Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Prof. Joyce Lazaro Ndalichako (14 total)

MHE. MASHIMBA M. NDAKI (K. n. y. MHE. LEAH J. KOMANYA) aliuliza:-
Mkoa wa Simiyu hauna Chuo cha Ufundi (VETA) na kuwa vijana wengi waliohitimu elimu ya msingi na sekondari:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga chuo cha ufundi ili vijana hao waweze kupata elimu ya ufundi na kuweza kujiajiri?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mkoa wa Simiyu tayari imeshatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Simiyu, katika bajeti ambayo Waheshimiwa Wabunge waliipitisha ya Wizara yangu, kiasi cha fedha cha shilingi 4,045,000,000 kimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ujenzi huo. Maandalizi ya awali ikiwemo kumpata mshauri elekezi, uandaaji wa michoro pamoja na makadirio ya ujenzi yaani Bills of Quantities (BOQ) na kumpata Mkandarasi yanatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2016 na ujenzi unatarajiwa kuanza rasmi mwezi Januari, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Simiyu ni kutoa mafunzo ya ufundi stadi na huduma kwa vijana wanaohitimu elimu ya msingi na sekondari katika Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu ili waweze kupata elimu ya ufundi na hivyo kuwawezesha kujiajiri.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Matatizo ya wanafunzi kutojua kusoma na kuandika pamoja na kutofanya vizuri katika mitihani yao mara zote lawama zinakwenda kwa Walimu.
Je, Serikali imefanya utafiti wa kina na kuona kama Mwalimu peke yake ndiye anayeweza kumfanya mwanafuzi aweze kufanikiwa katika masomo yake?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassor Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ufuatiliaji unaofanyika kupitia Wadhibiti wa Ubora wa Shule na wataalam mbalimbali wa elimu, imethibitika kwamba Mwalimu ana nafasi kubwa katika kumwezesha mwanafunzi kumudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu ili aweze kufanya vizuri zaidi katika masomo yake ya baadaye. Hata hivyo, ili Mwalimu aweze kufanya kazi yake kwa ufanisi na kumsaidia mwanafunzi ipasavyo, masuala mengine yanayopaswa kuzingatiwa ni pamoja na:-
Uwiano wa Mwalimu kwa wanafunzi katika darasa, upatikanaji wa vitabu, vifaa na zana stahiki, ushirikiano wa wazazi na jamii pamoja na mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia hayo, Serikali inachukua hatua mbalimbali za kuimarisha ufundishaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ikiwa ni pamoja na yafuatayo:-
Kwanza, kutoa mafunzo kazini kwa Walimu, Wadhibiti Ubora wa Shule na Wakuu wa Shule; kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara; kuhakikisha upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kujifunzia na kufundishia kwa wakati; na kuweka mazingira mazuri ya shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuwapa ushirikiano wa kutosha Walimu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Aidha, napenda kutumia nafasi hii kuwahimiza Waheshimiwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi kuweza kuwahamasisha wazazi/walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanafuatilia maendeleo ya watoto wao mara kwa mara ili waweze kumudu stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu na kufanya vizuri zaidi katika masomo yao.
MHE. RICHARD P. MBOGO (K.n.y. MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwepo na tatizo la wanafunzi wanaoingia vyuo vikuu kukosa mikopo na elimu ya juu ni suala la Muungano:-
