Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Anne Kilango Malecela (29 total)

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika,
nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, lakini naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, kwa mfano tu Wilaya ya Same mwaka 2016, wasichana wadogo waliopata mimba na kufukuzwa shule ni 64 ambao hawa ni wa O-Level ikiwa ina maana mimba hizi ni za utotoni. Mwaka huu 2017 mwezi wa Kwanza, wa Pili na wa Tatu, miezi mitatu tu wamefukuzwa wanafunzi wa shule kwa mimba za utotoni 42 na kati ya hao akiwepo mtoto wa darasa la sita ikiwa ina maana ni kati ya miaka 12 mpaka 14.
Mheshimiwa Spika, hivi Serikali haioni kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwa na mitaala ambayo itawafundisha watoto hawa kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari, ambayo itawafanya waelewe athari za kupata mimba utotoni ambazo ni muhimu sana? Mitaala hii itaweza kuwasaidia watoto hawa kujitambua na kufahamu umuhimu wa kutokukubali kupata mimba utotoni.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali
inafanya jitihada kubwa sana kupambana na madawa ya kulevya sasa hivi na naiunga mkono, nai-support na tunashukuru sana. Jitihada hii ni kwa sababu Serikali imeona athari hasa inayowapata vijana wa kiume na wa kike kwa
kutumia madawa ya kulevya, lakini watoto wa kike
wanapata athari mara mbili, kwanza athari ya madawa ya kulevya na mimba za utotoni.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuleta mkakati
mkubwa kama ule wa madawa ya kulevya ili tupunguze athari za mimba za utotoni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali linalohusiana na masuala ya mitaala kama ifuatavyo:-
Kimsingi katika elimu ya Msingi na elimu ya Sekondari wanafunzi wanapewa maarifa kuhusiana na masuala ya Kibaiolojia na sayansi yanayohusisha hata masuala ya maumbile ya miili yao, kwa hiyo kimsingi suala hilo linafanyika labda tunaloweza kuahidi hapa ni kutoa msisitizo wa kuona kwamba wanafunzi hao wanapewa dozi zaidi hasa kwa kuwachukua hawa watoto wa kike na kuwapa elimu ya ziada kwa ajili ya kuwanusuru katika mazingira hayo.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza tunao mpango wa kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao ni jumuishi kwa sekta takribani tisa za Serikali yetu na mpango huu umezinduliwa mwaka jana mwezi Desemba na Mawaziri tisa wa Serikali hii ya Awamu ya Tano na Mawaziri wameonesha comittment kubwa sana ya kuweka utaratibu
wa kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni lakini pia mimba za utotoni na vitendo vyote vinavyohusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike.
Mheshimiwa Spika, tunachokihitaji kwa sasa ni
kupewa fedha kwa ajili ya kutekeleza mpango huo na kwenye mpango huu tunalenga kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa kiwango cha asilimia isiyopungua 50 kufikia mwaka 2022. Kwa hivyo, mpango huu kama tutapangiwa fedha, tunapanga kuanza kuutekeleza mwezi Julai mwaka 2017. Kwa hivyo, mpango tunao pia tuna mikakati mbalimbali inayoendelea kama ya elimu ya malezi chanya (Positive Parenting Education) kwa watoto ambao umefanyika kwenye Wilaya 72 za Nchi yetu
na tunawalenga zaidi viongozi wa kimila, wazazi pamoja na watu mashuhuri wenye kufanya maamuzi kwenye jamii.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, napata taabu kidogo maana yake na mimi ni mwalimu, iwapo Serikali tutaacha kwenda kwenye specialization na tukafanya watoto wote wakasoma sayansi. Mimi nina wasiwasi kwamba tutapata wanasayansi wabovu zaidi.
Je, Serikali haioni kwamba specialization ni important kuliko ambavyo sasa tunakwenda kumfanya kila mtoto asome sayansi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, specialization inaanza na msingi na niseme tu kwamba tunawahitaji wataalam wa aina tofauti tofauti. Kuna hao specialization ambao wanakuwa wamekuwa vertical yaani anajikita katika eneo moja pia tunawahitaji wale ambao wanakua kimapana (wide knowledgeable people) ambao wanaweza wakaoanisha upande huu na upande huu. Kwa hiyo, katika ku-specialize kupo lakini lazima kuwe na msingi ni wa eneo gani ambalo huyu mtu atafanya specialization. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi. Hivi Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuwaangalia na wanawake wa vijijini, kwa sababu mipango mingine yote imefeli kwa wanawake wa vijijini kupata mikopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa yeye pia ni Kada wa Chama cha Mapinduzi, naomba nimkumbushe kwamba kwenye Ilani ya Uchaguzi pamewekwa maelekezo kwamba kila Halmashauri nchini itenge asilimia tano ya bajeti yake kutoka kwenye Own Source kwa ajili ya kuwakopesha akinamama, huu Mfuko unajulikana kama Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo wanawake wote, wakiwemo wanawake wa vijijini, hata wale anaowapenda sana wa kule Same, nao wanaweza wakatumia fursa hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi yetu ssi Waheshimiwa Wabunge ni kuingia kwenye vikao vya Halmashauri wakati tunapanga bajeti na kushiriki kuhakikisha asilimia tano ya akinamama inatengwa, asilimia tano ya vijana inatengwa. Pia tusiishie hapo, pesa zinapopatikana tuziweke pembeni pesa za Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wabunge ni Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ambayo huwa inahusika kugawa hizi pesa kwenye vikundi mbalimbali. Kwa hiyo baada ya kuwahamasisha wananchi wetu waombe mikopo hii ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, pia tushiriki kwenye vikao vile vya Halmashauri ambavyo vinagawa pesa hizi kwenye vikundi mbalimbali vya akina mama ili ziwafikie kwa uhakika wananchi hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kupitia Benki ya Wanawake tunatengeneza mifumo sasa ambayo itawafikia Watanzania popote pale walipo, hata wa kijijini, sasa hivi matumizi ya simu ni kwa zaidi ya watu milioni 36 hapa nchini, kwa hiyo njia hii itawafikia watu wengi zaidi hapa nchini kwetu. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wananchi wa Madaba wameonesha kuhamasika sana kulima tangawizi, hata mimi ninalima tangawizi Madaba. Je, Serikali haioni kwamba kiwanda cha Mamba Miamba ambacho kitakuwa tayari by March next year, kitahitaji tangawizi nyingi sana siyo kutoka Same tu pamoja na Madaba.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapatia wananchi wa Madaba ardhi ya uhakika ili walime tangawizi kwa wingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuchukue kilio cha mama vilevile kama kilio cha Mheshimiwa Joseph Mhagama. Serikali inaona umuhimu huo na tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha mambo pale yanakaa sawasawa wananchi walime tangawizi waje, kulisha katika kiwanda cha Mama Anne Kilango Malecela. (Makofi
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshmiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa masoko ya nje yanatawaliwa sana na ubora wa mazao na kwa kuwa wanunuzi wa tangawizi kule nje wanapenda sana organic ginger. Sasa Serikali ina mpango gani wa kupeleka elimu kwenye zile sehemu ambazo zinalima sana tangawizi kama vile Mkoa wa Kilimanjaro, Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Ruvuma?
Mheshimiwa Spika swali la pili, kwa kuwa Kiwanda cha Tangawizi cha Mamba Miamba kilichopo Wilayani Same kinategemea kuanza kusindika tangawizi ya kupeleka nje ya nchi katikati ya mwaka 2018.
Je, Serikali itatumia njia gani kuwafanya wananchi ambao wamekata tamaa kulima tangawizi kutokana na bei kushuka sana ili waendelee kulima tangawizi kwa sababu kiwanda hiki cha Mamba Miamba kitahitaji malighafi kwa wingi? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Spika, kwa idhini yako napenda nichukue fursa hii kumtambua Mama Malecela kama Malkia wa Tangawizi. Suala la tangawizi amelifanyia kazi sana. Nichukue fursa hii kushukuru Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo ameshughulikia pacha wangu, zimetengwa pesa nzuri zaidi ya shilingi bilioni
• kusudi hicho kiwanda kiwe na hadhi ya Kimataifa, kizingatie ubora kama nilivyoeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu maswali mawili uliyoniuliza, moja la ubora, Wizara yangu inayosimamia SIDO kwa kutambua suala la viwango, maeneo yote ninaojenga sasa katika mikoa yote mipya tunajenga ofisi za SIDO, sheli, maabara, mahali pa kuchakatia chakula kwa viwango vitakuwa ni kipaumbele; Katavi, Rukwa, Geita, Simiyu ndiyo nakwenda kuanza nalo na pesa tayari ninazo kama nilivyoeleza juzi. Kwa hiyo, nitawafundisha wananchi hasa akina mama kuzalisha vyakula kwa viwango vya kuuza Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa suala la pili kwamba tutafanyaje, ndiyo tangawizi ilikuwa inauzwa Sh.3,500 najua leo bei imeshuka, sawa sababu mojawapo ni muanguko wa bei za bidhaa, commodity price duniani zote zime-dive. Tutafanya nini?
