni shule kongwe. Wananchi wamejitahidi kadri walivyoweza lakini bajeti yake ni shilingi bilioni mbili. Serikali itatusaidiaje juu ya ujenzi wa shule hiyo ambayo iliungua moto mwaka 2016? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Salma Kikwete kwa sababu amekuwa akijitolea sana kuhusu kuinua elimu katika Mkoa wa Lindi, na hasa hii shule ya sekondari ya Lindi, ameichukua imekuwa kipaumbele kikubwa sana kwake. Kwa kweli namshukuru sana, ameongoza harambee nyingi, hata juzi tulikuwa kwenye harambee pale Dar es Salaam kwa ajili ya kuichangia hii shule na tukapata karibu shilingi milioni 282; na mwaka 2018 ilifanyika harambee zikapatikana shilingi milioni 550. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Salma Kikwete na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi na wananchi wa Lindi kwa ujumla kwamba shule hii ambayo iliungua madarasa tisa na ofisi tatu za Walimu mwaka 2016, mwaka ujao wa fedha tutahakikisha kwamba madarasa 27 na ofisi tisa za walimu ambazo wamepanga kujenga yatakamilika. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante. Pia namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Sheria Namba Tisa ya Mwaka 2010 inamzungumzia mtoto mwenye ulemavu kupata haki ya elimu pamoja na kulindwa. Watoto hawa wenye usonji, kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi wana mazingira tete. Sasa je, nili lini, au je, upi ni mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba watoto hawa wanapata elimu toshelezi katika mazingira yao ya miundombinu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, watoto wenye usonji kwa kawaida wanatakiwa kila watoto watano wawe na Mwalimu mmoja. Sasa katika majibu ya msingi tunaambiwa watoto wapo 1,416 na Walimu wapo 157, maana yake watoto hawa wanatiwa wawe na Walimu wasiopungua 283. Sasa je, ni lini Walimu hawa watapewa elimu stahiki ili waweze kuwapa watoto wenye ulemavu, hasa usonji elimu inayostahiki? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, yeye ni mdau mkubwa wa elimu na kwa kweli hasa katika elimu maalum ametoa mchango mkubwa sana wa mawazo kuhusu kuendeleza watoto hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wenye usonji mara nyingi huzaliwa kawaida na usonji huanza kuonekana baada ya mwaka mmoja na nusu hadi miaka miwili. Kwa hiyo, wazazi wengi wamekuwa wakipata shida ya kuwatambua vizuri kwamba huyu mtoto ana usonji, kwa hiyo, imekuwa vigumu hata kuwaratibu. Matokeo yake wengine wamekuwa labda wakiwapiga wanadhani ni watukutu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inao mpango maalum wa kwanza kuwatambua watoto hao wote na kuwasajili ili hatimaye tuhakikishe kwamba wote wanapata elimu kama ilivyo haki ya kila mtoto Mtanzania kupata elimu. kwa hiyo, mkakati wetu tutaanza zoezi la kuwatambua na kuwasajili ili hatimaye wapate elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, nakubaliana naye kwamba katika kila watoto watano wanatakiwa kuwa na Mwalimu mmoja lakini standard ambayo ni nzuri sana ya Kimataifa inatakiwa anapomfundisha amfundishe akiwa peke yake (one to one), hiyo ndiyo standard ya kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, upungufu wa walimu waliopo sasa hivi wanaofundisha shuleni ni mkubwa kama alivyoainisha. Hata hivyo, kwa kuwa tunao Walimu wengine ambao wameshapata mafunzo hayo kule Patandi halafu bado hawajahamishiwa kwenye hizo shule ambazo zinafundisha watoto hawa kwa sasa, ndiyo maana nimetoa agizo kwamba ifikapo Desemba wawe wamehamishiwa kwenye hizi shule ili kusudi watoto hawa waweze kupata haki yao ya msingi kabisa ya elimu.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa viwanda ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa letu, lengo la viwanda ni kuleta tija kwa Taifa na wananchi wake kwa ujumla ili waweze kunufaika.
Je, Serikali haioni kuwa sasa hivi ni wakati muafaka wa kwenda kutembelea kiwanda hicho kule Mtama?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa viwanda ni muhimu sana na viwanda hivi vitakapofanya kazi vizuri vitaweza kuwa na tija kubwa katika Taifa letu. Swali lake, je, hatuoni sababu ya kwenda kutembelea huko.
Mheshimiwa Spika, kama utakumbuka kwamba mwezi wa kwanza nilikuwa pia kwenye mzunguko katika Mkoa wa Lindi kufuatilia Kiwanda cha Wanga ambacho kinajengwa katika Jimbo hili la Mtama na kuweza kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zinakabili na hivi sasa hivi wanafanya vizuri. Kwa hiyo, vilevile katika masuala haya ya viwanda vya korosho tutafanya hivyo ili kuona kwamba viwanda hivyo vinaleta tija kwa ajili ya nchi yetu.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona, naomba niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Shule ya Msingi Majimatitu ina wanafunzi zaidi ya 4,000 hali ambayo husababisha wanafunzi wasipate haki yao ya msingi kitaaluma. Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka kuhakikisha shule hii inaongezewa madarasa pamoja na kwamba amesema kuna shule nyingi zinaongezewa madarasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, shule ambazo zina wanafunzi zaidi ya 1,500 ni shule ambazo kwa kweli zimezidiwa na wanafunzi wanaohitajika kuwa katika shule moja. Kwa maana kwa viwango ambavyo vinakubalika shule ikiwa na wanafunzi 4,000 kwa kweli ni suala ambalo linahitaji tulishughulikie haraka sana. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Kikwete na wadau wengine wote wa hii Shule ya Msingi Majimatitu kama kweli ina wanafunzi 4,000 basi tutapeleka jicho letu haraka sana ikiwezekana basi tuigawanye ile shule ziwe shule mbili. Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri wangu kwa majibu mazuri sana ya awali.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kuongezea tu kidogo, ni kweli shule ya Msingi Majimatitu mwaka jana darasa la kwanza peke yake walikuwa wanafunzi 1,200 na hii ni kutokana na programu ya elimu bure ambapo watoto wengi waliokuwa wanakosa fursa ya elimu wameenda pale. Serikali tulichokifanya ni kutafuta eneo lingine kwa ajili ya kujenga shule pacha jirani. Naomba niseme kwamba Serikali itafanya kila liwezekanalo ili ile shule pacha iweze kukamilika haraka iwezekanavyo tupunguze idadi ya wanafunzi walioko katika Shule ya Msingi Majimatitu.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana naomba niulize swali langu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa upatikanaji wa kivuko baina ya Kata ya Msinjahili na Kitumbikwera ulikuwa uende sambamba na ujenzi wa sehemu za kusubiria abiria; na kwa kuwa takribani mwaka mmoja umeshapita tangu kivuko kipatikane.
Je, lini Serikali itajenga sehemu za kusubiria abiria baina ya Kitumbikwera na Msinjahili ili kuwaondolea adha wananchi hawa?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa, kwa sababu suala hili amekuwa akilifuatilia sana ni muda mrefu na mimi nilifika eneo hili la kivuko na hali niliyoikuta pia nilitoa maelekezo ili tuweze kupata kibanda cha abiria na pia ujenzi wa huduma zingine.
Mheshimiwa Spika, ni furaha yangu tu kumueleza Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Lindi kwamba tumeshapata mkandarasi, ameshasaini Mkataba kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya abiria ya kusubiria usafiri, maeneo yote ya pande mbili za vivuko tutaweka pia huduma zingine kama vyoo vya kisasa na tumetoa maelekezo kwamba ujenzi uanze haraka kabla ya msimu wa mvua.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikupe tu taarifa kwamba tutasimamia kuhakikisha huduma muhimu katika maeneo haya yanapatikana haraka kabla ya mvua. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tunaamini na tunajua kwamba elimu ndiyo msingi wa kila kitu katika maisha ya mwanadamu na mafanikio ya elimu ni pamoja na kuwa na zana za kufundishia pamoja na kujifunzia. Kwa kuwa, vitabu vyetu vya kiada huchapishwa nje ya nchi yetu na tukiamini kwamba elimu ni jambo tete katika ustawi wa Taifa letu, je, ni lini vitabu hivi vya kiada vitachapishwa hapa nchini ukizingatia Serikali yetu ni ya viwanda? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru sana kwa kuleta swali hili hapa Bungeni na nitumie nafasi hii kuonyesha masikitiko yangu makubwa sana kwa makampuni ya Kitanzania ambayo yanafanya kazi ya uchapishaji. Haya Makampuni yametuangusha kweli kweli, tumelazimika kwenda kuchapa vitabu nje kwa sababu unapoyapa makampuni ya Kitanzania kwanza kuna mengine ambayo yamekuwa yanachapa vitabu, kitabu kimekaa kama sambusa yaani wanakata hovyo hovyo lakini pia wanatumia muda mrefu kuvichapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuhusu swali lake kwamba Serikali ina mpango gani, kutokana na changamoto hiyo, Serikali imeamua kununua mashine ya uchapaji na hapa tunapoongea tayari tumekwishaiagiza. Kwa hiyo, tunategemea hilo suala sasa tutakuwa tunalifanya wenyewe.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali kwa kutupatia Kivuko cha Msinjahili, Kitumbikwera kule Lindi. Je, ni lini Serikali itakamilisha eneo la kituo cha kupumzikia wasafiri au cha kusubiria wasafiri kati ya Msinjahili na upande wa Kitumbikwera? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Ni kweli kwamba tumerekebisha kivuko alichozungumza Mheshimiwa Mbunge na kwa kweli sasa hivi kimeshaanza kutumika. Kwenye package ya tenda aliyopata mkandarasi wa kujenga kivuko kile, tulimwambia aweke na sehemu ambako wananchi watapumzika. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafuatilia kuona kwamba sehemu ya kupumzika inatengenezwa.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri. Hospitali yetu ya Mkoa wa Lindi ya Sokoine haina gari la Mganga Mkuu wa Mkoa na hii hupelekea Mganga Mkuu wa Mkoa kutumia gari yake ya binafsi (private car). Je, ni lini hospitali yetu ya Lindi ya Mkoa itapelekewa gari kwa ajili ya Mganga Mkuu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Salma Kikwete kwa jinsi ambavyo amekuwa akilifuatilia jambo hili. Mimi binafsi ameshanifuata na suala hili nikalichukua na kulipeleka Ofisi ya Rais, TAMISEMI na tulikuwa tunafanya logistics juu ya tatizo hili na ukubwa wake. Naomba nimhakikishie, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imelipokea kwa sababu siyo hali ya kawaida kwa Mganga Mkuu wa Mkoa kutumia gari yake binafsi katika kufanya shughuli za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba atupe muda kwa kadri tutakavyoweza tukipata nafasi ya kwanza kabisa suala hili tutalitatua.