Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Anne Kilango Malecela (8 total)

MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza:-
Ndoa za utotoni kwa sasa zimekithiri sana na ndoa hizi zina athari kubwa ndani ya jamii:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutokomeza ndoa hizi za utotoni?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua athari kubwa zanazosababishwa na ndoa za utotoni katika jamii yetu ya Tanzania. Ndoa za utotoni zinawanyima watoto wa kike fursa ya kupata elimu na hivyo kusababisha umaskini miongoni mwao punde wanapokuwa watu wazima kwa kuwa wanakosa mbinu mbadala za kujikwamua kiuchumi kutokana na kukosa elimu. Aidha, mimba za utotoni ni hatari kwa afya ya mama na mtoto kwa kuwa maumbile ya kibaiolojia ya mtoto hayawezi kuhimili mchakato wa uzazi na mara nyingi mimba hizi zimesababisha vifo.
Mheshimiwa Spika, kulingana na takwimu za afya na idadi ya watu nchini za mwaka 2016, ndoa za utotoni zimeshamiri katika Mikoa ya Shinyanga kwa kiwango cha asilimia 59, Tabora kwa kiwango cha asilimia 58, Mara asilimia 55 na Dodoma asilimia 51.
Mheshimiwa Spika, kwa kukabiliana na changamoto hii, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya malezi chanya kwa wazazi na walezi ili waweze kutambua umuhimu wa kumwendeleza mtoto wa kike. Elimu hii imetolewa katika Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Miji 72 nchini. Msukumo umeongezwa zaidi katika kuelimisha familia, wazee wa mila na jamii kuachana na mila na tamaduni zilizopitwa na wakati za kuoza watoto wa kike. Mwaka 2015, Serikali ilizindua rasmi kampeni ya Kitaifa ya kutokomeza ndoa za utotoni ambayo iliwataka wadau wote zikiwemo familia kushirikiana kutokomeza kabisa ndoa za utotoni hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa muundo wa kisera na kisheria, Serikali imezifanyia maboresho sera na sheria ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa na mimba za utotoni mfano Sera ya Elimu ya mwaka 2014 inaelekeza kutolewa kwa elimu bure na ya msingi kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha nne pamoja na marekebisho ya Sheria ya Elimu, Sura ya 353 yaliyopitishwa na Bunge la 11 ambayo inatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 30 kwa mtu yeyote atakayempa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari.
Mheshimiwa Spika, tarehe 13 Desemba, 2016, Serikali ilizindua mpangokazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto uliojumuisha sekta zote zinazohusu wanawake na watoto kwa lengo la kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Mpangokazi huu ambao utaanza kutekelezwa mwezi Julai, 2017, umelenga zaidi kuzuia na kupunguza vitendo vyote vya ukatili dhidi ya watoto kwa asilimia 50 na umeweka lengo la kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 47 hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2022.
MHE. ANNE K. MALECELA atauliza:-
Watanzania wamehamasika sana na kilimo cha tangawizi na zao la tangawizi kwa sasa linalimwa siyo tu na wananchi wa Wilaya ya Same bali pia katika Mikoa kama Mbeya, Kigoma na Ruvuma.
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kulitafutia zao hilo soko la nje?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa tangawizi na viungo vingine katika sekta hii ambayo ni dhahiri mipango yetu ya kuvisimamia ikifanikiwa sekta hii itachangia sana uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, mipango na mikakati ya Serikali katika kutafuta soko la tangawizi pamoja na viungo vingine nje ya nchi ni pamoja na kuelimisha na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika sekta ya viungo ikiwemo tangawizi; kutafuta wateja wa zao hili kupitia Maonesho ya SIDO; Maonesho ya Kimataifa ya Julius Nyerere - Dar es Salaam na Maonesho ya Kiserikai tunayoyafanya nje ya nchi. Ili kudhibiti ubora wa viwango vya tangawizi, TIRDO imejenga maabara ya chakula yenye hadhi ya Kimataifa ili kuwawezesha wazalishaji wa tangawizi kufikia viwango vya masoko ya nje.
Mheshimiwa Spika, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa mpaka sasa tunayo makampuni 21 ambayo yanajishughulisha na kuuza viungo nje ya nchi ikiwemo tangawizi. Juhudi za Serikali ni kuona makampuni haya yanaweza kupata soko la ndani na nje ili kuwa na uwezo wa kununua tangawizi yote inayozalishwa kwa wingi na kwa bei yenye faida kwa mkulima.
MHE.SHALLY J. RAYMOND (K.n.y. ANNE K. MALECELA) aliuliza:
Tarafa ya Ndungu iliyoko Wilaya ya Same imesheheni uchumi mkubwa sana wa mazao ya chakula na biashara, Serikali ya Awamu ya Nne ya Chama cha Mapinduzi ililiona hilo na ikakubali kujenga barabara ya lami kutoka Mkomazi kupita Ndungu, Kisiwani hadi Same; barabara hiyo iliwekwa lami vipara vipara kwa kilomita tatu Kihurio, tano Kisiwani, tano Ndungu na tano Maore.
Je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kuunganisha vipande hivi ili kukamilisha barabara hii ya Mkomazi, Kisiwani hadi Same kwa kiwango cha Lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Kuteuliwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Same – Kisiwani – Mkomazi yenye urefu wa kilomita 100.5 ni barabara ya Mkoa inayojumuisha kilomita 96.46 zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kilimanjaro na kilomita 4.04 Mkoa wa Tanga. Kama alivyoeleza vizuri Mheshimiwa Mbunge sehemu tano za barabara hii, zenye jumla ya kilomita 21 zimejengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami barabara hii Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ilisaini Mkataba wenye thamani ya shilingi milioni 890.221 na Kampuni ya Kihandisi ya Advanced Engineering Solutions Limited ya hapa nchini, ikishirikiana na Kampuni ya Advanced Construction Centre ya Misri ili kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa kilomita zote 100.5 za barabara hii. Kazi hiyo ilianza tarehe 28 Juni, 2018 na inatarajiwa kukamilika tarehe 25 Machi, 2019. Kwa sasa taarifa ya awali ya mradi (Inception Report) imewasilishwa kwa ajili ya mapitio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa utekelezaji wa Mkataba huu kutawezesha kujulikana kwa gharama za ujenzi hivyo kuwezesha Serikali kuanza hatua za kutafuta fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami barabara hiyo, kwa awamu kadri fedha zitakavyopatikana. Wakati usanifu unaendelea Serikali katika mwaka wa fedha wa 2018/ 2019 imetenga jumla ya shilingi milioni 1,113.595 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza:-
Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF) umemuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuamua kukiboresha Kiwanda cha Tangawizi cha Mamba Miamba kilichoko Wilaya ya Same katika Jimbo la Same Mashariki.
Je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu sasa kuboresha barabara zinazoelekea Mamba Miamba Kiwandani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Kuteuliwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mwembe – Miamba – Ndugu yenye urefu wa kilometa 90.19 inayopita eneo la Mamba Miamba Kiwandani ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, barabara hii imetengewa jumla ya shilingi bilioni 1.487 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo ya muda maalum kwenye eneo lenye urefu wa kilometa 22.5 katika Vijiji vya Mtunguja, Mhezi, Kwizu, Marindi, Mshewa, Mwembe, Mbaga, Gohe, Kambeni na Manka pamoja na matengenezo ya kawaida yanayofanyika katika Vijiji vya Dindimo, Kanza na Miamba. Vilevile kufanyika matengenezo ya madaraja yatakayohusisha ujenzi wa madaraja (drifts) mapya mawili katika Kijiji cha Mbaga na ukarabati mkubwa wa Daraja la Mwerera lililopo katika Kijiji cha Mwerera.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 barabara hii pia imetengewa jumla ya shilingi bilioni 1.250 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo mbalimbali yakiwemo ya ukarabati na matengenezo ya kawaida na muda maalum.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo muhimu barabara hii ili iendelee kupitika bila matatizo muda wote.
MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza:-

Barabara ya Hedaru – Vunta – Myamba Wilaya ya Same ni korofi sana na kusababisha usafiri wa barabara ya Tarafa ya Mamba/Vunta kuwa mgumu:-

Je, Serikali inawasaidiaje Wananchi wa Tarafa ya Mamba/Vunta ili waweze kuendelea kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Kuteuliwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Hedaru – Vunta – Myamba yenye urefu wa Kilometa 42.2 inahudumiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (TARURA), Wilaya ya Same. Barabara hiyo ipo Ukanda wa Milimani na uhalibifu wake hunatokana na changamoto ya maji ya mvua yanayosababisha maporomoko ya udongo na kuchimbika kwa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, barabara hiyo ilitengewa kiasi cha shilingi Milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua na vivuko viwili. Uwekaji wa Miundombinu hiyo utapunguza uharibifu unaotokana na maji ya mvua. Kazi hizo zinaendelea kutekelezwa. Kwenye Mpango wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2019/2020, Serikali imeweka kipaumbele na kutenga jumla ya shilingi milioni 87.72 kwa ajili ya kuiwekea changarawe kwenye sehemu korofi.
MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza:-

Vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga bado ni tatizo nchini:-

Je, Serikali inafanya jitihada gani kupunguza na ikiwezekana kuondosha kabisa vifo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Kuteuliwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeboresha Vituo vya Afya zaidi ya 352 na vingine kujengwa upya ili vitoe huduma zote za afya ya uzazi kabla na wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua ikiwemo kumtoa mtoto tumboni kwa njia ya operesheni na kuzijengea uwezo wa kutoa huduma ya damu salama kwa watakaohitaji. Aidha, Hospitali 67 za Halmashauri zinajengwa ili huduma ziwafikie wananchi wote wa vijijini na mjini kwa usawa na urahisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vinakuwepo muda wote, Serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 270 mwaka 2018/2019. Juhudi hizi zimewezesha wajawazito kuendelea kupata huduma za afya ya uzazi na mtoto ikiwemo kinga tiba dhidi ya Malaria (SP), Fefol ambayo ni madini ya chuma na folic acid ambayo ni kinga tiba dhidi ya upungufu wa damu, vipimo vya shinikizo la damu, kaswende, wingi wa damu, sukari na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, aidha, mwezi Agosti 2019, Wizara ilizindua na kusambaza nchi nzima mwongozo wa kitaifa wa matibabu ya watoto wachanga na uanzishwaji wa vyumba maalum vya matibabu ya watoto wachanga “National Guideline for Neonatal Care and Establishment of Neonatal Care Units” mwongozo huu unalenga kuwajengea uwezo watoa hudumu juu ya huduma muhimu kwa watoto wachanga. Vilevile Wizara kwa kushirikiana na wadau wa UNICEF wameanza kusambaza vifaa mbalimbali kwa ajili ya vyumba hivyo maalum vya watoto wachanga kwa baadhi za hospitali za mikoa na Halmashauri.
MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza:-

Tarehe 8 Machi, 2019, Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli, alipokuwa Ikulu kwenye dhifa ya Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali Duniani aliutamka mwaka 2019 kuwa ni mwaka wa uwekezaji: -

Je, Serikali imejipangaje katika kutekeleza tamko hilo muhimu sana?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Kuteuliwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali inayolenga kuhakikisha tamko la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alilolitoa katika dhifa ya Waheshimiwa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania, la mwaka 2019 kuwa Mwaka wa Uwekezaji Tanzania, linatekelezwa ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza tamko hilo, Ofisi ya Waziri Mkuu imeanza kufanya mapitio ya Sera ya Uwekezaji ya mwaka 1996 pamoja na Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997 ili kuweka misingi imara ya kuboresha mazingira ya uwekezaji yatakayoendana na hali ya sasa ya kiuchumi duniani.

Aidha, Serikali imeongeza mkazo katika kuimarisha miundombinu wezeshi ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa nishati ya uhakika na ya bei nafuu, maji, mawasiliano, ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji ya reli, barabara, madaraja, anga, vivuko na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, Serikali imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mifumo ya Udhibiti wa Biashara (Blueprint Action Plan) ambapo hadi sasa Serikali imeweza kufuta na kuboresha tozo na ada 54 zilizoonekana ni kero kwa wawekezaji na wafanyabiashara kupitia bajeti ya mwaka 2019/2020. Hatua nyingine ni pamoja na kuondoa migongano na muingiliano wa majukumu miongoni mwa Mamlaka za Udhibiti kama vile Shirika la Viwango Tanzania na Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa na Vifaa Tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo mikoani vilevile Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kituo chetu cha Uwekezaji (TIC) imeendelea kushirikiana na Ofisi za Mikoa kuandaa makongamano ya uwekezaji yanayonadi vizuri fursa za uwekezaji mikoani. Kwa mwaka huu 2019 kwa mikoa ambayo tayari imeshafanya makongamano hayo ni takribani mikoa 9 na kwa sasa tunaendelea na maandalizi katika Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali imejidhatiti kuhakikisha changamoto zinazokabili wawekezaji nchini zinapatiwa ufumbuzi kupitia mikutano ya mashauriano kati ya Serikali na sekta binafsi katika ngazi za Mikoa na katika sekta mbalimbali. Kwa sasa tumeshafanya mikutano hiyo katika Mikoa ya Arusha, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Aidha, Serikali inaendelea kuvutia uwekezaji kutoka nje kwa kutekeleza ipasavyo diplomasia ya uchumi kupitia Balozi zetu za nje pamoja na kufanya mikutano ya kimkakati na wawekezaji wa nje waliowekeza nchini ili kuvutia uwekezaji zaidi na kufanya mashauriano nao.
MHE. ANNE K. MALECELA Aliuliza:-

Je, Serikali ilishawahi kulifanyia matengenezo yoyote muhimu gari lililotolewa na Mbunge kutoka kwa wafadhili toka Japan na kupelekwa Kituo cha Polisi Gonja katika Jimbo la Same Mashariki mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba ama napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela Mbunge wa Same Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi cha Gonja kilichopo Wilaya ya Same kina gari namba PT 1988 Toyota Land Cruiser, ambalo lililetwa hapo mnamo mwaka 2015 ili kuhudumia wananchi. Mnamo tarehe 22 Juni, 2021 gari hilo lilisimama kufanya kazi ili kulinda usalama wa watumiaji na katika kulifanyia ukaguzi gari hilo lilikutwa lina ubovu wa mfumo wa usukani, mfumo wa break, clutch plate, mfumo wa umeme, ball joints na kuisha kwa matairi na bush. Aidha, tathmini ya matengenezo ya gari hilo ni shilingi 4,500,000 na fedha za matengenezo zimeshaombwa kutoka Makao Makuu ya Polisi. Ninakushukuru.