Je, Serikali ya Muungano inaipatia SMZ kiasi gani cha fedha kwa mwaka kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu hutoa mikopo kwa kuzingatia kwamba muombaji ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, awe muhitaji aliyedahiliwa katika chuo cha elimu ya juu. Mikopo inayotolewa inatoa umuhimu wa kipekee kwa vipaumbele vya Taifa ambavyo ni Uhandisi wa Gesi na Mafuta, Sayansi za Afya, Ualimu, Ualimu wa Sayansi na Hisabati na Uhandisi wa Kilimo na Maji. Aidha, wanafunzi yatima na wale wenye ulemavu hupewa kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwepo kwa vyuo vya elimu ya juu Tanzania Bara na Visiwani. Aidha, Serikali inatambua kuwa fursa za kusoma elimu ya juu zinapatikana vyuo vyote vya elimu ya juu hapa nchini ambapo kumekuwepo na wanafunzi wa elimu ya juu wanaotoka Zanzibar na kusomea Tanzania Bara na wengine hutoka Tanzania Bara na kusomea vyuo vikuu vilivyoko Zanzibar. Hivyo basi, kupitia Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu Serikali inawatangazia wale wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu vyote nchini wanaohitaji mikopo kuomba mikopo bila kujali kama anatoka Tanzania Bara au Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba hakuna tengeo maalum la fedha kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kugharamia mikopo ya elimu ya juu. Mikopo inatolewa kwa muombaji aliyekidhi vigezo na sifa za kitaaluma bila kujali anakotoka sehemu gani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, katika fomu ya kuwasilisha maombi ya mikopo hii hakuna mahali panapomtaka muombaji kutaja anakotoka sehemu gani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo Bodi inawatambua waombaji wote kuwa ni Watanzania.
MHE. COSATO D. CHUMI (K.n.y. MHE. KASUKU S. BILAGO) aliuliza:-
(a) Je, Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 itaanza kutekelezwa lini katika kipengele cha Elimu ya Msingi (Chekechea - Kidato cha Nne)?
(b) Je, ni Walimu wangapi wa Sekondari wanahitajika ili kutekeleza Sera hiyo?
(c) Je, hali ya miundombinu katika shule zetu ikoje katika kutekeleza Sera hiyo.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kasuku Samson Bilago, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa kipengele cha Elimu Msingi ambapo watoto watasoma kwa miaka kumi mfululizo utaanza mara baada ya kupitishwa kwa mabadiliko ya Sheria ya Elimu, Sura ya 353 ya mwaka 1978 na Sheria nyingine zitakazoleta ufanisi katika utekelezaji wa kipengele hicho. Aidha, uwepo wa miundombinu ya kutosheleza na Walimu wa kutosha, vitazingatiwa kabla ya utekelezaji kuanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu zilizopo idadi ya Walimu wa sekondari ni 88,999 na kati yao 18,545 ni Walimu wa masomo ya sayansi na hisabati. Walimu 70,454 ni Walimu wa masomo ya lugha, sanaa na biashara. Hata hivyo, kuna upungufu wa Walimu 22,460 wa masomo ya sayansi na hisabati katika Shule za Sekondari na kuna ziada ya Walimu 7,988 wa masomo ya Sanaa, Lugha na Biashara. Uchambuzi wa mahitaji halisi ya miundombinu na Walimu wanaohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa Elimu Msingi unaendelea kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kupitia Halmashauri za Wilaya, Jiji na Manispaa, Serikali imeendelea kutenga fedha katika bajeti katika kila mwaka kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika shule za Msingi na Sekondari. Lengo ni kupunguza changamoto ya utoshelevu wa miundombinu kama vile vyumba vya madarasa na nyumba za Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 67.83 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu, ambazo tayari zimeshapokelewa kwenye halmashauri na zinatumika kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa nyumba za madarasa, ujenzi wa vyoo vya Walimu na wanafunzi na ujenzi wa nyumba za Walimu. Shule ambazo zinanufaika na hicho kiasi cha bilioni 67 jumla yake ni 528 nchini kote. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 48.3 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya shule za msingi na sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na uimarishaji wa miundombinu, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali inatarajiwa kuajiri Walimu 35,411 katika shule za msingi na sekondari, ili kuongeza idadi ya Walimu kwa lengo la kuongeza tija katika sekta ya elimu hapa nchini.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imeongeza makato kwa wanufaika wa mikopo kutoka asilimia 8 hadi 15 bila kuwashirikisha wadau mbalimbali pamoja na wanufaika wa mikopo.
• Je, Serikali haioni kwamba imevunja mkataba wa makubaliano kwa kuwa wakopaji walisaini mkataba wa asilimia 8 na siyo asilimia 15?
• Ongezeko la makato limewaathiri sana wakopaji na kuwafanya kuwa ombaomba na kuishi maisha magumu sana. Je, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu haioni kama litakuwa jambo la busara kusitisha makato hayo ya 15% mara moja ili kunusuru maisha ya watumishi waliokopa?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Paschal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijavunja mkataba wowote na wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu. Kilichofanyika mwaka 2016 katika marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo Sura ya 178 ni kuiboresha sheria hiyo kwa kutaja kiwango mahususi cha asilimia 15 kinachopaswa kukatwa kutoka mshahara ghafi wa wanufaika. Kabla ya marekebisho hayo kifungu cha 7(1)(h) kiliipa Serikali mamlaka ya kupanga kiwango cha makato na kubadilisha kiwango pale itakapoona inafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kukuhakikishia kuwa Serikali inafahamu umuhimu wa kuwashirikisha wadau katika marekebisho ya sheria yoyote, hivyo basi, katika mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Sura ya 178 ya mwaka 2016 wadau mbalimbali walishirikishwa na wadau hao ni pamoja na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi TUGHE na TUCTA, Chama cha Mawakili nchini (TLS) pamoja na wanafunzi kutoka Taasisi za Elimu ya Juu kama vile Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Elimu ya Biashara Dodoma pamoja na Chuo cha Mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makato ya asilimia 15 kutoka kwenye mshahara ghafi wa wanufaika wa mikopo yamewekwa kisheria kwa lengo la kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinarejeshwa kwa wakati ili ziweze kuwasomesha Watanzania wengine ambao wanauhitaji. Hivyo kwa sasa Serikali haina mpango wowote wa kusitisha makato hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu nchini kuhakikisha kwamba wanarejesha mikopo yao kwa wakati kwani wapo Watanzania wengi ambao wanahitaji mikopo hiyo ili iweze kuwanufaisha wahitaji wengine. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Hivi karibuni Serikali ilikusanya vitabu vyenye dosari vilivyosambazwa shule za msingi nchini.
i. Je, Serikali imepata hasara kiasi gani kutokana na dosari hiyo?
ii. Je, ni hatua zipi zimechukuliwa kwa waliosababisha hasara hizo?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali imeondoa vitabu ambavyo vilikuwa shuleni ambavyo vilisambazwa mwaka 2017 ambavyo vilibainika kuwa vina makosa. Katika utekelezaji wa hatua hiyo Serikali ilizingatia taarifa ya tathimini iliyofanyika kuhusu vitabu hivyo na taarifa hiyo iliainisha vitabu vilivyokuwa na makosa ya kimaudhui na vile ambavyo havikuwa na makosa ya kimaudhui. Vitabu ambavyo vimeondolewa shuleni ni vile ambavyo vina makosa ya kimaudhui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania limeiagiza Menejimenti ya Taasisi kupitia vitabu vyote vilivyoondolewa shuleni na kufanya tathimini ya ukubwa wa makosa ili hatimaye kukokotoa hasara iliyopatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania iliwasimamisha kazi watumishi 29 ili kupisha uchunguzi wa chanzo cha dosari mbalimbali za vitabu. Uchunguzi huu umefikia hatua ya watumishi hao kuandikiwa mashitaka ya kinidhamu ambapo yakithibitika hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.
MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA aliuliza:-
i. Je, Serikali ina mikakati gani ya kuboresha elimu ya awali?
ii. Kwa kuwa msingi mzuri wa elimu huanzia katika shule za awali. Je, Serikali haioni kuwa ni jambo la muhimu kuanzisha shule za awali na kuajiri walimu waliofuzu kutoa elimu hiyo katika shule za vitongoji hasa vijijini tofauti na ilivyo sasa ambapo jamii ndiyo inayozianzisha na kuziendesha shule hizo kwa kutumia walimu wasio na taaluma?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Steven Lemomo Kiruswa, Mbunge wa Longido kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya awali kabla ya mtoto kuanza darasa la kwanza na kwa kutambua umuhimu huo Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuboresha elimu hiyo ikiwemo kutenga vyuo 18 ambavyo vinatoa mafunzo kwa ajili ya kuandaa walimu wa elimu ya awali ili kuongeza idadi ya walimu wa kufundisha wanafunzi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali inaboresha mtaala na muhtasari wa elimu ya awali na kutoa mafunzo kwa walimu kwa ajili ya utekelezaji wa mtaala huo na kuandaa vitabu vya kiada vya aina sita pamoja na vitabu vya ziada 12 vya hadithi kwa ajili ya elimu ya awali ambavyo tayari vimekwishaandaliwa na sasa viko katika hatua ya uchapaji. Pia Serikali imehakikisha kuwa kila shule ya msingi inakuwa na darasa la elimu ya awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za elimu zinaelekeza watoto wa elimu ya awali wanapaswa kufundishwa na walimu waliosomea elimu ya awali au kupata mafunzo kazini kuhusu ufundishaji wa elimu ya awali. Hivyo Serikali itaendelea kuimarisha mafunzo ya ualimu wa elimu ya awali sambamba na kuendelea kuimarisha madarasa ya elimu ya awali.
MHE. ASHA ABDALLAH JUMA (K.n.y. MHE. KHADIJA NASSIR ALI) aliuliza:-
Sera yetu ya Elimu inatueleza kuwa elimu ya msingi ni hadi kidato cha nne.
Je, ni lini Serikali itaboresha kiwango hiki cha elimu ya msingi hadi kufika ngazi ya Ufundi Stadi yaani VETA?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa elimu wa Tanzania unasimamiwa na Sheria ya Elimu Na.25 ya mwaka 1978. Sheria hii inabainisha wazi kuwa elimu ya msingi ni miaka saba kuanzia Darasa la Kwanza hadi Darasa la Saba. Hivyo, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, elimu ya msingi inatolewa kwa muda wa miaka saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa elimu ya msingi kwa miaka saba bila kuunganisha na mafunzo ya ufundi stadi. Sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kwamba maudhui yaliyopo kwenye mtaala wa elimu ya msingi bado yanakidhi mahitaji ya sasa ya wahitimu wa ngazi hiyo ya elimu ya msingi lakini pia muda ambao wanafunzi wa elimu ya msingi wanakaa shuleni hauwezi kutosha kuunganisha na mafunzo ya ufundi stadi. Hivyo, mafunzo ya ufundi stadi yataendelea kutolewa na Mamlaka ya Ufundi Stadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza nafasi za udahili katika Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi. Juhudi hizi ni pamoja na kujenga Vyuo vipya vya Ufundi Stadi na vilevile kufanya ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ili viwe na mazingira fanisi ya kujifunzia na viweze kutoa mafunzo katika fani mablimbali.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-