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nini mpango kabambe wa Serikali kwa maeneo yale ambayo UKIMWI uko chini ya asilimia moja, kuhakikisha kwamba tatizo hili linaondolewa kabisa kwa maeneo hayo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzindua Taarifa ya Takwimu za UKIMWI tarehe 1 Desemba, 2017 nchi kwa ujumla tumeweza kujua hali ya UKIMWI katika mikoa yote. Tumeiagiza Tume ya Kudhibiti Ukimwi Nchini (TACAIDS) kuhakikisha kila mkoa unatengeneza mkakati wao kulingana na hali ya UKIMWI ilivyo katika mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale ambao maambukizi yao ni machache, viongozi wa mkoa na taasisi zinazohusika wahakikishe wana-retain ile hali ama kuhakikisha maambukizi hayapandi ama yanaondoka kabisa na ile mikoa ambayo maambukizi yako juu mikakati ya mkoa huo ni kuhakikisha maambukizi yanashuka chini. Kwa hiyo, kila mkoa unatengeneza mkakati kutokana na hali halisi katika mkoa husika. Kwa hiyo, Serikali inalisimamia sana suala hili na lengo letu ni kufika hiyo 90-90-90, ama huko mbele tuendane na matakwa ya kiulimwengu ya kufika 00-00-00. Kwa hiyo Serikali inazingatia sana suala hilo.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na majibu mazuri ya Serikali, naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, tatizo la zahanati katika nchi yetu limekuwa likipungua siku hadi siku lakini kwa baadhi ya maeneo, maeneo mengi wananchi wameweza kuweka nguvu kazi zao kuhakikisha kwamba zahanati zinapatikana ili kupunguza vifo vya akina mama na watoto. Je, lini Serikali itamaliza yale maboma yote kuhakikisha kwamba tatizo hili linaisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, swali hili linarandana sana na kituo cha afya kilichopo kule Lindi katika Kata ya Mnazi Mmoja. Je, ni lini watawahakikishia wananchi wa Lindi wanamaliza lile jengo pamoja na kwamba wameshawapa kiasi fulani cha fedha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la kumalizia maboma ambayo wananchi wameingiza nguvu zao, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Salma, naye ni shuhuda, jinsi ambavyo Serikali inaelekeza nguvu zake kuhakikisha kwamba maboma yote tunayamalizia hatua kwa hatua. Ndiyo maana tumeanza na ujenzi na ukamilishaji wa vituo vya afya 208 na juzi vimeongezeka viwili, tumekuwa na 210. Naomba nimhakikishie kwamba jitihada ambazo zimefanywa na wananchi Serikali itahakikisha kwamba tunamalizia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili linalohusiana na Kituo cha Afya cha Mnazi Mmoja, naomba nimpongeze Mheshimiwa Salma kwa jitihada zake za kuwapigania wananchi wa Mkoa wa Lindi. Nilipata fursa ya kwenda kutizama kazi ya ujenzi wa Kituo cha Afya Lindi, kazi niliyoiacha ilikuwa inaenda vizuri. Naamini katika muda ambao tumekubaliana kwamba vituo vya afya hivi vijengwe kwa kuzingatia miezi mitatu na wananchi wa Lindi kwa maana ya Kituo cha Afya Mnazi Mmoja kwa jitihada nilizoziona na nguvu kazi na ari yao ya kujitoa, naamini ndani ya muda huo kituo cha afya kitaweza kukamilika. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Ng’ombe ni muhimu sana katika ustawi wa Taifa letu la Tanzania na hulipatia Taifa takribani 7% kutokana na ng’ombe hao. Kwa kuwa makundi makubwa yanaingia ndani ya Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Lindi; na kwa kuwa ng’ombe wanapoingia ndani ya mikoa hiyo huleta uharibifu mkubwa sana wa mazingira; na tunafahamu mazingira ndiyo kila kitu katika uhai wa binadamu; natahadharisha hii ili yasije yakatokea kama yale yaliyotokea kule Ihefu hatimaye yakasababisha mabwawa kukauka na maji yakakosekana ndani ya nchi yetu. Je, nini kauli ya Serikali au mkakati wa Serikali katika kuhakikisha kwamba mazingira yanaboreshwa ili yasije yakaleta athari kwa Watanzania na nchi kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa mama Salma Kikwete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza mama yangu Mheshimiwa Salma Kikwete kwa kukiri na kukubali kuwa ng’ombe ni fursa kubwa sana kwa uchumi na ustawi wa Taifa letu. Kwa mtazamo huu wa kwamba ng’ombe ni fursa kubwa ya uchumi kwa Taifa letu, hivyo basi, ng’ombe ni fursa kubwa ya ustawi katika mikoa aliyoitaja ya Pwani na Lindi pia vilevile kwa uhamiaji wa ng’ombe wengi wanaoingia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tahadhari yake juu ya ulinzi wa mazingira, sisi Wizara ya Mifugo, tumeizingatia sana. Ndiyo maana mkakati wetu wa kuhakikisha kuwa tunalinda maeneo yanayotengwa mahususi kwa ajili ya wafugaji na kutoyasababishia kuhamishiwa kwa shughuli nyingine zozote za kibinadamu ikiwemo shughuli za kilimo, tutaendelea nao ili kuhakikisha tunalinda mazingira ya nchi yetu yasiharibiwe na vilevile kwa ustawi wa shughuli hizi za mifugo na shughuli nyingine za wananchi wetu.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 14 inasema kila mtu anayo haki ya kuishi. Mwanamke na mtoto hawatakiwi kufa hasa mama wakati analeta kiumbe kingine dunia. Tunaona vifo ni 556 kati ya vizazi hai 100,000 na kule kwa watoto 21 kati ya vizazi hai 1,000 na tunaambiwa tufikapo 2020 tufikie 10 kati ya vizazi hai 1,000. Je, Dira hii ifikapo 2020 au 2025 tunaweza kuifikia ili kunusuru maisha ya hawa wazazi pamoja na watoto wao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Salima Kikwete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali na Serikali hii ya Awamu ya Tano imedhamiria kabisa kuhakikisha kwamba tunapunguza vifo vya akina mama na watoto. Nikiri kauli ambayo ameisema Mheshimiwa Salma Kikwete kwamba ujauzito haujawahi kuwa ni ugonjwa na mama mjamzito hapaswi kufariki kutokana na uzazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe tu comfort Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imewekeza nguvu sana na kipaumbele chetu kikubwa sana ndani Wizara ni kuhakikisha tunapunguza vifo vya akinamama na watoto. Tumeongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba katika masuala ya uzazi; tumeboresha vituo vya afya; tumeendelea kutoa mafunzo kwa wataalam wetu wa afya na tumeendelea kuweka mifumo mbalimbali na kuhakikisha kwamba tunatoa hamasa katika jamii na viongozi wote katika ngazi zote kuwajibika. Mimi niseme tu in a very an official way kwamba tutakapofanya utafiti mwakani nina uhakika tutapata takwimu nzuri zaidi.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nataka kuuliza kuhusu suala la fidia; wananchi wa Mkuranga, Kibiti na Rufiji wanadai fidia zaidi ya miaka mitatu kutoka TANESCO. Sasa kutokana na mradi huu wa umeme wa Kinyerezi, je, ni lini wananchi hawa watalipwa hizo fidia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mama yetu Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, Mbunge wa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, lakini anahudumu Mikoa ya Pwani na Lindi kama ambavyo ameuliza masuala ya fidia ya mradi wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Somangafungu Kinyerezi. Kimsingi mradi huu fidia yake inalipwa na TANESCO na maeneo ambayo yalipitiwa na mradi huu kuanzia Kilwa, Kibiti, Rufiji, Mkuranga na maeneo ya Mbagala na Ilala Dar es Salaam, nataka nikiri kwamba kutokana na mradi huu takribani gharama yake kama isiyopungua bilioni 50 hivi, lakini TANESCO mpaka sasa hivi wamelipa zaidi ya bilioni 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti,natambua kwamba zipo changamoto za baadhi ya wananchi wachache na hata hivi karibuni tulipanga na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mkuranga kufanya kikao na Menejimenti ya TANESCO ili kuweza kutambua mpango wao mkakati wa kumalizia malipo ambayo yamesalia. Kwa hiyo, nimshukuru kwamba na tunamwalika Mheshimiwa Mbunge, Mama yetu Mama Salma Kikwete na Mheshimiwa Mbunge wa Rufiji na Mheshimiwa Mbunge wa Kilwa katika kikao hiko ili kutambua akina nani wamelipwa, akina nani hawajalipwa kwa sababu zipo changamoto pia katika suala zima la wanaojitokeza. Hata hivyo, nimwahidi kabisa kwamba TANESCO kwa kweli wamejipanga kulipa kwa sababu mradi huu ni lazima utajengwa kutokana na uwekezaji unataka kufanyika Mkoa wa Mtwara wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha megawati 300 na Somangafungu yenyewe wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha megawati 330. Kwa hiyo nimshukuru na kumpongeza kwa swali lake zuri hili. Ahsante sana.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niipongeze sana Serikali kwa kuunganisha barabara nyingi za nchi yetu kutoka Wilayani na Makao Makuu ya Mikoa yetu. Sambamba na hilo napenda niulize swali langu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Bungu - Nyamisati inaunganisha Wilaya ya Mafia na Kibiti. Sasa barabara hii iko chini ya kilometa 50 na kama mnavyojua historia, Mafia ni Kisiwa, wanatumia usafiri mmoja tu ambao ni ndege. Je, ni lini barabara hii itaunganishwa kwa kiwango cha lami ili kuwasaidia wananchi wa Mafia?
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kikwete kwa namna anavyofuatilia maendeleo ya sehemu mbalimbali. Kwa hiyo mara nyingi nimemsikia akizungumza juu ya Lindi, leo anazungumza juu ya Pwani, kwa hiyo nampongeza sana. Hata maeneo mengine, nimemsikia pia akiwasemea walimu kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la Nyamisati ni eneo muhimu sana. Nifahamishe tu Bunge lako pamoja na wananchi kwa ujumla, ni kwamba tunatengeneza gati katika eneo hili la Nyamisati kwa lengo la kuhudumia kivuko ambacho pia tumeanza hatua za manunuzi, kivuko ambacho kitatuvusha kutoka Nyamisati kwenda Kilindoni kule Mafia. Tunaendelea vizuri. Kwa hiyo, niwahakikishie tu wananchi hawa wa Nyamisati na wananchi wa Pwani na Watanzania kwa ujumla kwamba tutakuwa na kivuko ambacho kitatusaidia kupunguza usumbufu uliokuwepo kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapotengeneza kivuko pamoja na gati hii lazima ule mnyororo wa usafiri tuuweke vizuri. Ndiyo maana nami nimetembelea eneo hili kilometa kama 48 hivi kutoka Bungu kwenda Nyamisati ili kuhakikisha kwanza barabara tunaiweka katika ubora unaohitajika, lakini pia mipango yetu ipo ili tuje kuweka lami barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii muhimu itatusaidia pia kusafirisha mizigo mingi kutoka Nyamisati kwenda hata sehemu hii ambayo tunajenga umeme (Stiegler’s Gorge) kwa sababu barabara hii kutoka Kibiti kwenda Stiegler’s Gorge tumeiboresha na tunaamini kwamba gati hii ikiboreshwa kutakuwa na vyombo ambavyo vitabeba mizigo mizito kuja Nyamisati ambavyo vinaweza vikahitajika kwenda kwenye maeneo ya mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatumaini kwamba barabara hii kuiboresha pamoja na kuiweka kiwango cha lami itatusaidia sana kubeba mizigo na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsnate sana.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Barabara za lami hugharimu pesa nyingi za Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mara tu barabara hizo zinapojengwa, hubomolewa na kupitishwa miundombinu mingine, hatimaye hazirejeshwi katika ubora wake:-