Kazi ninayofanya sasa ni kutafuta masoko makubwa, masoko mengi ya Kimataifa ile demand pool iwawezeshe wananchi wetu waweze kuuza zaidi lakini zaidi kupitia ESDP II tutaongeza tija (productivity) katika uzalishaji kusudi watu walime sehemu kubwa kwa gharama ndogo ile productivity iweze kupeleka hiyo tangawizi. Kwa sababu kiwanda chako hakina mfano, tangawizi yote itakwenda Mamba, ichakatwe, tupeleke Bandari ya Tanga iende duniani kuuzwa.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Tanzania, wanajenga sana zahanati, madarasana mifereji.
Je, Serikali haiwezi kuwa na mpango Maalum kwamba wananchi wakijenga kiasi fulani Serikali nayo inakuwa na kiasi fulani inachukua kumalizia kwa sababu watanzania wanajenga mno? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ni kama amerudia yale ambayo nilikuwa nawaasa Waheshimiwa Wabunge, kwamba hakika kwa kushirikishana wananchi pamoja na Serikali kwa pamoja tunafika na ndiyo maana nikatoa mfano nilivyokuwa nimeenda Moshi Vijijini, Kituo cha Afya ya Kiaseni nimekuta wananchi wamejitoa na Serikali nayo ikapeleka nguvu, hakika tukishirikishana tutaweza kutoka. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi. Kwa kuwa mwaka 2015 nilipokuwa Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki nilitoa ufadhili wa gari la golisi kwenye Kituo cha Kata ya Maore kwa ajili ya Jimbo la Same Mashariki; nina uhakika Serikali inalifahamu hilo. Kwa kuwa, lile gari sasa halina matairi, linahitaji kufanyiwa maintainance kubwa. Je, Serikali mnatoa ahadi gani leo hapa ili wananchi wa Same Mashariki wasikie?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mhesimiwa Mbunge Anne Kilango Malecela kwa kusaidia kazi za Ofisi ya Polisi katika Jimbo la Same Mashariki kuweza kufanya kazi na wanakukumbuka sana. Nimefika mwenyewe Same nimeona wakikukumbuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Serikali inatambua jitihada alizofanya Mheshimiwa Mbunge na tutaongea na Kamanda wa Polisi wa Mkoa ili tuweze kuona namna ambavyo tunaweza tukaunga mkono jitihada hizo ambazo Mheshimiwa Mbunge ulizifanya. Hata hivyo niendelee kukuomba uendelee kuwakumbuka wananchi wa Same kwani wanakukumbuka sana ili vitu kama vile matairi wasiendelee kuvikosa, waendelee kupata kama ulivyokuwa unafanya.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi hii. Kwa kuwa Kata ya Mkomazi ni jirani sana na Kata Ndungu na kwa kuwa pale kwenye Kata Ndungu kuna skimu kubwa sana ya umwagiliaji ambayo inasaidia kilimo kikubwa cha mpunga. Skimu ile sasa imeonekana kwamba imechoka sana na maisha ya wananchi wa Kata ya Ndungu, Kihurio mpaka Kalemawe yapo hatarini; je, Mheshimiwa Waziri atakapotoka Korogwe pale Mkomazi kwa sababu Ndungu ni jirani anatuambia nini, atakuja kuona skimu ile?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nirudie tena ukisoma Tenzi za Rohoni inasema unapotembea na kuzuru wengine naomba usinipite Mwokozi, sitompita Mheshimiwa mama Anne Kilango katika kuhakikisha wananchi wake wanapata maji. (Makofi/Kicheko)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii. Kwa kweli wananchi wa Wilaya ya Same kwa ujumla wao wanajitahidi sana kujenga zahanati. Ningemwomba Mheshimiwa Waziri aone umuhimu wa Serikali kwenda kuona jitihada zile, naomba atuambie hapa ndani atakwenda lini na atatoa msaada gani kwa sababu hali ya wananchi hasa wa milimani upande wa afya ni mbaya sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Anne Kilango Malecela na wananchi wote wa Wilaya ya Same kwamba nitakapokwenda katika Wilaya ya Same sitaishia katika Jimbo la Same Magharibi peke yake bali nitapita mpaka kwenye Jimbo la Same Msahariki. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, swali langu kubwa hapa lilikuwa ni barabara zinazoelekea Mamba Miamba Kiwandani, basi naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali moja kubwa kidogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara zinazoelekea Mamba Miamba Kiwandani zipo za aina mbili, ya kwanza ni barabara inayounganisha Kiwanda cha Tangawizi na masoko ya ndani na nje ya nchi na barabara hii inatokea Mkomazi Kisiwani kwenda Same na barabara ya pili ni barabara zinazounganisha walima tangawizi (wakulima) na kiwanda chao.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Rais wa Awamu ya Nne mwaka 2009 alikuja Mamba Miamba yeye mwenyewe akaona jitihada za wananchi, akatoa bilioni 2 za kujenga barabara za kuwaunganisha wakulima na kiwanda chao. Je, Mheshimiwa Waziri huoni kwamba ili uelewe tatizo kubwa la miundombinu ya kiwanda kile ni vyema wewe mwenyewe ukawaahidi wananchi wa Mamba Miamba utakwenda lini kule ili uweze kujibu haya maswali vizuri, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nipo tayari kwenda, lakini uniruhusu nimpongeze tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu najua kupatikana kwa kiwanda hiki ni pamoja na juhudi zake, lakini niwashukuru na kuwapongeza Mkuu wa Wilaya kwa sababu Mkuu wa Wilaya pia amekuja akiwa na ombi la kutembelea maeneo haya. Natambua kwamba lazima tuboreshe barabara ambazo zinawahudumia wananchi kupeleka malighafi kwenye kiwanda hiki, lakini pia kutoa mazao yanayotokana na kiwanda hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia barabara hii ambayo nimeizungumza ni muhimu sana kwa sababu inapokwenda kuunganisha Mkomazi pia inatoa huduma kwa ajili ya utalii. kwa hiyo, nipo tayari Mheshimiwa Mbunge nitakuja Same tutembelee maeneo hayo. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza; je, Serikali ina mpango gani wa kuwavutia zaidi wawekezaji ambao wakija watawekeza kwenye viwanda vya kuongeza thamani mazao yetu kuliko viwanda vingine vyovyote.(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatetea wananchi wake hasa kwenye suala la viwanda ambalo linahusisha masuala la vitunguu na tangawizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili niseme kwa ufupi ya kwamba, kama Serikali tumeona ni vema kuendelea kutumia Balozi zetu, vilevile tumeona ni vema kufanya makongamano mbalimbali ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa ninavyozungumza mwaka jana Desemba, tulifanya mazungumzo na kongamano kubwa na Wafanyabishara kutoka China. Mwezi Desemba pia tulifanya kongamano kubwa na wafanyabiashara kutoka Jordani, tarehe 18 mwezi wa Nne tulifanya Kongamano kubwa sana na wawekezaji kutoka Ufaransa kwa lengo hilo hilo. Vile vile tarehe 23 - 24 Aprili tulikutana na watu kutoka Israel.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo letu kuwavutia wawekezaji wengi zaidi na kuwaomba kuja kuwekeza hasa katika maeneo haya ya kuongeza thamani. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hiyo Serikali inaendelea kuifanya. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, Wilaya ya Same, ni Wilaya ambayo takribani, eneo lake katika Mkoa wa Kilimanjaro ni 40% ya eneo zima la Mkoa wa Kilimanjaro. Lakini Wilaya ya Same mara kwa mara inatengewa pesa kidogo sana inapewa pesa zilizoko chini ya wilaya ambazo ni ndogo zaidi ya wilaya ile. Naomba Serikali ione kwamba haioni umuhimu wa kutenga pesa zinazolingana na ukubwa wa Wilaya ile ya Same ambayo ni takribani 40% ya eneo lote la Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili nakuja kwenye barabara hii ya Hedaru – Vunta – Myamba barabara hii ni korofi mno, sijawahi kuona barabara kama hii, Awamu ya Nne niliwanyenyekea hapa Bungeni kwamba barabara ya Mkomazi, Kisiwani Same, waiweke kwa vipande vipande, walifanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa barabara hii yenye kilomita 42.2 hii TARURA Same wamefanya tathmini ya kutengeneza barabara yote kwa ujumla, wakapata ni bilioni 1.8.Je, Serikali hamuoni kwamba kwa sababu wananchi hawa wanahangaika mno mkatengeneza vipande vipande ili mmalize tatizo lote, kuliko mnavyochukua vimilioni viwili vitatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniruhusu kwanza kabla ya kujibu maswali mawili ya nyongeza nimpongeze kipekee Mheshimiwa Kilango Malecela jinsi ambavyo amekuwa akipigania wananchi wake wa Same na sisi sote ni mashahidi Kiwanda kile cha Tangawizi kimejengwa ni kwa ajili ya kazi kubwa aliyofanya yeye.

Mheshimimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mgawanyo wa fedha umekuwa hauendani na uhalisia na hili ni swali ambalo limekuwa likiulizwa na Waheshimiwa Wabunge wengi na sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI baada ya kuliona hilo sasa hivi tuna-commission consultant kwa ajili ya kuja na formula nzuri itakayosaidia ili tunapogawa fedha twende na uhalisia. Kwa sababu formula inayotumika ndiyo iliyokuwa inatumika mwanzo kabla TARURA haijaanza kufanya kazi. kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Kilango Malecela na Wabunge wengine tuvute subira kwa sababu tayari consultant anafanya kazi atatuletea majibu na formula ambayo itakuwa nzuri kwa kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili anaona iko haja kwa ajili ya ukorofi wa ile barabara tuanze kujenga kwa kiwango cha lami walau kilometa chache chache at the end tuje tukamilishe kilometa zote 42. Ni wazo jema kwa sababu vinginevyo tunakuwa tunarudia fedha inatumika lakini kwa mazingira na jiografia ya barabara ambayo Mheshimiwa ametaja iko haja kubwa sana.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali ya Awamu ya Tano kwa jinsi ambavyo inajitahidi kuboresha afya ya Watanzania lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamoja na jitihada za Serikali lakini kuna tatizo kubwa ambalo liko vijijini na mijini, wanawake wengi bado wakiwa wajawazito hawana ile elimu ya kuona kwamba ni muhimu waende clinic. Sasa Serikali mnajitahidi kiasi gani kuhakikisha wanawake wakiwa wajawazito vijijini pamoja na mijini wanakwenda clinic? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, tafiti zilizofanywa katika nchi yetu ya Tanzania, bado watoto ambao wana chini ya umri wa mwezi mmoja baada ya kuzaliwa wanakufa kwa wingi na ukweli tafiti zimeonesha kwamba hawajapungua kabisa, wanaendelea kufa. Serikali mnaniambia nini katika hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpa pongezi sana amekuwa ni champion mkubwa sana katika masuala ya afya ya uzazi wa akina mama na mtoto. Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zake hizo.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijielekeze katika maswali mawili mawili ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyauliza. La kwanza ni kuhusiana na akina mama kwenda kliniki. Ni kweli, Serikali imewekeza juhudi kubwa sana katika kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya. Mwaka 2015 idadi ya akina mama ambao walikuwa wanakwenda clinic ilikuwa ni asilimia 38 kwa mara zote nne katika kipindi cha ujauzito lakini Serikali imeendelea kuweka juhudi, mikakati mbalimbali pamoja na kutoa elimu kwa akina mama, hivi tunavyoongea hadi kufikia Desemba 2019, asilimia 80 ya akina mama wanakwenda kiliniki.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii nayo ni hatua kubwa sana katika kuhakikisha akina mama wanapata elimu, ushauri katika kipindi chao cha ujauzito na hii inaweza kusababisha hata kupunguza vifo vya akina mama na watoto. Nitoe rai kwa akina mama wote na akina baba kwa sababu masuala haya ya ulezi wa ujauzito ni jukumu la wazazi wote wawili kuhakikisha kwamba kila mama mjamzito anafika kliniki kwa ajili ya kuweza kupata ushauri nasaha na jinsi gani ya kuweza kutunza ujauzito ule.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili vifo vya watoto chini ya mwezi mmoja, ni kweli katika takwimu ambazo hazishuki ni pamoja na hii. Katika mwaka 2015, tulikuwa na watoto wachanga chini ya mwezi mmoja wakifariki 26 kwa vizazi hai 100,000. Sasa hivi tunapoongelea Desemba mwaka jana imeshuka kwa unit moja tu mpaka 25 kwa vizazi hai 100,000.