Chunya ni moja kati ya Wilaya 10 nchini zilizopangiwa kujengewa Chuo cha VETA mwaka 2013.

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA (K.n.y WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Mwambalaswa Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo:-

Mheshimimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Elimu ya Ufundi na Maafunzo ya Ufundi Stadi katika kufikia azma ya Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Katika kutekeleza azma hiyo Serikali ina mkakati wa kuwa na Vyuo vya Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya hapa nchini. Ujenzi huu unafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimimiwa Spika, katika utekelezaji wa mpango huu wa ujenzi wa Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini, Wilaya ya Chunya ni moja kati ya Wilaya za kipaumbele zilizopo kwenye mpango wa ujenzi.

Mheshimimiwa Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2019/ 2020 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi kwa Wilaya 25 ikiwemo Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chunya. Kila chuo kimetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.5.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA (K.n.y. MHE. GRACE V. TENDEGA) aliuliza:-

Walimu wenye weledi wa kuwafundisha Watu Wenye Ulemavu ni wachache sana nchini.

Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha Walimu hao ni wa kutosha?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA) alijibu:-

Mheshimimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekonolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa Walimu wenye taaluma ya Elimu Maalum. Changamoto hii ina sababishwa na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wenye ulemavu kutokana na mabadiliko chanya ya kimtazamo na uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimimiwa Spika, mahitaji ya Walimu wa Elimu Maalum nchini ni Walimu 8,882 katika shule maalum na vitengo vinavyopokea wanafunzi wenye mahitaji maalum 706. Hadi kufikia Disemba 2018 Walimu 5,556 wenye taalum ya Elimu Maalum ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada walihitimu katika Vyuo mbalimbali nchini vikiwemo Chuo cha Ualimu Patandi na Chuo Kikuu Dodoma.

Mheshimimiwa Spika, Serikali imekamilika upanuzi wa Chuo cha Ualimu Patandi ili kukiongezea uwezo wa kudahili. Pia Chuo kimeanzisha kozi ya Elimu Maalum katika ngazi ya Astashahada kwa Walimu tarajali kwa mwaka wa masomo 2018/2019. Hatua hii itaongeza idadi ya Walimu wanaojiunga na mafunzo ya Ualimu wa Elimu Maalum ili kupunguza changamoto ya Walimu wenye taaluma ya Elimu Maalum wanaohitajika nchini.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-

Kumekuwa na utaratibu kwa Vyuo Vikuu Tanzania kuajiri Wahadhiri toka nje ya nchi kwa lengo la kukuza tafiti na taaluma katika vyuo hivyo:-

(a) Je, katika miaka 10 iliyopita, ni wahadhiri wangapi wameajiriwa katika Vyuo Vikuu Tanzania?

(b) Je, ni mafanikio gani kitaaluma na kiutafiti yameletwa na wahadhiri hao toka nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) K.n.y. WAZIRI WA
ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Vyuo Vikuu vimekuwa vikiajiri wanataaluma kutoka nje kwa malengo ya kuboresha hali ya taaluma na kujiimarisha katika masuala ya kiutafiti katika nyanja mabalimbali. Ajira ya wataalam wa kigeni hutolewa kwa kibali maalum na kwa mkataba kwa kuzingatia mahitaji ya utalamu yaliyopo katika chuo husika. Katika miaka 10 iliyopita, kati ya mwaka 2008 mpaka 2009, hadi 2018/2019, vyuo vikuu 17 yaani vya umma vinane na binafsi tisa, viliajiri wanataaluma wa kigeni 502. Aidha kutokana na jitihada za Serikali na vyuo vyenyewe kuendeleza wataalm wa ndani, wanataaluma wa kigeni wameendelea kupungua, hali iliyodhihirishwa na idadi ya wanataaluma wa kigeni waliopo nchini sasa kubaki 151 tu, hadi kufikia mwaka 2018/2019.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikio yaliyopatikana baada ya kuajiri wataalamu wageni ni pamoja na kupata wataalamu wa fani ambazo nchi haijajitoshereza, kuanzishwa kwa programu mpya katika vyuo mbalimbali, kusimamia tafiti za kitaaluma mbalimbali katika vyuo vilivyoajiri katika nyanja mbalimbali. Pia imesaidia kuwezesha uanzishwaji wa mashirikiano kati ya vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi na kuwezeshwa kupatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kitafiti vya kufundishia na kujifunzia na vya maabara. Ahsante.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-

Miaka iliyopita Serikali ilikuwa na nia ya kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika shule za msingi na za upili.

(a) Je, nini kilitokea kwa Serikali katika kutekeleza nia yake hiyo nzuri?

(b) Je, ni lini Serikali itaanza kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika shule za msingi na za Upili ili kukuza uelewa wa wanafunzi katika masomo yao?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKONOLIJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, suala la lugha ya kufundishia na kujifunzia ni suala la kisera kama ambavyo limeanishwa katika aya 3.219 na 3.220 ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014. Sera hiyo inabainisha matumizi ya lugha mbili za kufundishia na kujifunzia ambazo ni Kiswahili na Kiingereza na kwa sasa lugha ya Kiswahili inatumika kufundishia katika ngazi ya elimu ya awali na elimu ya msingi, vyuo vya ualimu ngazi ya cheti na vyuo vya ufundi stadi.