Je, Serikali inatuambia nini juu ya jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ujenzi wa barabara unachukua fedha nyingi, lakini niseme tu shughuli zozote zitakazohusisha kukata barabara lazima zifanyike kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, kama kuna mtu anakata barabara na kuacha uharibifu ni makosa. Nami nielekeze viongozi wote, Mameneja wote wa Mikoa; mtu ambaye atafanya shughuli za kibinadamu na kuharibu barabara bila kurejesha kwa ubora wake na bila kupata kibali kwa mujibu wa sheria ni makosa, wachukue hatua kwa mujibu wa sheria.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Lindi na Mtwara ni Mikoa jirani sana. Katika majibu yake ya Msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema gesi ya Mtwara itasambazwa majumbani katika Mkoa wa Mtwara, Pwani, pamoja na Dar es Salam, Lindi wameiruka. Sasa je, ni lini Lindi watasambaza gesi hii majumbani?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kwamba ni kweli mpango wa kwanza unaanza na Mikoa mitatu ya Dar es Salaam pamoja na Mtwara na Lindi. Kwa sasa tumeanza kusambaza Dar es Salaam na tarehe 40 mwezi huu wataanza kujenga mabomba Mtwara na tarehe 30 mwezi Mei wataanza utaratibu wa kujenga mradi wa kusambaza gesi majumbani Lindi.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nina swalo dogo la nyongeza, Jimbo la Mchinga, Jimbo la Mtama, eneo la Sudi, Jimbo la Lindi Mjini, hupitiwa na Bahari ya Hindi na vijana hutegemea uvuvi ili kujiongezea uchumi wao na vitendea kazi kwa kweli ni duni sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia vijana hawa boti ili waweze kuinua uchumi wao? Ahsante.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Salma Kikwete ameiandikia Wizara kuiomba kusaidia vijana hawa, lakini na hapa Bungeni amesimama kuuliza swali la nyongeza. Nilienda kwenye maeneo hayo kwa vijana hao ambao wanafanya shughuli zao vizuri sana za uvuvi. Ninachotaka kusema kwa ufupi tu, najua mahitaji ya boti ni makubwa, lakini kwa kuanzia tutampa boti moja kwa ajili ya vijana hao.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, mradi wa kuchakata gesi wa LNG Likong’o Lindi. Ni muda mrefu sana wananchi wa eneo la Likong’o hawafanyi shughuli zao za kilimo ili kujipatia mahitaji yao ya msingi na kuongeza uchumi wao binafsi na mradi huu ni muhimu sana kwa wananchi wa Lindi kwa ajili ya kuongeza uchumi wao, lakini si hilo tu bali ni Taifa kwa ujumla kwa sababu ni mradi mkubwa sana, Mheshimiwa Waziri.

Je, ni lini wananchi hawa wa Lindi hasa Likong’o watalipwa fidia zao kwa ajili ya kuinua vipato vyao na kuacha eneo hilo liendelee na kazi iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali la Mheshimiwa mama Salma Kikwete Mbunge wa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais juu ya suala la fidia la eneo la Likong’o ambalo tunatarajia kutekeleza mradi mkubwa wa kujenga kiwanga cha kuchakata gesi asilia ambayo imegundulika kwa wingi katika Mikoa ya Mtwara kwa kiasi cha trilioni cubic feet 55.

Mheshimiwa Spika, nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge mama Salma na wananchi wa Mkoa wa Lindi Serikali inatambua umuhimu wa mradi huu na ndiyo maana Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo ya kukwamua mkwamo ambao uliokuwepo kwa Wabia wale wa mradi wa kutaka kila mmoja tuzungumze naye kwa wakati tofauti na mazungumzo hayo yameanza kati ya kampuni ya BP SHELL pamoja na STATOIL ambayo kwa sasa hivi inajulikana kama equinor.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mazungumzo haya yameanza kwa kwa kuwa sasa hivi kuna kila dalili ya mradi huu kufanyika na taratibu zinaendelea na Kamati ya Wataalam wameshakaa suala la fidia kwa eneo hili limeshafanyiwa kazi na naomba nimualike Mheshimiwa Mama Salma Kikwete na Wabunge wote wa Mkoa wa Lindi kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwenye mkutano wa tarehe 21 mwezi huu wa 5 wa ku-raise awareness ya mradi huu na ambapo pia taarifa na uhakika wa ulipaji wafidia baada ya tathimini kukamilika itatolewa.

Mheshimiwa Spika, tunawashukuru wananchi wa Mkoa wa Lindi kwa uvumilivu wao tunakuja tarehe 21 na kwamba kila kitu Serikali imekiweka vizuri, ahsante sana.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Ili uweze kwenda chuo kikuu ni lazima uwe na ufaulu unaostahili na ufaulu huu unategemea jinsi ambavyo wanafunzi wametengenezwa, wanafunzi wamejengwa kuanzia ngazi ya Msingi hatimaye Sekondari, A-Level na O- Level.

Mheshimiwa Spika, hali ya ufaulu ndani ya Mkoa wa Lindi ni mbaya, ni mbaya! Mkoa wa Lindi bila kuzungusha, umekuwa wa mwisho katika ufaulu. Kwa misingi hii, kuwa wa mwisho si tatizo, unaweza ukawa wa mwisho katika mazingira ya kufanya vizuri, lakini unaweza kuwa wa mwisho katika mazingira ya kufanya vibaya.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuwa, Lindi tumekuwa wa mwisho katika mazingira ya kufanya vibaya, Je, Serikali ina mpango gani wa kuangalia changamoto zilizojitokeza ndani wa Mkoa wa Lindi mpaka kuwa wa mwisho? Na hii itapelekea kwamba kama Mheshimiwa Waziri husika akija na kuangalia nini changamoto zinazokabili Mkoa wa Lindi kuwa wa mwisho? Naomba Mheshimiwa Waziri, atengeneze ziara ili aje atambue changamoto zinazokabili Mkoa wa Lindi, pamoja wana Lindi wenyewe wameshakaa vikao vya mkakati kuangalia changamoto hizo. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze mama yetu Mama Salma Kikwete, hakika amekuwa mama mpambanaji sana kuhakikisha elimu inasonga mbele kwa wato wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nilichukue jambo hili na ni kweli, Lindi imekuwa haifanyi vizuri na ndiyo maana hapa kipindi cha katikati, Ofisi ya Rais TAMISEMI kuona hivyo, niliweza kumtuma Naibu wangu Waziri Waitara alikwenda Mkoani Lindi kwa ajili ya kutembelea miongoni mwa shule mbalimbali na mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo lengo letu kubwa ni kuboresha shule zile kwanza mazingira yawe rafiki zaidi na ndiyo maana maombi ambayo Mama Kikwete naye aliyaomba hasa katika shule mfano kama ile Lindi Sekondari. Ndiyo maana hata katika kipindi cha sasa hivi hapa, tutakwenda kuifanyia ukarabati shule yote ya Lindi Sekondari, lakini siyo Lindi Sekondari, isipokuwa kuzipitia shule za Lindi kuziweka katika mazingira rafiki.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mwenyewe nitafanya ziara maalumu Mkoani Lindi kwa ajili ya kuhakikisha jinsi gani tunafanya kuufanya mkoa huu sasa uinuke kielimu na ndiyo maana hata katika mgao wa walimu, kipaumbele chetu sasa hivi tunaona kwamba jinsi gani hata badaye tupeleke walimu wa kutosha na hata uhamisho wa walimu katika Mkoa wa Lindi hivi sasa tumesimamisha kaika mkoa ule kwa lengo kubwa kwamba mkoa huu tuweze kuu-promote uwe katika hali nzuri.

Mheshimiwa Spika, ahsante.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa mama yangu Salma Kikwete. Kwanza nimpongeze sana mama Salma Kikwete kwa kazi nzuri ambayo anaifanya katika kuhakikisha kwamba elimu inasonga mbele na hasa kwa mtoto wa kike.

Mheshimiwa Spika, na kuhusiana na swali lake, pamoja na majibu mazuri ambayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI ameyazungumzia kuangalia miundombinu, nami nimuahidi Mheshimiwa Mama Salma Kikwete kama Wizara ya Elimu, ambayo kazi yetu ni kuweka Sera ya Elimu na kuhakikisha kwamba viwango vya elimu vinafikiwa, tutafanya ukaguzi maalum katika Shule za Mkoa wa Lindi, ili tuweze kubaini changamoto ambazo zinapatikana na tuweze kuchukua hatua mahususi kuhakikisha kwamba Mkoa wa Lindi unainuka katika ufaulu kwa wanafunzi ambao wanasoma katika shule za sekondari na shule za msingi.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kwanza kabisa kwa masikitiko makubwa naomba nitoe pole zangu za dhati kwa wananchi waliopatwa na kadhia ya mvua na hasa katika Mkoa wetu wa Lindi kule Kilwa, Liwale pamoja na Lindi Vijijini na hasa katika eneo la Mchinga ambao watu wamepoteza makazi yao, mazao yao na vitu vingi mbalimbali, tunawapa pole sana kwa hilo.

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo nataka niulize swali langu la nyongeza kutokana na swali la msingi namba tisa kuhusu suala la x-ray, nitauliza suala la mashine ya dialysis. Tunajua na tunatambua kwamba ugonjwa wa kisukari unaongezeka siku hadi siku na kutokana na kuongezeka kwa ugonjwa wa kisukari unapelekea matatizo ya figo na matatizo ya figo yanapelekea watu kufanya dialysis. Dialysis hizi ziko katika maeneo machache hapa nchini kwetu Tanzania. Je, ni lini mashine za dialysis zitapelekwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Kikwete, Mbunge wa Viti Maalum/Mbunge wa Taifa lakini anawakilisha Mkoa wa Lindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunaona ongezeko kubwa sana la wagonjwa wa figo ambao wanahitaji huduma za kusafisha damu na ni kweli huduma hizi zimekuwa katika hospitali ngazi ya kanda na katika mikoa mingi huduma hii ilikuwa inakosekana hali ambayo ilikuwa inapelekea watu wengi kusafiri muda mrefu kwenda kupata huduma hii. Aina ya huduma hii inahitaji mtu apate dialysis mara tatu au nne kwa wiki ili aweze kuendelea na maisha yake. Serikali tumeliona hilo na sasa hivi tumepata dialysis machines takribani 45, tunazisambaza katika mikoa nane na mkoa ambao tutaanza nao ni pamoja na Mkoa wa Mtwara, Lindi hatujaiweka katika utaratibu huo.

Mheshimiwa Spika, kusudio letu ni kwamba kadri tunavyojenga uwezo na upatikanaji wa hizi mashine kwa sababu naomba niseme dialysis machine si kila mtu ambaye anaweza akaifanya, inahitaji utaalam, inahitaji miundombinu tofauti kabisa, inahitaji maji maalum, inahitaji manesi maalum, kwa hiyo tunaendelea kujenga na kwa kuanzia tunaanza na mikoa nane ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Mtwara, tunaamini kwamba huduma hii sasa tutakuwa tumeisogeza karibu zaidi na wananchi wa Mkoa wa Lindi wakati tunaendelea kujenga uwezo na baada ya hapo tutafika mikoa yote ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Lindi. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Tunatambua na tunajua kuwa maliasili ni kitu muhimu sana katika ustawi wa Taifa letu la Tanzania na huchangia pato la asilimia 17 kutokana na utalii huo. Mkoa wetu wa Lindi ni miongoni mwa sehemu ambazo zinapitiwa na Selous ambayo sasa hivi ni Mwalimu Nyerere National Park.

Mheshimiwa Spika, sasa katika Mkoa huu wa Lindi, kuna tatizo ambalo lipo katika Tarafa ya Melola, Kata ya Milola na Tarafa ya Mkinga, Kata ya Mchinga ambalo hili ni Jimbo la Mchinga. Wanyama kama tembo wanaingia katika maeneo hayo hata Mbunge wa Jimbo hilo Mheshimiwa Bobali ana ushahidi juu ya jambo hili. Pia wanyama hawa wanapoingia wanaleta uharibifu wa mazao na vilevile wanasababisha baadhi ya watu kupoteza maisha yao.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatuambia nini au inawaambia nini wananchi hawa juu ya uharibufu huo ambao umetokea katika maeneo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba majibu ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwa kweli naomba nikiri kwamba kutokana na mafanikio makubwa ya uhifadhi ambayo yametokea katika kipindi hiki cha Awamu ya Tano, migogoro mingi ya wanyama na binadamu imeripotiwa katika almost nchi nzima. Nakubaliana na Mheshimiwa Mama Salma kwamba katika maeneo ya Melola imeripotiwa sana kwamba tembo wanavamia makazi ya watu na kula mazao; lakini siyo huko tu, ni maeneo mengi, almost nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, tumeafanya nini kama Wizara? Moja, tumeelekeza taasisi zetu zote ikiwemo TAWA, TANAPA, TFS na Ngorongoro kuimarisha vitengo vinavyo-respond na matukio haya. Wote tumewaambia wawe na kikosi ambacho kipo tayari. Hata hivyo, imetokea mara nyingi kwamba wakati wanyama wanakuwepo kijiji kingine, wakati mwingine tumeshindwa kuwahi. Naomba nitumie fursa hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba tumetoa maelekezo na suala hili tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu fidia ya mazao, Wizara imerekebisha kanuni ili kuweza kutoa kifuta jasho na kifuta machozi kinachoridhisha. Kanuni hizo zimekamilika, tutahakikisha kwamba malipo haya yanawahi kwa waathirika ili kuweza angalau kuwafuta machozi na jasho kwa muda mu Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali langu la nyongeza. Kabla sijauliza swali la nyongeza naomba nitumie fursa hii kuwapongeza na kuwatakia heri wanafunzi wote wa Tanzania kwa kuanza mitihani yao ya kidato cha nne, tunawaombea Mwenyezi Mungu awasimamie, awabariki ili waweze kufanya vizuri mitihani yao.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niulize swali langu la nyongeza, kutokana na swali la msingi namba saba, nami nataka niulize kwamba, kuna suala la sumu kuvu ambalo lipo ndani ya karanga na lipo vile vile ndani ya mahindi na ukizingatia mahindi ni chakula chetu kikubwa na ni chakula cha msingi kutokana na utafiti uliofanyika. Je, wamefikia hatua gani kuhakikisha kwamba mahindi haya hayana sumu kuvu au yamepungua kwa kiasi gani? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mama yetu Salma Kikwete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli kuna ugonjwa hatari unaosababishwa na huu wa sumu kuvu unaosababishwa na fangasi wakuvu ambao ugonjwa huu umeleta athari kubwa hasa katika mikoa hii ya Kanda ya Kati hususan kwenye kule Wilaya ya Kondoa, Chemba na watu zaidi ya 19 walipoteza maisha.

Mheshimiwa Spika, kama Serikali baada ya kugundua hiyo kwanza sasa hivi tumekuja na programu ambayo imeanza tangu mwaka jana na tumetenga zaidi ya bilioni 35 kwa ajili moja kutoa elimu ya ugonjwa huu kwa umma, lakini pili kujenga miundombinu ya kuhifadhia mazao haya ambayo kama mahindi na karanga ili yasiweze kuathirika na sumu kuvu. Mikoa ambayo tumeilenga ni mikoa 10 na mikoa miwili ya Zanzibar na ikiwepo hii ya Kanda ya Kati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo moja kabisa ni kuwafikia wakulima kuwapa elimu sababu gani zinasababisha ugonjwa huu, madhara yake ni nini na kinga yake ni nini? Ili kuondokana na tatizo hili lililopo hapa nchini.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba niulize swali langu la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa ziarani Wilayani Ruangwa alitoa maelekezo kwamba barabara kutoka Ruangwa - Nachingwea - Masasi na Ruangwa -Nachingwea - Nanganga zijengwe kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Rais akitoa kauli inakuwa ni maagizo. Je, lini upembuzi yakinifu utaanza kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Salma Kikwete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Salma Kikwete ni kwamba upembuzi yakinifu na usanifu wa kina tumeshakamilisha. Ujenzi tumeshaanza na tayari tumeshajenga km 5. Kwa hiyo, maagizo ya Mheshimiwa Rais kama alivyosema ni sheria lazima tutayatekeleza.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwanza naomba nitoe pongezi zangu na niwatakie kheri wanafunzi wote wa kidato cha pili kote nchini kwa kuanza mitihani yao ya taifa leo hii.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, nataka nijikite kwenye swali la msingi. Kwenye Halmsahauri ya Lindi Vijijini sasa hivi ni Halmshauri ya Lindi Mjini kwenye Jimbo la Mchinga, Kata ya Mpingo kuna shule shikizi. Bahati nzuri hiyo shule shikizi wananchi wamejitahidi, wamejenga na kule kuna wafugaji huenda mwakani ikaanza. Tatizo letu ni vifaa vya vitakavyotumika kwa ajili ya wanafunzi wale kujifunza na kujifunzia.

Je, Serikali itatusaidiaje kwenye tatizo hili kwa ajili ya wale wafugaji waliopo kule? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mama yangu Mheshimiwa Salma Kikwete ambapo namuita kama Balozi wa Elimu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu Mheshimiwa mama Salma amechukua muda wake mwingi sana ku-invest kusaidia watoto wa Kitanzania wapate elimu. Kwa hiyo, mama tunakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, eneo hili ambalo amelizungumzia ni eneo la wafugaji, ni shule shikizi, kwa heshima ya mama yetu, naomba nimuagize Mkurugenzi wangu wa Elimu amuagize Afisa Elimu Mkoa atembelee haraka Shule hiyo Mpingo kwenda kufanya needs assessment kuona kuna jambo gani la haraka linatakiwa kurekebishwa mapema ili itakapofika Januari watoto waweze kupata matunda mazuri ya swali hili.

Kwa hiyo, namuagiza Mkurugenzi wangu aweze kufanya kazi hiyo haraka iwezekanavyo.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, awali ya yote napenda niipongeze Wizara ya Nishati hasa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kuifanya Tanzania inayomeremeta. Umeme ni maendeleo, umeme ni uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini kwenye Kata ya Kitumbikwela ambapo kuna Kijiji cha Sinde na Mnali itapatiwa umeme wa REA na maeneo mengine yote yaliyosalia hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa mama yangu Salma Kikwete, Mbunge wa Kuteuliwa na Mheshimiwa Rais.

Kwanza nimpongeze kwa kazi nzuri anayoifanya kutokana na heshima aliyopewa na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli katika Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Pwani, lakini swali lake limejielekeza kuulizia Kata ya Kitumbikwela, Vijiji vya Sinde na Mnali ni lini vitapata mradi wa REA. Nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mama Salma, natambua hii ni changamoto ambayo aliwasilishiwa alipofanya ziara lakini tumefanya mawasiliano na TANESCO kwa kuwa tuliwapa maelekezo ya kubaini maeneo ambayo yanaweza yakapelekewa miundombinu ya umeme kupitia kwao TANESCO na wamebaini maeneo 754. Moja ya maeneo ambayo wamebaini ni eneo la Kitumbikwela na kwa bajeti ya TANESCO ya mwaka 2019/2020 eneo hilo na vijiji ambavyo amevitaja ikiwemo Mnali vitapatiwa umeme katika kipindi hiki.

Kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge na maeneo ambayo Lindi yamesalia kati ya vijiji 150, Mkandarasi State Grid anaendelea na kazi na tutaratajia ifikapo Disemba, 2019 kazi itakamilika. Kwa hiyo niwape moyo Wananchi wa Mkoa wa Lindi na Waheshimiwa Wabunge wote akiwemo Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mbunge wa Jimbo la Ruangwa kwamba kazi ya mkandarasi inaendelea na tutamsimamia vizuri ili akamilishe. Ahsante sana.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nitaenda kwenye swali la msingi kuhusu non committable disease, 2016/2020 ulitengenezwa mkakati maalum kuhusiana na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukizwa.

Je, mkakati huu wamagonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza ulikuwa ni kwa nchi nzima au ulikuwa ni pilot project? Na kama ni pilot project kwa maeneo gani?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, mkakati ulikuwa ni pilot ama ulikuwa ni wan chi nzima. Utafiti kwa kawaida huwa ni pilot unachukuliwa eneo moja halafu kwa njia labda kama ya sampling kisha matokeo yanatokana na eneo lile yanaweza kuwa ndio matokeo elekezi. Kwa hivyo naomba nimuhakikishie mama yangu kuwa kwa maelezo ziada ya matokeo ya utafiti huu uliofanywa niko tayari baada ya Bunge kuweza kuzungumza na wataalam wetu na kumtafutia zile takwimu na kuweza kumpatia.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii.

Mheshimiwa Spika, bodaboda ni kitu chema na bodaboda imerahisisha usafiri, bodaboda imesaidia sana kuleta ajira kwa vijana wa Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, lakini kuna changamoto zinazoweza kujitokeza pale inapotokea bodaboda imesababisha ajali barabarani, baadhi yao kwa muda mfupi wanajaa eneo la tukio na hatimaye kuweza kuchukua hatua za papo kwa papo na matokeo yake wanaweza kusababisha vifo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, Serikali inachukua hatua gani juu ya kutoa elimu kwa waendesha bodaboda kwamba wasichukue hatua za mkononi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete, swali zuri na muhimu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli matukio kama haya yamekuwa yakitokea, na ni matukio ambayo yanasikitisha sana na hayakubaliki katika jamii iliyostaarabika kama jamii ya Watanzania na kwa hiyo, naendelea kutoa wito hapa, kwanza nichukue fursa hii nikitumia jukwaa hili la Bunge kama ni moja katika njia ya elimu kwa waendesha bodaboda wote nchini kuepuka kuchukua sheria mkononi na wale wote ambao wamekuwa wakifanya hivyo hatma yao haijawa njema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sidhani kama kuna mwendesha bodaboda ambaye anataka hatma ya maisha yake iishie gerezani au iishie kwa kuhukumiwa hukumu ya kunyongwa kwa kusababisha mauaji yasiyokuwa na lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niendee kusisitiza kwamba utaratibu wetu wa utoaji wa elimu kwa bodaboda utiliwe maanani na mkazo zaidi katika eneo la kuhakikisha kwamba waendesha bodaboda hawatumii, hawachukui sheria mkononi inapotokea matatizo ya usalama barabarani na kuacha vyombo na sheria za nchi zifuate mkondo wake. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba niulize swali la nyongeza kutokana na swali la msingi. Kwanza tunaishukuru Serikali kwa kutupatia fedha kwa kukarabati barabara tajwa ya Kilwa eneo la Rangi Tatu – Kongowe - Mikwabe na kadhalika. Barabara hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya mkoa wa Dar es Salaam na maeneo yake ya jirani, barabara hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya Mkoa wa Lindi, Mkoa wa Mtwara na kuelekea maeneo mengine. Sasa kwa kuwa barabara hii inajengwa nyakati za mchana na sasa hivi mkandarasi yuko kazini na imekuwa ni kero kubwa juzi wakati tukiwa Misri dunia sasa hivi ni kiganja tukiwa Misri tumepata taarifa na tumeona jinsi watu wa maeneo ya Dar es Salaam wale wanaokwenda Lindi na Mtwara wamekaa zaidi ya masaa manne wakisubiri kwa kuwa mkandarasi yuko barabarani. Sasa kwa nini kusiwe na utaratibu badala ya kujenga barabara hii mchana ijengwe jioni au usiku ili watu mchana waendelee na kazi zao kwa ajili ya kujipatia maendeleo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete, mama yangu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru pia kwa maelekezo yako kwa sababu na wewe nafikiri jambo hili umeliona, niseme tu kwamba, kwanza nilipokee kama ushauri kwamba tutafanyia kazi ili wananchi wasipate adha wakati wa matengenezo yanavyoendelea. Hata hivyo, niseme tu kwamba, matengenezo yanayoendelea nia yake kubwa ni kuhakikisha kwamba tunapunguza ule muda wananchi wanakaa barabarani tutapunguza msongamano, lakini pia tunapunguza ajali. Niseme tu kwamba tutalisimamia jambo hili kwa sababu suala la kujenga usiku na mchana tutaliangalia, lengo kwanza mradi huu ukamilike haraka ili wananchi waweze kupata hii huduma muhimu.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa na mjadala mrefu kidogo na Mheshimiwa Mbunge wa Mkuranga na tulikuwa tumezungumza juu ya suala hili, kuna baadhi ya mambo ambayo tayari tumeyatolea maelekezo. Hii ni pamoja na kuangalia kwamba tunapokuwa na matengenezo hasa hasa katika Jiji la Dar es Salaam tuone pia alternative route zingine ambazo zinaweza zikapunguza watumiaji wa barabara ili msongamano usiwe shida.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutaliangalia kwa umakini na nitalifuatilia ili sasa tuone kwamba kwanza mradi unafanyika kwa haraka, zoezi linakamilika kwa haraka, lakini ile adha wanayoipata wananchi iweze kuondoka. Kwa hiyo, nashukuru tutalichukua hili kwa umakini mkubwa na tutalisimamia kama Serikali ili shida hii iweze kuondoka kabisa.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba niulize swali la nyongeza, naamini kwamba kwa watu wale ambao wanategemea usafiri wao wa maji kivuko ni barabara. Sasa kwa kuwa kivuko ni barabara nataka kuzungumzia kivuko cha Lindi ambacho kinatoka Msinjaili kuelekea Kitumbikwera. Kivuko hiki ni muhimu sana kwa usafiri wa watu wa eneo lile. Sasa kivuko kile kimeshawahi kuharibika na kikapotea kikaelekea maeneo ya mbali. Kutokana na kupotea huko tunamshukuru Mungu hakikuweza kusababisha ajali ya kuua watu. Kwa kuwa kivuko hiki kinaharibika mara kwa mara; Je, Serikali ina mpango gani wa kututengenezea kwa uhakika ili kivuko hiki kiendelee kutumika katika eneo husika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama yangu amekuwa akifuatilia sana mambo mbalimbali hasa kwenye Mkoa wa Lindi, kwa hiyo nitumie nafasi hii kumpongeze. Niseme tu kwa ufupi kabisa tunafahamu umuhimu wa kivuko hiki na tunafahamu namna kivuko hiki kinavyowahudumia wananchi wa Lindi. Tumefanya kwa kweli maboresho makubwa sana katika eneo hili, tumetengeza eneo la maegesho ya kivuko, tumetengeneza nyumba kwa ajili ya abiria wanaovuka kwenda ng’ambo kule. Niseme tu kwa tatizo la kivuko hiki kweli kimekuwa na matatizo kidogo na tumefanya ukarabati mkubwa lakini nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga kwa sababu Bunge hili limetupitishia fedha za kutosha kwa ajili ya kuongeza vivuko katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapatazama pale, itakapokuwa imewezekana tutabadilisha injini ya kivuko hiki, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumejipanga ili tuone kwamba changamoto ambazo zilikuwa zinajitokeza na zinaendelea kujitokeza tutaendelea kuzitatua na kuziondoa kabisa. Kwa hiyo wananchi wa Lindi wawe na subira lakini niwape comfort tu kwamba, tumejipanga vizuri tutafanya maboresho makubwa pamoja na ile barabara ya kule ng’ambo tutaifanyia matengenezo ili wananchi baada ya kuvuka waweze kwenda na shughuli zao bila kikwazo chochote. Ahsante sana.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa tuko katika Wizara ya Ujenzi, na Wizara hii ndiyo inayoshughulikia barabara pamoja na madaraja, sasa nilitaka kuuliza swali linalohusu barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitutembelea kule Milola na tukampa kero yetu ya barabara ambayo inatoka Ngongo inapitia Rutamba, Milola hatimaye inamalizikia Ruangwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu alituahidi kwamba barabara ile itajengwa kwa kiwango cha lami.

Sasa, je, ni lini barabara ile itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongezala Mheshimiwa Salma Kikwete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu ipo kwenye mipango, na ninaamini usanifu wa awali unaweza ukaanza kwa sababu hatujapita bado kwenye bajeti. Niombe kujiridhisha, Mheshimiwa Salma nimuombe baada ya kikao hiki pengine tuweze kukutana naye ili tuweze kuona barabara hii iko kwenye mpango kwasababu sasa hivi tuko bajeti kwa hiyo ni ngumu kusema barabara hii iko kwenye hatua gani. Kama ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kama iko kwenye ilani naamini itakuwa ni barabara ambazo ziko kwenye matazimio ya kufanyiwa kazi na hasa upembuzi yakinifu. Ahsante.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Jimbo letu la Mkinga lina vituo vya afya viwili tu. Kituo cha kwanza ni Kitomanga na kituo cha pili ni Rutamba. Kituo cha Rutamba kipo katika hali mbaya sana. Hakikidhi haja za kutoa huduma za afya kama kituo.

Je, ni lini Serikali itatutengea pesa kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho? Kama itampendeza Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri naomba nifuatane nae akaone hicho kituo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUNGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa mama Salma Kikwete Mbunge wa Mkinga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Jimbo la Mkinga kuna upungufu mkubwa wa vituo vya afya na vituo vya afya vilivyopo ni chakavu ikiwepo Kituo cha Afya hiki cha Mtamba. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mama Salma Kikwete kwamba Serikali inatambua kwamba kuna uhitaji mkubwa sana wa vituo vya afya katika Jimbo la Mkinga na ninatambua kwamba kuna kila sababu ya kuweka jitihada za maksudi kuhakikisha tunakarabati Kituo cha Afya cha Mtamba ili kiweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nichukue nafasi hii kumhakikishia kwamba tutachukua hoja hii na kuiwekea kipaumbele katika awamu inayokuja ya ukarabati wa vituo vya afya ili kituo hiki pia kiweze kuwekewa fedha kwa ajili ya ukarabati na upanuzi ili kitoe huduma bora za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa mama Salma Kikwete kwamba tutaendelea kushirikiana kwa karibu sana, na Ofisi ya Rais TAMISEMI tuko tayari wakati wowote kushirikiana na kufuatana na Mheshimiwa mama Salma Kikwete. Baada ya kikao hiki tutapanga kuona uwezekano wa kupata fursa hiyo ili twende kushirikiana pale muda ambapo utaturuhusu.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Tunajua na tunakumbuka kwamba malezi bora ya mtoto yanaanzia katika umri mdogo na ili mtoto aweze kukua anahitaji malezi rafiki kutoka kwa wazazi na walezi.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba watoto hawa wanalelewa na hawa wazazi na walezi yanapowakuta mazingira mabaya mtoto anapoeleza kwa wazazi au walezi anatishwa na wakati mwingine wanaofanya vitendo hivyo wapo ndani ya familia hiyo hiyo, aidha inaweza ikawa ni mjomba, ndugu wa karibu, dada anaogopa kueleza tatizo matokeo yake mtoto anaumia na anaharibika sana kisaikolojia.

Je, Serikali hapa inatuambia nini? Na sababu kubwa ni mojawapo Tanzania ina utaratibu mzuri sana juu ya mpango wake kuna Jirani, kuna Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, kuna Kitongoji kila mtu linapotokea kila mtu analijua. Serikali mnatuambia nini juu ya jambo hili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili mmeeleza kwamba kuna mkakati ambao unamalizika, kuna MTAKUWWA, unaomalizika 2022 lakini kuna program ambayo imeandaliwa na mpaka sasa kuna vituo 30, vituo 10 vipo Dar es Salaam, vituo 20 viko Dodoma. Nini matokeo ya vituo hivi ambavyo ni vituo vya majaribio? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana namshukuru Mheshimiwa Salma Kikwete Mbunge wa Mchinga kwa maswali yake mazuri ya nyongeza na nashukuru sana ni kama ametoa semina hapa. Ni kweli katika swali lake la kwanza masuala ya walezi yanaanza tangu mtoto akiwa mdogo pia matatizo anayopata mtoto akiwa mdogo yanatokana na ile jamii anayoishi nayo ndani na ndivyo tafiti zinavyoonyesha kwamba athari ya kwanza ni wale ambao wanaomzunguka yule mtoto.

Mheshimiwa Spika, katika kulifanyia kazi hili Serikali tumejipanga kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii yetu na Maendeleo ya Jamii hivi sasa tunakwenda kuanzisha mpango kama tunavyofanya kwenye afya, huduma za mkoba au mobile kuzifikia hizi familia na kuzielimisha kaya kwa kaya kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, mwenyewe juzi nilitoka Mwanza kama mwezi mmoja umepita nilifika mpaka kwenye nyumba ambako mtoto aliketishwa anamuhudumia bibi haendi shule mpaka amefika miaka 9 nikajifunza mambo mengi. Kwa hiyo, tukaona kwamba tunavyowafikia wagonjwa wanaoumwa kwa mobile na kliniki tuanzishe hiyo kwenye maendeleo ya jamii ili tuguse kabisa hizi jamii na kuanza kuwalea wazazi wenyewe ili waje kuwalea watoto wote wakiwa na confidence moja.

Mheshimiwa Spika, katika masuala ya vituo hivi vya Dodoma na Dar es Salaam naomba nilipokee hili tumeshaanza evaluation kwa ajili ya kwenda kuona ile impact tuwasilishe taarifa kwenye kamati yetu na itakuja kufika Bungeni kwa ridhaa ya Spika then tunakwenda kupeleka nchi nzima, faida ni kubwa kuliko kutokuwa na vituo hivyo.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kusini ile tunayoita ya Kilwa-Mtwara nilizungumzia hapa ni barabara mbovu kuliko barabara nyingine zote. Sambamba na hilo tunawashukuru Serikali kwa kututengea hizo pesa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo. (Makofi)

Sasa swali langu ni kwamba Serikali imesema imetoa ushauri tusafirishe hiyo mizigo kwa njia ya bandari; je, meli ya mizigo kwa ajili ya kusafirisha hiyo cement iko tayari au lini itakuwa tayari?
NAIBU WAZIRI UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ni kuboresha usafirishaji na ndiyo maana Bandari ya Mtwara imepanuliwa ili iweze tu si kusafirisha mizigo mikubwa lakini pia kufungua Mikoa ya Kusini.

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti na tumesema tutakuwa na ujenzi wa meli kubwa itakayokuwa inafanya pwani ya Bahari ya Hindi, lakini nilichosema kwenye jibu langu la msingi, ni kuwahamasisha wafanyabiashara wa ndani na wa nje sasa kutumia bandari yetu, kutumia meli mbalimbali za kibiashara ambapo bandari hii ya Mtwara ina uwezo wa kupokea meli kubwa na uwezo wa kushusha shehena kubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge na wale ambao wanafanyabiashara; kupitia Bunge lako napenda kuwataarifu kuwa Bandari ya Mtwara sasa iko tayari kupokea mizigo mbalimbali kwa ajili ya kusafirisha hiyo mizigo na kupunguzia uzito barabara yetu ambayo sasa inaharibika mara kwa mara, ahsante. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kusini ile tunayoita ya Kilwa-Mtwara nilizungumzia hapa ni barabara mbovu kuliko barabara nyingine zote. Sambamba na hilo tunawashukuru Serikali kwa kututengea hizo pesa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo. (Makofi)

Sasa swali langu ni kwamba Serikali imesema imetoa ushauri tusafirishe hiyo mizigo kwa njia ya bandari; je, meli ya mizigo kwa ajili ya kusafirisha hiyo cement iko tayari au lini itakuwa tayari?
NAIBU WAZIRI UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ni kuboresha usafirishaji na ndiyo maana Bandari ya Mtwara imepanuliwa ili iweze tu si kusafirisha mizigo mikubwa lakini pia kufungua Mikoa ya Kusini.

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti na tumesema tutakuwa na ujenzi wa meli kubwa itakayokuwa inafanya pwani ya Bahari ya Hindi, lakini nilichosema kwenye jibu langu la msingi, ni kuwahamasisha wafanyabiashara wa ndani na wa nje sasa kutumia bandari yetu, kutumia meli mbalimbali za kibiashara ambapo bandari hii ya Mtwara ina uwezo wa kupokea meli kubwa na uwezo wa kushusha shehena kubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge na wale ambao wanafanyabiashara; kupitia Bunge lako napenda kuwataarifu kuwa Bandari ya Mtwara sasa iko tayari kupokea mizigo mbalimbali kwa ajili ya kusafirisha hiyo mizigo na kupunguzia uzito barabara yetu ambayo sasa inaharibika mara kwa mara, ahsante. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; swali langu linahusiana na suala la maaskari.

Mheshimiwa Spika, nini kauli ya Serikali juu ya kutuletea kituo katika Tarafa ya Milola, sababu ya msingi ni kwamba ndani ya tarafa ile kila usiku uchao, kila asubuhi kuna taarifa ambayo ninaipata juu ya wanyama hasa tembo kuja kuzunguka katika maeneo yale ambayo watu wanaishi na matokeo yake watu wanapoteza maisha yao na nilishasema watu wamepoteza maisha, mazao yanaharibika kila siku na tunaambiwa tulime, sasa hata kama watu watalima nini matokeo yake.

Naiomba Serikali inipe tamko au inihakikishie juu ya kuleta kituo katika eneo letu lile ili askari wale waweze kushughulika na wale wanyama, ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Mama Salma ni askari anakuwa wa Halmashauri au unataka wa Wizara?

MHE. SALMA R. KIKWETE: Ikiwa wa Halmashauri sawa, ikiwa ni wa Wizara sawa, lengo ni kuhakikisha kwamba askari wanakuwepo na maisha ya wananchi yanakuwa salama. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa
Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na utalii naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niwape pole kwanza wananchi wa eneo lile kwa kuendelea kuvamiwa na tembo, lakini Serikali itapeleka askari pale ambao wataenda kulinda ili kupunguza kadhia hii ya wanyama wakali na waharibifu kama tembo.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; kwanza nikupongeze wewe kwa kazi nzuri ambayo unaifanya kuelekea kuhitimisha Bunge letu la Bajeti.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize swali la nyongeza, lakini kabla ya kuuliza kwanza niipongeze Serikali na Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri na kubwa inayoifanya kwa sababu wakati Wizara ya Nishati inatoa taarifa yake ilisema itamalizia umeme REA Awamu ya Tatu vijiji vyote vya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, na ninataka niwahakikishie kwamba katika Jimbo langu la Mchinga wataalam wako kazini tangu tarehe 16 mwezi huu wa Juni wakiwa na mkandarasi anayeitwa Nakuroi Investment Company Limited wanafanya kazi nzuri sana. Vijiji vyote kama Kijiji cha Kiwawa, Mputwa, Ruvu na Mtamba, Luchemi, Lihimilo Mnyangala, Namkongo, Makangala na Luhoma; hivi vijiji vyote vimeshafikiwa, isipokuwa kuna vijiji viwili tu ambavyo vimesahaulika. (Makofi)

Nakuomba sana na ninaiomba Serikali katika awamu ile ya tatu wamalizie hivyo vijiji viwili ambavyo ni Kijiji cha Dimba na Kijiji cha Kitohave. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete, Mbunge wa Mchinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa shukrani kwa niaba ya Wizara, lakini na Serikali kwa Mheshimiwa Mbunge kuona kwamba Serikali kwa ujumla yake chini ya uongozi wa Mheshimiwa wa Mama Samia Suluhu Hassan imeamua kuhakikisha kwamba inawafikishia umeme Watanzania wote mahala walipo, na kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili kuhakikisha vijiji vyote ambavyo amekuwa amepelekewa umeme vinapelekewa.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya Wabunge wengine tunafurahi kwamba sasa wakandarasi katika maeneo yetu mengi tayari wako site, kazi tayari zimeanza za kufanya survey na kuhakiki vijiji ambavyo vimechukuliwa na vitapewa umeme.

Mheshimiwa Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wale ambao katika maeneo yao hawajawaona wakandarasi au wameendelea kupata changamoto ya mawasiliano na wakandarasi hao basi tuwasiliane ili tuweze kuhakikisha kwamba tunasimamiana ili katika muda ambao tumewahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba tutapeleka umeme katika maeneo yetu, tuweze kufikisha umeme kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, juzi Mheshimiwa Waziri alisema kwamba vilikuwa vimebaki vijiji kama 680 ambavyo havikuwa vimeingia kwenye ile awamu yetu, lakini tayari maelekezo yametolewa na vijiji vyote vilivyoko katika maeneo yetu vimechukuliwa na vitafanyiwa kazi katika Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili bila kuacha hata kijiji kimoja.

Mheshimiwa Spika, hii ni commitment ya Serikali kwamba ifikapo Disemba, 2022 vijiji vyote ambavyo viko katika maeneo yetu vitakuwa vimepata umeme na kuhakikisha kwamba wananchi wote wanaendelea kufarijika na huduma ya umeme kwa ajili ya maendeleo katika maeneo yetu nashukuru sana.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu SPika, maji ni uhai kwa viumbe vyote, maji ni muhimu kwa ustawi.

Naomba kuuliza swali langu, Jimbo langu la Mchinga halina maji safi na salama. Sasa ningeomba jimbo hili lifikiriwe kwa umakini mkubwa kupata maji safi na salama kutoka chanzo kikubwa cha Ng’apa.

Je, ni lini maji safi na salama ya bomba yatapelekwa katika Jimbo langu la Mchinga kwa ajili ya wananchi wa jimbo hilo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, dhati ya moyo kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Mama yangu Salma Kikwete, kiukweli ni Mbunge ambaye kwanza anajua changamoto za watu wake na anaelala na mgonjwa ndiye anayejua mihemo ya mgonjwa. Kwa hiyo, naomba nimpe upendeleo maalum kabisa moja kufika kwanza katika jimbo lake la Mchinga, lakini la pili tunatambua kweli tuna chanzo toshelevu pale Ng’apa ambapo tumejenga mradi ule wa Lindi. Tunataka tuyatoe maji ya pale Ng’apa ili kuhakikisha kwamba yanafika katika Jimbo la Mchinga ili wananchi wa Mchinga waweze kuondokana na tatizo hilo la maji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote nikupongeze kwa kazi kubwa na nzuri ambayo unaifanya katika Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. ((Makofi)

Mheshimiwa Spika, mawasiliano ni kila kitu katika maisha ya mwanadamu, bila mawsiliano kila kitu kinakuwa siyo sawasawa. Kwa muktadha huo; Jimbo la Mchinga lina tarafa nne ndani ya tarafa mbili angalau klidogo mawasiliano ya simu yanapatikana lakini ndani ya tarafa mbili nyingine, Tarafa ya Milola na Tarafa ya Mipingo hakuna kabisa mtandao. Kukosekana kwa mtandao unasababisha pale kuwa kama kisiwa.

Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itatuletea mtandao katika Tarafa ya Mpingo na Milola na hasa katika vijiji vya Mipingo, Namakwia, Namkongo, Matakwa na Kiwawa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete Mbunge wa Mchinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Salma Kikwete kwa kuendelea kuwapigania wananchi wake ili wapate huduma ya mawasiliano ili waweze kufanya shughuli zao za kibiashara kama ambavyo Watanzania wangetamani.

Mheshimiwa Spika, lakini kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba tunafiksiha mawasiliano kwa Watanzania wote. Hivyo basi changamoto kama hii inapotokea katika maeneo tofauti tofauti basi kama Serikali ni wajibu wetu kupokea changamoto hii ili tuhakikishe kwamba wataalamu wetu tuwatume katika maeneo specific ili wakapate ukubwa wa tatizo na namna ambavyo tutaenda kulishughulikia kulingana na eneo husika lenyewe. Ahsante.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote naomba niipongeze Serikali na Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kutupatia vifaa boti katika Jimbo letu la Mchinga. Sambamba na kutupatia mashine katika Jimbo letu la Mchinga na sasa hivi wako kwenye mchakato wa kutupatia hiyo boti. Halikadhalika wako kwenye mchakato mwingine wa kutujengea eneo ambalo wavuvi hawa wadogo wadogo hasa katika Jimbo langu la Mchinga, watajenga mwalo ili wavuvi wote wawe na sehemu ya uhakika ya kuuzia bidhaa zao kutoka kwenye Bahari yetu ya Hindi. Swali langu ni hili lifuatalo: - (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itaanza ujenzi huu wa mwalo katika Jimbo langu la Mchinga na hasa Kata ya Mchinga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mama yangu Salma Rashid Kikwete, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana ni ukweli kwamba Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan imepeleka mashine za kutosha. Lakini vile vile na Kamba ambazo zilikuwa ni maombi ya kwake yeye mwenyewe Mbunge wa Jimbo la Mchinga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na katika hilo pia vile vile Serikali ya Awamu ya Sita imetenga jumla ya shilingi milioni 800, kwa ajili ya kujenga Mwalo na sasa hivi tupo katika hatua tayari kwa pamoja kwa kushirikiana na wananchi wa Mchinga, tumeshachagua eneo litakalokwenda kujengwa ule mwalo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sasa tupo katika michoro na baadaye kupata BOQ ambapo jumla ya kiasi cha fedha kisichopungua Shilingi milioni 800 zimetengwa kufanya kazi hiyo. Ninaamini kazi hiyo itakapokamilika ndani ya mwaka huu wa fedha itawanufaisha wavuvi wa eneo hili la Mchinga na wengine katika Pwani ya Bahari ya Hindi. Ahsante sana. (Makofi)