Mheshimiwa Spika, lakini sisi kama Serikali tunajaribu kuweka hatua, kwanza kuhamasisha akina mama kwenda kliniki; pili kuhakikisha kwamba chanjo zote za msingi za watoto chini ya miaka mitano zinapatikana; kutoa elimu kwa watoa huduma wa afya pamoja na akina mama ikiwa ni pamoja na jinsi ya kutunza watoto njiti. Visababishi vikubwa vya watoto chini ya mwezi mmoja ni zile complication ambazo wanazipata wakati wa kupumua wakati wa kujifungua, maambukizi ya magonjwa ambayo wanayapata wakati wa kujifungua ikiwa ni pamoja na uzito wa chini.

Mheshimiwa Spika, hii ndiyo mikakati ambayo tumejaribu kuifanua kwa kupanua huduma za afya kuhakikisha kwamba akina mama wajawazito ambao wana pingamizi wanapata huduma kwa haraka. Tumepunguza sana maambukizi ya watoto hawa na kuhakikisha wale watoto njiti wanatunza kwa njia ya kangaroo motherhood ambapo kwa kiasi kikubwa tunaamini sasa tutapata matokeo makubwa sana. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kata hizi alizozitaja Mheshimiwa Dkt. David Mathayo ni Kata ambazo ziko kwenye milima mirefu. Naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba alikuja Same Mheshimiwa Dkt. Mathayo akaingia kwenye gari yake na mimi nikaingia kwenye gari yake tukazizungukia kata hizi zote ambazo zimetajwa hapa na Kata ya Vuje, kata ya Bombo, Kata ya Mtina kata ya Lugulu.

Mheshimiwa Waziri uliona hali halisi ya kata hizi kwamba ni korofi mno hazina mawasiliano ya uhakika pamoja na mawasiliano ya Barabara, Mheshimiwa Waziri unakuja na mikakati gani sasa ya kuhakikisha hizi kata ambazo ziko milimani zinaondoka na matatizo haya ahsante Mheshimiwa.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza uniruhusu tu nitoe shukrani kwamba nilivyofanya ziara katika maeneo haya nilipata ushirikiano wa hali ya juu sana kwa Mheshimiwa Mbunge lakini pia kwa viongozi wa wilaya, kwa hiyo nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na niseme tu yapo maeneo mbalimbali ambayo yanakuwa na changamoto kutokana na hali ya jiografia, eneo la Same hili linamilima lakini yapo maeneo mengine ambayo yana misitu ambayo hii ni vikwazo kwa mawasiliano kwa hiyo utaona changamoto ya mawasiliano imekuwa kubwa katika eneo hili kwa sababu ya hali ya jiografia kwa maana hiyo milima na misitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumejipanga kama Serikali ndiyo maana utaona katika awamu ya nne tuko kwenye hatua ya manunuzi, tutaendelea kuweka hiyo minara ambayo imetajwa na katika eneo hili tutakuwa na kata tano vijiji kumi na tatu na baada kusimika hiyo minara tutafanya tadhimini kuona maeneo yapi kutokana na geografia ambayo yatakuwa hayajapata tena mawasiliano kwahiyo hizi changamoto tunaendelea kuziondoa tunavyokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge mkakati mkumbwa uliokuwepo ni kuhakikisha kwamba tunaweka maeneo haya katika mipango yetu kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote. Lakini pia tunaweka bajeti ya kutosha tunavyokwenda ili sasa tuhakikishe kwamba baadaye tunamaliza changamoto ya mawasiliano katika eneo hili lakini unafahamu pia tunaendelea kufanya usanifu mkubwa katika barabara kutoka Same kwenda Mkomazi lakini tutakwenda mkinga kule tumejipanga ili tuondolee shida wananchi wa maeneo haya ambayo hali ya geografia inawaathiri sana kwa maana ya usafiri wa barabara hali ni mbaya lakini pia upande wa mawasiliano ahsante sana.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata jibu kwamba Serikali inashughulikia suala hili lakini naomba kuuliza swali moja tu la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Tanzania ni nchi mojawapo katika nchi 4 za Afrika ambazo zinalima pamba ambayo ni organic. Naomba Serikali iniambie ina mikakati gani ya kuwaalika wawekezaji katika zao hili la pamba nchini ili wafungue viwanda hapa nchini kuliko ambavyo tunauza pamba ghafi ambapo tunapata hasara sana? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akisimama imara katika kuhakikisha kwamba zao letu la pamba linaongezewa thamani ili badala ya kuuza zaidi ya asilimia 70 ya pamba yetu ghafi basi kwa kiasi kikubwa tunaweza kuiongezea thamani hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kama Serikali tunayo mikakati ya muda mfupi, wa kati pamoja na muda mrefu. Mfano ukiangalia katika nchi zingine kama Bangladesh na Ethiopia kwa upande wa Afrika ambazo zimefanikiwa unaangalia kuna mnyororo wa thamani, wapo ambao wameanzia katika utengenezaji wa nyuzi, mfano kama Bangladesh na Ethiopia wao wameanzia katika mnyororo wa mwisho kabisa wa kutengeneza mavazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika masuala ya mtaji, mfano mwekezaji mmoja tu ambaye anatengeneza mavazi anaweza akaajiri mpaka watu 20,000 lakini wakati huohuo mtaji wake anaoutumia inaweza ikawa ni dola milioni 3 mpaka milioni 4. Wakati ukianzia katika ngazi labda ya nyuzi pamoja na vitambaa inaweza ikakugharimu zaidi ya dola milioni 10 au zaidi na wakati huohuo ajira pia inakuwa sio nyingi sana. Kwa hiyo, kama Serikali tunatambua umuhimu wa mnyororo mzima wa thamani, tunachokifanya kwa sasa ni kuangalia sasa twende vipi, twende na hatua zote kwa upande huo wa mnyororo au tujikite zaidi kama ambavyo wenzetu wa Ethiopia wamefanya na ukizingatia kwamba hata hawazalishi pamba nyingi zaidi hai kama ambavyo tunafanya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nisema tu kwamba kwanza naendelea kuwapongeza wakulima wote wa pamba na naendelea kutoa rai kubwa waone ni kwa namna gani wanaboresha ubora wa pamba yenyewe wanayoizalisha kupitia kilimo. Ukiangalia katika uzalishaji wenyewe wa mavazi pamoja na nguo zetu kwa kiasi kikubwa zinahitaji kuwa na consistency katika mnyororo mzima. Haiwezekani leo ukawa na ubora wa aina hii halafu kesho una ubora mwingine. Kwa hiyo, niendelee kutoa rai kwa Maafisa wetu wa Ugani waendelee kutoa elimu kwa wakulima wetu wa pamba kuhakikisha kwamba katika uzalishaji wa pamba wanayoizalisha basi kuona kwamba inaendelea kuwa na ubora unaotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ukiangalia hata katika viwanda vyetu, pamba inayozalishwa ni takribani tani 300,000 mpaka 400,000 kwa mwaka. Katika msimu wa mwaka huu kwa makadirio ya Wizara ya Kilimo ni kuweza kupata takribani tani 450,000 lakini ukiangalia uwezo wa viwanda vyetu takribani 54 ni kuweza kuzalisha zaidi ya tani 786,000. Kwa hiyo, bado tuna upungufu ni lazima yote haya uzalishaji pamoja na kuboresha uwekezaji viweze kwenda sambamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni suala zima la mitaji. Ukiangalia katika sekta nzima ya uzalishaji wa nguo na mavazi, viwanda vinahitaji mitaji mikubwa sana. Si hilo tu, wapo ambao wamefanikiwa kama kina Jambo Spinning lakini wamejikuta wameshindwa kuendelea na uzalishaji. Hii ni kutokana na sababu kwanza mtaji ni mkubwa lakini akifanikiwa kuweka mtaji bado mazingira siyo wezeshi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachokifanya kama Serikali sasa hivi ni kuangalia sekta ndogo hii ya nguo na mavazi kupitia Mkakati wetu ule wa Nguo na Mavazi wa mwaka 2016 – 2020 kuweza kuona ni kwa namna gani sasa tutaweza kuweka vivutio maalum. Kwenye hili siwezi kusema tutaweka vivutio vya aina gani kwa kuwa tutatunga sheria pamoja, Mungu akijaalia nadhani muda si mrefu tutakuja na Muswada wa Sheria ya Uwekezaji ili tuweze kuangalia katika zile sekta ndogo mbalimbali, ni sekta zipi ndogo ambazo kama nchi tunaziwekea kipaumbele tukitambua kwamba ndizo zinaajiri watu wengi lakini tukitambua kwamba inakuwa na mnyororo mkubwa wa thamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Kilango na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamekuwa wakifuatilia sana uzalishaji wa pamba lakini zaidi uongezaji wa pamba na matumizi yake. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwa kuwa mwaka 2015 mimi mwenyewe niliifadhili Wizara ya Mambo ya Ndani gari la Polisi kutoka Japan, jipya, na nikalipeleka kwenye kituo cha Polisi kilichoko Maore kwa ajili ya Jimbo la Same Mashariki, lakini Serikali mpaka leo mnashindwa kutoa hata pesa kidogo kwa ajili ya kupeleka service gari lile. Waziri unaniambia nini sasa hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunathamini sana jitihada za Mheshimiwa Anna Kilango Malecela za kuweza kutusaidia gari kwa matumizi ya Jimbo la Same. Namhakikishia Mheshimiwa kwamba hatushindwi kufanya service hiyo gari; na kama kuna tatizo la service, basi tumelipokea na tutahakikisha kwamba gari hiyo inafanyiwa service ili iweze kutumika. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA:Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii. Jimbo la Mheshimiwa Mnzava ni mpakani na kijiji changu cha Kongei ambako nimezaliwa na umeme kwenye kijiji hiki umefika muda mrefu, lakini kuna Vitongoji vya Mabambara, Ihindi na Idurundi, huenda vimesahauriwa kabisa. Mheshimiwa Waziri unaniambia nini katika hili?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda nijibu swali moja la Mheshimiwa Mama yangu Anne Kilango Malecela na nimshukuru sana kwa kazi nzuri ya kufuatilia sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya nishati na kwa kuwa swali lake la nyongeza ameulizia katika usambazaji wa umeme kwenye vitongoji vilivyosalia katika Kijiji chake cha Kongei.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimtaarifu kwamba Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa tisa ambayo mradi wa ujazilizi awamu ya pili ambao upo hatua za kumpata mzabuni, Mkoa huu wa Kilimanjaro umo kwenye mikoa hiyo tisa na nimwagize Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kilimanjaro na wa Wilaya ya Same azingatie vile vijiji ambavyo vimepatiwa umeme kikiwemo Kongei, lakini vipo vitongoji ambavyo havina umeme ili waendelee kusambaza kupitia umeme wa ujazilizi awamu ya pili ambapo Bunge letu mmetupitishia takribani shilingi bilioni 169 na tunawashukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ukweli Halmashauri za Tanzania hazilingani upande wa vyanzo vya mapato, na kwa kuwa Halmashauri kama ya Wilaya ya Same vyanzo vya mapato ni vya chini mno, kwa hiyo, inasababisha wananchi wa Wilaya yetu wa Same kuwa maskini ukilinganisha na kwenye Wilaya nyingine ambazo wana vyanzo vikubwa vya mapato.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutafuta taratibu nzuri ya kufanya zile Halmashauri ambazo vyanzo vya mapato viko chini mno nao wakaongezewa ili wananchi wa Tanzania wawe katika uwiano unaolingana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti ya kiwango cha mapato katika Halmashauri inatokana na wigo wa ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri husika na kimsingi asilimia kumi kama ambavyo jibu la msingi limeeleza, linatokana na mapato ya ndani baada ya kutolewa vyanzo lindwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali inaona umuhimu wa kuona namna gani tunaweka mazingira mazuri zaidi kwa Halmashauri zile ambazo zina mapato ya chini zaidi, lakini jambo hili linahitaji kulifanyia tathmini, kulipitia na kuona njia nzuri zaidi ya kuendelea kuboresha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue wazo la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, kuweza kuona ni namna gani tunafanya ili tuweze kuboresha huduma hizi za mikopo ya asilimia 10. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata nafasi:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sisi wakati tunasoma miaka ya 70 sekondari tulikuwa na mchepuo wa needle work na cookery.

Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba, kwa needle work niliyoisoma miaka ile ya 70 nimeweza kushona kibiashara mpaka leo nafanya hiyo kazi. Hivi Serikali kweli hamuoni ni muhimu sana kuwafanya akinamama waweze kupata kitu ambacho watakibeba mpaka wakiwa watu wazima?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Malecela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Malecela, kama nilivyozungumza mwanzo kwamba, tuko kwenye mjadala, mjadala ambao utawahusisha vilevile Wabunge. Ninyi Waheshimiwa Wabunge ndio ambao mtaamua kwamba, vitu gani tuweke kwenye mitaala yetu kwa lengo la kuhakikisha tunatengeneza jamii, tunatengeneza kizazi ambacho kitakwenda kujitegemea katika nyanja hizo ambazo tunazihitaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wakati huo utakapofika Waheshimiwa Wabunge tutaomba tupokee maoni yenu na sisi bila tatizo lolote tutaingiza kwenye mitaala hiyo, ili kuhakikisha tunatengeneza Taifa lenye kujitegemea. Ahsante.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo ameyatoa na niongeze tu dogo kwamba, pamoja na maboresho ambayo tunayafanya, lakini hata sasa somo la needle work na cookery linafanyika, lakini kwa shule chache.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa nataka tu pia ifahamike hivyo kwamba, linaendelea kutolewa, lakini sio somo kwa wote. Kwa hiyo, tutazingatia kuona kuna umuhimu na tunakubaliana kwamba, kuna umuhimu wa kuhakikisha vijana wengi wa kitanzania wanapata ujuzi huo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata majibu ya Serikali, lakini sina raha na haya majibu, naomba kuuliza maswali mawili.

Kwa kuwa wakati wa Bunge la Kumi nilishauliza hili swali mara mbili, kwa sababu hili gari limekuwa bovu kwa muda mrefu; je, Serikali mnavyonijibu leo mko serious kweli hili gari litatengenezwa na litatengenezwa lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, hivi Serikali inafahamu kwamba hiki Kituo cha Polisi kipo Mahore na Mahore ni tambarare na asilimia 68 ya wananchi wa Jimbo la Same Mashariki wanaishi milimani na kama kituo kile kinakuwa hakina gari wale wananchi hawana ulinzi na maisha yao.

Je, Serikali mnalijua hilo na kama mnalijua mtafanya jitihada ya kutengeneza hili gari? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Same Mashariki kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba gari hili ni bovu na ni kweli kwamba ni muda mrefu, lakini ni ukweli pia ambao Mheshimiwa Mbunge hajausema. Gari hili alipewa baada ya yeye kutoa gari kwa Jeshi la Polisi aliyekuwa amepewa msaada na wafadhili wake, kwa ajili ya kituo hiki. Sasa kwa sababu gari lile aliyekuwa la kwake aliyekuwa amepewa lilikuwa la kisasa sana ambalo kwa kweli lisingeweza kupelekwa kule kijijini, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi walilibakiza kwa ajili ya shughuli za Makao Makuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo hii Mbunge anaposikitika hivi mbele yako niseme tu kwa niaba ya Serikali na Wizara tutaitengeneza hili gari mapema iwezekanavyo ili kutoa heshima na shukrani kwa Mheshimiwa Mbunge, lakini kwa nia njema tu ya kufanya ndugu zetu wale wa Same Mashariki, kule Mahore wapate huduma hii vizuri zaidi. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Skimu ya umwagiliaji ya Kata ya Ndungu ndiyo skimu kubwa katika Wilaya ya Same na skimu hii sasa inakwenda kufa. Sasa nimembembeleza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa muda mrefu, twende akaione, leo naomba aniambie tunakwenda lini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anne Malecela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni bahati kubembelezwa na mama. Nikiri kweli Mheshimiwa mama Kilango ameshaniomba twende jimboni kwake na nimhakikishie mama baada ya Bunge hili tutaenda Jimboni kwake pamoja. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwashukuru sana wananchi wa Kata ya Mtikwa kunipa kura nyingi sana bila shuruti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kuuliza swali la nyongeza kwa kuwa jumatatu ya pasaka mimi na Naibu Waziri wa Afya tulikwenda kuiona zahanati hii ya Kata ya Mtii na kwa kuwa wananchi wale wamefanya jitihada, niliyeanza kujenga ile zahanati ni mimi na wananchi, sasa wananchi walichomlilia Naibu Waziri wa Afya, wanaomba wajengewe nyumba ya Mganga.

Je, Serikali hamuoni kwamba wananchi wangu wamejitahidi sana kujenga zahanati ile wao wenyewe na Mbunge wao na Mbunge alipokuja aliweka kitu kidogo mkatusaidia kujenga nyumba ya mganga wa zahanati ile? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Anne Kilango Malecela na wananchi wa Jimbo la Same Mashariki kwa kazi kubwa walioifanya kuanzaujenzi wa Zahanati ya Mtii, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge amekuwa karibu sana na wananchi, amefanya ziara pale na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya na wameona kazi nzuri inayoendelea na wananchi wanatambua mchango mkubwa wa Serikali ambao unaendelea kutolewa katika ujenzi wa zahanati ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyojibu kwenye swali la msingi tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya Zahanati ya Mtii, lakini pamoja na kuweka bajeti kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mganga katika zahanati ile. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, huu uharibifu unaoletwa na wanyamapori ni mkubwa sana kwa nchi nzima na vifo vinatokea karibu kila siku tunaongea humu ndani. Hivi Serikali haioni inastahili kufanya zaidi ya inavyofanya sasa ili kuokoa maisha ya wananchi wetu? (Makofi)
NAIBU WIZARA WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali inatambua changamoto hii na wananchi kweli wamekuwa wakiathirika vikiwemo vifo ambavyo vinatokea. Hata hivyo, naendelea kusema kwamba changamoto ya wanyamapori wakali imekuwa kubwa na sababu kuu ni kwamba tumevamia maeneo ambayo ni mapito ya wanyama wakali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kuona haya yote, kwa sasa hivi tumejipanga kuandaa hivi vikosi kazi vya maaskari na tutagawa orodha ya watumishi wote ambao wanazunguka maeneo ya hifadhi kuhakikisha kwamba inapotokea athari yoyote au kuonekana kwa mnyama mkali yoyote basi taarifa itolewe kwa haraka ili tuweze kudhibiti hawa wanyama wakali. Kingine ni kuhakikisha kwamba tutakapokuwa tumewafundisha hawa wananchi kujua namna ya kujikinga na hawa wanyama wakali, basi tutakuwa tumeshirikiana kwa pamoja kuhakikisha kwamba maeneo yenye hifadhi yanahifadhiwa vizuri lakini na wananchi wanaendelea kujikinga na hawa wanyama wakali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwape pole sana wananchi wote ambao wamekuwa wakikutana na hii kadhia na hata Serikali siyo kwamba inapenda kuona wananchi wake wanaendelea kupata shida ya namna hii. Tunajipanga ili kuhakikisha kwamba kadhia inapungua ama kutoweka kabisa kwa sababu hata sisi imekuwa ni changamoto kubwa lakini tunajipanga kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa akina mama wa Jimbo la Same Magharibi wengi wao nao pia wako katika Machimbo haya ya Jasi na wanachimba jasi kwelikweli. Je, Serikali haioni kwamba ni muhimu hawa akina mama kupata mikopo maalum kwa sababu uchimbaji wa jasi unatumia pesa nyingi? Kama inawezakana, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuwapa mikopo akina mama wote wa Tanzania ambao wanachimba madini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Same Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu swali la msingi lilikuwa linataka tujenge barabara tuwasaidie, lakini miongoni mwa majibu ambayo tulikuwa tumetoa ni pamoja na kuwainua akina mama ambao wanafanya kazi katika machimbo hayo ya jasi.

Mheshimiwa Mbunge wa Same Mashariki amependekeza Serikali itenge fedha kwa ajili ya kupeleka mikopo na sisi sasa hivi katika moja ya sheria ambazo tulipitisha ndani ya Bunge ni kuhakikisha zile asilimia kumi za mikopo kutokana na mapato ya ndani zinakwenda katika hayo makundi ya akina mama, vijana na watu wenye mahitaji maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumelipokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na nafikiri moja ya kipaumbele ambacho tutakizingatia ni hicho. Ahsante.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde kwa majibu mazuri. Vile vile nampongeza Mheshimiwa Mama Anne Kilango, ame-raise humu ndani hoja ya msingi sana ya kutambua makundi maalum na hasa ya wanawake yenye mahitaji maalum ya mikopo kwa ajili ya shughuli za kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mama Anne Kilango, pia niwatangazie na Wabunge wengine wote, kupitia mpango maalum wa Serikali, tayari tumeanzisha mfuko maalum wa SUNVIN; tunauita hivyo kwa ajili ya ku-support shughuli hizi za akina mama na wafanyabiashara wadogo na wa kati ili waweze kuji- transform na kufanya biashara kubwa na hasa za uwekezaji kwenye viwanda, madini na shughuli nyingine zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, mnaweza kuwasiliana na Ofisi ya Waziri Mkuu ili mpate taarifa ya mfuko huo akina mama na Watanzania wengine waweze kuanza kuutumia. Tayari mfuko huo umeshakuwa na fedha na umeshaanza kutumika kufanya uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali nchini. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii. Kwa kuwa, Mkoa wa Kilimanjaro asilimia 40 ni Wilaya ya Same; na kwa kuwa Wilaya ya Same ina majimbo mawili; na Wilaya nzima ina Hospitali ya Wilaya moja: Je, Serikali haioni kwamba lile eneo ni kubwa sana, sasa upande wa Mashariki nao wapate japo Hospitali ya Wilaya moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, sera yetu ya sasa ni kwamba kila Halmashauri ya Wilaya ipate hospitali yenye hadhi ya wilaya na ndio maana kwenye bajeti hata ya mwaka huu ambayo tumeipitisha mwaka 2021/2022 Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuhakikisha hata zile Halmashauri ambazo hazikuwa na hospitali za Halmashauri tutazijenga mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili alilolileta hapa ni wazo kwamba angalau jimbo kwa imbo liweze kupata lakini tutaendelea kuzingatia kuleta huduma bora za afya katika maeneo yote ikiwemo kujenga vituo vya afya na zahanati kuhakikisha huduma zinawafikia walengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lengo la kwanza ni kuhakikisha kwamba tunamaliza kwanza Halmashauri zote halafu maombi mengine tutakuja kuyazingatia kulingana na mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, kwa kweli wakazi wengi wa Same ambao wanaishi karibu na Mkomazi National Park wapo kwenye risk kubwa ya kupata matatizo na kupoteza maisha yao. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri tulikuwa naye Jumamosi na Jumapili kule Same na ameona hali ilivyo, haoni kwamba ni vyema zile sehemu zote ambazo zina risk kubwa kukawepo askari ambao wanakuwepo kuwafukuza wale tembo kuliko kuacha hali ilivyo mpaka sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango, Mbunge wa Same Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tulienda ziara na Mheshimiwa Anne Kilango, changamoto ya tembo ipo, ni kweli na ni kubwa, lakini tulitoa maelekezo na naomba hili niendelee kuelekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwamba tutaweka kambi ambazo zitakuwa ni za doria kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanaishi kwa usalama.

Mheshimiwa Spika, na hili nikuahidi kwamba maeneo yote ambayo yana risk kubwa ya tembo, tutahakikisha kwamba askari wanaishi maeneo yale ili changamoto hii hasa kipindi hiki cha mavuno tuweze kuidhibiti na wananchi waishi kwa amani, ahsante. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kwenye Jimbo la Same Mashariki, Kata ya Ndungu pamoja na Kata ya Mahore kuna mashamba makubwa ya kilimo cha mkonge lakini anayemiliki mashamba hayo haonyeshi kujali zao lile.

Je, Serikali mnasema nini katika hilo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema moja ya mikakati ya Serikali ni kujihakikishia kuwa tuna malighafi za kutosha ambazo zitaenda kuchakatwa kwenye viwanda vyetu ambavyo tunavihamasisha kuanza kuvifufa sasa.

Kwa hiyo, moja ya mikakati ambayo tumeshaweka kupitia Wizara ya Kilimo ni kuwapa mikakati au kuhakikisha hawa wakulima wanaendeleza sasa haya mashamba ya mkonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hata hawa wa Same nakuahidi na Wabunge wapo hapa tunaendelea kujadiliana nao lakini kuhakikisha wanaenda kufufua mashamba hayo ili aweze kutoa raw material au malighafi kwenye viwanda ambavyo tunaendelea kuvifufua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi. Kwa sababu sehemu hizi mbili; Bendera na Mkomazi jambo kubwa wanalogombea ni mpaka kati ya Bendera na Mkomazi, ndiyo linapokuja suala la madini: Je, Serikali hamuoni ni muhimu sana Mkuu wa Mkoa akafika pale akaweka vizuri mpaka ule ili hili tatizo lililozungumzwa hapa ndani sasa hivi lisiendelee kutokea? Ahsante.

SPIKA: Haya tulikuwa na migogoro ya mipaka ya Wilaya kwa Wilaya, sasa huu mpaka wa Kata kwa Kata ambapo maana yake kuna vijiji na vijiji.

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, ni mpaka wa Mkoa wa Kilimanjaro na Mkoa wa Tanga, uko kati ya Bendera na Mkomazi.

SPIKA: Okay! Ni mipaka ya mikoa!

MHE. ANNE K. MALECELA: Ndiyo.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela. Kule kote ambako kuna migogoro ya tafsiri za mipaka sisi tunahusika. Kwa hiyo, hatutasita kwenda kutafsiri ardhini tafsiri ya mipaka iliyoainishwa na mwenye mamlaka. Tunazo GN, tutaifanya kazi hiyo. Nitaomba tu Mheshimiwa Kilango anipe maelezo ya ziada ili tuunde timu yetu ya pamoja ikafanye kazi hiyo. Hiyo ndiyo kazi yetu ya kutafsiri GN zilizoainisha mipaka na mwenye mamlaka. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika nashukuru kwa kupata nafasi. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kutumia pesa nyingi sana kujenga Daraja la Yangoma ambalo lilikuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi waliopo kwenye barabara hii. (Makofi)

Mheshimwia Spika, kulingana na ubora wa Daraja la Yongoma lililojengwa ambalo Naibu Waziri, Mheshimiwa Waitara, alikuja tukaenda kuliona. Kweli Serikali hamwoni kuna umuhimu wa kuijenga ile barabara iwe na hadhi sawa na lile daraja lililowekwa pale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela Mbunge wa Same Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru kwa kupongeza kazi nzuri ambayo imefanyika ya kujenga lile daraja. Pili, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kujenga daraja hilo maana yake ni maandalizi ya kuja kujenga pia barabara nzuri inayofanana na hilo kwa sababu hatutajenga tena.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana kwenye jibu letu la msingi tumesema tunatafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili sasa hiyo barabara iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Hiyo hatua hatuwezi kuiruka, ni lazima tuifanye na ndiyo maana tunatafuta hiyo fedha. Ahsante. (Makofi)