(b) Mheshimiwa Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali bado inaendelea kutumia lugha ua Kiingereza katika kufundishai na kujifunzia katika ngazi ya elimu ya sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu na hii ni kutokana na umuhimu wa lugha hiyo katika masuala ya kitaifa, ya kikanda na kimataifa kwa ajili ya mawasiliano na biashara ili kuwajengea wanafunzi ufahamu na umahiri katika lugha hiyo.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULLA aliuliza:-

Mkoa wa Geita hauna Chuo cha Serikali hata kimoja:-

Je ni lini Serikali itajenga Vyuo Mkoani Geita ikiwemo vya Afya na Madini?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa elimu inayotolewa katika ngazi ya vyuo katika kujenga ujuzi unaochochea maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla. Hivyo, ni azma ya Serikali kujenga na kuboresha vyuo vilivyopo katika mikoa mbalimbali nchini ili viweze kutoa elimu bora kwa wanafunzi wengi zaidi. Kwa sasa mkoa huu una Chuo kimoja cha Serikali cha Uuguzi ngazi ya kati (Geita School of Nursing). Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vingine viwili vya VETA. Wizara pia imepokea maombi kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita ya kukikabidhi Chuo cha Ujasiliamali kiitwacho Magogo ili kiwe chini ya Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA). Serikali imeridhia ombi hilo na taratibu za makabidhiano zinaendelea. Kwa kuwa vyuo hivi vimezungukwa na migodi, pamoja na fani zingine, Serikali itaangalia pia uwezekano wa kuanzisha fani ya madini.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Geita pia kuna tawi la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambacho hutoa masomo kwa ngazi ya elimu ya juu. Kwa kuwa masomo ya ngazi ya elimu ya juu ni suala la kitaifa, kwa sasa wananchi wa Geita wanashauriwa kuendelea kutumia vyuo vikuu vingine vilivyopo nchini.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanyia maboresho Mfumo wa Elimu Tanzania?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la uboreshaji wa utoaji wa elimu katika nchi yoyote ni endelevu, ambalo hutegemea mabadiliko yanayotokea katika nchi kwenye nyanja za kiuchumi na kijamii, pamoja na ulinganisho wa maendeleo ya sayansi na teknolojia. Katika nchi yetu, suala hili la uboreshaji wa mifumo ya elimu limekuwa likifanyika na hutegemea tathmini mbalimbali za kitaalamu zinazofanyika kwa nyakati tofauti.

Mheshimiwa Spika, mfano elimu ya sekondari ya chini (O level) kutambuliwa kuwa ni sehemu ya Elimumsingi kwa watoto wetu na inatolewa bila malipo ya ada. Aidha, katika elimu ya ualimu tumeongeza miaka ya kumwandaa mwalimu wa elimu ya awali kutoka miaka miwili kuwa miaka mitatu. Pamoja na mabadiliko hayo, Serikali imeendelea na uimarishaji wa elimu yetu kuwa ya umahiri (competence based) kutoka katika mfumo wa awali ambao ulimwandaa mhitimu kwa nadharia bila mafunzo kwa vitendo ya kutosha. Uboreshaji huu umefanyika sambamba na uimarishaji wa mitaala katika ngazi zote.

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mfumo wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi, Serikali imeunda Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta ambayo yanakuwa kiungo kati ya Vyuo vya Elimu ya Ufundi na wadau, vikiwemo viwanda na waajiri. Mabaraza hayo yatahakikisha kuwa mitaala inayotumika inakidhi mahitaji ya wadau na soko la ajira. Katika ngazi ya elimu ya juu, Serikali imeendelea kuhuisha na kuanzisha programu mbalimbali zinazotolewa ili kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaohitajika Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali, imeanzisha vituo atamizi katika taasisi za elimu ili kuhakisha wahitimu wanapata fursa za kulea mawazo na ubunifu wao. Maboresho haya yanalenga kuimarisha umahiri wa wahitimu wetu ili waweze kuajirika na pia kujiajiri.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa Mfumo wa Elimu unakidhi mahitaji ya soko Kitaifa, Kikanda na Kimataifa kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu.